1
KI 214 UFUNDISHAJI KISWAHILI KWA WAGENI
MBINU ZA UFUNDISHAJI KISWAHILI KWA WAGENI
I. Malengo ya ufundishaji lugha kwa wageni
Lengo kubwa ni kwamba ili mwanafunzi aweze kujua lugha hiyo kwa stadi zote za lugha ile.
Stadi za lugha ni 1. Kusikiliza 2.kuzungumza 3. Kusoma 4.kuandika 5. Sarufi 6. Utamaduni
wa lugha ile
Malengo ya jumla ya kufundisha ili ni pamoja na:-
1) Kumwezesha mwanafunzi ili aweze kumudu lugha.
2) Kumwezesha mwanafunzi aweze kuwasiliana na wazawa wa lugha husika
LUGHA YA KWANZA
Stern (1983) anasema kwamba “lugha ya kwanza lugha ambayo mtoto hupata kutoka kwa mama
yake mzazi angali mchanga.
LUGHA YA PILI
Stern (1983) anasema kwamba “ lugha ya pili si lugha ambayo mtoto/mtu aliipata alipoanza
kukua na kupata lugha. Hii ni lugha ya kujifunza,kwa maana ya kwamba mtu huyu huwa tayari
ana lugha nyingine.mfano. hapa Tanzania Kiswahili ni lugha ya pili kwa watu wengi
LUGHA YA KIGENI
Ni ile lugha ambayo unajifunza na kuitumia lakini wazungumzaji wake wako nje ya nchi au
mbali na jamii anapokaa mwanafunzi huyo. Mfn lugha ya kiingereza ni lugha ya kigeni hapa
Tanzania
MALENGO YA JUMLA YA UJIFUNZAJI NA UFUNDISHAJI WA LUGHA YA
KIGENI
Mara nyingi hii hutegemea taaasisi yenyewe lakini kuna malengo ambayo ni ya jumla:
1) Kutaka kuwasiliana na wenyeji wa sehemu /nchi husika
2) Kujiandaa kusafiri kwenda nchi nyingine kwa shughuli mbalimbali
3) Kwa ajili ya kufanya biashara
4) Kukidhi vigezo vya masomo
5) Kufanya utafiti katika taaluma husika
6) Ili kupata ajira nchi za ng‟ambo
KITU GANI KIANZE KUFUNDISHWA SASA?
Onyo: usijaribu kumfundisha mwanafunzi sarufi za lugha hiyo kwanza, utamfundisha ikibidi
lakini isiwe kipaumbele chako
Anza na salamu za kawaida, salamu katika utamaduni wa mwafrika ni kitu cha
muhimu sana, hivyo fundisha salamu,maana lengo ni kwamba huyo mtu aweze
kuwasiliana.
2
MALENGO YA UJUMLA YA UFUNDISHAJI LUGHA YA KISWAHILI KWA
WAGENI
a) Ili mwanafunzi wa Kiswahili ajue mambo yafuatayo:
i. Aweze kumudu lugha ya Kiswahili
ii. Aweze kuwasiliana na watumiaji wa lugha ya Kiswahili
iii. Ili wanafunzi waweze kung‟amua mambo yafuatayo:- Namna ya kusema jambo
gani? Mfano anataka kwenda chooni Asemee wapi? Kwa nini aseme? Kwa nani
aseme? Mazingira gani aseme?
iv. Ili kuwapa wanafunzi mbinu mbalimbali za kujifunza lugha ya Kiswahili.
Wanafunzi wafanye kwa vitendo ili waweze kujichukulia misamiati ya kutosha
v. Wanafunzi wang‟amue umuhimu wa lugha wanayojifunza
b) ili wanafunzi waweze kutimiza malengo haya, mwalimu ni lazima wape wanafunzi:
kuchunguzakugunduakutalii kuhusu lugha ya Kiswahili
c) wape uwezo wa kukuza lugha ya Kiswahili kila siku aweze kuongeza msamiati kwa
kusoma vitabu mbalimbali vya hadithi
d) wape nafasi kutumia mbinu mbalimbali lugha ili kukuza uelewa wao
e) wape uwezo wa kukuza fikra zao na kudadisi
f) wasaidie kufanya utumbuizi wa vipengele vya mfumo na utamaduni wa lugha ya
Kiswahili
NADHARIA KUU ZA UJIFUNZAJI LUGHA
Kuna mambo mawili ambayo waalimu tarajili wanapaswa kujua
1) mbinu za kujifunza lugha ya pili ni nyingi kama ilivyo waalimu wengi
2) manzingira halishi wakati wa ujifunzaji. Rogers (2001) anasema kwamba “ wakati
wa ufundishaji wa lugha ya kigeni hutumia mbinu mbalimbali kwa ajili ya
kuwasaidia wanafunzi wafikie malengo yao”
kuna nadharia kuu nne (4)za ujifunzaji lugha:
1) NADHARIA YA UHULKA
Mwasisi wake ni Noamy Chomsky (1957)
Wazo kuu lake ni kwamba: binadamu huzaliwa akiwa na uwezo lugha. Yaani kwenye
ubongo wake ana mfumo ambao huzaliwa nao kwa ajili ya kujifunza lugha. Ana kifaa
kinachoitwa LAD (Kifaa cha upataji lugha)
Naye Brown (2000) aliunga mkono mawazo haya. Mwingine aliyeunga mkono ni
Ellis (1997) walikuwa na hoja kwamba kuna kipindi mtu akifikia umri Fulani
hawezi kupata lugha sawasawa na wazawa wa lugha husika. Umri huo ni kuanzia
0-miezi 18. Kwa mujibu wa wataalamu hawa mazingira hayana msaada wowote
katika ujifunzaji lugha.
2) NADHARIA YA UTABIA (BEHAVIORISM)
Mwasisi wa nadharia hii ni J.B Watson. Wengine wanaoshadidia nadharia hii ni
Leornald Bloomfied, O.N Mowrer, B.F Skinner na A.W Staats
Edward Thorndike (1935) alikuwa wa kwanza kabisa kutafiti zaidi. Kwa mujibu
wa wanatabia ujifunzaji wa lugha ni mwigo kwa maana ya kwamba huiga kile
kinachosemwa na watu wanaomzunguka
3
Aliyetafiti zaidi katika nadharia ya ujifunzaji ni Burrhus Frederic (B.F) skinner ,
Huyu alikubali ni mwigo lakini akaongeza kuwa ni uimarikaji wa tabia, hivyo
mtoto mdogo hazaliwi na lugha bali huichota kutoka kwa wazazi wake
Wilga Rivers (1968)anasema mtoto hujifunza kupitia kujaribu na kukosea “trial
and error’ huendelea kufanya hivyo mpaka anapofikia matamshi ya jamii nzima.
Nadharia hii inayapa mazingira nafasi kubwa katika ujifunzaji lugha
Je mtu akitengwa na jamii anaweza kuwa na lugha?
3) NADHARIA YA UTAMBUZI
Nadharia hii iliasisiwa na Jean Piaget (1954)
Alidai kuwa binadamu anapozaliwa kuna kipindi maalum cha kupata lugha
Alidai kuwa kujifunza lugha ni sehemu ya makuzi ya binadamu, kwa kadiri
unavyokua ndivyo unavyozidi kupata lugha
Alidai kuwa mtoto hupata lugha kabla ya kuzaliwa.
Arth(2003) anadai kuwa mtoto hupata lugha kabla ya kuzaliwa,kuanzia 0-miezi
18
Nadharia hii haipingani na umuhimu wa mazingira katika ujifunzaji lugha
4) NADHARIA YA UUMBAJI
Nadharia hii iliasisiwa na Jerome Brunner
Wazo kuu la nadharia hii inasisitiza nafasi ya mama katika upataji lugha ya
kwanza
Mtoto hutengeneza lugha kutegemeana na mawasiliano ambayo mama yake
anayatumia
Alidai, ili mtoto aweze kupata lugha ni lazima mambo yafuatayo yatimizwe
Muktadha
Tajiriba (experience)
Upangilifu (organization)
Kujenga mazingira ya upekuzi (udadisi_
Hukaza zaidi kuhusu mazingira katika ujifunzaji lugha
Mwalimu awatie moyo wanafunzi kugundua mfumo wa lugha wao wenyewe
Mwalimu na wanafunzi wanapaswa kutumia sana majadiliano
NJIA ZA UJIFUNZAJI LUGHA YA KISWAHILI
Njia za ufundishaji Kiswahili ni nyingi kama na waalimu nao walivyo wengi, lakini njia hizi
itatengemea hali ya wanafunzi, hata hivyo njia zifutazo zinapendekezwa zitumike.
1. Njia ya majadiliano-njia hii haifai kwa mwanafunzi ambaye ndio kwa mara ya
kwanza anasikia Kiswahili. Lakini ni njia nzuri kwa mwanafunzi ambaye
amewahi kusikia habari za Kiswahili
2. Njia ya mahojiano. Mfano mwalimu aandae maswali, awaambie wanafunzi
wajipe vyeo mfano mmoja anakuwa daktari mwingine anakuwa mgonjwa n.k
3. Mchezo wa maswali. Kwa mfano. Kama wewe ungekuwa rais wa marekani
ungefanyaje kuhakikisha unakomesha ugaidi duniani? Watajibu na kujipatia
msamiati kibao
4. Njia ya uigizaji-mwli awape wanafunzi mwongozo wa maigizo
4
5. Njia ya maswali ya papo kwa papo (ana kwa ana) mfano: mimi ni Seni, wewe
ni nani?
6. Njia ya uwandani. Mfano ukitaka kuwafundisha misamiati ya sokoi wapeleke
sokoni.
7. Njia ya kutumia mazingira mbalimbali. Mfano kama mwalimu anataka
kuwafundisha michezo wapeleke uwanja wa mpira
8. Njia ya usomaji. Mfano kusoma pande nne za dunia,kuwapa matini mbalimbali
wanafunzi
9. Njia ya majadiliano funge. Yaani wanafunzi wanajadili vitu ambavyo
vimewekewa mipaka
Angalizo:uteuzi wa njia ipi itumike itategemea aina ya wanafunzi na kazi zao!
HULKA/TABIA YA UANAFUNZI KUJIFUNZA LUGHA
Wanafunzi hutofautiana kulingana na hulka zao, mwalimu anahitaji kuangalia mielekeo ya
wanafunzi wake. Baadhi ya tabia zao ni kama vile: ucheshi, hasira, aibu, hasira za kutojua,
hapendi kusahihishwa, mkimya nk
ATHARI ZA KIJAMII KUHUSU LUGHA/WANALUGHA
Kila jamii ina mtazamo wake kuhusu ujifunzaji lugha, mtazamo hasi ndio ambao huathiri
ujifunzaji lugha na kupelekea kutopata motisha wa kujifunza lugha. Baadhi ya mambo
yanayoathiri ni kama vile
i. Nia au lengo la kujifunza lugha hiyo
ii. Jinsia; inasemekana wanawake wanaweza kupata lugha kuliko wanaume
iii. Umri; umri mdogo ni rahisi kupata lugha kuliko umri mdogo
iv. Mazingira; mazingira mazuri yanavutia mwanafunzi kujifunza haraka
v. Umilisi wa lugha kama akiwa na umilisi mdogo
Malengo ya mwalimu ni kuhakikisha anafanya mambo yafuatayo:
i. Kuwatia motisha wa kujifunza lugha
ii. Kumsaidia kuondokana na hasira
iii. Kuondoa dhana potofu ya ujifunzaji lugha. Mf. Kuna wanaoamini kwamba
Kiswahili ni lugha ya kiislamu
iv. Kuondoa utata katika vipengele vya kisarufi
v. Kuwaelezea aina mbalimbail za lugha na mahali zinapotumika
Kuhusu matumizi ya lugha ya ishara ni muhimu sana kujua ishara zinazotumika katika jamii.
Hivyo mwalimu anapaswa awaeleze mambo yafuatayo;
i. Baadhi ya utamaduni huangalia usoni, tabasamu na kujiamini
ii. Matumizi ya mkono wa kushoto au wa kulia
iii. Kuonyesha vidole-jamii zingine haziruhusu kabisa
iv. Namna ya kusimama na kuelezea jambo
Ili kutimiza hayo yote mwalimu lazima awe na sifa zifuatazo:
i. Awe muwasilishaji mzuri
5
ii. Awe na mpangilio mzuri
iii. Awe mstahimilivu
iv. Awe na ujuzi wa kufundisha
v. Awe na uhusiano mzuri na wanafunzi
vi. Awe na maarifa ya somo
SIFA ZA MJIFUNZAJI LUGHA
a) Awe na utayari wa kujifunza lugha ya Kiswahili bila kulazimishwa
b) Afanye mazoezi ya kuitumia lugha hiyo
c) Atumie akili kupambanua dhana mbalimbali ili kugundua mambo ambayo jamii
Fulani inayafanya
d) Awe na uhuru wa kuzungumza lugha hiyo
e) Awe na ratiba ya kujifuza
f) Aweze kulinganua na kulinganisha lugha anayojifunza
g) Awe na ukarimu ili aweze kuwa na uhusiano na jamii husika
h) Awe mtendaji
i) Azingatie ubora ili aweze kujifunza zaidi
MOTISHA
Ni tabia au msukumo katika kutimiza malengo fulani. TUKI (2004) wanadai kuwa motisha ni
kitu kama fedha inayotolewa ili kumtia mtu hamasa kujifunza jambo.
Hata hivyo, si lazima umpe kitu bali unamtia moyo mwanafunzi na kumsaidia. Mwalimu
anapaswa kutumia motisha chanya sio hasi. Mfn hutakiwi kuchapa fimbo
Brown (1994) anasema kuwa motisha;
a) Ni kiwango cha uchaguzi ambacho unafanya kuhusu lengo unalotaka kufikia
b) Jitihada atumiazo mtu kufikia malengo hayo
SKINNER &WATTSON-hawa wanaangalia zawadi na uhimizaji kwa wanafunzi
pamoja na adhabu ili kufifisha na kujenga hali fulani
AINA ZA MOTISHA
1. Mwamko wa mjifunzaji mwanyewe
2. Mazingira mazuri ya kufundishia Kiswahili mfano, darasa, nje n.k
3. Jamii inayomzunguka ni motisha pia
4. Mwalimu anaweza kuwa motisha kwa mwanafunzi
5. Zana/vifaa vya kujifunzia pia ni motisha
MOTISHA IPO KATIKA MAKUNDI MIWILI
1. Motisha wa ndani-
Haitegemei vitu vya nje ya yenyewe
Hiki ni kile kinachoonekana kwa mjifunzaji lugha mwenyewe
Hii haibadiliki kulingana na muktadha wowote ule
2. Motisha wa nje
Ni aina ya motisha ambayo mwanafunzi hutegema kupewa, kupata, kusikia au kuona
6
Hivi vitamsaidia katika kujifunza lugha
Mwalimu wasaidie wanafunzi kutumia lugha kulingana na muktadha. Hapa kuna
mambo ya kuzingatia:-
a) Akili ya mwanafunzi: lazima utambue tofauti zao katika akili zao ili kujifunza lugha
b) Kipaji chao-kuna wengine wana vipaji vya kujifunza lugha
c) Umri-watu wazima huchelewa kujifunza lugha
d) Jinsia-inasemekana wanawake wanaweza kupata lugha haraka kuliko wanaume
UFUNDISHAJI LUGHA KIMAWASILIANO
Ni muhimu kuhakikisha kwamba katika kujifunza lugha ufundishaji uwe wa mawasiliano
Ni mbinu ya kufundisha lugha ngeni na lugha ya pili
Husisitiza mwingiliano maathiriano kama mbinu ya kujifunza lugha
KAZI ZA LUGHA
Van (1975) anasema kuwa kazi ya lugha ni:
a) Kutoa habari
Kusimulia
Kuuliza
Kutoa taarifa
b) Kutafuta taarifa za kitaaluma
c) Kuelezea mihemuko na misisimko. Mfno mapenzi, misisimko
d) Kuelezea masuala ya uadilifu.mfn kuomba msamaha, ibada etc
e) Kwenye mambo ya ushirikiano. Mfn kuamkia watu, kujitambulisha nk
Angalizo: hata kama mwanafunzi ana malengo mengine ya kujifunza lugha hiyo ni
lazima umfundishe umuhimu wa lugha hiyo kulingana na muktadha
MASHARTI YA KUZINGATIA
a) Azingatie majukumu ya kijamii mfn ataanzaje kuzungumza na mtu
asiyemjua? Watu wengine ni wenye mamlaka Fulani, hivyo kuna namna ya
kuzungumza nao
b) Majukumu ya kisaikolojia-mfano asipendelee upande wowote mfn
CHADEMA CUF na CCM
c) Mazingira ya lugha ilipo. Je ni lugha ya taifa? Watu wanaokuzunguka
wanatumiaje?
Angalizo: lugha sio sarufi tu au fonolojia bali ni chombo cha mawasiliano, hivyo
inahitaji kufundishwa kimawasiliano zaidi
MUKTADHA WA UFUNDISHAJI LUGHA
Haya ni mazingira halisi ambapo tukio la ufundishaji lugha hufanyika kwa kuzingatia
wadau wakuu watatu
a) Mwanafunzi
b) Mwalimu
7
c) Jamii
Pamoja na motisha ufundishaji uzingatie sana mambo yafuatayo:
Utoaji wa kazi na mazoezi mengi
Tumia lugha katika mazingira halisi na yanayostahili ukilenga kwenye stadi nne
za lugha
Matumizi ya lugha kwa kuzingatia muktadha
Utumizi wa mazingira halisi ya darasa.mfn picha, katuni. Nk
Himiza ushirikiano miongoni mwa wanafunzi baina yao na baina yako mwalimu
Tumia mbinu zaidi ya moja. Mfn vikundi, majibizano nk (rejea mbinu)
Fafanua kwa uangalifu masuala ya kisarufi
Ajue maono ya mwanafunzi. Mfn huzuni, ucheshi nk
Kuunda mazingira ya utani darasani
UFUNDISHAJI WA DARASA MSETO
TUKI (2013) Mseto ni hali ya kuwa na mchanganyiko wa makabila mbalimbali
kutengeneza kitu fulani
Hapa ni mchanganyiko wa darasa lenye wanafunzi wanaotoka sehemu mbalimbali na
wenye umri tofauti, malengo tofauti nk
Hivyo mwalimu inakubidi utofautishe sana katika ufundishaji wako na uwe makini ili
usije ukawakwaza wanafunzi wengine
NAMNA YA UFUNDISHAJI DARASA MSETO
a) Lazima mwalimu uwe na maarifa ya wanajamii mfn utamaduni wao. Kama ni wazungu,
wachina nk jua utamaduni wao
b) Uwe na usisitizaji wa lugha lengwa. Kama ni Kiswahili basi pendelea kutumia Kiswahili
ili usiwakwaze sana. Hata hivyo lazima wawe na lugha ambayo wewe unaijua
c) Tumia vitendo halisi, ishara nk
d) Arika wageni mbalimbali waje waeleze kuhusu lugha na mazingira
e) Puuza(ignore) malengo ya wanafunzi
f) Ufundishaji wa masuala ya utamaduni lazima ufungamane na muktadha husika
SIFA ZA MPATAJI LUGHA
Mpataji lugha ni lazima awe na sifa kuu mbili tu:
1. Umilisi wa kiisimu
Ni uwezo alio nao mjifunzaji lugha ambao unamwezesha kutofautisha viambo,
miundo tofauti ya lugha na msamiati wa lugha
pia kuweza kutamka lugha ile.
2. Umilisi wa kiisimujamii
Ni umilisi ambao mtumiaji wa lugha hupata lugha inayomwezesha kujifunza lugha na
kuzingatia muktadha
NADHARIA /MBINU /MIKABALA ZA KUJIFUNZA LUGHA YA KIGENI
Nadharia ni mkondo wa mawazo unaotumika kuelezea jambo
8
Mtesigwa(2009) anasema “ nadharia ni kiunzi cha mitazamo, mawazo au vitendo
vinavyohusisha uchunguzi, mpangilio na uchanganuzi wa matukio katika kukabili suala
fulani kisayansi
®kuna mambo mawili ambayo lazima tujikumbushe:
a) Njia za ufundishaji lugha ya kigeni ni nyingi kama waalimu walivyo
wengi
b) Kumbuka hali ya darasa. Tumia njia mbinu zaidi ya moja darasani,
usitumie njia moja tu.
Rogers&Richards (2001)wanasema kuwa tunapojiandaa kwenda kufundisha tunahitaji
kujiuliza maswali yafuatayo:-
a) Malengo ya ufundishaji lugha lengwa(LL) ni yapi? Mfano labda lengo lao
linaweza kuwa wanataka kuzungumza tu.
b) Upi ni msingi asili wa lugha lengwa na unaathiri vipi njia za kufundisha. Mfn
kaida za lugha ya Kiswahili ni zipi?
c) Ni misingi ipi inatumika kuchagua mambo katika ufundishaji lugha?
d) Ni misingi ipi ya upangiliaji wa mada. Mfano kwa kuzingatia suala la utamaduni,
mfano salamu nk
e) Je lugha mama ya mwanafunzi ina jukumu gani katika kujifunza lugha? Mfano
miundo ya lugha mama inafanana na lugha lengwa?
f) Je wanafunzi binafsi watumie mbinu zipi katika kujifunza lugha hiyo?
g) Je ni mbinu na vitendo vipi hufanikisha vizuri ujifunzaji lugha ya pili (kigeni)?
1. Mbinu ya tafsiri sauti
2. Mbinu ya moja kwa moja(direct method
3. Mbinu ya usomaji(reading approach method)
4. Kusikia na kusimulia (audiolingual method)
5. Kushirikisha jamii (community language learning method)
6. Mbinu ya ukimya (silence method)
7. Mbinu ya mawasiliano (communicative language approach)
8. Mbinu ya mwitiko jumuishi(total physical response)
9. Mbinu ya utambuzi (communitive code method)
10. Mbinu ya upendekezi (suggestopidia method)
wakati mwingine hujulikana kama mbinu ya kimapokeo. Huu ni mkabala ambao
ufundishaji wa lugha ya kigeni umejiegemeza katika sarufi ya lugha ya Kiratini.
Iliasisiwa/anzishwa na Meidinger (1783) na Ploetz (1849) wakati ule iliaminika kwamba
lugha ya kiratini ndiyo lugha pekee.
Nafasi ya lugha mama ilipuuzwa kwa kiasi kikubwa na ilijikita katika sarufi ya Kiratini,
na hivyo mwalimu alipaswa kujikita katika kufundisha sarufi ya Kiratini na vipengele
vingine vilipuuzwa
Huu ulikuwa ni mkabala elekezi-yaani unawaelekeza watu namna ya kutumia lugha na
sivyo wanajamii wanavyotumia lugha hiyo
9
Iliasisiwa na Gouin(1880)
Nadharia hii inazingatia uzungumzaji wa lugha husika
Mbinu zilizopaswa kufundishia ni zile zilizohamasisha wanafunzi kuzungumza. Mfn
mbinu ya majadiliano,uigizaji,maswali katika vikundi
Masomo yalianza kwa hadithi fupi halafu wanafunzi wanauliza maswali kuhusu hadithi
waliyosimuliwa na mwalimu aliwaambia watoe maoni yao kuhusu hadithi hiyo.
Matumizi ya vielelezo vilitumika zaidi. Mfano picha, ramani, katuni n.k
Kipengele vya sarufi kilifungushwa kwa kufuata muktadha halisi ambamo lugha
inatumika
Kipengele cha utamaduni kilifundishwa kwa uchache sana
Mbinu hii inatumika kufundishia kwa wanafunzi wanaojifunza lugha ya
kigeni ambao hawatarajiwi kutoka nje ya nchi ambapo lugha hiyo
inatumika
Malengo yake huwa kuendeleza uwezo wao wa kusoma ile lugha
Vipengele vinavyofundishwa ni vile vinavyohusu usomaji, hivyo
vipengele vingine havihusiki. Mkazo wake ni kwamba anayejifunza lugha
aweze kusoma vitu vingi kwa wakati mmoja.
Mbinu hii haimpi mjifunzaji lugha uwezo wa kuzungumza lugha husika
bali ni kuisoma tu.
4.
Nadharia hii ilitokana na haja ya ukarimani nchini marekani miaka 1940.
Iliasisiwa na Bloomfield (1942) na Fries (1945)
Msingi mkubwa wa nadharia hii ni kile kinachosemwa
Maandishi hayakupewa fursa kubwa bali kile kilichosemwa ndicho
kilikuwa cha muhimu sana. Bloomfield alisema kuwa lugha si katika
maandishi bali ni kile ambacho kinasemwa.
Inahusisha kusimulia mada mbalimbali na kupima uwezo wa kusikia
Walipenda sana kutumia miziki, nyimbo, usimulizi na ughanaji
Walisisitiza stadi ya kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika
Waliongeza kitu kingine cha kuona
Iliasisiwa na curran (1976)
Dai la nadharia hii ni lugha ni watu, kwa maana ya kwamba huwezi
kutenga jamii na lugha
Walidai kwamba ili uweze kumfundisha mwanafunzi mgeni basi nenda
kwenye jamii husika
Walidai pia kwamba kama utaamua kufundishia darasani bali darasa lako
lifanye angalau lifanane fanane na jamii ya lugha husika
Ili uweze kufundisha watu ni lazima ushirikishe watu wanaotumia lugha
hiyo.
10
Mwanafunzi atapata vichocheo vya aina nyingi katika jamii na kubaini ni
mambo gani yanafaa na mambo gani hayafai
Nadharia hii inaipa kipaumbele jamii kama chombo muhimu katika
kujifunza lugha
Nadharia hii inaamini kwamba kila lugha ina mfumo wake tofauti na
lugha nyingine, hivyo ufundishaji wa lugha ya pili ulenge kumfanya
mjifunzaji wa lugha kuwa mmilisi au kukaribia kuwa mmilisi wa lugha
anayojifunza
Nadharia hii inadai kwamba ujifunzaji wa aina yoyote ile unahusisha vitu
viwili.
Kichocheo Mwitikio mgeuko
(Mwalimu) (mwanafunzi)-(anabadilika)
Ili kuweza kutimiza hili, mwalimu anahitaji kujenga mazingira ya utani
katika darasa jambo ambalo litaleta matokeo mazuri ya umilisi wa lugha
husika
Nadharia hii inamhitaji mwalimu kufanya tathimini kwa wanafunzi
wake ili kubaini kama kuna badiliko
Nadharia hii inatokana na ukosoaji/udhaifu wa nadharia ya mbinu ya
sarufi na ile ya moja kwa moja
Ilianzishwa mwaka 1970
Wanadai kwamba mwanafunzi apewe vipengele vyote vya lugha kwa
ujumla mwanafunzi kumpa maarifa mapana kuhusu lugha, kumpakanuni
za msingi kuhusu lugha, halafu yeye mwenyewe kulingana na utambuzi
wake aweze kuielewa lugha.
Uwafundishe kanunu za msingi. Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili ni
lazima ujue ngeli za majina-hii itakusaidia kutumia nomino katika
mazingira tofauti tofauti, vitenzi-waeleze namna ambavyo vinaweza kukaa
peke yake kama sentensi
Nadharia hii pia hujulikana kama mkabala asilia.
Iliasisiwa na James Asher 1969
Inatilia mkazo mfumo na muundo wa lugha.
Kama ilivyo nadharia ya usikizi nadharia hii pia inasisitiza umuhimu wa kumudu
mazungumzo kama sehemu ya umilisi wa lugha
Ufundishaji uhusishe mazoezi ya kurudia rudia ambayo angalau unamfanya mwanafunzi
kumudu anachojifunza
Nadharia hii inasisitiza matumizi ya vitendo na ishara mbalimbali kama nyenzo mojawapo
katika kujifunza lugha.
Ilianzishwa na Lonzano georgi (1979)
11
Nadharia hii inayapa mazingira bora ya ujifunzaji lugha kama nyenzo muhimu mojawapo
katika kujifunza lugha. Hii inamaanisha kwamba mazingira yanayotumika kujifunzia
lugha ni lazima yamkumbushe mwanafunzi kile alichojifunza jana yake
Wanaelezea namna ya mkao wakati wa kufundisha wanafunzi wageni. Mkao katika darasa
uwe ni wa kutazamana, maana yake vikae kwa duara.
Wanasisitiza matumizi ya mziki laini na mziki nyororo
Inasisitiza maingiliano na maathiriano katika ya mwalimu, mwanafunzi na jamii
Wanakaza kwamba kujifunza lugha ni kujifunza kuwasiliana.
Kujua lugha kwa hakika sio kujua kanuni za lugha ile bali ni kujua namna ya kuwasiliana
na watu wa jamii ile kwa kuzingatia mikitadha mbalimbali ambamo lugha hiyo inatumika
Ni nadharia ambayo imeshaididiwa na wataalam wengi akiwamo Noamy Chomsky
Hii ndiyo nadharia ambayo inafaa kutumia kwa ajili ya kujifunza lugha
Hapa inamaanisha uwezo alio nao mtu wa kutumia lugha Fulani.
Viwango hivi viliwekwa na shirika/taasisi moja isiyokuwa ya kibiashara wala kiserikali
liitwalo Interagence Language Round Table (ILRT)
Kulingana na shirika hili wajifunzaji lugha wako katika viwango vitatu
a) Wanafunzi wa daraja la msingi (Kisw.DAMSA) Beginners Level
b) Wanafunzi wa daraja la kati (DAKATI)Intermediate Level
c) Wanafunzi wa daraja la juu (DAJUU) Advanced Level
a) Wanafunzi wa daraja la msingi (Kisw.DAMSA) Beginners Level
Daraja limegawanyika katika viwango hivi
Kiwango cha 0-mwanafunzi hawezi kabisa kuzungumza lugha
Kiwango cha +0-mwanafunzi amekaririshwa tu mahitaji muhimu
akibadilishiwa tu basi Amepotea
Kiwango cha 1-mwanafunzi anaweza kusitahimili mazungumzo ya ana kwa ana ila hawezi
kuanzisha mazungumzo
Kiwango cha +1-huyu anaweza kuanzisha mazungumzo yeye mwenyewe, hata hivyo ni
kwa ajili ya kukidhi matarajio yake
b) Wanafunzi wa daraja la kati (DAKATI)Intermediate Level
Daraja la 2-lugha si kamilifu lakini anaeleweka kwa urahisi
Kiwango cha 3-anaweza kuzungumza lugha kwa muundo sahihi, ana msamiati wa mazingira
fulani fulani tu ili kukidhi mahitaji ya kitaaluma
Anaweza kukithi mahitaji ya kitaaluma
2+Lugha yake si kamilifu lakini anaweza kueleweka kwa urahisi
3mwanafunzi ana uwezo wa kuzungumza lugha kwa usahihi, ana msamiati toshelevu kwa
mazingira fulani fulani tu.
3+mwanafunzi ana uwezo wa kuzungumza lugha kwa muundo sahihi na ana uwezo wa
kukidhi mahitaji ya kitaaluma
4mwanafunzi ana uwezo wa kutumia lugha kwa usahihi na ufasaha katika viwango vyote
vya lugha. Yaani fonolojia-matamshi, sintakisia-miundo, mofolojia-maumbo
12
Huweza kutoa maana ya viambo mbalimbali kulingana na muktadha
4+uwezo wa mzungumzaji wa kiwango cha juu kabisa katika mawanda yote lugha: yaani
fasihi na isimu
Ana uwezo wa kutumia kwa kuzingatia utamaduni wa lugha husika
Anaelekea kulingana na wazawa wa lugha husika
5usitadi wa lugha alio nao ni wa kiwango cha mmilisi wa lugha aliyeboboea
Ana sifa za kudhihilisha wakati wa lugha anayojifunza.
Suala la uteuzi wa vitabu vya kufundishia lina ugumu unaotokana na mambo yafuatayo:
Yaani malengo tofauti ya:
Malengo tofauti ya wanafunzi
Malengo tofauti ya taasisi
Malengo tofauti ya waajiri
Malengo tofauti ya waalimu
Malengo tofauti ya wazazi/walezi
Tutafafanua utofauti huo kwa namna ifuatayo:
Malengo tofauti ya mwanafunzi:-mfano viwango tofauti vya wanafunzi
kitabia, kiuchumi, kiuelewa, kiutamaduni,kiumilisi
viwango tofauti za wanafunzi mfano kiwango cha kati,juu nk
tofauti za kimaamzi. Mfano taasisi moja tu ihusike katika uandaaji wa vitabu vya
kufundishia mfano wizara ya elimu
uzingatizi tofauti wa vitabu. Mfano,bei, mwonekano, upatikanaji wake
Malengo ya kozi inabidi yaangaliwe
Wanafunzi walengwa ni akina nani?
Mkabala utakaotumia kufundishia
Stadi za lugha. Je kitabu kimekidhi stadi zote za lugha?
Ubora wa mazoezi yaliyotolewa ndani ya kitabu
Mfuatano wa masomo/mada. Ngumu? rahisi? Nk
Msamiati
Hali ya jumla ya kiisimu jamii. Je kitabu kimetumia lahaja, lugha rasmi, vigezo vya
kiutamaduni
Muundo mzima wa kitabu. Chapa yake ni ndogo au kubwa?
a) Kila somo/kitabu kiwe na lengo mahususi la kumsaidia mwanafunzi kuwasiliana
b) Kila kitabu kiwe na matini ya lugha kama izungumzwayo na wazawa
c) Kila kitabu kiwe na kielelezo cha mazingira halisi. Mfano salamu
d) Msamiati na sarufi ukidhi matakwa ya wanafunzi
13
e) Utumizi wa vilelezo halisi kama vile picha,magazeti, tangazo, kadi nk
f) Kila kitabu lazima kiorodheshe sauti zilizo katika lugha husika ili aweze
kuzielewa.
UCHAMBUZI WA DOSARI
Maana yake:
Uchambuzi wa dosari ni njia ya kuainisha, kupambanua na kufafanua dosari mbalimbali
za wajifunzaji wa lugha ya kigeni/lugha ya pili
Suala la uchambuzi wa dosari liliasisiwa na Corder (1967) ambapo yeye anaeleza maana
ya dosari kuwa ni ukiukwaji wa kanuni na taratibu za lugha lengwa
Mambo yanayoshughulikiwa na wanausasanyuzi; wanashughulikia mambo makuu
manne
a) Jinsi mjifunzaji anavyoilewa lugha ya kigeni anayojifunza
b) Jinsi mjifunzaji anavyojifunza lugha ya kigeni/mbinu anazotumia
c) Matatizo anayokabiliana nayo wakati anajifunza lugha ya kigeni
d) Kung‟amua mchakato/kutambua michakato inayotumiwa katika kujifunza lugha
ya kigeni
UMUHIMU WA DOSARI/DHIMA YA DOSARI KWA WAJIFUNZAJI
LUGHA YA PILI
Dosari zinazofanywa na wanafunzi wanaojifunza lugha ya kigeni hutumiwa kama kioo
kinachoakisi hali halisi iliyofikiwa na wajipatiaji wa lugha ya pili.
Dosari hizi humpatia mwalimu nafasi ya kutathimini jitihada zilizofikiwa na wanafunzi
wake kwa minajili ya kuboresha au kuendeleza mbinu za ujifunzaji lugha na humsaidia
mwalimu kubadilisha vifaa anavyotumia katika ufundishaji.
Kwa ujumla umuhimu wa dosari unaangaliwa katika namna kuu nne
a) Kwa upande wa mwalimu
Huonyesha jitihada zilizofikiwa na wanafunzi na kusaidia kuboresha
b) Kwa watafiti
Huonyesha jinsi lugha inavyopatikana/inavyoamiliwa
c) Kwa mwanafunzi
Humsaidia mwanafunzi kujua ruwaza/partern ya maendeleo ya
mwanafunzi alipofikia
d) Kwa waandaa mitalaa
Huwasaidia kuboresha uandaaji wa vitabu na machapisho mbalimbali kwa
kujifunza
AINA ZA DOSARI
Aina hizi za dosari zimeainishwa kutokana na mbinu wanazotumia wanafunzi kujifunza lugha.
1. Dosari majumui/majumuisho
Hizi ni dosari ambazo mwanafunzi hutumia kanuni ya jumla ya lugha ya kwanza na
kuitumia katika lugha ya pili. Hii inasabisha kukiuka matumizi ya lugha lengwa.
Mfano katika lugha ya kiingereza vitenzi vingi huongeza “ed” mwanafunzi wa
14
mswahili wa kiingereza anaweza kupata shida kwani anaweza kuwa anaongeza ed
katika kila kitenzi jambo ambalo sio sahihi.
2. Uepukaji/avoidance
Ni ule utaratibu wa mjifunzaji lugha ya kigeni kujaribu kuepuka matumizi ya
kanuni/maumbo/miundo fulani ya lugha. Kwa mfano mwanafunzi anajaribu
kuepuka matumizi ya neno fulani anatajaribu kuliepuka hilo neno na kutumia neno
lingine jambo ambalo litasababisha makosa.
Hata hivyo si rahisi kujua kama mtu fulani amekwepa matumizi ya neno fulani
3. Urahisishaji
Mwanafunzi anapoamua kurahisisha muundo wa lugha fulani hujikuta katika
dosari
4. Uhawilishaji
Uhamishaji wa miundo na kaida za lugha ya kwanza kwenda lugha ya pili.
Miundo hii inapohamishwa basi hukiuka miundo ya lugha ya pili.
Kwa mfano baadhi ya jamii ya watanzania hukiuka sana kanuni za Kiswahili.
Mfano Wanyakyusa wa hawawezi kusema “chama” bali “kyama” pia Wakinga
hawawezi kusema “viatu” bali wanasema “fyatu”
5. Utumizi ziada/over use
Ni kuongeza matumizi yasiyohitajika katika utumizi wa lugha
MISINGI YA UAINISHAJI WA DOSARI
Hapa ni kwa kuzingatia Nyanja kuu za lugha:
a) Dosari za kifonolojia/ukiushi wa matamshi-lugha zingine zina toni zingine hazina.
b) Dosari ya kimaumbo/kimsamiati-yaani upangaliaji wa vipashio vinavyounda maneno.
Mfano uwingi wa nomino za kiingereza hupachikwa mwisho tofauti kabisa na lugha
ya Kiswahili ambapo haitabiliki. Mfano pia katika lugha ya Kiswahili neno moja
linaweza kuwa na sifa ya kuwa sentensi, mfano “ninasoma” jambo ambalo kwa
kiingereza haiwezekani kuwa neno moja “ I read”
c) Dosari za kimuundo-taratibu tofauti tofauti zinazotumika kuunda vipashio. Kila lugha
ina utaratibu wake. Mfano. My brother-yangu kaka-mfumo huo hauwezekani kuwa
sawa
d) dosari za kimaana/kisemantiki- maana huwa ni tofauti tofauti
e) Dosari za kipragmatiki-hii ni miktadha mbalimbali mfano sokoni, kanisani
dosari kulingana na athari za kimawasiliano
Ni uainishaji wa dosari kulingana na uelewekaji/kutokueleweka kwa ujumbe
uliotolewa na mjifunzaji lugha. Kwa kuzingatia kigezo hiki tunapata aina mbili za
dosari.
1. Dosari za kimalimwengu/global errors-ni dosari ambazo zinafanya usemi
uliotolewa na mjifunzaji lugha kutoeleweka kabisa
2. Dosari za kienyeji/local errors-ni semi zinazotolewa na mjifunzaji wa lugha ya
pili ambazo haziko sahihi lakini zinaeleweka na msikilizaji. Mfano “I angry”
mfano mwingine ni “ninataka kura”-akiwa jikoni au akiwa katika jukwaa
anasema “ninataka kula”- hizi zinaeleweka na wasikilizaji japo haziko sahihi.
USHUGHULIKIAJI WA DOSARI ZA WANAFUNZI
15
Kila mwanafunzi wa lugha ya pili huwa ana dosari katika kujifunza lugha ya pili. Ni
jambo la msingi kushughulikia dosari za wanafunzi, lakini angalia ni wakati gani
ushughulikie dosari hizo, hii ni kulingana na muktadha wa darasa: aina ya wanafunzi;
haiba yao, mihemko, aina ya dosari, umri n.k. Hata hivyo ikiwezekana dosari hizo ziweze
kushughulikiwa ili kusaidia zisijirudie rudie.
Wataalamu wengine wanaona kwamba dosari zisishughulikiwe. Mfano Krashen na
Terrell(1983) husema kuwa mwanafunzi aachwe mwenyewe atazidi kugundua dosari
hizo na atashughulikia mwenyewe.
Kathleen Bailey (1985)anapendekeza uamuzi wa aina saba
a) Puuza dosari hizo
b) Dosari zishughulikiwe papo kwa papo
c) Kuhusisha wengine katika kurekebisha dosari hizo. Mfano miongoni mwa wanafunzi hao
hao unaweza kuhusisha na wakakosoana wenyewe
d) Kuhusisha wanafunzi mahususi-yaani kumtumia mwanafunzi wa karibu na mwenzake
kumsahihisha mwingine.
e) Kumrudia mfanyaji dosari/ mfano unaweza kumwambia “unaweza kufikiri zaidi juu ya
hilo?”
f) Kuwaruhusu wanafunzi wengine kutoa tathmini.
g) Kumpa nafasi ya kujaribu tena na tena mfanyaji wa dosari baada ya vitendo fulani
kufanyika ndani ya darasa.
Mwisho wa yote lazima vitu vifuatavyo viwe vimejitokeza:-
1. Usahihi na uhalali wa dosari uwe umedhihilika
2. Sehemu na mahali dosari imefanyika iwe imebainishwa wazi wazi. Mfano kama ni
kwenye neno, tungo nk
3. Nafasi ya kurudia na kujirekebisha kwa mfanyaji dosari iwe imetolewa
4. Mifano mbalimbali ya dosari na usahihi wa semi uwe umetolewa na kuonyeshwa kwa
uwazi
5. Aina ya dosari iwe imeonyeshwa. Mfano kama ni dosari ya kimpangilio, kimatamshi nk
6. Marekebisho yawe yamefanywa kwa mifano anuai
7. Mhusika awe amesifiwa/kama ameepuka hizo dosari
MAMBO YANAYOATHIRI UJIFUNZAJI/UPATAJI LUGHA YA PILI/KIGENI
Mambo hayo ni yale ama yanayomwezesha au yanamkwamisha mpataji lugha kupata lugha.
Tutaangalia kwa mujibu wa Martland (1997)
1. Umri
Mtu mwenye umri mdogo ana ahueni zaidi katika kujifunza lugha kuliko mtu ambaye
umri umeenda. Mtoto ambaye hajabalehe mfano miaka kabla ya tisa (9). Hii inatokana
na kwamba mtu mzima tayari anakuwa na lugha nyingine ambayo inasigana na lugha
anayojifunza
2. Hali ya kiuchumi ya mjifunzaji lugha:
Mtu wa tabaka la chini hawezi kutumia vitu vya kisasa ili kupata lugha, maana vifaa
hivyo ni vya gharama kubwa.
16
3. Hali ya darasa:
Darasa ambalo limejengewa mazingira ya utani, wanafunzi wanamudu haraka sana
kupata lugha.
Hii inajumuisha michezo mbalimbali katika darasa hilo
4. Msaada wa kifamilia/community support:
Ikiwa mwanafunzi lugha anayojifunza inatumika ndani ya jamii hiyo, atapata haraka
sana lugha kuliko mwanafunzi ambaye anajifunza lugha ambayo wazungumzaji wake
hawako hapo.
Mfano: Mtanzania anayetaka kujifunza kiingereza anapata shida kwa sababu
wazungumzaji wake wako nje ya nchi
5. Motisha:
Motisha ni kipengele muhimu sana katika ujifunzaji lugha
Mwanafunzi aliye na motisha ya ndani atapata lugha haraka kuliko anayepata motisha
ya nje. Ref. motisha
6. Kiwango cha elimu:
Mtu mwenye kiwango kikubwa cha elimu ana uwezo mkubwa sana wa kupata lugha
kuliko mtu ambaye hana elimu kabisa.
7. Matarajio:
Kama mjifunzaji lugha ana lengo la kufanya utafiti sehemu fulani, matarajio yake ni
kujifunza lugha na kuimudu ili akafanye kazi yake.
Kama mwanafunzi hana matarajio yoyote basi itakuwa ngumu kupata lugha.
8. Haiba
Wanafunzi wacheshi hupata lugha haraka kuliko wanafunzi ambao sio wacheshi.
Wachesi hupenda kujichanganya sana.
9. Mtazamo wa utamaduni wa ujifunzaji lugha ya kigeni/pili.
Mwanafunzi kama ana mtazamo hasi na lugha anayojifunza basi itakuwa ngumu sana
kupata lugha.
Mtazamo chanya ndio utakaomsaidia mjifunzaji lugha kupata lugha.
10. Uwezo wa kumudu lugha ya kwanza:
Uwezo wa lugha ya kwanza una kawaida ya kuathiri umuduji wa lugha ya pili, hasa
inapotokea kwamba lugha ya kwanza ni tofauti kabisa na mfumo wa lugha ya pili.
(Nozalle (2012) 11. Viigwa (role models in the community)
Hii ni kwamba kuna mtu gani katika jamii ambaye ni mtu maarufu unataka uzungumze
kama yeye? Hii itakusaidia kwa sababu mjifunzaji lugha atajaribu kujitahidi
azungumze kama mtu huyo.
12. Muktadha/mazingira
Mazingira ni muhimu katika upataji lugha
TOFAUTI ZA UPATAJI WA LUGHA YA KWANZA NA LUGHA YA PILI/KIGENI
Kuna tofauti kubwa kati ya upataji wa lugha ya kwanza na lugha ya pili. Kila mtu ana lugha ya
kwanza. Wataalam wanaokuwepo hapa kushadidia hili ni Ellis (1994) na Bley Vroman (1988)
Hawa wanabainisha hoja tisa, kama ifuatavyo:
17
1. Mafanikio kwa ujumla: mtoto anapopata lugha ya kwanza huipata lugha ile kwa usahihi
katika Nyanja zote, japo anaweza asiweze kutofautisha uchambuzi kiisimu lakini
wapataji lugha ya pili hupata mafaniko katika maeneo fulani fulani tu katika lugha
wajifunzayo.
2. Kushindwa(failure): katika upataji wa lugha ya kwanza kushindwa hakupo labda kama
ana ulemavu fulani lakini kwa wapataji lugha ya pili kushindwa ni jambo la kawaida
3. Utofauti baina ya wajifunzaji/wapataji lugha (variation): wajipatiaji wa lugha ya kwanza
hawana tofauti yoyote katika upataji lugha, yaani wakifikia umri fulani labda kama miaka
3 hivi wote watakuwa wamepata, kama atakuwa hajapata lugha mpaka miaka 9 basi huyo
atakuwa na matatizo (msukuku-kukoma kujifunza lugha (fossilization )lakini lakini
wajifunzaji wa lugha ya pili kuna tofauti kubwa sana, utakuta mwishoni mwa kozi mmoja
amemudu na mwingine bado
4. Malengo/goals: lengo la mjipatiaji lugha ya kwanza ni umili wa lugha hiyo katika
viwango vyote lakini lengo la mjipatiaji lugha ya pili ni kupata maudhui na umilisi
kidogo
5. Usukuku(ukakamaaji): suala la usukuku halipo kwa mtoto anayejipatia lugha ya kwanza
lakini kwa mjipatiaji lugha ya pili hii ni hali ya kawaida kabisa(soma Han1998-2013).
6. Uvumbuzi/ughamuzi: wajipatiaji wa lugha ya kwanza huendelea kujipatia lugha ya
kwanza katika ughamzi bwete (kujisahihisaha dosari pasipo kujua) lakini mpataji lugha
ya pili huwa katika ughamzi tambuzi.
7. Maelekezo/instruction: ujipatiaji wa lugha ya kwanza hauhitaji maelekezo, labda kidogo
kwa ajili ya kuchochea lakini mjipatiaji wa lugha ya pili anahitaji maelekezo ya kina na
sahihi na kwa utaratibu maalumu.
8. Uthibitisho hasi:katika ujipatiaji wa lugha ya kwanza usahihishaji wa dosari haumsaidii
mpataji wa lugha ya kwanza kupata lugha ile lakini katika upataji wa lugha ya pili ni
muhimu kufanya masahihisho ili kumpa mwelekeo sahihi.
9. Athari hisivu (affective factor): mjipatiaji wa lugha ya kwanza hakuna kitu
kinachomwathiri kujipatia lugha ya kwanza, mfano hafikilii kwamba atakosea,
atachekwa bali yeye hutamka tu lakini katika ujipatiaji wa lugha ya pili athari hisivu zina
msaada sana katika kupata lugha. Mfano mwanafunzi mcheshi, hucheka atapata lugha
haraka kuliko mkimya.
10. Muda: mtoto huchukua muda mfupi kati ya miezi 36 anakuwa mmilisi wa lugha lakini
mjipatiaji wa lugha ya pili hutumia muda mrefu sana. Inachukua miaka kama tisa
UTAYARISHAJI WA MBINU ZA UFUNDISHAJI
A. UTAYARISHAJI WA SOMO:
Hapa tunaangalia muundo wa andalio la somo (lesson plan) unahitaji kuangalia mambo haya:
1. Muda
2. Mada
3. Malengo-ie kitu gani kitokee katika somo hilo. Mfano mwisho
wa somo mwanafunzi aweze kutaja aina ya „nomino‟
4. Mazingira/muktadha-darasa, aina ya wanafunzi.
Shajala
Logbook
Mhitasali
18
MUUNDO WA ANDALIO LA SOMO
Andalio la somo linatakiwa kuwa na mambo yafuatayo
1. Malengo ya jumla (main objective)-haya ni mabadiliko ya muda mrefu yanayotakiwa
kutokea kwa muda mrefu. mfanoMwanafunzi aweze kutathimini….mwanafunzi aweze
kufahamu…
Mara nyingi malengo haya hayabadiliki
2. Malengo mahusus/malengo wezeshi
Haya ni malengo ya muda mfupi
Haya ni malengo ambalo ni la kudumu lakini lengo lake ni kusaidia lengo la
jumla
Tofauti kati ya malengo mahusus na malengo ya jumla ni kwamba malengo ya
jumla hayapimiki ilhali malengo mahusus yanaweza kupimika
Malengo mahususi ni mabadiliko ya muda mfupi ilhali malengo ya jumla ni
mabadiliko ya muda mrefu
Mwanafunzi aweze kutaja viungo vya binadamu vilivyo katika
kichwa…mwanafunzi aweze kulinganisha na kulinganua
Mwanafunzi aweze kuonyesha viungo vya mwili..
Kubainisha viungo vya mwili
3. Mada kuu.
Kila unapoenda kufundisha lazima kunakuwa na maada. Mfano wa mada ni Usafiri
wa Anga
4. Mada ndogo:
Kama mada yako itakuwa hapo juu, mfano Usafiri wa Anga, mada ndogo inaweza
kuwa,kuwasili kwa ndege, kukata tiketi, kufika uwanja wa ndege, mahali uwanja
wa ndege ulipo, hali ya miundombinu kwenda uwanja wa ndege nk
Kama ikiwa mada kuu ni familia: basi mada ndogo yaweza kuwa aina za familia
5. Zaka za kufundishia
Hakuna somo lisilo na zana za kufundishia. Mfano kama ni usafiri wa anga.
Unaweza kuchora picha ya mwanza, kuwapa ramani nk.
6. Utaratibu wa somo/yaani darasani
Somo lolote linakuwa na:
a) Utangulizi-tanguliza somo lako, kama sio mara ya kwanza wape chemsha bongo,
kama ni kwa mara ya kwanza unaweza kuanza na hadithi. Hii itakusaidia kuvuta
usikivu wa wanafunzi. Pia unaweza kuwaruhusu wanafunzi wakuulize maswali
kuhusu wanaelewa nini kuhusu kile unachoenda kukifundisha
b) Uwasilishaji wa kiini cha somo:- unaweza kuandaa maswali, unaweza kuandaa
makundi ya wanafunzi wachache wachache.
c) Utumizi/utendaji wa wanafunzi. Hapa mwalimu unategeneza mazoezi, kazi binafsi,
mazoezi mengine ambayo watafanya wenyewe, maswali ya papo kwa papo au
mazungumzo
7. Kazi ya nyumbani
Haifai hata kidogo kuwafundisha wanafunzi wageni kumaliza kuwafundisha na
kuwaacha bila kuwapa zoezi lolote la kufanya
Zoezi hilo lihusishe vile ambavyo mwanfunzi amesoma darasani.
Mfano wa zoezi: Mtafute mtu yeyote kule mitaani muulize maswali haya. Wewe ni
nani, unasoma? Umeoa? Je unapenda nini? Nk
Hii itakusaidia sana kujua wapi palipo na udhaifu ili uwee kuwasaidia wanafunzi
kama hajaelewa.
8. Tathmini/
19
Ni lazima kujitathimini wenyewe kama wameelewa au la.
UONGOZI WA DARASA/UTHIBITI WA DARASA 1. Upangaji wa darasa/ je darasa limepangiliwaje? Je watu wote wako sana?
2. Mbinu za ufundishaji/mbinu zinazopendekezwa ili uweze kulitawala darasa ni mbinu shirikishi.
Usiwe mwongeaje tu wewe mwenyewe. Pia tumia mbinu za kuona.
3. Uimara wa mwalimu/lazima mwalimu ujiamini katika ufundishaji wako. Usionyeshe kuyumba
hata kidogo, kumbuka mara utakapoyumba hawatakuamini tena hata kama ukifundisha vizuri.
Kama wakikuuliza swali ambalo hulijui jaribu kuwashirikisha, kama na wao hawajui basi
waambie utawapata jibu siku nyingine. Unahitaji kuwa msafi. Uwe mbunifu.
4. Mwonekano wa darasa/ lazima darasa liwe linaonekana. Kusiwepo na sauti nyingine inayoingia
ndani
5. Matumizi ya ubao au power point. Vionekane vizuri
6. Sauti ya mwalimu-je sauti yako inasikika vizuri? Hakikisha sauti yako inasikika kwa wanafunzi
wote. Uwe na uwezo wa kuimudu lugha vizuri.
7. Ukubalifu wa mambo ambayo hukufundisha/hukupanga kuyafundisha..kama wanafunzi wakitaka
kufundishwa kitu Fulani ambacho wewe hukujiandaa kuwafundisha, itategemea hali ya darasa
UTAYARISHAJI WA MITIHANI
Huu ni mchakato wa upimaji wa maarifa/ujuzi ambao wanafunzi wameupata tangu mwanzo wa kozi hadi
mwisho wa kozi. Kipengele hiki ni cha muhimu sana hivyo lazima lifanyike kwa ustadi na ubunifu
mkubwa.
Malengo ya mitihani lazima yalenge kupima mambo manne
1. Ulenge kupima maarifa na ujuzi aliyopata mjifunzaji lugha.
2. Kupima mbinu mbalimbali alizotumia mwalimu kufundishia kama zimeeleweka au la.
3. Mitihani imelenga kupima mitaala
4. Mitihani inapima uwezo wa kuchochea kujifunza maarifa mapya.
AINA ZA UPIMAJI
1. Upimaji rasmi-huu ni upimaji unaofanyika mwisho mwa kozi na hufanyika mara moja tu.
Hupima viwango vyote ambavyo alijifunza mwanafunzi.
2. Upimaji usio rasmi-mwanafunzi anapimwa wakati somo linaendelea,mfano mazoezi, mitihani nk.
Mara nyingine upimaji huu huitwa upimaji umbaji KANUNI ZA UPIMAJI
1. Kuwapa wanafunzi muda wa kujiandaa-wape muundo wa mtihani ulivyo
2. Hakikisha jaribio lako linapima wanafunzi kitu walichojifunza
3. Hakikisha kwamba jaribio lako lina uhalisia/reality
4. Hakikisha kwamba jaribio lako/mtihani wako linachochea utendaji
***ili kutimiza haya, unapaswa
1. Hakikisha unaondoa utata katika mtihani huo/maswali yawe bayana/yawe wazi.
2. Muda wa kufanya mtihani huo uzingatie
3. Kuwepo na umakini katika uandishi/ avoid typing errors.
4. Hakikisha haurudii majaribio
5. Hakikisha wanafunzi wako hawaibii/kuangaliziana katika mtihani/cheating
***mwisho wa somo la Kiswahili kwa Wageni***