fokasi 2015-2019 “uzima tele kwa wote“ mission in solidarity · pdf filemasomo ya...

17
Fokasi 2015-2019 “Uzima tele kwa wote“ Mission in Solidarity Kitabu cha Mwongozo Kusoma Biblia kwa kutumia macho ya Jamii nyingine

Upload: ngonga

Post on 24-Feb-2018

368 views

Category:

Documents


13 download

TRANSCRIPT

Fokasi 2015-2019

“Uzima tele kwa wote“

Mission in Solidarity Kitabu cha Mwongozo

Kusoma Biblia kwa kutumia macho ya Jamii nyingine

Yaliyomo

Tahariri Gabriele Mayer

Timu ya kimataifa ya mradi huu

Mradi wa kusoma Biblia wa EMS

Kushirikishana Biblia

Maombi ya Ufunguzi wa kipindi Riley Edwards-Raudonat

Maombi ya kufunga kipindi Riley Edwards-Raudonat

Masomo ya Biblia

Isaya 2 Royce Victor

Marko 9 Alfred Moto-poh

Wafilipi 2 Tiny Maslene Irawani

2 Wafalme 7 Kwon-Ho Rhee

Luka 24 Anne Heitmann

Baadhi ya mapendekezo kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo Timu ya Mradi

Tahariri Wapendwa wasomaji,

Fokasi mpya ya EMS 2015 – 2019 ni: „UZIMA TELE KWA WOTE“

Kwa hakika ni ombi kubwa linalogusa mambo mengi! Ni maneno matamu tu? Je maneno haya yana maana yeyote? Au ni maono tuliyonayo kama wakristo na yanayotuunganisha na watu wa dini nyingine?

Nini maana ya „uzima tele“? Je, ni kwa jinsi gani watu wote wanaweza kushirikishwa ikiwa hali zetu za kisiasa, kijamii na kiuchumi hazina misingi ya haki na usawa?

Katika ushirika wa kimataifa wa EMS, kwa pamoja tunataka kujenga maono ya „Uzima Tele kwa wote“ na hasa kuwalenga wale waliotengwa. Sisi kama wakristo wote, wake kwa waume tumeitwa kupeleka matuamini hasa kwa watu wanyonge wasiokuwa na sauti katika jamii.

Kwa maana hiyo basi, si kwa bahati sehemu ya pili ya kichwa cha Fokasi ni jina la EMS: „Mission in Solidarity“ (Misheni katika mshikamano)

Hii inahimiza ushirikiano wa watu wa matabaka tofauti tofauti. Sisi kama ushirika wa EMS tunajua faida zinazoletwa na ushirikiano katika tofauti hizi. Tunajua uzoefu unaopatikana katika kuheshimiana na kujitahidi kuelewana zaidi. Hili ni lengo la mradi wetu mpya wa Biblia, litakalofikiwa kwa usomaji wa Biblia katika ushirikiano wakitamaduni na kwa kufanya jambo la kuonyesha mshikamano kati ya vikundi rafiki katika muda watakaokuwa pamoja.

Mnakaribishwa sana kushiriki !

Salamu nyingi za upendo kutoka kwa timu ya kimataifa ya mradi na uongozi wa EMS,

Gabriele Mayer (Mradi wa kusoma Biblia)

Kerstin Neumann (Fokasi 2015-2019)

Timu ya kimataifa ya mradi: Paul-Bernhard Elwert ni mwanafuzi wa Theologia ya kiprotestanti, mwanachama wa mtandao wa vijana wa EMS na mjumbe wa bodi ya uendeshaji wa Misheni ya Basel tawi la Ujerumani.

Anne Heitmann ni mchungaji wa kanisa la kiprotestanti la Baden, mkuu wa kitengo cha misheni na ekumeni katika kanisa la Evangelischer Oberkirchenrat la Karlsruhe na mwanachama wa baraza la misheni la EMS.

Dr. Gabriele Mayer ni mkuu wa kitengo cha wanawake na jinsia na kuanzia mwezi wa saba 2015 ni msimamizi wa kitengo cha elimu cha kiekumeni katika EMS.

Alfred Moto-poh ni mchungaji wa kanisa la Presbiterian la Kameruni (PCC). Amekuwa mfanyakazi wa kiekumeni katika kanisa la kiprotestanti la Baden, tangu mwaka 2012.

Tiny Maslena Irawani ni mchungaji wa kanisa la Luwu huko Indonesia. Ni mfanyakazi wa kiekumeni katika kanisa la kiprotestanti la Baden, na pia ni mjumbe wa bodi ya ushauri ya wanawake ya EMS.

Kwon Ho Rhe ni mchungaji wa kanisa la kipresbiterian la Korea (PCK), na pia ni mfanyakazi wa kitengo cha elimu cha kiekumeni, anaesimamia hasa maswala ya Asia katika EMS

Emmanuel Kwame Tettey ni msharika wa kanisa la kipresbiterian nchini Ghana (PCG). Mwaka 2010 alishiriki kwenye kazi za kujitolea za programu ya vijana ya kiekumeni. Pia ni muwakilishi wa vijana katika mkutano mkuu wa EMS na mratibu wa mradi wa Biblia kanda ya Ghana.

Dr. Royce Victor ni mchungaji wa kanisa la India Kusini (Church of South India-CSI). Alikuwa mwalimu wa Theologia katika mji wa Thiruvananthapuram/Kerala. Ni afisa ushirikiano wa CSI-EMS chennai/India. Pia, ni mratibu wa mradi wa Biblia kanda ya India.

Usomaji wa Biblia kwa kutumia macho ya jamii nyingine EMS - Mradi wa Kusoma Biblia

Mradi huu unahusu nini? Kwa kupitia mradi huu EMS inasaidia vikundi vya jamii, tamaduni na mataifa mbalimbali kuungana katika kusoma Biblia kwa pamoja. Ushirikiano huu utaundwa na vikundi viwili vya jamii tofauti. Vikundi vilivyoungana, vitachagua neno moja na kisha, vitabadilishana uelewa wa neno hilo. Hivyo, kila kikundi kitajifunza kutoka kwa kikundi rafiki na kupata uelewa mpya na picha mpya ya jinsi neno la Mungu linavyofanya kazi katika jamii nyingine. Kitendea kazi katika mradi huu ni mwongozo, utakaopatikana kuanzia mwezi Novemba 2015. Ndani yake kutakuwa na maandiko sita ya biblia yanayohusu mada maalum yaliyochaguliwa na timu ya kimataifa ya mradi huu ili kurahisisha mabadilishano ya uelewa wa neno. Jinsi itakavyofanyika: Vikundi viwili vitaungana, vitasoma Biblia kwa kutumia lugha zao na uelewa wao au miwani ya mazingira na tamaduni wanayoishi. Kisha, kikundi kimoja kitatuma ripoti yao kwa kikundi rafiki kilichopo katika nchi nyingine kwa lugha ya kiingereza na kikundi rafiki kitafanya hivyo pia. Nani anaweza kushiriki? Wewe pamoja na watu wengine wanaopenda na wenye utayari (kikundi chako), kupitia EMS mtatafuta kikundi rafiki kinachotoka katika mazingira, kanisa, lugha au nchi tofauti na yako mwenyewe. Kwa mfano, vikundi ambavyo tayari vina ushirikiano wa kimataifa vinaweza kupata njia mpya ya kudumisha mahusiano yao. Vikundi vya usharika au makanisa vinaweza kuwasiliana na makanisa nje ya nchi. Vijana wanaweza kubadilishana neno na vijana wa nchi nyingine. Vikundi vya wanawake na wanawake wa nchi nyingine. Wanafunzi wa vyuo vya Biblia wanaweza kuwasiliana na wanafunzi wa vyuo vingine pia. Ushirikiano wa vikundi mbalimbali unawezekana! Lengo ni nini? Uelewa wa tamaduni tofauti unaweza kuendelezwa kwa njia ya "kusoma Biblia kwa kutumia miwani tofauti za kitamaduni". Unaweza kupata uelewa mpya, wa ajabu na unaohamasisha katika neno la Mungu. Jambo muhimu ni kwamba kila kikundi kitaonyesha jinsi neno la Mungu linavyogusa uhalisia wa maisha yao katika mazingira yao wanapoishi. Kwa mfumo huu inawezekana kutengeneza jambo la mshikamano au tendo la kusaidiana ambalo litawaunganisha kikundi chako na kikundi rafiki. Katika warsha tatu (zinazotegemewa kufanyika Ujerumani, Ghana na India) wawakilishi wa vikundi rafiki watakutana na kushirikishana matunda ya safari yao ya pamoja katika kusoma neno la Mungu. Jinsi ya kushiriki Jiandikishe kama kikundi kati ya mwezi novemba 2015 na Machi 2016 katika tovuti ifuatayo; https://ems-online.org/en/active-worldwide/international-bible-project/ Tujulishe kama unahitaji msaada wa kutafuta kikundi rafiki, tutafurahi kukusaidia. Mwongozo wa mradi wa usomaji Biblia unapatikana kwa kiswahili, kijerumani, kiingereza na kiindoneshia kupitia tovuti ifuatayo: www.ems-online.org au unaweza kutumiwa kwa kuandika ombi lako kwa barua pepe kwenda: [email protected] Ili kurahisisha mchakato huu, kikundi chako na kikundi rafiki kikubaliane na kuchagua maandiko mawili au matatu ya Biblia . Muda wa kusoma biblia na wa kutuma ripoti inabidi upangwe na uweze kufuatwa.

Kushirikishana Biblia (Bible Sharing)

Ni njia maalum ya kusoma Biblia kwa pamoja katika vikundi, iliyoanzia huko nchini Afrika Kusini. Mfumo huu wa kushirikishana Biblia, unampa kila mtu nafasi ya kuchangia na kuelezea kwa uhuru, ujumbe wa maandiko ya Biblia juu ya maisha yake.

Tunapendekeza hatua saba, katika kushirikishana Biblia:

1. Ufunguzi

Mwongozaji wa kikundi au mwanakikundi yeyote afungue kwa sala. Mnaweza pia kuimba wimbo, kama sehemu ya ufunguzi au kutumia njia nyingine yeyote inayowapendeza.

2. Kusoma Neno la Mungu

Kila mwanakikundi afungue kifungu cha Biblia, kilichopangwa kusomwa na wanakikundi wote. Mwanakikundi mmoja asome neno hilo kwa sauti, mara moja au mbili, na kufuatiwa na muda wa kimya, ili kutafakari neno hilo.

3. Kuyapa sauti maandiko ya Biblia

Kutoka katika neno lililosomwa, wanakikundi wanatakiwa kutamka kwa sauti sentesi moja, neno moja au sehemu ya sentensi, ambayo inaugusa moyo wake kwa namna ya pekee (kama ilivyoandikwa kwenye Biblia, bila ya kuongeza neno lolote) . Kila baada ya neno au sentensi iliyotamkwa, kuwe nafasi fupi ya ukimya, kabla ya mwanakikundi mwingine kutamka neno lake.

4. Tafakari kwa kimya

Mwongozaji awape wanakikundi muda wa kukaa kimya. Katika kimya hiki, wanakikundi watafakari na kusikiliza maneno yaliyotamkwa, kwa masikio yao ya rohoni.

5. Kushirikishana

Wanakikundi washirikishane sababu za wao kuguswa na neno au sentesi waliyoitamka. Wanaweza pia kuelezea hisia hasi juu ya neno hilo. Maelezo ya kihistoria ya kifungu hicho cha biblia yanaweza pia kutumika (unaweza kurejea mchango wa timu ya mradi huu katika kitabu hiki). Dhumuni kuu ni kujua jinsi neno la Mungu linavyozungumza nasi, katika hali zetu na maisha yetu ya kila siku. Kutokana na kwamba mradi huu unakwenda duniani kote, ni muhimu kila mmoja wetu apewe nafasi ya kusikilzwa na kusikiliza. Kwa njia hii tutaweza kujifunza kutoka kwa kila mmoja wetu na hata kuwafikia walio nje ya mipaka yetu.

6. Kufanya jambo au mambo kwa pamoja

Nchini Afrika Kusini wakati wa utawala wa kibaguzi wa makaburu, ilikuwa ni muhimu kwa kikundi cha kushirikishana Biblia kufanya jambo au shughuli ya pamoja baada ya kusoma neno la Mungu. Je ni jambo gani/tendo gani la mshikamano mnaloweza kulianzisha na kikundi chenu rafiki?

7. Kufunga Kipindi

Kipindi hiki cha kushirikishana Biblia kitafungwa kwa sala, nyimbo au vyote kwa pamoja.

Sala ya Kufungua kipindi

Mungu, mfariji na mkombozi wetu:

Tunakushukuru kwa zawadi ya neno lako.

Neno hili umetupa kwa njia ya Biblia ili tulishike, tulisome na kujifunza, liwe changamoto na mwongozo tunavyojitahidi kuishi maisha yetu sawa na mapenzi yako. Mara nyingi neno lako moja linazungumza nasi kwa namna tofauti tofauti. Hii inatupa nafasi ya kusikiliza na kujifunza kutoka kwa kila mmoja wetu. Utupe roho ya utayari tunapojitahidi kufanya hili. Kaa nasi sasa tunapokuja katika neno lako.

Bariki majadiliano yetu.

Wape ujasiri wote walio na jukumu gumu la kufanikisha mawasiliano kwa kuandika mawazo tutakayoyakusanya wakati wa kikao hiki.

Yote tutakayofanya au kuyasema leo, yafanyike katika amani,

Amani ambayo ipo juu ya uelewa wote.

Amen.

Sala ya kufunga kipindi

Mungu mwema na mwenye neema:

Tunashukuru kwa muda uliotupa tukae pamoja.

Neno lako linatuunganisha kila wakati, tuwapo mbali au tuwapo karibu.

Neno lako liendelee kuwa kiunganishi kati yetu, hata tutakapokutana tena.

Wabariki wote wanaoshiriki katika mradi huu wa kusoma Biblia.

Tupe nguvu ya kuendelea mbele, pale shauku yetu inapopungua.

Tupe ujasiri wa kusema kwa ushujaa kile tunachoamini neno lako linatufundisha.

Tupe unyenyekevu, tukubali kuwa uelewa wa wengine unaweza kuwa wa faida kama ulivyo uelewa wetu.

Tufundishe kuenenda katika umoja, kama tukiwa Ulaya, Afrika au Asia.

Tuwezeshe kutimiza lengo hili. Tunaomba yote tunayoyafanya yasaidie amani na maelewano kati ya watu wote, popote walipo.

Amen.

MASOMO YA BIBLIA

Isaya 2 |Mwaliko wa hija ya amani katika uwepo wa Mungu.

Nje ya jengo la umoja wa mataifa kuna ukuta wenye maandishi yasemayo, “nao watafua panga zao ziwe majembe…“ (Isaya 2:4). Mstari huu unashabihiana na ibara ya 2(4) ya mkataba wa Umoja wa Mataifa isemayo, “Wanachama wote katika mahusiano yao ya kimataifa watajizuia kutishia au kutumia nguvu…“

Isaya 2:1-5 inazungumzia wakati ujao wa nyumba ya Mungu, Isaya 2:6-22 inazungumzia hukumu juu ya nyumba ya Yakobo. “Mungu ni chanzo cha haki na amani“ hili ndilo neno kuu na kiunganishi katika sehemu hizi mbili, zinazoelekeza wakati ujao. Kujishusha kwa mataifa na safari yao ya kwenda mbele za Mungu(Isaya 2:2-4), ilikuwa ni mada iliyotawala majadiliano ya kitheologia, katika kipindi cha kuishi uhamishoni na baada ya hapo. Huu ni wakati ambapo, maswala ya amani na haki yalianza kuwa muhimu kwa watu katika nyanja za kimataifa.

Mistari hii inazungumzia safari ya Watu wengi kuelekea Sayuni, mji wa Mungu na kiini cha utawala wake, ili kuitafuta amani na haki yake Mungu. Maandiko haya hayazungumzii mtu mmoja, bali safari ya pamoja (kama kundi) – hii ni changamoto kwa tabia ya ubinafsi na umimi. Dhamira kuu ya safari hii: ni kufanya kazi kwa pamoja ili kuuleta utawala wa Mungu duniani. Katika mstari wa tatu Mungu haonyeshwi kama mfalme, bali kama mwalimu – mtazamo wa makuhani wa Israel katika zama za kale. Baada ya mataifa kujifunza mafundisho ya kimungu, wakaharibu silaha zao za vita. Si Mungu aliyeharibu silaha, ila ni watu waliobadilisha tabia zao ili ziwe zenye manufaa kwa ustawi wa viumbe vyote. Mataifa yanakuja sayuni kujifunza njia za haki kutoka kwa Bwana. Safari hii, ni kwa ajili ya kujifunza thamani ya haki na amani na kupeleka tunu hizi muhimu sehemu nyingine duniani.

Isaiah 2:6-22 inazungumzia hukumu ya Mungu juu ya wale walio kikwazo cha amani na haki. Kila mtu pamoja na watu wa Mungu watatendewa kwa usawa, hakuna sisi na wale mbele ya Mungu. Mistari hii ni mwaliko kutoka kwa Mungu kwenda mbele zake, ili kujifunza haki na amani na kuipeleka duniani na kuwaonya wale wanaotegemea zaidi mafanikio yao, tabia zao na mitazamo yao ya kidunia (mstari wa 8).

Andiko hili linazungumzia mabadiliko kutoka kwenye umimi, mafarakano na ugomvi kwenda kwenye umoja, amani na mapatano. Mafarakano na chuki vinaendelea hata katika nyakati mpya. Lakini kutakua na suluhisho la amani litakalozidi matamanio binafsi na ya kimataifa. Kuna tofauti zilizopo kati ‘Sayuni’ bora (Isaiah 2:2-4) na sifa ya sasa ya watu wake. Hii inafanunuliwa mara nyingi katika mfano wa urefu na kina. Sayuni kama mlima mrefu lakini watu wake wakiwa wamejishusha katika hali ya chini kabisa. Hali hii inahitaji kwenda mbele za Mungu na kuchota amani na haki kwa ajili ya ulimwengu.

Maswali kwa kikundi

• Ni jinsi gani wakristo kama watu binafsi na kama usharika wanaweza kutumika kuleta amani na haki katika jamii?

• Katika mazingira yako unayoishi: Ni wapi unapoona alama za mabadiliko kutoka kwenye uadui mpaka kufikia upatanisho?

• Je, kuna hatua zozote za kuonyesha mshikamano, unazoweza kuhitaji kutoka kwa kikundi chako rafiki cha kusoma Biblia?

Marko 9:33-37/41 | Ni nani aliye Mkuu?

Katika maandiko yetu tunakutana na mgogoro, wanafunzi wanabishana ni nani aliye mkuu kati yao. Mvutano huu unatokea muda mfupi tu, baada ya Yesu kuwaeleza habari za mateso yake, kufa na kufufuka kwake. Kwa hakika wanafunzi hawakuelewa neno lile alilolisema Yesu. Kutokuelewa huku ni matokeo ya matazamio yao ya kuwa na mfalme mshindi, kuliko mwalimu anaesulubiwa. Hii inaonyesha wazo la ukuu walilokuwa nalo na tulilonalo sisi pia. Je, hatudhani kwamba ukuu unatokana na cheo, mamlaka, hadhi kubwa na utajiri? Utumishi unahusiana nini na ukuu?

Mamlaka na vyeo ni sehemu muhimu katika maisha yetu. Kwa mfano nchini kameruni hafla nyingi za kiofisi hukwama, kwasababu wageni hudhani kwamba nafasi zao katika jamii haziendani na viti walivyoandaliwa kukaa. Wakati mwingine watu hugombana kwasababu ya vyeo. Shughuli za Kisiasa pia zinaweza kukwama kama “ego au nafsi ya mtu anavyojiona” haikuelezewa vizuri (haikutiliwa maanani).

Vipimo vya ufalme wa Mungu si vipimo vya dunia hii. Si vibaya kutaka kujulikana na kuheshimiwa. Haya ni mahitaji muhimu kwa binadamu, lakini ni kwa jinsi gani tunapata mahitaji haya? Dunia inafuata mpangilio wa kipiramidi unaokuwa mwembamba kadri unavyoelekea juu. Lakini tunamuona Yesu anageuza mpangilio huu juu chini, kwa kusema kwamba wakuu ni wale wanaojishusha. Ukuu unapatikana kwa wale wanaowakaribisha na kuwajali walio wadogo kati yao. Kazi ya Yesu ilikuwa ni kuwaokoa, kuwaponya na kuwarudisha kwake watu wanyonge na waliosukwasukwa na mawimbi ya maisha. Yesu alikuja kama aletaye imani, tumaini na maisha mapya kwa kila mwenye huzuni na mashaka na kwa wale waliokata tamaa.

Je unataka kuwa mkuu? Basi, chukua kila aina ya cheo au ukuu uliopata kulingana na vipimo vya dunia hii na uutumie. Tumia nafasi hiyo kama chanzo cha kuwasaidia wengine na kushirikiana nao matunda ya nafasi yako. Kujishusha chini ya walio wadogo, kutakusaidia katika kuwapenda na kuwatunza. Badala ya wadogo kukujali na kukuinua wewe, wajali na uwainue wadogo kwa kuwahudumia. Katika ufalme wa Mungu kuhudumia wanyonge kutakubaliwa na msaada utakaoufanya kwa upendo utakumbukwa na utalipwa mbele za Mungu, hata kama uliowatendea watasahau. Yesu Kristo alikuja duniani ili kuwa mtumishi. Yesu Kristo alitoa uhai wake ili kuwakomboa watu wote. Inatupasa kufuata mfano wake na kulipa nafasi neno la Mungu, ili kwa kupitia maisha yetu liwafikie watu wote. Basi sisi na mataifa yetu tuache kuutafuta ukuu wa dunia hii miongoni mwetu, ila tuishi kwa amani na kila mmoja wetu. Hii ndio njia inayoleta matumaini katika jitihada za kuondokana na migogoro tulionayo katika dunia ya leo. Kwa njia hii tunaweza kuyafikia maisha yenye uzima tele ambayo Yesu anatuahidi kwenye kitabu cha Yohana 10:10. Haya ni maisha yenye ukamilifu katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na ukombozi wa waliokandamizwa na waliotengwa, kuponywa na kuunganishwa kwa mahusiano yaliyovunjika, na kufanywa upya kwa amani na haki.

Maswali kwa kikundi

• Ni jinsi gani watu wa kanisa lako au jamii yako wanajaribu kuwa bora kuliko wengine? Taja ubaya na uzuri wake.

• Je kung’ang’ania madaraka kuna maana gani katika jamii yako? • Inabidi watu waliotengwa na wanaoteseka wapewe nafasi sawa, ili waweze kutumia zile

fursa ambazo Mungu ameweka mbele yao, bila ya vikwazo vinavyotokana na ubinafsi na mifumo ya kijamii isiyokuwa ya haki. Je, tunawezaje kuonyesha mshikamano kwao?

Wafilipi 2:1-10 | Kuishi pamoja katika hali tofauti

1. Hii ni barua iliyoandikwa na Paulo kwa Wafilipi. Washarika wa usharika huu walikuwa ni wakristo, pamoja na waisraeli waliobadili msimamo wao na kuwa wakristo. Kulikuwa na migogoro katika usharika huu, iliyompelekea Paulo kuwaonya katika barua zake, kwamba tofauti zao zisiharibu maisha ya Usharika. Paulo anasema kutofautiana ni jambo la kawaida, lakini pale palipo na tofauti - kuna lengo la pamoja. Hivyo anapendekeza kukubaliana na tofauti zilizopo na kuhudumiana.

2. Mungu ameumba dunia na vilivyomo ndani yake kwa jinsi na namna tofauti, mimea na wanyama visivyofanana, wanadamu wenye sura tofauti na vipawa tofauti na kila mmoja ana akili zake na mawazo yake tofauti. Lengo la utofauti huu, ni kupendeza kwa pamoja kama ulivyo upinde wa mvua, uzuri wake huonekana kwasababu ya kuwepo kwa rangi zake tofauti zinazoshikamana na kuonekana kwa pamoja. Paulo anataka washarika wa Filipi kuungana mioyoni mwao, mawazoni mwao, katika upendo, katika akili zao na malengo yao ili kila mmoja aweze kumjali na kumhudumia mwingine badala ya kujiangalia yeye mwenyewe. Paulo anatoa mfano mmoja akisema: Mungu ndiye mfalme mkuu wa ulimwengu, lakini bado anataka kuja kututembelea, kwa kupitia Yesu Kristo aliyejitoa kwa ajili ya watu wake. Ndio maana Yesu alijishusha akawa mwanadamu. Mungu hajifikirii yeye mwenyewe tu, bali anatufikiria na kutuhudumia. Mungu anafanya haya kwa unyenyekevu na upendo. Yesu alikuja duniani ili kututoa dhambini. Mungu anatukubali sisi tuliokuwa waovu, jinsi tulivyo. Nchi ya Indonesia imeundwa na visiwa vikubwa vitano na mamia ya visiwa vidogo vidogo. Waindonesia wana tamaduni, makabila na dini tofauti. Kutokufanana kwa sifa za kijografia za visiwa hivi, kumesababisha uwepo wa aina mbalimbali za udongo, wenye rutuba katika viwango tofauti kutoka kisiwa kimoja kwenda kingine. Tofauti hii ya udongo inapelekea kutokulingana kwa hali za kiuchumi za watu. Utofauti wa maisha ya watu ni sehemu ya nchi ya Indonesia, ambayo wakati mwingine husababisha kutokea kwa migogoro, hasa ile inayohusiana na dini. Mfano ni mgogoro uliotokea mwaka 2006 mpaka 2008 katika miji ya Ambon na Poso. Kwa mtazamo wangu, inabidi tuone uzuri uliopo katika tamaduni hizi tofauti, walizonazo waindonesia. Kila mji nchini Indonesia una sifa za kipekee, ambazo zinaweza kuwa utajiri kwa watu wa Indonesia na kuweza kutumiwa vyema na vizazi vijavyo. Umoja katika hali tofauti unapendeza kama kutakuwa na usawa kati yetu katika kutoa na kupokea kwa kila mmoja wetu.

Maswali kwa kikundi

• Ni kwa jinsi gani unakutana na tofauti za kimawazo, kitamaduni na kidini? • Ni wapi zinapokunufaisha na ni wapi zinapokuwa changamoto kwako? • Vikwazo gani vinaweza kukwamisha kuishi pamoja mkiwa na maoni, tamaduni na dini

tofauti? • Ni kitu gani kinaweza kusaidia kuepusha tofauti zisilete migogoro?

2 Wafalme 7:3-11 | Mungu anatenda kwa kutumia wale waliotengwa na jamii

Wanaume wanne wenye ukoma, waliishi maisha ya shida yaliyojaa mateso mbele ya lango la mji. Wakati ule katika Israeli watu wenye ukoma walionekana kuwa najisi (wachafu) na hivyo kutengwa na jamii. (Mambo ya walawi 13:45-46). Watu hawa wanne wenye ukoma walikuwa ‘nje’ ya mji kwa namna nyingi. Walikataliwa na kubaguliwa kwasababu ya ugonjwa waliokuwa nao. Wamekuwa ni watu waliotengwa, wasioweza kupata malazi hata katika nyakati zile hatari za vita. Mmoja wao hakutaka kukata tamaa ya maisha. Aliona kuna njia mbili tu zilizobaki: kurudi mjini au kwenda kwa majeshi ya maadui, bila ya kujua matokeo yatakavyokuwa.

Kwanini hawakutaka kwenda mjini? Mji wa Samaria kwao ulikuwa kama “historia yao ya kukandamizwa”, kutokana na tamaduni zake na mfumo wake wa kijamii hakukuwa na uwezekano wa kwenda. Wakati huohuo mji wa Samaria ulikuwa na janga la njaa kali, na hivyo kuwa tazamio lisilokuwa na matumaini. Njia ya pili, ni kwenda kwa majeshi ya maadui. Inaweza kuwa fursa kwa maisha ya baadaye, japokuwa ilijaa sintofahamu. Kulikuwa na hatari ya kuuawa na maadui. Hata hivyo walijaribu kuifuata njia ile iliyoonekana kuwa na bahati ndogo zaidi: “…..wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu.” (2 Wafalme 7:4)

Hili si neno linaloonyesha kutokujali, bali ni neno la matumaini. Matumaini ya maisha yenye ubora kwa siku za baadaye. Kwani kukata tamaa ni sawa na kujihukumu adhabu ya kifo. Lakini kila mtu mwenye matumaini bila ya kujali ukubwa au umri, anajifungua kutoka katika vifungo vya kihistoria au katika hali ya sasa ya kupoteza matumaini. Mtu wa aina hii yuko tayari kupiga hatua na kuikaribisha kesho iliyo bora zaidi. Na pia anaweza kuona kwamba Mungu wa uzima anakuja kwetu kila wakati.

Wale watu wanne wenye ukoma walipokifikia kituo cha washami, walishangazwa kuona kwamba jeshi lile la maadui limetoweka, kwa hiyo ile hali ya hatari ilitoweka pia. Mungu anatutia moyo kuzipinga nguvu zenye kuharibu uzima wetu na kupiga hatua kuiendea njia ile ya uzima. Hivyo basi, kwa kupitia Roho wake Mtakatifu, Mungu anaweza kutenda kazi kwa watu wote wenye hamu ya kuufikia uzima. Naye Mungu wa uzima anakutana nao katika safari yao na kuwaongoza kuufikia uzima tele. Siku ya ukombozi utokao kwa Mungu i karibu.

Baada ya watu wenye ukoma kuona wokovu wa Mungu, walisukumwa na wajibu wa kupeleka habari hizi njema kwa mji wa Samaria (2Wafalme 7:9). Hii ndio kazi iliyowapasa kuitimiza (linganisha na 1Wakorintho). Kwa hiyo walikwenda kuiitarifu Samaria kuwa jeshi la maadui limetoweka. Na kwa kutumia hazina ile iliyopatikana katika jeshi la washami, watu wa Samaria waliweza kushinda janga la njaa. Nao wakaona Mungu akiingilia kati, kwa kutumia watu wale waliokuwa wamekataliwa na kutengwa na pia kulazimishwa kuishi pembezoni mwa mji. Watu hawa wameonyesha kuwakumbuka watu wa mji ule, kwa kutenda mema katika kipindi kigumu cha njaa, kwa kuwashirikisha habari hizi njema. Mungu aliwasaidia na kuwatia moyo wale waliotengwa kufanya maamuzi yale magumu na ya hatari. Baada ya hapo wakasikia mioyoni mwao kwamba wametumwa kupeleka habari njema duniani.

Maswali kwa kikundi

• Katika mazingira yako ni watu gani waliotengwa, wanaoweza kufananishwa na wale wanne wenye ukoma, wanaolazimishwa kuishi pembezoni mwa jamii au nje kabisa ya maisha ya kawaida ya jamii yako?

• Tunaweza kujifunza nini kutoka kwa watu hawa wanaojitahidi kupambana ili kupata maisha yale yenye hadhi ya kibinadamu?

• Ni jinsi gani tunaweza kushirikiana nao kwa kuwatendea jambo jema? Ni kwa njia gani kikundi chako rafiki kinaweza kukusaidia katika kufanikisha hili?

Luka 24:13-35 | Pasaka yenye kutia nguvu

Luka anaelezea mabadiliko ya kushangaza, yaliyowatokea walipokuwa njiani kutoka Yerusalem kwenda Emau: Tunaiona “njia ya ndani” ya wanafunzi waliyoipitia: kutoka kwenye huzuni, kukatishwa tamaa na kujitoa kwao mpaka kuifikia imani mpya na tumaini jipya. Karibu kila mstari unaweza kuonyesha kutembea kwao, kufikiri kwao na hata hisia zao. Baadaye wanafunzi wakabadilisha mwelekeo wao wa ndani na hata ule wa nje. Yote haya yanatokea wakiwa njiani. Jambo hili lenye kuleta matumaini haliwezi kutokea kama mtu hajaamua kuanza kuondoka. Bila ya mabadiliko ya mazingira ni vigumu kubadilisha mtazamo wako. Kwa hiyo, si bure kwamba neno hili linaanzia katikati ya mji wa Yerusalem kuelekea nje ya mji na kurudi.

Mtiririko wa matukio haya unatuonyesha “sehemu kuu nne za njia” waliyoipitia wanafunzi

Kwenda pamoja: Yesu anaandamana na wanafuzi akiwa kama mchungaji, anayewasaidia kuzungumzia jambo lile linalowaumiza mioyo. Kinachoshangaza : wanafunzi wanamwaga uchungu uliojaza mioyo yao kwa mtu wasiyemjua, anayewasikiliza na kutembea pamoja nao. Hatua ya kwanza ya tendo la kichungaji lakini pia la ki-misionari ni kusikiliza, ili kujua na kuelewa hali ya watu husika. Injili inawafikia watu katika “kutembea pamoja nao” na “kuishi pamoja nao”. Tafsiri mpya: Kisha “mtu yule asiyejulikana” anawaeleza wanafunzi neno la Mungu na kuwafunulia tafsiri mpya inayogusa hali yao. Hii inatutia moyo pia kusoma Biblia kwa macho ya jamii nyingine na kujaribu kutumia mtazamo mpya. Ukarimu kwa wageni: Mwishoni, wanafunzi wakaonyesha ukarimu kwa mtu yule wasiyemjua kwa kumfanya mgeni wao, ila yeye akawa mwenyeji kwao. Katika kuwamegea mkate, macho yao yakafumbuliwa. Yesu anawatokea, kama yeye aletaye ukamilifu, si tu kwa maneno yake ila hata kwa matendo yake. Tukio hili linatukumbusha pia “Utamaduni wa Ukarimu” ambao ni wa thamani katika nchi nyingi hata leo. Mara nyingi ukarimu unaonekana, pale ambapo watu hawana vitu vingi kuweza kugawana na wengine: kama pale mtu anapotembelea kijiji cha kiindoneshia au wakimbizi wanaotafuta hifadhi ujerumani. Kupeleka ujumbe Wakati wa chakula cha pamoja wanafunzi wakatambua: “Bwana amefufuka kwelikweli.” Waliyoyaona yalikuwa na umuhimu pale tu “waliposimama”, kurudi na kupeleka ujumbe – pamoja na wale wengine walioiona Pasaka tofauti na wao. Wanafunzi hawakuyadharau matukio haya, hawakuyachukulia kuwa kama ushindani ila kama uthibitisho. Kukutana tena kwa pamoja katika Yerusalem ni picha nzuri ya “tofauti zilizopatanishwa” katika ushuhuda wa injili ileile moja.

Maswali kwa kikundi

• Kubadilisha mazingira: Luka 24 ni hadithi ya njia inayokutanisha kwa ishara sehemu mbili, iliyo “pembeni” na “katikati”. Katika eneo lako ni nani au ni watu gani wanaosimama “katikati” na wanaosimama “pembeni”? Ni yupi mwenye sauti kati yao na ni yupi anaesikilizwa zaidi? Ni yupi asiesikilizwa? Ni ujumbe gani walionao wale walio pembezoni kulingana na mtazamo wetu? Ni njia zipi zinazotuleta pamoja?

• Kwa kutumia mifumo yote ya fahamu: kuzungumza na kusikiliza, kuonja na kuona, kusikiliza moyo wako, kusali na kumsifu Mungu: hizi ni sifa kuu za kitabu cha Luka 24. Maandiko haya yanatualika kushuhudia na kuelewa kwa kutumia milango yetu yote ya fahamu, ili kuona jinsi Mungu afanyavyo kazi kati yetu tungali “katika njia zetu”. Hivyo basi maandiko haya ni uhamasisho wa kupeleka “injili inayodhihirika katika maneno na hata vitendo”. Ni kwa jinsi gani ujumbe wa injili ya kuwekwa huru inaweza kuwafikia watu, kwa kupitia mifumo yote ya fahamu? Waelezee kikundi rafiki baadhi ya mifano inayoonekana katika jamii yako.

• Ukarimu kwa wageni: Je, ukarimu kwa wageni una umuhimu gani kwa jamii yako? Na katika ibada zenu? Je kuna kitu chochote kilichobadilika kwako au ulichojifunza kwa kuwa mwenyeji au mgeni? Basi kwa nini tusifanye ibada ya ukarimu kwa ajili ya kila mmoja wetu!

Mathayo 15:21-28 | Alienda mbali hata kuweza kupanua mipaka

Yesu aliondoka kwa kujitenga na makutano. Je, pengine alihitaji muda wa kupumzika? Alikwenda kwenye eneo ambalo watu hawakumjua na alikotumaini kupata nafasi ya utulivu: bila ya kutegemea kukutana na kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Kwa wakati ule uelewa wake wa kazi ya misioni ulikuwa ni mdogo haukuwa mpana, maana alijiona bado hajaitwa kuwaendea watu wa nje ya mipaka ya Taifa la Israeli.

Hapa tunaona mtazamo wa tofauti kabisa alionao mwanamke Mkananayo. Mwenyeji huyu wa mipaka ile (Tiro na Sidoni), alikuwa tayari kwenda mbali, kwa kuvuka mipaka yake ya kawaida ili kutafuta msaada kwa ajili ya afya ya binti yake aliyekuwa mgonjwa. Hakuvuka mipaka ya heshima pekee, bali pia kwa kupaza sauti katika njia kuu, alivuruga utulivu uliokuwepo katika kundi lililomfuata na kumzunguka Yesu. Mwanamke huyu anayeonekana kuwa “kero kwa jamii”, anamsogelea Yesu na kumpazia sauti na kukiri wazi kuwa yeye ni Mkuu na Mwana wa Daudi -Mfalme wa nchi ya jirani na yake. Mwanamke huyu Mkananayo, anaonyesha imani aliyokuwa nayo, kuwa Yesu ana nguvu ya uponyaji, ambayo ingeweza kumponya yeye na binti yake “walio wageni na watu wa imani nyingine”. Lakini Yesu anaonekana kunyamaza kimya. Kwanini? Wanafunzi wa kike na wa kiume wanamhimiza Yesu amsaidie yule mwanamke – ili tu waweze kurudisha utulivu uliokuwepo, wakisisitiza “mwache aende zake; kwa maana anatupigia kelele nyuma yetu”.

Kuna kipindi katika harakati za Yesu ilibidi kujiuliza, kama ilikuwa ni halali kwa “Habari Njema” kuwafikia watu waliokuwa nje ya mipaka yao ya kijiografia na ya kidini. Je, Yesu angebeba jukumu hata la wale “wengine” pia? (wa nje ya Israeli). Hili ni swali lililowaumiza vichwa wengi wakati ule. Katika mchakato wa harakati hizi changa za Yesu, hatua za kujifunza zilikuwa zimeanza zikimweka Yesu kama kiini (sehemu muhimu) katika kuleta mabadiliko.

Katika Injili ya Mathayo na Injili ya Luka, mwanamke anachangia katika mabadiliko ya “kupanua upeo” wa Yesu; mwanamke asiyekuwa na jina kwa wasomaji, asiyekuwa na haki mbele ya sheria, ambaye mwanzoni hata Yesu hakumuwekea umakini, maana hakuonekana kama mwanadamu ila aliitwa kuwa ni mbwa.

Je, hivi ndivyo tunavyoujua wasifu wa Yesu kutokana na usomaji wetu wa Biblia? Tabia au mtazamo huu wa kukataa na wa kuumiza hauna budi kuvuruga picha ya Yesu tuliyonayo. Je, hakuwa tayari kuwasaidia hata wale waishio pembezoni?

Katika sehemu inayofuata, tunamwona Yesu, kama mtu aliyemsikivu na anayethubutu kubadili mtazamo wake wa zamani. Anakubali kuongozwa na yule mwanamke anayeishi pembezoni, kwa kuwa na mtazamo mpya. Mwaka 2013 Baraza la makanisa duniani liliandaa kauli mbiu iliyobeba mtazamo wa kiekumeni, isemayo “Pamoja katika kuuelekea uzima: Misioni na uinjilisti katika kubadili mtazamo wa ulimwengu”. Mission yaweza kufanyika pia kwa kuanzia maeneo ya pembezoni, nasi tukaweza kujifunza kutoka kwa wale waishio huko pembezoni.

Mwanamke huyu Mkananayo asiyetajwa kwa jina, tunaona alikuwa jasiri, hakukubaliana na hali ya kukataliwa na Yesu. Kwa utulivu kabisa katika mazungumzo yake, anajenga utetezi wa hoja ulio endelevu. Huenda alikuwa ameshakutana na hali ya kubaguliwa na kukatishwa tamaa – na hivyo kuweza kuamsha nguvu ya ujasiri wake. Hapana, hakubali kuondolewa/kutengwa mbali na Yesu. Makombo yaliyoanguka kutoka mezani aliyaona kuwa yanamtosha, kwani aliamini kuwa yana nguvu

ya uponyaji kwa ajili yake na kwa binti yake aliyekuwa mgonjwa. Naye akasema kwa urahisi: “Ndiyo, Bwana, lakini hata.....”

Tunapomtazama Yesu, tunaona mabadiliko ya mtazamo na hata uvumilivu wake. Yesu ananyamaza, na kumuacha yule Mwanamke Mkananayo wa pembezoni atoe hoja yake – ndipo anatambua mwelekeo mpya katika upinzani uliokuwa wa amani wa mwanamke huyu. Sasa Yesu anaona imani yake kubwa kuwa sababu ya ung’ang’anizi wake. Hamuoni tena kama mvurugaji/kero, au kama aendaye mbali, bali kama mwanamke mwenye imani ya ajabu. Kwa hiyo ni wazi; Yesu hakutumwa kwa kondoo wa Israeli tu, kwani mipaka hii ilifunguliwa. Injili sasa ni lazima iende hata nje ya mipaka ya Israeli na kuwafikia watu wa ulimwengu wote.

Maswali kwa Kikundi

• Elezea “kuomba kitu/msaada” kunaonekanaje katika utamaduni wako? • Maneno “Makombo” na “Mbwa” yana maana gani katika maisha ya kila siku ya jamii yako? • Ni kitu au tendo gani linaweza kuwa ni ishara ya mshikamano? • Unawajua watu katika kanisa lako/nchi yako wanaoendeleza utetezi wa haki za wale walio

pembezoni / wanaodharauliwa?

Baadhi ya mapendekezo kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo

Hapa utaona baadhi ya njia mbalimbali zinazoweza kuongeza ubunifu, pale mnapokutana kwa ajili ya kusoma Biblia. Mapendekezo haya yanaweza kuwasaidia kubuni njia nyingine mbadala, mbali na kusikiliza na kuongea, zitakazowawezesha kujifunza neno la Mungu.

Isaya 2

Zoezi, jinsi ya kuingilia kati mgogoro fulani, na kisha kujadili kile mlichojifunza (changamoto au ugumu, faida n.k): watu wawili waigize kama wanapigana (wanaweza kuvaa glovu za ndondi ili kuepusha majeraha). Watu wawili wengine waingilie kati. Wengine washangilie na kuwachochea wale wawili wapigane. Mwishowe, wale wahusika (waliopigana na waliosuluhisha)waelezee mwenendo wa tukio lile na jinsi walivyojisikia.

Marko 9

Jaribu na kikundi chako, kutengeneza picha inayoonyesha kitendo cha „kung’ang’ania madaraka“. Kwa mfano, Katika mfumo wa kuigiza, mnaweza kutengeneza ‚pozi la pamoja‘(au picha ya mnato) la mtu anaeng’ang’ania madaraka na wale wanaotaka kuichukua nafasi yake. Anaeng’ang’ania madaraka atakaa kwenye kiti na kuwakatalia, kuwatishia au kuwasukuma wengine wanaotaka kukaa kwenye kiti kile.

Mnaweza mkaandaa mpangilio tofauti wa kukaa. Kwa mfano : • kukaa katika duara • kukaa sehemu tofauti tofauti. Kwa mfano, Kiti, sofa, stuli, kigoda na kwenye sakafu kwa muda

fulani au katika kipindi kizima cha kusoma Biblia. • muhimu: Inabidi mjadiliane na kubadilishana sehemu zile za kukaa. Kila mmoja atoe mtazamo

jinsi alivyojisikia kulingana na pale alipokaa na kusema anawaonaje wale waliokaa chini kwenye sakafu.

Wafilipi 2

• Mjadiliane katika kikundi chenu: ni wapi mnapoona tofauti ya utamaduni wenu na utamaduni wa kikundi rafiki?

• Je mnaweza kuunda kazi ya sanaa, inayoonyesha amani na maridhiano/upatanisho baada ya tofauti zilizokuwepo kabla. Nyenzo: Mchanga-Maua-kwenye sakafu (wazo kutoka India)

• Kitambaa kikubwa kilichowekwa alama za mikono yenu kwa kutumia rangi mbalimbali (wazo kutoka Brazil)

• Kuchora „dirisha la Kanisa“ kwenye kioo (wazo kutoka ujerumani) • Kutengeneza upinde wa mvua kwa kutumia vitu vyenye rangi mbalimbali kutoka kwenye eneo

lenu.

2 Wafalme 7

Andaeni mchezo wa kuigiza wenye matukio mawili au matatu ya hadithi ya „waliotengwa na jamii na waliookolewa kutoka kwenye janga la njaa“:

• Tukio la kwanza: Nje ya ukuta wa mji, wenye ukoma wanne wanateseka kwa njaa.

• Tukio la pili: ndani ya mji, watu wanateseka kwa njaa na wanaogopa majeshi ya maadui. • Tukio la tatu: kambi ya maadui inaonekana na kuwa msaada kwa watu wale.

Luka 24

Tafadhali jadili, neno “pembezoni” na neno “katikati” yana maana gani kwako. Fasili yake inategemea pia mtazamo wa mtu. Swali linalofuata linaweza kukusaidia: “Ni nani mwenye sauti anaesikilizwa kwenye jamii yako? Ni nani asiyesikilizwa?”

Andaa ibada kwenye usharika wako, inayohusu mada ya “ukarimu” na muwaalike watu wasiokuja kwenye ibada mara kwa mara, wawe sehemu ya maandalizi.

Andaa jioni moja mtakayokuwa “njiani” na kujaribu kuishi vipengele vya maandiko haya ya Biblia katika maeneo tofauti . Kwa mfano hatua ya kwanza iwe Yerusalem – mtembee na mtu msiyemjua – na kuwa na chakula cha pamoja (mnaweza kufanya na kikundi kingine).

Mathayo 15

Andaeni igizo linalohusu kukutana kwa Yesu na mwanamke yule mkananayo, mkipenda mnaweza pia kurekodi igizo lenu. Kwa mfano, mwanamke yule mkananayo anaweza kuwakilishwa na mhusika mwenye sifa ya watu wanaotengwa au wanaoishi pembezoni/wanaodharauliwa katika jamii yako.

Taarifa za Chapisho

Kitabu hiki cha mwongozo ni kitendea kazi cha mradi wa kusoma Biblia „ Kusoma Biblia kwa kutumia macho ya jamii nyingine“ ambayo ni sehemu ya Lengo kuu la EMS kwa mwaka 2015 – 2016 lenye kichwa kisemacho „ Uzima tele kwa wote – Mission in Solidarity“ (Misheni katika mshikamano). Kitabu cha mwongozo kinapatikana kwa lugha ya Kijerumani, Kiingereza, Kiindonesia na Kiswahili.

Shusha kutoka: https://ems-online.org/en/active-worldwide/international-bible-project

Tafadhali tuma maswali yako kwenda: [email protected] (kwa kingereza)

[email protected] (kwa kiswahili)

Mhusika: Dr. Gabriele Mayer

Wahariri: Timu ya kimataifa ya mradi (tazama ukurasa wa 2)

Tafsiri kwa Kiswahili: Frank Fabian Daffa, Waandishi

Vogelsangstraße 62 l 70197 Stuttgart, Germany

Simu: +49 711 636 78 -43

Faksi: +49 711 636 78 -45

Barua pepe: [email protected]

Tutembelee katika tovuti yetu: www.ems-online.org