barua ya wazi kwa rais kikwete

Upload: anonymous-x8qgwff

Post on 03-Jun-2018

308 views

Category:

Documents


2 download

TRANSCRIPT

  • 8/12/2019 Barua Ya Wazi Kwa Rais Kikwete

    1/4

    Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

    Dk. Jakaya Mrisho Kikwete

    Ikulu

    P O Box 9120

    Dar es Salaam

    Yah: Hotuba Yako ya Kuwagawa Watanzania

    Mheshimiwa Rais,

    Tumelazimika kuandika barua hii kwako kama kiongozi wa juu wa taifa letu ili kukuonesha

    namna ambavyo tumesikitishwa na matamshi yako wakati wa ufunguzi wa Bunge Maalum la

    Katiba mjini Dodoma. Tukiwa sehemu ya jamii kubwa ya Kizanzibari tuishio nje ya nchi

    yetu, hotuba yako imetutia khofu kubwa kulenga kwake zaidi kwenye kuvunja na sio kujenga

    mustakbali mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hotuba yako Mheshimiwa Rais,

    haikuzingatia maslahi ya Muungano wetu kwa misingi ya umoja unaonendana na matakwa yawananchi walio wengi.

    Tunakuandikia barua hii kukuzindua kile ambacho tumekiona kinakwenda tafauti na akhlaki

    zako. Ukweli ni kwamba kwa muda wote wa kipindi chako cha utawala tumekuwa

    tukikutazama kama ni tarajio jipya lililojengeka kwa misingi ya haki, insaaf na kioo cha

    uadilifu kwa pande mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano.

    Tunazungumza nawe moja kwa moja sio tu kama kiongozi wa taifa, bali pia kama mtu

    tuliyempa matumaini hayo. Wewe ni mtu wa mwisho kwetu kuamini kuwa anaweza kujenga

    khofu badala ya matumaini, batili badala ya halali, kitisho badala ya nasaha na mgawanyikobadala ya utangamano.

    Mheshimiwa Rais,

    Ulichokifanya siku ya tarehe 21 Machi 2013 ni kuzua taharuki kwa raia wa Jamhuri ya

    Muungano hasa kwa ndugu zetu wa Kizanzibari waishio upande wa pili wa Muungano huo.

    Ulichofanya ni kulihusisha jeshi letu linalothaminiwa dunia nzima kwa misingi ya heshima

    kwa kusaidia pakubwa kuifanya Jamhuri yetu kuwa ndio kisiwa cha amani kwa takribani

    miaka yote 50 ya Muungano wetu. Hakujawahi katika historia ya Tanzania kwa rais kuzuwa

    hisia za mapinduzi ya kijeshi kama hoja mbadala ya kuviza maoni ya walio wengi katika

    kiwango ambacho wewe umefanya.

    Mheshimiwa Rais,

    Ulikuwa umejizolea sifa kwa kuwa mmoja wa viongozi wachache wa Tanzania ambao

    hawakuonea haya mtafaruku wa kisiasa visiwani Zanzibar na ukaamua kuuvalia njuga ili

    kuhakikisha kuwa unatulizwa kwa amani. Kwa Wazanzibari wengi walio ndani na nje ya

    nchi, matarajio yao yalikuwa ni kwamba wewe ungelisimimia haki yao ndani ya Muungano

    kwa uadilifu mkubwa haidhuru maoni waliyonayo kuhusu muundo wa Muungano

    yanatafautiana na yako.

    Tulikutegemea kuwa msimamizi wa haki uliyejizatiti kuhakikisha chembechembe za ubaguzizinakufa katika kipindi chako cha utawala. Tulikutegemea usimame imara kusimamia hilo

  • 8/12/2019 Barua Ya Wazi Kwa Rais Kikwete

    2/4

    maana ndiyo misingi ya kiuongozi. Hatukutegemea hata kidogo uyumbe na uyumbishwe na

    kundi la wahafidhina ndani na nje ya Chama chako cha Mapinduzi (CCM), kwani maslahi

    mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu zaidi kuliko maslahi finyu ya

    makundi hayo ya kihafidhina. Lakini leo hii umekwenda kinyume hata na imani yako kwa

    kuwabeza Wazanzibari waishio Tanganyika bila ya kuthamini mchango wao mkubwa katika

    ukuwaji wa uchumi katika Muungano huu.

    Tukukumbushe Mheshimiwa Rais, ikiwa umesahau, kuwa ni Zanzibar ndiyo iliyoungana na

    Tanganyika. Si Wapemba wala Waunguja. Sawa na sisi kusema kwamba hatukuungana na

    Wadengereko au Wanyamwezi waishio visiwani Zanzibar, bali ni Tanganyika kwa jumla

    kama nchi iliyo na makabila zaidi ya 100 ambayo tokea awali tumekuwa pamoja kwa misingi

    ya udugu kabla hata ya Muungano wa nchi zetu.

    Pili tukukumbushe Mheshimiwa Rais kwamba suala la kuuvunja Muungano halijawahi kuwa

    sehemu ya mjadala mkuu kwenye Rasimu ya Katiba. Ni wewe na wenzako ndio ambao

    munalizusha kila mara kwa mintarafu hiyo hiyo ya kutisha. Lakini hata kama hayo yatakuwa

    ndio matokeo ya munayoyataka, basi tukukumbushe kuwa Waunguja na Wapemba waishio

    Tanganyika wataathirika sawa sawa na mtetemeko wa Muungano kama ilivyo kwa

    Watanganyika waishio visiwani. Si walima vitunguu tu ambao husaidia katika ulipaji wa kodi

    inayotumika kuijenga Tanganyika watakaoathirika na uvunjwaji wa Muungano, bali kila

    mmoja wetu.

    Inashutsha sana kwa rais wa nchi mwenye heshima duniani kukiuka misingi ya usawa kwa

    kuwalenga jamii ya watu anaowaongoza kwa vitisho badala ya kuwahakikishia ulinzi hasa

    kwa vile ndie jemedari mkuu wa jeshi aliyeapa kuwalinda wananchi wote wa Muungano huukwa nguvu zote alizopewa kikatiba.

    Hatukuzuii kutetea na kulinda mfumo wa serikali mbili hasa ukiwa mwenyekiti wa chama

    chako kilichojizatiti katika mfumo huu wa sasa. Lakini ukiwa kama ni rais wa nchi inakupasa

    kuzitafautisha sehemu hizi mbili za kimamlaka ili kuwe na ufanisi wa demokrasia

    iliyokuchaguwa na kukupa hadhi ya rais wa Muungano huu.

    Hivi kweli hakukuwa na hoja nzito za kuulinda mfumo wa sasa bila ya kuwaingiza wananchi

    katika mzozo mkubwa utaoleta nyufa katika taasisi tunayotarajia kuilinda na kuiimarisha?

    Umeamsha hisia kwamba ni Wapemba pekee kama ulivyotuita tunaofaidika na

    Muungano huu na kuendeleza kampeni ya chuki juu yetu, badala ya kuwazindua wananchi

    michango ya pande zote mbili katika ukuwaji wa uchumi na pia misingi ya amani

    tunayojivunia. Umekiuka maadili ya uongozi uliotukuka ulioapa kuitekeleza ukiwa ni mkuu

    wa Muungano huu na kudharau michango yetu Wazanzibari katika sekta zote za maendeleo

    ya Tanganyika.

    Tukukumbushe tena Mheshimiwa Rais kwamba huna uhalali wa kuunganisha mfumo wa

    Serikali Tatu na uwezekano wa kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi. Umekuwa mmoja wa

    wapatanishi wa mzozo wa Madagascar, kwa mfano, na unajuwa kwamba mapinduzi ni zao la

  • 8/12/2019 Barua Ya Wazi Kwa Rais Kikwete

    3/4

    wapenda madaraka, wasiopenda kuwasikiliza wananchi walio wengi pamoja na uendeshwaji

    wa nchi kwa misingi isiyoendana na haki, uadilifu na ihsani.

    Mfumo wa muungano unahitaji ithibati nzito kutoka kwa wananchi wa pande zote mbili.

    Haiwi sawa kuendeleza hamasa za kisiasa kwa kuzidharau hisia na matakwa ya walio wengi

    kwa kisingizio cha kuendeleza siasa za kuwaridhisha Wazanzibari pekee.

    Hiyo ni sawa na rushwa ya upande mmoja, na ulaghai wa hali ya juu kwa upande mwengine,

    kwa vile kero za Muungano hazipo kwa Wazanzibari pekee. Tunahitaji mfumo utaokuwa na

    nguvu ya matakwa ya pande zote mbili, utakaoweza kudumu na kuwa tunu kwa Afrika

    nzima.

    Miaka 50 ya Muungano huu wetu mbali ya kwamba hakuna aliyejaribu kujiunga nasi kwa

    kutokuwa na manufaa, bali hata wengine walioungana hawakuwahi kuutazama huu wetu

    kama kigezo cha kuungana.

    Kwa kuendeleza mfumo wa sasa katika jitihada za kutiatia viraka, zipo ishara nzito kwamba

    sio tu kwamba Muungano hautadumu, bali pia utazua machafuko makubwa na kuzitia nchi

    zetu katika giza la historia chafu na dowa litaanza kwako kwa kuogopa kivuli chako

    mwenyewe. Ni vigumu kwa wakuu wa nchi kupima hali halisi ya nchi kwa kusikiliza

    wapambe waliojipenyeza kwa fitna na kukisema kile ambacho wakuu hupenda kukisikia.

    Kwa sasa angalizo kwako ni kuangalia mazingira yalivyo hasa katika Muungano na muamko

    wa wananchi katika mabadiliko waliyoyategemea zaidi kutoka kwako.

    Mheshimiwa Rais,

    Tunakuusia tena kama tunavyoziusia nafsi zetu, wasikilize wananchi walio wengi na

    matakwa yao katika ujenzi wa Muungano mpya utakaokuwa madhubuti na utakaoacha jina

    lako kuwa kwenye kumbukumbu njema kwa vizazi vijavyo. Haki, usawa na heshima baina

    ya pande hizi mbili ndio ziwe dira kwako katika kuleta mustakbali wa mabadiliko

    yatayotuweka katika Muungano utakaothaminiwa na kutunzwa na kila mdau.

    Matarajio yetu katika kipindi chako ni mageuzi ya kweli yanayoendana na wakati,

    yatakayoangalia matakwa ya wananchi na kuhakikisha hekima zako na busara zitaweza

    kuzaa matunda makubwa yatayoweza kuwa neema kwa vizazi vijavyo.

    Mheshimiwa Rais,

    Khofu ni adui mkubwa wa mabadiliko ya kweli na yaliyo thabiti. Ulichaguliwa kwa

    matarajio makubwa kwa vile ulionyesha wazi kuwa miongoni mwa wachache walio na dira

    ya mapatano, ukuwaji wa amani na mapambazuko ya demokrasia nchini.

    Tanzania iliweza kubadili mfumo wa vyama vingi na kubeza waliokuwa na khofu ya

    mabadiliko. Zanzibar iliweza kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo kwa upande

    mkubwa imerejesha imani kwa wananchi na hata wawekezaji na kuwa ni chombezo kwa

    wengine majirani kufuatia.

  • 8/12/2019 Barua Ya Wazi Kwa Rais Kikwete

    4/4

    Na kwa hili la mabadiliko ya mfumo wa Muungano tuna hakika ndio nafasi pekee ya

    Muungano mpya utakaobeba haki, usawa na heshima kwa kila mwananchi wa nchi zetu hizi.

    Mheshimiwa Rais,

    Tumekuandikia haya yote kwa kuwa tunaamini kuwa ukitaka unaweza kurekebisha pale

    ulipoteleza. Wewe ni mwanaadamu licha ya kuwa kiongozi mkuu wa nchi. Una nafasi ya

    kufanya makosa, lakini una nafasi kubwa zaidi ya kusahihisha makosa yako, maana makosa

    yako yana uzito mkubwa na wa kipekee kwa hatima ya taifa.

    Tunakunasihi uipitie tena hotuba yako, weka sawa ulimopinda, safisha ulimochafua. Nchi

    inataka uongozi wako kukwamuka na kusonga mbele. Haitaki vitisho wala khofu zako.

    Ukihisi ni maamuzi magumu zaidi, rudi kwa wananchi na uwaulize tena kwa uwazi matakwa

    yao juu ya mfumo wa Muungano wa nchi zetu. Sote tunataka Tanzania kwanza pia hapana

    shaka, lakini kwa maana gani ya Tanzania kwanza?

    Tanzania kwanza isiyobebwa na shengesha za mfumo butu wa sasa.

    Tanzania kwanza isiyoviza ukweli wa kuwepo kwa Zanzibar na Tanganyika zinazojiendesha

    kwa ufanisi.

    Tanzania kwanza iliyojidhatiti katika Muungano wa heshima, usawa na haki.

    Tanzania kwanza iliyobebwa na matashi na matakwa ya wananchi.

    Tanzania kwanza ya Serikali Tatu sio moja ya kuimeza Zanzibar na isiyotenda haki kwa

    Tanganyika.

    Ahsante.

    Hassan M Khamis

    Mwenyekiti ZAWA UK