somo la kwanza - mwalimu wa kiswahili · hata hivyo, nadharia hii inayodai kuwa kiswahili ni lugha...

86
KENYATTA UNIVERSITY INSTITUTE OF OPEN LEARNING AKS 102 HISTORICAL DEVELOPMENT OF KISWAHILI JACKTONE O. ONYANGO IDARA YA KISWAHILI NA LUGHA ZA KIAFRIKA,

Upload: others

Post on 13-Jan-2020

70 views

Category:

Documents


1 download

TRANSCRIPT

KENYATTA UNIVERSITY INSTITUTE OF OPEN LEARNING

AKS 102 HISTORICAL DEVELOPMENT OF KISWAHILI

JACKTONE O. ONYANGO

IDARA YA KISWAHILI NA LUGHA ZA KIAFRIKA,

YALIYOMO

SOMO LA MADA UKURASA

Madhumuni ………………………………………… iii Orodha ya Vifupisho ……………………………….. iv 1: Chimbuko la Kiswahili ……………………………… 1

2: Maenezi ya Kiswahili ………………………………. 14 3: Lahaja za Kiswahili …………………………………. 27 4: Usanifishaji wa Kiswahili …………………………… 38 5: Sera ya lugha katika Afrika Mashariki ………………. 45 6: Ukuzaji wa Msamiati na Istilahi ……………………… 63 7: Kiswahili barani Afrika na kwingineko ……………… 74 Marejeleo ya Ziada ……………………………………. 81

ii

MADHUMUNI

Madhumuni ya jumla ya kozi hii ni kuwawezesha wanafunzi kuelewa asili ya

lugha ya Kiswahili pamoja na hatua za maendeleo ambazo imepitia kufikia sasa. Aidha,

kozi hii inakusudia kuwawezesha wanafunzi kutimiza madhumuni maalum yafuatayo:

1. Kutathmini nadharia mbalimbali kuhusu asili ya Waswahili na lugha ya Kiswahili.

2. Kufafanua sababu zilizochangia kusambaza Kiswahili kutoka pwani hadi bara ya

Afrika Mashariki kabla ya uhuru.

3. Kueleza vigezo vilivyozingatiwa katika kusanifisha Kiswahili.

4. Kujadili juhudi zinazofanywa katika ukuzaji na uendelezaji wa istilahi za

Kiswahili.

5. Kujadili matatizo yanayokumba juhudi za kustawisha Kiswahili pamoja na mbinu

za kuyatatua.

iii

ORODHA YA VIFUPISHO

1. C.M.S. ----- Church Missionary Society.

2. COMESA ----- Common Market for Eastern and Southern Africa.

3. C.P.E. ----- Certificate of Primary Education.

4. G.C.S.E. ----- General Certificate of Secondary Education.

5. K.C.P.E. ----- Kenya Certificate of Primary Education.

6. K.C.S.E. ----- Kenya Certificate of Secondary Education.

7. K.K.A.M. ----- Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

8. P.T.A. ----- Preferential Trade Area

9. TIQET ----- Totally Integrated Quality Education and Training.

10. TUKI ----- Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.

11. U.M.C.A. ----- Universities Mission to Central Africa.

12. U.P.C. ----- Uganda Peoples Congress.

iv

SOMO LA 1

CHIMBUKO LA KISWAHILI

1.0 Utangulizi

Katika mada hii, nitazijadili nadharia tatu ambazo zimetolewa kuhusu chanzo cha Kiswahili na Waswahili. Aidha, nitadondoa ushahidi mbalimbali wa kihistoria na kiisimu ambao unadhihirisha uzito na udhaifu wa nadharia hizo. Nadharia ni maelezo yanayotoa mwanga na kuweka wazi ukweli kuhusu swala fulani linalochunguzwa; na Isimu ni uchunguzi wa lugha kwa kuzingatia misingi ya kisayansi.

1.1 Madhumuni

Baada ya kulipitia somo hili, ninatarajia kwamba utaweza: (i) Kutoa ushahidi wa kihistoria unaothibitisha kuwa Kiswahili ni lugha asili

ya Kibantu huku ukionyesha uzito na udhaifu wake. (ii) Kutoa ushahidi wa kiisimu unaodhihirisha kuwa Kiswahili ni lugha

mojawapo ya lugha za Kibantu.

1.2 Lugha ya Kiswahili ilitoka wapi? Katika fasihi simulizi ya Waswahili, wazee wa pwani wanadai kwamba walitoka

sehemu za kaskazini ya pwani ya Kenya mahali panapoitwa Shungwaya karibu na mji wa Lamu. Kutoka Shungwaya, Waswahili walihamia sehemu mbalimbali za pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu walikumbwa na matatizo mbalimbali. Matatizo hayo ni pamoja na njaa, vita, magonjwa na ongezeko kubwa la idadi yao.

Wazee hawa wa pwani wanasema kuwa zamani waliitwa ‘Wangozi’, na

Waswahili ni jina la kubandikwa tu. Aidha wanadai kuwa Kiswahili cha asili ni Kingozi. Kulingana na mapokeo ya Waswahili, asili ya kuitwa ‘Wangozi’ ni kwamba zamani watu hao walikuwa wakipima mashamba yao kwa kutumia kanda za ngozi na walivaa nguo zilizotengenezwa kutoka kwa ngozi (Mbaabu, 1985:1–5).

Hata hivyo, miongoni mwa Waswahili wenyewe hakuna makubaliano kuhusu

asili ya jina ‘Waswahili’ na ‘Kiswahili.’ Kuna wale wanaodai kuwa jina Waswahili lilitolewa na kijana wa Kingozi alipoulizwa na wasafiri wa Kiarabu kuwa wao ni kina

1

nani? Akawaambia kuwa ‘sisi ni Wa-ziwa-hili au Wa-siwa-hili,’ yaani wenyeji wa pwaa hizi au wenyeji wa kisiwa hiki kikubwa. Inaaminika kuwa jina hili liliendelea kubadilika na wakati jinsi lilivyotumiwa hadi tukawa na neno ‘Waswahili.’

Kuna wengine wanaosema kuwa neno Swahili lina asili ya neno la Kiarabu.

Wanasema kwamba Waarabu walikuja na kuwakuta watu wakiishi pwani na wakawaita watu hao Sahil na wingi wake ni Sawahil, yaani watu wa pwani au ufuo. Waarabu waliokuja pwani waliita sehemu hii ya Bara Afrika Al-Sahil (Pwani maalum). Kwa hivyo neno ‘Wa-swahili’ lina maana ya watu wanaoishi pwani. Kiambishi Ki- katika neno ‘Ki-swahili’ ni cha asili ya Kibantu na kina maana ya lugha. Kwa hivyo hii ni lugha ya watu wanaoishi pwani. Wana-elimu-chimbo wanasema kuwa jina ‘Kiswahili’ lilianza kutumika katika sehemu ya kaskazini ya pwani ya Kenya karibu na mji wa Lamu kati ya mwaka 700 na 800 baada ya Kristo (Mbaabu, 1978:3).

Zoezi la 1.1

* Je, kwa maoni yako, unafikiri asili ya neno ‘Kiswahili’ ni nini ? Watafiti wa Kiswahili, kama vile Mbaabu (1985:1), wanasema kuwa kuna

Waswahili wa aina tatu kutegemea asili yao. Hawa ni:

(i) Waswahili wenye asili ya Kibantu ambao zamani walijulikana kama Wangozi. Hawa ndio Waswahili asili na wamegawanyika katika makabila madogomadogo, kwa mfano, Wabarawa wanaoishi pwani ya Somali. Nchini Kenya, makabila hayo ni pamoja na Wa-Amu, Wa-Pate, Wa-Aunya, Wa-Siu, Wa-Shella, Wa-Malindi, Wa-Kilifi, Wa-Mvita, Wa-Mtang’ata, Wa-Kilindini, Wa-Jomvu, na Wa-Vanga. Nchini Tanzania, kuna makabila kama vile Wa-Mafia, Wa-Mrima na Wa-Tumbatu.

(ii) Waswahili waliozaliwa kutokana na ndoa kati ya Waarabu na Waswahili asili. Wanaume wa Kiarabu walipokuwa wakija kufanya biashara katika pwani ya Afrika Mashariki, walikuwa wakikaa kwa muda mrefu kabla ya kurejea makwao. Kwa hivyo baadhi yao waliamua kuishi pwani na wakaanza kufunga ndoa na wanawake Waswahili. Kwa sababu ya ndoa hizo, baadhi ya Waswahili huwa na ngozi nyepesi na nywele za singa kama Waarabu.

(iii) Waswahili waliotoka katika makabila mengine ya Kiafrika. Hawa ni watu walioishi na Waswahili kwa muda mrefu, wakaacha mila zao na kuufuata

utamaduni wa Waswahili. Walifanywa wenyeji wa jamii ya Waswahili baada ya wazee kukutana na kuamua kwamba watu hao watoe ada iliyoitwa umji au uwanati. Baadhi ya watu hawa ni wale waliokuwa watumwa na wengine waliotoka bara wakahamia pwani kwa sababu mbalimbali.

2

Licha ya maoni hayo, bado hakuna makubaliano kuhusu chanzo au chimbuko la Waswahili na Kiswahili, kwa hivyo kumekuwa na mgogoro kuhusu swala hili. Watafiti wameuendeleza mgogoro huu kwa kupendekeza nadharia tatu zifuatazo ili kuelezea chimbuko la Kiswahili:

1.3 Kiswahili ni Lugha ya Kiarabu

Wafuasi wa nadharia hii ni pamoja na Stigand, Reusch, Knappert na wasomi

wengineo (Whiteley, 1969:7-8; na Ndungo & Mwai, 1991:2-3). Hawa wanadai kwamba Kiswahili ni moja kati ya lahaja za Kiarabu. Vile vile wanasema kuwa utamaduni wa Waswahili ni utanzu wa utamaduni wa Waarabu. Wanatoa ushahidi ufuatao ili kuthibitisha madai yao:

Kwanza , wanasema kuwa lugha ya Kiswahili imekopa maneno mengi sana ya

Kiarabu. Baadhi ya maneno hayo ni kama yafuatayo: Kiswahili chenye asili ya Kiarabu Kiswahili asilia daima milele fahamu elewa katibu mwandishi elimu ujuzi hadhi cheo nadra tukizi ratibu panga tisa kenda ghadhabu hasira Pili, wanasema kuwa lugha ya Kiswahili imefungamana na mafunzo ya dini ya

Kiislamu, na Waswahili wengi ni waislamu. Wao hutumia majina ya dini ya Kiislamu kama vile Mohamed, Ramadhani, Rajabu, Maulidi, Haji, Idi, Mwanaidi, Juma, Mwajuma, Rehema na mengineyo. Aidha, baadhi ya maneno ya Kiswahili yaliyokopwa kutoka Kiarabu yanahusiana na nyakati ambapo waislamu huswali, kwa mfano, alfajiri, adhuhuri, alasiri, thenashara na magharibi. Inajulikana kwamba dini ya Kiislamu ililetwa pwani ya Afrika Mashariki na Waarabu na ilienezwa kwa lugha ya Kiarabu. Kwa sababu hiyo, vifungu vya Qurhan tukufu aghalabu hukaririwa kwa Kiarabu. Hali kadhalika, waandishi wa tenzi za Kiswahili, ambao walikuwa wakitumia hati za Kiarabu, mara nyingi walikuwa wakitanguliza tungo zao kwa kumshukuru Allah na mtume Mohamed. Waswahili pia hufanya sherehe za Maulidi mjini Lamu kila mwaka ambazo zinahusu kuzaliwa kwa mtume Mohamed. Kwa hivyo, Kiswahili na dini ya kiislamu ni kama chanda na pete.

Tatu, nyimbo za taarab hapo awali zilikuwa zikiimbwa kwa mashairi ya Kiarabu,

ndipo baadaye zikaanza kuimbwa kwa mashairi ya Kiswahili. Ohly (1973:84) anasema kuwa Waswahili walilazimishwa kutunga na kuimba mashairi ya kiislamu yaliyoitwa ‘maghazi’ ndipo wangeweza kuepuka kufanywa watumwa wa Waarabu.

3

Mwisho, wanasema kuwa ustaarabu wa Uswahilini umebuniwa na kuimarishwa na wageni waliotoka nchi za Mashariki kama vile Uarabuni, Uajemi, Uturuki, na Uhindi. Ustaarabu huo ni pamoja na mijengo, mavazi, vyakula na vinywaji. Kwa mfano, mavazi ya Waswahili kama vile buibui, mtandio, kanzu, kikoi na kofia ya kiislamu yalitoka Uarabuni. Navyo vyakula vya Waswahili vilivyotoka Uhindi ni kama vile ladu, papuri, na papai.

Hata hivyo, nadharia hii inayodai kuwa Kiswahili ni lugha ya Kiarabu ina

upungufu ufuatao: Kwanza, watafiti wa lugha ya Kiarabu wanasema kuwa lugha ya Kiswahili haikuzungumzwa Uarabuni wala hakuna lahaja yoyote ya Kiswahili inayopatikana huko.

Pili, ukopaji wa maneno ya kigeni ni jambo la kawaida katika kila lugha. Sio

Kiswahili tu ambacho kimekopa maneno ya Kiarabu, bali lugha zingine pia zimekopa. Hizi ni pamoja na Kihausa huko Afrika Magharibi, Kiurdu huko Pakistani na India, na Kimalay kinachozungumzwa huko Malay. Ingawa lugha hizi zote zimekopa maneno ya Kiarabu, hazijaitwa lugha za Kiarabu wala utamaduni wao haujaitwa wa Kiarabu. Kwa nini basi Kiswahili kiitwe lugha ya Kiarabu?

Tatu, lugha ya Kiswahili haikukopa maneno ya Kiarabu pekee bali imekopa pia

maneno ya lugha zingine, kwa mfano: Lugha iliyokopesha Maneno yaliyokopwa Kiingereza daktari, hospitali, kalenda. Kihindi dobi, jando, bima, hundi. Kiajemi bandari, mnara, nanga. Kireno mvinyo, padre, bendera, parafujo. Kituruki balozi, bahasha, baruti, korokoroni.

Ikiwa ni hivyo, mbona basi Kiswahili hakijaitwa lahaja ya lugha hizo? Kadhalika, ingawa maneno hayo yamekopwa, ni dhahiri kwamba yametoholewa na kufuata muundo wa maneno ya asili ya Kibantu. Kwa mfano, maneno ya Kiarabu kama vile ‘waqt’ (wakati), ‘adab’ (adabu), na ‘tajir’ (tajiri). Kuna pia maneno ya Kiingereza kama vile ‘doctor’ (daktari), ‘hospital’ (hospitali), na ‘television’ (televisheni). Zoezi la 1.2

* Orodhesha maneno mengine hamsini ya Kiswahili yaliyokopwa kutoka lugha mbalimbali za kigeni na uzitaje lugha hizo. Nne, miji ya Uswahilini kama vile Pate, Lamu na Kilwa ilikuwa imestawi hata

kabla ya Waarabu kuja pwani. Madai kwamba wageni ndio waliobuni na kuimarisha

4

ustaarabu na miji ya Uswahilini yanatokana na Wazungu. Kwa kuwa miji hii iliwahi kukaliwa na hata kutawaliwa na Waarabu, Wareno na wageni wengineo, haiwi ni sababu ya kuifanya kuwa imebuniwa na wao. Hata Wazungu pia waliikalia na kuitawala miji hii, lakini hawawezi kudai kuwa wao ndio walioianzisha. Basi kama wanavyosema Chiraghdin na Mnyampala (1977:xii):

“…lugha ya Kiswahili ni vivyo hivyo; haikubuniwa na Waarabu wala na kabila nyengine yoyote. Waarabu waliikuta lugha hii wakaipiga pambaja; na kwa maingiliano ya utamaduni na utawala, maneno machache ya lugha yao yakaingia katika lugha hii ya Kiswahili – jambo ambalo lafanyika katika lugha zote.”

Kumbuka

!Kihistoria, tunajua kwamba ilikuwa kawaida ya Wazungu kudai hivyo

kila walipoyaona mafanikio ya aina yoyote barani Afrika. Kwa mfano, walidai kwamba yale mapiramidi yaliyojengwa nchini Misri na ule ufalme wa Mwene Mutapa nchini Zimbabwe ni ustaarabu ulioletwa na wageni. Walidhani kwamba Mwafrika hana akili ya kubuni na kustawisha mambo kama hayo, kwani waliamini kuwa Afrika ni ‘bara lenye giza totoro’, au kwa maneno mengine ni ‘bara jeusi.’ Kwa hivyo, tujihadhari na hizo propaganda za Wazungu. Mwisho, Kiswahili sio lahaja ya Kiarabu kwa sababu utamaduni wa Waswahili

unahusiana sana na utamaduni wa jamii zingine za Kiafrika. Kwa mfano, desturi wanazofuata Waswahili katika kuwapatia watoto wao majina, malezi, harusi matanga na itikadi zao kama vile pepo na uchawi, zinafanana na desturi za jamii nyingi za Kiafrika (Tazama: Mbaabu, 1985B). Aidha, Chiraghdin na Mnyampala (1977:x) wanasema kwamba zamani Waswahili walikuwa wakifuata asili au nasaba yao kwa kuhesabu ukoo kukeni, kama zilivyo jamii nyingi za Kiafrika. Hii ina maana kwamba fahari ya Mswahili iko kwa mama wala si kwa baba. Kwa hivyo, Waswahili walikubali tu kufuata dini ya Kiislamu lakini hawakubadilisha mila na desturi zao za Kiafrika wala kubadilisha lugha yao.

Kwa sababu ya upungufu huo, ni dhahiri kwamba madai ya nadharia hii kuhusu

chimbuko la Kiswahili sio ya kweli, kwa hivyo inabidi tuangalie nadharia nyingine.

1.4 Kiswahili ni Lugha ya Mseto Wafuasi wa nadharia hii ni pamoja na Steere, Taylor, Broomfield na Johnson

(Ndungo & Mwai, 1991:14-16). Hawa wanadai kwamba Kiswahili ni mchanganyiko wa

5

lugha za Kiafrika na lugha za kigeni kama vile Kiarabu, Kiajemi, Kituruki na lugha zingine.

Ushahidi ufuatao umetolewa ili kuthibitisha madai ya nadharia hii: Kwanza, Johnson anadai kwamba Waarabu walipokuja pwani kwa shughuli za bishara, aghalabu hawakuandamana na mabibi zao kutoka Uarabuni. Kwa sababu hiyo, kulikuwa na uhaba wa wanawake wa Kiarabu, kwa hivyo Waarabu wakaanza kufunga ndoa na wanawake wa Kibantu na kuzaa nao watoto. Watoto hao walijifunza maneno ya Kiarabu kutoka kwa baba zao na maneno ya Kibantu kutoka kwa mama zao; kwa hivyo vizazi vilivyofuata vikawa na lugha ya Kiswahili iliyo na mchanganyiko wa maneno ya lugha mbalimbali.

Johnson anadai kwamba maneno ya Kiarabu na Kiajemi ambayo watoto hao

walijifunza kutoka kwa baba zao yalihusu vita, ubaharia, usafiri na vyombo vya ufundi. Lakini maneno ya Kibantu waliyojifunza kutoka kwa mama zao yalihusu kilimo, ufugaji, chakula na maisha ya kila siku.

Kumbuka

!Je, umewahi kusikia Waswahili wakiitwa chotara, suriama, wanaharamu,

shombe, wakosa kabila au hafukasti? Hii ni kwa sababu wanaaminika kuwa walizaliwa na wazazi wa rangi mbalimbali. Kihistoria, tunajua kwamba kule Afrika Kusini watu wa aina hiyo walibandikwa jina mulattoes, ilihali kule Marekani walikuwa wakiitwa mestizos. Haya yote ni majina ya kashfa. Pili, Broomfield naye anadai kwamba kulikuwa na haja ya Waarabu kuwasiliana

na watumwa wa Kibantu. Kwa hivyo ilibidi wachanganye maneno ya lugha za Kibantu na yale ya Kiarabu ili waweze kuelewana wakati walipokuwa wakifanya kazi za utumwa. Kutokana na mchanganyiko au mseto huo wa maneno, lugha ya Kiswahili ikachimbuka.

Hata hivyo, nadharia hii inayodai kuwa Kiswahili ni lugha ya mseto ina upungufu

ufuatao: Kwanza, kama vile Mbaabu (1978:3) anavyosema, lugha mbili katika ndoa haziwezi kuzaa nyingine, kwani lugha hazichanganyikani jinsi watu wa asili au rangi tofauti wanavyochanganyika.

Zoezi la 1.3

* Eleza upungufu wa nadharia inayodai kwamba Kiswahili ni lugha ya mseto.

6

Pili, watafiti wa Kiswahili wamethibitisha kwamba takriban asilimia 60% ya maneno yote ya Kiswahili ni ya asili ya Kibantu ilihali asilimia 30% ndiyo yenye asili ya Kiarabu. Asilimia 10% ya maneno hayo yanatoka katika lugha zingine kama vile Kiingereza, Kireno, Kiajemi, Kihindi na lugha mbalimbali za Kibantu.

Mwisho, kama vile Chimerah (1998:31) anavyosema, Kiswahili sio lugha ya

mseto kwa sababu sarufi yake haifanani na sarufi ya Kiarabu wala ya lugha zingine za kigeni bali inakaribiana na sarufi ya lugha zingine za Kibantu. Tutaifafanua hoja hii katika nadharia itakayofuata.

Hoja tulizotoa hapo juu zinaonyesha wazi kuwa madai ya nadharia hii kuhusiana

na chimbuko la Kiswahili sio ya kweli. Ingawa wanaume wa Kiarabu waliwaoa wanawake wa Kibantu, ndoa za aina hii haziwezi kuzalisha lugha mpya. Hali kadhalika, ukosefu wa lugha ya mawasiliano baina ya Waarabu na watumwa haungeweza kusababisha chimbuko la Kiswahili; kwa hivyo tutaangalia nadharia ya mwisho.

1.5 Kiswahili ni Lugha ya Kibantu

Wafuasi wa nadharia hii ni pamoja na Greenberg (1966), Guthrie (1948),

Chiraghdin na Mnyampala (1977), Whiteley (1969), Mbaabu (1978) na Chimerah (1998). Hawa wanadai kwamba Kiswahili ni lugha ya Kiafrika yenye asili ya Kibantu, kwa hivyo inafanana na lugha zingine za aina hii kama vile Kikuyu, Kiganda na Kinyamwezi.

Ushahidi wa aina mbalimbali umetolewa ili kuthibitisha madai ya nadharia hii.

Kwanza, tutadondoa ushahidi wa kihistoria kisha tuangalie ushahidi wa kiisimu. Ushahidi wa kihistoria unajumlisha vipengele vifuatavyo:

(a) Maandishi ya kale ya Kiswahili Mashairi ya kale yanathibitisha kwamba lugha ya Kiswahili ilikuwa

ikizungumzwa nyakati hizo kabla ya Waarabu kufika pwani ya Afrika Mashariki. Ifuatayo ni mifano ya mashairi hayo:

Kwanza, ni Utenzi wa Hamziya. Utenzi huu una maneno mengi ya Kingozi

ambacho kilikuwa Kiswahili cha kale. Maneno hayo ni pamoja na ‘maninga’ (macho), ‘ng’andu’ (dhahabu), ‘pulika’ (sikiza) na ‘mtendele’ (mumetenda). Pili, ni Utenzi wa Tambuka. Utenzi huu uliandikwa katika lahaja ya Kipate inayozungumzwa kisiwani Pate. Tatu, ni Utenzi wa Al-Inkishafi ambao uliandikwa katika lahaja ya Kiamu. Nne, ni Utenzi wa Liyongo na Takhmisa ya Liyongo ambazo ziliandikwa katika lahaja ya Kingozi. Tano, ni Utenzi wa Mwana Kupona ambao uliandikwa katika lahaja ya Kiamu. Mwisho, ni Habari za Wakilindi ambayo ni masimulizi yaliyoandikwa katika lahaja ya Kingozi.

Uchambuzi umeonyesha kwamba lugha iliyotumika katika maandishi hayo

inafanana kimuundo na lugha za Kibantu, kwa hivyo Kiswahili ni lugha ya Kibantu. Hata hivyo, tukumbuke kwamba tenzi nyingi za Kiswahili ziliandikwa kati ya karne ya 17 na 18. Kabla ya wakati huo, lugha ya Kiswahili ilikuwa ikizungumzwa kwa sababu Waswahili walikuwa na fasihi simulizi yao ambayo ni kongwe zaidi kuliko fasihi andishi.

7

(b) Historia Simulizi ya miji ya Uswahilini Historia Simulizi ya Waswahili inapatikana katika tarihi za Lamu, Kilwa na Pate

ambazo ziliandikwa katika karne ya 16. Tarihi ni kumbukumbu za matukio ya kihistoria yaliyopangwa kulingana na nyakati. Uchambuzi wa tarihi hizi unatufunulia mambo mbalimbali kuhusu asili ya Kiswahili.

Kwanza, katika Tarihi ya Lamu, tunaelezwa kwamba makundi matatu

yanayounda koo za jamii yote ya Lamu yanajulikana kwa majina ya Kiswahili, ambayo ni Kina Mti, Mfamao na Ungwana wa Yumbe.

Pili, katika Tarihi ya Kilwa, tunaelezwa kwamba Sultani wa kwanza wa Kilwa,

yaani Ibn Hussein, alijulikana kwa lakabu “nguo mingi.” Naye mwanawe aliyekuwa akitawala mji wa Mafia alijulikana kwa lakabu “mkoma watu.” Kwa vile yote haya ni maneno ya Kiswahili, hii inaonyesha kwamba wenyeji wa Kilwa na Mafia walikuwa wakitumia lugha ya Kiswahili kuwasiliana (Whiteley, 1969:34).

Tatu, katika tarihi ya Pate, kuna maneno mengi ya Kibantu yaliyotumiwa, ambayo

ni pamoja na “yumbe” (jumbe), “wavaa ng’andu” (waliokuwa wakivaa mapambo ya dhahabu) na “Wang’andu” (makazi ya waliokuwa wakivaa mapambo ya dhahabu). Hii inaonyesha kwamba wenyeji wa Pate walikuwa wenye asili ya Kibantu, walikuwa na viongozi wao walioitwa ‘jumbe’ na walikuwa wakivaa mapambo ya dhahabu.

(c) Wasafiri wa zamani Wasafiri wa zamani walipoutembelea mwambao wa Afrika Mashariki waliona na

kuandika kuhusu mambo mbalimbali. Walidai kwamba waliona miji iliyostawi na ambayo ilikuwa na wenyeji weusi waliokuwa na lugha yao. Wasafiri hao ni pamoja na Al– Masud, Al- Idris, Ibn Battuta na Mgiriki ambaye hakujitambulisha jina.

Al- Masud alitembelea pwani ya Afrika Mashariki mnamo karne ya 10. Yeye

alisema kuwa watu wa Zanj, yaani nchi ya watu weusi kuanzia Sofala hadi Mogadishu, walikuwa na wafalme wao na Mungu ambaye walimwita “Mkulungulu.” Alieleza kuwa chakula cha watu hao kilikuwa ndizi na mtama. Pia alitaja neno “kilazi” (Whiteley, 1969:32). Kama wanavyosema Chiraghdin na Mnyampala (1977), huenda ikawa neno ‘Mkulungulu’ baadaye lilibadilika likawa ‘Mulungu’ na hatimaye likawa ‘Mungu;’ nalo neno ‘kilazi’ lilibadilika likawa ‘kiazi.’

Al- idris alitembelea mwambao wa Afrika Mashariki mnamo karne ya 12 na

akaandika kitabu kiitwacho Kitab Rujar. Alitaja miji ya Malindi na Mombasa na akasema kwamba jina la zamani la kisiwa cha Zanzibar lilikuwa ‘Unguja.’ Pia aliandika baadhi ya majina ya ndizi katika Kiswahili, kwa mfano ‘kikonde,’ ‘kisukari,’ ‘muriani,’ na ‘mkono wa tembo’ (Whiteley, 1969:28-29).

Ibn Battuta, ambaye alizuru pwani mnamo karne ya 14, alisema kwamba alitembelea nchi ya “Swahili” (Whiteley, 1969:35). Yeye ndiye msafiri wa zamani kabisa kutaja nchi ya Waswahili. Alieleza kwamba watu wa Mombasa walikuwa wakinunua nafaka kutoka nchi ya Waswahili. Watafiti wanakisia kwamba huenda ikawa nchi inayozungumziwa ilikuwa katika eneo la mto Ozi. Pia alisema kwamba alipofika Kilwa,

8

alikutana na washairi wenyeji waliokuwa wakiandika mashairi na tenzi katika lugha ya Kiswahili.

Kulikuwa pia na msafiri Mgiriki ambaye hakujitambulisha jina. Yadaiwa kwamba

aliandika kitabu kinachoitwa The Periplus of the Erythrean Sea, yaani “Kitabu cha Maelezo kuhusu Bahari ya Hindi.” Alikiandikia mjini Alexandria mnamo karne ya 1, yaani mwaka wa 100 baada ya Kristo. Katika kitabu hicho alitaja bandari mbalimbali na miji ya Azania, yaani eneo la Afrika Mashariki. Kitabu hicho pia kinadokeza mambo machache kuhusu utamaduni wa Waswahili, kwa mfano, kinazungumzia habari za ‘mitepe’, ‘ngalawa’ na ‘madema ya kuvulia.’ Hii inaonyesha kwamba Waswahili walikuwa wavuvi. Watafiti wanafikiria kwamba huenda ikawa miji hiyo iliyotajwa ilijengwa na Waswahili. Kama wangekuwa wageni walioijenga, vile walivyodai wasomi wa Kizungu, basi tungetarajia kuona athari zao katika vizazi vilivyofuata. Kufikia sasa athari hizo bado hazipo. Ushahidi huu wote unathibitisha kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu iliyokuwa ikizungumzwa huko pwani kabla ya kuja kwa Waarabu. Maelezo zaidi kuhusu wasafiri wa zamani yameandikwa na Freeman-Grenville (1962).

(d) Msamiati na Methali za Kiswahili Tunapochunguza msamiati na methali za Kiswahili, tunapata fununu kuhusu

utamaduni na mazingira ya watu walioitumia lugha ya Kiswahili. Msamiati umejaa mambo ya kibaharia na uundaji wa vyombo vya baharini kama vile mtumbwi, dau, ngalawa, mashua na jahazi.

Methali za Kiswahili zimejaa taswira ambazo zarejelea mazingira ya pwani.

Mifano ni kama vile; ‘Mwenda tezi na omo, marejeo ni ngamani,’ ‘Usisahau ubaharia kwa sababu ya unahodha,’ ‘Hasira ya mkizi furaha ya mvuvi,’ ‘Dau la mnyonge haliendi joshi, likienda ni Mwenyezi Mungu kupenda,’ na ‘Nazi mbovu harabu ya nzima.’

Kwa hivyo ushahidi huo unaonyesha wazi kwamba Kiswahili kilizuka katika

mazingira ya pwani na kina wazungumzaji wake asili, lakini sio mchanganyiko wa lugha. Baada ya kudondoa ushahidi huo wa kihistoria, tutauchunguza sasa ushahidi wa kiisimu.

(e) Ushahidi wa Kiisimu Huu ni ushahidi unaotokana na utafiti wa sayansi ya lugha, yaani ‘Isimu.’

Wanaisimu waliofanya utafiti huo ni pamoja na Greenberg, Guthrie, Hinnebusch na Mbaabu.

Greenberg (1966) anasema kwamba Kiswahili kiko katika kundi la lugha za Kibantu zilizotawanyika kutoka sehemu za Niger – Congo. Pia alibainisha makundi mengine kama vile lugha za Kiniloti, lugha za Kikushiti na lugha za Kihaza.

Naye Guthrie (1967) alionyesha uhusiano uliopo kati ya lugha ya Kiswahili na

lugha zingine za Kibantu. Alichunguza lugha 200 za Kibantu kwa kuzingatia jumla ya maneno 22,000 katika lugha hizo. Aligundua kwamba mashina 2,300 yamezagaa katika lugha mbalimbali za Kibantu, na Kiswahili ni miongoni mwa lugha hizo. Guthrie aligundua kwamba Kiswahili kililingana na Kikongo kwa asilimia 44% ya mashina hayo. ‘Mashina’ ni maneno yanayohusiana kimaana ambayo yametokana na asili au chanzo

9

kimoja. Baadhi ya msamiati aliouchunguza Guthrie ni pamoja na asili ya neno “Bantu” linalomaanisha ‘watu’ au ‘wanadamu’ na ambalo umoja wake ni “Muntu.” Shina la neno hili limo katika lugha nyingi za watu wa jamii hii ya Kibantu, kwa mfano:

Lugha Umoja Wingi Kiswahili mtu watu Kimeru muntu antu Kikamba mundu andu Kiganda omundu abandu Kisotho muthu bathu Kizulu umuntu ubantu Kishona munhu vanhu Kikuria omonto abanto Kiluyia omundu abandu Kikuyu mûndû andû Wanaisimu wengine pia wamefanya utafiti ambao umetilia nguvu matokeo ya

utafiti wa Guthrie kwamba Kiswahili ni lugha asili ya Kibantu. Wao wameonyesha kwamba Kiswahili kina sifa zifuatazo za kiisimu ambazo zinapatikana katika lugha za Kibantu:

Kwanza, lugha za Kibantu zina mpangilio wa majina katika makundi au ‘ngeli.’ Ifuatayo ni mifano michache ya ngeli za majina ya Kiswahili na Kikuyu:

Kiswahili Kikuyu m – wa mtu – watu m – a mundu – andu m – mi mti – miti m – mi muti – miti ji – ma jiwe – mawe i – ma ihiga – mahiga ki – vi kiti – viti gi – i giti – iti Vile vile, viambishi awali vya ngeli za majina ya Kibantu hudhihirika katika

upatanisho wa kisarufi. Sifa hii haipatikani katika lugha za Kiniloti, kama inavyoonekana katika mifano ifuatayo:

Lugha za Kibantu Lugha za Kiniloti Kiswahili: Kitabu hiki ni kikubwa Dholuo : Buku ni duong’ Kikuria : Egetabo keno nekenene Kimaasai: O kitabu ni Ekegusii : Egetabo eka nekenene Pili, lugha za Kibantu hudhihirisha mnyambuliko wa vitenzi. Kukinyambua

kitenzi ni kukiongezea viambishi kwenye mzizi wake ili kukipa maana mahsusi. Kitenzi chaweza kunyambuliwa katika jinsi mbalimbali ikiwa ni pamoja na jinsi ya kutendana, kutendeka, kutendatenda, na kadhalika. Ifuatayo ni mifano michache kutoka lugha tatu za Kibantu:

Kutenda Kutendana Kutendeka Kutendatenda Kiswahili : fanya fanyana fanyika fanyafanya Kikamba : ika ikana ikika ikaika

10

Kikuria : kora koorana koreka korakora Tatu, lugha za Kibantu aghalabu huwa na mfumo wa silabi wazi, yaani kila silabi

ya neno lenye asili ya Kibantu huishia kwa vokali. Muundo huu hukosekana iwapo konsonanti moja kati ya mbili zinazofuatana ni ya nazali, kama vile /m/ au /n/. Hivyo basi, maneno mengi ya Kiswahili huwa na muundo wa Konsonanti – Vokali – Konsonanti – Vokali, yaani KV-KV… Kwa mfano: ‘kisu,’ ‘piga,’ na ‘kulima.’ Maneno yasiyofuata muundo huu ni kama vile, ‘mfupi,’ ‘mbuzi,’ ‘nta,’ ‘ndoa,’ na ‘nguo.’

Nne, lugha za Kibantu huunganisha mofimu ili kuunda neno au sentensi ya neno

moja. Mofimu ni kipashio kidogo kabisa chenye maana ambacho huunda neno. Kwa mfano, neno la Kiswahili “alichokipigania” linaweza kugawanywa katika mofimu nane, yaani, a – li – cho – ki – pig – an – i – a . Maana ya vipashio hivi ni kama ifuatavyo:

a - kiambishi cha nafsi ya tatu katika umoja. li - kiambishi cha wakati uliopita. cho - kiambishi cha urejeshi. ki - kiambishi cha ngeli ya saba. pig - mzizi au kiini cha kitenzi. an - kiambishi cha jinsi ya kutendana. i - kiambishi cha jinsi ya kutendea. a - kiishio. Tano, katika lugha za Kibantu kuna uwezekano wa kuunda majina (nomino)

kutokana na vitenzi, kuunda vitenzi kutokana na majina, kuunda vitenzi kutokana na vivumishi, na pia kuunda majina kutokana na vivumishi, kama inavyodhihirika katika mifano ifuatayo:

Kitenzi Jina Jina Kitenzi cheza - mchezo moto - motisha imba - wimbo hamasa - hamasisha Kivumishi Kitenzi Kivumishi Nomino bora - boresha bora - ubora safi - safisha safi - usafi Hata hivyo, ulinganifu huo wa kisarufi haumaanishi kwamba hakuna tofauti

zozote za kiisimu kati ya Kiswahili na lugha zingine za Kibantu. Kwa mfano, tofauti moja inayojitokeza ni kwamba Kikuyu, Kikamba na Kiluyia ni lugha za toni lakini Kiswahili sio lugha ya toni. Lugha ya toni ni lugha ambayo hutofautisha maana za maneno kutegemea mpando au mshuko wa sauti katika silabi za neno, kwa mfano:

Kikuyu Kikamba Kiluyia iria - ‘maziwa’ mwaki - ‘moto’ ingira - ‘njia’ iria - ‘ziwa’ (lake) mwaki - ‘mwashi’ ingira - ‘ingia’

11

Ukosefu wa toni katika Kiswahili sio sababu muhimu ya kutilia shaka ubantu wa lugha hii. Hii ni kwa sababu hakuna utafiti uliowahi kufanywa ukathibitisha kwamba lugha zote za Kibantu barani Afrika ni za toni (Chimera, 1998:29). Kwa ujumla, ushahidi wa kihistoria na kiisimu uliotolewa unathibitisha kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu. Hata hivyo, kuna matatizo yafuatayo ambayo humkumba mtafiti wa Kiswahili anayetegemea ushahidi wa kihistoria:

Kwanza, kuna uwezekano kwamba mambo mengi yaliyosimuliwa yalisahaulika

kabla ya kuwekwa katika maandishi. Pili, huenda ikawa baadhi ya wasafiri walionakili habari za pwani walikuwa wakieneza uvumi, kama yule Mgiriki anayesemekana kuwa aliandika kitabu akiwa huko Alexandria. Tatu, miswada mingi iliyokuwa na habari muhimu kuhusu historia ya Kiswahili ilipotea wakati wa vita, mingine iliteketea, mingine iliibwa na Wazungu waliokuwa wakiikusanya wakaipeleka Ulaya, mingine ilifichwa na familia za Waswahili na mingine iliharibika tu kutokana na unyevu, mvua au kuliwa na mchwa. Mwisho, hati za Kiarabu zilizotumiwa kuandikia miswada hazikuwa na baadhi ya herufi za Kiswahili; hali hii ilitatiza sana shughuli za kuyatafsiri maandishi hayo ya Kiarabu kwa Kiswahili kwa sababu baadhi ya maneno hayakuendelezwa sawasawa.

Zoezi la 1.4

* Kwa kutoa mifano, fafanua vipengele vitano vya kiisimu vinavyothibitisha kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu

1.6 Hitimisho

Katika somo hili nimejadili chanzo cha lugha ya Kiswahili kwa kuzingatia

nadharia tatu. Kulingana na ushahidi uliopo, inaelekea kwamba Kiswahili ni lugha halisi ya Kiafrika yenye asili ya Kibantu. Lugha hii ilikuwa ikizungumzwa sehemu za pwani ya Afrika Mashariki kabla ya kuja kwa Waarabu na Wazungu. Kama vile Mbotela (1999:12) anavyosema, “…ingawa jina la lugha ni la asili ya Kiarabu, lugha yenyewe ni ya asili ya Kibantu.” Athari za kigeni zinazopatikana katika Kiswahili ni jambo lisiloweza kuepukika; hii ni kwa sababu ya ushirikiano uliokuwepo kwa muda mrefu baina ya Waswahili na wageni waliotembelea mwambao wa Afrika Mashariki.

Katika somo lijalo, nitazungumzia vyombo vilivyosaidia kueneza Kiswahili

kutoka pwani hadi bara.

12

1.7 Maswali

? 1. “Ushahidi wa kihistoria ni muhimu katika kujadili swala la chimbuko la

Kiswahili.” Jadili kauli hii kwa kurejelea ushahidi huo. 2. Huku ukidondoa ushahidi wa kiisimu, jadili madai kwamba Kiswahili ni

lugha asili ya Kiafrika. 3. “Kama Kiswahili si lahaja ya Kiarabu, basi ni lugha ya mseto.” Tathmini

madai haya. 1.8 Marejeleo ya Lazima Chacha, L. M. (1995). “Chimbuko la Kiswahili,” katika BARAGUMU, Juzuu la 2 Nam.

1&2 uk. 1-17. Chimerah, R. M. (1998). Kiswahili: Past, Present and Future Horizons. Nairobi: Nairobi

University Press. Chiraghdin, S. na M. Mnyampala (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: O.U.P. Mbaabu, I. (1985). New Horizons in Kiswahili. Nairobi: Kenya Literature Bureau. Ndungo, C. na W. Mwai (1991). Kiswahili Part Two: Historical Modern Development in

Kiswahili. Nairobi: Nairobi University Press. *** Marejeleo ya ziada yanapatikana katika somo la mwisho.

13

SOMO LA 2

MAENEZI YA KISWAHILI 2.0 Utangulizi

Lugha ya Kiswahili haizungumzwi tu Afrika Mashariki pekee, bali imeenea hadi

Afrika ya Kati na hata kuvuka mipaka ya Bara Afrika. Je, Kiswahili kilienezwa vipi kutoka pwani hadi bara ya Tanzania, Kenya, Uganda, na Afrika ya Kati? Katika mada hii, nitavijadili vyombo vitatu vilivyochangia kukuza na kusambaza Kiswahili kutoka pwani hadi bara kabla ya uhuru. Vyombo hivyo ni, misafara ya Waarabu, utawala wa Wakoloni na Wamishenari pamoja na Walowezi. Msafara ni kikundi cha watu wanaosafiri pamoja; Mkoloni ni mtu anayetawala katika nchi ambayo si yake kwa niaba au kwa manufaa ya nchi yake; Mishenari ni kikundi cha watu wanaotumikia na kueneza dini hasa ya Kikristo; na Mlowezi ni mtu aliyehamia katika nchi isiyokuwa yake akachukua ardhi na kujenga huko.

2.1 Madhumuni

Baada ya kulipitia somo hili, ninatarajia kwamba utaweza: (i) Kueleza jinsi Waarabu walivyochangia kukua na kuenea kwa Kiswahili

bara. (ii) Kueleza jinsi utawala wa Wajerumani na Waingereza ulivyoathiri kukua

na kuenea kwa Kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki kabla ya uhuru. (iii) Kufafanua mchango wa Wamishenari na Walowezi katika ukuzaji na

usambazaji wa Kiswahili bara.

2.2 Misafara ya Waarabu

(A) TANGANYIKA Kufikia mwisho wa karne ya kumi na nane, lugha ya Kiswahili ilikuwa ingali

yatumiwa kama chombo cha mawasiliano ya wakazi wa pwani na visiwani pekee. Lakini kuanzia karne ya kumi na tisa, lugha hii ilianza kupenya sehemu za bara ikitumiwa kama chombo cha mawasiliano ya kibiashara. Huu ulikuwa wakati wa enzi ya Seyyid Said na wanawe, ambapo kisiwa cha Unguja kilikuwa kimestawi sana katika biashara.

Kwa mujibu wa Whiteley (1969:42), misafara mingi ya wafanya biashara

iliondoka pwani ya nchi ya Tanganyika ikielekea bara kuanzia mwaka 1800 hadi 1850. Misafara hiyo ilikuwa ikiongozwa na Waarabu, miongoni mwao alikuwa Hamed bin

14

Muhammed el Murjebi, yaani “Tippu Tip.” Wadhamini wa misafara hiyo walikuwa Wahindi matajiri waliokuwa wakifanya biashara pwani; lakini kuanzia mwaka 1839, Seyyid Said pia alianza kuwa mdhamini baada ya kugundua kuwa misafara hiyo ingeweza kustawisha zaidi uchumi wa kisiwa maarufu cha Unguja.

Tippu Tip alifanya safari yake ya tatu kutoka Unguja hadi Zaire (Jamhuri ya

Kidemokrasia ya Congo) mnamo mwaka 1870 baada ya Kristo, na alikuwa na wafuasi wengi sana waliomsaidia kubeba bidhaa za thamani kubwa kutoka pwani kwenda bara. Kwa mfano, kumbukumbu za kihistoria zasema kwamba walipofika Urungu karibu na Ziwa Tanganyika, walikuwa takriban watu 4,000. Hii ina maana kwamba msafara huo ulipoanza ulikuwa na watu wengi zaidi, lakini baadaye wakaanza kupungua kwa sababu wengine walifia njiani kutokana na mateso ya biashara hiyo ya utumwa. Sehemu ambazo misafara hiyo ilipitia ni pamoja na Unyamwezi, Tabora, Ujiji, Urungu na Katanga. Bidhaa walizobeba kwenda kuuza bara ni pamoja na shanga, nguo, bizari, baruti, na sabuni.

Whiteley (1969:49) anasema kwamba ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha kwamba Kiswahili kilitumiwa katika misafara hiyo, inajulikana kuwa misafara yenyewe ilishirikisha watu kutoka pwani waliozungumza Kiswahili. Tippu Tip mwenyewe anasema kwamba msafara wake uliwashirikisha wafuasi 500 kutoka Unguja na wengine walikuwa wakichukuliwa kutoka njiani. Pia alikuwa akiwaita wafuasi wake “Waungwana,” ambao yamkini walikuwa Waswahili kutoka pwani. Naye Mbaabu (1991:2) anasema kwamba kwa vile misafara hiyo ilipitia katika maeneo ya wazungumzaji wa lugha tofauti, huenda ikawa wasafiri hao walitumia Kiswahili kwa kuwasiliana, kwa hivyo wakasaidia kukieneza Kiswahili bara.

Ushahidi uliopo unaonyesha kwamba kulikuwa na misafara mingi nchini

Tanganyika kuliko nchini Kenya, na misafara hiyo ilikuwa ikianzia Kilwa, Bagamoyo na Pangani ikielekea bara. Katika sehemu ifuatayo, tutaangalia jinsi hali ilivyokuwa nchini Kenya.

(B) KENYA

Nchini Kenya kulikuwa na misafara michache ambayo ilikuwa ikianzia Mwembe Tayari, Lamu na Malindi ikielekea bara. Kulingana na Whiteley (1969), misafara hiyo ilikuwa michache kwa sababu ilitatizwa na mambo yafuatayo:

Kwanza, Wamaasai walikuwa tishio kwa wafanya biashara kwa sababu

hawakukubali msafara wowote kupenya eneo lao, kwani wangeuteka nyara na kupora bidhaa na hata kuwadhuru wafanya biashara. Pili, baadhi ya makabila kama vile Wakikuyu na Wanandi hawakuwa na moyo wa kushirikiana sana na Waswahili. Mbaabu (1991:5) anasema kuwa Shiundu, kiongozi wa Wanga, na mwanawe Mumia ndio walioshirikiana sana na Waswahili. Tatu, vita vya kuvizia vilivyopiganwa na Wamazrui ili kupinga utawala wa Seyyid Said viliathiri pwani ya Mombasa na vitongoji vyake na kuifanya biashara kuwa ya hatari; kwa hivyo misafara mingi haikuenda bara. Mwisho, hali ya ukame iliyopatikana katika baadhi ya sehemu za Kenya ilikuwa pingamizi kubwa kwa wasafiri. Kwa mfano, katika Mkoa wa Mashariki na Mashariki Kaskazini, kulikuwa na kiangazi, ukosefu wa maji na wanyama wa pori (Mbaabu, 1985:5).

15

Licha ya kukumbwa na matatizo hayo, kuna ushahidi unaothibitisha kwamba kuna misafara michache iliyoweza kupenya hadi sehemu mbalimbali nchini Kenya. Kwa mfano, wasafiri hao walibuni mitaa sehemu za bara ambayo majina yake ni ya kutoka pwani. Mjini Nairobi, mitaa hiyo ni kama vile Pangani, Pumwani na Shauri Moyo. Mitaa hii bado ina athari za mambo ya kipwani; kwa mfano, mtaa wa Pangani umeathiriwa sana na dini ya Kiislamu (Bujira, 1974). Hali kadhalika, kufikia sasa kuna baadhi ya watu wanaoishi katika vituo vya misafara sehemu za bara ambao asili yao ni pwani. Vile vile kuna watu wengine huko pwani wenye asili ya bara, hasa waliotoka Ukambani (Chiraghdin & Mnyampala, 1977:72).

Zoezi la 2.1

* Eleza kwa nini wafanya biashara Waarabu walifanikiwa sana kueneza Kiswahili nchini Tanganyika kuliko nchini Kenya. Kuna pia ushahidi unaoonyesha kwamba Wamaasai hawakuwa wakatili wakati

wote, kinyume na wanavyodhaniwa. Kwanza, kulikuwa na Mzungu aliyeitwa Thomas ambaye alienda Umasaini akiongozwa na misafara ya Waarabu. Pili, Mzungu mwingine aliyeitwa Lugard alipitia Malindi kuelekea Uganda akiongozwa na misafara hiyo. Tatu, mfanya biashara aliyejulikana kama Sudi wa Muslimi alikuwa akibeba ng’ombe wa morani kutoka Umasaini akipeleka pwani. Mwisho, mfanya biashara mwingine kwa jina Umari wa Kombo, alikuwa akibeba nta na shanga kutoka Malindi akipeleka sehemu za Kajiado ambako alipata pembe za ndovu na ngozi za chui na simba. Kwa hivyo, huenda ikawa madai yaliyotolewa dhidi ya Wamaasai yalitokana na uhasama wa kikabila. Huenda ikawa viongozi wa kikabila, kama vile Chifu Kivoi wa Ukambani, ndiyo waliokuwa wakieneza uvumi huo kama njama ya kuwazuia Waarabu kufanya biashara na Wamaasai. Huenda ilikuwa hivyo kwa sababu Salim (1973:31) anasema kwamba Kivoi alikuwa mfanya biashara mashuhuri na pia rafiki mkubwa wa Liwali wa Mombasa. McIntosh katika Ogot (1968:213) pia anasema kwamba Chifu Kivoi alijulikana sana kwa Waarabu wa Mombasa.

Katika sehemu inayofuata, tutaangalia jinsi ambavyo Kiswahili kilienezwa nchini Uganda na pia katika Afrika ya Kati.

(C) UGANDA

Misafara ya Waarabu ilifika pia nchini Uganda na kueneza Kiswahili huko. Tippu Tip anasema kuwa mfalme wa Buganda, Kabaka Mutesa, alikuwa akiwatuma Waarabu wakamletee bidhaa kutoka pwani kisha akawalipa pembe za ndovu. Kabaka Mutesa alijifunza Kiswahili na Kiarabu na alizingatia pia sherehe ya Kiislamu ya kila mwaka ya kufunga Ramadhani tangu mwaka 1867 hadi 1877 baada ya Kristo.

Hali kadhalika, lugha ya Kiswahili ilitumiwa kila siku katika makao makuu ya

Kabaka; pia ilitumiwa katika shughuli za biashara na hata kueneza dini ya Kiislamu. Vile

16

vile, maandishi ya Kiswahili yalianza kutumika katika baraza za kifalme za Buganda na Bunyoro kabla ya kuja kwa Waingereza. Kwa hivyo, ni dhahiri kwamba misafara hiyo ilichangia pakubwa kueneza Kiswahili bara. Je, hali ilikuwa vipi huko Afrika ya Kati?

(D) AFRIKA YA KATI

Misafara ya Waarabu ilieneza Kiswahili hadi nchini Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) kabla ya wakoloni wa Kibelgiji kufika huko. Wenyeji wa Zaire waliwaita walioshiriki katika misafara hiyo “Waungwana,” kumaanisha “watu huru,” na lugha yao ya Kiswahili wakaiita “Kingwana,” yaani lugha ya watu huru. Makabila ya Zaire yaliyokutana na misafara ya Waarabu, kama vile Wamanyema na Wabangubangu, yalianza kujifunza lugha ya Kingwana (Kiswahili) ili kurahisisha mawasiliano ya kibiashara.

Waarabu walifanya juhudi za kuanzisha nchi huru ya Zaire kwa jina “Congo Free State” lakini wakashindwa na watawala wa Kibelgiji. Kwa hivyo, baadhi ya Waarabu walitoroka wakarudi Tanganyika na kwingineko, lakini wengi walibaki wakaendelea kutumia Kingwana katika sehemu kama vile Kassongo, Tongoni na Myangwe. Baadhi ya Waarabu hao walifika pia nchini Burundi na kusambaza Kiswahili hasa mjini Bujumbura, lakini hawakuruhusiwa kuingia nchini Rwanda wakati huo (Ndungo & Mwai, 1991:89-90).

Kutokana na maelezo hayo, inadhihirika kwamba zifuatazo ndizo athari kuu za

Waarabu katika kukuza na kueneza Kiswahili bara: (i) Hati za Kiarabu Waarabu walileta hati zilizotumiwa katika maandishi ya Kiswahili. Kutokana na

haya, mambo mengi yaliweza kuhifadhiwa kwa maandishi ikiwa ni pamoja na fasihi simulizi ya Kiswahili. Kwa njia hii, Kiswahili kiliweza kukua na kuenea kwa vile maandishi hayo yangesomwa na yeyote yule aliyejua kusoma. Hata hivyo, mara nyingine hati za Kiarabu zilihitilafiana na matamshi halisi ya Kiswahili, jambo ambalo lilitatiza juhudi za kutafsiri maandishi hayo. Kwa mfano, sauti za Kiswahili ambazo hazimo katika hati za Kiarabu ni pamoja na /e/, /o/, /ch/, /ny/, /ng’/ na /v/.

(ii) Biashara Misafara ya wafanya biashara Waarabu ilikuwa ikitumia Kiswahili kwa

mawasiliano na hivyo basi lugha hii ikaenea sehemu mbalimbali. Biashara hiyo ilikiwezesha Kiswahili kukopa maneno tofauti kutoka lugha za kigeni na hivyo kuupanua msamiati wake. Aidha, matumizi ya Kiswahili yalijikita zaidi katika vituo mbalimbali vilivyokuwa kwenye njia za misafara hiyo ya wafanya biashara. Hata hivyo, biashara hiyo ilikiuka maadili na haki za kibinadamu kwa sababu watumwa waliteswa sana.

(iii) Dini ya Kiislamu Waarabu walipowasili walianza kueneza dini yao ya Kiislamu kwa wenyeji wa

pwani ya Afrika Mashariki na hata bara. Walianzisha madrassa ambayo walitumia kufundishia Waafrika dini ya Kiislamu. Lugha ya Kiswahili ilitumiwa kuwafundishia Waafrika kusoma na kuandika kwa hati za Kiarabu ili kuielewa Qur’an tukufu. Mafunzo hayo yaliwawezesha Waafrika kuandika mambo mengi kwa Kiswahili na kuyasambaza

17

kwa watu wengi wa bara. Hali hii ndiyo iliyosababisha madai kwamba ‘Kiswahili na Uislamu haviwezi kutenganishwa.’ Baadhi ya watu walikipinga Kiswahili kwa sababu walikinasibisha na dini ya Kiislamu na hivyo basi wakakizuia kuenea sehemu zingine. Miongoni mwa watu hao walikuwa Wamishenari kwa sababu walihofia kwamba dini ya Kiislamu ingewazuia kueneza dini yao ya Kikristo. Hapo awali, tulitaja kwamba baadhi ya mitaa iliyobuniwa na wasafiri kutoka pwani, kama vile Pangani, bado inadhihirisha athari za Kiislamu.

(iv) Ndoa Waarabu walipofika pwani walianza kufunga ndoa na Waswahili. Hali hii

ilisababisha kizazi kipya cha Waswahili ambao walikopa maneno mengi ya Kiarabu na hivyo kuukuza msamiati wa lugha hii. Baadhi ya maneno hayo yalihusu dini, biashara, vyakula na vyombo vya kusafiria. Hali hii pia imedunisha Kiswahili kwa sababu baadhi ya watu walianza kufikiria kwamba Kiswahili ni lugha ya kigeni iliyoletwa na Waarabu.

Kwa muhtasari, athari za Waarabu zilikuwa nzuri kwa kiasi kikubwa kwani

walisaidia sana kueneza Kiswahili bara. Hata hivyo, tumegundua kwamba uzuri huo haukukosa dosari ambazo pia zimechangia kukitweza Kiswahili kwa upande mwingine. Kwa hivyo tunaweza kuhitimisha mchango wa Waarabu katika maenezi ya Kiswahili kwa methali kwamba, ‘Uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti;’ au ‘Uzuri wa kuyu ndani mabuu.’ Sasa tuangalie mchango wa wakoloni katika kueneza Kiswahili bara.

2.3 Utawala wa Wakoloni

(A) TANGANYIKA (i) Kipindi cha Wajerumani

Je, Wajerumani walichangia vipi maenezi ya Kiswahili nchini Tanganyika kabla ya uhuru? Wajerumani walitawala Tanganyika kati ya mwaka 1885 na 1916. Walipokuja walikuta kwamba lugha ya Kiswahili ilikuwa imeenea sana nchini humo kutokana na misafara ya Waarabu. Hata hivyo, badala ya kuchagua Kiswahili kama lugha ya utawala, waliamua kutumia lugha ya Kijerumani katika utawala na elimu. Walijaribu kufunza masomo yote kwa Kijerumani katika shule walizozianzisha lakini juhudi hizo hazikufua dafu. Hii ni kwa sababu hawakuzingatia ukweli kwamba Kiswahili ndiyo lugha iliyokuwa imeenea zaidi nchini Tanganyika wakati huo. Kwa hivyo punde si punde iliwabidi wabadili nia yao na kutumia Kiswahili katika utawala na elimu. Inaelekea kwamba walifanya hivyo kwa maslahi yao wenyewe wala si kwa maslahi ya wananchi wa Tanganyika.

Whiteley (1971) anasema kwamba Wajerumani waliamua kukitumia Kiswahili

katika utawala na shuleni kwa sababu waliogopa kwamba kama Waafrika wangeendelea kufunzwa Kijerumani, lugha hii ingewawezesha kusoma maandishi “hatari” ambayo yangeamsha ari yao ya kisiasa. Vile vile, Chiraghdin (1977:69) anamnukuu Marcia Wright (1965) ambaye alidai kwamba, sababu moja iliyotolewa na wenyeji Wajerumani ya kutotoa mafunzo hayo kwa Kijerumani ni kwamba:

“…ni bora na ni busara kisiasa tusimfunulie Mwafrika siri yetu kwa yeye kukijua Kijerumani.”

18

Maana ya usemi huu ni kwamba, maandishi ya Kijerumani yangewawezesha Waafrika kujifunza mambo mengi yanayohusiana na harakati za ukombozi, na hatimaye wangemgeukia Mjerumani na kumpiga vita ili kumfukuza kutoka nchini Tanganyika. Hata hivyo, Wajerumani walisaidia kukuza na kueneza Kiswahili kwa njia zifuatazo:

Kwanza, waliwalazimisha wafanya kazi wote wa serikali kujifunza Kiswahili. Yeyote ambaye hangekimudu Kiswahili hakuruhusiwa kuajiriwa katika serikali ya Mjerumani. Hali hii iliwatia ari Waafrika wengi ambao walianza kujifunza Kiswahili ili wapate fursa ya kuajiriwa.

Pili, Wajerumani nao walilazimika kujifunza Kiswahili ili waweze kutumika

katika utawala huo. Walipotoka Ujerumani walishauriwa kujifunza Kiswahili huko kwao kabla ya kuja Tanganyika, na hali hii ilikisaidia Kiswahili kuenea sana. Hata hivyo, baadhi ya Waafrika walikipinga Kiswahili kwa sababu walikinasibisha na utawala dhalimu wa Mjerumani.

Tatu, watawala Wajerumani waliwateua wawakilishi wao, yaani akida, (kwa

majina mengine jumbe au liwali), katika sehemu mbalimbali za nchi na wawakilishi hao walipaswa pia kujifunza Kiswahili. Aidha, ripoti zote walizotoa kwa viongozi wao Wajerumani ziliandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Ripoti yoyote ambayo haikuandikwa kwa Kiswahili ingeweza kupuuzwa, na hivyo basi hali hii ilichangia sana kukua na kuenea kwa Kiswahili. Hata hivyo, baadhi ya Waafrika walikipinga Kiswahili kwa sababu walikinasibisha na hao maakida, ambao walikuwa wakiwakilisha utawala wa dhuluma.

Nne, wafanyakazi wengine kama vile makarani walikuwa wakihamishwa kila

mara kutoka sehemu moja hadi nyingine. Katika uhamishaji huo, Kiswahili kilitumiwa kwa vile wafanyakazi wangepelekwa sehemu yoyote bila kujali kama wangefahamu lugha ya wenyeji wa huko au la. Kwa sababu hiyo, Wajerumani walianzisha shule kwa madhumuni ya kuwafunza Waafrika wachache ambao wangetumika serikalini kufanya kazi ndogondogo kama za ofisini, mahakamani na katika ulinzi. Hatua hii ilisaidia lugha ya Kiswahili kukua na kuenea kwa sababu ilitumiwa kufundishia shuleni.

Mwisho, Wajerumani walianzisha mashamba makubwa ya kahawa, majani chai

na mkonge; katika mashamba hayo, wafanyakazi walikuwa Waafrika kutoka pwani na bara mwa Tanganyika ambao walitumia Kiswahili kuwasiliana. Hali hii ilieneza sana matumizi ya Kiswahili katika mashamba ya aina hii. Hali kadhalika, wafanyakazi hao waliporejea makwao waliendelea kutumia Kiswahili na hata wakaingiza katika lugha hii maneno kutoka lugha zao za kwanza, hivyo basi wakachangia upanuzi wa msamiati wa Kiswahili. Mifano ya maneno hayo ni kama vile ‘Bunge’ kutoka lugha ya Ha na ‘Ikulu’ kutoka lugha ya Kinyamwezi. Tuangalie sasa hali ilivyokuwa wakati wa utawala wa Waingereza.

19

(ii) Kipindi cha Waingereza

Je, Waingereza walichangia vipi maenezi ya Kiswahili nchini Tanganyika kabla ya uhuru? Utawala wa Waingereza uliingia nchini Tanganyika baada ya vita vikuu vya kwanza vya ulimwengu vilivyotokea kati ya mwaka 1914 na 1918. Waingereza walisaidia kueneza Kiswahili kwa njia zifuatazo:

Kwanza, walianza kutumia Kiswahili kufundishia katika shule za msingi nayo

lugha ya Kiingereza ikatumiwa kufundishia katika shule za sekondari na vyuo. Katika viwango vya juu vya elimu, lugha ya Kiswahili ilifundishwa tu kama somo miongoni mwa masomo mengine. Hata hivyo, kutokana na sera hiyo Kiswahili kilipewa nafasi ya chini ofisini kwa sababu kilitumiwa na watu wa tabaka la chini.

Pili, watumishi wote wa serikali na wale wa madhehebu ya kidini waliamrishwa

kuufanya na kufuzu mtihani mgumu wa Kiswahili kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi zilizohusiana moja kwa moja na maisha ya wananchi. Kazi hizo ni pamoja na biashara, kilimo na uinjilisti.

Tatu, lugha ya Kiswahili pia ilitumiwa mahakamani katika kushughulikia kesi za

Waafrika. Ingawa ripoti na hukumu za kesi hizo ziliandikwa kwa Kiingereza, baadaye zilitafsiriwa kwa Kiswahili ili kuwawezesha washtakiwa kuzielewa.

Mwisho, Waingereza pia walikitumia Kiswahili kama lugha ya jeshi zima

lililoitwa King’s African Rifles (K.A.R), yaani ‘Jeshi la Waafrika la Mfalme.’ Jeshi hili lilikuwa likitumika katika nchi zote za Afrika Mashariki, na kwa njia hii Kiswahili kiliweza kukua na kuenea bara.

Ni dhahiri kwamba ingawa Waingereza walikitumia Kiswahili kueneza siasa zao

nchini Tanganyika, lugha iliyotumiwa kutekeleza shughuli muhimu za serikali ni Kiingereza. Mwafrika angeweza tu kuajiriwa kazi za ngazi za juu pamoja na kupandishwa cheo haraka kazini iwapo alifaulu vyema katika lugha ya Kiingereza. Kwa hivyo, ijapokuwa lugha ya Kiswahili ilisisitizwa sana shuleni, ofisini na kufanywa katika mitihani, ilipewa tu nafasi ya pili baada ya Kiingereza. Kwa sababu hiyo, utawala wa Waingereza ulishusha pia hadhi ya Kiswahili nchini Tanganyika. Sera yao kuhusu lugha iliwafanya wananchi kukichukia Kiswahili na kukiona kama lugha duni ambayo haingewafaa sana isipokuwa katika viwango vya chini. Sasa tuangalie hali ilivyokuwa nchini Kenya wakati wa utawala wa Waingereza.

(B) KENYA Kipindi cha Waingereza Kusudi la Waingereza nchini Kenya lilikuwa kudidimiza Kiswahili tangu

mwanzo wa utawala wao (Ndungo & Mwai, 1991:145). Walitatiza maenezi ya Kiswahili kwa njia zifuatazo:

Kwanza, walikitumia Kiswahili kuendesha shughuli zao za kiutawala kama vile

kuwekeana mikataba na wenyeji, na walifanya hivyo kwa maslahi yao wenyewe. Kwa

20

mfano, mkataba uliowekwa baina ya kampuni ya Imperial British East Africa (I.B.E.A) na Ketonga, kiongozi wa Ukambani, mnamo mwaka 1887 uliandikwa katika Kiswahili na Bw Bashir Mchangamwe.

Pili, Waingereza waliwatawala wenyeji kimabavu huku wakiwatumia Waswahili,

kwa hivyo Kiswahili kilihusishwa na utawala wa dhuluma. Kwa sababu hii, watu wengi wa bara walianza kukipinga Kiswahili na kukizuia kuenea. Wenyeji wa bara waliwaona Waswahili kama watu wadanganyifu waliotumiwa na Waingereza kama vikaragosi au vibaraka ili kuimarisha utawala wa kikoloni. Kufikia leo kuna baadhi ya watu wanaoamini kwamba Mswahili ni mtu asiyeaminika pamoja na lugha yake; eti asili yake haijulikani, lugha yake (Kiswahili) hutumiwa tu kuwadanganya watu, na hivyo basi mtu yeyote anayezungumza lugha hii haaminiki. Hii ndiyo sababu unapozungumza na mtu ambaye haamini ukweli wa yale unayosema, huenda akakwambia kwamba “wewe ni Mswahili” au “usiniletee Kiswahili chako.”

Tatu, katika elimu, Waingereza walisisitiza matumizi ya Kiingereza na lugha za

kwanza huku wakipuuza Kiswahili. Sera hii iliimarishwa zaidi hasa baada ya Vita Vikuu vya Pili ambapo serikali ya kikoloni ilihofia kwamba huenda Waafrika wakakitumia Kiswahili kama chombo cha kuwaunganisha dhidi ya wakoloni. Kwa hivyo, walianza kuhimiza matumizi ya lugha za kwanza shuleni ili kuwagawanya Wakenya katika misingi ya kikabila ndipo waweze kuwatawala bila shida. Kulingana na Chacha Nyaigoti Chacha (2001), Waingereza walikuwa maadui wakubwa wa Kiswahili kwa sababu “sera zao hazikuwa na mwelekeo mzuri hasa nchini Kenya; walifurahia kuwaona watu katika makabila”.

Ingawa Waingereza walitatiza maenezi ya Kiswahili kwa njia hizo, ni kweli pia

kwamba walichangia maendeleo ya lugha hii kwa namna nyingine. Kama anavyosema Gorman (1974), kuanzishwa kwa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (K.K.A.M) mnamo mwaka 1930, na Shirika la uchapishaji vitabu la East Africa Literature Bureau mnamo mwaka 1948, kulitokana na sera ya kikoloni ya Waingereza. Hebu tuangalie jinsi hali ilivyokuwa nchini Uganda katika sehemu inayofuatia. Zoezi la 2.2

* Eleza kwa nini baadhi ya viongozi wa kikabila walikubali au kukataa kushirikiana na watawala wa kikoloni nchini Kenya. (C) UGANDA Kipindi cha Waingereza Nchini Uganda, lugha ya Kiswahili haikupewa nafasi ya kuenea kwa sababu

ilipingwa vikali na Waganda na Wamishenari. Waingereza nchini Uganda walitambua umuhimu wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano katika Afrika ya Mashariki. Kwa

21

hivyo, walipendekeza kwamba Kiswahili kiwe lugha rasmi ya utawala na mafunzo shuleni.

Watawala hao waliandaa vikao mbalimbali ili kujadili swala la lugha ambapo mapendekezo yalitolewa kuhusu kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi. Mnamo mwaka 1927, Gavana wa Uganda aliyejulikana kama W. G. Gowers, aliandika makala ambamo alitoa mapendekezo kwamba Kiswahili kitumiwe kufundishia katika eneo kubwa la utawala wao isipokuwa katika himaya ya Buganda. Aidha, alipendekeza kwamba lugha ya Kiswahili iongezwe katika orodha ya masomo katika Buganda, Bunyoro, Tororo na Ankole. Mapendekezo hayo yalilenga katika kufuata mfano wa Kenya na Tanzania kwani Gavana huyo alitaka Kiswahili kisomeshwe kuanzia shule za msingi.

Lakini Waganda, wakiongozwa na Mfalme Kabaka Chwa, waliyapinga vikali

mapendekezo hayo ya Waingereza huku wakitoa sababu zifuatazo: Kwanza, walisema kwamba kukubali matumizi ya Kiswahili nchini mwao lilikuwa jambo hatari kwani wangepoteza cheo na utukufu wa kabila la Baganda. Pili, walidai kwamba Waingereza walikuwa na njama ya kuziunganisha nchi zote za Afrika Mashariki kuwa jumuiya moja, kwa hivyo Waganda wangeweza kupoteza taifa lao la Buganda. Tatu, walidai kwamba lugha ya Kiswahili ilikuwa ya kigeni kwao ambayo ililetwa na Waarabu. Nne, walisema kwamba hawakuona haja ya kufundishwa Kiswahili shuleni eti kwa sababu ilikuwa rahisi kuijua lugha hii bila kuhitaji mafunzo yoyote. Mwisho, walidai kwamba walitamani sana kujifunza Kiingereza eti kwa sababu lugha hii ilikuwa “ufunguo wa kila kitu.” Kwa maoni yao, Kiswahili hakingewafaa kwa njia yoyote.

Ili kupinga kukua na kuenea kwa Kiswahili na badala yake kuendeleza Kiganda,

Waganda walichukua hatua zifuatazo: Kwanza, waliwachagua wajumbe wao kuwakilisha ufalme wa Buganda katika sehemu mbalimbali za nchi ya Uganda. Pili, walianza kutafsiri maandishi mbalimbali kwa lugha ya Kiganda. Kwa hivyo, kufikia mwanzo wa karne ya ishirini, Kiganda kilikuwa na maandishi mengi zaidi kuliko Kiswahili nchini humo.

Kufuatia maoni hayo ya Waganda, serikali ililazimika kupitisha matumizi ya

Kiingereza kama lugha rasmi ya utawala na kuanza kudidimiza Kiswahili. Kufikia mwaka 1953, Tume ya Kifalme ya Afrika Mashariki ilipiga marufuku matumizi ya Kiswahili nchini Uganda ili Waganda wasikitumie kama chombo cha kuwaunganisha dhidi ya utawala wa kikoloni. Sasa tuangalie jinsi Wamishenari na Walowezi walivyoathiri kukua na kuenea kwa Kiswahili katika Afrika Mashariki kabla ya uhuru.

2.4 Wamishenari na Walowezi

(A) TANGANYIKA Walowezi (au masetla) hawakuathiri sana kukua na kuenea kwa Kiswahili nchini

Tanganyika kwa sababu walikuwa wachache sana. Lakini Wamishenari walikuwa wengi mno na hivyo basi walichangia kukua na kuenea kwa Kiswahili kwa njia zifuatazo:

Kwanza, baadhi ya Wamishenari waliifanyia lugha ya Kiswahili utafiti na wakaandika vitabu. Kwa mfano, Askofu Edward Steere wa dhehebu la Universities Mission to Central Africa (U.M.C.A) aliandika kitabu kiitwacho A Handbook of the Swahili Language as Spoken in Zanzibar mnamo mwaka 1870, katika lahaja ya Kiunguja. Naye Ludwig Krapf wa dhehebu la Church Missionary Society (C.M.S)

22

aliandika kitabu kiitwacho Outline of the Elements of the Kiswahili Language with Special Reference to the Kinika Dialect mnamo mwaka 1850. Kitabu hicho alikiandika katika lahaja ya Kimvita. Pia aliandika kamusi inayoitwa Dictionary of the Swahili Language mnamo mwaka 1882 (Mbaabu, 1991:8-9).

Pili, Wamishenari walifungua shule nyingi ambazo zilitoa mafunzo katika fani

mbalimbali kama vile useremala na uashi, ambapo lugha ya kufundishia ilikuwa Kiswahili. Tatu, walianzisha vituo vya kueneza Injili ambapo lugha ya Kiswahili ilitumiwa katika mahubiri (Whiteley, 1969:53). Whiteley anasema kwamba aghalabu vituo hivyo vilijengwa kwenye njia za misafara ili kurahisisha mawasiliano baina ya Wamishenari hao. Kwa mfano, kulikuwa na vituo huko Mombasa, Zanzibar, Tanga, Bagamoyo, Ujiji na Tabora. Kwa mujibu wa Askofu Steere, lugha ya Kiswahili iliwafaa sana katika ‘kuzielezea fikira zao za kidini’ na pia ilikuwa kama ‘ufunguo wa kuzijulia lugha zingine za pande hizi za Afrika.’ Nne, walitafsiri maandiko ya Biblia kwa Kiswahili ili Waafrika waweze kujisomea kwa urahisi, na pia wakatunga nyimbo za kiroho, kwa mfano ‘Tenzi za Rohoni.’

Mwisho, Wamishenari walianza kuchapisha magazeti kwa lugha ya Kiswahili.

Kwa mfano, gazeti la ‘Habari za Wakilindi’ lilianzishwa mwaka wa 1905 na dhehebu la U.M.C.A. Gazeti la ‘Pwani na Bara’ lilianzishwa mwaka wa 1910 na dhehebu la German Protestant Missionaries. Nalo gazeti la ‘Rafiki Yangu’ lilianzishwa mwaka wa 1910 na dhehebu la Wakatoliki ambapo maudhui yake yaliegemea upande wa dini. Kulikuwa pia na madhehebu mengine kama vile White Fathers, The French Holy Ghost Fathers, The London Missionary Society, na German Protestant Missionaries. Kwa vile magazeti haya yote yaliandikwa kwa Kiswahili, yalichangia sana kukua na kuenea kwa lugha hii. Hata hivyo, lengo la baadhi ya Wamishenari hao lilikuwa kumsaidia Mjerumani kuudhibiti utawala wake nchini humo.

(B) KENYA Maoni ya Walowezi, Wamishenari na Watawala wa kikoloni kuhusu sera ya

lugha nchini Kenya yalihitilafiana kila mara kwa sababu makundi haya yote yalikuwa na malengo tofauti. Wamishenari walikuwa katika mstari wa mbele kuhusu mambo ya elimu nchini Kenya, kwani shule nyingi zilizokuwepo nchini humu wakati wa utawala wa Mwingereza zilikuwa mikononi mwao. Lakini mtazamo wao kuhusu matumizi ya lugha shuleni ulihitilafiana kutoka dhehebu moja hadi lingine.

Mnamo mwaka 1901, dhehebu la United Missionary lilipendekeza kwamba lugha

za kikabila zitumiwe kufundishia katika miaka mitatu ya kwanza katika shule za vijijini na Kiswahili kitumiwe katika darasa la nne na la tano. Lakini serikali ya Mwingereza ilipendekeza kwamba Kiingereza kikuzwe kama lugha ya mawasiliano kote nchini. Bw Michael Grigg ambaye alikuwa Gavana alisisitiza kwamba hapangekuwa na matumizi ya lugha mbili katika mahakama yao au shuleni.

Msimamo huo wa serikali ulipingwa vikali na Walowezi na Wamishenari. Baadhi

ya Wamishenari walishikilia kwamba ingefaa watumie lugha za kikabila katika kueneza Injili badala ya kutumia Kiingereza. Waliamini kwamba ni rahisi kuifikia roho ya mtu na

23

kuzifikia fikira zake iwapo utaitumia lugha yake. Zaidi ya hayo, walishikilia kuwa ni rahisi kumfundisha mtoto katika lugha yake mwenyewe badala ya kutumia lugha ya kigeni.

Lakini baadhi ya madhehebu ya kidini yalipinga matumizi ya Kiswahili kwa madai kuwa Kiswahili ni lugha iliyofungamanishwa na Uislamu. Kwa hivyo, walifikiria kwamba kukuza Kiswahili ni sawa na kueneza Uislamu, jambo ambalo lingewazuia kueneza Ukristo. Hata hivyo, Wamishenari wengine waliona kwamba ni afadhali waendelee kutumia Kiswahili kwa vile hii ndiyo lugha iliyokuwa ikitumiwa na watu wengi. Kwa hivyo hawakuona haja ya kutumia Kiingereza wala lugha za kikabila.

Walowezi nao walipinga matumizi ya Kiingereza kama lugha ya mawasiliano

kwa madai kwamba, ‘kuwafundisha Waafrika Kiingereza ni kama kujivua nguo mbele yao’. Walisema kwamba kuwafunza Kiingereza ni kama kuwapa Waafrika chombo cha kisiasa ambacho wangetumia kupinga utawala wa Waingereza, na bila shaka hali hii ingetatiza juhudi zao za unyonyaji. Walishikilia kwamba kuwafunza Kiingereza kungeleta vurugu kwa vile Waafrika hao wangeanza kuunda vyama vya wafanyakazi ili kudai haki zao.

Walowezi hao walifikiria kwamba elimu ambayo ingewafaa Waafrika ni ile iliyowaandaa kufanya kazi za mikono na kazi hizi hazikuhitaji ujuzi wa lugha ya Kiingereza. Bw Grogan, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Walowezi, alisema kwamba hakuweza kufikiria tukio la hatari zaidi:

“…kuliko sisi (Waingereza) kuwafundisha lugha hii (Kiingereza) watu hawa (Waafrika) ambao elimu yao ya kufaa ni kufanya kazi mashambani.” Zaidi ya hayo, Walowezi hawakutaka kujifunza Kiswahili sanifu kwani

walikidharau sana. Waliamini kuwa Kiswahili ni lugha ya kusema na “maboi” na hivyo basi ni lugha duni. Walikuwa wakizungumza aina ya Kiswahili kilichokuwa na makosa mengi sana ya kisarufi ambacho kiliitwa Kisetla. Kutokana na kasumba hiyo ya Walowezi kuhusu Kiswahili, baadhi ya Waafrika waliathirika sana hivi kwamba walianza kukiona Kiswahili kama lugha duni iliyotumiwa kuwadharau.

Baada ya mabishano makali baina ya Watawala, Wamishenari na Walowezi,

maoni ya Walowezi yalichukuliwa na hivyo basi Kiingereza kikapigwa marufuku katika shule zote za Waafrika. Kupigwa marufuku kwa Kiingereza na kudharauliwa kwa Kiswahili ni miongoni mwa sababu zilizowafanya Waafrika kuanzisha shule zao ambazo zilitumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia. Wakikuyu ndiyo waliokuwa katika mstari wa mbele kwa kuanzisha shule zao zilizojulikana kama Kikuyu Independent Schools Association na Kikuyu Karinga Educational Association.

Hali kadhalika, vyama vya Waafrika vya kisiasa pia vilitumia Kiswahili kama

lugha ya kupigania uhuru. Kwa mfano, mnamo mwaka 1922, Harry Thuku alitumia Kiswahili kama chombo cha kuwaunganisha wafanyakazi Waafrika mjini Nairobi ili wapinge ubaguzi wa rangi na sheria za kikoloni zilizowalazimisha Waafrika kubeba vitambulisho (Ndungo & Mwai, 1991:63).

24

Mzozo huu kuhusu sera ya lugha nchini Kenya unathibitisha kwamba Kiswahili kilikuwa katika njia panda: Watawala wa kikoloni walikipinga eti kingewaunganisha Waafrika ilihali Walowezi walikiunga mkono wakidai eti ni lugha ya “maboi.” Baadhi ya Wamishenari pia walikipinga wakidai eti kilifungamana na dini ya Kiislamu, kwa hivyo wakapendekeza lugha za kikabila zitumiwe shuleni. Wengine nao wakakiunga mkono huku wakishikilia kwamba Kiswahili ni lugha mwafaka ya kuhubiria Injili.

Zaidi ya hayo, ufundishaji wa Kiswahili shuleni ulikumbwa pia na matatizo

mawili; kwanza, ni ukosefu wa vitabu vya kutosha, na pili, ni uhaba wa walimu wenye ujuzi wa kufundisha lugha hizo. Matatizo haya yote ndiyo yaliyosababisha kuanzishwa kwa tume zisizopungua kumi na tano nchini Kenya ili kushughulikia swala la sera ya lugha. Hata hivyo, utafiti uliofanywa na Gorman (1974) na Mbaabu (1991) umeonyesha kwamba, tume nyingi zilizoanzishwa zilipendekeza matumizi ya lugha za kikabila na Kiingereza na kupinga matumizi ya Kiswahili. Mifano ni kama vile Tume ya Phelps-Stokes (1924), Kamati kuhusu Elimu ya Juu (1941), Tume ya Beecher (1949) na Tume ya Kifalme ya Afrika Mashariki (1953-1955). Kwa hivyo, tume hizo zilizuia juhudi za kukuza na kueneza Kiswahili nchini Kenya kabla ya uhuru. Sasa tuangalie jinsi Wamishenari na Walowezi walivyochangia maenezi ya Kiswahili nchini Uganda.

Zoezi la 2.3

* Taja majina ya shule mbalimbali nchini Kenya zilizoanzishwa na Wamishenari. (C) UGANDA Kama ilivyokuwa kule Tanganyika, mchango wa Walowezi katika maenezi ya

Kiswahili nchini Uganda haukujitokeza kwa sababu walikuwa wachache mno. Lakini mchango wa Wamishenari ulijitokeza pale walipokitumia Kiswahili kueneza dini ya Kikristo. Kwa mfano, mnamo mwaka 1878, mzungu mmoja aliyeitwa Bishop Mackay alisema:

“Kwa bahati nzuri, Kiswahili kinafahamika sana. Nami nakijua vizuri na nina vipande vingi vya Agano la Kale na Agano Jipya kwa lugha ya Kiswahili. Basi mara nyingi huweza kumsomea Neno la Mungu mfalme na Baraza lake lote.”

Ingawa mwanzoni Wamishenari hao walikitumia Kiswahili kueneza dini ya

Kikristo, punde si punde walianza kukipinga huku wakidai kwamba kilifungamanishwa na dini ya Kiislamu. Kwa hivyo, walianza kupendekeza matumizi ya lugha ya Kiganda kama lugha ya mawasiliano, huku wakidai kwamba ni rahisi kuifikia roho ya mtu kwa kutumia lugha yake ya asili. Zaidi ya hayo, walidai kwamba Kiswahili ni lugha iliyotumiwa katika biashara ya watumwa, na hivyo basi walianza kuichukia. Kwa hivyo, huo uhasama baina ya dini ya Kiislamu na ya Kikristo, na pia kuihusisha lugha ya

25

Kiswahili na biashara ya utumwa, ni baadhi ya sababu zilizozuia kukua na kuenea kwa Kiswahili nchini Uganda kabla ya uhuru. 2.5 Hitimisho

Katika somo hili nimejadili mchango wa Waarabu, Watawala wa kikoloni, Wamishenari na Walowezi katika kukieneza Kiswahili kutoka pwani hadi bara kabla ya uhuru. Ushahidi uliopo unaonyesha kwamba ingawa walichangia maenezi ya Kiswahili kwa njia tofauti, walifanya pia mambo fulani ambayo yalizuia Kiswahili kuenea. Kwa hivyo, kama anavyosema Chacha Nyaigoti Chacha (2001), miongoni mwa watu hao kulikuwa na marafiki na maadui wa Kiswahili. Katika somo lijalo, nitazungumzia lahaja mbalimbali za Kiswahili.

2.6 Maswali

? 1. “Sera ya lugha ya Waingereza ilitatiza kukua na kuenea kwa Kiswahili nchini Kenya,” Jadili kauli hii kwa tafsili. 2. “Wajerumani na Wamishenari walikuwa marafiki wakubwa wa Kiswahili”. Jadili kauli hii huku ukieleza jinsi walivyochangia maenezi ya lugha hii katika Afrika Mashariki. 3. Fafanua sababu zilizotatiza kukua na kuenea kwa Kiswahili nchini Uganda kabla ya uhuru.

2.7 Marejeleo ya Lazima Chiraghdin, S. na M. Mnyampala (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: O.U.P. Mbaabu, I. (1991). “The Impact of Language Policy on the Development of Kiswahili in

Kenya, 1930-1990.” Ph.D Thesis, Howard University. Ndungo, C. na W. Mwai (1991). Kiswahili Part Two: Historical Modern Development in

Kiswahili. Nairobi: Nairobi University Press. Whiteley, W.H. (1969). Kiswahili: The Rise of a National Language. London: Methuen. ***Marejeleo ya ziada yanapatikana katika somo la mwisho.

26

SOMO LA 3

LAHAJA ZA KISWAHILI 3.0 Utangulizi

Katika somo hili nitaziainisha lahaja muhimu za Kiswahili huku nikionyesha mahali zinapozungumzwa. Aidha, nitabainisha tofauti za kifonolojia na kimofolojia kati ya lahaja hizo na Kiswahili Sanifu. Kadhalika nitatoa mifano ya washairi wa kale walioandika mashairi yao katika lahaja hizo. Kabla ya kufanya hivyo, nitaeleza kwanza maana ya lahaja na jinsi lahaja zinavyozuka.

3.1 Madhumuni

Baada ya kulipitia somo hili, ninatarajia kwamba utaweza: (i) Kuziainisha lahaja muhimu za Kiswahili na kuonyesha mahali

zinapozungumzwa. (ii) Kubainisha tofauti muhimu za kifonolojia na kimofolojia kati ya lahaja

hizo na Kiswahili Sanifu. (iii) Kuandika baadhi ya mashairi yaliyoandikwa kwa Kiamu na Kimvita kwa

Kiswahili Sanifu. 3.2 Lahaja ni nini?

Lahaja ni aina ya uzungumzaji unaotumiwa na kikundi cha watu, aghalabu katika eneo maalumu, na hutofautiana na uzungumzaji wa vikundi vingine vya lugha hiyo moja katika matamshi, msamiati na kwa nadra sana katika sarufi. Musau (1990:34) anasema kwamba aghalabu aina hizi za uzungumzaji huwa hazitatizi mawasiliano kati ya kijopo kimoja cha jamii inayozungumza lugha moja na kile kingine. 3.3 Lahaja huzuka vipi?

Lahaja huzuka kutokana na vizuizi vinavyoibuka kati ya makundi ya watu wanaozungumza lugha moja. Kulingana na Chambers na Trudgill (1980), vizuizi hivi vinaweza kuwa vya kijiografia au kijamii. Vizuizi vya kijiografia ni kama vile milima, mito, misitu, bahari, mipaka na umbali. Trudgill (1974:43) anasema kwamba wakati watu wanaozungumza lugha moja wakiishi maeneo tofauti kwa kutengwa na umbali fulani na wenzao, lugha yao itaanza kuwa tofauti, hasa ikiwa hakuna uhusiano mkubwa wa kimawasiliano kati ya makundi haya. Wana-elimulahaja wanasema kwamba jambo muhimu katika uzukaji wa lahaja ni wakati; kwamba lugha hupokezwa kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine, na baada ya muda mrefu, mabadiliko ya matamshi, sarufi na msamiati hutokea.

27

Trudgill (1974:17), Wardhaugh (1977:220) na Yule (1985:191) wanatofautisha aina mbili kuu za lahaja, nazo ni lahaja za kijiografia na lahaja za kijamii. Lahaja za kijiografia ni zile ambazo huzungumzwa katika eneo fulani, nazo hutokea wakati watu wa lugha moja wanapohamia maeneo tofauti kisha wakatengwa kimawasiliano kutokana na vizuizi vilivyotajwa hapo juu. Lahaja za Kiswahili nitakazojadili katika somo hili ni za kijiografia, kwa mfano Kiunguja, Kimvita na Kiamu. Lahaja za kijamii ni zile ambazo hutumiwa na makundi ya watu kulingana na tabaka lao, elimu, kazi wanayofanya, pato lao, umri, uana na vipengele vingine vya kijamii. Nchini Kenya, Sheng’ ni mfano mzuri wa lahaja ya kijamii ambayo huzungumzwa hasa na vijana wa mjini; vile vile Kisetla ni lahaja ya kijamii iliyokuwa ikizungumzwa na walowezi (masetla) wakati wa ukoloni. Zoezi la 3.1

* Taja lahaja zinazopatikana katika lugha yako iwapo zipo kisha ueleze namna ambavyo zilizuka.

3.4 Uainishaji wa Lahaja za Kiswahili

Lahaja za Kiswahili zinapatikana pwani ya Afrika Mashariki na katika visiwa mbalimbali vilivyo karibu na pwani. Visiwa hivyo ni pamoja na Lamu, Mafia, Kilwa, Unguja, Pemba na Ngazija. Kufikia sasa, hakujakuwa na makubaliano kuhusu idadi kamili ya lahaja za Kiswahili na mipaka yake. Kwa mfano, Stigand (1915) anasema ni lahaja 14; Prins (1961) na Polome (1967) wanasema ni lahaja 15; Chiraghdin na Mnyampala (1977) na Mbaabu (1978) wanasema ni lahaja 20; Bakari (1982) anasema ni lahaja 18; naye Kapinga (1983) anasema ni lahaja 22. Je, unafikiri ni kwa nini wanatofautiana?

Kutokubaliana huko kunatokana na sababu mbili. Kwanza, uchunguzi ambao

umewahi kufanywa kuhusiana na lahaja za Kiswahili si mkamilifu. Pili, wachunguzi ambao kufikia sasa wameandika kuhusu lahaja za Kiswahili hawakutumia mbinu zinazofanana katika kuziainisha lahaja hizo. Baadhi yao walitumia kigezo cha kimsamiati ilihali wengine walitumia vigezo vya kifonolojia na kimofolojia ili kuziainisha lahaja hizo. Aidha, wachunguzi hawajakubaliana kuhusu jinsi ya kuzigawanya lahaja hizo kijiografia kutegemea mahali zinapozungumzwa. Hata hivyo, lahaja zifuatazo 18 zimetajwa na waandishi wengi na zinaweza kugawanywa kijiografia katika maeneo matatu, yaani lahaja za pwani, lahaja za visiwani na lahaja za bara. Lahaja za pwani na za visiwani ndizo lahaja asilia za Kiswahili, lakini hizo za bara zilizuka baada ya Kiswahili kuenezwa sehemu za bara na zimeathiriwa zaidi na lugha mbalimbali za huko bara.

Maelezo yafuatayo yanatokana na utafiti wa Chiraghdin & Mnyampala (1977:25-

53), Bakari (1982) na watafiti wengine.

28

1. LAHAJA ZA PWANI (A) PWANI YA KASKAZINI (i) Kitikuu

Lahaja hii pia huitwa Kibajuni na huzungumzwa sehemu za Kismayu nchini Somalia. Tofauti za kifonolojia kati ya Kiswahili sanifu na lahaja hii ni kwamba, sauti [ ny ] hutamkwa kama [ n ], nayo sauti [ mz ] hutamkwa kama [ nd ], kwa mfano:

nyumba --- numba nyoka --- noka mzee --- ndhee mzuri --- ndhuri (ii) Chimbalazi Lahaja hii pia huitwa Chimiini au Kibrava na huzungumzwa nchini Somalia

katikati ya Mogadishu na Kismayu. Tofauti za kifonolojia kati ya Kiswahili sanifu na lahaja hii ni kwamba, sauti [ k ] hutamkwa kama [ ch ], nayo sauti [ s ] hutamkwa kama [ sh ], kwa mfano: kitu --- chintu

sikio --- shikilo (B) PWANI YA KATI

(i) Chijomvu Lahaja hii huzungumzwa na watu wachache sehemu za Jomvu, nje ya kisiwa cha

Mombasa. Sauti [ m ] hutamkwa kama [ n ], nayo sauti [ k ] hutamkwa kama [ ch ]. Mifano ni kama vile: mlevi --- nlevi mtu --- ntu kiongozi --- chiongozi kisu --- chisu (ii) Kimvita Lahaja hii huzungumzwa huko Mombasa na maeneo yaliyo karibu. Ina baadhi ya

maneno kutoka lahaja za kaskazini na zile za kusini, na ilitumiwa na washairi wa kale. Ingawa inafanana sana na Kiswahili sanifu, kunazo pia tofauti zifuatazo za kimatamshi:

Sauti [ ch ] hutamkwa kama [ t ], kwa mfano: wacha --- wata bichi --- biti mchanga --- mtanga mchuzi --- mtuzi Sauti [ nj ] hutamkwa kama [ nd ], kwa mfano: nje --- nde njia --- ndia njoo --- ndoo kuvunja --- kuvunda Sauti [ t ] hutamkwa kama [ t ], kwa mfano: tena --- tena joto --- joto

29

mtoto --- mtoto Sauti [ d ] hutamkwa kama [ d ], kwa mfano: damu --- damu adui --- adui Moja kati ya tofauti za kimofolojia ni kwamba, viwakilishi nafsi hubadilishwa. Kwa mfano: mimi --- miye sisi --- swiswi ni mimi --- ndimi ni sisi --- ndiswi ni nyinyi --- ndinywi Tofauti nyingine ya kimofolojia ni kwamba, aghalabu kiwakilishi nafsi {ni-}

huondolewa kisha sauti [ k ] na [ t ] hutamkwa kwa mpumuo, kwa mfano: nikifika --- ’kifika nikitoka --- ’kitoka nikaja --- ’kaja nikapata --- ’kapata nitakwenda --- ’takwenda (C) PWANI YA KUSINI

(i) Chichifundi Lahaja hii huzungumzwa sehemu za Shimoni, Vanga na Wasini zilizo kusini ya

pwani ya Kenya. Inatofautiana kifonolojia na Kiswahili sanifu kama ifuatavyo: Sauti [ t ] hutamkwa kama [ r ], kwa mfano: tuma --- ruma mtoto --- mroro mti --- mri Sauti [ p ] hutamkwa kama [ β ], kwa mfano: tapika --- raβika mfupa --- mfuβa kupita --- kuβira Sauti [ g ] hutamkwa kama [ j ], kwa mfano: ngisi --- njisi genge --- jenje agiza --- ajiza (ii) Kimtangata Lahaja hii huzungumzwa katikati ya Pangani na Tanga nchini Tanzania.

Inatofautiana kifonolojia na Kiswahili sanifu kwa njia zifuatazo: Sauti [ ch ] hutamkwa kama [ ky ], kwa mfano: changu --- kyangu

30

chombo --- kyombo cheupe --- kyeupe chochote --- kyokyote Lahaja hii hutumia mpumuo katika sauti za vipasuo ili kutofautisha maana za

maneno kama inavyodhihirika katika mifano ifuatayo: taa (lamp) --- t’aa (skate) kaa (ember) --- k’aa (crab) paa (roof) --- p’aa (gazelle) Ifuatayo ni mifano michache ya tofauti za kimsamiati: chumvi --- munyu mgonjwa --- mkongo tafuta --- pweta kurudi --- *kuuya wasiwasi --- jekejeke *Neno ‘kuuya’ hutumika katika methali isemayo, “Mchama ago hanyele, huenda

akauya papo.” Je, maana ya methali hii ni nini? (iii) Kivumba Lahaja hii huzungumzwa zaidi sehemu za Wasini na Vanga na maeneo yaliyo

karibu. Inafanana kidogo na Chichifundi. Zifuatazo ni tofauti za kifonolojia kati ya lahaja hii na Kiswahili sanifu:

Sauti [ p ] hutamkwa kama [ β ] na sauti [ t ] hutamkwa kama [ r ], kwa mfano: kupata --- kuβara kupita --- kuβira taja --- raja matope --- maroβe mafuta --- mafura mtoto --- mroro tambua --- rambua uta --- ura Sauti [ ch ] hutamkwa kama [ ky ], kwa mfano: chakula --- kyakula cheo --- kyeo chuo --- kyuo chumba --- kyumba Sauti [ nd ] hutamkwa kama [ nj ], kwa mfano: ndewe --- njewe winda --- winja andika --- anjika

31

2. LAHAJA ZA VISIWANI (i) Kiunguja Lahaja hii huzungumzwa kisiwani Unguja (Zanzibar) na ndiyo iliyotumiwa kama

msingi wa kusanifisha Kiswahili wakati wa ukoloni. Ni lahaja iliyotumiwa hasa na watawala wa Kiarabu katika eneo la Unguja mjini. Kisiwa cha Unguja kilikuwa kitovu cha biashara ya Waarabu ambao walikitumia Kiunguja kama chombo cha mawasiliano katika misafara yao iliyoelekea bara. Kwa sababu hiyo, Kiunguja kilienezwa zaidi sehemu za bara kuliko lahaja nyingine yoyote. Kwa vile Kiunguja ndiyo msingi wa lugha sanifu ya Kiswahili, hakuna tofauti kubwa kati ya lahaja hii na Kiswahili Sanifu.

(ii) Kitumbatu na Kihadimu Lahaja ya Kitumbatu huzungumzwa katika kisiwa cha Tumbatu kilichoko

kaskazini ya Unguja na kusini ya Pemba. Inakaribiana sana na lahaja ya Kihadimu (Kimakunduchi) ambayo huzungumzwa kusini mwa Unguja. Baadhi ya maneno ya lahaja hizi ni kama yafuatayo:

fukuza --- angasa mstari --- mdolongwa onja --- dota foka --- fwaka

(iii) Kingazija na Kinzuani Lahaja hizi huzungumzwa katika visiwa vya Komoro. Kingazija hupatikana

kwenye kisiwa cha Grand Comoro ambacho ni kikubwa zaidi kuliko visiwa vyote vya Komoro. Nacho Kinzuani kinapatikana kwenye kisiwa cha Nzuani. Mifano ya maneno ya Kingazija ni kama vile:

njaa --- nzaa funika --- finiha mtungi --- mtunzi samaki --- nswi kinyongo --- shonde alfajiri --- mashekuu (iv) Kipemba Lahaja hii huzungumzwa kisiwani Pemba isipokuwa sehemu za kusini. Inafanana

kidogo na lahaja ya Kiunguja na Kimtangata. Ifuatayo ni mifano ya maneno ya lahaja hii: mkaidi --- mkalagavu maua --- jigila sema --- tongoa kijana mdogo --- kibunju (v) Kisiu na Kipate Lahaja ya Kisiu huzungumzwa katika mji wa Siyu kwenye kisiwa cha Pate.

Inafanana sana na lahaja ya Kipate ambayo pia huzungumzwa kisiwani humo. Ifuatayo ni mifano michache ya maneno ya Kisiu:

mtu --- nchu mtumbwi --- nchumbwi

32

mwenzio --- mwendio kushiba --- kufura (vi) Kiamu Lahaja hii huzungumzwa katika kisiwa cha Lamu ambacho zamani kiliitwa

“Kiwa-Ndeo,” yaani ‘kisiwa cha majivuno.’ Hii ilikuwa lahaja ya usomi na ushairi katika karne zilizopita. Washairi maarufu waliotumia Kiamu katika tungo zao ni pamoja na Muyaka bin Haji (1776-1840), Sayyid Abdalla bin Nassir (1718-1815), Mwana Kupona binti Mshamu, Ali Koti (1776-1834), Bakari bin Mwengo (1760-1830) na Zahidi Mngumi (1758-1828). Tofauti za kifonolojia kati ya Kiamu na Kiswahili sanifu ni:

Sauti [ v ] na [ vy ] hutamkwa kama [ z ], kwa mfano: vita --- zita viatu --- ziatu vyombo --- zombo viazi --- ziazi Sauti [ j ] hutamkwa kama [ y ], kwa mfano: kijakazi --- kiyakazi moja --- moya jambo --- yambo Sauti [ ch ] hutamkwa kama [ t ], kwa mfano: kicheko --- kiteko mchanga --- mtanga chungu --- tungu Sauti [ l ] hupotea inapopatikana katikati ya vokali mbili, kwa mfano: kale --- kae makelele --- makee mbele --- mbee upele --- upee Sauti [ g ] hudondoshwa inapopatikana katikati ya vokali mbili, kwa mfano: mbegu --- mbeu ndugu --- nduu kutegua --- kuteua kugawanya --- kuawanya Aghalabu sauti [ nz ] hutamkwa kama [ nd ], kwa mfano: kwanza --- kwanda kufunza --- kufunda inzi --- indi Sauti [ h ] hutamkwa kama [ s ] hasa ikiwa mwanzoni mwa neno, kwa mfano: huu --- suu

33

hao --- sao hayo --- sayo hii --- sii Sauti [ nj ] hutamkwa kama [ nd ], kwa mfano: njia --- ndia njiwa --- ndiwa kuonja --- kuonda nje --- nde Tofauti moja ya kimofolojia ni kwamba, kiambishi {-le} hutumiwa kama kiishio

cha vitenzi katika baadhi ya mashairi yaliyoandikwa zamani kwa Kiamu. Kiambishi hiki huonyesha kwamba kitendo kilifanyika na kukamilika, kwa mfano:

koma --- komile nena --- nenile tenda --- tendile pita --- pitile ziwe --- ziwele Mbali na lahaja hizo, kulikuwa pia na lahaja ya Kingozi ambayo haipo sasa lakini

baadhi ya maneno yake yamehifadhika katika mashairi ya kale ya Kiswahili. Hii inaaminika kuwa lahaja ya mwanzo kabisa ya Kiswahili ambayo ilizaa lahaja mbalimbali zilizoenea pwani na visiwani. Baadhi ya maneno ya Kingozi ni kama vile “ng’andu” (dhahabu), “nswi” (samaki) na “mulungu” (Mungu).

3. LAHAJA ZA BARA Hizi ni lahaja ambazo zilizuka baada ya Kiswahili kuenezwa kutoka visiwani na

pwani kuelekea bara, na nyingi zimeathiriwa na lugha za bara. Mifano ni kama vile:

(i) Kimgao Lahaja hii inapatikana kwenye zile njia zilizofuatwa na misafara ya wafanya

biashara Waarabu nchini Tanzania. Katika lahaja hii, sauti [ k ] hutamkwa kama [ ch ] na sauti [ r ] huchopekwa katikati ya vokali mbili zinapofuatana, kwa mfano:

kingine --- chingine kichwa --- chichwa lia --- lira ingia --- ingira

(ii) Kingwana Lahaja hii huzungumzwa sehemu za mashariki ya nchi ya Zaire (Jamhuri ya

Kidemokrasia ya Congo) hasa upande wa Katanga. Ni mchanganyiko wa Kiswahili, lugha za kienyeji za sehemu hizo na Kifaransa kidogo. Mifano ya maneno ya Kingwana ni kama:

ndugu --- nduku kazi --- kasi kushinda --- kusinda

34

zamani --- samani rudi --- ludi barabara --- balabala alikwenda --- alikwendaga thelathini --- makumi matatu arobaini --- makumi manne

Zoezi la 3.2

* Eleza matatizo mbalimbali yanayowakumba watafiti wanapojaribu kuhesabu na kuainisha lahaja za Kiswahili.

3.5 Hitimisho

Katika somo hili nimeeleza maana ya lahaja na jinsi zinavyozuka. Aidha nimeainisha lahaja mbalimbali za Kiswahili, nikataja mahali zinapozungumzwa pamoja na kubainisha tofauti za kifonolojia na kimofolojia kati ya lahaja hizo na Kiswahili sanifu. Pia nimetaja baadhi ya washairi wa zamani waliotumia lahaja za Kimvita na Kiamu katika tungo zao. Utenzi wa Al-Inkishafi (S.A.A. Nassir) na Utenzi wa Mwana Kupona ni mifano ya tungo hizo. Somo lijalo litahusu usanifishaji wa Kiswahili.

3.6 Maswali

? 1. Huku ukitoa mifano mwafaka, bainisha tofauti za kifonolojia na kimofolojia

kati ya lahaja za Kimvita, Kivumba na Kiswahili Sanifu. 2. (i) Uandike ubeti ufuatao katika Kiswahili Sanifu kisha uitaje lahaja aliyoitumia mtunzi: “Malimwengu yote yawatiile na dunia yao iwaokele Wachenenda zitwa zao zilele mato mafumbizi wayafumbiye.” S.A.A. Nassir, Al-Inkishafi, ub. 35 (ii) Kwa kutoa mifano kutoka katika ubeti huo na kwingineko, zibainishe

sifa tisa zinazoitofautisha lahaja hiyo na Kiswahili Sanifu.

35

3.7 Marejeleo ya Lazima Bakari, M. (1982). “The Morphophonology of Kenyan Swahili Dialects.” Unpublished

Ph.D thesis, University of Nairobi. Chiraghdin, S. na M. Mnyampala (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: O.U.P. Mbaabu, I. (1978). Kiswahili Lugha ya Taifa. Nairobi: Kenya Literature Bureau. Musau, P.M. (1990). Swahili Part Three: Kiswahili in the Twentieth Century. Nairobi:

University of Nairobi. ***Marejeleo ya ziada yanapatikana katika somo la mwisho.

36

RAMANI YA PWANI YA AFRIKA MASHARIKI IMENAKILIWA KUTOKA KHALID (1977:V)

37

SOMO LA 4

USANIFISHAJI WA KISWAHILI 4.0 Utangulizi

Katika somo hili nitazungumzia harakati za kusanifisha Kiswahili kabla ya uhuru. Maswala nitakayoangazia ni pamoja na sababu za kusanifisha Kiswahili, malengo ya awali ya Kamati iliyosanifisha Kiswahili, mafanikio na matatizo ya Kamati hiyo na haja ya kusanifisha Kiswahili upya.

4.1 Madhumuni

Baada ya kulipitia somo hili, ninatarajia kwamba utaweza: (i) Kueleza maana ya usanifishaji wa lugha. (ii) Kueleza hatua za usanifishaji wa lugha. (iii) Kufafanua sababu za usanifishaji wa Kiswahili. (iv) Kueleza malengo ya Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. (v) Kutathmini mafanikio na matatizo ya Kamati ya Kiswahili. (vi) Kueleza umuhimu wa kusanifisha Kiswahili upya.

4.2 Maana ya Usanifishaji

Kusanifisha lugha ni utaratibu wa kuondoa tofauti zote za kilahaja, kimaeneo na kitabaka katika orthografia, msamiati, sarufi na matamshi. Mbaabu (1985:204) anasema kwamba orthografia inastahili kusanifishwa ili kupata mtindo mmoja wa kuandika kila neno katika lugha kulingana na matamshi. Kwa hivyo, lugha sanifu au lahaja sanifu ni aina ya usemi unaokubaliwa katika jamii kama lugha wastani ya mawasiliano. Lugha hiyo inastahili kutumiwa katika maandishi, matangazo na mazungumzo rasmi.

4.3 Hatua za Usanifishaji

Kuna hatua nne muhimu ambazo hufuatwa katika kuisanifisha lugha. Kwa mujibu wa Mazrui (1981:10) akimnukuu Haugen (1966), hatua hizo ni kama zifuatazo:

(i) Kuichagua lugha moja au lahaja moja ya usanifishaji miongoni mwa lugha au lahaja nyingi.

(ii) Kuiweka lugha au lahaja hiyo katika maandishi ambapo utaratibu wa kuendeleza maneno huamuliwa, na herufi za konsonanti na vokali zitakazotumiwa katika maandishi huchaguliwa.

(iii) Kuipanua lugha au lahaja sanifu kimatumizi ambapo uamuzi hutolewa kuhusu mahali lugha hiyo itakapotumiwa, kwa mfano redioni, magazetini, vitabuni, shuleni, mahakamani na bungeni.

38

(iv) Kuiendeleza au kuikuza lugha hiyo sanifu kwa kutumia vyombo vya habari kama vile magazeti, redio na runinga. Pia inaweza kukuzwa katika taasisi za elimu kwa kuiandikia vitabu vya sarufi na kamusi.

Hata hivyo, ingawa hatua hizi hutenganishwa kinadharia, katika utekelezaji huwa

zinaingiliana. Kwa mfano, hatua ya tatu na ya nne zinaweza kutekelezwa sambamba. Aidha, usanifishaji lugha ni shughuli inayopaswa kuendelea wakati wote kwa sababu lugha hubadilika daima ili kukidhi mahitaji ya watumizi wake. 4.4 Sababu za Usanifishaji wa Kiswahili

Shughuli za kusanifisha Kiswahili zilianza rasmi mnamo mwaka wa 1930. Lakini je, kulikuwa na haja gani Kiswahili kusanifishwa wakati huo wa ukoloni? Usanifishaji wa Kiswahili ulitokana na kuwepo kwa lahaja nyingi za Kiswahili. Hali hii ilitatiza sana shughuli za kidini na za kielimu ambazo zilihitaji kuendeshwa kwa lahaja moja iliyoeleweka na watu wote.

Kuna sababu mbili za kidini zilizopelekea kusanifishwa kwa Kiswahili. Kwanza,

kulikuwa na haja ya kutoa mafunzo ya dini na mahubiri ya Injili kwa lahaja moja. Wamishenari kama vile Krapf wa dhehebu la C.M.S na Askofu Steere wa dhehebu la U.M.C.A walikuwa na haja ya kutumia lahaja moja ili kuepuka hali ya kutoelewana katika mahubiri, mafundisho na maandishi yao. Krapf na wenzake walikuwa wakitumia Kimvita ilhali Askofu Steere na wenzake walikuwa wakitumia Kiunguja. Pili, kulikuwa na haja ya kutafsiri maandiko ya Biblia Takatifu kwa lahaja moja ili watu wengi wayasome kisha waupokee wokovu.

Hali kadhalika kulikuwa na sababu mbili za kielimu zilizopelekea kusanifishwa

kwa Kiswahili. Kwanza, kulikuwa na haja ya kutumia lahaja moja kufundishia shuleni ili kudumisha mawasiliano kati ya walimu na wanafunzi. Pili, kulikuwa na haja ya uandishi wa vitabu vya elimu kwa kutumia lahaja moja. Wakati sera ya lugha nchini Kenya ilipohimiza kwamba lugha za kwanza zitumiwe kufundishia shuleni, kulizuka tatizo la orthografia katika uandishi wa vitabu. Kila lugha ya kwanza iliyotumiwa ilihitaji kuwa na mfumo mmoja wa kimaandishi. Wakati huo lugha ya Kiswahili ilikuwa ikitumia hati za Kiarabu na Kirumi pamoja. Kwa vile hali hii ilileta gharama kubwa ya uchapishaji wa vitabu, kulikuwa na haja ya kuiteua lugha moja (Kiswahili) na kuisanifisha ili itumiwe katika elimu (Mbaabu, 1991:21-22).

Ili kukabiliana na matatizo hayo ya kidini na kielimu, nchi za Afrika Mashariki ziliungana na kuanzisha Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (K.K.A.M) mwaka wa 1930 ili kuisanifisha na kuikuza lugha ya Kiswahili. Nchi hizo zilikuwa Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar. K.K.A.M ilikuwa na makao yake katika miji mbalimbali. Ilikuwa na makao yake mjini Dar es Salaam kati ya mwaka 1930-1942, mjini Nairobi kati ya mwaka 1942-1952, mjini Makerere kati ya mwaka 1952-1962, mjini Mombasa kati ya mwaka 1962-1964, kisha ikapelekwa tena mjini Dar es Salaam mwaka 1964 na kuwekwa chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam. Shughuli za Kamati hiyo zilikatizwa mwaka huo na badala yake Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ikaundwa. Mbaabu (1991a) anaeleza zaidi kuhusu shughuli za K.K.A.M. Hebu sasa tuangalie malengo ya K.K.A.M wakati ilipoundwa.

39

Zoezi la 4.1

* Eleza maana ya ‘usanifishaji’ kisha ufafanue hatua muhimu ambazo hufuatwa wakati lugha inaposanifishwa.

4.5 Malengo ya K.K.A.M.

Yafuatayo ni baadhi ya malengo ya awali ya K.K.A.M: (i) Kusanifisha maandishi ili kuhakikisha kwamba kuna mtindo mmoja

unaotumika katika nchi zote zinazohusika. (ii) Kuchapisha kamusi za kutumiwa shuleni ili kuonyesha matumizi sahihi ya

msamiati wa zamani na msamiati ulioazimwa. (iii) Kuhakikisha kuwa sarufi imesanifishwa kwa kuchapisha vitabu vya sarufi. (iv) Kuwatia moyo na kuwasaidia waandishi ambao lugha yao ya kwanza ni

Kiswahili. (v) Kuwashauri waandishi wote kuhusu vitabu walivyokusudia kuandika. (vi) Kutoa orodha ya vitabu vya lazima na vya ziada vilivyohitajika mashuleni. (vii) Kuvitafsiri au kuviandika upya kwa Kiswahili vitabu vilivyopendekezwa. (viii) Kuwapasha waandishi habari zozote kuhusu mbinu tofauti za kufundishia

katika kila nchi. (ix) Kujibu maswali yote yanayohusu lugha ya Kiswahili na maandishi yake. (x) Kufanya jambo lolote lile ambalo lingesaidia kuyatimiza madhumuni

hayo. Lakini je, K.K.A.M ilifanikiwa kutekeleza malengo hayo?

4.6 Utekelezaji wa Malengo ya K.K.A.M. (A) Mafanikio ya K.K.A.M

(i) Kamati hiyo ilitoa makamusi mawili, yaani kamusi ya Kiswahili – Kiswahili (1935) na kamusi ya Kiswahili – Kiingereza na Kiingereza – Kiswahili (1939).

(ii) Kamati ilitoa jarida lililojulikana kama ILC – Bulletin ambalo hapo awali lilikuwa likitolewa bure kwa wale waliokuwa wakipenda.

(iii) Kamati ilikuwa ikiyajibu maswali ya umma kuhusu maneno mapya, asili ya maneno na maneno yaliyoazimwa, kisha maneno yaliyokubaliwa yalichapishwa katika I.L.C – Bulletin.

(iv) Kamati iliandaa mashindano ya kuandika insha na vitabu ili kuwatia ari waandishi wa Kiswahili. Shaaban Robert alikuwa miongoni mwa waandishi waliowahi kushinda katika mashindano hayo.

(v) Kamati ilikuwa ikitafsiri vitabu vya fasihi na vya sayansi kwa Kiswahili, na ilizingatia uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili Sanifu ili kuwashawishi waandishi wapya. Gorman (1974:425) anasema kuwa vitabu vingi

40

vilichapishwa hasa kuanzia mwaka wa 1948 wakati shirika la uchapishaji la East Africa Literature Bureau lilipoundwa.

(vi) Kamati ilisimamia utafiti wa lahaja za Kiswahili kama vile Kimvita, Chichifundi, Kimtang’ata, Kivumba, Kipemba, Kihadimu, Chijomvu, Kitikuu na Chimiini. Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa katika vijalizo vilivyoitwa Studies in Swahili Dialects.

(vii) Mafanikio makubwa yalipatikana katika usawazishaji wa orthografia kwa kutumia hati (herufi) za Kirumi kwa sababu lugha ya Kiswahili iliendelezwa kwa mtindo mmoja.

(viii) Kamati ilikusanya hati za kale na miswada mbalimbali ya historia na fasihi ya Kiswahili.

Kwa hivyo ni dhahiri kwamba K.K.A.M ilifanikiwa kutekeleza malengo mengi. Hata hivyo, Kamati hiyo ilikumbwa pia na matatizo mbalimbali.

(B) Matatizo ya K.K.A.M (i) Vitabu vingi vilivyotolewa na kamati hiyo viliandikwa na Wazungu wala

sio wenyeji wa lugha ya Kiswahili. (ii) Vitabu vingi vilivyoidhinishwa vilikuwa tafsiri za vitabu vya Kiingereza,

kwa mfano, “Kisiwa Chenye Hazina” (The Treasure Island), “Mashimo ya Mfalme Suleiman” (King Solomon’s Mines) na “Safari za Gulliver” (Gulliver’s Travels).

(iii) Kamati hiyo mwanzoni ilitawaliwa na Wazungu pekee ambao walikuwa kumi na saba. Waafrika wanne wa kwanza walichaguliwa tu mwaka 1939.

(iv) K.K.A.M haikushirikisha Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) katika kusanifisha Kiswahili, kwa hivyo, kuna tofauti nyingi kati ya Kiswahili cha JKK (Kingwana) na Kiswahili Sanifu.

(v) Kulikuwa na mgogoro baina ya wanakamati wenyewe na hali hii ilitatiza shughuli za Kamati hiyo.

(vi) Makao ya Kamati yalikuwa yakihamishwa kila mara na hali hii ilisababisha kupotea kwa vifaa vya Kamati hiyo na miswada kuibwa.

(vii) Nchi wanachama zilichelewa kulipa michango na hivyo basi kutatiza shughuli za Kamati hiyo.

(viii) Mauzo ya jarida la ILC – Bulletin yalikuwa haba na hivyo basi Kamati haikuweza kugharamia shughuli zake zote.

(ix) Vita Vikuu vya Pili vya Ulimwengu (1939-1945) viliathiri vibaya shughuli za Kamati hiyo kwa sababu kulikuwa na ukosefu wa usalama.

(x) Kulikuwa na pingamizi kutoka kwa Waganda ambao hawakutaka lugha ya Kiswahili kuenezwa nchini mwao.

(xi) Maneno mengi sana yaliazimwa kutoka lugha ya Kiingereza, kwa mfano, eropleni, motaboti, swichi, globu na mengineyo. Chiraghdin na Mnyampala (1977:60) wanasema kuwa hata sarufi ya Kiswahili Sanifu pia iliandikwa kwa kurejelea sarufi ya Kiingereza.

(xii) Kulikuwa na ukosefu wa misaada ya kifedha kwa hivyo ikawa vigumu kuendesha shughuli za Kamati.

(xiii) Kule mashuleni, Mazrui (1981:50-55) anasema kwamba Wazungu waliwashurutisha wanafunzi Waswahili kujiepusha na lahaja zao na

41

kufuata sarufi na matamshi ya “Ki-Standard” huku wakiambiwa kwamba lugha (lahaja) zao wenyewe zilikuwa na makosa.

Matatizo hayo ndiyo yaliyoharakisha kuvunjika kwa K.K.A.M. Hata hivyo,

Kamati hiyo tayari ilikuwa imeweka msingi bora wa lugha sanifu ya Kiswahili. Kiunguja ndiyo lahaja iliyotumiwa kama msingi wa kusanifisha Kiswahili. Lakini kwa nini lahaja zingine zote zikaachwa na Kiunguja kuchaguliwa?

4.7 Sababu za Kuchaguliwa kwa Kiunguja

K.K.A.M ilichagua Kiunguja kama msingi wa kusanifisha Kiswahili kwa sababu mbalimbali. Kwanza, lahaja ya Kiunguja ilikuwa imeenea sana kuliko Kimvita na lahaja zingine. Pili, Kiunguja kilikuwa rahisi sana kufahamika kuliko Kimvita kwani matamshi ya Kimvita yaliwatatanisha watu wengi. Tatu, Kiunguja kilikuwa kimefanyiwa uchunguzi mwingi na watangulizi kama vile Askofu Steere, na kilikuwa kimetumiwa sana katika mahubiri na hata vitabuni. Mwisho, Kiunguja kilikuwa lugha ya biashara na pia lugha ya Zanzibar, kisiwa ambacho kilikuwa kitovu cha shughuli nyingi za kibiashara na kiutawala katika Afrika Mashariki. Kwa hivyo, umaarufu wa Zanzibar wakati huo ulikipatia Kiunguja hadhi kubwa kuliko Kimvita cha Mombasa.

Waandishi kama vile Abdalla Khalid (1977) wana maoni tofauti. Khalid anadai

kwamba kuteuliwa kwa Kiunguja kulikuwa ni njama ya Wazungu ya kutaka kuendeleza utumwa. Anasema kwamba Kimvita ndicho kilistahili kuteuliwa kwa sababu mbili. Kwanza anadai kwamba lahaja ya Kimvita ni rahisi kueleweka kuliko lahaja zingine kwa sababu inazungumzwa mjini Mombasa, eneo ambalo lipo katikati ya lahaja za kaskazini na zile za kusini. Pili, anasema kwamba Kimvita kina historia ndefu ya maandishi ya kifasihi kuliko lahaja zingine. Khalid anakiona Kiunguja kama lahaja ya “kijingajinga” kwa vile imechafuliwa na Kiarabu na inatumiwa na watumwa.

Kwa sababu hizo, Abdalla Khalid anapendekeza kwamba Kiswahili kisanifishwe

upya kwa kutumia lahaja ya Kimvita. Lakini Mbaabu (1985) anapinga pendekezo hilo huku akisema kwamba hatua ya kusanifisha Kiswahili upya kwa kutumia Kimvita ina gharama kubwa na hivyo hatuwezi kuichukua. Je, wewe una maoni gani, Kiswahili kisanifishwe upya au la?

4.8 Haja ya Kukisanifisha Kiswahili Upya

Mukhwana (1995) anashangaa kama kweli Kiswahili Sanifu kipo au la. Anashangaa kwa sababu siku hizi kuna ‘viswahili’ vya aina nyingi ambavyo vinatofautiana kimatamshi, kimaendelezo, kisarufi na kimsamiati. Kila anayezungumza ‘kiswahili’ chake anafikiri ndicho sanifu zaidi kuliko ‘viswahili’ vya wengine. Kwa hivyo Mukhwana anahitimisha kwamba, “Kiswahili sanifu hakipo, kwa sasa hufikirika tu.”

Ni muhimu kufahamu kwamba usanifishaji wa lugha ni jambo linaloendelea

wakati wote, na hivi leo, Kiswahili kinastahili kusanifishwa upya kwa sababu zifuatazo: Kwanza, kuna haja ya kutumia mtindo mmoja wa kuandika kila neno katika

Kiswahili. Hivi sivyo ilivyo katika Kamusi Sanifu ya Kiswahili (1981) ambayo

42

inaandika baadhi ya maneno ya Kiswahili kwa njia tofauti, kwa mfano: drili/dereli; dreva/dereva; filimu/filamu; glopu/globu; finika/funika; mazoea/mazowea; na maneno mengineyo.

Pili, msamiati wa kilahaja ambao unakubalika katika mashairi na tungo zingine, umepenya katika riwaya na unazusha tisho kubwa kwa Kiswahili Sanifu. Kumekuwa na madai kwamba hata waandishi wasifika wamekuwa wakitumia Kiswahili kisicho sanifu katika riwaya zao na hivyo kuwapotosha wasomaji. Kwa mfano, maneno kama vile kua, tua, sikia na lia huandikwa na watu wengi kama kuwa, tuwa, sikiya na liya.

Tatu, Kiswahili kisanifishwe upya ili kukabiliana na athari za Sheng’. Sheng’ ni

usemi unaotumiwa na watu wengi (hasa vijana) mjini na ambao huchanganya maneno ya Kiswahili, Kiingereza na lugha za kienyeji. Kwa vile Sheng’ hutumia sarufi ya Kiswahili, watu wengi wanapozoea kuizungumza, wao hufikiria kwamba wanazungumza Kiswahili Sanifu. Aidha, Mbaabu (1991b) anasema kwamba kuna maneno ya Sheng’ ambayo yamezoeleka lakini hatujui iwapo matumizi ya maneno hayo yanaweza kukubalika kama maneno ya Kiswahili Sanifu au la, kwa mfano:

kobole/kubule --- “shilingi tano” mitumba/metumba --- “nguo kuukuu” ushago/oshago --- “bara” kusare --- “kukata tamaa”

Sheng’ imeathiri jamii nzima kwa jumla kwa vile inatumiwa shuleni, magazetini, redioni na kwingineko. Tusipofahamu ni maneno yapi yanakubalika katika Kiswahili Sanifu, na namna ya kuyaandika, itakuwa vigumu kutofautisha kati ya lugha sanifu na lugha isiyo sanifu. Zoezi la 4.2

* Eleza kwa nini lahaja ya Kiunguja ilichaguliwa kuwa msingi wa kusanifisha lugha ya Kiswahili na wala sio Kimvita au Kiamu..

Nne, Kiswahili kisanifishwe upya ili tuweze kupata istilahi mwafaka tunazohitaji

kutumia katika nyanja mbalimbali kama vile za kisayansi, kiteknolojia, kibiashara, kiutamaduni, na kisiasa. Aidha, istilahi zinazotumiwa katika nyanja zingine hubadilika kila wakati kulingana na mfumo uliopo wa kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kwa mfano, Gibbe (1983:149) anasema kwamba wakati wa ukoloni nchini Tanzania, ‘D.C’ (District Commissioner) alikuwa akiitwa “Bwana Shauri” lakini sasa anaitwa “Katibu wa Chama wa Wilaya.” Kadhalika wakati wa ukoloni ‘Agricultural Officer’ alikuwa akiitwa “Bwana Shamba” lakini sasa anaitwa “Afisa Kilimo.” Kwa hivyo, istilahi kama hizo zikiwa katika kamusi zinafaa kusanifishwa upya.

Mwisho, Kiswahili kinahitaji kusanifishwa upya ili kudumisha mawasiliano ya

kitaifa na kimataifa. Nchi ya Tanzania ikiendelea kuunda istilahi bila kushirikiana na nchi

43

zingine zinazotumia Kiswahili, kutazuka tatizo la kimawasiliano baina ya nchi hizo, na pengine huenda istilahi hizo zisikubaliwe na nchi zingine. Kwa hivyo, ni dhahiri kwamba umuhimu wa kusanifisha Kiswahili upya upo. 4.9 Hitimisho

Katika somo hili nimejadili maswala mbalimbali kuhusu usanifishaji wa Kiswahili. Moja kati ya maswala hayo ni umuhimu wa kusanifisha upya Kiswahili. Ingawa nimethibitisha kwamba haja ya kusanifisha Kiswahili upya ipo, hatuwezi kulikubali pendekezo la Abdalla Khalid (1977) eti Kiswahili kisanifishwe upya kwa kutumia Kimvita. Sababu za kutokubali ni nyingi; kwanza, ni kwamba tofauti kati ya Kimvita na Kiswahili Sanifu ni ndogo sana. Pili, vitabu vya Kimvita havipo. Tatu, walimu waliohitimu kufunza Kimvita hawapo. Mwisho, gharama ya kuliziba pengo hilo, yaani ukosefu wa vitabu na walimu, ni kubwa sana. Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba Kimvita sasa kisahaulike, la! Bali kinaweza kutumika katika miktadha mwafaka ya mazungumzo au maandishi, kwa mfano katika ushairi. Katika somo lijalo, tutazungumzia sera ya lugha katika Afrika Mashariki.

4.10 Maswali

?

1. Eleza ni kwa nini lugha ya Kiswahili ilisanifishwa wakati wa ukoloni. 2. Tathmini mchango wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki

(K.K.A.M) katika kusanifisha lugha ya Kiswahili. 3. “Kiswahili kinahitaji kusanifishwa upya.” Jadili kauli hii.

4.11 Marejeleo ya Lazima Khalid, Abdallah (1977). The Liberation of Swahili from European Appropriation.

Nairobi: East Africa Literaure Bureau. Mazrui, A. M. (1981). “Acceptability in a Planned Standard: The Case of Swahili in

Kenya.” Ph.D Thesis, Stanford University. Mbaabu, I. (1991a). Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili. Nairobi: Longman Kenya Ltd. Mukhwana, A. (1995). “Kiswahili Sanifu: Je Kipo?” katika BARAGUMU, Juzuu la 2

Nam. 1&2 uk. 18-24. ***Marejeleo ya ziada yanapatikana katika somo la mwisho.

44

SOMO LA 5

SERA YA LUGHA KATIKA AFRIKA MASHARIKI 5.0 Utangulizi

Katika somo hili, nitafafanua mchango wa vyombo mbalimbali ambavyo vimetumiwa kustawisha Kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki baada ya uhuru. Aidha, nitaeleza matatizo yanayovikumba vyombo hivyo huku nikizingatia sera ya lugha ilivyo nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Pia nitazungumzia athari za Sheng’ kwa Kiswahili Sanifu pamoja na kutaja hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuendeleza Kiswahili. Sera ya lugha ni mpango wa serikali kuhusu matumizi ya lugha nchini. Je, baada ya uhuru, serikali tatu za Afrika Mashariki zimekuwa na mpango gani kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili na ustawishaji wake? Je, Kiswahili kinahitajika kutumiwa wapi, na nani, kwa njia gani, na kikuzwe vipi? Haya ndiyo maswali ya kimsingi nitakayojadili katika mada hii.

5.1 Madhumuni

Baaada ya kulipitia somo hili, ninatarajia kwamba utaweza: (i) Kufafanua mchango wa vyombo mbalimbali ambavyo vimetumiwa

kustawisha lugha ya Kiswahili nchini Tanzania, Kenya na Uganda baada ya uhuru.

(ii) Kueleza matatizo yanayovikumba vyombo vinavyotumiwa kustawisha Kiswahili na jinsi yanavyoweza kutatuliwa.

5.2 Sera ya Lugha nchini Tanzania baada ya Uhuru

Ingawa ukweli wa historia ni kwamba chanzo cha lugha ya Kiswahili ni Kenya, mataifa mengi yanaitazama Tanzania kama chanzo cha Kiswahili kwa sababu kimestawi sana na kuenea kote nchini. Mara tu baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, Kiswahili kilitangazwa kuwa lugha ya taifa, na mwaka 1967 kilitangazwa kuwa lugha rasmi sambamba na Kiingereza katika shughuli za utawala, elimu, biashara na shughuli nyinginezo. Ili lugha hii iweze kutekeleza majukumu hayo, serikali ya Tanzania imefuata sera thabiti ambapo vyombo mbalimbali vinavyoshughulikia ukuzaji wa Kiswahili vimeundwa. Vyombo hivyo ni kama vifuatavyo (Maganga, 1983:93-103):

(A) WIZARA YA ELIMU NA UTAMADUNI Wizara hii ilianzisha kamati maalum iliyojishughulisha na somo la Kiswahili na

pia walimu wa lugha hii. Sehemu ya utamaduni nayo ilichukua jukumu la kuzitalii tanzu za fasihi simulizi kama vile nyimbo, ngoma na ngano, na baadaye kuzitafsiri kwa Kiswahili ili wananchi wengi waweze kuzifahamu.

45

Wizara hiyo pia ina idara ya sanaa na lugha ambayo hushughulikia vikundi vya sanaa za maonyesho vya aina mbalimbali. Kuna vikundi vya muziki na taarab ambavyo hutumia lugha ya Kiswahili katika utunzi wao wa nyimbo. Pia kuna vikundi vya michezo ya kuigiza ambavyo ni vya shule za upili na Chuo Kikuu. Aidha, kuna shirika la filamu ambalo hutoa filamu za kuelimisha na kuburudisha kwa lugha ya Kiswahili.

(B) KAMATI YA KUTAFSIRI SHERIA Mara tu baada ya uhuru, Sheikh Amri Kaluta Abeid aliunda kamati ya wataalamu

kumi wa Kiswahili ili kutafsiri sheria kwa Kiswahili. Kutokana na juhudi za wanakamati hao, kamusi rasmi ya sheria ilitolewa mwaka wa 1967. Ingawa istilahi za kisheria zilitafsiriwa kwa Kiswahili, sheria za Tanzania zilikuwa zingali katika Kiingereza. Hii ni kwa sababu baadhi ya vipengele vya sheria havikuwa rahisi kutafsiriwa. Pia wanasheria wengi hawakuwa Watanzania na hivyo basi hawakufahamu Kiswahili.

(C) TAASISI YA ELIMU YA TANZANIA (TET) Taasisi hii ilianzishwa mnamo mwaka 1966 na kazi yake ni kukuza na

kutathmini mitaala. TET huandaa miongozo ya masomo pamoja na vifaa kama vile vitabu vinavyohitajika kutumika katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. TET pia hutayarisha orodha ya istilahi za Kiswahili na kuzitolea maelezo na visawe vyake vya Kiingereza kwa ajili ya matumizi ya shuleni. Taasisi imekwishaandaa orodha kadhaa za istilahi kwa ajili ya masomo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Elimu ya Siasa, Historia, Fizikia, Jiografia, Kilimo, Biashara, Uchumi, Biolojia, Kemia na Elimu ya Ufundi.

(D) TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA Taasisi hii iliundwa mnamo mwaka wa 1963 kama chombo cha kutoa masomo ya

jioni kwa wananchi. Pamoja na kufundisha masomo mengine, taasisi hii imekuwa ikiwafundisha watu wazima stadi za kusoma na kuandika Kiswahili. Wanafunzi wanapojifunza stadi hizo, papo hapo wanajifunza maarifa fulani kama vile kilimo bora, afya njema na chakula bora. Taasisi hii pia imekuwa ikitoa masomo ya Kiswahili kwa njia ya Posta.

(E) BARAZA LA KISWAHILI LA TANZANIA (BAKITA) Hili ni shirika la umma lililoanzishwa na serikali mnamo mwaka 1967 ili

kuendeleza lugha ya Kiswahili nchini Tanzania pamoja na kufuatilia maendeleo yake katika nchi za nje. Kwa mujibu wa Mbaabu (1991b: 155), BAKITA lina idara tano, yaani:

(i) Idara ya Lugha na Fasihi. Idara hii huchunguza na kusahihisha matumizi ya Kiswahili katika matangazo ya redio na matumizi mengineyo. Pia hufanya utafiti kuhusu fasihi simulizi ya lugha za Tanzania.

(ii) Idara ya Uchapishaji. (iii) Idara ya Tafsiri na Ukalimani. (iv) Idara ya Istilahi na Kamusi. (v) Idara ya Fedha. Istilahi mpya zinapopendekezwa, ni sharti ziidhinishwe na Bakita ndipo zianze

kutumiwa na wananchi. Baadaye BAKITA huchapisha orodha ya istilahi sanifu

46

zilizoidhinishwa katika mfululizo wa majarida yanayoitwa Tafsiri Sanifu. Pia BAKITA huchapisha majarida mengine kama vile Lugha Yetu na Jifunze Kiswahili Uwafunze Wengine. Kamusi ya kitaaluma inayoitwa Agronomy and Animal Husbandry Dictionary (1988) pia ilichapishwa na BAKITA kwa lengo la kueneza lugha sanifu ya Kiswahili.

(F) CHAMA CHA USANIFU WA KISWAHILI NA USHAIRI TANZANIA

(UKUTA) Chama hiki kilikuwa kikiongozwa na Mathias Mnyampala na kilikuwa na

malengo manne yafuatayo: (i) Kuhimiza uigizaji na mambo mengine ya utamaduni. (ii) Kuandika kamusi na sarufi iliyofaa zaidi kuliko zile zilizokuwa zikitumika

wakati huo. (iii) Kuamsha ari ya kuandika vitabu kuhusu mada mbalimbali za Kiswahili

pamoja na ushairi na kutafuta mbinu za kuchapisha kazi zao. (iv) Kuhimiza matumizi ya ushairi wa Kiswahili na pia kuhakikisha kuwa

lugha hii haichafuliwi na lugha zingine. (G) TAASISI YA KISWAHILI NA LUGHA ZA KIGENI (TAKILUKI) Kwa mujibu wa Bwenge (1994:20), taasisi hii ilianzishwa mnamo mwaka 1979

kisiwani Zanzibar. Mbali na kufundisha Kiswahili kwa wageni na lugha za kigeni kwa wenyeji, TAKILUKI hujishughulisha na utafiti kuhusu lahaja na hadhi zake, muundo wa lahaja hizo, matumizi yake na hali yake ya baadaye kisiwani Zanzibar. TAKILUKI pia hufanya utafiti kuhusu fonolojia, mofolojia, sintaksia na kuhifadhi msamiati wa lahaja zinazojibainisha. Aidha, TAKILUKI hufanya utafiti kuhusu vipengele vya fasihi simulizi na fasihi andishi iliyofungamana na lahaja za visiwani.

(H) TAASISI YA UCHUNGUZI WA KISWAHILI (TUKI) Taasisi hii iko katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. TUKI ndiyo taasisi pekee

duniani ambayo kazi yake kuu ni utafiti wa Kiswahili katika nyanja zake zote pamoja na ufundishaji na usambazaji wake. TUKI iliundwa baada ya shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (K.K.A.M) kukatizwa mwaka wa 1964. Taasisi hii imegawanywa katika sehemu sita zifuatazo:

(i) Sehemu ya Leksikografia Jukumu la sehemu hii ni kuzipitia na kuzirekebisha kamusi za kwanza za

K.K.A.M pale inapohitajika. Mnamo mwaka 1981, TUKI ilichapisha Kamusi ya Kiswahili Sanifu, na mwaka wa 1990 ikachapisha kamusi zingine mbili, yaani, Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha, na pia Kamusi Sanifu ya Biolojia, Fizikia na Kemia. Mwaka wa 1996, TUKI ilichapisha Kamusi ya Kiingereza – Kiswahili. Pia imechapisha Istilahi za Ufundi wa Magari na Matrekta (1997), Kamusi ya Sheria (1999) na Kamusi ya Biashara na Uchumi (1999). Aidha, TUKI inafanya mipango ya kuchapisha kamusi zingine.

(ii) Sehemu ya Isimu Sehemu hii hufanya utafiti kuhusu fonolojia, mofolojia na vipengele vingine vya

isimu ili kuchapisha vitabu vya sarufi.

47

(iii) Sehemu ya Fasihi Sehemu hii hukusanya fasihi simulizi kutoka katika lugha mbalimbali za Tanzania

na kutafsiri katika Kiswahili. (iv) Sehemu ya Istilahi na Tafsiri Jukumu la sehemu hii ni kuunda istilahi mpya na pia kutoa ushauri kwa serikali,

mashirika ya kimataifa, mashirika ya kibinafsi na watu binafsi kuhusu mambo ya tafsiri. Sehemu hii vilevile imejihusisha na kuandaa vikao vya kimataifa kuhusu usanifishaji wa istilahi za Fizikia, Kemia na Isimu.

(v) Sehemu ya Uchapishaji Sehemu hii hufanikisha uchapishaji wa matokeo ya utafiti wa TUKI kupitia kwa

majarida ya Kiswahili na Mulika. (vi) Sehemu ya Utawala Sehemu hii hushughulikia usimamizi wa TUKI kwa jumla. Zaidi ya hayo, baadhi ya watafiti wa TUKI hushiriki kufundisha katika idara za

Kiswahili, Fasihi, Lugha za Kigeni na Isimu, na pia Kitivo cha Elimu. (I) IDARA YA KISWAHILI – CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM Idara hii ilianzishwa mwaka wa 1970 na hufanya kazi ya kufundisha pamoja na

utafiti kuhusu Kiswahili. Idara hii hufundisha kozi za isimu na fasihi ya Kiswahili kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza; na pia hushirikiana na Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu kufundisha wanafunzi wa shahada ya pili wanaochukua mafunzo ya Isimu. Aidha, idara hii husimamia utafiti wa wanafunzi wanaofanya masomo ya shahada ya tatu katika vipengele vya lugha na fasihi ya Kiswahili. Pia idara hii huchapisha jarida la Kioo cha Lugha (Mfululizo mpya) ambalo mwanzoni lilikuwa likichapishwa na Chama cha Kiswahili.

(J) CHAMA CHA KISWAHILI – CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM Chama hiki kiliundwa na wanafunzi waanzilishi wa Idara ya Kiswahili ambao

walikusudia kuleta mapinduzi katika kuendeleza Kiswahili na kupinga madai kwamba Kiswahili ni lugha duni. Chama hiki kilikuwa kikichapisha jarida la Zinduko na Kioo cha Lugha (Mfululizo wa zamani). Hata hivyo, kuchapishwa kwa majarida hayo kulikoma baada ya chama hicho kuzorota na kufifia. Jarida la Kioo cha Lugha (Mfululizo mpya) limefufuliwa na Idara ya Kiswahili ambayo ilianza kulichapisha upya mwaka wa 1995.

(K) VYOMBO VYA HABARI Idhaa zinazotangaza kwa Kiswahili nchini Tanzania ni Radio Tanzania, Dar es

Salaam, Sauti ya Tanzania, Zanzibar, Radio Free Africa, Mwanza, Redio Habari Maalum, Arusha, Redio Tumaini, na East Africa F.M. Pia kuna magazeti mengi sana ya Kiswahili yanayochapishwa na mashirika ya kidini, makampuni na hata watu binafsi. Mifano ni kama vile Mtanzania, Nipashe, Kasheshe, Majira, Rai, Bingwa, Dimba, Lete Raha, Taifa Letu, Sanifu, Mwananchi, Komesha, Maisha, Wiki Hii, na magazeti mengineyo. Pia kuna majarida ya kitaaluma yanayochapishwa nchini Tanzania kama vile, Mulika, Kiswahili, na Kioo cha Lugha. Kwa ujumla, Kiswahili kinachotumiwa katika redio na magazeti ya Tanzania ni cha kuvutia zaidi kuliko kile kinachotumiwa katika

48

vyombo vya habari nchini Kenya. Hata hivyo, wakati mwingine waandishi wa magazeti ya Tanzania hukiuka kanuni za uundaji wa msamiati na istilahi mpya za Kiswahili.

Ingawa sera ya lugha nchini Tanzania imeisaidia lugha ya Kiswahili kupiga hatua

kubwa katika matumizi, sera hiyo bado haijatekelezwa kikamilifu. Punde tu baada ya kupata uhuru, serikali ilisema kwamba Kiswahili kitakuwa lugha rasmi ya kufundishia katika shule za msingi na elimu ya juu. Lakini mnamo mwaka 1983, serikali hiyo ilibadili nia yake na ikasema kwamba Kiingereza sasa kitaendelea kuwa lugha ya kufundishia elimu ya juu kwa muda mrefu ujao. Kufikia sasa Kiingereza bado kinatumiwa, jambo ambalo linazidi kuwakera wataalamu wa Kiswahili. Kwa mfano, Mekacha (1995) anauliza, “Kwa nini bado Kiingereza ni lugha ya kufundishia elimu ya juu Tanzania?” Mekacha anasema kwamba serikali inaogopa kubadili sera ya lugha (yaani kukitumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia elimu ya juu) kwa sababu zifuatazo:

(i) Maendeleo Serikali inaogopa kwamba Kiswahili kikitumiwa kufundishia elimu ya juu, basi

Tanzania itabakia nyuma kimaendeleo na huenda ikatengwa na ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

(ii) Wafadhili na Wahisani Serikali inaogopa kwamba ikifanya mabadiliko hayo, huenda ikawaudhi wafadhili

ambao hawatakuwa tayari kuyagharamia kifedha. Wahisani wengine nao pia huenda wakaipuuza Tanzania kwa kukataa kuipa misaada.

(iii) Ukoko wa Kikoloni Baadhi ya viongozi na watu wengine bado wana kasumba ya kikoloni; wanaamini

kwamba Mwafrika hana chochote kilicho bora isipokuwa kile cha mkoloni wa zamani. Kwa hivyo wameishilia kuiga mambo ya kigeni ikiwa ni pamoja na lugha, elimu, mavazi na hata mifumo ya kisiasa. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Ngugi wa Thiong’o (1986) akaandika kitabu kiitwacho Decolonising the Mind, akikusudia kuwazindua Waafrika wenzake dhidi ya ukoloni mamboleo.

(v) Kujifungia katika Wigo ‘Wigo’ au ‘ukigo’ ni ua unaozunguka boma. Hii ina maana kwamba, baadhi ya

watu wa matabaka ya juu walio ndani na nje ya Tanzania wanataka kulinda matakwa na maslahi yao. Katika mfumo wa elimu wa sasa, Kiingereza kinawachuja wanaoweza na wasioweza kulipa gharama ya kukimudu. Hivi sasa watoto wa tabaka tawala wanapelekwa katika shule za msingi zinazofundisha kwa Kiingereza ndani na nje ya nchi. Watoto hawa watabakia katika tabaka la juu na hatimaye ndio watakaorithi hatamu za uchumi na utawala wa nchi. Lakini wale wasiojiweza kifedha, wanabakia kuwatumikia hao wachache.

(vi) Urazini kwa Wachache Viongozi wanaogopa kwamba Kiswahili kikitumiwa kufundishia elimu ya juu,

basi maarifa na utaalamu wa kiwango cha juu utasambaa kwa watu wengi, ambao sasa wataanza kushiriki kikamilifu katika mijadala muhimu ya kisiasa. Viongozi hao

49

wangependa mijadala hii iendelee kuendeshwa kwa Kiingereza ili urazini ubakie tu kwa watu wachache.

Kwa hivyo, inaelekea kwamba sababu za sera ya lugha kutobadilika nchini Tanzania ni za kisiasa. Sasa tuangalie hali ilivyo nchini Kenya.

Zoezi la 5.1

* Tathmini kiwango cha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vituo vya redio na magazeti ya Tanzania na Kenya.

5.3 Sera ya Lugha nchini Kenya baada ya Uhuru Baada ya uhuru, sera ya lugha nchini Kenya imeongozwa na mapendekezo ya

tume zilizoteuliwa kuchunguza maswala yanayohusu Kiswahili. Pia sera hiyo imetokana na maagizo ya watu mashuhuri. Tutazingatia matumizi ya Kiswahili katika elimu, shughuli za serikali na vyombo vya habari.

(A) ELIMU Tume mbalimbali ziliundwa ili kutoa mapendekezo kuhusu matumizi ya lugha

shuleni na vyuoni. Tume hizo ni kama zifuatazo: (a) Tume ya Ominde (1964) “The Kenya Education Commission Report” Tume hii ilitoa mapendekezo yafuatayo: (i) Lugha ya kufundishia shuleni iendelee kuwa Kiingereza. (ii) Kiswahili kiwe somo la kufundishwa shuleni bila kutahiniwa. (iii) Idara ya Kiswahili ianzishwe katika Chuo Kikuu cha Nairobi. (iv) Mafunzo ya Kiswahili kwa walimu wa shule za msingi yaendeshwe

wakati wa likizo. (v) Kozi maalum za Kiswahili zianzishwe kwa wakufunzi wa vyuo vya

ualimu. Mambo yafuatayo yalitekelezwa: (i) Kozi za kuwapandisha walimu vyeo zilianzishwa katika Chuo Kikuu

Kishiriki cha Kenyatta kuanzia mwaka wa 1978. (ii) Idara ya Isimu na Lugha za Kiafrika ilianzishwa katika Chuo Kikuu cha

Nairobi mwaka wa 1969 ambapo Kiswahili kilianza kufundishwa. (b) Tume ya Wamalwa (1972) “The Training Review Committee” Tume hii ilitoa mapendekezo yafuatayo: (i) Lugha za kimataifa kama vile Kifaransa na Kijerumani zifundishwe.

50

(ii) Kozi za Kiswahili zianzishwe katika Taasisi ya Usimamizi ya Kenya na Taasisi ya kutoa Mafunzo kwa Watumishi wa Serikali. Hii ni kwa sababu kulikuwa na watumishi wengi wa umma, wakiwemo wakuu wa wilaya, ambao hawakuweza kuwasiliana kwa lugha ya taifa.

Mambo yafuatayo yalitekelezwa: (i) Kozi za lugha za kigeni zilianzishwa katika Chuo Kikuu cha Nairobi na

Chuo Kikuu cha Kenyatta. (ii) Vyuo vingi vya kutoa shahada za diploma nchini vilianza kufundisha

lugha za kigeni. (c) Tume ya Gachathi (1976) “The National Committee on Educational Objectives and Policies” Tume hii ilitoa mapendekezo yafuatayo: (i) Kiswahili kiwe somo la lazima na la kutahiniwa katika shule za msingi, za

upili na vyuo vikuu. (ii) Kiingereza kifundishwe kama somo kuanzia darasa la kwanza kisha kiwe

lugha ya kufundishia kunzia darasa la nne. (iii) Lugha za kienyeji zitumiwe kufundishia kuanzia darasa la kwanza hadi la

tatu. (iv) Walimu wengi wa Kiswahili wapewe mafunzo. (v) Elimu ya ngumbaro iendeshwe kwa lugha za kienyeji. Yaliyotekelezwa sio mengi. Pendekezo la (i) na la (iv) yalianza kutekelezwa tu baada ya Tume ya Mackay kuanzisha mfumo wa elimu wa 8-4-4. Pendekezo la (iii) na la (v) hayakutekelezwa kikamilifu kwa sababu haikuwezekana kuchapisha vitabu katika lugha zote za kienyeji ambazo ni zaidi ya lugha 40, wala watu wa kuviandika vitabu hivyo hawakuwepo. Pia haikuwezekana kutoa mafunzo kwa walimu wa kufundisha lugha hizo zote. (d) Tume ya Mackay (1981) “Report of the Presidential Working Party on the Establishment of the Second

University in Kenya” Tume hii ilipendekeza yafuatayo: (i) Mfumo wa elimu wa 7-4-2-3 ubadilishwe na kuwa 8-4-4. (ii) Chuo Kikuu cha pili kianzishwe na Kiswahili kifunzwe chuoni humo

kama somo la lazima. Hii ni kwa sababu kulikuwa na wanafunzi wengi waliofuzu kutoka chuoni lakini hawakuweza kujieleza kwa ufasaha katika lugha ya taifa.

Mambo yafuatayo yalitekelezwa: (i) Mfumo wa elimu wa 8-4-4 ulianzishwa mwaka wa 1982 ambapo

Kiswahili kilianza kuwa somo la lazima na la kutahiniwa katika mtihani wa darasa la nane (K.C.P.E – 1985) na kidato cha nne (K.C.S.E – 1989).

(ii) Chuo Kikuu cha Moi kilianzishwa pamoja na Idara ya Kiswahili mwaka wa 1987.

(iii) Wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika vyuo vikuu vya kitaifa walianza kufunzwa vipengele vya Kiswahili kama sehemu ya kozi ya lazima ya mawasiliano.

51

(e) Tume ya Kamunge (1988) “Report of the Presidential Working Party on Education and Manpower

Training for the next decade and beyond” Uchunguzi uliofanywa na tume hiyo ulionyesha kwamba usajilishaji wa wanafunzi wa ngumbaro ulianza kupungua baada ya kufikia kilele mwaka wa 1978. Hii ni kwa sababu vitabu mwafaka vya kusomwa katika baadhi ya lugha za kienyeji havikuwepo. Kwa hivyo ilipendekezwa kwamba vitabu hiyo viandikwe katika lugha mbalimbali za kienyeji. Lakini kama Mbaabu (1991b) anavyosema, ingefaa zaidi kama vitabu hivyo vingeandikwa kwa Kiswahili ambayo ni lugha ya taifa. (f) Tume ya Koech (1999) Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyopendekezwa: (i) Mfumo wa elimu wa 8-4-4 ubadilishwe na kuitwa TIQET (Totally

Integrated Quality Education and Training) ambapo mtihani wa C.P.E utafanywa katika darasa la saba na mtihani wa G.C.S.E utafanywa katika kidato cha nne.

(ii) Lugha ya Kiswahili, lugha ya Kiingereza na hesabu yawe masomo ya lazima katika shule za msingi na za upili.

(iii) Lugha ya Kiswahili na Fasihi ya Kiswahili yafundishwe kama masomo mawili tofauti. Kadhalika Lugha ya Kiingereza na Fasihi ya Kiingereza yafundishwe kama masomo mawili tofauti.

(iv) Wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu waruhusiwe kujifunza kwa lugha zao za kwanza (lugha ya mama) kwa sababu wengi wao hawawezi kuwasiliana kwa Kiingereza. Lakini wale wanaosomea mjini watumie Kiswahili.

(v) Masomo ya kiutendaji yafundishwe katika shule za msingi lakini yasitahiniwe kwa sababu yanapoteza wakati na tena yanawavunja moyo wanafunzi, wazazi na walimu.

(vi) Katika mtihani wa C.P.E, masomo matano pekee yatahiniwe badala ya masomo saba yanayotahiniwa katika K.C.P.E.

(vii) Katika mtihani wa G.C.S.E, kiwango cha chini cha masomo yatakayotahiniwa ni masomo saba lakini alama zitatolewa katika masomo sita ambayo mwanafunzi atafanya vyema zaidi.

(viii) Mtihani wa kidato cha nne (G.C.S.E) ufanywe mara mbili kwa mwaka ambapo wanafunzi wanaofeli mara ya kwanza wanaweza kuruhusiwa kuufanya tena mara ya pili.

Baadhi ya mapendekezo hayo tayari yameanza kutekelezwa. Hata hivyo, msimamo wa serikali ni kwamba utekelezaji kamili wa ripoti ya Koech utagharimu pesa nyingi sana, hivyo basi, baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa yatafanyiwa marekebisho kabla ya kutekelezwa.

Kati ya Tume hizo zote zilizoundwa baada ya uhuru, Tume ya Mackay ndiyo imechangia zaidi maendeleo ya Kiswahili nchini licha ya matatizo yaliyoukumba mfumo wa elimu wa 8-4-4.

52

(B) SHUGHULI ZA SERIKALI Matumizi ya Kiswahili kama lugha ya taifa katika shughuli za serikali kwa ujumla

yanajitokeza kwa njia zifuatazo: (i) Mawasiliano ya kila siku baina ya wananchi, wanasiasa na maafisa wa

serikali. Kwa mujibu wa King’ei (2001:102), moja kati ya sifa za usemi wa kisiasa nchini Kenya ni kubadili na kuchanganya msimbo, na hali hii hutatiza maendeleo ya Kiswahili.

(ii) Bungeni: Ni wabunge wachache sana ambao hutumia Kiswahili katika mijadala, hasa wale watokao pwani na labda wale wasiokimudu Kiingereza vizuri. Kiingereza ndicho hutumiwa kuendeshea mambo mengi ya Bungeni.

(iii) Mahakama: Kiswahili hupewa nafasi ndogo sana wakati wa kundesha kesi katika mahakama ndogo. Kiingereza hutumiwa wakati mwingi kuendesha shughuli za mahakamani.

(iv) Magereza: Kiswahili hutumiwa katika kuendesha shughuli za magereza ingawa stakabadhi nyingi huandikwa kwa Kiingereza.

(v) Katiba: Hivi sasa Katiba ya Kenya yapatikana tu kwa lugha ya Kiingereza ingawa watu wengi wamependekeza kwamba ingetafsiriwa pia kwa Kiswahili ili wananchi wengi waisome na kuzielewa sheria za nchi hii sawasawa, pamoja na kuzijua haki zao. Ili kutimiza lengo hilo la kuwaelimisha wananchi kikatiba, msomi wa Kiswahili, Prof Kimani Njogu, amekuwa akichapisha mfululizo wa makala yanayoitwa “Zijue Haki Zako” katika gazeti la Taifa Leo. Ingawa hatuna uhakika kwamba Katiba Mpya ijayo itatafsiriwa kwa Kiswahili, tunafahamu kwamba kamati inayosimamia urekebishaji wa Katiba imekuwa ikikusanya maoni ya wananchi wengi kwa Kiswahili.

(vi) Sherehe za kitaifa: Sherehe muhimu za kitaifa na hotuba zinazosomwa katika sherehe hizo huwa kwa Kiingereza lakini Kiswahili hupewa nafasi ya pembezoni tu.

(vii) Mikutano ya hadhara ya wanasiasa huendeshwa kwa Kiswahili katika sehemu nyingi nchini isipokuwa mikutano ya sehemu fulani za vijijini.

(viii) Vituo vya Polisi na kambi za Wanajeshi pia hutumia Kiswahili. (ix) Viapo vya watumishi wa serikali huendeshwa kwa Kiswahili. Watumishi hao

ni pamoja na Rais, Mawaziri na wasaidizi wao, na pia Mahakimu. (x) Baadhi ya vyeti kama vile vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa na vya kifo,

huandikwa kwa Kiingereza na Kiswahili pia. Kwa ujumla, nafasi ya Kiswahili katika shughuli za serikali ni duni

ikilinganishwa na nafasi ya lugha ya Kiingereza. Serikali ya Kenya haijabuni sera dhahiri ya kuendeleza Kiswahili kama lugha ya taifa. Mara nyingi lugha rasmi ya Kiingereza na hata lugha za kikabila hutumiwa katika miktadha ambamo lugha ya taifa (Kiswahili) ingepaswa kutumiwa, na jambo hili linatatiza maendeleo ya Kiswahili.

(C) VYOMBO VYA HABARI Vyombo vya habari vinajumlisha redio, runinga, magazeti, majarida, filamu na

tarakilishi, yaani ‘kompyuta.’ Idhaa zinazotangaza kwa Kiswahili nchini Kenya ni pamoja na Kenya Broadcasting Corporation (K.B.C), Nation F.M., Radio Citizen, Baraka F.M., Pwani F.M., Iqra F.M., Kameme F.M., East F.M., na Redio Sayare (Sauti

53

ya Rehema) mjini Eldoret. Hali kadhalika vituo vya runinga vinavyotumia Kiswahili ni pamoja na K.B.C., Nation TV, Kenya Television Network (K.T.N), na Family TV.

Kwa mfano, katika redio ya K.B.C., vipindi vinavyoendeleza Kiswahili ni pamoja

na ‘Lugha Yetu,’ ‘Ongea Lugha Sanifu ya Kiswahili,’ ‘Ukwasi wa Lugha,’ ‘Chemsha Bongo,’ na ‘Ushikwapo Shikamana.’ Katika runinga ya K.B.C., kuna vipindi kama ‘Sanaa ya Kiswahili,’ ‘Tausi,’ ‘Vituko,’ na ‘Burudani la Taarabu.’ Katika redio ya Nation F.M., kuna kipindi cha ‘Kamusi ya Changamka,’ na katika runinga ya Nation, kuna ‘Lulu ya Nation.’ Hata vipindi vya kidini pia vimechangia sana ustawi wa Kiswahili.

Zoezi la 5.2

* Taja vituo mbalimbali vya redio nchini Kenya ambavyo hutangaza kwa Kiswahili kisha ueleze ni vipi lugha hii inaendelezwa katika vituo hivyo. Ingawa vituo hivi vya redio na runinga vimesaidia kuendeleza Kiswahili katika

habari, matangazo na vipindi, vinakumbwa pia na matatizo mbalimbali. Matatizo hayo yametokana hasa na kuwekwa huru kwa sekta ya habari na utangazaji, jambo ambalo limeleta ushindani mkali baina ya vyombo vya habari, ambavyo vinang’ang’ania wasikilizaji na watazamaji. Kulingana na Musau (2001:39), tatizo kuu ni kwamba, nchini Kenya hakuna sera dhahiri katika vyombo vya habari inayoendeleza Kiswahili na kuhifadhi utamaduni wa kitaifa. Inaonekana kwamba vituo vingi vya redio na runinga hutangaza kwa Kiingereza na kuonyesha vipindi vya kigeni. Ifuatayo ni mifano ya matatizo yanayokumba redio na runinga nchini:

Kwanza, kuchipuka kwa vituo vingi vya redio kumesababisha visa vingi vya

matumizi ya kilugha cha Sheng’ na madoido mengi yasiyostahili. Watangazaji hao hufanya hivyo ili kuwavutia wasikilizaji wengi bila kujali iwapo wanatatiza ustawishaji wa Kiswahili au la.

Pili, katika vipindi vingi vya kuburudisha hasa michezo ya kuigiza na pia

matangazo ya kibiashara, ni jambo la kawaida kupata kanuni za sarufi ya Kiswahili zikivunjwa makusudi ili kuwafurahisha wasikilizaji na watazamaji, lakini ni mwiko kuvunja kanuni za sarufi ya Kiingereza.

Tatu, baadhi ya watangazaji hawana ujuzi wa kutosha katika Kiswahili na hivyo

huitumia lugha hii visivyo; hata baadhi ya vipindi hurekodiwa vibaya kwa sababu ya ukosefu wa ujuzi.

Nne, mawimbi ya runinga huwa hayawafikii watu wengine kwa sababu sehemu zingine za Kenya ziko katikati ya milima

54

Tano, Idhaa nyingi humu nchini hazina kibali cha kutangaza kote nchini; hutoa matangazo yao katika miji mikubwa hasa Nairobi na Mombasa.

Sita, vituo vingi hasa vya F.M hutumia ama lugha za kienyeji au Kiingereza, na

jambo hili linaweza kuzidisha hisia za kikabila na utegemeaji wa vipindi vinavyoendeleza utamaduni wa kimagharibi.

Saba, vituo vya runinga pia huwa na mwelekeo mbaya kuhusu Kiswahili kwa

kuamini kuwa Kiswahili ni lugha duni kuliko Kiingereza, na eti haiwezi kujimudu kimawasiliano katika siasa, sayansi, uchumi, kilimo na teknolojia. Wanakitumia katika habari pekee au katika vipindi vya kuburudisha na visivyohitaji mada ngumu. Kiswahili kinafanywa kama lugha ya watu wasiochukulia maisha kwa umuhimu unaofaa au lugha ya mzaha na utani!

Nane, Kiswahili kinapotumiwa katika habari, mara nyingi habari zenyewe huwa

zimeandikwa kwanza na kuhaririwa kwa Kiingereza, kisha zikatafsiriwa kwa Kiswahili bila kujali maana inayojitokeza.

Tisa, mara nyingi vipindi vyenye manufaa hutoweka baada ya kukosa wafadhili,

kwa mfano, Kiswahili Radio Programme na Hadithi za Kale; aidha, wasanii wa baadhi ya vipindi vya redio na runinga wakifariki, hakuna wa kuliziba pengo hilo.

Kumi, baadhi ya vipindi vya Kiswahili vyenye manufaa kwa wanafunzi na

wasomi wengi hutangazwa wakati usiofaa. Mwisho, vituo vya redio na runinga mara kwa mara hushutumu sana habari za

magazeti na hivyo hutatiza usomaji wa magazeti hayo; kwa sababu hiyo, watu wengi huhusisha habari za magazeti na uvumi au uwongo.

Kwa upande mwingine, uchapishaji wa magazeti ya Kiswahili nchini Kenya ni

jambo la kusikitisha sana. Hivi sasa kuna magazeti mawili tu, gazeti la Taifa Leo ambalo huchapishwa kila siku na toleo la Jumapili, na pia gazeti la Jamhuri ambalo hutolewa mara chache. Taifa Leo ndilo gazeti kongwe zaidi la Kiswahili hapa nchini. Gazeti la Jamhuri ni jipya na halijakita mizizi kikamilifu. Ni gazeti ambalo lina mwelekeo unaofaa wa kukuza Kiswahili na linashughulikia mada ngumu zinazohusu lugha na maisha ya kijamii. Gazeti hili lina uwezo wa kuleta sura mpya katika ramani ya vyombo vya habari nchini Kenya. Kinyume na hali ilivyo nchini Tanzania, nchini Kenya magazeti mengi na majarida huchapishwa kwa Kiingereza na lugha za kikabila kama vile Kikuyu na Dholuo.

Kuna pia vijarida vya Kiswahili ambavyo huchapishwa na makampuni ya

kibinafsi na mashirika ya kidini lakini havisambazwi sehemu nyingi. Kwa ujumla, magazeti ya Kiswahili yanayochapishwa nchini Kenya yamechangia ukuzaji wa lugha ya Kiswahili kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na kuandika habari, makala, mashairi, mafumbo ya kujaza maneno, methali, vitendawili, tahakiki za vitabu vipya, hadithi, matangazo, majaribio ya mitihani ya Kiswahili, maoni, na hata kuchora vibonzo. Onyango (2000:8) katika makala yanayoitwa “Magazeti ndiyo uti wa mgongo katika

55

ustawishaji wa Kiswahili,” yaliyochapishwa katika Jamhuri, Desemba 17 – 30, 2000, ameeleza kwa utondoti mchango wa magazeti katika ukuzaji wa Kiswahili; amesisitiza kwamba magazeti yanapotumiwa vilivyo, yanaweza kustawisha lugha hii na wakati huo huo kuwafahamisha, kuwaelimisha na kuwaburudisha kikamilifu wananchi. Hata hivyo, magazeti ya Kiswahili pia yanakumbwa na matatizo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na yafuatayo:

(i) Magazeti hayo huwa na habari chache za kutafsiriwa kutoka magazeti ya Kiingereza.

(ii) Wakati mwingine habari hutafsiriwa kwa njia inayopotosha ujumbe. Habari huandikwa na kuhaririwa harakaharaka katika hekaheka za kuchapisha magazeti ili yawafikie wasomaji mapema, na hali hii husababisha makosa mengi ya tafsiri, maendelezo na mtiririko.

(iii) Magazeti hayo huwa na kurasa chache na pia safu chache zisizowatosheleza wasomaji wengi.

(iv) Ukosefu wa istilahi za Kiswahili za kuwakilisha dhana ngeni zinazojitokeza katika uandishi wa magazeti ya Kiswahili.

(v) Kutozingatia sajili za lugha magazetini kwa ajili ya safu mbalimbali. (vi) Ukoko wa kikoloni miongoni mwa Wakenya wenye kisomo cha juu

wanaodharau magazeti yaliyoandikwa kwa Kiswahili na chochote chenye asili ya Kiafrika.

(vii) Matumizi ya lugha potofu isiyozingatia kanuni za Kiswahili Sanifu, yaani Sheng’, pamoja na uchapishaji mbovu.

(viii) Ukosefu wa matangazo mbalimbali, kwa mfano ya kibiashara na ya nafasi za kazi.

(ix) Baadhi ya waandishi wa habari za magazeti hawana ujuzi wa kutosha katika Kiswahili.

(x) Uhaba wa magazeti na majarida ya Kiswahili. (xi) Uhaba wa wanunuzi na wasomaji wa magazeti ya Kiswahili. (xii) Magazeti hayo hayasambazwi hadi sehemu zingine za nchi. (xiii) Ukosefu wa sera dhahiri ya kukuza Kiswahili katika vyombo vya habari kwa

ujumla. (xiv) Sheria zinazokandamiza uhuru wa uandishi habari, kwa mfano, kutoza

magazeti dhamana ya juu sana kabla ya kuruhusiwa kuchapishwa, na kupeleka nakala za gazeti kwa msajili kabla ya gazeti hilo kutolewa.

Kwa ujumla, matumizi ya Kiswahili katika elimu, shughuli za serikali na vyombo

vya habari nchini Kenya, yanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa sera dhahiri. Baadhi ya watafiti (kwa mfano, Mbaabu, 1991b) wanafikiria kwamba, ukosefu wa sera dhahiri ya kuendeleza Kiswahili nchini Kenya ni moja kati ya sababu zilizochangia kuzuka kwa kilugha cha Sheng’.

Kuna madai kwamba Sheng’ haikuzuka nchini Tanzania kwa sababu sera ya

lugha nchini humo ilikuwa wazi tangu mwanzo, na ililenga katika kukikuza Kiswahili kama lugha ya taifa ya kuwaunganisha wananchi na pia kama lugha rasmi. Licha ya Tanzania kuwa na makabila mengi kuliko Kenya, Kiswahili kimewawezesha kuwa na umoja na kuepuka hisia za ukabila, kinyume na hali ilivyo nchini Kenya. Tangu

56

ilipojipatia uhuru, Tanzania imeunda vyombo mbalimbali vya kuikuza lugha ya Kiswahili ili kukidhi mahitaji yao ya mawasiliano katika nyanja mbalimbali. Ingawa Kenya pia imeunda baadhi ya hivyo vyombo, bado haijafikia kiwango cha Tanzania katika kuendeleza Kiswahili.

(D) SHENG’ NI ‘LUGHA’ GANI? Sheng’ ni kilugha cha mseto kinachotumia maneno ya Kiswahili, Kiingereza na

lugha za kienyeji kama vile Dholuo, Kikuyu na Kiluyia pamoja. Ingawa Sheng’ huchanganya maneno kutoka lugha mbalimbali, inafikiriwa kwamba neno lenyewe lilibuniwa kutokana na maneno ya lugha mbili, yaani, “Sh–” kutoka kwa neno “Swahili” na “-eng” kutoka kwa neno English.” Vilevile, Sheng’ hutumia sarufi inayoelekea kufanana na sarufi ya Kiswahili; kwa mfano, “Oti amekick boli,” yaani, “Otieno ameupiga mpira.” Muundo wa kisarufi wa sentensi hii ni: Kiima + Kitenzi + Yambwa.

Maandishi ya kwanza kabisa kuhusu kilugha cha Sheng’ yalichapishwa katika

magazeti ya Daily Nation ya mwezi wa Februari na Machi mwaka wa 1984. Inasemekana kwamba kilugha hiki kilianza kuzungumzwa na vijana wa sehemu za Eastlands katika mitaa ya mabanda ya jiji la Nairobi, na baadaye kikaenea katika miji mingine kote nchini Kenya. Ingawa bado haieleweki kikamilifu ni kwa nini kilugha cha Sheng’ kilizuka nchini Kenya wakati huo, utafiti wa kiisimu na kiisimu-jamii unaonyesha kwamba sababu tatu zifuatazo ndizo zilichangia sana kuzuka kwa Sheng’:

Kwanza, vijana walihisi kwamba kuna haja ya kutumia lugha rahisi (sahili) ya

mawasiliano ambayo haitawafunga katika kuzingatia kanuni nyingi za kisarufi. Kwa hivyo inaelekea kwamba kwa kiasi fulani, watumiaji wa Sheng’ mara nyingi huwa ni watu wazembe walioshindwa kabisa kuzimudu kanuni za sarufi ya Kiswahili Sanifu. Hii ndiyo sababu maneno mengi ya Sheng’ huundwa kwa kutumia utaratibu wa ufupishaji na ubadilishaji wa silabi za neno, kwa mfano:

Hosi --- ‘hosipitali’ (hospital) Hedi --- ‘mwalimu mkuu’ (headmaster or headmistress) Futi --- ‘mchezo wa kandanda’ (football) Progi --- ‘kipindi cha redio au runinga’ (program) Gava --- ‘serikali’ (government) Thao --- ‘shilingi alfu moja’ (A thousand shillings) Daro --- ‘darasa’ (classroom) Pili, vijana walihisi kwamba kuna haja ya kubuni lugha fulani ambayo

ingewawezesha kuwasiliana kisiri ili watu wengine wasielewe mazungumzo yao. Hii ndiyo sababu maneno mengi ya Sheng’ si ya kudumu, bali hutumiwa kwa muda mfupi kisha yanabadilishwa inapogunduliwa kwamba watu wengi wameyafahamu. Kwa hivyo Sheng’ ni kilugha cha mpito. Mifano ya maneno hayo ni kama vile:

Makopaa, karao --- ‘polisi’ Fathee, mdoss, buda, mbuyu --- ‘baba’ Panch, kobole, ngovo, --- ‘sarafu ya shilingi tano’

57

Tatu, vijana kutoka makabila mbalimbali walitaka kujitambulisha kijamii kama kikundi cha watu wa kisasa waliostaarabika, lakini sio watu wa kizazi cha zamani. Walitaka kujitambulisha kama watu wanaozungumza lugha moja ya kuvutia na inayotamkika vizuri, watu wanaoishi mijini wala si mashambani (vijijini), watu walio na matatizo yanayofanana, watu walio na fikira zinazofanana, na watu walioendelea kimavazi, kimuziki, kimapenzi, na katika starehe nyinginezo. Ama kwa kweli, sababu moja inayowafanya watu wengi kuipenda na kuikumbatia Sheng’ ni ule mvuto, mnato na mkato wa matamshi yake. Kwa mfano, chunguza maneno yafuatayo:

Vifit --- ‘vizuri sana’ Tumefist --- ‘tumekula’ Tukonekt --- ‘tukutane’ Maspidi --- ‘haraka sana’ Anadraiv --- ‘anaendesha gari’ Amenoki --- ‘amekasirika sana’ Nibaie --- ‘ninunulie’ Falla --- ‘mjinga’ Mastoneface --- ‘sura mbaya’ Echessa (1990:53) anasema kwamba, kilugha cha Sheng’ ni muhimu sana hasa

kwa vijana na watu wasiokuwa na elimu ya kutosha kwa sababu, wanapokumbwa na tatizo la lugha, ile hali ya kubadili na kuchanganya Kiingereza na Kiswahili huwarahisishia mawasiliano. Hata hivyo, Sheng’ huathiri zaidi Kiswahili kuliko inavyoathiri Kiingereza kwa sababu hutumia sarufi inayofanana na ya Kiswahili. Kwa sababu hiyo, watu wengi hushindwa kutofautisha maneno ya Sheng’ na ya Kiswahili Sanifu, na jambo hili linatatiza sana maendeleo ya lugha hii. Utafiti unaonyesha kwamba siku hizi Sheng’ hutumiwa na jamii nzima; vijana kwa wazee, waalimu kwa wanafunzi, na wazazi kwa watoto, wote hawa wamo mbioni kukisakama Kiswahili na mitindo ya Sheng’. Kama anavyosema Momanyi (2001:87):

“…lugha ya Kiswahili imefika kwenye njia panda kwani idadi kubwa ya watu hawawezi kupambanua matumizi bora ya lugha ni yapi.” Mimi binafsi ninaamini kwamba, kilugha cha Sheng’ hakiwezi kutoweka kamwe

kwa sababu kimekita mizizi katika jamii nzima na kina umuhimu wake kimawasiliano. Hata hivyo, Kiswahili Sanifu bado kinaweza kustawishwa ikiwa wananchi watatambua umuhimu wa lugha hii, na ikiwa serikali ya Kenya itaunga mkono kivitendo harakati za kuiendeleza lugha ya Kiswahili. Baadhi ya hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuendeleza Kiswahili nchini Kenya ni pamoja na zifuatazo:

Kwanza, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ianzishwe katika Chuo Kikuu cha

Kenyatta (tayari imeanzishwa). Pili, serikali ishiriki kikamilifu katika maandalizi ya vikao vya Kiswahili kama vile warsha, semina na makongamano, na isaidie kutekeleza maazimio yanayopitishwa. Kwa mfano, inaweza kufadhili miradi inayokusudiwa kuendeleza Kiswahili. Tatu, kamati ya wasomi wa Kiswahili kutoka Afrika Mashariki na Kati iundwe ili kusanifisha istilahi na kuandaa pamoja mikakati ya kukuza Kiswahili. Mwisho, vyama vya Kiswahili vinavyoundwa shuleni, vyuoni, magazetini na

58

kwingineko, vishirikiane na wote wanaohusika ili kutafuta mbinu za kuboresha mafunzo ya Kiswahili na matumizi bora ya lugha hii nchini Kenya. Wale wanaohusika ni pamoja na wachapishaji magazeti, majarida na vitabu, watangazaji wa redio na runinga, wanafunzi, waalimu na wahadhiri, wasimamizi wa shule na vyuo, na watumishi wa serikali. Sasa tuangalie sera ya lugha nchini Uganda.

5.4 Sera ya Lugha nchini Uganda baada ya Uhuru

Baada ya Uganda kupata uhuru mwaka wa 1962, chama cha U.P.C kiliungana na chama cha Kabaka Yekka kuunda serikali. Ingawa Rais Milton Obote wa U.P.C alikusudia kukiteuwa Kiswahili kuwa lugha ya taifa, alipingwa na chama cha Kabaka Yekka ambacho kilipendelea lugha ya Kiganda. Aidha, makabila mengine pia yalitaka lugha zao zitumike serikalini na hali hii imezidisha ukabila nchini humo.

Baada ya Rais Idi Amin kuipindua serikali mwaka wa 1971, alijaribu kuleta

umoja kwa kuamuru kwamba Kiswahili kitumike kama lugha pekee ya taifa. Aliwatumia wanajeshi wake kuitekeleza amri hii kimabavu, jambo ambalo liliwafanya Waganda wengi kukichukia Kiswahili kufikia sasa. Hivi sasa hakuna lugha moja ambayo imetangazwa kuwa lugha ya taifa au lugha rasmi kwani ni lugha nyingi tu ambazo hutumiwa. Hata hivyo, vifuatavyo ni vyombo vichache ambavyo vimetumiwa kueneza Kiswahili nchini Uganda baada ya uhuru:

(A) CHUO KIKUU CHA MAKERERE Chuo hiki kina taasisi ya lugha ambamo Kiswahili hufundiswa katika kiwango

cha shahada ya kwanza. Tatizo kubwa ni kwamba mara nyingine hakuna wanafunzi wa kujisajili. Pia wahadhiri hawapatikani kwa urahisi na lugha ya Kiswahili haina maabara ambayo ni muhimu katika kuwafunza wanafunzi lugha kwa mara ya kwanza. Aidha, kuna uhaba wa vitabu na makala za Kiswahili zenye maudhui ya kiwango cha juu. Vilevile, Mukama (1989:6) anasema kwamba hawana fedha za kugharamia masomo ya wanafunzi ambao wangependa kujiendeleza katika Kiswahili ili warudi baadaye kufundisha Kiswahili idarani. Kuna pia Chuo Kikuu cha Kiislamu mjini Mbale na Kiswahili ni miongoni mwa masomo yanayofundishwa chuoni humo.

(B) BARAZA LA MITIHANI LA TAIFA Baraza hili linakitambua Kiswahili kama somo la kutahiniwa katika shule za upili

lakini hakifunzwi katika shule za msingi. Hata hivyo, kwa sababu ya ukosefu wa vitabu na miongozo ya masomo ya Kiswahili, ni wanafunzi wachache tu ambao hujitolea kuufanya mtihani wa kidato cha nne na cha sita, ambapo wengi hushindwa na kukata tamaa. Wizara ya Elimu iliombwa isaidie kusuluhisha tatizo hilo lakini bado hatua madhubuti hazijachukuliwa. Kwa sababu hiyo, Mukama anasema kwamba Kiswahili kimeachwa kujiuza na kujieneza chenyewe.

(C) REDIO NA RUNINGA Takriban lugha kumi na mbili za kienyeji hutumika katika Radio Uganda, lakini

Kiganda na Kiingereza ndizo hutumika sana kwenye runinga. Balinda na Ruhangalinda (1994:21) wanasema kwamba ingawa vipindi vya Kiswahili pia hutangazwa katika Radio Uganda, watangazaji wengi hawana ujuzi wa kutosha wa lugha hii. Kadhalika, kuna

59

baadhi ya maafisa wanaojitahidi kuangamiza matangazo ya Kiswahili na kuendeleza lugha za kienyeji. Kwa hivyo changamoto kubwa sasa ni kuanzishwa upya Idhaa ya Kiswahili inayojitegemea. Lakini tatizo ni kwamba hivi sasa, Uganda bado haina lugha moja ya taifa; kuna watu wanaotaka lugha ya Kiswahili itumiwe ili kudumisha amani nchini, ilhali wengine wangependa kutumia mojawapo ya lugha za kienyeji. Lugha hizo ni pamoja na Luganda, Ateso, Runyoro, Rutooro, Runyankore, Rukiga, Luo na Karamojong’. Kiingereza na baadhi ya lugha hizo za kienyeji hutumika kama lugha rasmi ingawa serikali bado haijatangaza msimamo kamili.

(D) MAGAZETI Kiganda na Kiingereza hutumika zaidi magazetini kuliko lugha zingine. Hivi sasa

hakuna gazeti wala jarida lolote la Kiswahili nchini humo. Magazeti ya Kiswahili ambayo yaliwahi kuchapishwa kwa muda mfupi ni pamoja na “Mkombozi,” “Habari za Uganda Police,” “Mwenzako,” na kijarida kilichoitwa “Lulu ya Afrika.” Kawoya (1985:38) anasema kwamba yote hayo yalitoweka kwa sababu ya uhaba wa wasomaji.

(E) IDARA YA JESHI, POLISI NA MAGEREZA Idara hizi pia husaidia kukuza Kiswahili hata ingawa ni Kiswahili cha

mazungumzo tu. Maoni ya wasomi wengi wanaotoka Uganda, (kwa mfano, Bukenya, Kawoya, Senoga-Zake na Mukama) ni kwamba, Waganda wengi wanakichukia Kiswahili kwa sababu wanakinasibisha na Idara hizi ambazo zina sifa mbaya sana. Kwa mfano, Senoga-Zake (mahojiano na yeye) anasema kwamba mwanajeshi anapotaka kumwua mtu, lugha anayotumia ni Kiswahili. Naye Bukenya (mahojiano na yeye) anasema kwamba wenye Idara hizo hutumia Kiswahili kuwanyanyasa wananchi. Kawoya (1985:39) anasema kwamba Kiswahili hutumiwa na mapolisi wanapowanyanyasa raia kwenye mipaka ya nchi hiyo. Naye Wardhaugh (1987:201) anaeleza kwamba Kiswahili kinanasibishwa na lile jeshi lililokaribishwa nchini Uganda kutoka Tanzania na ambalo lilifanya makao nchini humo kwa muda mrefu hata Waganda wakaanza kuwachukia wanajeshi hao. Anasema kwamba Kiswahili huchukuliwa kama lugha ya barabarani tu ambayo mtu hawezi kujivunia anapoizungumza.

Kwa sababu ya kudharauliwa hivyo na wananchi, imekuwa vigumu sana kuikuza

na kuieneza lugha ya Kiswahili nchini Uganda. Licha ya vikwazo hivyo, wasomi wengi bado wanaona kwamba kuna matumaini ya kuendeleza Kiswahili nchini humo. Bukenya (mahojiano na yeye) anasema kwamba Rais Museveni anakiunga mkono Kiswahili na anakielewa vizuri sana. Ladefoged (1971:30) na Kawoya (1985:44) wanasema kwamba serikali hiyo ikiamua kubadilisha sera yake ya lugha, bila shaka mielekeo ya wananchi kuhusu lugha hii pia itabadilika. Naye Mukama (1989:11) anasema kwamba yeye na wenzake bado wanaamini kwamba Kiswahili “hakitakufa” nchini humo, na wanatumai kwamba wapenzi wa Kiswahili watajitokeza kuwasaidia katika jitihada zao za kuikuza lugha hii nchini Uganda. 5.5 Hitimisho

Katika somo hili, nimejadili kwa tafsili sera ya lugha nchini Tanzania, Kenya na Uganda baada ya uhuru, huku nikizingatia mchango wa vyombo mbalimbali ambavyo vimetumiwa kustawisha Kiswahili katika nchi hizo. Aidha nimeeleza matatizo

60

yanayovikumba vyombo hivyo na nikataja baadhi ya hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuendeleza Kiswahili. Vilevile tumezungumzia swala la Sheng’ na athari zake kwa Kiswahili Sanifu. Katika somo lijalo, nitazungumzia uundaji wa msamiati na istilahi. 5.6 Maswali

? 1. Eleza jinsi sera ya lugha nchini Tanzania ilivyosaidia lugha ya Kiswahili

kupiga hatua kubwa katika matumizi nchini humo kuliko nchini Kenya baada ya uhuru.

2. Tathmini mchango wa Tume ya Mackay (1981) na Tume ya Koech (1999) katika kustawisha Kiswahili nchini Kenya.

3. Huku ukitoa mifano mwafaka, jadili mchango wa vyombo vitatu vya habari katika ukuzaji wa Kiswahili nchini Kenya, kisha uonyeshe matatizo yanayovikumba na jinsi yanavyoweza kutatuliwa.

4. Eleza ni vipi Sheng’ inavyoathiri maendeleo ya Kiswahili nchini Kenya na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuikabili.

5. “Juhudi za kuendeleza Kiswahili nchini Uganda baada ya uhuru bado hazijafaulu.” Jadili kauli hii.

5.7 Marejeleo ya Lazima Balinda, D.N. na A.A. Ruhangalinda (1994). “Sera ya Matumizi ya Kiswahili: Matatizo,

Mafanikio, na Taathira za Matangazo ya Kiswahili kwa jumla nchini Uganda,” katika Kijarida cha CHAKA (Chama cha Kiswahili cha Afrika), Nambari 1., uk. 21-22.

Echessa, P.G. (1990). “A Study of the Word Structure and Processes involved in Word Formation in Sheng’: A Case Study of Eastlands Area of Nairobi.” M.A. Thesis, Kenyatta University.

King’ei, K. (2001). Language, Political Communucation and Development: A Brief Analysis of Contemporary Kenyan Political Discourse,” katika Kiswahili: A Tool for Development – The Multidisciplinary Approach. Eldoret: Moi University Press.

Maganga, C. (1983). “Juhudi za Ukuzaji wa Kiswahili Tanzania Bara,” katika Lugha ya Kiswahili: Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.

Marshad, H.A. (1993). Kiswahili au Kiingereza? (Nchini Kenya). Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Mbaabu, I. (1991b). “The Impact of Language Policy on the Development of Kiswahili in

Kenya, 1930-1990.” Ph.D. Thesis, Howard University.

61

Mekacha, R.D.K. (1995). “Kwa nini Bado Kiingereza ni Lugha ya Kufundishia Elimu ya Juu Tanzania?” katika KIOO CHA LUGHA (Mfululizo Mpya), Juzuu la 1 Nam. 2, uk.28-44.

Mlacha, S.A.K. (mh.) (1995). Kiswahili na Vyombo vya Habari. Dar es Salaam: TUKI. Mlacha, S.A.K. (mh.) (1995). Kiswahili katika Kanda ya Afrika Mashariki. Dar es

Salaam: TUKI. Momanyi, C. (2001). “Matumizi ya Kiswahili katika Njia Panda: Mtazamo wa Kiisimu-

Jamii,” katika Kiswahili: A Tool for Development – The Multidisciplinary Approach. Eldoret: Moi University Press.

Mukama, R. (1989). “Hali na Hadhi ya Kiswahili nchini Uganda,” katika Usanifishaji wa Istilahi za Kiswahili: Makala za Semina ya Kimataifa. Dar es Salaam: TUKI.

Musau, P.M. (2001). “Freeing the Airwaves or Cultural Enslavement: The Case of Media in Kenya,” katika Kiswahili: A Tool for Development – The Multidisciplinary Approach. Eldoret: Moi University Press.

Musavi, L.M. (2001). “Magazeti ya Kiswahili na Maendeleo nchini Kenya,” katika Kiswahili: A Tool for Development – The Multidisciplinary Approach. Eldoret: Moi University Press.

Onyango, J.O. (2000). “Magazeti ndiyo uti wa mgongo katika ustawishaji wa Kiswahili,” katika Gazeti la Jamhuri, Desemba 17-30, 2000 uk. 8.

***Marejeleo ya ziada yanapatikana katika somo la mwisho.

62

SOMO LA 6

UKUZAJI WA MSAMIATI NA ISTILAHI 6.0 Utangulizi

Katika somo hili, nitafafanua mbinu mbalimbali zinazotumiwa kuundia msamiati na istilahi za Kiswahili. Pia nitaeleza matatizo ambayo yamejitokeza katika harakati za kuunda istilahi za Kiswahili na jinsi yanavyoweza kutatuliwa. Nitaanza kwa kueleza namna somo hili linavyohusiana na maswala ya historia ya Kiswahili.

Tangu zamani, wageni mbalimbali waliowahi kutembelea pwani ya Afrika

Mashariki waliwaathiri Waswahili kwa njia mbalimbali. Wageni hao ni pamoja na Waarabu, Wareno, Wahindi, Waingereza na wengineo (Tazama Somo la Kwanza). Moja kati ya athari walizoleta ni kuingiza msamiati wa kigeni katika Kiswahili ili kutosheleza mawasiliano ya kila siku katika nyanja mbalimbali za maisha. Nyanja hizo ni pamoja na biashara, elimu, siasa, kilimo na teknolojia.

Tangu enzi za wasafiri wa zamani na wakoloni mpaka sasa, kumetokea

maendeleo makubwa katika nyanja hizi ambayo yamesababisha haja ya kuunda msamiati na istilahi mpya ambazo zinahitaji kutumiwa ili kutosheleza mawasiliano katika nyanja hizo. Aidha, wakati mwingine lugha inapotumiwa kwa miaka mingi, baadhi ya maneno yake yanaweza kuchakaa, kubadili au kupoteza maana yake kwa sababu ya mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika jamii. Ili Kiswahili kiweze kutumiwa kikamilifu katika nyanja mbalimbali za maisha, ni lazima kiwe na istilahi za kutosha. Kwa sababu hiyo, ni muhimu kujadili mbinu mbalimbali ambazo hutumiwa kuunda istilahi mpya za Kiswahili kwa ajili ya kutosheleza mawasiliano katika nyanja mbalimbali.

Kwa ambavyo somo hili linahusu uundaji wa istilahi katika Kiswahili, ni muhimu

turejelee pia visawe vya istilahi hizo katika lugha za kigeni kama vile Kiingereza. Ni muhimu kutafsiri istilahi hizo kwa sababu ‘tafsiri’ ni miongoni mwa mbinu za uundaji wa msamiati na istilahi (Tazama mbinu nambari ‘D’). Kwa ambavyo tafsiri huhusisha matumizi ya maneno ya lugha mbili tofauti, itabidi tutumie maneno mengi ya Kiingereza katika somo hili ili liweze kueleweka vilivyo (hata kama hii ni kozi ya Kiswahili).

Kulingana na Kamusi ya Kiswahili Sanifu (TUKI, 1981:187), ‘msamiati’ ni

jumla ya maneno yanayotumiwa na watu katika lugha. Nayo Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (TUKI, 1990:56) inaeleza kwamba, ‘istilahi’ ni mfumo wa msamiati maalum unaotumiwa katika uwanja fulani mahsusi. Katika Kiingereza, msamiati ni ‘vocabulary’ ilhali istilahi ni ‘terminology.’ Ukuzaji wa msamiati na istilahi ni jambo la kawaida katika lugha zote. Maneno mapya huundwa katika lugha ili kutosheleza mahitaji ya mawasiliano. Tatizo kubwa linalozuia matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali za maisha ni ukosefu wa istilahi za kutosha.

63

6.1 Madhumuni

Baada ya kulipitia somo hili, ninatarajia kwamba utaweza: (i) Kufafanua mbinu mbalimbali zinazotumiwa kuundia msamiati na istilahi

za Kiswahili. (ii) Kueleza matatizo yanayokumba uundaji wa istilahi za Kiswahili na jinsi

yanavyoweza kutatuliwa.

6.2 Mbinu za Uundaji wa Msamiati na Istilahi

Watafiti wengi wa Kiswahili wamezungumzia mbinu mbalimbali zinazoweza kutumiwa kuundia msamiati na istilahi za Kiswahili. Hawa ni pamoja na Mbughuni (1989:103-109), Tumbo-Masabo na Mwansoko (1992), Kiango (1995:46-54), Chimerah (1998b) na wengineo. Zifuatazo ni baadhi ya mbinu hizo:

(A) URADIDI (TAKRIRI) Ni urudiaji wa neno zima au sehemu ya neno hilo ili kupata neno jipya lenye

maana tofauti. Mifano ni kama ifuatayo: Nyoko --- Nyokonyoko Tinga --- Tingatinga Bata --- Batabata Mbele --- Kimbelembele (B) UPANUZI WA MAANA Ni kulipatia neno fulani maana mpya katika matumizi. Maana mpya huwa kama

kivuli cha maana asili ya neno hilo. Mifano ni kama ifuatayo: (i) Kifaru: Maana asili --- Aina ya mnyama mkubwa tena mkali afananaye

na kiboko na mwenye kipusa usoni. Maana mpya --- Gari la chuma la kivita lenye mzinga. (ii) Kupe: Maana asili --- Mdudu mdogo agandaye mwilini na kufyonza

damu ya wanyama. Maana mpya --- Mnyonyaji; mtu aishiye kwa jasho la wengine. (iii) Kigogo: Maana asili --- Kipande kikubwa cha mti ulioanguka au

kukatwa. Maana mpya --- Mtu mwenye madaraka makubwa mahali pake pa

kazi; au kiongozi wa ngazi ya juu. (iv) Mkereketwa: Maana asili --- Kukereketa ni kuasha kooni au kinywani. Mara nyingi kitu kinapomwasha mtu, huwa kinamuudhi. Maana mpya --- Mtu aliyetopea katika ushabiki wa chama,

itikadi, dini, na kadhalika, ambaye anaudhiwa na changamoto kutoka kwa wapinzani wake.

64

(C) UTOHOZI Ni kuyapatia maneno yaliyokopwa matamshi na maandishi ya lugha pokezi.

Mifano ni kama ifuatayo: Office --- Ofisi au Afisi Bicycle --- Baiskeli Bank --- Banki au Benki Television --- Televisheni Census --- Sensa. Waqt (Kiarabu) --- Wakati Hakim (Kiarabu) --- Hakimu (D) KUTAFSIRI Katika mbinu hii, maana ya neno lililokopwa hutolewa kwa lugha nyingine, yaani

lugha pokezi. Mifano ni kama ifuatayo: Right Angle --- Pembemraba Beanfly --- Nziharage Armyworm --- Viwavijeshi Bud disease --- Ugonjwa wa vichomozi Safety Period --- Kipindi Salama Secondary School --- Shule ya Upili Absurd --- Ubwege Dialogism --- Usemezo Deconstruction --- Udenguzi Leader of the Opposition --- Kiongozi wa Upinzani Scramble for the Presidency --- Kinyang’anyiro cha Urais (E) UFUPISHAJI Ufupishaji wa Akronimu ni uunganishaji wa sehemu ya kwanza ya maneno

mawili au zaidi. Mifano ni kama ifuatayo: UKIMWI --- Upungufu wa Kinga Mwilini CHAKITA --- Chama cha Kiswahili cha Taifa WAKITA --- Waandishi wa Kiswahili wa Taifa TUKI --- Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili GAREX --- Garissa Express KAMATA --- Kampuni ya Mabasi Tanzania KAUDO --- Kampuni ya Usafiri Dodoma SHIHATA --- Shirika la Habari Tanzania Vifupisho vingine ni kama vile FAO, UNICEF, NATO, UNEP,na UNESCO. (F) UHULUTISHAJI Ni kuunganisha visehemu mbalimbali vya maneno mawili au zaidi ili kubuni

neno moja la mchanganyiko. Kwa kawaida sehemu ya mwanzo ya neno la kwanza huunganishwa na sehemu ya mwisho ya neno la pili, kwa mfano:

Runinga --- (Rununu + Maninga), yaani ‘Television.’ Katika Kiswahili cha zamani, ‘Rununu’ ni sauti inayosikika kutoka mbali, na ‘Maninga’ ni macho yanayoona mbali.

65

Tarakilishi --- Mtambo au mashini inayopanga tarakimu kama akili, yaani ‘Computer.’

Utandaridhi --- Utamaduni unaotanda ardhi, yaani ‘Globalization.’ Msikwao --- Mtu asiye na kwao, yaani ‘Vagrant’ au ‘Vagabond.’ Chajio --- Chakula cha jioni, yaani ‘Supper.’ Chamcha --- Chakula cha mchana, yaani ‘Lunch.’ Fupaja --- Fupa la paja, yaani ‘Thigh bone.’ Kidukari --- Kidudu kikulacho sukari, yaani ‘Aphid.’ Kidungata --- Kidudu kinachokula unga na nta, yaani ‘Mealy bug.’ Kinyotomvu --- Kidudu kinachonyonya utomvu, yaani ‘Plant bug.’ Kiuwadudu --- Dawa au kemikali iuwayo wadudu, yaani ‘Insecticide.’ Maneno ya Kiingereza yaliyoundwa kwa kuufuata utaratibu huo ni kama vile: Brunch --- Chakula kinachojumlisha Breakfast + Lunch. Infortainment --- Information + Entertainment. Fantabulous --- Fantastic + Fabulous. (G) UAMBATANISHAJI Ni kuunganisha maneno mawili pamoja ili kuunda neno moja. Maneno

yanayounganishwa yanaweza kuwa ya aina mbalimbali, kwa mfano: Nomino + Nomino Mwana + nchi ‘Mwananchi’ (citizen) Mwana + sesere ‘Mwanasesere’ (doll) Mwana + siasa ‘Mwanasiasa’ (politician) Ngao + mwili ‘Ngaomwili’ (antibiotic) Nomino + Kivumishi Siasa + kali ‘Siasakali’ (leftist) Mwana + haramu ‘Mwanaharamu’ (illegitimate child) Soko + huria ‘Sokohuria’ (open market) (Kiambishi awali) + Kitenzi + Nomino

Ki + pima + mwendo ‘Kipimamwendo’ (speedometer) Ki + daka + tonge ‘Kidakatonge’ (epiglottis)

Ki + fungua + mimba ‘Kifunguamimba’ (first-born child) Ki + tinda + mimba ‘Kitindamimba’ (last-born child) Ki + tega + uchumi ‘Kitegauchumi’ (investment) Ki + paaza + sauti ‘Kipaazasauti’ (microphone) Ki + amsha + kinywa ‘Kiamshakinywa’ (breakfirst) M + cheza + shere ‘Mchezashere’ (player of mockery tricks) M + piga + debe ‘Mpigadebe’ (supporter) M + chimba + kaburi ‘Mchimbakaburi’ (grave digger) M + cheza + kamari ‘Mchezakamari’ (gambler) M + fanya + kazi ‘Mfanyakazi’ (worker) (Kiambishi awali) + Kitenzi + Kivumishi Ki + ona + mbali ‘Kionambali’ (binoculars)

66

(H) UNYAMBUAJI Ni upachikaji wa viambishi awali na viambishi tamati kwenye mzizi wa neno ili

kuunda (ma)neno tofauti, kwa mfano: Pika --- m + pishi ‘mpishi’ (kutokana na ‘m + pika + ji’) Fuga --- m + fuga + ji ‘mfugaji’ Tega --- m + tego ‘mtego’ Chana --- ki + chan + u + o ‘kichanuo’ Ingia --- ki + ingi + li + o ‘kiingilio’ Ziba --- ki + zib + o ‘kizibo’ Chochea --- ki + choche + o ‘kichocheo’ au ‘u + choche + zi’ Funga --- ki + fung + o ‘kifungo’ Geuza --- ma + geuz + i Shinda --- m + shind + i ‘mshindi’ au ‘u + shind + i’ (victory) m + shind + e ‘mshinde’ au ‘u + shind + e’ (defeat) Taka --- ma + tak + w + a ‘matakwa’ Penda --- zi + li + zo + pend + w + a ‘zilizopendwa’ Epuka --- zi + si + zo + epuk + ik + a ‘zisizoepukika’ Halali --- halali + sha ‘halalisha’ Haramu --- harami + sha ‘haramisha’ Bora --- bor + esh + a ‘boresha’ au ‘u + bora’ Binafsi --- u + binafsi + sha + ji ‘ubinafsishaji’ (privatization) Tajiri --- tajiri + sha ‘tajirisha’ Fukara --- fukar + ish + a (I) KUBUNI Ni kuvumbua neno jipya kisha kulipachika maana fulani. Kuna ubunaji wa

kinasibu (arbitrary coinage) ambapo hakuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya neno lililobuniwa na kitu kinachotajwa na neno hilo. Aidha, maneno hayo hubuniwa kwa kuzingatia kanuni za kiisimu za lugha husika, kwa mfano:

Golo --- ‘solar system’ Kisopo --- ‘radar’ (Tazama: Kiango, 1995:47). Kuna pia ubunaji wa kutumia vigezo mahsusi ambapo neno linalobuniwa huwa na

uhusiano fulani na kitu kinachotajwa na neno hilo; yaani, maana ya neno hilo hudokeza au huashiria sifa fulani ya kitu kinachotajwa. Sifa hizo na mifano ni kama ifuatavyo:

(i) Sifa ya kimaumbile Mizizipau (Aerial roots) --- yaani mizizi hiyo inaning’inia kama mapau ya

nyumba ambayo hayafiki ardhini bali hukaa juujuu. Ndege (Aeroplane) --- yaani chombo hiki kinafanana na ndege anayepuruka

angani. Kipanya (Computer mouse) --- yaani ni kifaa kinachofanana na panya

ambacho hutumiwa kwenye tarakilishi. (ii) Sifa ya kitabia Pikipiki --- yaani chombo hicho hutoa mlio unaosikika hivyo, pikipikipiki…

67

Tingatinga --- je, mlio wa chombo hiki pia husikika hivyo, tingatingatinga…? Au neno hili limetokana na mwendo wake wa kuyumbayumba, yaani kutingatinga?

Kengele --- yaani mlio wake pia husikika hivyo, kengelengelengele… Haya yote ni maneno ya tanakali sauti. Kifauwongo --- ni mdudu anayejifanya kuwa amekufa wakati anaposhikwa.

Pia ni aina ya mmea (acacia mimosa pudica) anayejifanya amenyauka wakati anapoguswa. Kibaolojia, hii ni mbinu inayotumiwa na viumbe ili kujihami dhidi ya adui.

Gari la moshi --- yaani gari hili hutoa moshi mwingi linapoendeshwa. (iii) Sifa ya kimatumizi Fumbatio --- (Abdomen); yaani kitu hiki kinatumiwa kama fuko (mfuko

mkubwa) ambamo ndani yake mnazuia vitu kama ini (liver), nyongo (spleen) na figo (kidney). Kwa hivyo kitu hiki kimefumbatia vitu fulani ndani ya tumbo la kiumbe.

Shikio --- (Handle); yaani kitu hiki kinatumiwa kushikia kitu kingine. Kibanio --- (Clothes peg); yaani kitu hiki hutumiwa kubania au kuning’iniza

nguo kwenye kamba ya kuanikia. (J) KUINGIZA MANENO YA LAHAJA NA YA LUGHA ZA KIBANTU Kuna wanalugha wanaopendekeza kwamba msamiati mpya wa Kiswahili utolewe

katika lugha za Kibantu ilhali wengine wanapendekeza kwamba utolewe katika lahaja za Kiswahili. Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) linapendekeza kwamba tunapoukosa msamiati wa Kiswahili, kwanza tuutafute katika lahaja za Kiswahili; tusipoupata, basi tujaribu katika lugha za Kibantu; tukishindwa, basi tuangalie katika Kiarabu; na kama hatupati kabisa, basi tutumie tu Kiingereza. Were-Mwaro (2001:301) anasisitiza umuhimu wa kutumia msamiati wa zamani wa Kiswahili anaposema:

“Ufufuaji wa msamiati wa zamani wa Kiswahili ni mbinu inyopaswa kuzingatiwa na wanalugha wote wa Kiswahili katika shughuli ya utandawazi kutokana na umuhimu wake. Hapana lugha hata moja ulimwenguni ambayo imefikia upeo wa juu kiuchumi na kiteknolojia kwa kutegemea sana lugha za kigeni.”

Ifuatayo ni mifano ya maneno kutoka kwa lahaja za Kiswahili na lugha za Kibantu: Bunge --- (Paliament); kutoka lugha ya ‘Ha’ nchini Tanzania. Ikulu --- (Statehouse); kutoka lugha ya ‘Kinyamwezi’ nchini Tanzania (TZ). Kitivo --- (Faculty); kutoka lugha ya ‘Kipare’ nchini Tanzania. Ngeli --- (Noun class); kutoka lugha ya ‘Kihaya’ nchini Tanzania. Kabwela --- (Ordinary citizen); kutoka lugha ya ‘Kinyamwezi’ nchini TZ. Kidomozi --- (Leaf minor); kutoka lugha ya ‘Kibondei’ nchini Tanzania. Fukuzi --- (Weevils); kutoka lugha ya Kingoni. Ngozi --- (Leaf curl); kutoka lahaja ya ‘Kimtang’ata.’ Njeo --- (Tense); kutoka lahaja ya ‘Kiamu’ nchini Kenya. Mbolezi --- (Elegiac poetry); kutoka lahaja ya ‘Kimvita’ nchini Kenya.

68

Sheikh Ahmed Nabhany katika mswada unaoitwa Kandi ya Kiswahili (1978) amefufua maneno yafuatayo kutoka Kiswahili asili cha zamani:

Kiswahili asili Kiswahili Sanifu (maneno yaliyoazimwa) Maloleo --- macho Mafumo --- mikuki Matayo --- lawama Mwiya --- wakati Uhazigi --- zahanati Udandi --- kalamu (penseli au kalamu ya mate) Maenga --- hesabu Msamiati mwingine wa zamani ambao umefufuliwa ni pamaoja na: Nyuni --- ndege Munyu --- chumvi Ulili --- malazi Ndisha --- vitamini Gango --- hospitali Nswi --- samaki Jopo --- paneli Kuna maneno mengine ambayo yamekopwa kutoka lugha za Kenya na

yamezoeleka sana kimatumizi hivi kwamba watu wengi hufikiria kuwa ni maneno ya Kiswahili. Kwa mfano, ‘githeri’ (pure) kutoka lugha ya Kikikuyu, na ‘omena’ (dagaa) kutoka lugha ya Dholuo. Maneno asili ya Kiswahili ni hayo yaliyo katika mabano.

Je, kwa maoni yako, unafikiri kwamba istilahi zote za Kiswahili zilizoundwa kwa kutumia mbinu hizo nilizoeleza zinafaa au hazifai?

Zoezi la 6.1

* Taja maneno mengine ya Kiswahili yaliyoundwa kwa kutumia mbinu nilizoeleza hapo juu.

6.3 Matatizo ya Uundaji wa Msamiati na Istilahi

Ukweli ni kwamba, baadhi ya istilahi za Kiswahili ambazo zimeundwa kufikia sasa zinakabiliwa na matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na yafuatayo:

Kwanza, kuna istilahi mbalimbali ambazo hutumiwa kurejelea dhana moja, yaani

zinatumiwa kama visawe (synonyms). Mifano ni kama vile: Nuklia / Tonoradi --- ‘Nuclear bomb’ Kansa / Saratani --- ‘Cancer’ Kolera / Kipindupindu --- ‘Cholera’ Vokali / Irabu --- ‘Vowel’ Nomino / Jina --- ‘Noun’

69

Saikolojia / Elimunafsia --- ‘Psychology’ Mkoa / Jimbo --- ‘Province’ Digrii / Shahada --- ‘Degree’ Uhandisi / Elimumitambo --- ‘Engineering’ Diploma / Stashahada --- ‘Diploma’ Mifano sita ya kwanza inaonyesha kwamba neno la kutoholewa na la kutafsiriwa

yanatumika yote pamoja. Kwa nini iwe hivyo? Vilevile, istilahi zingine zimetafsiriwa kwa njia ya kutatanisha na kupotosha. Kwa mfano, mtangazaji wa Nation F.M, Ken Walibora, akinukuliwa katika gazeti la Jamhuri (Desemba 17-30, 2000 uk. 9), anazungumzia maneno yafuatayo:

‘Make love’ --- Kula uroda au kufanya mapenzi? ‘Pickpockets’ --- Wezi wa mifuko au wadokozi wa mifukoni au wanyakuzi wa

vibeti? ‘Commercial prostitutes’ --- Makahaba wa kibiashara au wanaouza ngono? Pili, kuna istilahi ambazo zimetafsiriwa neno kwa neno, yaani tafsiri sisisi, na

hivyo basi kupotosha maana. Alama ya kinyota inaonyesha kosa. Mifano ni kama vile: ‘Cold war’ --- *Vita baridi ‘Cocktail party’ --- *Karamu ya mkia wa jogoo ‘Round table meeting’ --- *Mkutano wa meza duara ‘Red carpet reception’ --- *Makaribisho ya zulia jekundu Tatu, kuna istilahi nyingi ambazo zimekopwa na kutoholewa hata pale ambapo

neno asilia la Kiswahili au la lugha yoyote ya Kibantu lingetumiwa, kwa mfano: Neno lililokopwa Neno asili la Kiswahili Daktari --- ‘Tabibu au mganga’ Hospitali --- ‘Gango’ Dhahabu --- ‘Ng’andu’ Nne, kuna istilahi ambazo huendelezwa kwa njia tofauti kutegemea matamshi au

maandishi ya maneno yanayokopwa. Mifano ni kama vile: Ofisi / Afisi ? --- ‘Office’ Ofisa / Afisa ? --- ‘Officer’ Banki / Benki ? --- ‘Bank’ Agosti / Ogasti ? --- ‘August’ Disemba / Desemba ? --- ‘December’ Dansi / Densi ? --- ‘Dance’ Atomi / Atomu ? --- ‘Atom’ Entomoloji / Entomolojia ? --- ‘Entomology’ Sasa ni neno lipi lililo sahihi? Tutazingatia matamshi au maandishi? Kwa nini

hatuwezi kuwa na utaratibu mmoja wa kuunda istilahi za Kiswahili? Tano, kuna uhaba wa istilahi ambazo zimeundwa kwani hazitoshelezi

mawasiliano katika nyanja mbalimbali. Hii ina maana kwamba kuna vitu na dhana nyingi

70

ambazo bado hazijaundiwa istilahi za Kiswahili. Onyango na Musau (2000) wamelitambua tatizo hili katika ufundishaji wa kozi ya Lugha ya Pili ndipo wakapendekeza zaidi ya istilahi tisini za kiisimu zinazoweza kutumiwa katika kozi hiyo. Chimera (1998b) pia amelitambua tatizo hilo ndipo akapendekeza istilahi zinazohusiana na teknolojia ya tarakilishi (computer). Mifano ya istilahi hizo ni kama vile:

Kichapishi --- ‘Keyboard’ Kipanya --- ‘Computer mouse’ Mulishi --- ‘Monitor’ Kiwaa --- ‘Screen’ Thakala --- ‘Hard disk’ Sita, kuna istilahi nyingi zinazoundwa bila ushirikiano, yaani watu wanajiundia tu

kibinafsi na kuanza kuzitumia istilahi zao bila kushauriana na wenzao kwingineko. Vilevile, nchi ya Tanzania hujiundia istilahi zake bila kushirikiana na Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na nchi zingine zinazotumia Kiswahili. Istilahi zinazoundwa kwa njia hii haziwezi kukubalika na watumiaji wa lugha. Mifano ni kama vile:

‘Mobile phone’ --- Simu ya mkono / simu sogezi / simu tembezi / simu ya mfukoni/ simu tamba / simu ya rununu.

‘E – mail’ --- Barua pepe / tarifalishi. ‘University’ --- Ndaki / zutafindaki. Saba, kuna istilahi nyingi ambazo zimeundwa lakini hazijasanifishwa. Nchini

Kenya, tatizo ni kwamba kufikia sasa bado hakuna Baraza la kusanifisha na kuidhinisha matumizi ya istilahi zinazoundwa. Ingawa washiriki wa kipindi cha ‘Lugha Yetu’ katika K.B.C Redio hupendekeza istilahi mpya, kipindi hicho hakina mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya istilahi yoyote. Mifano ya istilahi zinazohitaji kusanifishwa ni pamoja na:

Utandaridhi / utandawazi / urari mataifa / ugolobishaji --- ‘Globalization.’ Muundo msingi / miundo mbinu / amara --- ‘Infrastructure.’ Mzunguko / kiplefti / kizingwa --- ‘Roundabout.’ Nane, kuna istilahi ambazo zimeundwa pasipo kuzingatia kanuni za sarufi ya

Kiswahili; baadhi ya istilahi ni ndefu mno kupita kiasi, kwa mfano: Elimumagonjwawanawake --- ‘Gynaecology.’ Sehemu ya uwakilishi bungeni --- ‘Constituency.’ Tisa, kuna istilahi zinazobeba vivuli vya maana, yaani zina zaidi ya maana moja.

Mifano ni kama vile ‘Kupe,’ ‘Kigogo,’ na ‘Kifaru,’ kama tulivyoona katika mbinu ya Upanuzi wa maana.

Kumi, kuna istilahi ambazo haziwezi kunyambulishwa zikazalisha istilahi zingine

za kikoa. Mfano wa istilahi inayoweza kunyambulika ni kama vile ‘Sumaku’ ambayo inaweza kuzalisha ‘sumakisha’ na ‘usumaku.’ Tazama pia ‘Globe’ – ‘global,’ ‘globalize,’ na ‘globalization.’ Je, istilahi ‘Urari mataifa’ inaweza kunyambulika hivyo?

Mwisho, istilahi nyingi ambazo zimeundwa hazijasambazwa kwa wasomi na wapenzi wa Kiswahili ili zijadiliwe. Kuhusu swala hili, vyombo vya habari vinaweza

71

kutekeleza wajibu muhimu. Kwa mfano, kipindi cha ‘Kamusi ya Changamka’ katika redio ya Nation F.M kinafanya kazi nzuri sana ya kusambaza istilahi za Kiswahili. Je, matatizo haya yanaweza kutatuliwa vipi?

Zoezi la 6.2

* Mbali na istilahi zilizotajwa katika kitabu hiki, taja istilahi zingine kumi za Kiswahili ambazo hutumiwa kama visawe. Matatizo haya yanayokumba uundaji wa istilahi za Kiswahili yanaweza

kutatuliwa iwapo mambo yafuatayo yatazingatiwa: kwanza ni kutumia mbinu mwafaka za uundaji wa istilahi. Mbinu moja inaweza kufaa kuundia istilahi fulani lakini isifae kuundia istilahi nyingine. Pili, ni kufuata utaratibu mmoja unaofahamika katika kuunda istilahi. Tatu, waundaji wa istilahi lazima washirikiane katika shughuli hii; ikiwezekana Baraza la kimataifa liundwe ili kuwaleta pamoja waundaji wa istilahi za Kiswahili. Nne, waundaji wahakikishe kwamba istilahi wanazounda zinatimiza sifa zifuatazo: istilahi ziwe sahihi, ziwe fupi, ziweze kuandikwa na kutamkwa kwa urahisi, ziweze kunyambulika kwa urahisi ili kuzalisha istilahi nyingine za kikoa, zizingatie vilivyo sarufi ya lugha zinamoundwa, na kila istilahi iwakilishe dhana moja tu kila inapowezekana (yaani isiwe na vivuli vya maana). Tumbo- Masabo na Mwansoko (1992:17), Mwansoko (1998:32) na Kiingi (2001:206) wanakubaliana kwamba hizo ndizo sifa zinazotambulisha istilahi mwafaka.

6.4 Hitimisho

Katika somo hili, nimefafanua mbinu mbalimbali ambazo hutumiwa kuundia msamiati na istilahi za Kiswahili. Pia nimezungumzia matatizo yanayojitokeza katika istilahi zilizoundwa na jinsi yanavyoweza kutatuliwa. Katika somo lijalo la mwisho, nitazungumzia matumizi ya Kiswahili barani Afrika na kwingineko.

6.5 Maswali

? 1. Kwa kutoa mifano, fafanua mbinu mbalimbali zinazotumiwa kuundia

msamiati na istilahi za Kiswahili. 2. Huku ukitoa mifano, jadili matatizo yanayokumba uundaji wa istilahi za

Kiswahili na jinsi yanavyoweza kutatuliwa.

72

6.6 Marejeleo ya Lazima Chimera, R.M. (1998b). “Kiswahili Jana na Leo na Kesho: Swala la Msamiati.” Makala

yaliyowasilishwa katika Kongamano la Kiswahili la kimataifa, Septemba 23 – 25, Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi.

Kiango, J.G. (1995). “Uundaji wa Msamiati Mpya katika Kiswahili,” katika KIOO CHA LUGHA, Juzuu la 1, Nam. 1.

Kiingi, K.B. (2001). “The Kamusi Sanifu ya Biolojia, Fizikia na Kemia and the PEGITOSCA Criterion,” katika Kiswahili: A Tool for Development – The Multidisciplinary Approach. Eldoret: Moi University Press.

King’ei, K. (1998). “The Challenge of Expanding the Lexicon of an African Language: The Case of Kiswahili in East Africa.” A Paper presented at the Workshop on the Harmonisation and Standardization of African Languages at the Centre of Advanced Studies on Africa, Cape Town, South Africa, October 1-2, 1998.

Mbughuni, P. (1989). “Zoezi la Kuunda Istilahi za Fasihi: Matatizo na Mafanikio,” katika

Usanifishaji wa Istilahi za Kiswahili: Makala ya Semina ya Kimataifa. Dar es Salaam: TUKI.

Mwansoko, H.J.M. (1989). “Nidhamu katika Utumiaji wa Istilahi za Kiswahili: Mifano kutoka Fani ya Isimu,” katika MULIKA Nam. 24.

Onyango, J.O. (2000). “Tatizo la Istilahi katika Ufundishaji wa Kiswahili kama Lugha ya

Pili.” Makala yaliyowasilishwa katika Kongamano la kimataifa, Mei 10 – 12, Chuo Kikuu cha Maseno, Kisumu.

Onyango, J.O. na P.M. Musau (2000). “Uundaji wa Istilahi za Kiisimu: Mapendekezo katika kozi ya Lugha ya Pili.” Makala yaliyowasilishwa katika Kongamano la kimataifa, Oktoba 3 – 6, Fort Jesus, Mombasa.

(Yamechapishwa katika Kiswahili, Vol. 65, 2002:59-85). Tumbo-Masabo, Z.N.Z. na H.J.M. Mwansoko (1992). Kiongozi cha Uundaji wa Istilahi

za Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI. Were-Mwaro, B.G. (2001). “Utandawazi wa Kiswahili kwa Kufufua Msamiati wa

Zamani,” katika Kiswahili: A Tool for Development – The Multidisciplinary Approach. Eldoret: Moi University Press.

***Marejeleo ya ziada yanapatikana katika somo la mwisho.

73

SOMO LA 7

KISWAHILI BARANI AFRIKA NA KWINGINEKO 7.0 Utangulizi

Katika somo hili la mwisho, nitaeleza kwa ujumla jinsi lugha ya Kiswahili inavyotumiwa ndani na nje ya bara la Afrika, huku nikizingatia sifa zinazoitambulisha kama lugha ya kimataifa. Lugha ya kimataifa ni lugha inayotumiwa katika mataifa mbalimbali ili kutekeleza shughuli za mawasiliano, utangazaji, biashara, diplomasia, elimu, na kadhalika. Aidha, nitaeleza jinsi Kiswahili kinavyoweza kutumiwa ili kuimarisha umoja katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati. 7.1 Madhumuni

Baada ya kulipitia somo hili, ninatarajia kwamba utaweza: (i) Kueleza sifa zinazotambulisha Kiswahili kama lugha ya kimataifa. (ii) Kueleza jinsi Kiswahili kinavyoweza kuimarisha umoja katika Afrika

Mashariki na Kati.

7.2 Sifa za Kiswahili kama Lugha ya Kimataifa

Siku hizi lugha ya Kiswahili haizungumzwi tu pwani na visiwani kama ilivyokuwa zamani, bali imeenea zaidi na kuvuka mipaka ya Afrika Mashariki na Kati hadi Ulaya. Kiswahili sasa kinazo baadhi ya sifa zinazotambulisha lugha za kimataifa kama vile Kiingereza, Kijerumani, Kifaransa, na lugha nyinginezo. Hata hivyo, bado Kiswahili hakijakubalika kikamilifu kutumiwa katika vikao vya kimataifa na kuendesha shughuli rasmi za kimataifa. Zifuatazo ni sifa zinazoitambulisha Kiswahili kama lugha ya kimataifa:

Kwanza, lugha ya Kiswahili hufundishwa katika vyuo vikuu mbalimbali barani Afrika, huko Marekani na nchi za Ulaya kama vile Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Ubelgiji. Kijarida cha CHAKA, yaani Chama cha Kiswahili cha Afrika (1994:25-26), kimekusanya jumla ya asasi arubaini na sita zinazoshughulikia Kiswahili barani Afrika na kwingineko. Hivi sasa asasi hizo zimekuwa nyingi zaidi. Ifuatayo ni mifano ya vyuo vikuu vinavyofundisha Kiswahili:

• KENYA: -- Chuo Kikuu cha Nairobi

-- Chuo Kikuu cha Kenyatta -- Chuo Kikuu cha Moi -- Chuo Kikuu cha Egerton

-- Chuo Kikuu cha Maseno

74

-- Chuo Kikuu cha Baraton -- Vyuo vingine vya kibinafsi, kwa mfano, Catholic.

• TANZANIA: -- Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na vyuo vingine. • UGANDA: -- Chuo Kikuu cha Makerere, na Chuo Kikuu cha Kiislamu (Mbale). • RWANDA: -- Chuo Kikuu cha Rwanda, Idara ya Lugha na Fasihi za Kiafrika. • BURUNDI: -- Chuo Kikuu cha Burundi, Idara ya Lugha na Fasihi za Kiafrika. • ZIMBABWE: -- Chuo Kikuu cha Harare, Idara ya Lugha za Kiafrika. • NIGERIA: -- University of Port Harcourt, Department of African Languages and

Linguistics.

• SUDAN: -- University of Khartoum, Institute of African and Asian Studies, Department of Sudanese and African Languages.

• INDIA: -- University of Bombay, The Library of the Centre of East African

Studies.

• CHINA: -- Beijing Foreign Studies University, Swahili Section Library. • UNITED KINGDOM: -- University of London, School of Oriental and African

Studies. • RUSSIA: -- University of Moscow, Institute of Asian and African Countries.

• SOUTH KOREA: -- Hankuk University of Foreign Studies, The Library,

Department of Swahili.

• JAPAN: -- Tokyo University of Foreign Studies, Institute for the Study of Languages anad Cultures of Asia and Africa.

• GERMANY: -- Universitat zu Koln, Institut fur Afrikanistik.

• U.S.A: -- University of Florida, Department of African and Asian Languages and

Literature.

-- University of California - Los Angeles, African Studies Centre. -- Chuo Kikuu cha Howard, Idara ya Taaluma ya Kiafrika. -- University of Wisconsin – Madison, Department of African Languages

and Literature.

Vilevile nchini Marekani, kuna mpango wa kufundisha Kiswahili kwa wataalamu ambao wanatarajia kuja Afrika Mashariki kufanya kazi zao. Hawa ni pamoja na mabalozi, waandishi wa magazeti, wanajeshi, madaktari, wahandisi na wengineo. Mashirika yanayoendesha mpango huu wa mafunzo ni pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa (United Nations Agencies), Shirika la Upashaji Habari la Marekani (United States Information Service, USIS), na Mashirika ya Kutafsiri.

75

Pili, lugha ya Kiswahili hutangazwa katika Idhaa mbalimbali barani Afrika, Marekani na Ulaya. Katika somo la tano, tulitaja baadhi ya Idhaa zinazotangaza kwa Kiswahili katika Afrika Mashariki. Sasa ifuatayo ni mifano ya Idhaa zinazotangaza kwa Kiswahili kutoka nje ya Afrika Mashariki:

• RWANDA: -- Redio Rwanda, Kigali. • BURUNDI: -- Redio Burundi. • SOUTH AFRICA: -- Channel Africa, Johannesburg. • INDIA: -- All Radio India. • CHINA: -- Redio China Kimataifa, Beijing. • U.S.A: -- Idhaa ya Kiswahili, Voice of America (VoA), Washington D.C. • UNITED KINGDOM: -- Idhaa ya Kiswahili, British Broadcasting Corporation

(BBC), London. • GERMANY: -- Sauti ya Ujerumani, Radio Deutsche-Welle, Cologne.

Kwa ujumla, Idhaa hizi huchangia sana kukuza na kueneza Kiswahili kote

ulimwenguni. Idhaa ya Kiswahili ya BBC na Sauti ya Ujerumani, kwa mfano, hutangaza kwa Kiswahili cha kuvutia sana, hufanya utafiti mwingi wanapokusanya habari, na aghalabu hutangaza habari hizo bila mapendeleo yoyote. Kwa sababu hizo, watu wengi wa Afrika Mashariki na Kati hupenda kusikiliza habari, vipindi na matangazo ya Idhaa hizo masaa ya alfajiri na jioni. Katika BBC kuna kipindi cha “Makala ya Kiswahili,” na katika Sauti ya Ujerumani kuna kipindi cha “Baraza la Msamiati.” Kuna vipindi vingine ambavyo pia hutangazwa. Watangazaji wengi maarufu wa Idhaa hizo hunyakuliwa kutoka Tanzania na Kenya kwa sababu ya ujuzi wao katika Kiswahili, na pia kwa sababu ya mishahara mikubwa inayolipwa na Idhaa hizo. Hata hivyo, kwa ujumla, Idhaa hizo hutangaza habari na vipindi vya Kiswahili kwa muda mfupi sana, na pia hazina vipindi vingi vya Kiswahili.

Zoezi la 7.1

* Taja vipindi vya Kiswahili ambavyo hutangazwa katika vituo vya redio nilivyotaja hapo juu. Tatu, kuna majarida ya Kiswahili yanayochapishwa katika mataifa mbalimbali.

Tayari tunajua yale yanayochapishwa katika Afrika Mashariki (tazama somo la tano). Nchini Rwanda, kuna jarida la ‘Mwanga’ ambalo huchapishwa katika Chuo Kikuu cha Rwanda. Nchini Sweden, kuna jarida la ‘Lugha’ ambalo huchapishwa katika Chuo Kikuu cha Uppsala. Nchini Ujerumani, kuna jarida la ‘Swahili Forum’ ambalo huchapishwa katika Chuo Kikuu cha Cologne.

Mwisho, hivi sasa lugha ya Kiswahili inasemekana kuwa katika nafasi ya kumi

miongoni mwa lugha za kimataifa zilizo na idadi kubwa ya wazungumzaji kote

76

ulimwenguni. Wazungumzaji wa Kiswahili ulimwenguni wanakadiriwa kuwa takriban watu milioni mia moja.

Kwa hivyo ni wazi kwamba kimaenezi, Kiswahili ni lugha ya kimataifa. Maadui

wa Kiswahili wamedai kwamba lugha hii haiwezi ikatumika kikamilifu katika mawasiliano kama lugha zingine za kimataifa eti kwa sababu haijitoshelezi kimsamiati. Hiki ndicho kizingiti kikubwa kinachoizuia lugha hii kutumika katika mijadala ya kisayansi, kiteknolojia, kisiasa na kiuchumi, na pia katika vikao vya kimataifa kama vile COMESA.

Kuna wasomi mbalimbali ambao wamekanusha madai hayo kwa kusema kwamba, Kiswahili kinaweza kutumika kikamilifu kama lugha ya kimataifa iwapo shughuli za ukuzaji istilahi zitaimarishwa na istilahi hizo zisambazwe kwa kutumia teknolojia ya kisasa, yaani mtandao (internet). Wole Soyinka na Ali Mazrui ni wasomi maarufu wa Kiafrika ambao wamesema kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya pekee inayoweza kutumiwa kuunganisha mataifa ya bara la Afrika kwa sababu ina sifa zinazohitajika (tazama: Mazrui na Mazrui, 1995; na Chimera, 1998:146). Buliba (2001:57) anadondoa baadhi ya sifa hizo kama ifuatavyo:

Kwanza, Kiswahili tayari kimetumika kwa mafanikio makubwa kuwaunganisha

watu wa eneo la Afrika Mashariki. Pili, Kiswahili kinasemwa na idadi kubwa zaidi ya watu kuzidi lugha nyingine zote zilizowahi kupendekezwa kuwa lingua franca. Tatu, Kiswahili kinaweza kutumiwa na watu wengi wa bara hili bila tatizo kwani ni lugha ya Kibantu. Nne, Kiswahili kina historia ndefu ya maandishi na hifadhi kubwa ya fasihi. Mwisho, ili kwenda sambamba na mabadiliko ya kijamii, ya kisayansi na ya kiufundi, Kiswahili kimeonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kukopa na kuswahilisha maneno ya lugha nyingine.

Kihore (1983:37) anasema kwamba, kuhusishwa kwa Kiswahili na Mataifa ya Kiafrika – jambo ambalo halijafanyiwa lugha nyingine yoyote barani – kumesaidia sana kuimarisha ufungamano wa wenyeji wengi Waafrika kwa Kiswahili, kwani wameanza kukitumia kama kitambulisho chao. Lakini kulingana na Mateene (1989:111), wakati wa Kiswahili kutambuliwa kikamilifu bado haujawadia, kwani anasema:

“…Kiswahili kina bahati mbaya ya kujikuta kinatumiwa katika mazingara ambayo viongozi wengi bado wana mawazo ya kikoloni ya kufikiri kwamba lugha zao za taifa haziwezi kutumika katika shughuli rasmi au za kiserikali. Kiswahili kitatambuliwa kama lugha ya mawasiliano kati ya nchi za Afrika wakati viongozi wa Afrika watakuwa wamepitisha sera za lugha ambazo zinazipendelea lugha za taifa za Afrika. Ukweli ni kwamba kushindwa huku kwa ushirikiano kati ya nchi za Afrika kuhusu lugha, ni mfano tu wa kutokuwa na ushirikiano katika nyanja zingine kama vile utamaduni, habari, biashara, fedha na kadhalika. Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) bado uko mbali katika kufikia malengo yake mbalimbali.” Msanjila (1997:63-65) anasema kwamba Kiswahili hakitumiwi katika mikutano

ya OAU (Organisation of African Unity) [sasa shirika hili linaitwa African Union] kwa

77

sababu tatu: Kwanza ni ubeberu wa kiisimu; yaani, hii ni hali ambapo mataifa mengi ya Kiafrika aghalabu hutumia lugha za kigeni kuendeshea shughuli zao za kisiasa, kielimu, kitamaduni, kiutawala na kiuchumi. Pili, ni ukosefu wa sera za lugha zinazofaa, ambapo lugha za kigeni kama vile Kiingereza, Kifaransa na Kireno hutumiwa kutekeleza majukumu muhimu serikalini, katika elimu, mahakamani na katika sayansi na teknolojia. Lugha za Kiafrika, kwa upande mwingine, hupewa majukumu finyu sana. Tatu, ni kwamba serikali za Kiafrika zimekosa kutenga pesa za kugharamia shughuli za kuendeleza Kiswahili ili iweze kuwa lugha ya kutumiwa katika vikao vya OAU.

Ili Kiswahili na lugha zingine za Kiafrika ziweze kutumiwa kama lugha za

mawasiliano ya kimataifa barani Afrika, Msanjila anapendekeza kwamba, viongozi wa Kiafrika wanapaswa kubuni upya na kukubali sera itakayoruhusu matumizi ya Kiswahili na lugha zingine za Kiafrika katika mikutano ya OAU. Anapendekeza kwamba lugha hizo zaweza kusomeshwa shuleni na vyuoni na pia kutumiwa kufundishia pale inapowezekana. Anasema kwamba sera hii itawamotisha watu wa Afrika kujifunza lugha zingine za Kiafrika na hali hii itaimarisha utambulisho wa Kiafrika na umoja wa Kiafrika. Mbaabu (1995:83) pia anasisitiza kwamba, ustawishaji wa lugha hizo za Kiafrika utasaidia sana kuhifadhi utambulisho wa kiutamaduni na hivyo basi kupunguza utegemeaji wa utamaduni wa kigeni.

Kwa ujumla, maoni ya wasomi hao yanaonyesha kwamba lugha ya Kiswahili

inaweza kutumiwa kuimarisha umoja kati ya nchi za Kiafrika. Je, jambo hili linawezekana kwa njia gani?

7.3 Kiswahili kama Chombo cha Kuimarisha Umoja.

Sisi wasomi na wapenzi wa Kiswahili tunaamini kwamba, Kiswahili kikipewa nafasi ya kutumika kikamilifu, kinaweza kusaidia kuimarisha umoja katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati kupitia kwa njia zifuatazo:

Kwanza, ni kufundisha Kiswahili katika vyuo vikuu na pia shule zote za Afrika

Mashariki na Kati. Kwa njia hii, wahadhiri na waalimu wa Kiswahili wanaweza kuajiriwa katika nchi yoyote. Kwa mfano, hivi karibuni waalimu walitoka nchini Kenya kwenda kufundisha katika visiwa vya Ushelisheli.

Pili, ni kutangaza Kiswahili katika vituo vingi vya redio na runinga za nchi za

Afrika Mashariki na Kati ambapo vituo hivyo vinaweza pia kuwa na mpango wa kubadilishana vipindi kwa Kiswahili. Kwa mfano, shirika la URTNA huwezesha ubadilishanaji wa vipindi vya runinga barani Afrika.

Tatu, ni kuwa na soko la pamoja la uuzaji wa vitabu vya Kiswahili. Kwa njia hii,

vitabu vinavyochapishwa nchini Kenya vinaweza pia kuuzwa katika nchi zingine na vikatumika katika shule na vyuo vya huko. Ushirikiano huu ni kama ule wa soko la pamoja la mazao.

Nne, ni kuwa na Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki na Kati linalojumuisha

wasomi na wapenzi wa Kiswahili kutoka nchi zote za Afrika Mashariki na Kati. Kwa njia

78

hii, wataweza kushirikiana katika usanifishaji na ukuzaji wa Kiswahili na pia kuepuka tatizo la kuwa na ‘viswahili’ vya kimaeneo.

Tano, ni kutumia Kiswahili kama lugha rasmi ya mawasiliano katika vikao vya

Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo tayari imefufuliwa, na pia katika vikao vingine vya kibiashara kama vile COMESA, PTA na vikao vinginevyo. Kwa mfano, litakuwa jambo la busara iwapo Bunge la Afrika Mashariki litaendesha shughuli zake kwa Kiswahili.

Sita, ni kuyachapisha na kuyasambaza magazeti na majarida ya Kiswahili katika

nchi zote za Afrika Mashariki na Kati. Majarida na magazeti hayo ni pamoja na Mulika, Kiswahili, Majira, Kasheshe, Taifa Leo, Jamhuri, na mengine mengi.

Saba, ni kuhimiza bendi za wanamuziki wa Afrika Mashariki na Kati kutunga

nyimbo nyingi kwa Kiswahili, na bendi hizo ziweze kuzuru nchi jirani ili kuwatumbuiza wananchi wa huko. Hata vikundi vya wanasarakasi, kwa mfano ‘Vitimbi’ nchini Kenya, vinaweza kufanya ziara kama hizo katika nchi jirani ili kuonyesha sanaa zao. Ushirikiano huu wa kimuziki na kisanaa unaweza kuchangia sana kuimarisha umoja wa kiutamaduni.

Mwisho, ni kutumia Kiswahili kama lugha ya taifa na pia lugha rasmi ya

kuendeshea shughuli za serikali katika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati. Shughuli hizo ni pamoja na za bunge, za mahakama, za marekebisho ya katiba, na za diplomasia.

7.4 Hitimisho

Kwa muhtasari, katika somo hili nimeonyesha sifa zinazotambulisha Kiswahili kama lugha ya kimataifa. Pia nimeeleza jinsi lugha hii inavyoweza kutumiwa ili kuimarisha umoja katika nchi za Afrika Mashariki na Kati. Imeonekana waziwazi kwamba Kiswahili kinaweza kutumiwa kuimarisha umoja wa kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni, na hivyo kuchangia katika maendeleo ya nchi za kanda hii ya Afrika Mashariki na Kati. Jambo hili litawezekana iwapo mataifa ya kanda hii yatazichunguza kwa makini na kuzirekebisha sera zao za lugha, ili kuipa lugha ya Kiswahili kipaumbele katika maswala ya kitaifa na kimataifa.

7.5 Maswali

? 1. “Kiswahili sio lugha ya Afrika Mashariki tu, bali ni lugha ya kimataifa.” Jadili kauli hii. 2. Ni vipi Kiswahili kinavyoweza kusaidia kuimarisha umoja katika Afrika

Mashariki na Kati?

79

7.6 Marejeleo ya Lazima Buliba, A.F. (2001). “Lugha, Utamaduni na Jamii katika Maendeleo ya Kitaifa na

Kimataifa,” katika Kiswahili: A Tool for Development – The Multidisciplinary Approach. Eldoret: Moi University Press.

Bwenge, C. (mh.) (1994). “Asasi zinazoshughulikia Kiswahili Barani Afrika na Kwingineko,” katika Kijarida cha CHAKA (Chama cha Kiswahili cha Afrika). Toleo Nambari 1, uk. 25-26. Dar es Salaam: TUKI.

Kihore, Y.M. (1983). “Nafasi ya Kiswahili Barani Afrika,” katika MULIKA Nambari 15, uk. 32-39.

Mateene, K. (1989). “Nafasi ya Kiswahili katika Kuleta Umoja wa Afrika,” katika Usanifishaji wa Istilahi za Kiswahili: Makala za Semina ya Kimataifa. Dar es Salaam: TUKI.

Mazrui, A.A. na A.M. Mazrui (1995). Swahili State and Society: The Political Economy of an African Language. Nairobi: E.A.E.P.

Mbaabu, I. (1995). “Linguistic and Cultural Dependency in Africa,” katika BARAGUMU, Juzuu la 2 Nam. 1-2 uk. 72-86.

Msanjila, Y.P. (1997). “Towards A Policy on the Use of Kiswahili in Africa,” katika KISWAHILI, Juzuu la 60, uk. 61-67.

80

***MAREJELEO YA ZIADA Bakari, M. (1982). “The Morphophonology of Kenyan Swahili Dialects.” Unpublished

Ph.D. Thesis, University of Nairobi. Chacha, Nyaigotti-Chacha (2001). “Marafiki na Maadui wa Kiswahili.” Hotuba

iliyotolewa katika Kongamano la Kiswahili la Kimataifa, Oktoba 3-6, Thompson Falls Lodge, Nyahururu.

Chambers, J.K. & P. Trudgill (1980). Dialectology. Cambridge: C.U.P. Chimera, R. (1998). Kiswahili: Past, Present and Future Horizons. Nairobi: N.U.P. Chiraghdin, S. na M. Mnyampala (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: O.U.P. Gibbe, A.G. (1983). “Maendeleo ya Istilahi za Kiswahili,” katika Lugha ya Kiswahili:

Makala ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili (1). Dar es Salaam: TUKI.

Gorman, T.P. (1974). “The Development of Language Policy in Kenya with Particular Reference to the Educational System,” in Whiteley, W.H. (ed.) Language in Kenya. Nairobi: O.U.P.

Greenberg, J. (1966). The Languages of Africa. U.S.A: I.U.F. Grenville, Freeman G.S.O. (1962). The East African Coast. Clarendon. Guthrie, M. (1967). The Classification of the Bantu Languages. London: Dawsons of Pall Hinnebusch, T.J. (1973). “Prefixes, Sound Change, and Sub-grouping in the Coastal

Kenyan Bantu Languges.” Ph.D. Thesis, U.C.L.A., Michigan. Jamhuri Ripota (2000). “Matatizo ya vyombo vya habari yafichuliwa: Wasomi wa vyuo

vikuu watoa suluhisho,” katika Gazeti la Jamhuri, Desemba 17-30, 2000. Kapinga, M.C. (1983). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: TUKI. Kawoya, Vin. F.K. (1985). “Kiswahili in Uganda,” in J. Maw & D. Parkin (eds.) Swahili

Language Society. Khalid, A. (1977). The Liberation of Swahili from European Appropriation. Nairobi:

E.A.L.B. Ladefoged, P. et. al (eds.) (1971). Language in Uganda. Nairobi: O.U.P. Marshad, H.A. (1993). Kiswahili au Kiingereza? (Nchini Kenya). Nairobi: Jomo

Kenyatta Foundation. Mbaabu, I. (1978). Kiswahili Lugha ya Taifa. Nairobi: Kenya Literature Bureau. Mbaabu, I. (1978b). “Language Planning in Kenya: Some Practical Considerations,” in

LUGHA, Vol. 5 No. 3. Mbaabu, I. (1985). New Horizons in Kiswahili. Nairobi: K.L.B. Mbaabu, I. (1985b). Utamaduni wa Waswahili. Nairobi: Kenya Publishing and Book

Marketing Co. Mbaabu, I. (1991a). Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili. Nairobi: Longman. Mbotela, W. (1999). “Kiswahili: Si lugha geni ilivyoaminika,” katika Gazeti la TAIFA LEO, Juni 19, 1999 uk. 12. Ndungo, C. na W. Mwai (1991). Kiswahili Part Two: Historical Modern Development in

Kiswahili. Nairobi: Nairobi University Press. Ogot, B.A. et. al (eds.) (1968). ZAMANI: A Survey of East African History. Nairobi:

E.A.P.H.

81

82

Ohly, R. (1973). “Historical Approach to Swahili Literature: As Heretofore An Open Question,” in KISWAHILI, Vol. 43 / 2.

Polome, E.C. (1967). Swahili Language Handbook. Washington D.C., Centre for Applied Linguistics.

Prins, A.H.J. (1961). The Swahili Speaking People of Zanzibar and the East African Coast. London: International African Institute.

Salim, A.L. (1973). Swahili Speaking Peoples of Kenya’s Coast, 1895 – 1965. Nairobi: E.A.P.H.

Stigand, C.H. (1951). The Land of Zinj. London: Frank Cass. Wardhaugh, R. (1977). Introduction to Linguistics. Toronto: McGraw–Hill Book Co. Wardhaugh, R. (1987). Languages in Competition. Oxford: Basil Blackwell Co. Whiteley, W.H. (1969). Swahili: The Rise of a National Language. London: Methuen. Whiteley, W.H. (ed.) (1974). Language in Kenya. Nairobi: O.U.P. MAJARIDA NA MAGAZETI 1. MULIKA 2. KISWAHILI 3. KIOO CHA LUGHA 4. LUGHA 5. MWAMKO 6. BARAGUMU 7. MAGAZETI YA TAIFA LEO NA JAMHURI. ***Vilevile kuna marejeleo ya lazima baada ya kila somo.