tafakuri kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa na … · kitaifa zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa...
TRANSCRIPT
TAFAKURI KUHUSU SERIKALI YA
UMOJA WA KITAIFA NA
UHUSIANO WAKE NA KATIBA
MPYA YA TANZANIA.
Waraka uliowasilishwa na Nd. Ibrahim Mzee
Ibrahim, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar,
na Katibu wa Zamani wa Baraza la
Wawakilishi, katika semina ya kuwajengea
uwezo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
juu ya Wajibu wa Wajumbe katika Bunge la
Katiba, iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli
ya Coconut Beach Resorts, Marumbi
Zanzibar, tarehe 2-3 Disemba 2013.
Waraka huu umechapishwa kwa ufadhili wa
Mradi wa Kuimarisha Vyombo vya
Kutunga Sheria – Legislature Support
Project (LSP) unaoratibiwa na UNDP.
1
Utangulizi
Katika mada hii tutajaribu kueleza kuhusu
mambo matatu makubwa. Tutaanza na
historia ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja
wa Kitaifa hapa Zanzibar. Tutafafanua
masharti yaliyomo kwenye Katiba ya
Zanzibar ya 1984 kama ilivyorekebishwa
mnamo mwaka 2010 kuhusu Serikali ya
Umoja wa Kitaifa. Tutamalizia kwa kugusia
mambo ya kuyatafakari katika muktadha wa
katiba mpya ya Tanzania.
2
Azimio la Baraza la Wawakilishi
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar mnamo
tarehe 28 na 29 Januari 2010 lilijadili hoja ya
mapendekezo ya kuundwa kwa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Hoja hiyo
iliwasilishwa kwenye Baraza la Wawakilishi
na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa
Jimbo la Mgogoni Pemba Mheshimiwa
Abubakar Khamis Bakary.
Katika hoja hiyo, Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi waliombwa kupongeza na
kuridhia mazungumzo ya maridhiano
yaliyofanyika tarehe 5 Novemba 2009 baina
ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mheshimiwa Dr. Amani Abeid Karume
ambaye alikuwa pia ni Makamo Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar,
na Mhe. Seif Shariff Hamad – Katibu Mkuu
wa chama cha Civic United Front (CUF).
Aidha, wajumbe waliombwa wakubali
3
kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba 2010.
Baraza la Wawakilishi liliikubali hoja hiyo
kwa masharti kwamba kufanyike kura ya
maoni kwa ajili ya kutafuta ridhaa ya
wananchi kuhusu jambo hilo na Serikali ilete
mswada wa sheria kwenye Baraza ili
utengenezwe utaratibu wa kisheria wa
kuendesha kura ya maoni. Maamuzi hayo ya
Baraza yalipitishwa kwa azimio lilokuwa na
vifungu 12.
Kwenye majadiliano ya Baraza la
Wawakilishi kuhusu azimio hilo, ilielezwa na
wajumbe mbali mbali kuwa maridhiano ya
kisiasa baina ya CCM na CUF yamefikiwa ili
kuondoa migogoro na mivutano ya kisiasa
Zanzibar iliyodumu kwa muda mrefu tangu
kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za vyama
4
vingi Tanzania na hususan Zanzibar kuanzia
mwaka 1992.
ya kisiasa
Uchaguzi wa kwanza katika mfumo wa
vyama vingi tangu baada ya Mapinduzi ya
1964 ulifanyika mwaka 1995 ambapo
mivutano ya kisiasa ilijitokeza wazi wazi
baina ya vyama viwili vikuu vya siasa hapa
Zanzibar yaani CCM na CUF. Uhasama na
chuki za kisiasa zilishika kasi. Chama cha
upinzani CUF kilikataa kuyatambua matokeo
ya uchaguzi wa Rais na pia kilikataa
kumtambua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi ambaye wakati huo
alikuwa Mheshimiwa Dr. Salmin Amour
Juma.
Aidha, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
wa Upande wa Upinzani (CUF) walisusia
vikao vya Baraza kwani walihudhuria vikao
hivyo kwa kupangilia ili wasipoteze sifa tu za
5
kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
kwa mujibu wa Katiba. Vile vile, Wajumbe
wa Baraza la Wawawkilishi wa Upande wa
Upinzani walikuwa hawazungumzi wala
kuchangia chochote kwenye mijadala
iliyoendeshwa kwenye vikao vya Baraza.
Katika mwendelezo wa matukio hayo, wakati
Rais alipokuwa akienda kulihutubia Baraza,
wajumbe wa CUF walikuwa wakitoka nje ya
ukumbi wa mkutano wa Baraza.
Matokeo ya chaguzi zilizofanyika 1995, 2000
na 2005 yalionyesha waziwazi kwamba jamii
ya Zanzibar imegawika pande mbili kisiasa
zenye wafuasi wengi kila upande kiasi
ambacho kukaribiana sana kwa matokeo ya
chaguzi hizo kunaufanya upande ulioshindwa
kuyatilia mashaka na kutoyakubali matokeo
hayo. Mwaka 1995 mgombea urais kutoka
CCM alipata kura 50.2% wakati mgombea
urais kutoka CUF alipata kura 49.8%.
Mwaka 2000 mgombea urais kutoka CCM
6
alipata kura 56% na mgombea urais kutoka
CUF alipata 44%. Mwaka 2005 mgombea
urais kutoka CCM alipata kura 53% wakati
mgombea urais kutoka CUF alipata kura
47%. Hata mwaka 2010 mgombea urais wa
CCM alipata kura 50.1% na mgombea urais
wa CUF alipata kura 49.1%.
Hali ya matokeo kukaribiana ilijitokeza pia
kwenye chaguzi za wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kwani mwaka 1995 CCM
ilipata majimbo 26 na CUF ilipata majimbo
24. Baadae, baada ya idadi ya majimbo ya
Pemba kupungua na idadi ya majimbo ya
Unguja kuongezeka, mwaka 2000 CCM
ilipata majimbo 35 na CUF ilipata majimbo
15. Mwaka 2005 CCM ilipata majimbo 31
wakati ambapo CUF ilipata majimbo 19.
Mwaka 2010 CCM imepata majimbo 28
wakati CUF imepata majimbo 22.
7
Mgogoro wa kukataa kutambua na
kuyakubali matokeo katika chaguzi hizo
uliathiri uchumi wa nchi, Washirika wa
Maendeleo waliisusia na kuiwekea vikwazo
Zanzibar na uliwagawa wananchi wa Unguja
na Pemba kisiasa na hata kwenye mambo yao
ya kawaida ya kijamii kama vile harusi na
maziko.
Uchaguzi wa mwaka 2000 na wa mwaka
2005
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 ulifanyika
katika mazingira yale yale ya chuki na
uhasama wa kisiasa. Kwa mara nyengine tena
chama cha CUF kilikataa kuyatambua
matokeo ya uchaguzi na pia kilikataa
kumtambua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dr. Amani Abeid
Karume. Baada ya uchaguzi, Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi wa upande wa
upinzani (CUF) hawakuhudhuria kabisa
vikao vya Baraza la Wawakilishi na
8
hawakwenda Barazani hata kuapa kiapo cha
uaminifu.
Kutokana na hali hiyo, baada ya mikutano
mitatu ya Baraza kupita bila ya wajumbe hao
kuhudhuria kwenye vikao vya Baraza,
walipoteza sifa za kuwa wawakilishi na
hivyo kupoteza viti vyao kwenye Baraza la
wawakilishi. Matukio ya kuhuzunisha pia
yalitokea tarehe 26 na 27 Januari 2001 kwa
baadhi ya wananchi kupoteza maisha yao na
wengine kwenda ukimbizi kwenye nchi jirani
ya Kenya.
Uchaguzi Mkuu mwengine ulifanyika mwaka
2005 na kwa mara nyengine tena Chama cha
Wananchi CUF kilikataa kuyatambua
matokeo ya uchaguzi wa Rais na pia kilikataa
kumtambua Rais Amani Abeid Karume.
9
Jitihada za Usuluhishi
Jitihada za usuluhishi zilianza kwa
Muwafaka wa Mwanzo kusainiwa tarehe 9
Juni 1999 baina ya CCM na CUF ili kufanya
mazungumzo ya kutatua hali iliyojitokeza
baada ya uchaguzi mkuu wa 1995
(Muwafaka wa Kwanza: Mhe. Mkema na
Mhe. Mloo). Kamati ya Pamoja ya CCM na
CUF yenye Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kumi na nne, yaani saba kutoka
kila upande, iliundwa ili kufanya
mazungumzo chini ya usuluhishi wa Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Madola wa wakati huo
Chief Emeka Anyaokou. Kamati hiyo ilianza
kazi mwezi wa Septemba 1999 na kumaliza
mchakato wa mazungumzo mnamo mwezi
wa Julai 2000 na kuwasilisha ripoti Serikalini
yenye mapendekezo ya mambo
yanayohitajika kufanywa ili kutekeleza
muwafaka huo wa kisiasa.
10
Serikali iliandaa Mswada wa Marekebisho ya
Katiba na kupelekwa kwenye Baraza la
Wawakilishi, lakini mswada huo haukupita
kwani ulikataliwa na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kutoka Chama cha Upinzani
CUF ambao walikuwa hawakuridhika na
marekebisho yaliyokuwemo kwenye mswada
huo. Kwa wakati huo Wajumbe wa upande
wa Chama Tawala CCM idadi yao ilikuwa
haitimii theluthi mbili ya Wajumbe wote wa
Baraza iliyohitajika kwa ajili ya kupitisha
marekebisho hayo ya Katiba yaliyotokana na
muwafaka wa kwanza.
Muwafaka wa pili kati ya CCM na CUF
ulisainiwa tarehe 10 Oktoba 2001
(Muwafaka wa Pili: Mhe Mangula na Mhe
Seif Shariff) na baadae mnamo tarehe 30
Novemba 2001 Sheria Nambari 10 ya 2001
ilipitishwa na Baraza la Wawakilishi kwa
madhumuni ya kuunda Tume ya Pamoja ya
Rais ya Kusimamia Utekelezaji wa
11
Muwafaka wa Kisiasa baina ya CCM na
CUF. Tume hiyo ilikuwa na Wajumbe kumi
ambapo watano ni kutoka CCM na watano
kutoka CUF.
Kifungu cha 5 (2) (b) cha Sheria hiyo
Nambari 10 ya 2001 kilitamka wazi wazi
kwamba miongoni mwa majukumu na kazi
za Tume hiyo ni kuanzisha na kufanya
mazungumzo yatayoshirikisha CCM na CUF
kwa madhumuni ya kufungua maeneo
mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo
uwezekano wa kuunda serikali ya umoja wa
kitaifa kwa ridhaa ya wananchi na kwa haja
ya kuamua mustakbala wa Zanzibar katika
nyanja za uchumi, demokrasia na mambo
mengineyo1.
1 Section 5(2)(b) of an Act No. 10 of 2001,
among the functions of the Joint Presidential
Supervisory Commission is to “initiate and
engage in dialogue involving CCM and CUF with
the aim of opening different areas of co-operation
which includes the possibility of forming a
12
Matokeo ya mazungumzo ya Tume hiyo
ndiyo yaliyopelekea kufanyika kwa
Marekebisho ya Nane na Marekebisho ya
Tisa ya Katiba ya Zanzibar mnamo mwaka
2002 na 2003, ili kuingiza kwenye Katiba
yale mambo yaliyokubalika kwenye
muwafaka huo. Hata hivyo, suala la serikali
ya umoja wa kitaifa halikuingizwa kwenye
marekebisho ya Katiba wala halikutekelezwa.
Mabadiliko makubwa yaliyofanyika kwenye
Katiba kupitia Marekebisho ya Nane na ya
Tisa yalikuwa ni kuweka Muundo wa Tume
ya Uchaguzi inayojumuisha Makamishna
kutoka kwenye vyama vya siasa na pia
kuweka utaratibu wa Mheshimiwa Rais
kuteua angalau watu wawili kuwa Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi kutoka upande wa
government of national unity by consent of the
people, and the need to determine the future of
Zanzibar in the spheres of politics, democracy and
other matters”
13
upinzani, miongoni mwa nafasi kumi za
uteuzi wa Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi ambazo zipo kwa mujibu wa
Katiba. Halikadhalika, Uchaguzi Mdogo
ulifanyika ili kujaza nafasi za Uwakilishi za
Majimbo ya Pemba yaliyokuwa wazi tangu
2001 kutokana na Wawakilishi wa Upinzani
kupoteza sifa kwa kutohudhuria vikao. Hatua
hizo zilileta utulivu kidogo hadi kufikia
uchaguzi wa mwaka 2005.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
kwenye hotuba yake ya tarehe 30 Disemba
2005 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, alionyesha nia ya dhati ya
kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar
unaojitokeza kila mara baada ya uchaguzi
Mkuu. Katika kutekeleza azma hiyo, Kamati
ya pamoja ya CCM na CUF iliundwa.
14
Kamati hiyo iliongozwa na Makatibu Wakuu
wa vyama hivyo, na ikafanya mazungumzo
ya kina kule Bagamoyo na kutoa
mapendekezo yake kwa vyama husika
likiwemo suala la uanzishwaji wa serikali ya
umoja wa kitaifa Zanzibar.
Kwa upande wa CCM, mapendekezo hayo
yalipowasilishwa kwenye Halmashauri Kuu
ya Taifa (NEC) katika kikao cha tarehe 29
hadi 30 Machi 2008 kilichofanyika Butiama
yalikubaliwa lakini NEC ya CCM iliona
kuwa suala la uanzishwaji wa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa ni vyema, kwa uzito na
umuhimu wake, lipelekwe kwa wananchi
moja kwa moja ili kupata ridhaa yao kwa njia
ya kura ya maoni. Chama cha CUF kwa
wakati ule hakikuridhishwa na uamuzi huo
wa NEC ya CCM na kikatangaza rasmi
kujiondoa kwenye mazungumzo.
15
Hatua hiyo ilipelekea kukwama tena kwa
mazungumzo ya muwafaka ambao
ungelikuwa ni muwafaka wa tatu tangu
kuanza tena kwa siasa za vyama vingi hapa
Zanzibar. Muwafaka huo ulififia baada ya
CUF kujitoa kwenye mazungumzo kufuatia
maamuzi ya NEC ya CCM Butiama.
Historia hii fupi ya miafaka hapa Zanzibar
baada ya kuanza tena kwa siasa za vyama
vingi, inaonyesha kwamba Muwafaka wa
kwanza wa 1999 chini ya Uongozi wa Dr.
Salmin Amour Juma haukutekelezwa hata
kidogo. Muwafaka wa pili wa 2001 chini ya
Uongozi wa Dr. Aman Abeid Karume
ulitekelezwa kwa kiasi fulani kwa kufanywa
marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya 1984
(Marekebisho ya Nane 2002 na Marekebisho
ya Tisa 2003). Hata hivyo, siasa za chuki
zilirejea na kujitokeza tena kwenye Uchaguzi
Mkuu wa 2005.
16
Kwa bahati nzuri muwafaka huu wa tatu
ulifufuka Novemba 2009 baada ya
mazungumzo ya tarehe 5 Novemba 2009
baina ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr.
Amani Abeid Karume na Mheshimiwa
Katibu Mkuu wa Chama wa Wananchi CUF
Maalim Seif Sharif Hamad.
Muwafaka huu wa Tatu ulianza kuonyesha
dalili za matumaini ya mafanikio kwa sababu
suala la ushirikiano katika madaraka (power
sharing) kwa njia ya uundwaji wa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa lilipewa kipaumbele.
Mwafaka huu sasa unajulikana kwa umaarufu
kama “Maridhiano”.
Kamati ya Watu Sita
Kifungu cha Kumi na moja 11 cha Azimio la
Baraza kilielekeza kuundwa kwa Kamati ya
Watu Sita ya Kusimamia Utekelezaji wa
Maamuzi ya Baraza kuhusu hoja ya
17
uanzishwaji wa Serikali ya umoja wa kitaifa
hadi kukamilika kwake. Kwa mujibu wa
Kifungu hicho, Kamati hiyo ilitakiwa iwe na
Wajumbe watatu kutoka upande wa chama
kinachounda Serikali (CCM) na watatu
kutoka upande wa Upinzani.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimwa
Pandu Ameir Kificho aliunda Kamati hiyo
kwa kuteua Wajumbe Sita, kama
ilivyoelekezwa kwenye kifungu tulichokitaja
hapo juu. Wajumbe watatu miongoni mwao
walichaguliwa kutoka CCM – Chama
kinachounda Serikali; na Wajumbe wengine
watatu walichaguliwa kutoka CUF ambacho
kilikuwa Chama cha Upinzani ndani ya
Baraza la Wawakilishi kwa wakati huo.
Wajumbe wa kamati hiyo walipokutana
walichagua Mwenyekiti wa Kamati na
Makamo Mwenyekiti wa kamati kutoka
miongoni mwao.Wajumbe hao sita
walioteuliwa na Mheshimiwa Spika kuunda
18
kamati ya watu sita kwa mujibu wa
maelekezo ya Azimio la Baraza ni:-
1 Mhe. Ali Mzee Ali CCM Mwenyekiti
2
Mhe. Abubakar Khamis
Bakary CUF
Makamo
Mwenyekiti
3 Mhe. Ali Abdalla Ali CCM Mjumbe
4 Mhe. Haji Omar Kheri CCM Mjumbe
5
Mhe. Nassor Ahmed
Mazrui CUF Mjumbe
6 Mhe. Zakiya Omar Juma CUF Mjumbe
Sekretarieti ya Kamati ilikuwa ni Ndugu
Ibrahim Mzee Ibrahim, aliyekuwa Katibu wa
Baraza la Wawakilishi na Ndugu Mdungi
Makame Mdungi (aliyekuwa Mkuu wa Idara
19
ya Utawala) Afisi ya Baraza la Wawakilishi.
Kamati ya Watu Sita ilijifunza ndani ya nchi
na nje ya nchi na ilitoa elimu kwa jamii
Unguja na Pemba.
Kura ya Maoni
Sheria Nambari 6 ya 2010 kuhusu uendeshaji
wa kura ya maoni ilipitishwa na Baraza la
Wawakilishi mnamo mwezi wa Machi 2010
na kutiwa saini na Mheshimiwa Rais mnamo
mwezi wa Aprili 2010. Wananchi wa
Zanzibar walipiga kura ya maoni siku ya
Jumamosi tarehe 31 Julai 2010. Kura hiyo
ilikuwa na lengo la kutafuta ridhaa ya
wananchi katika kuamua iwapo wanalikubali
wazo la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba 2010.
Kupigwa kwa kura hiyo ya maoni ilikuwa ni
utekelezaji wa kifungu nambari mbili cha
Azimio la Baraza ambacho kilieleza kwamba
Kimsingi, Baraza limekubali kwamba ipo
20
haja ya kufanywa kura ya maoni
(referendum) itayowashirikisha wananchi
moja kwa moja katika kupata ridhaa ya
wananchi kuhusu uanzishwaji wa mfumo na
muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Zanzibar.
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilitangaza
matokeo ya kura ya maoni siku ya Jumapili
ya tarehe 01/08/2010. Matokeo hayo yalitoa
ushindi wa kura za NDIO kwa aslimia
66.40% dhidi ya kura za HAPANA asilimia
33.90%.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 11(1) cha
Sheria ya Kura ya Maoni Nambari 6 ya 2010,
ushindi wa Kura ya Maoni utaamuliwa kwa
wingi wa kura. Hivyo, kwa mujibu wa
matokeo hayo, Wazanzibari waliopiga kura
ya NDIO kuunga mkono kuundwa kwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar baada
21
ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010
walishinda.
Kwa mujibu wa kifungu cha sheria
kilichotajwa hapo juu, Serikali ililazimika
kuyakubali matokeo yoyote ya Kura ya
Maoni. Hivyo, Serikali mpya ikaundwa
baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa
Oktoba 2010 ambayo ikatambulika kuwa ni
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye
Muundo wa Umoja wa Kitaifa kama
inavyoelekeza Katiba ya Zanzibar kwenye
kifungu cha 9(3), baada ya kufanyiwa
marekebisho. Marekebisho hayo yalifanywa
kwenye Mkutano wa Ishirini na Moja wa
Baraza la Saba la Wawakilishi mnamo
mwezi wa Ogasti 2010.
Madhumuni ya Serikali ya Umoja wa
Kitaifa
Kifungu cha tano cha Azimio la Baraza la
Wawakilishi lililotajwa hapo juu kilisisitiza
22
kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa
itakayoundwa Zanzibar itaendelea kuheshimu
na kuthamini misingi mikuu ya Mapinduzi ya
tarehe 12 Januari 1964. Katika mjadala
uliofanyika kwenye Baraza la Wawakilishi
ilibainishwa kuwa misingi hiyo ni ile
iliyotajwa na kuwekwa kisheria kwenye
Dikrii Nambari 6 ya 1964. Misingi hiyo ni
Usawa, Maridhiano, na Umoja.
Baada ya kufanyika kwa Kura ya Maoni
tarehe 31 Julai 2010 na baada ya kufanywa
kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya
Zanzibar ya 1984, Katiba imeanisha kuwepo
kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye
muundo wa Umoja wa Kitaifa ambayo
itajumuisha mawaziri kutoka vyama tofauti
vya siasa kulingana na uwiano wa viti
ambavyo vyama vya siasa vimepata kwenye
Baraza la Wawakilishi.
Uzoefu wa chaguzi zilizopita unaonyesha
kwamba kwa hapa Zanzibar ni vyama vya
23
CCM na CUF tu ndivyo vimekuwa vikipata
viti kwenye Baraza la Wawakilishi. Kifungu
cha 9 (3) cha Katiba kinaeleza kwamba
“Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar utakuwa ni wa Umoja wa Kitaifa na
utendaji wa kazi zake utafanywa katika
utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa
umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia”
Serikali ya Umoja wa kitaifa inafanana na
serikali ya mseto kwa kuwa aina zote hizo
mbili za serikali zinashirikisha mawaziri
kutoka vyama tofauti vya siasa lakini
zinatofautiana katika sababu za kuwepo kwa
serikali hizo. Serikali ya mseto inatokana na
kutokuwepo kwa mshindi mwenye wingi wa
viti vya kutosha kwenye Bunge/ Baraza kwa
ajili ya kuunda serikali wakati ambapo
serikali ya umoja wa kitaifa haitokani na
kutokuwepo kwa mshindi mwenye viti vya
kutosha kwenye Bunge bali inatokana na
matatizo mahsusi katika nchi husika,
matatizo ambayo utatuzi wake umewekwa
24
kwenye Katiba kwamba ni kuwa na serikali
inayoshirikisha vyama mbali mbali vya siasa.
Kwa kawaida katika nchi nyingi kunapokuwa
na serikali ya mseto ambayo ina mawaziri
kutoka kwenye vyama viwili au zaidi vya
siasa, bado kunakuwepo vyama vyengine
ndani ya Bunge ambavyo hufanyakazi ya
upinzani. Lakini Serikali ya Umoja wa
Kitaifa huwa na hali tofauti, na hiyo ni kwa
sababu hujumuisha mawaziri kutoka vyama
vyote vya siasa vyenye uwakilishi kwenye
Bunge/ Baraza; kwa maneno mengine ni
kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni
serikali ya vyama vyote vya siasa vilivyomo
Bungeni na kunakuwa hakuna Upande wa
Upinzani kwani vyama vyote vilivyomo
Bungeni/Barazani huwa vimo pia serikalini
kwa maana kwamba vimetoa mawaziri.
25
Mabadiliko ya Kanuni na Taratibu za
Baraza kutokana na kuanzishwa kwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Katika mazingira ya sasa ya kikatiba kwa
Zanzibar ambapo mawaziri wanapatikana
kutoka kwenye vyama vyote vya siasa
vilivyomo kwenye Baraza la Wawakilishi,
ina maana kuwa hakuna chama cha siasa
ndani ya Baraza la Wawakilishi
kinachofanyakazi ya upinzani kama chama
kwani vyama vyote vilivyomo kwenye
Baraza kwa kiasi fulani viko upande wa
serikali kwa sababu vimetoa mawaziri. Kwa
maneno mengine ni kwamba kwa sasa
hakuna Kiongozi wa Upinzani wala Upande
wa Upinzani ndani ya Baraza la Wawakilishi
wala mawaziri vivuli.
Majukumu ya wajumbe wote wa Baraza la
Wawakilishi kutoka vyama mbali mbali
ambao si mawaziri wala si manaibu mawaziri
ni kuikosoa na kuiwajibisha serikali. Hii ina
26
maana kwamba yale majukumu yaliyokuwa
yakitekelezwa na Upande wa Upinzani
pamoja na ''backbenchers'' wa chama tawala
sasa yanahamia rasmi kwa ''backbenchers''
wa vyama vyote vilivyomo kwenye Baraza la
Wawakilishi.
Kulikuwa na hofu (hasa kwa wataalamu
mbalimbali wa nchi za Ulaya na asasi za
kiraia) kwamba kutokuwepo kwa kambi
rasmi ya upinzani kwenye Baraza
kutasababisha kudumaa kwa demokrasia na
kupwaya au kudorora kwa Baraza. Lakini,
uzoefu wa miaka mitatu ya Serikali ya
Umoja wa Kitaifa haukuonyesha hivyo.
Kilichoonekana ni kuimarika kwa
demokrasia, wajumbe wa Baraza wamekuwa
huru zaidi kutoa maoni yao na
''backbenchers'' wote kwa pamoja
wanashirikiana kuiwajibisha serikali. Mfano
uliowazi ni kuundwa kwa kamati teule nne
na matokeo yake yameanza kuonekana.
27
Masharti yaliyomo kwenye Katiba
kufuatia Marekebisho ya Kumi
Muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
kwa mujibu wa Marekebisho ya Kumi ya
Katiba ni kuwa na Rais mtendaji, Makamo
wa Kwanza wa Rais atakaeteuliwa na Rais
baada ya kushauriana na chama cha siasa
kilichopata nafasi ya pili katika matokeo ya
kura ya uchaguzi wa Rais, Makamo wa Pili
wa Rais atakaeteuliwa na Rais kutoka
miongoni mwa wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kutoka katika chama cha siasa
anachotoka Rais. Pia, Rais kwa kushauriana
na Makamo wote wawili atataeua Mawaziri
kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kwa kuzingatia uwiano wa viti
vya majimbo kwa vyama vya siasa vilivyomo
ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Vifuatavyo ni baadhi ya vifungu vilivyomo
katika Katiba ya Zanzibar kufuatia
marekebisho ya Kumi ya Katiba hiyo:-
28
Kutamkwa kwamba muundo wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni
wa Umoja wa Kitaifa (Kifungu cha 9
(3) cha Katiba).
Kuanzishwa kwa wadhifa wa
Makamo wa Kwanza na Makamo wa
Pili wa Rais na kufutwa kwa wadhifa
wa Waziri Kiongozi (Kifungu cha 39
(1) cha Katiba).
Mawaziri kuteuliwa na Rais kutoka
miongoni mwa wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi kwa kuzingatia
uwiano wa viti vya majimbo kwa
vyama vya siasa vilivyomo ndani ya
Baraza la Wawakilishi (Vifungu vya
42 (2) na 43 (2) vya Katiba).
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
chini ya mamlaka ya Rais ndiyo
itakuwa na uwezo wa kufanya
maamuzi juu ya sera za serikali „kwa
29
ujumla (Kifungu cha 43 (5) cha
Katiba).
Kutamkwa bayana kwamba Zanzibar
ni nchi, na mipaka yake, na ni moja
ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, na uwezo
wa Rais kuigawa Zanzibar katika
Mikoa na Wilaya na maeneo
mengine, na kutamkwa kuwa Rais
wa Zanzibar ni Mkuu wa nchi ya
Zanzibar (Vifungu vya 1, 2, 2A, na
26).
Kuweka masharti kuwa baadhi ya
vifungu vya Katiba haviwezi
kurekebishwa na Baraza la
Wawakilishi hadi kwanza kufanywe
kura ya maoni (Kifungu kipya cha
80A). Mfano wa vifungu
visivyoweza kurekebishwa
isipokuwa ifanywe kwanza kura ya
30
maoni ni vifungu vyote vilotajwa
hapo juu kwenye sehemu hii.
Taratibu muhimu za Uendeshaji Serikali
ya Umoja wa Kitaifa
Serikali ya Umoja wa kitaifa kwa kawaida
huendeshwa kwa kufuata taratibu zile zile
muhimu za uendeshaji serikali zikiwemo
zifuatazo:
Uwajibikaji wa Pamoja (Collective
Responsibility) wa mawaziri mbele
ya Baraza la Wawakilishi (Kifungu
cha 43 (5) cha Katiba).
Mawaziri kutoka vyama mbali mbali
vya siasa wanawajibika kufuata na
kuheshimu matakwa ya kudhibiti na
kutotoa siri za Baraza la Mawaziri
(Confideniality) (Kifungu cha 46 cha
Katiba na Sheria ya Viapo).
Wajibu wa mawaziri kuwa wawazi,
wakweli na kutoa majibu au maelezo
31
sahihi mbele ya Baraza la
Wawakilishi (Transparency,
Truthfulness and Accuracy). (Kanuni
za Baraza la Wawakilishi)
Uwajibikaji binafsi wa kila waziri
katika Baraza la Wawakilishi kwa
majukumu ya wizara anayoiongoza
hususan kuhusu sera, maamuzi na
matendo ya wizara hiyo (Individual
or Ministerial Responsibility)
(Kifungu cha 50 (1) cha Katiba).
Kutenganisha siasa (sera) na
Utendaji (Dichotomy of politics and
administration) (Kifungu cha 50 (1)
cha Katiba).
Wajibu wa kila waziri kutokuwa na
mgongano wa kimaslahi (Conflict of
Interest) baina ya majukumu yake ya
kazi ya uwaziri na maslahi yake
binafsi.(Kifungu cha 83 (3) cha
Katiba).
32
Wajibu wa kila waziri kutenganisha
utekelezaji wa majukumu yake ya
uwaziri na majukumu yake ya
uwakilishi wa jimbo lake la
uchaguzi.
Marufuku kwa waziri yoyote
kutumia mali au rasilimali za serikali
ikiwemo watendaji wa serikali kwa
ajili ya shughuli za chama cha siasa.
Wajibu wa kila waziri kuhakikisha
kwamba uteuzi anaoufanya kwa ajili
ya nyadhifa mbali mbali haufanyi
kisiasa bali kwa mujibu wa sifa na
kwa mujibu wa matakwa ya sheria na
taratibu zilizopo (Kifungu cha 69 (4)
(a) cha Katiba).
Ni mwiko kwa kiongozi kupokea
kipato cha kificho, au rushwa au
kushiriki katika mambo yoyote ya
magendo (Kifungu cha 69 (4) (b) cha
Katiba.
33
Vyeo vyote vya madaraka ni
dhamana na vipo kwa faida na
manufaa ya umma na wale wote
walio na madaraka watawajibika ama
moja kwa moja kwa umma au kupitia
vyombo vya uwakilishi (Kifungu cha
10 (h) cha Katiba).
Mambo ya kuyatafakari
(i) Rasimu ya katiba mpya
imeelekeza kwamba mambo
yasiyo ya muungano yako
mikononi mwa washirka wa
muungano na yatawekwa
kwenye katiba zao. Hii
inamaanisha kuwa Mfumo
wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa uliomo kwenye
Katiba ya Zanzibar kwa
ujumla hautoathirika.
34
(ii) Rasimu ya katiba mpya ya
Tanzania imefuata utaratibu
kama ule wa Katiba ya
Zanzibar wa kutamka
kwamba baadhi ya mambo
kwenye katiba hiyo
hayawezi kufanyiwa
marekebisho mpaka kwanza
ifanywe kura ya maoni.
Mambo hayo ni kuongeza au
kupunguza jambo lolote la
muungano, na uwepo wa
jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
(iii) Jee ipo haja ya kuwa na
utaratibu wa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa katika
katiba mpya ya Tanzania?
(iv) Marekebisho ya Nane ya
Katiba ya Zanzibar
yalianzisha utaratibu wa
35
kuwa na Tume ya Uchaguzi
yenye uwakilishi wa vyama
vya siasa. Jee tunakubaliana
na utaratibu uliopendekezwa
wa kuunda Tume Huru ya
Uchaguzi ya Tanzania kwa
utaratibu uliopendekezwa
kwenye rasimu ya awali ya
Tume ya Mabadiliko ya
Katiba bila ya kuwa na
uwakilishi wa vyama vya
siasa kwenye Tume hiyo?
(v) Endapo kutakuwa na
mabadiliko katika baadhi ya
mambo kwenye katiba mpya
ya Tanzania, itakuwaje kwa
upande wa Zanzibar kwa
mambo ambayo
hayabadilishiki isipokuwa
kwanza ipigwe kura ya
maoni? Kwa mfano:
36
(a) Kifungu cha 26 cha Katiba ya
Zanzibar hakiwezi kufanyiwa
marekebisho mpaka kwanza kufanyike
kura ya maoni. Kifungu cha 26 (2) (d)
kinataja miongono mwa sifa za mtu
kuweza kuwa Rais ni kuwa mwanachama
na mgombea aliyependekezwa na chama
cha siasa kilichosajiliwa kwa mujibu wa
Sheria ya Vyama vya Siasa ya 1992.
Endapo suala la mgombea binafsi
litakubalika na kuingizwa kwenye katiba
mpya ya Tanzania kwa chaguzi za
muungano, jee kwa upande wa chaguzi
za Zanzibar tutafanyaje? Tutafanya kura
ya maoni na kurekebisha katiba au bado
tutaendelea kuzuia mgombea binafsi?
(b) Mapendekezo ya rasimu ya awali ya
katiba mpya ya Tanzania yalipendekeza
mawaziri wa serikali ya muungano
wasiwe wabunge. Tumeona kwamba
vifungu vya 42 (2) na 43 (2) vya Katiba
ya Zanzibar vimeweka utaratibu kwamba
37
mawaziri watateuliwa kutoka miongoni
mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
na vifungu hivyo navyo haviwezi
kubadilishwa isipokuwa kwanza ifanywe
kura ya maoni, jee ikitokea hivyo
tutafanya kura ya maoni au tutabakia na
mfumo wetu tuliouzowea?