kenyatta university institute of open learning€¦ · kutokana na maelezo ya jumla ya sera ya...
TRANSCRIPT
1
DRAFT
KENYATTA UNIVERSITY
INSTITUTE OF OPEN LEARNING
ECT 313: MBINU ZA LUGHA NA FASIHI
(KISWAHILI METHODS)
VINCENT. F. KAWOYA
CHARLOTTE. W. RYANGA.
2
UTANGULIZI.
Kiswahili ni miongoni mwa masomo ya lazima katika kiwango cha elimu ya msingi
na sekondari humu nchini. Ukweli huu unadhirihisha uzito unaopewa lugha hii katika
mfumo wa maisha humu nchini.
Mwongozo huu unalenga kutoa mapendekezo ya kuelekeza wanafunzi na wasomi
wengine katika misingi ya kufundisha Kiswahili kwa njia inayofaa katika mazingira
ambamo watapaswa kufundishia.
Mwalimu akifundisha akitumia mbinu zinazostahili, matokeo yake ni kwamba
wanafunzi watakuwa na hamu ya kujifunza na kujivunia Kiswahili, ambayo ni lugha ya
taifa na kimataifa.
Ikiwa baada ya kuusoma mwongozo huu msomaji atahisi kwamba umepungukiwa
katika sehemu fulani, anashauriwa asikate tamaa. Lazima hii iwe changamoto kwake
kufidia upungufu aliougundua.
Ni matumaini yetu kwamba mwongozo huu utachangia kuchochea watu
wanaojishughulisha na usambazaji wa Kiswahili ili waweze kubuni mbinu za kufundishia
ambazo zinajikita katika misingi madhubuti ya ufahamu wa mfumo wa lugha pamoja na
hali halisi ya Kiswahili.
3
YALIYOMO.
SOMO La 1 Hadhi ya Kiswahili
1.1 Lugha ni Kitambulisho cha Ubinadamu…………………………………………5
1.2 Sera za Lugha…………………………………………………………………….6
1.3 Kiswahili Ulimwenguni………………………………………………………….7
1.4 Mikakati ya Usambazaji na Upanuzi wa Kiswahili……………………………...8
SOMO La 2. Maana na Sifa za Lugha.
2.1 Sifa za Lugha…………………………………………………………………...10
2.2 Kanuni za Kufundishia…………………………………………………………16
SOMO LA 3 Ufundishaji wa Lugha ya Pili
3.1 Mbinu ya Kimapokeo…………………………………………………………...19
3.2 Mbinu ya Moja kwa Moja………………………………………………………20
3.3 Mbinu ya Uzungumzi……………………………………………………………21
3.4 Mbinu ya Kimawasiliano………………………………………………………...21
3.5 Msingi wa Mbinu ya Kimawasiliano…………………………………………….23
SOMO LA 4 Maandalizi ya Mwalimu
4.1 Silabasi…………………………………………………………………………….25
4.2 Maazimio ya Kazi…………………………………………………………………27
4.3 Mpango wa Kipindi……………………………………………………………….33
SOMO LA 5. Kusikiliza na Kuongea.
5.1 Umuhimu wa Kusikiliza……………………………………………………………42
5.2 Kusikiliza kwa Ufahamu……………………………………………………………43
5.3 Vizuizi vya Ufahamu sikizi……………………………………………………… 44
5.4 Kufanikisha Ufahamu sikizi………………………………………………………..49
5.5 Umuhimu wa Kuongea……………………………………………………………. 52
5.6 Matatizo ya Kimatamshi……………………………………………………………53
5.7 Kufundisha Matamshi………………………………………………………………58
5.8 Kufundisha Kuongea……………………………………………………………….63
5.9 Njia za Kufundishia Mazungumzo………………………………………………...65
SOMO La 6 Kusoma na Kuandika.
6.1 Kusoma kwa Sauti…………………………………………………………………68
6.2 Matatizo ya Kusoma kwa Sauti……………………………………………………69
6.3 Kusoma Kimoyomoyo…………………………………………………………….71
6.4 Maswali ya Ufahamu………………………………………………………………72
6.5 Kuandika Ufupisho…………………………………………………………………74
6.6 Kuandika Imla……………………………………………………………………...76
6.7 Uandishi wa Insha………………………………………………………………….77
SOMO La 7. Sarufi na Matumizi ya Lugha
7.1 Matatizo ya Kimsamiati na Kisarufi……………………………………………….85
7.2 Uhusiano Kati ya Maneno…………………………………………………………89
4
7.3 Kufundisha Msamiati………………………………………………………...90
7.4 Ujuzi wa Sarufi……………………………………………………………….97
7.5 Kufundisha Sarufi…………………………………………………………….98
SOMO La 8. Fasihi.
8.1 Dhana ya Fasihi…………………………………………………………….106
8.2 Dhima ya Fasihi…………………………………………………………….106
8.3 Mitazamo Tofauti ya Maana ya Fasihi……………………………………..107
8.4 Tanzu za Fasihi……………………………………………………………..109
8.5 Uchambuzi wa Fasihi……………………………………………………….115
MAREJEREO………………………………………………………………… 119
5
SOMO 1
HADHI YA KISWAHILI NA SERA ZA ELIMU
1.0 Utangulizi
Mara nyingi mwalimu wa lugha anapofunza lugha huingilia moja kwa moja
visehemu vinavyoorodheshwa katika mtaala. Ni nadra mwalimu kuanza kwa kuwaelezea
wanafunzi umuhimu wa lugha hususa lugha ya Kiswahili, kando na kuwa somo la lazima
kwenye ratiba ya shule. Mwelekeo huu hausaidii mwanafunzi kuwa na motisha ama
msukumo wa kumpa matamanio ya kujifunza Kiswahili kwa bidii. Hali hii huendelezwa
na fikra za watu wengi kwamba Kiswahili hakisaidii mtu anayetafuta kazi kuajiriwa, kwa
ambavyo Kiingereza hutumika kwa mahojiano na mawasiliano ya kikazi maofisini. Hii ni
kwa mujibu wa kuwa hadi sasa Kiingereza ndiyo lugha inayotambulikana kuwa rasmi
nchini Kenya.
Ili mwalimu aweze kutayarisha wanafunzi waweze kupata ari ya kupata matokeo mazuri,
ni bora tangu awali kuwaeleza umuhimu wa lugha hii, kuifahamu na kuiongea vyema.
Kiswahili kina nafasi yake nchini Kenya kama lugha ya taifa na hivyo kurahisisha
mawasiliano katika hali ya wingi wa lugha; na vile vile kama lugha inayounganisha, na
kuyatambulisha mataifa ya Afrika Mashariki, na hivi sasa, lugha mojawapo mashuhuri ya
Umoja wa Mataifa ya bara la Afrika.
MADHUMUNI YA SOMO
Kufikia Mwisho wa somo hili, inatarajiwa kwamba utaweza:
Kutambua umuhimu wa Kiswahili
Kueleza maana na sera ya lugha
Kutambua umataifa wa Kiswahili
1.1 Lugha ni kitambulisho cha ubinadamu
Lugha imesemekana kuwa sifa ya kuwabainisha viumbe vingine na binadamu.
Hivyo lugha ni muhimu kwa mawasiliano baina ya makundi ya watu na miongoni mwa
binadamu. Lugha yoyote ile hutambulisha jamii inayoitumia, na kudhihirisha utamaduni
wake. Utamaduni hudhihirika kutokana na uwasilishaji wa itikadi mbalimbali, mila za
kijamii, matamanio ya jamii na kadhalika. Pia matumizi ya lugha katika jamii huleta
ukuruba wao na kuchochea umoja, katika matumizi yake kwenye midahalo ya kijamii.
Hivyo tunaposema lugha hufungamana na utamaduni wa jamii ni kusema kwamba lugha
inapata mantiki yake kutokana na hadhi za maisha ya jamii ile. Jambo hili ni muhimu
6
kwa mwanafunzi kujua tangu mwanzo ili aweze kuelewa utata unaozingira Kiswahili
kama lugha ya taifa miongoni mwa makabila yenye lugha nyingi.
Tujuavyo, taifa moja linaweza kuwa na lugha nyingi. Nchini Kenya tuna takriban
lugha 45 , kulingana pengine na makabila yaliyomo. Kawaida kila lugha hujaribu
kujipendekeza ama kila kabila huwa na matamanio ya lugha yake kuwa lugha ya taifa.
Hizi ni hisia za kawaida na penye lugha nyingi, uchaguzi wa lugha zitakazotumika rasmi
lazima ufanywe kwa kituo na umakinifu, ili kuondoa hamaki na shinikizo za ukabila.
Aidha wanafunzi wafahamishwe kuwa ujuzi wa lugha hutambulika kwa uwezo wa
kuongea, kuiandika na kuisoma lugha hiyo.
1.2 Sera za lugha
Sera ni mfumo ama utaratibu fulani unaofuatwa katika kuchagua jambo fulani.
Kwa hivyo tunapozungumzia sera ya lugha tunamaanisha utaratibu unaoongoza uteuzi
wa lugha zitakazotumiwa kirasmi nchini. Sera ya lugha nchini Kenya ina historia ndefu
tangu enzi za ukoloni hadi leo. Sera zimeendelea kubadilika kulingana na mahitaji ya
nchi wakati baada ya wakati, kwa mfano, kufikia Tume ya Mackay 1981 alipokikweza
hadhi Kiswahili kufunzwa kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu. Jambo hili
lilisababishwa na ufahamu kuwa Kiswahili ni lugha muhimu. Kwa mujibu wa Ferguson
(1968), lugha muhimu ni ile iliyo na sifa zifuatazo:
1. Kwamba inaongewa na zaidi ya watu asilimia 25 wenyeji, ama na zaidi ya watu
milioni moja;
2. Kwamba ni lugha rasmi ya nchi
3. Kwamba ni lugha ya elimu ya zaidi ya asilimia 50 ya waliofuzu vyuo vya upili
nchini.
Kuna ithibati nyingi kuonyesha kuwa Kiswahili kimefikia sifa hizi. Fergurson
anaendelea kusema kwamba lugha huwa na hadhi maalumu nchini inapotumika katika
mojawapo ya njia hizi:
1. Kutumika kwa minajili ya mahubiri ya kidini
2. Kutumika kwa minajili ya kisomo
3. Kufunzwa kama somo mojawapo katika shule za upili
4. Kutumika kama lugha ya mawasiliano na watu wengi nchini
5. Kutumika katika utendakazi wa kundi moja la watu nchini
Kulingana na vidokezo hivi vya Fergurson, umashuhuri wa Kiswahili hautiliwi
tashwishi kamwe. Kiswahili kimechangia ujenzi wa taifa pakubwa. Pamoja na kufunzwa
shule, kimechangia maarifa ya kuchambua na kuelewa nyenzo za kudumisha jamii
kuyatawala mazingira yake. Tena, kimewakweza watu na kuwaingiza katika utamaduni
wa kisasa kwa ukubalifu wake katika matumizi ya kiteknolojia hivi majuzi.
Sera hizi za lugha zimeongozwa na mabadiliko mengi ya mifumo ya kisiasa.
Pamoja na mifumo ya kisiasa pengine tungesema kwamba sera hizi zingejumuisha
matamanio ya jamii ya kutaka kuhusishwa katika ujenzi, utawala wa nchi na maendeleo
ya kiuchumi. Kwa mfano hadi sasa kufanywa kwa Kiswahili lugha ya taifa kumewasaidia
wengi wasio na kisomo rasmi kujihusisha na maendeleo nchini kwa kuweza kuchangia
katika mijadala iliyopo kwa lugha wanayoifahamu – Kiswahili. Wanafunzi waelezwe
7
wazi kwamba kufunzwa kwa Kiswahili katika viwango vyote vya shule, huleta
utangamano miongoni mwa makabila tofauti kwa kujumuisha utamaduni wa Mwafrika.
1.3 Kiswahili ulimwenguni
Ni muhimu kuwafahamisha wanafunzi jinsi Kiswahili kilivyoenea ulimwenguni
katika nyanja zote za maisha. Sasa kinafunzwa katika vyuo vikuu mbalimbali huko
ulaya, kwa mfano, nchini Uingereza, SOAS (School of Oriental and African Studies),
Chuo cha Gent Ubelgiji, nchini Ujerumani, huko Marekani
Hadhi ya Kiswahili imeendelea kuimarika kuambatana na historia ya Kiswahili.
Kiswahili kimeendelea kupanuka katika msamiati na hali ya matumizi yake kiasi cha
kuweza kutumika katika ufunzaji wa mitaala tofauti na katika utafiti pia. Ukuaji wa hadhi
umesaidiwa na sera mbalimbali za elimu na lugha nchini Afrika Mashariki, hasa
Tanzania na Kenya.
Kufikia karne hii ya ishirini na moja, lugha ya Kiswahili imefahamika
ulimwenguni kote. Inasemekana kwamba Kiswahili sasa ni miongoni mwa lugha saba
ulimwenguni, zinazotambulikana na Umoja wa Mataifa (UN). Lugha maarufu nyinginezo
ni pamoja na Kifransa, Kirusi, Kihispanyola, Kichina, Kiarabu na Kiingereza.
Kuambatana na matumizi ya kimataifa, Kiingereza hutumiwa na mataifa 92, kama lugha
ya pekee iliyotumika katika mikutano ya kimataifa kwa muda mrefu. Matumizi haya
yanalingana na nyakati za historia, Uingereza ilipotawala koloni nyingi ulimwenguni.
Kifransa kilifuatia kikiongewa katika mataifa 31. Nyenzo zake za kikoloni zafahamika
kihistoria.
Lugha ya tatu kwa upana wa matumizi ni Kihispanyola, kikitumika kwenye
mataifa 21; Kihispanyola kilifuatwa na Kiarabu, kilichowahi kutumika miongoni mwa
mataifa 18. Upana huu wa matumizi ni kwa ajili ya Bara Arabu na mkondo wote wa nchi
za kasikazini mwa Afrika , ambako Kiarabu kimechukua nafasi ya lugha nyinginezo
asilia za nchi hizo kama Kimisri. Lugha ya Wamisri wa jadi ilipotea kabisa na Kiarabu
kuchukua nafasi yake. Pengine haya yalitokea wakati wa vita vya Jihadi, vya
kuwasilimisha ‘makafiri” kama walivyojulikana wasiokuwa Waislamu. Baada ya
Kiarabu, lugha nyingine ni Kichina kinachotumika katika mataifa 2, na Kirusi katika taifa
1 tu. Takwimu hizi ni kulingana na The World Almanac and Book of Facts (1983). Ni
jambo la kujivunia kwamba Kiswahili kimejiunga na mataifa haya, ijapo matumizi yake
yamesambaa miongoni mwa mataifa mengi Barani Afrika na hata Ulaya na Marekani.
Ambapo nyingi za lugha zilizotajwa zilikuwa za mababe wa ukoloni, lugha ngeni,
hivyo kusambazwa kwa msukumo wa utawala huu barani Afrika, Kiswahili kinyume cha
hayo, kilijipendekeza chenyewe kwa watumizi wake. Ni kweli kwamba enzi za ukoloni
Kiswahili kilitumiwa kwa utawala, lakini ni lugha iliyopatikana Afrika Mashariki na
kukubalika moja kwa moja kama mojawapo ya lugha nyinginezo za Kiafrika.
Ni muhimu tufahamu kwamba kutambulikana kwa lugha yo yote ulimwenguni si
jambo dogo. Kuchaguliwa kwa Kiswahili kama lugha mojawapo ya ulimwengu
hakukutokea tu hivi ghafla bin vu. Mataifa ya Kiafrika barani humu tayari walikuwa
wamekitambua kuwa lugha mashuhuri inayoweza kutumika kwa manufaa ya mataifa
yote, wala tu si Afrika Mashariki kulikochimbuka lugha hii. Viongozi wa Umoja wa
Mataifa Barani Afrika walitambua yafuatayo:
(1) Jinsi kilivyowasaidia wakoloni kuleta umoja miongoni mwa wale waliowatawala,
hivyo wakayaona manufaa yake katika kuwaunganisha watu;
8
(2) Kwamba lugha hii haikujikita katika uhasama wa kikabila, kwa ambavyo matumizi
yake yameenea kote, na kuwa lugha ya taifa nchini Kenya na Tanzania, ukubalifu
huu ukapanua mipaka yake zaidi ya ile ya kikabila;
(3) Kwamba kunawiri kwa biashara miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki na
Kati kumebainika kwa sababu ya matumizi ya Kiswahili, katika maingiliano ya
Wanyarwanda, Warundi, Waganda, Watanzania, Wakenya na Wakongo.
Hivi karibuni Kiswahili kimechaguliwa na mataifa ya Kiafrika, katika vikao vya
Umoja wa Mataifa (AU) kuwa lugha rasmi mojawapo zitakazotumiwa katika
mawasiliano Barani Afrika. Tayari Kiswahili nchini Kongo ni mojawapo ya lugha nne
zilizochaguliwa kuwa za taifa miongoni mwa zaidi ya lugha takriban mia mbili
zinazozungumzwa nchini humo. Sababu tatu zajitokeza kuhusu kukubalika kwa
Kiswahili:
1) Urahisi wake wa maongezi,
2) Kusambaa kwake na,
3) Ukwasi pamoja na utamaduni wake wa kifasihi miongoni mwa sifa
nyinginezo za lugha hii zilizotangulia kutajwa.
Hivi sasa Kiswahili si tu lugha tambulishi ya eneo la Afrika Mashariki bali
imejumuisha bara lote la Afrika.
ZOEZI 1.1
Utafiti wa maktabani:
1. Kutokana na maelezo ya jumla ya sera ya lugha kwenye matini, soma
vitabu maktabani na uandike kwa ufupi sera za lugha zilizokuwepo nchini
Kenya tangu tupate uhuru, mwaka 1963.
2. Kwa kutumia maelezo uliyopewa kwenye matini, fafanua jinsi matumizi
ya lugha yo yote ile yanavyowatambulisha watu mjini Nairobi.
1.3.1 Mikakati ya usambazaji na upanuzi wa Kiswahili
Wanafunzi wanahitaji kufahamishwa kwamba usambaaji wa Kiswahili
ulimwenguni umekifanya kitambulike kama lugha ya kimataifa. Tangu jadi Kiswahili
kimwekuwa lugha teule ya mawasiliano, na usambazaji wake ulisababishwa na mambo
mbalimbali. Awali enzi za ukoloni, Kiswahili kilisambazwa na wakoloni, wamishenari
katika jitihada zao za kufunza dini; na Waarabu vile vile pamoja na wakoloni katika
biashara zao za watumwa na pembe za ndovu. Biashara hizi ziliwapeleka wageni hao
bara ya Afrika Mashariki hadi kufikia maeneo ya Afrika ya Kati, kama Zaire, Rwanda na
Burundi.
Baadaye usambazaji uliendelezwa na wamishenari waliojitahidi kuwafunza
Waafrika dini yao ya Kikristo, na kufanya juhudi za kuwaelimisha kwa kufunza kusoma
9
na kuandika. Masomo haya yalifunzwa kwa lugha ya Kiswahili, kwa kuchelea
kuwafunza Waafrika lugha ya mabwana zao Waingereza. La ziada ni kwamba Kiswahili
pia kilieleweka miongoni mwa makabila mengi nchini Kenya na kwingineko, na hivyo
kuwa lugha rahisi kuchaguliwa kwa shughuli hii.
Ipo mikakati mingi ya kuendeleza matumizi ya Kiswahili tangu uhuru
ulipopatikana mwaka wa 1964 hadi sasa. Kwa mfano, Mzee Jomo Kenyatta alikitangaza
Kiswahili kuwa lugha ya taifa nchini Kenya. Baadaye akatangaza kwamba kingeweza
kutumiwa kwa mijadala bungeni. Nyakati hizo pia magazeti ya Kiswahili yalianzishwa,
kama “Sauti ya Pwani,” “Taifa Leo” kwa mfano. Vyombo vya habari pia vilifungua
idhaa nyingi za Kiswahili. Tayari juhudi za kuandika makamusi zilikuwa zinaendelea.
Baadhi ya vipindi vya redio vilianzishwa kujadili fasihi na msamiati na matumizi ya
Kiswahili kwa jumla.
Hadi sasa Kiswahili kimetamalaki nyanja nyingi za matumizi ya kawaida na ya
kitaaluma. Makamusi mengi yameandikwa, na hivi sasa, huko Marekani juhudi
zimekithiri kutayarisha kamusi ambayo itatumiwa kwenye taraklishi ili kuwasaidia
waandishi kwa lugha ya Kiswahili, kuweza kusahihisha lugha yao. Matayarisho haya
yanafanywa kwa mujibu wa MICROSOFT kampuni kubwa ya taraklishi. Ambapo tayari
Kiswahili kilikuwa kikifunzwa baadhi ya nchi za Magharibi na chache za Mashariki,
kuweko kwa kamusi ya Kiswahili kwenye taraklishi kutasambaza lugha hii zaidi kote
ulimwenguni, wengi wakiweza kuifanyia utafiti na kuitumia kuandika ripoti zao.
Teknolojia hii imesaidia sana katika kuendeleza hadhi na matumizi ya Kiswahili
ulimwenguni.
Aidha yapo makamusi yaliyoandikwa kuchangia ujuzi kulingana na istilahi za
kitaaluma, kama zile za fasihi, sayansi, mazingira, utabibu, isimu na kadhalika. Sera ya
serikali kufuatia Tume ya Mackay ndiyo hasa iliyokiingiza Kiswahili katika ratiba za
shule zote nchini Kenya, kuanzia shule za msingi hadi za upili. Kwa hivyo si lugha ya
kiholela tena ama ile ya watu wasio kisomo kama ilivyotambulika zamani. Itambulike
kuwa Kiswahili kimekuwa somo muhimu hata katika vyuo vikuu vya kitaifa nchini
TAFAKARI
Zingatia sehemu unayoishi iwapo ni mjini ama kijijini. Kuna ushahidi gani
kwamba matumizi ya Kiswahili yanasambaa miongoni mwa waongezi wa
lugha nyinginezo? Ungetoa mapendekezo gani kuwasaidia watu hao
kujifunza lugha hiyo kwa njia bora zaidi?
ZOEZI 1.2
1. Eleza mielekeo iliyopo miongoni mwa jamii yako kuhusu matumizi ya
Kiswahili. Je kuna upinzani wo wote?
2. Kwa kutumia maelezo uliyopewa mwanzo, eleza jinsi matumizi ya lugha
yanavyotambulisha watu jijini Nairobi.
3. Zingatia matumizi ya Kiswahili mahali unapoishi. Je ni mbinu gani
unazoweza kutumia ili kuendeleza matumizi ya kiswahili sanifu?
10
SOMO 2
MAANA NA SIFA ZA LUGHA
2.0 Utangulizi
Ikiwa mwalimu wa lugha anataka kuukabili vizuri ufundishaji wa lugha, hana
budi kufahamu vilivyo maana ya lugha pamoja na sifa za kimsingi ambazo
zinaitambulisha lugha kama chombo maalum. Kanuni na mbinu za kufundishia Kiswahili
pia ni lazima zihusishwe na ufahamu kamili wa maana na sifa za lugha. Kwa kufanya
hivyo, mwalimu anaweza kufundisha Kiswahili kwa njia inayofaa akitilia maanani
ukweli halisi wa lugha.
MADHUMUNI YA SOMO
Kufikia mwisho wa somo hili, inatarajiwa kwamba utaweza:
Kutaja na kufafanua sifa mbali mbali za lugha.
Kupendekeza kanuni za kufundisha Kiswahili unazoweza kupata kutokana na sifa
ulizotaja
Kufafanua maana ya lugha.
2.1. Sifa za lugha.
Je, lugha ni kitu gani na ina sifa gani maalum? Wataalamu wa lugha wanaeleza
maana ya lugha kwa namna mbalimbali, lakini hata hivyo huwa wanakubaliana juu ya
mambo ya kimsingi ambayo yanaiainisha lugha na kuitambulisha kwa njia maalum. Kwa
ufupi mambo hayo ni kama yafuatayo:
(a). Lugha ni mfumo kamili.
(b). Lugha ni mfumo wa sauti nasibu.
(c ) Sauti za lugha ni za kutamkwa.
(d) Lugha ni chombo cha mawasiliano.
(e) Lugha hufungamana na utamaduni wa jamii.
(f) Mfumo wa lugha ni wenye ubunifu.
2.1a. Mfumo kamili
Katika mkutadha huu, tunaposema kwamba lugha ni mfumo kamili huwa
tunataka kutilia mkazo ukweli kwamba lugha haitumiwi segemnege. Huwa inatumiwa
kwa kufuata kanuni fulani katika utaratibu maalum unaokubaliwa na wanajamii wa lugha
husika. Kwa mfano, vitamkwa vya lugha vinaunganishwa pamoja kwa utaratibu maalum
11
ili kuunda maneno. Vilevile maneno nayo huwa yaunganishwa kwa mpangilio maalum ili kuunda sentensi.
Kwa mfano, lugha ya Kiswahili ina baadhi ya konsonanti na vokali zifuatazo: /i/, /a/, /b/, /m/, /s/. Kutokana na vitamkwa hivi vichache inawezekana kuunda maneno kama
yafuatayo: bima, sima, simba, siasa, sisi, bibi, mimi, mimba, miiba, iba, imba, imbia,
msiba n.k….Haya ni maneno ambayo yanaundwa kwa kuzingatia utaratibu maalum
unaokubalika katika Kiswahili. Kwa upande mwingine, maneno yafuatayo, hata ingawa
yameundwa kutokana na vitamkwa vinavyopatikana katika Kiswahili, yanakiuka
utaratibu wa Kiswahili. Hayakubaliki kama maneno ya Kiswahili:*sbaini, *bsimai *bmia
*smia.
Vitamkwa katika mifano hii vimelundikwa ovyo ovyo bila kuzingatia kanuni
zinazotawala mfuatano wa vitamkwa katika Kiswahili, na kuishia na maneno ambayo
hayana maana.
Pia maneno yakitamkwa yanatamkwa kwa kuzingatia kanuni maalum. Kwa
mfano, katika Kiswahili watu huwa wanatumia shadda. Shadda yenyewe huwa haitumiwi
bila utaratibu. Kwa kawaida shadda inawekwa kwenye silabi inayotangulia ile ya
mwisho. Kutokana na utimizaji wa kanuni hii, neno linapopanuka shadda huhamishwa.
Mifano ifuatayo inabainisha ukweli huu:
kanisa, kanisani.
karibu, karibuni.
tumeona, tumeonana.
Zaidi ya hayo, maneno nayo yanapaswa kupangwa kwa utaratibu maalum ili yalete maana. Kwa mfano, katika Kiingereza inakubalika kusema: Where is my new
book?, Where are my new tables? Kwa upande mwingine, lugha ya Kiswahili na baadhi
ya lugha zingine haziruhusu mpangilio wa namna hii. Ni kosa , kwa mfano, katika
Kiswahili kusema:
* Wapi kiko changu kipya kitabu?
* Wapi ziko zangu mpya meza?
Bila kuzingatia utaratibu unaokubalika lugha inakosa ufasaha wake. Kwa mfano
mtu akisema “Manyumba hizi ni za City Council”, hapana shaka kwamba mtu huhyu
ametumia maneno ya lugha ya Kiswahili, lakini ovyo ovyo bila kufuata utaratibu
unaokubalika. Hakuzingatia utaratibu wa ngeli za Kiswahili. Neno nyumba katika
Kiswahili halibadiliki umbo katika wingi. Limo katika ngeli ambayo majina yake
hayatumii kiambisho awali ma-. Pia msemaji huyu huwa amevunja kanuni za sarufi ya
Kiswahili anaposema nyumba hizi ni ya city council. Kwa mujibu wa utaratibu wa
Kiswahili anatakiwa kusema: nyumba hizi ni za…. Mifano ifuatayo inaonyesha zaidi
ukweli kwamba lugha ni mfumo:
12
Ukichunguza kwa makini jinsi majina haya yanavyobadilika kutoka umoja na
kuwekwa katika hali ya wingi utaona kwamba kuna utaratibu unaofuatwa. Utagundua,
kwa mfano kwamba majina yenye silabi mbili huwa yanatanguliza na kiambisho ny- k.m.
uzi- nyuzi, wembe- nyembe. Yale yenye zaidi ya silabi mbili hudondosha kiambisho u-.
Kwa upande mwingine baadhi ya majina ambayo silabi yake inayofuata kiambisho awali
u- ni /b/ huwa yanadondosha kiambisho awali u- na kutumia /m/ badala yake.
Ifuatayo ni mifano mingine inayodhihirisha kwamba lugha ina utaratibu wake
maalum.
Ukichunguza maneno yanayofupishwa katika mifano hii utaona kwamba
mabadiliko yanatokana kwanza katika kimilishi. Irabu ya mwisho katika kimilishi
inahamishwa na kutumiwa badala ya irabu ya silabi ya kwanza. Kisha baada ya kuwekwa
kwa irabu hiyo silabi mpya inaunganishwa na jina; na matokeo yake ni jina na kimilishi
kama neno moja.
Majina Majina
Umoja. Wingi
ufa
uzi
uso
wembe
wayo
ukuta
utepe
ubawa
ubao
wavu
upande
unyoya
nyufa
nyuzi
nyuso
nyembe
nyayo
kuta
tepe
mbawa
mbao
nyavu
pande
nyoya
Fungu la maneno Ufupisho
Kundu lake
Mwana wake
Baba yake
Ndugu yake
Mbacha wako
Kundule
Mwanawe
Babaye
Nduguye
mbachawo
13
Maana nyingine ya kauli hii ni kwamba lugha iwayo yo yote inajitosheleza kama
chombo kinachoweza kutegemewa na jamii ili kutekeleza mahitaji yao ya kimawasiliano
katika mfumo wa maisha yao. Hakuna lugha ambayo ni duni.
2.1 b. Mfumo wa sauti nasibu
Je, nini maana ya kusema kwamba lugha ni mfumo wa sauti nasibu? Maana
mojawapo ya kauli hii ni kwamba hakuna uhusiano wa moja kwa moja wala wa kudumu
kati ya maneno yanayotumiwa kuashiria vitu au dhana fulani na vitu hivyo
vinavyoashiriwa au dhana inayoashiriwa. Hakuna sababu yo yote ya kimsingi kwa nini
sauti maalum zinatumiwa kuashiria kitu au jambo fulani na wala siyo sauti zingine. Kwa
mfano, mtu ambaye hafahamu lugha ya Kifransa akisikia neno “lait”, hakuna kielelezo
cho chote katika neno hilo ambacho kinaweza kumsaidia kuelewa kile
kinachozungumziwa. Vilevile Mfransa ambaye hafahamu Kiswahili, akisikia neno
“maziwa” hawezi kukisia kwamba neno hilo lina maana ya lait ya Kifransa. Hakuna cho
chote ndani ya neno kinachoweza kusaidia mtu kutambua maana yake. Jambo hili
linawezekana tu katika maneno machache yanayofuata mwigo wa sauti, na ambayo kwa
Kingereza huitwa “Onomatopoeic”. Sauti ambazo hutumiwa kurejelea mambo na hali
tofauti zilizuka kisadfa bila kikao maalum cha watu kuamua kuhusu jinsi vitu fulani
vinastahili kuitwa. Vitu huitwa kama vinavyoitwa kwa sababu watu wa jamii ya lugha
fulani ndivyo walivyozoea kulingana na mfumo wa maisha yao.
Unasibu wa lugha unachangia katika kutumia maneno ya lugha kwa namna kama
zifuatazo:
(i). Kutumia neno moja kuashiria vitu/ maana tofauti.
(ii). Kutumia maneno tofauti kuashiria kitu kimoja /dhana moja. Kwa mfano, kila
mojawapo katika maneno yafuatayo linaweza kuambatanishwa na zaidi ya maana moja:
panda, kata, meza, mbuzi, kaa….. .Katika lugha ya Kiswahili na Kiitaliano kuna neno
vita ambalo hufanana kimatamshi katika lugha zote mbili lakini linatumiwa kwa maana
tofauti kabisa. Maana ya vita ya Kiitaliano ni uhai katika Kiswahili! Mfano mwingine ni
neno mzigo la Kiswahili ambalo linafanana na neno muzigo katika Luganda. Kimatumizi
maneno haya hayana uhusiano wo wote. Muzigo katika Luganda humaanisha mafuta ya
kupikia au kujikapa. Hali kama hii inabainisha unasibu wa lugha.Vilevile maneno shida
na taabu yanaweza kutumiwa kurejelea dhana moja.
Zaidi ya haya, kauli isemayo kwamba lugha ni mfumo uliyo nasibu inaweza
kufasiriwa kumaanisha kuwa wakati fulani matumizi yake yanaelekea kukosa mantiki.
Kwa mfano, mfumo wa Kiswahili unaruhusu sentensi kama zifuatazo ambazo zinaenda
kinyume na matarajio ya ukweli wa mambo katika maisha ya kila siku:
Nasikia njaa.
Nasikia usingizi.
Tusikate tamaa.
Sijakata shauri bado.
Tupige magoti tuombe.
Je, mtu anawezaje kusikia njia au usingizi? Kwani usingizi na njaa vinatoa sauti?
Pia inawezekanaje kwa mtu kukata tamaa au shauri wakati ambapo tunajua kwamba
tamaa na shauri haviwezi kuonekana na kushikwa kwa mkono? Na je, kupiga magoti
kuna maana ya kuchukua fimbo au kifa cho chote kile na kisha kuyatwanga?
14
Jibu ni kwamba miundo kama hii inawezekana kutokana na hali kwamba lugha
kimsingi, ni mfumo ulio nasibu. Ni kutokana na hali hii ndipo mara kadhaa matumiza ya
lugha yanaelekea kukosa msimamo ulio thabiti na wazi. Hali hii inaonyeshwa katika
jedwali lifuatalo linaloonyesha baadhi ya maneno ya Kiswahili katika umoja na wingi.
Maneno ya kundi (a) yamo katika ukoo wa majina ya watu. Isipokuwa neno
mtume katika wingi maneno mengine katika kundi hili huanza na kiambisho awali wa-.
Kutofanana na maneno mengine katika kundi hili, neno mtume linatumia kiambisho mi-
kama vile yanavyofanya maneno ya kundi la (b). Je kwa nini tuseme mitume na wala si
watume?.
Tukichunguza maneno katika kundi (c) ni wazi kwamba hata ingawa yote katika
hali ya umoja yanaanza na ji-, katika hali ya wingi baadhi yake yanadondosha kiambisho
hiki na kutumia ma- badala yake, wakati ambapo mengine yanahifadhi kiambisho hiki na
kukitanguliza na kiambisho ma- cha wingi. Ikiwa mwanafunzi atauliza kwa nini tusiseme
majicho badala ya macho au mapu badala ya majipu haitawezekana kumweleza kwa nini
inakuwa hivyo, isipokuwa kusema tu haya ndiyo mazoea ya lugha ya Kiswahili!
Kutokana na mifano hii ni wazi kuwa mwalimu wa Kiswahili hapaswi
kujishughulisha na maswali ya kimantiki anapofundisha Kiswahili. La maana na manufaa
zaidi ni kuwaelekeza wanafunzi ili waweze kutumia Kiswahili kuwasiliana kwa urahisi
na ufahamu wakizingatia utaratibu wa matumizi yake. Lengo kuu la kufundisha lugha
siyo kuihakiki kimantiki, bali ni kufanikisha uwezo wa kuwasiliana ipasavyo.
2.1 c Sauti za Kutamkwa
Kwa kawaida binadamu hufanya sauti nyingi katika hali ya maisha yake ya kila
siku. Kwa mfano, anaweza kutoa sauti kwa kugonganisha vyombo na kutokana na
kukanyaga ardhi anapotembea. Anaweza pia kukohoa au kupiga chafya na wakati
Umoja Wingi
(a) mzazi
mvuvi
mtume
(a) wazazi
wavuvi
mitume
(b) mkeka
mtego
mkate
(b) mikeka
mitego
mikate
(c) jiwe
jicho
jambo
jibu
jipu
(c) mawe
macho
mambo
majibu
majipu
15
mwingine kucheka. Umuhimu wa sauti zitokanazo na vitendo kama hivi ni kwamba
kutokana na sauti hizo wanaoshuhudia wanaweza kupata fununu kuhusu hali ya yule mtu
anayetoa sauti hizo. Hakuna, kwa mfano, jinsi unavyoweza kuchambua kicheko na
kuonyesha vitamkwa mbali mbali vinavyounganishwa kukiunda. Vile vile hakuna jinsi
unavyoweza kubainisha vitamkwa mahsusi vinavyounda kikohozi au chafya. Lakini kwa
upande mwingine unaweza kubainisha wazi vitamkwa vinavyounda maneno tofauti. Kwa
mujibu wa wataalamu wa lugha sauti hizo hazina hadhi ya kiisimu. Kimsingi , sauti za
lugha ni zile tu ambazo hujitokeza katika utaratibu kamili kupitia mdomo wa binadamu
kutokana na kushiriki kwa viungo kadhaa vinavyohusika katika utamkaji.
2.1 d Chombo cha Mawasiliano.
Kazi kuu ya lugha ni kufanikisha uhusiano kati ya binadamu au kuwawezesha
kuendeleza maisha yao ya kila siku. Lugha ya pamoja husaidia kufanikisha mawasiliano
katika vipengele mbali mbali vya maisha ya binadamu. Ili watu waweze kupashana
habari na kubadilishana mawazo wanahitaji kuwa na chombo cha mawasiliano. Na
chombo hiki ni lugha.
Kwa misingi ya kiisimu mawasiliano ya lugha yanashirikisha stadi zifuatazo
ambazo zinaingiliana na kutiliana nguvu: kusikiliza, kuongea, kusoma na kuandika kwa
ufahamu lugha anayojifunza.
2.1 e Lugha Hufungamana na Utamaduni.
Lugha haichimbuki katika ombwe tupu, bali ni zao la utamaduni fulani. Kwa
hivyo lugha iwayo yo yote, kwa kiasi fulani inabeba utamaduni wa jamii ulioichipuza,
pamoja na kuathiriwa na utamaduni huo. Kwa mfano, watu ambao huishi katika
mazingira yaliyo karibu na bahari wana maneno mengi yanayoambatana na shughuli
mbalimbali zinazoendelea baharini.
Sifa mojawapo ya utamaduni ni kwamba aghalabu unabadilika kufuatana na
mabadiliko ya wakati. Na jambo hili linapotokea lugha nayo pia haina budi kubadilika ili iweze kuwiana na mabadiliko. Ni kutokana na hali hii ndipo lugha inaweza kujitosheleza
kama chombo cha mawasiliano ya jamii inayohusika. Mifano ya mabadiliko hayo ni
kama vile maneno mapya kubuniwa au kukopwa na kuingizwa katika lugha. Zaidi ya
hayo baadhi ya maneno yanaweza kupanuliwa na kuzingatia upeo mpana wa maana.
Mifano ya maneno yaliyoingia katika Kiswahili hivi karibuni ni kama vile: ukimwi,
tarakirishi, barua pepe, utandawazi, n.k…. Mifano kama hii inaonyesha kuwa lugha ni
mfumo ulio wazi.
Ni muhimu kwa mwalimu wa lugha kutambua kuwa kuna uhusiano mkubwa
baina ya lugha na utamaduni. Wakati wa kufundisha anaweza kukumbana na misemo
ambayo ni vigumu kueleza maana yake bila kuelewa utamaduni uliochipuza misemo
hiyo. Misemo mingi kama vile methali imejikita katika utamaduni. Mwalimu
anapofundisha misemo hiyo hana budi kuelewa utamaduni wake. Hali kadhalika,
wanafunzi wanapojifunza lugha nyingine wanaweza kuathiriwa na utamaduni wa jamii
zao hadi kiasi cha kuhamisha misemo ya jamii zao na kuitumia katika lugha
wanayojifunza. Matokeo ya jambo hili ni kwamba huenda misemo hiyo isieleweke katika
mkutadha wa utamaduni wa lugha ya pili, au pengine inaweza kueleweka kwa namna
16
isiyotarajiwa. Ni muhimu sana kwa mtu ye yote anayejifunza lugha kujitahidi kutofasiri
misemo ya lugha anayojifunza kwa misingi ya utamaduni wa jamii ya lugha yake ya
kwanza. Unaweza kuelewa maneno yote yanayotumiwa lakini ukashindwa kuelewa
ujumbe unaowasilishwa kwa kutozingatia utamaduni wa wazawa wa lugha husika. Kwa
mfano, Mtanzania anapotaka kununua anaweza kutumia neno omba. Akitaka, kwa
mfano, kununua nyama anaweza kusema, “Naomba kilo mbili za nyama”. Katika
mazingira ya Kenya, wasikilizaji huenda wakafikiria kuwa msemaji huyu anataka
kupewa nyama ya bure. Kusema kweli jambo hili lilitokea hapo Githurai. Mama mmoja
mtanzania alimwambia mwuzaji kuwa anaomba kilo mbili za nyama. Jama alifyoka na
kumwambia kuwa akitaka nyama ni lazima alipe!
Aidha askari Mtanzania anaweza kumwambia mshukiwa “Naomba
twandamane….”. Kwa mtu ambaye amelelewa katika mazingira ambamo askari hawana
sifa ya kutumia lugha kwa upole, anaweza akafikiria kuwa ana hiari ya kutoandamana na
askari huyu. Amri ya askari huenda asiielewe kama amri kwa sababu ya mazoea ya
utamaduni wa jamii yake. Mifano hii inakufundisha wewe kama mwalimu kwamba
ukitaka wanafunzi wako waimudu vizuri lugha unayofundisha huna budi kuwadokezea
kuhusu utamaduni wa jamii ya lugha hiyo.
Lugha ni kama kioo cha utamaduni wa jamii. Kwa hivyo mwalimu anaweza
kufundisha utamaduni wa jamii fulani kupitia lugha anapofundisha methali. Methali
zifuatazo, kwa mfano zimebobea utamaduni wa watu wa pwani ambao unaweza kutatiza
wanafunzi kutoka sehemu zisizo za pwani:
Mgema akisiwa tembo hutilia maji.
Usiache mbachao kwa msala upitao.
Aliyekupa kiti ndiye kanipa kuti.
Mgaagaa na upwa hali wali mkavu.
Mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani.
2.1. f Ubunifu wa lugha.
Lugha ni chombo chenye ubunifu. Hali hii inawezesha binadamu, kwa mfano,
kuunda maneno chungu nzima kutokana na idadi ndogo ya vitamkwa vinavyopatikana
katika lugha. Vilivile kutokana na maneno machache watu wanaweza kuunda sentensi
zisizo na idadi kamili. Pamoja na haya, mtu anapoimudu lugha fulani anaweza kuibuka
na miundo mipya ya sentensi ambayo haijawahi kutamkwa hapo awali na watu wengine.
Sifa hii ya lugha huchangia kuipa lugha uhai ambao huifanya kuwa chombo ambacho
kinajitosheleza kwa mawasiliano ya jamii. Ubunifu husaidia lugha kuendelea kupanuka
kila uchao kwa kupokea na kuingiza maneno mapya.
2.2 Kanuni za kufundishia.
Je mwalimu anaweza kupata maarifa gani ya kanuni za kufundisha lugha
kutokana na sifa zilizotajwa hapo mbeleni?
Miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuhusu sifa za lugha ni kwamba ni mfumo
kamili wa sauti za kutamkwa. Kauli hii inabainisha kwamba lugha imejikita katika
utaratibu wa sauti. Kwa hivyo, ufundishaji wa lugha zungumzi unapaswa kupewa uzito
unaostahili katika mpango wa kufundisha lugha. Pamoja na hayo mwalimu wa lugha
17
anatakiwa kuwa na fununu kuhusu viungo vinavyohusika katika utoaji wa sauti na jinsi
viungo hivyo vinavyohusika katika utoaji wa sauti. Jambo hili litamsaidia mwalimu
katika juhudi za kushughulikia matatizo ya kimatamshi ambayo huenda yakawakumba
wanafunzi wake.
Na mashauri unayoweza kupata kutokana na kauli isemayo kuwa lugha ni mfumo
kamili ni kwamba somo la lugha linapaswa kuendeshwa kwa utaratibu maalum na
kuzingatia uhalisia wa lugha inayohusika. Kila lugha inapaswa kufundishwa kama
chombo ambacho kinajitosheleza. Haipaswi kufundishwa kupitia lugha nyingine. Pia
haifai kwa mwalimu kufundisha wanafunzi matamshi ya maneno na maana tu bila
kuwaonyesha namna ya kupanga maneno hayo katika utaratibu kamili unaokubalika na
jamii husika. Kwa vile lugha ni mpangilio kamili wa maneno, mwalimu anashauriwa
asifundishe tu maneno bila kuyatumia katika vielelezo vya sentensi. Sentensi hutoa
mkutadha bora wa kubainishia matumizi ya maneno.
Kutokana na unasibu wa lugha, mashauri yanayoweza kupatikana ni kwamba
mwalimu anapofundisha hapaswi kujishughulisha na maswali ya kimantiki. La maana na
manufaa zaidi ni kufundisha lugha kama vile ilivyo ili wanafunzi waweze kuitumia
kuwasiliana kwa urahisi bila kutatizika wala kuwatatiza wengine. Na ikiwa lugha ni
chombo cha mawasiliano, mwalimu anashauriwa kuhakikisha kuwa anafundisha akiwa
anatilia mkazo juu ya uwezo wa kuwasiliana. Lazima afundishe kwa kutumia mbinu
ambazo zitachochea mawasiliano miongoni mwa wanafunzi.
Ni jukumu lako kama mwalimu kuona kwamba wanafunzi wako wanashirikishwa
vya kutosha katika shughuli kamili za matumizi ya Kiswahili. Washirikishwe kama
wahusika wawasilishaji wa ujumbe. Washirikishwe pia kama wahusika wapokezi wa
ujumbe. Unapaswa kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata fursa ya kuendeleza stadi
zote za lguha: kusikiliza, kuongea, kusoma na kuandika.
Kwa ufupi ufanikishaji wa mawasiliano upewe kipaumbele katika mpango wa
kufundisha lugha. Ni lazima wanafunzi wakuze uwezo wa kuwasilisha na kupokea
ujumbe bila shida.
Kauli nyingine ni ile isemayo kuwa lugha hufungamana na utamaduni. Neno
utamaduni aghalabu huashiria mambo kama vile mila, desturi, itikadi, na mfumo wa
maisha kwa jumla. Lugha ni kama kioo cha utamaduni wa jamii ya watu wanaohusika.
Hii ina maana kuwa, kwa kiasi fulani, lugha inamulika hali ya maisha ya watu
wanaoitumia, matarajio yao, mtazamo wao wa maisha, pamoja na mazingira yao kwa
ujumla. Kwa hivyo, mwalimu anashauriwa kutilia maanani uwezekano wa mwingiliano
wa utamaduni kati ya lugha ya wanafunzi na Kiswahili wakati anapofundisha. Mtu
anaweza kufahamu maneno yanayotumiwa katika msemo fulani, lakini hata hivyo
huenda akashindwa kuelewa ujumbe uliyomo ndani kutokana na hali ya utamaduni
wenye kuchipuza msemo huo. Hali kadhalika, lugha hubadilika kufuatana na mabadiliko
ya utamaduni. Kwa hivyo, mwalimu naye ni lazima awe tayari kufundisha akizingatia
matokeo ya mabadiliko ya wakati.
Kauli ya mwisho ni ile isemayo kuwa lugha ni mfumo wenye ubunifu. Ukweli
huu unamdokezea mwalimu kwamba anapofundisha wanafunzi lugha, ni lazima awape
nafasi tele kujifunza namna mbalimbali za matumizi ya lugha. Wapewe nafasi ya
kushuhudia na kushiriki katika mitindo tofauti ya lugha ndipo nao waweze kuitumia
kivyao.
18
2.3 HITIMISHO
Somo hili limejishughulisha hasa na sifa za kimsingi zinazoiainisha lugha.
Kutokana na sifa hizi mwalimu wa Kiswahili anaweza kupata maarifa kadhaa ambayo
yanaweza kumsaidia katika kufundisha. Kwa kurejelea sifa hizo zilizotajwa tunaweza
kufasiri lugha kwa njia kama ifuatayo:
Lugha ni mfumo kamili ulio nasibu wa sauti za kutamkwa ambao jamii ya watu
wa utamaduni fulani hutumia kwa madhumuni ya kuwasiliana.
Kutokana na ufafanuzi huu ni wazi kwamba lugha asilia ni lugha ya kusema.
Lugha ya kuandika ni kiwakilishi tu cha lugha ya kusema. Ni kutokana na ukweli huu
ndipo tunaona kuwa kuna watu wengi ambao wanaweza kuzungumza lugha yao bila
kujua jinsi ya kuandika lugha hiyo.
ZOEZI 2
1. Ukitoa mifano mwafaka ya kutilia maki jibu lako, fafanua zaidi sifa za
lugha
2. Taja sifa za lugha zozote tatu, na kwa kila mojawapo ya sifa hizo eleza
kanuni za kufundisha Kiswahili unazoweza kupata kutoka kwake
3. Toa fasiri yako ya neno lugha ukizingatia sifa za kimsingi
zinazoitambulisha lugha.
19
SOMO 3
UFUNDISHAJI WA LUGHA YA PILI.
3.0 Utangulizi
Kuna mikabala/ mikondo mbalimbali katika historia ya ufundishaji wa lugha ya
pili ambayo imewahi kutumiwa. Baadhi ya mikabala hiyo, mpaka sasa imeendelea
kuathiri ufundishaji wa lugha ya pili. Ujuzi wa mikabala hiyo ni jambo muhimu kwa
mwalimu wa Kiswahili kwa sababu unaweza kumsaidia kupata fununu kuhusu asili ya
mbinu tofauti tofauti zinazotumiwa kufundisha lugha ya pili. Hapo awali mbinu hizi
zililenga hasa ufundishaji wa lugha ya Kingereza kama lugha ya pili. Hata hivyo, baadhi
ya mambo ambayo hupendekezwa katika mbinu hizo yanaweza kumsaidia mwalimu
ambaye anajishughulisha na ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya pili.
Madhumuni Ya Somo
Kufikia mwisho wa somo hili utaweza kutoa mifano ya mbinu za
kufundishia lugha na kueleza jinsi kila mojawapo ya mbinu hizo
inaweza kutumiwa katika ufundishaji wa Kiswahili.
3.1 Mbinu Ya Kimapokeo
Hii ni mbinu ambayo hapo awali ilitumika kama njia ya kufundishia lugha za
kijadi kama vile Kiyonani na Kilatini. Ilitawala ufundishaji wa lugha za kizungu na
kigeni kati ya miaka 1840 na 1940. Lengo kuu la mbinu hii ni kufanikisha ufahamu wa
sarufi pamoja na uwezo wa kuandikia kwa usahihi katika lugha inayolengwa. Pia
inalenga kuwezesha mwanafunzi kuwa na upeo mpana wa msamiati unaotumika sana
katika lugha ya uandishi katika lugha husika, ili hatimaye aweze kuthamini umuhimu
pamoja na thamani ya nakala zinazohusika.
Katika mazingira ya darasani, mwalimu anatazamiwa kutekeleza malengo haya
kwa kushirikisha wanafunzi katika kazi ya kutafsiri mara kwa mara kutoka lugha zao
hadi katika lugha inayofunzwa. Kabla ya kutafsiri, wanafunzi wanapaswa kwanza
kijifunza maneno ya lugha inayolengwa ili waweze kutafsiri katika lugha mpya. Pamoja
na hayo, wanafunzi wanapewa maelezo marefu kuhusu sheria za kisarufi. Kisha
wanapewa zoezi la kutunga sentensi ili kubainisha ufahamu wao wa sheria hizo. Uwezo
wa mwanafunzi katika kutafsiri huwa ndicho kigezo muhimu kinachotumiwa kama
chombo cha kupima ustadi wake katika kipengele cha sarufi na msamiati.
Udhaifu hasa wa mbinu hii ni kwamba haitilii mkazo juu ya matamshi sahihi
pamoja na stadi za kimawasiliano. Inasisitiza sana ujuzi wa sheria za kisarufi bila kupatia
wanafunzi nafasi ya kutosha kujieleza kutokana na nafsi zao. Matokeo ya kujishughulisha
sana na ufundishaji wa kanuni na vighairi ni kwamba waalimu huishia kwa kufundisha
20
wanafunzi lugha ya ulimwengu wa vitabu, lugha isiyokuwa na uhai, na ambayo mara
nyingi haina manufaa katika ufanikishaji wa mawasiliano ya kawaida.
Utumiaji wa mbinu hii unalifanya somo la lugha kukosa ubunifu unaotakikana.
Wanafunzi hawapati nafasi ya kutumia lugha kama chombo wanachoweza kukitegemea
kutekeleza mahitaji yao ya kimawasiliano. Shughuli ya kujifunza lugha inageuka kuwa
zoezi la kukariri maneno chungu nzima na kanuni kemkem za kisarufi. Hakuna hakikisho
kwamba baada ya kukariri maneno na kanuni wanafunzi watakuwa na uwezo wa kutumia
kanuni na maneno vilivyokaririwa katika mawasiliano ya nje ya darasa. Shughuli ya
kufundisha na kujifunza lugha inakuwa kama zoezi la kuchemsha bongo tu.
3.2. Mbinu Ya Moja Kwa Moja
Hali ya kutoridhika na mbinu ya kimapokeo ni miongoni mwa mambo ambayo
yalichangia kuibuka kwa mbinu ya moja kwa moja. Iliibuka katika karne ya 19 kuchukua
mahali pa mbinu ya kimapokeo. Wanaopendelea mbinu hii hushikilia kwamba njia
mwafaka ya kujifunza lugha ya pili ni kukabiliana nayo moja kwa moja na kuitumia
kama vile mtoto mdogo anavyofanya anapojifunza lugha ya mama. Kulingana na mbinu
hii ni marufuku kutumia lugha ya wanafunzi au lugha nyingine yo yote ile.
Mbinu hii husisitiza umilisi wa lugha bila tafsiri wala maelezo rasmi juu ya sheria
za kisarufi. Wanafunzi wanatakiwa kijifunza lugha kwa kushirikishwa kikamilifu kama
wahusika watendaji katika matumizi tofauti tofauti ya lugha. Inasisitizwa kwamba ikiwa
maana inaweza kuwasilishwa moja kwa moja kwa kushirikisha maono au vitendo hakuna
haja ya kutafsiri.
Kwa upande wa sarufi, mbinu hii inashikilia kwamba njia bora ya kuendeleza
ufahamu wake ni kutokana na uzoefu wa kutumia mara kwa mara lugha inayohusika.
Mwanafunzi akipewa fursa ya kutosha kukumbana na matumizi ya lugha, itakuwa rahisi
kwake kutambua na kujifunza sheria zinazotawala sarufi ya lugha hiyo.
Mbinu hii inasisitiza haja ya kutoa nafasi kwa mwanafunzi ya kujifunza lugha
kama vile mtoto anavyojifunza lugha yake ya kwanza. Mtoto anajifunza na kuimudu
lugha kwa kukumbana nayo moja kwa moja katika mkutadha maalum wa mawasiliano.
Hakuna mtu anayemfafanulia kanuni za kisarufi za lugha yake. Hata hivyo anazing’amua
kanuni hizo yeye mwenyewe baada ya kushuhudia matumizi yake katika vielelezo vya
sentensi. Huwa anajifunza lugha ya jamii yake katika mazingira yanayoshirikisha vitendo
na maono. Ushirikishaji wa maono na vitendo unachangia kujenga hali ambayo husaidia
mtoto kukisia maana ya kile kinachosemwa. Anajifunza lugha ya jamii yake kwa
kusikiliza kwanza na baadaye kuigiza yale anayosikiza.
Kwa mujibu wa mbinu hii mwalimu anapofundisha lugha ya pili anashauriwa
kutotegemea tafsiri. Anashauriwa vile vile kutofundisha moja kwa moja sheria za
kisarufi. Ana wajibu wa kuambatanisha ufundishaji wake na vitendo, uigizaji na
mazungumzo. Lakini ikiwa mwalimu hana budi kufundisha sarufi, inafaa ufundishaji wa
sarufi uzingatie kiwango cha matumizi ya lugha huko mkazo ukitiliwa juu ya madondoo
ya kisarufi yanayotumika sana sana hasa katika mazungumzo.
Kwa mujibu wa mbinu hii, dhima ya mwalimu ni kupanga na kufanikisha utumizi
wa lugha badala ya kujishughulisha na ufafanuzi pamoja na uchambuzi wa kanuni za
kisarufi. Ili mwalimu aweze kufaulu kutumia mbinu hii anapaswa kuwa na ujuzi wa
kiwango cha hali ya juu katika lugha anayofundisha. Ni lazima pia awe na ubunifu wa
21
kumwezesha kuwasilisha maana bila kutumia lugha nyingine yo yote zaidi ya ile ambayo
anafundisha. Anatarajiwa pia kujitahidi kujenga mazingira ya kufundishia ambayo
yanakaribia kufanana yale ya lugha ya kwanza. Mazingira hayo yanatarajiwa kufanikisha
ufahamu wa lugha kupitia mazoezi ya kusikiliza pamoja na mazungumzo. Lazima yawe
mazingira ambayo yanaweza kuchangia katika kuhamasisha mwanafunzi kutaka
kujifunza lugha inayohusika.
Kwa kawaida mtoto anapojifunza lugha yake ya kwanza anakuwa na hamu ya
kujifunza lugha hiyo ili aweze kutangamana na jamii ya watu wanaomzunguka. Jamii
hiyo pia humsaidia kuendelea kwa kumtia shime. Pamoja na hayo mtoto huwa na muda
mwingi wa kusikia na kutumia lugha hiyo. Lugha inakuwa sehemu ya maisha yake ya
kila siku.
3.3 Mbinu Ya Uzungumzi.
Mbinu hii ilizuka na kukita mizizi katika miaka ya 1950 kutokana na mwamko
mpya nchini Amerika wa kujishughulisha na ufunzaji wa lugha za kigeni. Tukio muhimu
ambalo lilichangia pakubwa kuamsha ari ya Wamerika katika lugha za kigeni ilitokea
mnamo mwaka wa 1957. Mwaka huo Warusi walifaulu kupeleka chombo chao (sputnik)
angani. Jambo hili lilikuwa changamoto kubwa kwa taifa la Amerika. Kufuatia tukio hilo,
serikali ya Amerika iliamua kujishughulisha kikamilifu katika ufundishaji wa lugha za
kigeni ili isiachwe nyuma katika maendeleo ya kisayansi.
Jambo ambalo linapewa kipaumbele katika mbinu hii ni ufasaha wa kuzungumza.
Ufasaha unaotarajiwa unahusu matamshi bora, sarufi, pamoja na uwezo wa kuitikia upesi
na kwa urahisi katika hali tofauti zinazohusisha utumizi wa lugha katika mazungumzo.
Ufahamu sikizi, matamshi, sarufi na msamiati vinapofundishwa huwa kama njia
mojawapo ya kufanikisha ufasaha wa kuzungumza. Vilevile wanafunzi
wanaposhirikishwa katika kuandika na kusoma mambo haya yanaambatanishwa na ustadi
wa kutumia lugha ya mazungumzo.
Kulingana na mbinu hii, stadi za lugha zinastahili kufundishwa kwa kuzingatia
mfuatano huu: Kusikiliza, Kuongea, Kusoma na Kuandika.
Katika hatua za mwanzo mwanzo, kusoma na kuandika vinachukuliwa tu kama
mambo ambayo yanaweza kuchangia kuimarisha ustadi wa kusikiliza na kuongea.
Vinatiliwa mkazo zaidi katika viwango vya juu wakati ambapo wanafunzi wana uzoefu
unaofaa ili kuweza kukabiliana na mitindo zaidi ya lugha ya kimaandishi.
Madondoo ya lugha yanapofundishwa kwa kutumia mbinu hii huwa
yanawasilishwa kupitia mjadala ambao ni chombo muhimu cha kutoa mkutadha wa
kufundishia kile kinacholengwa. Zaidi ya kushiriki katika mjadala, wanafunzi huwa
wanatakiwa, mara kwa mara, kukariri vielelezo vya sentensi.
3.4 Mbinu Ya Mawasiliano.
Msingi wa mbinu hii ni imani kwamba kazi kuu ya lugha ni kufanikisha
maingiliano pamoja na mawasiliano katika jamii. Lugha ni chombo ambacho
kinamwezesha binadamu kushirikiana na watu wengine na pia kutekeleza mahitaji ya
maisha yake. Kwa hivyo, kulingana na waasisi wa mbinu hii, lengo kuu la kufundisha
22
lugha ni kuwezesha mwanafunzi kuwa na uwezo wa kuwasiliana akitumia lugha
inayohusika.
Njia moja ya kuhakikisha kuwa mwanafunzi anakuwa na uwezo wa kuwasiliana
ni, kwanza, kumpa fursa ya kushiriki kama mhusika mpokezi. Mwanafunzi anapata fursa
ya kupanua upeo wake wa lugha kupitia kusikiliza na kusoma. Baada ya kushiriki katika
matumizi ya lugha akiwa mhusika mpokezi mwanafunzi anashirikishwa kama mhusika
mwanzilishi wa mawasiliano. Kulingana na waasisi wa mbinu ya mawasiliano, lugha
ambayo ni ya maana / manufaa kwa wanafunzi inatilia nguvu juhudi za kujifunza. Kwa
hivyo ni muhimu kwa walimu kuhakikisha kwamba wanapochagua kazi ya wanafunzi
wanatilia maanani uwezo wa kazi hiyo wa kuwashirikisha katika matumizi ya lugha
yenye maana na uhalisi.
Kwa kawaida, mawasiliano hufanyika katika mazingira ya watu wakiwa katika
vikundi. Pia, aghalabu, mawasiliano huchukua mkondo wa mazungumzo (conversation)
na majidiliano (discussion). Wakizingatia ukweli huu, wanaounga mkono mbinu ya
kimawasiliano wanapendekeza kugawanya wanafunzi katika vikundi vidogo vidogo. Hii
ni njia bora ya kuendeleza uwezo wa wanafunzi wa kuwasiliana kwa kutumia lugha
inayofundishwa. Wakiwa katika vikundi vya watu wachache, wanafunzi wanakuwa na
fursa bora ya kutumia lugha halisi. Pia wanapata nafasi ya kujieleza kwa ufasaha bila
wasiwasi. Ustadi katika kusoma na kuandika unaweza kukuzwa kutokana na msingi
imara wa kutumia lugha kwa uhalisi.
Je jukumu hasa la mwalimu ni nini? Kwa mujibu wa waasisi wa mbinu hii,
jukumu la mwalimu ni kuhamasisha wanafunzi na kutoa kwao nafasi ya kujieleza katika
lugha inayohusika. Ana wajibu wa kuhamasisha wanafunzi kutumia lugha kwa njia
mbalimbali. Anapaswa pia kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata fursa ya kujieleza.
Pamoja na hayo, mwalimu ana wajibu kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaelewa vizuri
kwa nini wanafundishwa kile wanachofundishwa. Hivi ndivyo watakavyoweza kushiriki
kwa njia ya maana na manufaa kwao. Vilevile ni lazima mwalimu ahakikishe kuwa
wanafunzi wake wanahusika zaidi kuliko vile anavyohusika mwenyewe.
Aidha, mwalimu anashauriwa kushirikisha wanafunzi katika vitendo ambavyo
vinaweza kuwalazimisha kuwasiliana kwa kutumia lugha inayofaa kulingana na
mkutadha. Kwa maneno mengine, mwalimu anapaswa kubuni hali na mazingira ambamo
wanafunzi hawawezi kukidhi mahitaji na matarajio yao bila kuwasiliana. Wakijikuta
katika mazingira ya namna hii hawatakuwa na budi kutafuta ufumbuzi kwa kutumia
lugha. Kwa ufupi, mwalimu anaweza kusaidia kuendeleza uwezo wa wanafunzi wa
kuwasiliana wakitumia lugha kwa kuzingatia mfuatano wa hatua zifuatazo:
1. Mapokezi ya lugha.
2. Ufafanuzi / Maelezo
3. Majaribio ya matumizi ya lugha
4. Mawasiliano huru
Katika hatua ya mapokezi wanafunzi wanashiriki kama wahusika wapokezi. Kazi
yao katika hatua hii ni kupokea ujumbe unaowasilishwa na watu wengine na kupata
maana ya ujunbe unaowasilishwa. Wanaweza kutekeleza jambo hili kupitia zoezi la
kusikiliza au kusoma. Zoezi la kusikiliza husaidia wanafunzi kupata nafasi ya kupanua
upeo wa lugha. Kupitia zoezi hili wanaweza kujifunza msamiati mpya na miundo
23
mbalimbali ya kisarufi. Vilevile wanafunzi wanaimarisha ujuzi wao wa yale ambayo
wamejifunza tayari.
Kwa upande mwingine, katika hatua ya ufafanuzi (maelezo) mwalimu anaweza
kudondoa madondoo fulani ya lugha ambayo wanafunzi wamewahi kukumbana nayo,
katika zoezi la kusikia na kusoma. Kisha anatoa maelezo kuhusu madondoo hayo ili wanafunzi wayatilie maanani zaidi kuliko mengine kwa wakati huo. Baada ya
kuhakikisha kwamba wanafunzi wanafahamu kiini cha somo mwalimu anawapa
wanafunzi nafasi ya kujaribu kutumia madondoo hayo katika vielelezo vya sentensi
wakizingatia maagizo yaliyotolewa.
Katika hatua ya mawasiliano huru wanafunzi wanapata fursa zaidi ya kujieleza
bila kufuata maagizo ya mwalimu. Wanaweza kujieleza kwa njia halisi kulingana na
mahitaji ya mawasiliano katika mkutadha unaohusika. Wanafunzi watateua lugha
kulingana na hali halisi inayowakabili wakati huo. Mawasiliano huru huwapa wanafunzi
fursa ya kutambua kuwa lugha siyo somo ambalo linajikita katika mipaka ya mazingira
ya darasani tu., lakini pia ni chombo cha mawasiliano nje ya mipaka ya darasa.
Mawasiliano huria huwapa wanafunzi nafasi ya kutumia lugha kwa njia ya ubunifu katika
miktadha tofauti tofauti ya kijamii. Wanatumia lugha bila usimamizi wa mwalimu, lakini
kulingana na hali halisi katika mazingira ya mawasiliano. Huwa wajitegemea wao
wenyewe. Kadiri wanavyoshiriki katika mikutadha tofauti ya mawasiliano na kushuhudia
jinsi lugha inavyotumiwa, ndivyo wanavyoendelea kukuza na kuimarisha uwezo wao wa
kimawasiliano (communicative competence). Uwezo huu ni muhimu kwa mwanafunzi
kwa sababu akiwa nao anaweza kufasiri lugha kwa njia iliyo sahihi akizingatia mkutadha
unaohusika. Na akifanya hivyo anaweza kuitikia kama inavyotarajiwa. Kwa mfano
mwalimu akiingia darasani ambamo mna joto jingi na agundue kuwa madirisha
yamefungwa, anaweza akasema: Mbona joto limezidi sana humu ndani. Mwanafunzi
mwenye uwezo wa kimawasiliano atatambua kuwa mwalimu angetaka madirisha
yafunguliwe, na ataitikia kwa kuyafungua. Yule asiyekuwa na uwezo huo atachukulia
usemi wa mwalimu kama kauli ya kawaida tu.
3.5 Msingi wa Mbinu ya Kimawasiliano
Asili ya mbinu ya kimawasiliano ni imani inayoshikilia kwamba:
(a) Lugha ni mfumo wa kueleza maana.
(b) Jukumu kuu la lugha ni kufanikisha maingiliano na mawasiliano baina ya
watu.
(c) Shughuli ambazo zinachangia kufanikisha ufahamu wa lugha ni zile
ambazo zinatoa kwa wanafunzi nafasi ya kushiriki katika mawasiliano
halisi (real communication).
(d) Vitendo vinavyohusisha matumizi ya lugha ili kutekeleza shughuli za
maana (meaningful tasks) husaidia kufanikisha ujuzi wa lugha.
(e) Lugha yenye maana kwa wanafunzi inaimarisha hali ya kujifunza.
(f) Mawasiliano hufanyika ikiwa wale wanaohusika wana hamu (motisha) ya
kuwasiliana.
24
3.6 HITIMISHO.
Somo hili limezungumzia baadhi ya mikabala (mbinu) tofauti inayotambulikana
katika historia ya ufundishaji wa lugha ya pili. Ni jukumu la mwalimu kuteua na kutumia
mbinu inayofaa kulingana na matarajio yake. Lakini, kwa vyo vyote vile mwalimu
anapaswa kutilia maanani kiwango cha wanafunzi, jambo linalotiliwa mkazo, uwezo
wake, idadi ya wanafunzi na kupatikana kwa vifaa vya kufundishia.
ZOEZI 3.
Eleza jinsi unavyoweza kufundisha mambo yafuatayo ukitumia
mbinu ya mawasiliano:
(a). Kauli ya kutendea.
(b) Matumizi ya –ki- na kwa.
25
SOMO LA 4
MAANDALIZI YA MWALIMU.
4.0 Utangulizi:
Matayarisho ni jambo la lazima katika utekelezaji wa kazi ya aina yo yote. Haifai
kwa mtu kutegemea kupata matokeo mazuri katika kazi anayofanya ikiwa ataikabili ovyo
ovyo bila kujitayarisha kwa kazi hiyo. Kila mfanya kazi anahitaji kujitayarisha na
kujihami kulingana na kazi yake. Njia mojawapo ya kujihami ni kuhahakikisha kwamba
ana vifaa vya utekelzaji wa kazi inayohusika.
Je unaweza kujihami namna gani kuikabili kazi ya kufundisha? Ni hatua gani
ambazo utachukua kuhakikisha kwamba kazi yako inafanyika kwa utaratibu mzuri?
Katika somo hili tutajadili vyombo muhimu unavyohitaji katika maandalizi yako
kwa kazi ya kufundisha. Na vyombo hivi ni: Silabasi, Maazimio ya kazi, na Mpango wa
kipindi cha somo.
MADHUMINI YA SOMO
Kufikia mwisho wa somo hili, inatarajiwa kwamba utaweza:
(i) Kueleza umuhimu wa silabasi, maazimio ya kazi na
mpango wa kipindi cha somo, katika taaluma ya uwalimu
(ii) Kutayarisha maazimio ya kazi na mpango wa kipindi cha
somo.
(iii) Kutoa sababu kueleza kwa nini mambo fulani yanapaswa
kuonyeshwa katika vyombo vya kufundishia
vinavyohusika.
4.1 Silabasi.
Miongoni mwa hatua ambazo unapaswa kuchukua ili uweze kujihami ipasavyo
kwa kazi ya kufundisha ni kuhakikisha kwamba unafahamu yaliyomo katika Silabasi ya
Kiswahili. Silabasi ni chombo muhimu kinachotayarishwa na wakuza mtaala nchini ili kuwaongoza waalimu kuhusu madhumuni ya ujumla ya somo, madhumuni mahsusi ya
26
vitengo vya somo, pamoja na yale yanayotarajiwa kufundishwa katika viwango tofauti
vya elimu shuleni.
Je, unaweza kufikiria jinsi mambo yangekuwa nchini kama kusingekuweko
silabasi ya pamoja? Matokeo yangekuwa kwamba kila mwalimu angefundisha mambo
tofauti kulingana na matakwa yake, jambo ambalo lingesababisha viwango tofauti vya
elimu nchini. Pia ingekuwa vigumu kwa baraza la mitihani nchini kuwa na kielelezo bora
cha kutumia kama kigezo wakati wa kutahini wanafunzi mwishoni mwa masomo yao.
Kuwepo kwa silabasi kunahakikisha kwamba waalimu wote wanafuata mwongozo sawa
pamoja na kuwa na mwelekeo sawa katika ufundishaji wa somo linalohusika. Kupitia
silabasi wizara ya elimu inaweza, kwa kiasi fulani, kudhibiti mfumo wa elimu nchini na
kuhakikisha kwamba waalimu wanatekeleza wajibu wao sambamba na sera za elimu
nchini.
Je, unayakumbuka mambo ya kimsingi ambayo yanatiliwa mkazo na sera za
elimu nchini Kenya? Ni lazima uyakumbuke mambo hayo kwa sababu ufundishaji wa
Kiswahili, kama vile ulivyo ufundishaji wa masomo mengine, ni lazima uchangie katika
utekelezaji wa madhumuni ya kitaifa. Kwa muhtasari, shabaha za elimu za kitaifa nchini
Kenya zinalenga kutoa elimu ya kuelekeza vijana katika mambo yafuatayo:
(a) Umoja wa taifa.
(b) Maendeleo ya taifa kiunchumi na kijamii.
(c) Maendeleo ya mtu binafsi.
(d) Usawa wa kijamii.
(e) Uthamini na ukuzaji wa utamaduni.
(f) Mwamko wa kimataifa.
Mambo haya, bila shaka , yalitiliwa maanani na wakuza mtaala wakati wa
kutayarisha silabasi. Nawe pia, ukiwa mtekelezaji mkuu wa sera za elimu, huna budi
kuyatilia maanani unapotekeleza wajibu wako wa kufundisha.
Kimuundo mpangilio wa silabasi ya Kiswahili ni hivi kwamba ina sehemu ya
madhumuni ya ujumla ya somo na mgawanyiko wa somo zima katika vitengo vinne
vifuatavyo:
(i) Kusikiliza na kuzungumza.
(ii) Sarufi na matumizi ya lugha.
(iii) Kusoma.
(iv) Kuandika.
Somo zima limegawanyika katika vitengo hivi kuanzia kidato cha kwanza mpaka
kidato cha nne. Pia kila kitengo kinachohusika kinaambatanishwa na shabaha mahsusi
zinazotarajiwa kutekelezwa. Na mambo yanayotarajiwa kufundishwa katika kila kidato
yameorodheshwa chini ya kitengo cha somo kinachohusika.
Kutokana na silabasi hii unaweza kujiandaa kukabili ufundishaji wa somo kwa
kutayarisha maazimio ya kazi, ambayo ni chombo kingine muhimu katika taaluma ya
uwalimu. Kwa hivyo, kabla ya kutayarisha maazimio ya kazi huna budi kuichunguza kwa
undani silabasi ya somo lako ili ufahamu vizuri yaliyomo ndani yake. Ni kufuatia
ufahamu wa mambo haya ndipo utakapokuwa tayari kuukabili vyema ufundishaji wa
somo lako. Itakuwia rahisi, kwa mfano, kuamua kuhusu vitabu vinavyostahili kutumiwa
27
na wanafunzi ukitumia silabasi kama kielelezo cha kimsingi cha kupimia utoshelevu wa
vitabu hivyo.
ZOEZI 4.1
(a) Chagua shabaha yo yote ya elimu ya kitaifa, na kisha ueleze
jinsi ufundishaji wa Kiswahili shuleni unavyoweza kuchangia
katika ufanikishaji wa shabaha hiyo.
(b) Eleza umuhimu wa silabasi katika utaratibu wa kufundisha.
4.2 Maazimio Ya Kazi.
Katika sehemu iliyotangulia hapo mbeleni tulizungumza juu ya silabasi kama
kimojawapo cha vyombo muhimu katika utekelezaji wa kazi ya kufundisha. Pamoja na
kuwa na silabasi ni lazima mwalimu awe na chombo kingine; na chombo hiki ni
maazimio ya kazi.
Je, maazimio ya kazi ni nini? Na nini umuhimu wake katika taaluma ya uwalimu?
Maazimio ya kazi hutayarishwa kutokana na silabasi. Kwa hivyo ili uweze
kufaulu kutayarisha maazimio ya kazi yanayofaa ni lazima kwanza uwe na ufahamu
mzuri wa silabasi ya somo linalohusika. Maazimio ya kazi ni mpangilio wa mada ambazo
wewe kama mwalimu unaazimia kufundisha katika mfululizo wa vipindi maalum wakati
wa msimu fulani wa masomo. Msimu wa masomo huchukua mwaka mzima ambao
hugawanyika katika mihula mitatu. Na muhula wa masomo huwa na karibu wiki kumi na
tatu hivi. Maazimio ya kazi hutayarishwa kwa kuzingatia mpangilio wa mambo haya.
Wakati wa kutayarisha maazimio ya kazi unadondoa kutoka silabasi mada mbalimbali
ambazo unatarajia kufundisha katika muda fulani. Baada ya kuzidondoa mada hizo
unazivunjavunja katika sehemu ndogondogo kurahisisha ufunzaji wake kwa ufahamu
rahisi. Kisha inakubidi kuzipanga kwa mfuatano wa kimantiki, ukitanguliza kwa mfano
mada zisizo ngumu na kuziweka zile ngumu baadaye.
Kwa ufupi, utayarishaji wa maazimio ya kazi unajishughulisha na uteuzi wa
mada, vipengele vya mada, ufafanuzi wa malengo, uteuzi wa kazi ya wanafunzi pamoja
na vifaa vya kufundishia. Vile vile unajishughulisha na makadirio ya muda ambao
utahitajika kukamilisha ufundishaji wa mada mbalimbali. Muda unaohitajika lazima
ukadiriwe kulingana na kiwango cha ugumu wa mada inayohusika pamoja na upana
wake.
Licha ya kuwa na silabasi, unahitaji kuwa na vitabu vya somo la Kiswahili wakati
wa kutayarisha maazimio ya kazi. Hivi vitakusaidia katika utaratibu wa kuteua kazi na
mazoezi ya kushirikisha wanafunzi ili kufanikisha malengo yaliyowekwa. Silabasi inataja
tu yale yanayohitajika kufundishwa. Ni wajibu wako kama mwalimu kuamua jinsi ya
kufundisha mambo hayo na kuwashirikisha wanafunzi wako. Hapo ndipo vitabu vya
somo la Kiswahili vinapoweza kukusaidia.
28
ZOEZI 4.2
Je, maazimio ya kazi yana umuhimu gani, na yana faida gani
kwako kama mwalimu? Hebu fikiria kwa makini swali hili na ujaribu
kulijibu mwenyewe kabla ya kuendelea na maelezo yafuatayo.
4.3 Umuhimu Wa Maazimio ya Kazi.
Kwa upande wako kama mwalimu maazimio ya kazi yanakusaidia kutambua
kiasi cha kazi ambayo utakabiliana nayo wakati ujao. Kupitia mpangilio wa kazi unajua
mpangilio wa vipindi utakavyofundisha wakati fulani wa muhula pamoja na mambo
ambayo utayatilia mkazo katika vipindi tofauti. Kwa kurejelea mpangilio huo
unaoonyeshwa katika maazimio ya kazi unaweza kupanga mapema kwa wakati unaofaa
mikakati ya kutumia kukabiliana na uendeshaji wa vipindi vyako. Unaweza kuamua juu
ya vifaa vya kufundishia vinavyohitajika, kuvitafuta na kuvipanga kwa wakati unaofaa
kabla muda wa kufundisha haujawadia. Ikiwa una mada fulani ambazo unahitaji kujua
zaidi juu yake unaweza kuzifanyia utafiti mapema ili usihangaike sana wakati wa
kufundisha unapofika. Vile vile maazimio ya kazi ni chombo muhimu ambacho kinaweza
kukusaidia kuhakikisha kwamba mada za somo lako zinapangwa kwa mtiririko bora
kulingana na jinsi zinavyohusiana na kuingiliana. Hali kadhalika yanakuwezesha
kujitathimini na kuhakikisha kwamba ufundishaji wako unaenda sambamba na masharti
ya silabasi na kuzingatia yanayotarajiwa kuzingatiwa katika kiwango kinachohusika na
kwa muda unaofaa.
Kwa upande mwingine, maazimio ya kazi yanaweza kutumiwa kama
kumbukumbu ya kazi kwako binafsi, pamoja na kwa mwalimu mwingine ambaye
pengine huenda akalazimika kuchukua mahali pako. Katika hali kama hii mwalimu mpya
atakuwa na kielelezo cha kumsaidia kuendelea na kazi iliyoanzwa na mwalimu
mwenzake. Hali kadhalika, maazimio ya kazi ni kifaa bora cha marejeleo wakati wa
kutayarisha kazi ya kutathimini maendeleo ya wanafunzi mwishoni mwa msimu wa
masomo.
Zaidi ya haya, ni chombo mwafaka kinachoweza kutumiwa na wakaguzi pamoja
na wasimamizi wa elimu wakati wanapotaka kufuatilia na kutathimini utendaji kazi wa
mwalimu. Vile vile maazimio ya kazi yanahitajika wakati wa kutayarisha mpango wa
kipindi. Baadhi ya mambo yanayowekwa katika mpango wa kipindi hudondolewa kutoka
maazimio ya kazi.
4.4 Muundo wa Maazimio Ya Kazi
Siyo lazima muundo wa maazimio unaotumiwa na waalimu uwe unafanana.
Unaweza kubadilika kutoka shule moja hadi nyingine. Hata hivyo yapo mambo ya
29
kimsingi ambayo ni lazima yashirikishwe katika maazimio yo yote ya kazi. Mambo hayo
yanaweza kupangwa katika vipengele vifuatavyo:
(i) Madhumuni ya muhula
(ii) Mwezi
(iii) Juma / Wiki
(iv) Kipindi
(v) Mada / Yaliyomo
(vi) Madhumuni / Malengo ya kipindi
(vii) Mazoezi / Kazi ya wanafunzi
(viii) Vifaa / Marejeleo
(ix) Maoni
Kwa kawaida msimu wa masomo unagawanyika katika mihula mitatu: muhula wa
kwanza, wa pili, na wa tatu. Maazimio ya kazi inafaa yatayarishwe kwa kuzingatia
mfuatano wa mihula, kila muhula ukiwa na maazimio yake. Kwa hivyo unapotayarisha
kazi ya muhula ni lazima uonyeshe maazimio yanayohusika ni ya muhula gani.
Pamoja na hayo, kila muhula inafaa ufafanue madhumuni ya ujumla ambayo
unatarajia kutimiza katika muhula unaohusika. Ni kutokana na madhumuni hayo ndipo
baadaye unapoweza kupata madhumuni maalum ya vipindi.
Kuhusu mwezi, unachohitaji kutaja ni mwezi wa kufundishia. Kwa mfano, kama
ni muhula wa kwanza, mwezi unaweza kuwa wa kwanza (Januari), wa pili (Februari), au
wa tatu (Machi). Kwa sababu mwezi wenyewe hugawanyika katika majuma/ wiki, inafaa
pia kuonyesha ni wiki gani katika mwezi ambapo unapanga kufundisha jambo fulani. Ni
vizuri pia uonyeshe ni kipindi cha ngapi wiki hiyo. Kwa hivyo kabla ya kutayarisha
maazimio ya kazi ni lazima uchunguze katika ratiba ya masomo ya shule ili ujue idadi ya
vipindi ambavyo unatarajiwa kufundisha kila wiki katika somo lako. Kwa kawaida
vipindi vya Kiswahili huwa ni vitano kila wiki lakini vinaweza vikawa vingi au vichache
zaidi kulingana na mpango wa shule.
Mada ni kiini cha somo au funzo muhimu katika kipindi fulani. Kwa mfano, mada
inaweza kuwa: Insha ya methali. Kama hiyo ndiyo mada ya kipindi chako inakubidi pia
ujiulize kile ambacho unatarajia wanafunzi wafanye kuhusu mada inayohusika. Tuseme,
kwa mfano, kwamba unataka wanafunzi wako waandike insha inayobainisha ukweli wa
methali fulani. Ni lazima ueleze jambo hili kwa kauli maalum; na unapofanya hivyo
utakuwa unatoa lengo la kipindi.
30
ZOEZI 4. 3 B
Je, unaweza kuandika lengo mwafaka la kipindi kutokana na
mada hii?
Pamoja na kufafanua malengo / madhumuni maalum ya kipindi ni lazima
upendekeze kazi ya kushirikisha wanafunzi wakati kipindi cha somo kinapoendelea. Kazi
ya kushirikisha wanafunzi ni lazima ihusiane na mada inayohusika pamoja na malengo
yaliyowekwa. Kazi yenyewe inalenga kuchangia katika utekelezaji wa malengo
yaliyofafanuliwa. Wakati mwingine kazi hii hujulikana kama enabling objectives kwa
Kingereza. Ni kupitia mazoezi haya / kazi hii ndipo malengo yanayotarajiwa kufikiwa
yanapoweza kutimizwa.
Hali kadhalika, unapotayarisha maazimio ya kazi unahitaji vifaa ambavyo huenda
ukavitumia wakati wa kufundisha. Hivi navyo vimetengewa nafasi yake katika muundo
wa maazimio ya kazi.
Sehemu nyingine muhimu ni ile ya maoni. Katika sehemu ya maoni unapaswa
kutoa maelezo kuhusu jinsi mada fulani ilivyofundishwa. Unaeleza jambo lo lote ambalo
huenda lilitokea na kuathiri utekelezaji wa mpango wako. Kila unapoandika maoni
kuhusu kipindi cha somo huwa unajitathimini utendaji kazi wako. Maoni unayoandika
yanalenga kukusaidia unapojiandaa kwa vipindi vitakavyofuata baadaye. Ikiwa kwa
mfano, kipindi chako kilikuwa cha kufana, inafaa ueleze mambo ambayo yalichangia
kukifanikisha. Hali kadhalika, ikiwa kipindi hakikufaulu kama ilivyotarajiwa inafaa
uonyeshe hatua unazopanga kuchukua ili kurekebisha hali. Kwa hivyo, ni lazima utilie
maanani sana mambo unayoandika kama maoni
31
MFANO WA MAAZIMIO YA KAZI
MUHULA: 1 KIDATO I
Madhumuni/ Malengo: Kufikia mwisho wa muhula wanafunzi wataweza : (1) Kukuza kipawa cha kusikiliza kwa makini na kusoma kwa ufahamu.
(2) Kusikiliza na kuongea kwa matamshi bora.
(3) Kuzingatia sarufi bora na matumizi ya maneno ya aina mbali mbali.
(4) Kuandika insha fupi zenye ukamilifu wa mawazo
MWEZI JUMA KIPINDI YALIYOMO MUDHUMUNI/ MAZOEZI / KAZI YA VI
MALENGO WANAFUNZI VI
February 1 1 Ufahamu Wanafunzi wasikilize Kusikiliza hadithi. Na
2004 Sikizi/ Fasihi kwa makini na kujibu Kutaja hoja muhimu had
Simulizi maswali ya ufahamu katika hadithi hiyo. nya
Kusoma hadithi. ma
Kueleza msamiati
mgumu.
Kujibu maswali ya
ufahamu.
Kutumia maneno
mapya katika sentensi
2 Matamshi/ Wanafunzi watambue na Kusikiliza. Na
maneno kuzingatia matamshi bora Kunakili makosa ya Ta
yanayotatani Wapambanue sauti kimatamshi (Ta
sha zinazokaribiana yanayofanywa na 18/
kimatamshi kimatamshi wenzao.
Kusoma kwa sauti
Kujadiliana katika
vikundi.
Kutamka maneno.
Kutunga sentensi.
Kujibu maswali ya
ufahamu n.k…
MWEZI JUMA KIPINDI YALIYOMO/
MADHUMUNI/
MAZOEZI/ KAZI
VITA
MADA MALENGO YA WANAFUNZI VIFA
3 Kuandika Insha Wanafunzi waandike Kuangalia picha Picha
insha fupi zinazoonyeshwa na zinazo
isiyopungua kurasa mwalimu. matum
nne kuhusu matumizi Kutunga sentensi mbali
ya maji nyumbani. juu ya picha hizo. ya ma
Kuigiza vitendo maish
kadhaa vinavyohusu
matumizi ya maji.
Kueleza mambo
yanayoigizwa n.k…
4 Msamiati/ Maneno Wanafunzi watunge Kutaja maneno
siku.
32
yenye maana zaidi sentensi kubainisha
yenye maana zaidi Picha
ya moja (Panda) maana tofauti za neno ya moja. ya had
panda.
Wataje maneno
mengine yenye
maana zaidi ya moja
na kuyatunia katika
sentensi tofauti.
Kuangalia picha.
Kutunga sentensi
juu ya picha hizo.
Kusoma nakala.
Kutaja maana za
neno panda
zinazojitokeza
katika kifungu cha
taarifa
kinachohusika.
Kutunga sentensi
Kujibu maswali ya
ufahamu.
MWEZI JUMA KIPINDI YALIYOMO/
MADHUMUNI/
MAZOEZI/
VITA
MADA MALENGO KAZI YA VIFA
WANAFUNZI
February 5 Sarufi/ Ngeli ya 5/6 Wanafunzi waweze Kuangalia picha. Kadi y
2004 ( li-, ya- ) kutumia majina ya Kuulizana na Nakal
ngeli ya 5/6 katika kujibu maswali hadith
sentensi wakitumia juu ya picha. “Kijan
viambisho mwafaka Kutumia majina Mapen
vya sifa na viarifa. ya 5/6. ( li-, ya- ) Mafun
Kusoma hadithi. Kiswa
Kugeuza katika
umoja na wingi
majina ya 5/6.
Kutunga sentensi.
Kujibu maswali
ya ufahamu.
u.k 8
33
Katika mfano wetu tumeonyesha mpangilio wa vipindi vya muda wa wiki moja tu
ya kwanza. Kwa kufuata mfano huu unaweza kuendelea kuonyesha mpangilio wa vipindi
katika wiki ya pili, tatu na nne. Unapounganisha mpangilio wa vipindi katika wiki moja
hadi nyingine kwa miezi kama mitatu hivi, utaishia kwa kupata maazimio ua muhula
mmoja. Kwa sababu tumezingatia wiki moja tu, kuna mambo mengi ambayo
hayakuonyeshwa katika mpangilio wetu wa kazi. Mara kwa mara, kwa mfano, unahitaji
kuwapatia wanafunzi kazi ya kutathimini maendeleo yao. Na mwishoni mwa muhula,
wanafunzi watahitajika kufanya mtihani wa muhula. Mambo hayo yote unashauriwa
kuyaonyesha katika maazimio ya kazi.
ZOEZI 4.3 C
Chagua kidato cho chote unachotarajia kufundisha katika muhula
fulani. Ukirejelea silabasi ya Kiswahili pamoja na vitabu vya
Kiswahili vinavyopendekezwa kwa kidato kinachohusika, andaa
maazimio ya kazi ya wiki moja. Kisha mwonyoshe mwalimu
mwenzako kazi hiyo na umwombe aikosoe kazi yako.
4.5 Mpango wa Kipindi.
Mpango wa kipindi ni nini? Na una umuhimu gani kwako kama
mwalimu?
Mpango wa kipindi unatayarishwa kutokana na maazimio ya kazi.
Unapotayarisha mpango wa kipindi huwa unaonyesha kile unachotarajia kufundisha
katika muda wa kipindi fulani cha somo au vipindi (kama viwili hivi) na jinsi
unavyotarajia kuukabili ufundishaji wake. Kuwa na mpango wa kipindi ni kwa maana
sana kwa sababu unakupa uwezo wa kuendesha somo ukiwa na mwelekeo maalum
pasipo kubabaika. Mpango wa kipindi ni kama ramani ya barabara inayokuonyesha njia
tofauti unazopaswa kufuata ili kufika vizuri mwisho wa safari yako. Kwa kuzingatia
utaratibu wa mpango wa kipindi mwalimu anakuwa na uhakika kwamba wanafunzi
wanashirikishwa na kushughulikiwa kwa njia inayofaa kwanzia mwanzo wa kipindi hadi
mwisho wake.
34
Kama vile kuhusu maazimio ya kazi, utayarishajui wa mpango wa kipindi nao pia
una masharti yake ambayo unawajibika kutimiza. Kwa ufupi masharti hayo yanahusu
vipengele vifuatavyo unavyoshauriwa kuonyesha katika kila mpango wako wa kipindi
cha somo:
(i) Mada
(ii) Madhumini / Malengo
(iii) Yaliyomo
(iv) Mazoezi / Kazi ya wanafunzi
(v) Marejeleo / Vifaa
(vi) Muda
35
Mpangilio wa vipengele hivi unaonyeshwa katika mfano wa mpango wa kipindi
ufuatao
MFANO WA MPANGO WA KIPINDI
SCHOOL: BIAFRA Kidato 1A
Mada: Kuandika / Insha Wakati 11.00-12.00
MADHUMUNI (MALENGO): Kufikia mwisho wa kipindi wanafunzi
. wataandika hadithi ya maneno 200 hivi iliyo na:
(a) matukio yanayoenekana kama yametokea kweli
(b) mifano maridhawa.
(c) msamiati wa kuvutia na kumalizika hivi: kuona
vile tulimpigia makofi mwenzetu kumshangilia
kwa uhodari wake.
MUDA YALIYOMO MAZOEZI/ KAZI YA
KUSHIRIKISHA WANAFUNZI
MAREJEREO
VIFAA
dak 5 Utangulizi:
maelezo ya maneno
rinda,
tiara,
kujiuzulu,
pengo
Wanafunzi wangalie mwalimu
akichora picha ya mama mnene na
tiara ubaoni. Wasikilize maelezo ya
mwalimu.
(i). Picha ya
mama
akifukuzwa na
mlinzi
(ii) Mchoro
wa tiara
dak 15 Mwili:
Hadithi ya ‘Rinda
lapeperuka kama
tiara’
Wanfunzi wataisoma hii hadithi kila
mmoja kimya kimya. Kisha
wataandika katika vikundi sababu
zote zilizofanya hii hadithi ipendeze.
Nakala ya
hadithi “Rinda
lapeperuka
kama tiara’ dak 10 Yanayopendeza
- matukio kama
ya kweli
- mifano
- msamiati wa
kuvutia
Wanafunzi wamwongoze mwalimu
akiandika ubaoni yote yale
yanayopendeza:
Kama kweli Mifano Msamiati
Makadara mbio za umati
Nairobi hatua kuinua mkwaju
ratili mia chache aliamuru
mbili kortini kukanyaga
hatua kama one, two akaamua
kumi hivi n.k. mama watu wa hivi
mlinzi hivi
mama, mama hakuwa
na wasi wasi
pengo
lilipanuka.
dak 10 Tamati
Kazi ya kuandika
hadithi
Wanafunzi waaandike hadithi zao
kufuatana na mfano uliotolewa.
Jaribio la hadithi zao liwe taayari
juma lifuatalo.
Daftari zao za
kazi
36
4.6 Vipengele vya Mpango wa Kipindi
Kila mojawapo ya vipengele vilivyo katika mpangilio wa kipindi kina umuhimu
wake maalum. Tutajaribu kueleza umuhimu huo kwa ufupi.
Mada
Kila kipindi lazima kiwe na jambo maalum ambalo kinalenga kulishughulikia na
kulitilia mkazo. Jambo hilo ambalo hujitokeza kama kiini cha kipindi ndilo hujulikana
kama mada. Kwa hivyo, kwa kila kipindi cha somo ambacho unafundisha ni lazima
uamue juu ya jambo muhimu ambalo litatawala mkondo wa mafunzo yako. Mambo yote
ambayo utayashughulikia darasani wakati wa kipindi yalenge kufanikisha ufafanuzi wa
mada yako kuu. Katika mpango wa kipindi uliotolewa kama mfano mada ni Insha; na
yale mambo yote ambayo yanapendekezwa kuonyeshwa na mwalimu pamoja na yale ya
kuwashughulisha wanafunzi yana lengo la kuandaa wanafunzi kwa zoezi la kuandika
insha.
Mada za kushughulikia katika vipindi vyako vya somo unazipata kutoka
maazimio yako ya kazi. Umuhimu wa kutaja mada katika mpango wa kipindi ni kwamba
mada inatoa, kwa kiasi fulani, mkutadha wa mafunzo yako na kukuongoza kuhusu
maenezi yake.
Madhumuni / Malengo.
Kwa kawaida, wakati unapofunga safari, huwa huamki kwa ghafla na kwenda
binvu bila mwelekeo maalum. Ikiwa utafanya hivyo, safari inaweza ikaishia kwa
kuhatarisha maisha yako au kwa kutokuwa na faida yo yote.
Taaluma ya kufundisha inaweza kufananishwa na ufungaji wa safari. Kama vile
msafiri anavyopaswa kujua kule anakoelekea kabla hajaanza safari yake, ndivyo pia nawe
kama mwalimu unavyopaswa kujua mwelekeo wa somo lako kabla hujaanza kufundisha.
Na njia mojawapo ya kujua mwelekeo huo ni kuwa na madhumuni / malengo ya kipindi.
Lengo au madhumuni ya kipindi ni kauli maalum inayofafanua kile ambacho
mwanafunzi anatarajiwa kufanya kufikia mwisho wa kipindi fulani cha somo. Matarajio
hayo ndiyo yatakuwa kama dira ya kukuongoza wakati wa kuendesha somo lako, na
kuhakikisha kwamba unafuata utaratibu unaofaa. Mara nyingi vipindi vya lugha
vinaendeshwa ovyo ovyo na kukosa kuwa na manufaa kwa wanafunzi kutokana na
ukweli kwamba waalimu huwa wanafundisha bila kuwa na lengo wazi
wanalolishughulikia. Katika hali kama hiyo zoezi la kufundisha linakuwa kama mchezo
wa bahati nasibu.
Kwa upande mwingine, lengo ni kielelezo bora ambacho kinaweza kutumiwa
kama kigezo cha kupimia kufaulu au kutofaulu kwa somo. Baadaya kipindi fulani, kwa
mfano, utarejelea lengo lako uliloweka wakati unapotunga maswali ya kutahini
wanafunzi juu ya kiini cha somo kinachohusika.
37
ZOEZI 4.4 A
Kwa maoni yako ni masharti gani ambayo yanapaswa
kuzingatiwa wakati wa kufafanua lengo la kipindi? Jibu
swali hili kabla ya kuendelea na maelezo yafuatayo.
Miongoni mwa masharti ambayo unapaswa kuzingatia wakati unapofafanua lengo
la kipindi ni pamoja na yafuatayo:
Kuhakikisha kwamba lengo lina uwiano na mada inayohusika.
Lifafanuliwe hivi kwamba linaweza kutimizika katika muda uliopo wa kipindi
cha somo.
Lazima lifafanuliwe kinaganaga kwa viarifa vinavyorejelea vitendo vilivyo
wazi.
Liegemee upande wa mwanafunzi na wala siyo upande wa mwalimu.
Litaje wazi wazi kile kinachotarajiwa kufanywa na mwanafunzi kufikia
mwisho wa kipindi.
Ni lazima lijikite katika maenezi ya stadi maalum pamoja na kuwa na kipimo / kikomo fulani cha utekelezaji.
Je, ina maana gni kusema kwamba lengo ni lazima liwe na uwiano na mada?
Kauli hii inamaanisha kwamba lengo linapaswa kuwa na uhusiano wa kimantiki na kiini
au wazo kuu la kipindi. Lijishughulishe na mambo ambayo hayana uhusiano wo wote na
wazo kuu linalotarajiwa kuzungumziwa katika kipindi. Kwa mfano wakati wa kipindi cha
somo la fasihi kama unazungumzia wahusika na sifa zao katika kitabu fulani, utakosea
kutayarisha lengo ambalo badala ya kushughulikia kutaja na kueleza sifa za wahusika
fulani, litawataka wanafunzi kufafanua na kutoa mifano ya tamathali mbali mbali za
usemi.
Kwa upande wa muda wa kipindi, unapofafanua lengo ni lazima utilie maanani
muda utakaohitajika kutekeleza lengo hilo. Lisiwe lengo ambalo haliwezi kutimizika
katika muda uliyowekwa au ambalo linahitaji muda kidogo zaidi kuliko ule uliyowekwa.
Kwa hivyo, unaweza kuwa na lengo moja au zaidi ya moja kulingana na kiasi cha muda
ulio nao.
Viarifa vinavyorejelea vitendo wazi ni viarifa vya namna gani? Ni vipi kwa
mfano, kati ya viarifa vifuatavyo vinaweza kuelezwa kuwa vinarejelea vitendo wazi?
Kutaja, kujua, kutoa mifano, kufahamu, kueleza maana, kufurahia, kuthamini…..? Na
vipi kati ya viarifa hivi vinafaa kutumika katika ufafanuzi wa lengo la kipindi cha somo?
Ni vipi havistahili kutumika, na kwa nini?
Hivi vifuatavyo ndivyo havistahili kutumiwa: kujua, kufahamu, kufurahia,
kuthamini. Havistahili kwa sababu vinaashiria vitendo ambavyo utimilifu wake hauwezi
kutambulika moja kwa moja kwa njia iliyo wazi. Havina kielelezo cho chote ambacho
kinaweza kusaidia kutambua kama mambo vinayoashiria yametimilika. Kwa mfano,
ukitaka kutambua ikiwa mwanafunzi anafurahia au anathamini jambo fulani utahitaji
kuchunguza mwenendo wake na vitendo vyake vya nje. Kwa upande mwingine, viarifa
38
vifuatavyo vinafaa kutumika: kutaja, kutoa mifano, kueleza maana. Utimilifu wake
unaweza kutambulika moja kwa moja bila shida. Ukipanga, kwa mfano, kwamba
wanafunzi wataeleza maana ya dhana fulani na kutoa mifano ya kuonyesha dhana hiyo,
unaweza kutambua moja kwa moja ikiwa wametekeleza matarajio yako au la.
Shule ni mahali pa kumsaidia mwanafinzi kujiendeleza kimasomo, na mambo
yanayotendeka darasani yanakusudia kuchangia ufanisi wa jambo hili. Kwa hivyo wakati
unapotayarisha mpango wa kipindi ni lazima uyape kipaumbele mahitaji ya mwanafunzi.
Ili hukakikisha kwamba mahitaji ya mwanafunzi yanazingatiwa kikamilifu wakati wa
kipindi cha somo unashauriwa kufafanua lengo la kipindi kwa kumshirikisha
mwanafunzi kama mhusika mtendaji mkuu. Sababu mojawapo ya kufanya hivi ni
kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapewa fursa ya kushughulika kikamilifu katika
kipindi. Kwa mujibu wa sharti hili, kwa mfano, utakuwa umekosea kuandika lengo kama
lifuatalo: Kufikia mwisho wa kipindi mwalimu ataeleza maana ya “ubwege” na kutoa
mifano ya kutilia maki maelezo yake kutoka tamthilia ya Amezidi.
Kosa la lengo hili ni pale ambapo mwalimu ametumiwa badala ya mwanafunzi.
Lengo limeegemea upande wa mwalimu badala ya mwanafunzi, jambo ambalo linaenda
kinyume na maelezo yaliyotolewa kuhusu ufafanuzi wa lengo la kipindi.
Unapojiandaa kufundisha huwa unatarajia kwamba malengo unayojiwekea
yatafikiwa katika muda mahsusi. Unapoandika lengo la kipindi ni bora urejelee muda huo
unaotarajiwa kutumiwa ili kutimiza lengo lililowekwa. Kauli isemayo kwamba lengo
litaje kile kinachotarajiwa kufanywa na wanafunzi kufikia mwisho wa kipindi
inazungumzia jambo hili. Kwa kawaida, somo la Kiswahili linachukua muda wa kipindi
kimoja; na ukiwa zaidi huwa hauzidi vipindi viwili mfululizo. Katika mfano wa lengo
ambao ulitolewa hapo awali, unaweza kuona kwamba sharti hili limezingatiwa kulingana
na maneno yanayotumiwa katika sehemu ya utangulizi. Maneno hayo yanataja wakati
ambapo lengo linalohusika linatarajiwa kutekelezwa. Ni muhimu kwako kama mwalimu
kuzingatia jambo hili kwa sababu litakuwa kumbusho kwako kuhusu kiasi cha muda ulio
nao usije ukapanga kazi ambayo hailingani na muda wa kufundishia.
Je, tunamaanisha nini kusema kwamba lengo ni lazima lijikite katika maenezi ya
stadi maalum ya lugha? Kama tujuavyo, lugha ni somo ambalo limejikita sana sana
katika umilisi na uimarishaji wa stadi mbali mbali za mawasiliano. Kutokana na ukweli
huu, unashauriwa kuona kwamba unapotayarisha lengo la kipindi unatilia maanani stadi
fulani ya lugha. Na wakati wa kufundisha huna budi kushirikisha wanafunzi wako katika
mazoezi yanayoambatanisha stadi hiyo.
Jambo jingine ambalo ni muhimu katika lengo la kipindi ni kipimo / kikomo cha
utekelezaji. Hiki ni kama kiwango cha ufanisi ambacho unatarajia mwanafunzi ataweza
kufikia. Ni kigezo ambacho unaweza kutumia kutathimini mafanikio ya wanafunzi
pamoja na uwezo wao kuhusu mada iliyoshughulikiwa. Tukirejelea mada ya ubwege,
kwa mfano, tunaweza kuandika lengo kama lifuatalo: Kufikia mwisho wa kipindi
mwanafunzi ataeleza kwa kuandika maana ya ubwege na kutoa, angalau, mifano minne
ya kutilia maki maelezo yake kutoka tathimilia ya AMEZIDI.
Kulingana na matarajio ya lengo hili, kuna idadi ya mifano ambayo mwanafunzi
anatakiwa kutoa. Idadi hii inatoa kielelezo cha utendaji kinachotarajiwa kwa upande wa
mwanafunzi kama ushahidi kwamba amefikia kiwango kinachotarajiwa. Kila
mwanafunzi ambaye angetimiza idadi ya mifano iliyowekwa ingesemekana kuwa
amefikia kile kiwango kinachohitajika. Lengo hili pia limetimiza masharti mengine
39
yaliyotajwa katika maelezo kuhusu utayarishaji wa lengo la kipindi kwa jumla. Kwa
mfano, limeeleza wazi wazi jinsi mwanafunzi anavyotarajiwa kueleza maana ya ubwege.
Limejikita katika maenezi ya stadi ya uandishi. Hata ingawa wakati wa kipindi wanafunzi
wanaweza kushiriki katika mazungumzo, ni wazi kulingana na lengo kwamba
kipaumbele katika kipindi kitapewa stadi ya uandishi.
ZOEZI 4.6 B
Onyesha ikiwa, kwa maoni yako malengo
yafuatayo yemefafanuliwa kwa utaratibu unaofaa kwa
kuweka alama ( X) katika nafasi iliyoachwa pembeni
mwa lengo husika.
Kufikia mwisho wa kipindi SAWA SI SAWA
1. Wanafunzi watafahamu sifa za shairi.
2. Wanafunzi watatoa, angalau mifano mitatu ya
tasfida kutoka kifungu cha habari
watakachosoma.
3. Wanfunzi watajua maana ya majina ya majazi.
4. Nitafundisha maneno yenye maana zaidi ya moja
5. Wanafunzi watafafanua maana ya moja kati ya
methali zifuatazo na kuandika insha ya maneno
kama 500 hivi ambayo inabainisha ukweli wa
methali hiyo.
Nyani haoni kundule.
Fimbo ya mbali haiui nyoka
Nazi haishindani na jiwe.
6. Wanafunzi watandika insha juu ya
mmomonyoko wa udongo
40
ZOEZI 4.6 C
Chagua mada zo zote nne kutoka silabasi ya Kiswahili
zinazopendekezwa kufundishwa katika kidato fulani. Kwa
kuzingatia masharti ya ufafanuzi wa malengo ya kipindi,
andika lengo mwafaka linaloambatana na mada inayohusika.
Yaliyomo
Kila unapochagua mada ya kufundisha katika kipindi fulani cha somo huna budi
kuamua ni mambo gani ambayo unapanga kuzungumzia au kugusia juu ya mada hiyo.
Maelezo ya vitengo vya ndani vya mada ndiyo hujenga yale yaliyomo katika kipindi
fulani. Kwa maneno mengine, yaliyomo ni mgawanyiko wa vijisehemu vidogo vidogo
vya mada inayohusika. Ni muhimu kwako kama mwalimu kuonyesha mgawanyiko huo
kwa sababu unapofanya hivyo unapata mwongozo kuhusu mambo mbali mbali ambayo
utagusia katika hatua tofauti za kipindi chako cha somo. Unapata nafasi ya kufikiria juu
ya mambo hayo mapema kabla ya somo; na wakati wa somo unapata nafasi ya kuendesha
somo lako kwa mtiririko unaofaa bila kuchanganyikiwa kimawazo wala kuwakanganya
wanafunzi wako.
Tuchukue mfano wa mada kama Ushairi katika kipindi cha somo la fasihi. Baada
ya kufafanua lengo kuambatana na mada hii ni wajibu wako kuvunjavunja na
kuigawanya mada yako katika vipengele tofauti ambavyo unatarajia kugusia katika hatua
tofauti za kufundisha somo. Inakubidi uonyehse ni jambo gani litashughulikiwa katika
hatua ya utangulizi, ya mwili/ upanuzi, na tamati/ hitimisho. Katika utangulizi, kwa
mfano, unaweza kuwa na yaliyomo kama vile:
(i) Marejeleo ya kipindi kilichotangulia.
(ii) Tanzu za fasihi andishi.
Na katika sehemu ya mwili wa kipindi unaweza kuwa na yaliyomo kama vile:
(i) Tofauti za ushairi na fani nyingine za fasihi.
(ii) Aina za mashairi
(iii) Sifa za kimsingi za shairi n.k……
Katika sehemu ya tamati (utamamatisho) miongoni mwa mambo ambayo
unaweza kupendekeza ni kama vile:
(i) Muhtasari wa somo.
(ii) Kazi ya zoezi n.k…….
Mazoezi ya /Kazi ya Wanafunzi
Mazoezi ya wanafunzi yanaonyesha mambo ambayo wanafunzi
watajishughulisha nayo katika kila hatua ya kipindi cha somo. Ni lazima uhakikishe
kwamba mazoezi ambayo yanapendekezwa yana uhusiano na yaliyomo yanayohusika.
Pia unapaswa kutoa mazoezi ya aina tofauti. Mazoezi ya wanafunzi yanatofautiana kabisa
na yaliyomo pamoja na shughuli zako kama mwalimu. Kwa hivyo, usieleze shughuli za
mwalimu katika sehemu ya mpango wa kipindi ambayo inatengwa kwa mazoezi.
41
Kutofanana na yaliyomo, mazoezi ya wanafunzi hufafanuliwa katika vielelezo vya
sentensi, wakati ambapo yaliyomo yanaonyeshwa tu kwa vifungu vya maneno ambayo
hayatowi taarifa kamili. Yaliyomo ni vichwa tu vya yale yanayoshughulikiwa lakini
mazoezi hutaja kikamilifu vitendo vya wanafunzi.
Marejeleo / Vifaa:
Hivi ni vyombo vyote ambavyo utavitegemea katika utekelezaji wa kazi yako ya
kufundisha. Mfano ni kama vile vitabu, vitu halisi, picha, michoro n.k….
Muda:
Unapoandaa mpango wa kipindi ni jambo la busara kuonyesha wakati unaotarajia
kutumia ili kukamilisha hatua tofauti za kipindi chako. Makadirio ya muda ni muhimu
kwa sababu husaidia kuhakikisha kwamba kipindi kinafululiza kwa mwendo unofaa.
HITIMISHO
Somo hili limegusia mambo muhimu ambayo unawajibika kufanya ili kujiandaa
kwa kazi ya kufundisha. Unashauriwa kwamba ni lazima usikose kujihami kwa kuwa na
silabasi, maazimio ya kazi, pamoja na mpango wa kipindi. Vyombo hivi vitatu
vinahusiana na kuathiriana. Silabasi ni chombo ambacho mwalimu hutegemea
anapotayarisha maazimio ya kazi; na ni kutokana na maazimio ya kazi ndipo anatayarisha
mpango wa kipindi. Ni wajibu wako kama mwalimu kuhakikisha kwamba unapata
silabasi ya somo lako mapema ili uichunguze kwa undani na kufahamu vilivyo kile
unachotarajiwa kufanya kulingana na silabasi hiyo. Kisha unaweza kuandaa maazimio ya
kazi ambayo yatakufaa wakati wa kuandaa mipango yako ya vipindi vya somo.
ZOEZI 4.6 D
Ukirejelea mada zo zote tatu kati ya mada nne ulizochagua
katika zoezi 4.6 C, tayarisha mpango kabambe wa kipindi
unaolenga kushughulikia kila mojawapo ya mada hizo.
( ie. mipango mitatu)
42
SOMO LA 5
KUSIKILIZA NA KUONGEA
5.0 Utangulizi.
Kusikiliza na kuongea ni stadi muhimu sana katika utaratibu wa kujifunza na
kufundisha lugha. Pia stadi hizi mbili hutegemewa zaidi katika shughuli za mawasiliano
ya kila siku kuliko Kusoma na Kuandika. Kulingana na wataalamu, kusikiliza na kuongea
vinachukua karibu asilimia 75%, ya shughuli za mawasiliano ya kila siku. Kwa upande
mwingine, kusoma na kuandika vinachukua karibu asilimia 25%. Kwa mujibu wa
wataalamu hao, kusikiliza kwenyewe kunachukua karibu asilimia 45%, hali ambapo
kuongea kunachukua asilimia 30%.
Katika somo hili, tutatoa mapendekezo ya mambo ambayo unaweza kufanya ili kusaidia wanafunzi wako kuendeleza na kuimarisha uwezo wao wa kusikiliza na kuongea
Kiswahili kwa ufahamu.
MADHUMUNI YA SOMO.
Kufikia mwisho wa somo hili utaweza:
Kueleza umuhimu wa kusikiliza na kuongea katika
utaratibu wa kufundisha Kiswahili.
Kupendekeza mbinu mwafaka unazoweza kutumia
kusaidia wanafunzi wenye shida za kusikiliza kwa
ufahamu.
Kupendekeza mbinu tofauti unazoweza kutumia kukuza
uwezo wa wanafunzi wa kujieleza kwa ufasaha wa lugha
na matamshi bora.
5.1 Umuhimu Wa Kusikiliza.
Kulingana na ukweli wa mambo katika shule, kusikiliza na kuongea havitiliwi
sana mkazo katika mfumo wa elimu. Hata mwishoni mwa masomo mitihani inajikita
katika lugha andishi. Kutokana na hali hii, hata ufundishaji wa lugha unaelekea
kuegemea zaidi katika lugha ya uandishi kuliko lugha ya uzungumzi. Ukiwa mwalimu
wa Kiswahili unashauriwa kutofuata mtindo huu wa kufundisha ambao unawanyima
wanafunzi nafasi ya kuidhibiti lugha kikamilifu na kuzimudu mbinu zake zote za
mawasiliano.
Uwezo wa kusikiliza ni muhimu sana katika kipengele cha mawasiliano na
uhusiano wa kibinadamu. Kwa kawaida ni rahisi zaidi kuwasiliana na kuelewana na mtu
mwenye umakinifu wa kusikiliza kuliko yule ambaye anakosa umakinifu. Pia, katika
43
mkutadha wa mazingira ya darasani kusikiliza ni muhimu sana kutokana na ukweli
kwamba mafunzo ya darasani hutegemea sana lugha ya mazungumzo. Ili aweze kufaidika
kutokana na mafunzo hayo, ni lazima mwanafunzi awe na uwezo wa kusikiliza na
kufahamu ipasavyo. Hali kadhalika, kupitia mazoezi ya kusikiliza mwanafunzi anapata
fursa ya kupanua upeo wa msamiati wake pamoja na ujuzi wa sarufi. Kadiri
anavyosikiliza ndivyo anavyozidi kuimarisha ujuzi wake wa msamiati pamoja na sarufi.
Ikiwa unataka wanafunzi wako waimarishe ujuzi wao wa Kiswahili una wajibu wa
kuwashirikisha katika vipindi vya kusikiliza mazungumzo tofauti ya Kiswahili.
Vilevile kusikiliza kunasaidia katika juhudi za kufundisha matamshi. Ili mwanafunzi aweze kutamka vizuri, ni lazima kwanza awe na uwezo wa kupambanua
sauti zinazohusika katika usikizi wake. Bila uwezo huu ataishia kwa kutamka maneno na
kuzungumza kwa namna ambayo inakanganya.
ZOEZI 5.1
Eleza kwa nini watu hujishughulisha na kusikiliza
yale wanayoyasikiliza.
5.2 Kusikiliza Kwa Ufahamu (Ufahamu Sikizi).
Je, ufahamu sikizi unahusu nini? Na ni mambo gani ambayo huenda yakamzuia
mwanafunzi kusikiliza kwa ufahamu?
Ufahamu sikizi ni fani ya lugha ya uzungumzi ambayo kwayo msikilizaji hupokea
ujumbe wa mzungumzaji na kuuambatanisha na maana inayotakikana. Ni fani ambayo
inahusisha utoaji wa ujumbe na upokeaji wake kupitia sauti. Madhumuni hasa ya
kushirikisha wanafunzi katika zoezi la kusikiliza kwa ufahamu ni kuwaelekeza katika
misingi ya kuwawezesha:
Kuwa na umakinifu katika kusikiliza
Kupokea ipasavyo ujumbe unaowalishwa katika mazungumzo
Kuambatanisha ujumbe unaopokelewa na maana sahihi na kuitikia ipasavyo.
Kudhibiti ujumbe unaopokelewa katika kumbukumbu.
Kutambua mambo muhimu na kuyatenganisha na yasiyo muhimu.
Kila moja kati ya mambo ambayo yametajwa lina umuhimu katika ufanisi wa
ufahamu. Mwanafunzi kwa mfano, akiwa mmakinifu atasikiliza kwa uangalifu akitilia
maanani kila jambo linalosemwa. Hatapoteza kwa urahisi mwelekeo wake katika
kusikiliza. Huwa na uwezo wa kujikinga dhidi ya mambo yanayoweza kukatiza usikizi
wake na kutatiza ufahamu wake. Anaweza kutambua uhusiano na mwingiliano kati ya
yanayosemwa pamoja na kufuata vizuri mtiririko wa mawazo katika mazungumzo. Vile
vile anaweza kujihusisha vilivyo na mkondo wa mazungumzo na kuitikia kama
inavyostahili kulingana na hali ya mazungumzo hayo. Kwa kufuatilia mwitiko wa
wanafunzi wewe kama mwalimu unaweza kutambua jinsi mazungumzo yako
yanavyopokelewa. Unaweza kutambua ikiwa mazungumzo hayo yanaibua hisia
zinazostahili au la.
44
Umakinifu ni jambo la kimsingi na ambalo pia husaidia kufanikisha utekelezaji
wa madhumuni mengine yaliyotajwa. Mwanafunzi asipokuwa na umakinifu, kwa mfano,
hawezi kutambua kwa urahisi mambo muhimu na yale yasiyo muhimu. Hawezi pia
kuupokea ipasavyo ujumbe unaowasilishwa na kuuambatanisha na maana inayotarajiwa.
Hali kadhalika hatakawia kusahau yale anayosikiliza. Na ikiwa kufikia mwisho wa zoezi
la kusikiliza atakuwa amesahau yaliyozungumzwa hali hii itaathiri vibaya kiwango cha
ufahamu wake.
ZOEZI 5.2
Jaribu kufananua kwa undani zaidi madhumuni ya zoezi
la ufahamu yaliyotajwa.
5.3 Vizuizi Vya Ufahamu Sikizi.
Je, unaweza kukumbuka wakati wo wote ambapo wewe ukiwa mhusika
msikilizaji umewahi kushindwa kusikiliza kwa ufahamu? Unaweza kukumbuka ni kwa
sababu gani hukuweza kusikiliza kwa ufahamu? Je, unaweza pia kukumbuka wakati
mwingine, ambapo wewe ukiwa mhusika mzungumzaji, wale waliokusikiliza
walishindwa kukusikiliza kwa ufahamu? Chanzo hasa cha hali hiyo kilikuwa nini?
Hali kama hiyo inaweza kutokea na kutatiza kiwango cha ufahamu wa wanafunzi.
Wewe kama mwalimu una wajibu kuelewa matatizo yanayohusika ili uweze
kuhakikisha kwamba wanafunzi wako wanaepukana nayo wakati wanaposikiliza. Kwa
ufupi matatizo haya yanaweza kuainishwa katika makundi yafuatayo:
Chanzo cha habari ( Mzungumzaji)
Msikilizaji
Mazingira
Ujumbe husika
.
Chanzo Cha Habari.
Aghalabu kusikiliza kunaambatana na kuzungumza. Unaposikiliza, ule ujumbe
unaopokea huwa haujitokezi katika ombwe tupu. Unawasilishwa na mtu fulani moja kwa
moja au kupitia chombo fulani cha mawasiliano. Upokezi wa ujumbe unaohusika
unaweza kufanikishwa au kutatizwa na yule anayeutoa au chombo kinachotumiwa
kuwasilisha ujumbe huo. Chanzo cha habari kinaweza kutatiza ufahamu sikizi kwa
sababu kama zifuatazo:
Matamshi mabaya
Uteuzi mbaya wa maneno.
Mpangilio mbaya wa mawazo.
45
Upazaji wa sauti.
Hulka ya mzungumzaji
Wakati unaposikiliza huwa unapokea ujumbe unaowasilishwa na mzungumzaji
kupitia maneno anayotamka. Ikiwa mzungumzaji ana shida ya kimatamshi huenda
akatamka vibaya na kuishia kwa kupotosha maana. Kwa mfano, maneno yafuatayo
yanatakiwa kutamkwa kwa njia tofauti: fua, vua; pua, bua. Ikiwa mzungumzaji ana
shida ya kutofautisha kati ya /f/ na /v/, /p/ na /v/ atachanganya matamshi ya maneno
yenye vitamkwa hivi na kuishia kwa kupotosha maana, jambo ambalo litamfanya
msikilizaji atafsiri ujumbe kwa njia isiyokusudiwa. Tuchukue mfano wa mzazi ambaye
anatoa agizo kama hili kwa mtoto mchanga: “Usisahau kuvua soksi zako kabla ya
kulala”. Kwa sababu ya utiifu wake, mtoto anaweza kuitikia kulingana jinsi anavyoelewa.
Lakini baadaye mtoto huyu atagundua kwamba kitendo alichofanya siyo kile ambacho
kilikusudiwa na mzazi wake wakati alipotoa agizo! Mtoto anashindwa kusikiliza kwa
ufahamu kwa sababu ya matamshi ya mzazi wake. Mfano mwingine wa tatizo la
kimatamshi unahusu ile hali ya kugeuza mfuatano wa vitamkwa katika maneno. Tamthili
ya hii ni maneno haya: karibuni, kaburini, sitini, tisini, kusihi, kuhisi.
Ukichunguza maneno haya utatambua kwamba yana vitamkwa sawa ila tu
mfuatano wa vitamkwa hivyo ndio unatofautiana. Mzungumzaji asipokuwa mwangalifu
huenda akatamka neno lingine badala ya lile alilokusudia na kumfanya msikilizaji
asielewe ujumbe kama inavyostahili.
Jambo lingine ambalo linaweza kumkanganya mwanafunzi na kumfanya asiweze
kusikiliza kwa ufahamu ni uteuzi mbaya wa maneno yanayotumiwa na mzungumzaji
kuwasilisha ujumbe wake. Maneno ni chombo muhimu kinachotegemewa katika
mawasiliano ya lugha. Ikiwa unataka ujumbe wako ueleweke vizuri huna budi kutumia
maneno yanayofaa. Kwa mfano, ikiwa utatumia neno mpunga badala ya mchele
utawakanganya wasikilizaji wako. Kulingana na matumizi ya Kiswahili sanifu kwa
mfano kuna tofauti kubwa kati ya neno sana na zaidi, lakini kuna watu ambao
hawang’amui tofauti kati ya maneno hayo na huwa wanatumia neno zaidi katika
mkutadha ambamo neno mwafaka lingekuwa sana. Ukisema kwa mfano, ‘Nimechoka
zaidi”, badala ya kusema “ Nimechoka sana”, msikilizaji ambaye anaimudu vizuri lugha
ya Kiswahili ataelewa kwamba unalinganisha hali yako ya kuchoka na ya mtu mwingine
au watu wengine ambao pia wamechoka. Kile ambacho ataelewa ni kwamba wewe
umechoka zaidi kuliko wao. Mfano mwingine unahusu matumizi ya –dogo na –chache.
Wapo watu ambao hutumia –dogo badala ya –chache. Usipokuwa mwangalifu unaweza
kupotoshwa na matumizi yao ya neno hilo. Chanzo cha tatizo hili pengine ni kwamba
katika lugha zao za mama dhana ya idadi na ukubwa huwasilishwa na neno moja tu
wakati ambapo katika Kiswahili kila dhana huwasilishwa kwa kutumia neno tofauti.
Kama mzungumzaji ana shida ya kung’amua maenezi ya maana za maneno huenda
akakanganya wasikilizaji wake. Wasipokuwa waangalifu na kufasiri ujumbe kwa
kuzingatia vizuri mkutadha wa matumizi wa maneno yanayohusika wanaweza kushindwa
kuelewa ujumbe ipasavyo.
Wakati mwingine, wanafunzi au wasikilizaji wanaweza kukosa kusikiliza kwa
ufahamu kutokana na hali ya kuudhiwa na mzungumzaji. Ikiwa mazungumzo
yanamwudhi msikilizaji, bila shaka atakosa hamu ya kusikiliza kwa makini, jambo
ambalo litaathiri vibaya hali yake ya ufahamu. Mzungumzaji anaweza kuwaudhi vipi
46
wasikilizaji wake? Anaweza kuwaudhi , kwa mfano kama lugh ayake inachochea hisia za
chuki. Pengine anaweza kuwaudhi kwa kutotumia lugha kwa uangalifu na kuishia kwa
kuwakosea heshima wasikilizaji wake kutokana na mifano anayoitoa kutilia maki
mazungumzo yake. Mifano hiyo inaweza kuwa inawahusu baadhi ya wasikilizaji, na
wanaweza kuyachukulia mazungumzo kama kwamba yanawalenga wao makusudi! Ikiwa
ni hivyo, huenda wakaamua kuyapuza mazungumzo hayo na kutosikiliza.
Kwa hivyo, ni wajibu wako kama mwalimu kuhakikisha kwamba unatilia
maanani hisia za wanafunzi juu ya mambo yanayotumiwa kufundishia ufahamu.
Kitu kingine kuhusu chanzo cha habari ambacho kinaweza kutatiza ufahamu wa
msikilizaji ni upangaji wa mawazo mbaya katika mazungumzo. Ujumbe ambao
unaeleweka kwa urahisi ni ule ambao unawekwa katika muundo maalum wa
kimawasiliano. Wazo kuu la ujumbe huo labainika wazi na ufafanuzi wake unajitokeza
kwa mtiririko bora wa mawazo. Lakini mawazo yakilundikwa ovyo ovyo bila mfululizo
wa kimantiki, msikilizaji anaweza kukanganywa na kushindwa kusikiliza kwa ufahamu.
Itakuwa vigumu kwake kuupokea na kuzingatia vizuri ujumbe unaowasilishwa.
Mawasiliano huwa hayajakamilika kabla ujumbe haujamfikia mhusika mpokezi.
Katika mkutadha wa mazungumzo, mawasiliano hukamilika wakati ambapo msikilizaji
amesikia ujumbe huo. Mzungumzaji akiwa na shida ya kutoa sauti kwa njia ya kusikika
ufahamu nao hautawezekana. Kwa hivyo, wakati unaposhirikisha wanafunzi katika zoezi
la ufahamu sikizi ni lazima uhakikishe kwamba ujumbe unaohusika unawafikia vizuri
wanafunzi wako.
Mara nyingi pia hali na tabia ya mzungumzaji kwa jumla vinaweza kuchangia
kufanikisha au kutatiza ufahamu wa msikilizaji. Ni kweli, nyumba si mlango; lakini pia
ni kweli kwamba bila mlango nyumba huwa haifai kitu. Vile vile kama mlango wa
nyumba haupitiki nyumba yenyewe haina faida! Hulka ya mzungumzaji inaweza
kufananishwa na mlango wa nyumba. Pia ujumbe unaowasilishwa unaweza
kufananishwa na nyumba. Ikiwa mlango wa nyumba unavutia, huenda watazamaji
wakitamani kuingia ndani ya nyumba hiyo wajionee yale yaliyomo. Lakini kama uchafu
umelundikana kwenye mlango ambao nao pia umekaa segemnege watazamaji
hawatakuwa na hamu ya kutaka kuingia ndani ya nyumba hiyo. Matokeo yake ni
kwamba hawataweza kujua vitu vilivyomo ndani ya nyumba. Hali kadhalika, katika
mkutadha wa mazungumzo kama hulka ya mzungumzaji hairidhishi na kuvutia, itakuwa
vigumu kwa wasikilizaji kusikiliza kwa makini. Na matokeo ya utovu wa umakinifu ni
kukosekana kwa ufahamu unaofaa.
Msikizaji:
Kuna mambo ambayo yanaweza kumzuia mtu kusikiliza kwa ufahamu ambayo
chanzo chake ni hali ya msikilizaji mwenyewe. Baadhi ya mambo hayo ni kama vile:
Kutosikiliza kwa dhati.
Usikizi mbaya.
Ufasiri wa maana kwa njia isiyofaa.
Uhakiki wa kupindukia.
Udhaifu katika lugha.
Mtu ambaye anasikiliza kwa dhati anatia bidii katika shughuli hiyo. Hutia bidii
kwa sababu huwa na ari ya kusikiliza; lakini akikosa ari hatajishughulisha kwa bidii. Kwa
47
sababu ya kutokuwa na ari huenda akasikiliza bila umakinifu, jambo ambalo linachangia
hali ya kutofahamu ipasavyo. Atashindwa kufahamu kwa sababu hatashughulikia
kikamilifu yale yanayosemwa. Kwa hivyo, wewe kama mwalimu ukitaka wanafunzi
wako wasikilize kwa dhati na makini ni lazima uwahamasishe na kuhakikisha kwamba
wanaposikiliza wanakuwa na lengo mahsusi la kusikiliza. Hivyo ndivyo wanvyoweza
kusikiliza kwa dhati na kufahamu yasemwayo. Bila kuwa na lengo mahsusi watasikiliza
ili kutimiza mradi tu. Lakini wakielewa vizuri matarajio ya zoezi la kusikiliza
watajishughulisha inavyostahili. Jambo lingine ambalo linaweza kuwafanya wanafunzi
kutosikiliza kwa dhati ni uchovu wa kimwili na kiakili. Ikiwa unataka washiriki kwa njia
inayofaa huna budi kulishughulikia tatizo hili.
Je, na usikizi mbaya ni usikizi wa namna gani? Na unatokana na nini? Mfano
mmoja wa usikizi mbaya ni ile hali ya kutosikia yale yanayosemwa kwa sababu pengine
ya matatizo ya kimaumbile. Mfano mwingine unahusu ile hali ya kushindwa kung’amua
tofauti za kimatamshi kati ya maneno yanayotofautiana kwa misingi ya kimatamshi.
Mwanafunzi akiwa na shida ya namna hii atakumbwa na shida ya kuelewa ipasavyo
wakati wa mazungumzo. Wanafunzi walio wengi wanaweza kukumbwa na tatizo hili
kutokana na tofauti baina ya mfumo wa sauti wa Kiswahili na ule wa lugha zao za mama.
Kwa mfano, kama mwanafunzi hasikii tofauti kati ya maneno yafuatayo, atakuwa na
shida ya kuelewa maana inayokusudiwa maneno haya yanapotumiwa katika
mazungumzo:
doa: ndoa
buni: mbuni
sima: zima
msasi: mzazi
kuku: gugu
mtutu: mdudu
chombo: shombo
chana: jana
fua: vua
pua: bua
Ikiwa maneno haya yangetumiwa hivi kwamba si rahisi kutambua maana
kulingana na mkutadha wa matumizi, mwanafunzi angekanganywa na kuwa na shida ya
kusikiliza kwa ufahamu. Vile vile, mwanafunzi anaweza kushindwa kusikiliza kwa
ufahamu kama hafuati mtindo unaostahili kupata maana ya maneno yaliyo mapya kwake.
Kuna uwezekano kwamba kila neno jipya linapotokea mwanafunzi anasita na kwanza
kufikiria juu ya maana ya neno jipya. Kila anapofanya hivyo huwa anakosa kufuata
kikamilifu mkondo wa mazungumzo. Matokeo ya jambo hili ni kwamba huenda asielewe
ipasavyo kiini cha ujumbe unaowasilishwa.
Kwa hivyo, ni wajibu wa mwalimu kuwahimiza wanafunzi wasijaribu kutafuta
maana ya neno moja moja. Badala yake wajaribu kutambua maana kwa kuzingatia
uhusiano wake na maneno mengine katika mkutadha wa sentensi nzima. Hata kama si
rahisi kutekeleza jambo hili ni bora zaidi kuendelea kusikiliza kuliko kushughulikia
maana ya neno moja tu. Wanafunzi washauriwe kwamba kila wanaposikia neno lo lote
jipya ni vizuri waliandike halafu watafute maana yake baadaye.
48
Je, kwa nini inafaa kuhimiza wanafunzi watafute maana kwa kuzingatia uhusiano
kati ya maneno katika mkutadha wa sentensi nzima?
Kwa kawaida mawasiliano ya lugha hufanyika kwa mtindo wa kutumia maneno
katika vielelezi vya sentensi ambazo kwa msingi wake kila neno hupata maana maalumu.
Tukizungumza kuhusu sifa za lugha tulisema kuwa ni mfumo nasibu. Maana mojawapo
ya kauli hii ni kwamba vipashio mbali mbali vya lugha vimo katika mpangilio maalum.
Mfano mmoja wa vipashio vya lugha ni maneno. Aghalabu maneno hupata maana
kutokana na mwingiliano wake ma maneno mengine katika mkutadha wa sentensi.
Maana yake inageuka kutoka mkutadha mmoja hadi mwingine. Kwa mfano maneno
kama vile piga, kata hupata maana tofauti kutokana na maneno mengine yanayoambatana
nayo katika sentensi. Hata maneno ambayo kwa kawaida huwa na maana iliyo wazi
yanaweza kupata maana isio ya kawaida yakitumiwa katika mkutadha usiyo wa kawaida.
Tuchukue mfano kama vile: kigeugeu, simba, sungura, fisi. Maneno haya yakitumiwa
katika mkutadha usio wa kawaida, msikilizaji inambidi kuzingatia maana yake kwa
mtazamo wa kijamii. Asipofanya hivyo atakosa kuelewa maana inayowasilishwa katika
mazungumzo yanayohusika.
Kizuizi kingine cha ufahamu sikizi ni tabia ya kuhakiki kwa namna ya kupindukia
wakati wa kusikiliza. Kuna wanafunzi ambao hawawezi kujizuia kukosoa mzungumzaji
au ujumbe unaowasilishwa wakati wanaposikiliza. Badala ya kuzingatia ujumbe
wanaweza, kwa mfano kujishughulisha na makosa yanayofanywa na mzungumzaji.
Pengine wanajifanya kuwa wanajua vya kutosha kuhusu mada inayoshughulikiwa katika
mazungumzo. Wanafunzi wa namna hii hawana nafasi ya kusikiliza kwa dhati, na
hatimaye wanashindwa kuelewa kiini cha ujumbe.
Njia mojawapo ya kusaidia wanafunzi wa namna hii ni kuwahimiza wasikilize
kwanza kabla ya kumkosoa mzungumzaji na ujumbe wake. Baada ya kuupokea ujumbe
watakuwa na nafasi bora zaidi ya kukosoa. Hata mzungumzaji mwenye shida ya lugha
anayo maarifa ya maana ambayo hayastahili kupuzwa. Kama walivyosema wahenga
“Baniani mbaya kiatu chake dawa”. Kuna kizuizi kingine cha ufahamu sikizi ambacho ni kama kinyume cha ukosoaji.
Msikilizaji anaweza kuvutiwa na kukumbwa na msisimko wa yanayosemwa na mtindo
wa kuwasilishwa kwake hivi kwamba hazingatii maana ya ujumbe tena.
Usikilizaji wa aina hizi mbili una kasoro na haustahili. Wanafunzi wakizoea
kusikiliza kwa namna hizi hawawezi kutathimini ujumbe kwa msingi na mtazamo wa
haki. Inafaa wahimizwe kukawilisha ukosoaji na ushabiki wao hadi watakapomaliza
kusikiliza.
Mazimgira:
Mawasiliano hayafanyiki katika ombwe tupu. Watu wanapozungumza na
kusikiliza wanafanya hivyo katika mazingira maalum ya kimaumbile na kijamii. Hali ya
mambo ndani ya darasa inaweza kuchangia kufanikisha au kutatiza mawasiliano ya
darasani. Ikiwa kwa mfano wakati zoezi la kusikiliza linapoendelea hakuna utulivu ndani
ya darasa au kuna kelele nje karibu na darasa itakuwa vigumu kwa wanafunzi kusikiliza
kama inavyostahili.
Kwa upande mwingine, hali ya kimaumbile ndani ya darasa inaweza kuwafanya
wanafunzi wakose utulivu kimwili na kiakili. Uhaba wa nafasi, kwa mfano, unaweza
kusababisha mfinyano kwa kiasi ambapo wanafunzi hawawezi kukaa kwa utulivu
49
kuweza kuzingatia kikamilifu ujumbe unaowasilishwa na mzungumzaji. Katika hali kama
hii inakuwa shida kusikiliza kwa ufahamu.
Habari (Ujumbe).
Ujumbe unaowasilishwa unaweza kutatiza msikilizaji na kumfanya asielewe.
Mazungumzo, kwa mfano, yakijikita katika mambo ambayo hayawavutii wanafunzi
watakosa ari ya kusikiliza kwa makini. Vile vile kama mazungumzo yanashughulikia
mambo ambayo hayana uwiano na kiwango cha uwezo wa wanafunzi si rahisi kwao
kuyafuata kwa ufahamu.
Licha ya haya, ujumbe unaohusika ukikosa kuwa na muundo unaobainika wazi
huenda wanafunzi wakakanganywa na kutoelewa vizuri.
ZOEZI 5.3
(i) Ukitoa mifano maridhawa kutilia maki jibu lako onyesha jinsi
mwanafunzi mwenyewe binafsi anavyoweza kuwa ndiye chanzo
cha kutosikiliza kwa ufahamu.
(ii) Pendekeza mambo unayoweza kufanya ili kuboresha uwezo wake
wa kusikiliza kwa ufahamu kamili.
B.
(i) Ukitoa mifano inayofaa eleza jinsi hali ya kimazingira
inavyoweza kutatiza shughuli za wanafunzi za kusikiliza kwa
ufahamu.
(ii) Ni hatua gani unazoweza kuchukua ili kuhakikisha kwamba hali
ya kimazingira darasani haitatizi juhudi za wanafunzi za
kusikiliza?
5.4 Kufanikisha Ufahamu Sikizi
Ufahamu ni mfanyiko wa ndani. Mwalimu hana uwezo wa moja kwa moja juu
yake. Hata hivyo kuna baadhi ya mambo ambayo anaweza kufanya, na kupitia mambo
hayo akachangia ufanikishaji wa mfanyiko wa ufahamu.
Kwa ufupi mambo haya yanaweza kugawanyika katika vipengele vifuatavyo:
50
Uteuzi bora
Maandalizi bora
Uwasilishaji bora
Mazingira bora
Uteuzi Bora
Ni wajibu wako kama mwalimu kuona kwamba unateua mapema kabla ya kipindi
mambo ambayo unataka wanafunzi wasikilize. Usingoje dakika chache kabla ya kipindi
ndipo uamue kuhusu mambo hayo. Unapochagua matini ya usikizi ni lazima uhakikishe
kwamba maudhui yake pamoja na lugha vinawiana vizuri na kiwango cha wanafunzi.
Maudhui yake yawe ya kuvutia na kuwatia changamoto vya kutosha. Pia ni lazima
uhakikishe kwamba huchagui matini ambayo usikilizaji wake utachukua muda wote wa
kipindi. Inafaa usikilizaji uwe sehemu ndogo tu ya kipindi kizima.
Baada ya kuteua matini inayofaa kufundishia unashauriwa kuipitia kwa uangalifu
ili uweze kutambua ni wapi katika matini yako wanafunzi wanahitaji kupewa usaidizi na
usaidizi huo utakuwa wa namna gani.
Maandalizi Bora
Maandalizi yanahusu ile hali ya kujihami kwa mwalimu kabla ya kipindi pamoja
na hatua anazochukua anapofika darasani ili kutayarisha wanafunzi kushiriki katika
shughuli za kipindi.
Kwa mfano, uteuzi wa mambo yanayotarajiwa kushughulikiwa darasani ni hatua
mojawapo ya maandalizi ya mwalimu kabla ya kipindi. Pia uteuzi wa mbinu zinazofaa
kutumia kuendesha kipindi ni hatua muhimu katika maandalizi ya mwalimu kabla ya
kipindi. Hali kadhalika wakati wa maandalizi haya mwalimu anatarajiwa kuamua kuhusu
muda utakaohitajika kwa shughuli ya zoezi la kusikiliza, na muda ambao utatumiwa kwa
shughuli nyingine. Haitarajiwi kuwa zoezi la kusikiliza litachukua muda wote wa kipindi.
Linapaswa kuambatanishwa na ufundishaji wa mambo mengine. Kwa hivyo ni muhimu
kwa mwalimu kuamua mapema jinsi zoezi hili litakavyoambatanishwa na ufundishaji wa
mambo mengine.
Kisha mwalimu anapofika darasani inambidi kuona kwamba wanafunzi
wanatayarishwa kukipokea kipindi cha somo kinachohusika. Matayarisho haya ni
muhimu sana, na hayastahili kupuuzwa. Mwalimu asifyatuke moja kwa moja kama risasi
na kuwashirikisha wanafunzi katika zoezi la kusikiliza kabla ya kuhakikisha kwamba
amejenga mazingira bora ya kufanikisha zoezi hilo.
Je unaweza kuyajenga namna gani mazingira ya kufanikisha shughuli ya
kusikiliza kwa ufahamu?
Ukweli ni kwamba hakuna mbinu yoyote ambayo ni ya lazima kwa kila
mwalimu. Lakini kwa vyo vyote vile ni lazima utoe utangulizi hivi kwamba unaweza
kudhibiti mwelekeo wa mawazo ya wanafunzi na kuwatamanisha kujihusisha na yale
yanayoendelea. Mambo ambayo unayatenda inafaa yalenge maudhui muhimu ya zoezi,
51
licha ya kuwiana na kiwango cha wanafunzi wako. Mifano ya baadhi ya mambo ambayo
unaweza kufanya ili kuwatayarisha wanafunzi kwa shughuli hii ni pamoja na:
Kuwatia chonjo kwa namna yo yote inayofaa.
Kuhakikisha kuwa kuna hali ya ututlivu.
Kuwatia changamoto kwa kuwauliza maswali yanayolenga mada kuu ya
kipindi n. k…
Mifano ya mambo yanayoweza kufanywa ili kuwatia chonjo wanafunzi ni kama
vile:
Maonyesho ya picha zinazowiana na matarajio ya mada kuu.
Maigizo ya mambo yenye uwiano na mada kuu.
Maelezo mafupi juu ya malengo ya kipindi.
Uwasilishaji Bora
Ili shughuli ya kusikiliza iwe ya maana na manufaa kwa wanafunzi ni wajibu
wako kama mwalimu kuzingatia masharti yafuatayo:
Matamshi ya mzungumzaji yawe ya kueleweka.
Sauti ya mzungumzaji iwe ya kusikika na yenye kiimbo sahihi kuwiana na
maana inayowasilishwa.
Mzungumzaji azingatie kikamilifu vituo, na kuzungumza kwa mwendo
unaofaa. Asizungumze kwa kasi sana wala kwa kujikokota.
Sauti ya mzungumzaji iwe ya kuvutia.
Ukiamua kufundisha ukitegemea ukanda wa sauti inafaa uchague ukanda kwa
kutilia maani masharti haya. Pia, ukiamua wewe mwenyewe kusoma kwa sauti ni lazima
uzingatie masharti haya unaposoma. Masharti haya yakitiliwa maanani ni njia moja ya
kuhakikisha kuwa wanafunzi wanashawishiwa na kushirikishwa kwa njia ya maana na
manufaa.
Mazingira Bora
Mazingira bora kwa shughuli ya kusikiliza ni yale yenye utulivu na ushirikiano
bora kati ya wanaohusika. Kwa hivyo, kabla ya kuwashirikisha wanafunzi katika
kusikiliza ni wajibu wako kuona kwamba kuna hali ya utulivu miongoni mwa wanafunzi.
Kila mwanafunzi ni lazima ajihisi kuwa amestarehe na kutokuwa na wasiwasi.
Usichangie katika kuzusha hali ya wasiwasi na utovu wa utulivu kupitia vitendo
vyako na matamshi yako. Aidha ikiwa kuna wanafunzi ambao wana shida ya kusikia
washughulikie ipasavyo na kuona kwamba wanakaa karibu na chanzo cha habari. Pia
kama kuna kitu cho chote ndani ya darasa ambacho kinaweza kuwasumbua wanafunzi na
kuwazuia kusikiliza kwa makini, ikiwezekana kitu hicho kiondolewe kwa muda au
kifunikwe.
Wanafunzi wakimaliza kusikiliza unaweza kuwaongoza kuzungumza juu ya yale
waliyoyasikia. Wapewe nafasi ya kutoa maoni yao pamoja na kujibu maswali ya
ufahamu juu yake.
52
ZOEZI 5.4
A. Ni mambo gani ambayo watoto wa shule hupendelea kusikiliza? Je, kwa
maoni yako, mambo hayo yanafaa kufundishia ufahamu sikizi katika
somo la Kiswahili au la? Toa sababu za kutilia nguvu jibu lako.
B. Ukirejelea matini yo yote ya usikizi ambayo
ungependa kutumia kufundishia ufahamu sikizi katika kidato fulani eleza
mambo ambayo utayafanya katika utangulizi ukiwa na lengo la kuiteka
nadhari ya wanafunzi ili waweze kusikiliza kwa makini na ufahamu bora.
5.5 Umuhimu Wa Kuongea.
Katika sehemu za somo zilizotangulia tumegusia fani ya ufahamu sikizi mkazo
ukutiliwa hasa juu ya mambo ambayo wewe kama mwalimu unaweza kufanya ili kusadia
wanafunzi wawe na uwezo wa kusikiliza na kupokea kwa ufahamu mzuri ujumbe
unaowasilishwa katika mazungumzo. Maelezo haya yanahusu hasa wajibu wa
mwanafunzi kama mhusika mpokezi wa ujumbe unaowasilishwa.
Katika sehemu za somo zinazofuata tutajishughulisha hasa na mbinu unazoweza
kutumia kusaidia wanafunzi kuwa na uwezo wa kuongea vizuri na kuwasilisha ujumbe
walio nao kwa njia inayofahamika. Lakini kabla ya kuzungumzia mbinu hizo inatupasa
kwanza tuelewe mambo ya kimsingi kuhusu kuongea. Moja kati ya mambo haya ni
umuhimu wake. Je, kwa maoni yako kuongea kuna umuhimu gani katika utaratibu wa
kujifunza na kufundisha Kiswahili? Kuna ubaya wo wote wa kufundisha Kiswahili bila
kushughulikia rasmi uwezo wa kuongea?
Sababu moja ya kutilia mkazo uwezo wa kuongea ni kwamba wanafunzi
wanaposhiriki katika shughuli ya kuongea wanapata fursa ya kutumia msamiati wa aina
tofauti katika mkutadha maalum wa mawasiliano. Pia wanapata fursa ya kuendeleza na
kuimarisha ujuzi wa sarufi. Bila kuongea wanafunzi wasingekuwa na fursa ya kuzoea
kuwasiliana wakitumia maneno mbalimbali pamoja na miundo ya kisarufi ambavyo
wanatarajiwa kudhibiti matumizi yake. Kupitia kuongea, vile vile wanafunzi wanaweza
kupanua fikra zao pamoja na kukuza uwezo wa kujieleza kwa mtiririko wa mawazo juu
ya jambo fulani. Kwa mfano, mwanafunzi akiagizwa na mwalimu atetee au apinge kauli
fulani itambidi kutafuta hoja, kufikiria juu yake, na kuziwasilisha kwa namna ambayo
inaweza kushawishi msikilizaji akubaliane naye.
Hali kadhalika zoezi la kuongea ni muhimu kwa kuendeleza matamshi.
Mwanafunzi akiongea, huwa anatamka maneno yaliyoundwa kwa mpangilio wa
vitamkwa vinavyopatikana katika lugha husika. Kwa hivyo kupitia zoezi la kuongea
mwanafunzi anaweza kusaidiwa kutambua makosa yake ya kimatamshi na
kuyarekebisha. Ni muhimu kuona kwamba mwanafunzi anakuwa na matamshi bora kwa
sababu matamshi sahihi yanachangia katika kufanikisha mawasiliano, lakini yasipokuwa
sahihi yanaweza kutatiza hali ya mawasiliano na kuzusha hali ya kutoelewana.
53
Kwa upande mwingine kuongea ni muhimu kutokana na ukweli kwamba uzoefu
ambao mwanafunzi anapata kupitia uzungumzi unakuwa msingi bora kwa ufanisi wake
katika lugha ya uandishi. Mwanafunzi akizoea kuongea kwa njia inayofaa itakuwa rahisi
kwake pia kuandika kwa njia inayofaa. Lakini mwanafunzi akiwa, kwa mfano, na
mazoea ya kutamka vibaya kuna uwezekano kwamba matamshi yake mabaya yataathiri
maandishi yake. Mara kadhaa watu wana tabia ya kuandika kama wanavyotamka. Kwa
hivyo njia mojawapo ya kuboresha uandishi wa wanafunzi ni kuhakikisha kwamba
wanaongea Kiswahili kwa matamshi bora.
Kuongea ni muhimu pia kwa mtazamo wa kijamii. Uwezo wa kuongea unasaidia
kujenga uhusiano na kudumisha utangamano wa kijamiii. Bila uwezo huu inakuwa
vigumu kwa watu kupashana habari na kuendeleza maisha yao. Ili mwanafunzi aweze
kukabiliana na hali ya maisha ya kila siku inampasa kujua jinsi ya kuongea na watu
katika miktadha mbali mbali ya mawasiliano.
Yapo mambo ya kimsingi ambayo yanawiana na uwezo huu na kuchangia
kuufanikisha. Moja kati ya mambo hayo ni matamshi. Sasa tutazungumzia jambo hili
kwa undani katika maelezo yatakayofuata.
ZOEZI 5.5
Jadili umuhimu wa kushughulikia uwezo wa
kuongea katika ufundishaji wa somo la
Kiswahili.
5.6 Matatizo Ya Kimatamshi.
Kuna makosa ya aina tofauti ambayo wanafunzi wanafanya wanapoongea
Kiswahili. Makosa hayo hutokea kwa sababu tofauti. Yale ambayo yanashuhudiwa sana
yanaweza kuainishwa katika makundi yafuatayo:
Mpishano wa vitamkwa.
Upachikaji wa vitamkwa.
Udondoshaji wa vitamkwa.
Ni muhimu kwako kama mwalimu kuelewa aina ya kosa linalofanywa na
mwanafunzi ili uweze kushughulikia urekebishaji wake kwa kutumia mbinu inayofaa.
Mpishano Wa Vitamkwa.
Kosa hili hutokea wakati ambapo badala ya kutamka kitamkwa kinachotarajiwa
mwanafunzi anatamka kingine kinachokaribiana nacho. Mifano ifuatayo inabainisha aina
ya kosa hili:
54
Je, chanzo cha kosa hili ni nini? Linaweza kutokea kutokana na ukweli kwamba
kitamkwa kinachotarajiwa hakipatikani katika lugha ya mama ya mwanafunzi. Anatamka
kitamkwa ambacho amezoea katika lugha yake.
Kosa la kutamka: mbaka badala ya mpaka, kubima badala ya kupima, na mbira
badala ya mpira linaweza kuchukuliwa kama kosa la mpishano wa vitamkwa lakini
chanzo chake ni tofauti na kile cha matamshi ya maneno mengine. Asili yake siyo utovu
katika lugha ya mwanafunzi wa kitamkwa kinachotarajiwa.
Vitamkwa vyote vinavyohusika vinapatikana katika lugha ya mama ya
mwanafunzi na pia katika Kiswahili. Mwanafunzi anayehusika huwa anatamka hivyo
kufuatana na kanuni za kifonolojia za lugha ya mama. Kwa mfano, katika lugha ya
Kinandi kuna /p/ na /k/ lakini vitamkwa hivi vikitokea katikati ya vokali vinageuka na
kutamkwa kama /b/ na /g/ mtawalia. Hii ni sababu kwa nini unaweza kusikia wanafunzi
kutoka jamii hii wakitamka * kugata badala ya kukata na * kubima badala ya kupima.
Mfano mwingine wa kutamka kimakosa maneno ya Kiswahili kwa kuzingatia
kanuni za kifonolojia za lugha ya mama unahusu kitamkwa /p/. Katika Kinandi kitamkwa
hiki kinapotanguliwa na /m/ huwa kinatamkwa kama /b/ . Kwa sababu ya kuzingatia
kanuni hii ya fonolojia ya lugha yao ya mama wanafunzi kutoka jamii hii wanatamka
neno mpira kama *mbira na mpaka kama *mbaka. Kwa wanafunzi hawa matamshi ya
vitamkwa vinayohusika yanategemea mazingira ya kifonolojia. Vimo katika mpishano
wa kimazingira.
Neno linalotarajiwa Neno linalotamkwa
mdudu
mzazi
uchumi
gugu
vuta
vua
chombo
mbishi
bua
kupima
kugawa
mpaka
mpira
mtutu
msasi
ujumi
kuku
futa
fua
shombo
mpishi
pua
kubima *
kukawa
mbaka *
mbira *
55
Upachikaji Wa Vitamkwa:
Kosa hili hutokea wakati ambapo mwanafunzi hutamka neno linalohusika kwa
kuweka kitamkwa cha ziada kwenye neno hilo na kuishia na neno tofauti na lile
lililokusudiwa. Mifano ifuatayo inabainisha aina ya kosa linalohusika:
Katika Kikamba, kwa mfano, vitamkwa /d/, /b/ na /g/ vinapotokea mwanzoni
mwa neno ni lazima viwe vimetanguliwa na sauti ya kipua. Kwa kuzingatia sharti hili
wanafunzi kutoka jamii hii wanapokabiliana na maneno ya Kiswahili yenye miundo
ambayo katika lugha yao inahitaji sauti ya kipua hupachika sauti hiyo ili kutimiza
masharti ya matumizi ya lugha yao.
Wakati mwingine upachikaji wa vitamkwa hutokea wanafunzi wanapokabiliana
na maneno ya Kiswahili yenye mfuatano wa konsonanti. Wanapachika vokali ili kurahisisha matamshi kufuatana na mpangilio wa vitamkwa katika lugha zao za mama
ambao, aghalabu, hauruhusu mfuatano wa namna hiyo. Ifuatayo ni mifano inayobainisha
jambo hili:
Neno linalotarajiwa Neno linalotamkwa
doa
buni
bali
basi
dawa
gari
ndoa
mbuni
mbali
mbasi *
ndawa *
ngari *
56
Hali kadhalika baadhi ya wanafunzi hupachika vokali mwanzoni mwa maneno ili
kurahihisha matamshi ya mfuatano wa konsonanti. Jambo hili linatokea sana hasa katika
maneno yenye muundo wa silabi moja kama vile katika mifuano ifuatayo:
Udondoshaji Wa Vitamkwa.
Kosa hili hutokea wakati ambapo kitamkwa kimoja kinafutwa na kutotamkwa
kama katika mifano ifuatayo:
Matamshi Sahihi Matamshi Yasiyo Sahihi
alfajiri
umri
ilmradi
halmashauri
amrisha
kunradhi
jamhuri
alhamisi
alifajiri
umuri
ilimuradi
halimashauri
amurisha
kuniradhi
jamuhuri
alihamisi
Matamshi Sahihi Matamshi Yasiyo Sahihi
nje
nchi
nzi
mbu
mbwa
inje
inchi
inzi
umbu
umbwa
57
Matokeo ya kutamka namna hii ni kwamba mwanafunzi huishia kwa kuwasilisha
maana iliyo tofauti na ile iliyokusudiwa. Pia, wakati mwingine, huishia kwa kutamka
maneno ambayo hayana maana yo yote katika Kiswahili. Kwa kawaida, wasikilizaji
wanaweza kupokea maana iliyokusudiwa kutokana na mkutadha wa mawasiliano. Lakini
kuna wakati ambapo matamshi yakiwa mabaya, wanaweza kushindwa kupokea ujumbe
kwa maana iliyokusudiwa. Hali kama hii hutokea wakati ambapo hakuna kielelezo katika
mkutadha wa mawasiliano kinachoweza kuwasaidia kukisia maana.
Matatizo haya ambayo yamezungumziwa ndiyo matatizo sugu. Kuna aina
nyingine za matatizo ambayo huenda yakijitokeza hata ingawa si sana. Wakati mwingine,
kwa mfno, baadhi ya wanafunzi wanakumbwa na aina za shida za kimatamshi zifuatazo:
Kuunganisha vitamkwa
Kutenganisha vitamkwa
Kuunganisha Vitamkwa
Kosa hili linatokea wakati ambapo mwanafunzi anashindwa kutenganisha
vitamkwa vinavyotakiwa kutenganishwa na badala yake kuvitamka kama kwamba ni
silabi moja. Tatizo hili linahusu maneno yenye vitamkwa /p/ na /b/ vikitanguliwa na
kitamkwa /m/. Ikiwa kitamkwa /m/ kinasimamia silabi kamili ni lazima matamshi ya
neno linalohusika yaonyeshe hivyo kwa kutokitamka kama kwamba kinaungana kisilabi
na kitamkwa /p/ na /b/ kinachofuatia. Maneno mpaka na mbaya katika sentensi zifuatazo
yanastahili kutamkwa kwa njia ambayo inabainisha kwamba /m/ katika maneno haya ni
silabi kamili:
Neno linalotarajiwa Neno linalotamkwa
ndege
ngumi
ngao
mbuni
mbali
mbawa
mbele
kidimbwi
mazingira
mazingaombwe
kindakindaki
dondosha
dege
gumi
gao
buni
bali
bawa
bele
kidibwi
mazigira
mazigaobwe
kidakidaki
dodosha
58
(i) Tulikutana karibu na m.paka wa Kenya na Uganda.
(ii) Kijana huyu ni m.baya sana.
Lakini ikiwa mzungumzaji atatamka /m/ kama kwamba si silabi kamili atakuwa
amefanya kosa la kuunganisha vitamkwa.
Kutenganisha Vitamkwa.
Kosa hili ni kinyume cha lile la kuunganisha vitamkwa. Badala ya kutamka
vitamkwa vinavyofuatana kama silabi moja mwanafunzi huvitamka kama kwamba ni
silabi tofauti za neno. Kwa mfano, maneno mpaka na mbaya katika sentensi zifuatazo
yanapaswa kutamkwa kwa njia ambayo inadhihirisha kwamba /m/ katika maneno haya si
silabi kamili:
(iii) Mtoto hakulala mpaka asubuhi
(iv) Saa yangu ni mbaya.
Ni lazima /m/ itamkwe pamoja na vitamkwa viwili vinavyofuatia kama silabi
moja ya neno. Lakini, ikiwa mwanafunzi ataitamka kama kwamba ni silabi kamili
atakuwa amefanya kosa la kutenganisha vitamkwa.
Sentesni zifuatazo zinaweza kukusaidia kuelewa vizuri zaidi dhana ya
kuunganisha na kutenganisha vitamkwa katika matamshi ya maneno ya Kiswahili:
(v) Kijana mbaya ana sura mbaya.
(vi) Hatutasimama mpaka mpaka wa nchi.
ZOEZI 5.6
Ukitoa mifano inayofaa eleza sababu nyingine
zaidi ambazo kwa maoni yako huwafanya
wanafunzi waongee Kiswahili kwa makosa ya
kimatamshi.
5.7 Kufundisha Matamshi.
Ufanisi wa mwanafunzi katika matamshi unategemea, kwa kiasi fulani, uwezo
wake wa kusikia, kupambanua (kuchanganua) katika usikizi wake na pia katika
uzungumzi wake vitamkwa mbalimbali vya lugha. Kwa hivyo, wewe kama mwalimu wa
Kiswahili ni lazima uhakikishe kwamba unasitawisha uwezo huu ili wanafunzi wako
waweze kuongea Kiswahili kwa matamshi bora. Ili kutekeleza jambo hili inakubidi
uzingatie hatua za kimsingi zifuatazo:
59
Kuendeleza upokezi sikizi.
Kuendeleza upambanuzi sikizi.
Kuendeleza upambanuzi zungumzi.
Hatua hizi zinalenga hasa kushirikisha wanafunzi katika matumizi ya lugha
ambayo yatawapatia mazoea mema ya kuwasaidia kuongea kwa matamshi bora.
Zinalenga pia kuwasaidia kutambua makosa ya kimatamshi na kuyarekebisha.
Upokezi Sikizi.
Upokezi sikizi unahusu ile hali ya msikilizaji ambayo kwayo masikio yake
hunakili sauti. Upokezi sikizi wa sauti unamwezesha mwanafunzi kuzoea sauti za lugha
fulani na kuzitofautisha na zile za lugha nyingine. Kinachopaswa kushughulikiwa katika
hatua hii ni kuona kwamba mwanafunzi anapata fursa ya kusikia matamshi sahihi ya
Kiswahili ambayo anaweza kuyaiga. Mkazo katika hatua hii unatiliwa juu ya kutoa fursa
kwa wanafunzi ya kupokea na kusikia matamshi ya vitamkwa mbalimbali katika
muktadha wa mfululizo wa maneno.
Baada ya kushirikisha wanafunzi katika zoezi la ukuzaji wa usikizi, unaweza
kuwashirikisha katika hatua nyingine ambayo ni ya upambanuzi sikizi.
Upambanuzi Sikizi.
Licha ya kuwa na uwezo wa kunakili sauti katika masikio yake, ni lazima
mwanafunzi awe na uwezo wa kuchanganua sauti mbalimbali anazosikia. Ni lazima
abainishe katika usikizi wake kwamba hayachanganyi maneno ambayo yanakaribiana
kimatamshi. Bila uwezo huu matamshi yake yatakuwa ya kukanganya kwa sababu
atatamka kulingana na usikizi wake wenye kukanganya, na ataishia kwa kuwakanganya
wasikilizaji. Pia, hata yeye mwenyewe atakuwa na shida ya kusikiliza kwa ufahamu.
Kile kinachoshughulikiwa katika hatua hii ni kuona kuwa mwanafunzi
anayapokea kwa usahihi maneno yanayotamkwa bila kuyageuza kutokana na
kuchanganya vitamkwa vinavyounda maneno hayo. Unapotamka, kwa mfano, mzazi
mwanafunzi inatakiwa asikie vivyo hivyo na wala siyo msazi, au msasi. Vile vile
ukitamka karibuni ni lazima asikie viyo hivyo na wala siyo kaburini. Licha ya kusikia ni
lazima mwanafunzi aonyeshe kwamba anasikia kwa usahihi. Njia mojawapo ya
kuendeleza na kutathimini uwezo wa mwanafunzi wa kuchanganua sauti katika usikizi
wake ni kumtaka afanye kitendo ambacho utekelezaji wake unategemea usikizi sahihi wa
vitamkwa vinavyounda neno. Kwa mfano, ukimwambia mwanafunzi kuvuta kiti, na
badala ya kufanya hivyo anakifuta, itakuwa wazi kwamba ana shida ya upambanuzi
sikizi wa vitamkwa /v/ na /f/. Hali kadhalika ukimwambia aandike neno mfugo na badala
ya kuandika neno hilo aandike mfuko, utajua kuwa katika usikizi wake ana shida ya
kuchanganya vitamkwa /g/ na /k/.
Mwanafunzi huyu anahitaji mazoezi ya kusikiza ambayo humpa fursa ya kusikia
matamshi ya vitamkwa vinavyomkanganya.
60
Upambanuzi Zungumzi.
Katika hatua ya upokezi na upambanuzi sikizi mwanafunzi anashirikishwa katika
somo kama mhusika msikilizaji. Kazi yake ni kutega masikio na kupokea matamshi ya
mwalimu au mzungumzaji mwingine ambaye matamshi yake yanatumiwa kama mfano.
Kwa upande mwingine katika hatua ya upambanuzi zungumzi mwanafunzi
anashirikishwa kama mhusika mzungumzaji. Kazi yake ni kubainisha uwezo wake wa
kupambanua vitamkwa kupitia matamshi yake mwenyewe kama mhusika mzungumzaji.
Kinachoshughulikiwa katika hatua hii ni kuona kwamba mwanafunzi anatamka
maneno kwa kuzingatia matamshi sahihi ya vitamkwa vinavyounda maneno
yanayohusika. Lakini ni lazima tukumbuke kwamba uwezo huu unaambatana na uwezo
wa mwanafunzi wa kusikia na kung’amua matamshi hayo katika usikizi wake. Bila
kufanya hivyo itakuwa vigumu kwake kutamka kama inavyostahili na ataongea kwa njia
ambayo haifahamiki kwa urahisi. Kutokana na uwezo wa kupambanua vitamkwa katika
uzungumzaji mwanafunzi hatachanganya matamshi ya jozi za maneno zifuatazo:
dhamini
nadhiri
karamu
mdudu
mbishi
mchango
upupu
thamini
nathiri
kalamu
mtutu
mpishi
mjango
ububu
Kwa ufupi, unapofundisha matamshi unaweza kutumia kinasa sauti, au
kuwasomea kwa sauti wanafunzi wasikilize jinsi maneno mbali mbali yanavyotamkwa,
na kisha wajaribu kuiga matamshi hayo. Unaweza , kwa mfano kuzipitia hatua hizi tatu
zilizozungumziwa kwa kutumia jozi finyu za maneno. Maneno ya jozi finyu huwa
yameundwa na vitamkwa vinavyofanana isipokuwa kimoja tu. Pia mpangilio wa
vitamkwa hivyo katika maneno hayo unafanana. Ufuatao ni mfano wa jozi finyu za
maneno na maelezo kuhusu jinsi unavyoweza kuzitumia ukirejelea mfuatano wa hatua
hizi tatu za kimsingi: Upokezi sikizi, Upambanuzi sikizi, Upambanuzi zungumzi.
61
A
_____________________
1. mpishi
2. papa
3. chombo
4. msasi
5. mtutu
6. fahari
7 dhana
8 nathiri
9 sima
10. kuku
B
__________________
mbishi
baba
shombo
mzazi
mdudu
fahali
zana
nadhiri
zima
gugu
Upokezi Sikizi / Hatua ya kwanza.
Unasoma kwa sauti maneno katika sehemu ya A ukianza na neno la kwanza
mpaka la kumi huku wanafunzi wakisikiliza matamshi yako. Kisha unasoma maneno
katika sehemu ya B ukianza na neno la kwanza mpaka la kumi.
Upambanuzi Sikizi / Hatua ya Pili.
Unatamka maneno jozi kwa jozi huku wanafunzi wakisikiliza matamshi ya
maneno hayo. K. m:
mpishi – mbishi
nathiri – nadhiri
kuku - gugu.
fahari - fahali.
Katika hatua hii unaweza kutamka neno fulani na kuwaambia wanafunzi
waonyeshe neno ulilotamka. Kwa mfano, ukitamka neno nadhiri mwanafunzi anaweza
kujibu kwa kusema kwamba ni 8 B. Ukitamka shombo jibu linaweza kuwa 3A. Lengo
katika hatua hii ni kuendeleza uwezo wa mwanafunzi wa kung’amua maneno
yanayotamkwa. Kwa hivyo ni lazima uhakikishe kwamba zoezi lo lote katika hatua hii
linachangia kufanikisha uwezo huu.
Upambanuzi Zungumzi / Hatua ya tatu
Kama ilivyoelezwa hapo awali lengo katika hatua hii ni kumshirikisha kama
mhusika mzungumzaji. Kwa hivyo, ukirejelea jozi finyu za maneno unaweza kuonyesha
62
baadhi ya maneno na kumtaka mwanafunzi ayatamke. Akifanya makosa unamsaidia kwa
kutamka maneno hayo tena.
Katika maelezo haya tumependekeza utumiaji wa maneno ili kufundisha
matamshi. Siyo lazima ufundishe kwa kutumia maneno tu; unaweza kufundisha kwa
kutumia maneno yenye vitamkwa unavyotaka kushughulikia katika vielelezo vya
sentensi. Mbinu hii hutoa fursa kwa mwanafunzi ya kujifunza mambo mengine
yanayoambatana na matamshi, kwa mfano shadda na kiimbo. Sentensi hutoa mkutadha
bora wa kufundishia mambo haya. Sentensi kama zifuatazo ni mfano bora wa
kufundishia matamshi:
(a) Mpishi huyu ni mbishi sana.
(b) Mzazi wake ni msasi hodari.
(c) Chombo hiki chanunka shombo
(d) Zima moto huo baada ya kupika sima.
Wanafunzi wanaweza kukusikiliza ukisoma sentensi hizi kwa sauti na kisha
wanajaribu kuzisoma wao wenyewe.
Njia nyingine unazoweza kutumia kuendeleza upambanuzi sikizi ni kama vile:
Kutamka neno linaloashiria kitu fulani na kumtaka mwanafunzi aonyeshe kitu
kinachoashiriwa. Kwa mfano: basi, pasi; kamba, gamba; pua, bua.
Kumwambia mwanafunzi kutimiza kitendo fulani. Kwa mfano: pika – piga;
futa – vuta; soma – zoma.
Kutamka maneno yanayotofautiana kimatamshi na kumtaka mwanafunzi
aeleze kama umetamka neno moja mara mbili au maneno mawili yaliyo
tofauti. Kwa mfano:
(a) Mama huyu ni mbishi kweli kweli
(b) Mama huyu ni mpishi kweli kweli
Kutamka neno fulani zaidi ya mara moja na kumtaka mwanafunzi aeleze
kama umetamka maneno tofauti au neno moja zaidi ya mara moja.
Kutoa zoezi la imla.
Kwa upande mwingine, upambanuzi zungumzi unaweza kuendelezwa kwa
kushirikisha wanafunzi katika mazoezi kama yafuatayo:
Kujibu maswali yanayoshirikisha vitamkwa unavyotaka kushughulikia. Kwa
mfano, kuonyesha kitu fulani au kuigiza kitendo fulani na kumtaka
mwanafunzi aeleze anachoona…..
Kukamilisha msemo kwa kutamka neno linalofaa
Kusoma kwa sauti.
63
ZOEZI 5.7
A. Eleza kikamilifu hatua ambazo utachukua kusaidia wanafunzi
ambao wana shida ya kutofautisha katika matamshi yao kati ya
maneno yenye vitamkwa vinavyowakilishwa na mfuatano wa
herufi zifuatazo:
(i) ch -sh
(ii) dh - th
B. Mwanafunzi wako ametamka sentensi ifuatayo: Nimeshidwa
kuufuga mlago wa nyuba yagu kwa ufuguo huu
(i) Ainisha kosa ambalo amefanya..
(ii) Utachukua hatua gani kumsaidia mwanafunzi huyu ili aweze
kutambua na kurekebisha kosa lake?
5.8 Kufundisha Kuongea / Mazungumzo.
Lengo kubwa la kushirikisha mwanafunzi katika zoezi la kuongea ni kumwezesha
kujieleza bila shida, kwa matamshi mazuri, kiimbo kinachotakikana na kwa mfululizo
bora wa mawazo.
Ili kufanikisha lengo hili kuna mambo muhimu ambayo, kama mwalimu
unashauriwa kutilia maanani. Baadhi ya mambo hayo ni kama yafuatayo:
Uteuzi wa mada.
Maandalizi ya wanafunzi.
Kutia shime.
Kushirikisha kila mwanafunzi.
Uteuzi Wa Mada
Unapochagua mada za kuzungumzia unapaswa kuwa mwangalifu kuona kuwa
unachagua mambo yanayoambatana na kiwango pamoja na uzoefu wa wanafunzi wako.
64
Mada unazochagua inafaa ziambatane na mambo wayajuayo wanafunzi na ambayo
yanawahusu katika maisha yao ya kila siku. Ziwe mada za kuvutia na kugusia hisia zao.
Pia, ni wajibu wako kuhakikisha kwamba unachagua mada ambazo zina
vipengele vya kutosha vya kuzungumzia. Kama sivyo wanafunzi hawatachangia vya
kutosha na huenda wakaishia kwa kuzungumzia mambo ambayo hayana uhusiano na
mada inayohusika. Lakini mada ikiwa na vipengele vya kutosha inakuwa rahisi
kushirikisha wanafunzi waliyo wengi.
Maandalizi Ya Wanafunzi.
Mazungumzo hayafanyiki katika ombwe tupu. Yanafanyika katika mazingira
maalum ya kijamii. Kwa hivyo kabla hujashirikisha wanafunzi katika shughuli ya
kuongea ni wajibu wako kuhakikisha kwamba hakuna cho chote ambacho kinaweza
kuwazuia kushiriki na kujieleza darasani.
Wakati mwingine baadhi ya wanafunzi husita kushiriki katika mazungumzo kwa
sababu ya hofu na haya. Huwa wanahofia kuwa wenzao huenda wakawacheka. Wengine
wanaogopa kukaripiwa na mwalimu hali ambapo kuna wale ambao wanaogopa kufanya
makosa. Ni wajibu wako kuwatuliza na kuwaondolea hofu wanafunzi. Kuhusu ufanyaji
wa makosa inafaa uwafahamishe kuwa hakuna asiyefanya makosa. Pia wajulishe
kwamba wakiogopa kufanya makosa hawatajifunza lugha kwa sababu makosa ni jambo
la kawaida katika matumizi ya lugha.
Ni muhimu pia kuhakikisha kwamba wanafunzi wanafahamu vizuri lengo la
mazungumzo.
Kutia Shime
Jiepushe na tabia ya kukosoa wanafunzi wakati wanapochangia katika
mazungumzo. Unapofanya hivyo unawavunja moyo. Mwanafunzi akifanya kosa, liandike
kisha ulishughulikie baadaye. Pia jitahidi kuwatia shime wanafunzi wakati wanapoongea.
Unaweza kutekeleza jambo hili kwa kufanya mambo kama yafuatayo:
Kusikiliza kwa makini na kuonyesha kwa mwitiko wa mwili wako kuwa
unasikiliza.
Kuwapongeza wanafunzi.
Kuuliza maswali ya udadisi ambayo yanalenga kusaidia wanafunzi kujieleza
bora zaidi.
Kushirikisha Kila Mwanafunzi.
Ni wajibu wako kuona kuwa kila mwanafunzi anapata fursa ya kushiriki katika
mazungumzo. Usiache wanafunzi wachache ambao huwa wanataka sana kuongea wawe
ndio wanatawala. Wanafunzi wanaoogopa kuongea unaweza kuwatia moyo kwa
kuwauliza maswali rahisi nao waweze kuchangia.
65
ZOEZI 5.8
A. Kwa maoni yako ni mambo gani ambayo
huwafanya wanafunzi kushindwa kushiriki
kikamilifu katika mazungumzo?
B. Unaweza kuchukua hatua gani kushughulikia
matatizo hayo uliyotaja?
5.9. Njia Za Kufundishia Mazungumzo.
Ziko njia mbali mbali ambazo unaweza kutumia ili kutoa nafasi kwa wanafunzi
ya kujieleza katika mazungumzo. Miongoni mwa njia hizo ni hizi zifuatazo:
Majadiliano ya vikundi.
Maigizo.
Masimulizi.
Majibizano.
Majadiliano Ya Vikundi
Katika ufafanuzi wa lugha tulisema kuwa ni chombo cha mawasiliano. Na njia
moja ya kufanikisha mawasiliano miongoni mwa wanafunzi ni kuwaweka katika vikundi
vidogo vidogo ili wajadiliane juu ya mada fulani. Wakiwa katika vikundi vya watu
wachache wanafunzi wanapata fursa nzuri ya kutumia lugha halisi. Kila mwanafunzi
hupata nafasi ya kujieleza kwa uwezo wake bila wasi wasi. Hata wanafunzi ambao kwa
kawaida huogopa kuongea hadharani hujitolea kuongea wakiwa katika kikundi cha watu
wachache.
Jukumu lako kama mwalimu ni kuona kwamba wanafunzi katika kila kikundi
wanafanya kazi waliyopewa kulingana na maagizo uliyotoa. Ni lazima uhakikishe
kwamba wanaelewa vizuri kile wanachotarajiwa kufanya.
Maigizo:
Maigizo yanaweza kutokana na vitabu vinavyotumiwa darasani. Yanaweza pia
kutokana na tukio lo lote ambalo wanafunzi wameshuhudia. Wanafunzi wachache
waigize mbele ya darasa huko wengine wakitazama na kusikiliza.
Uzuri wa kuigiza ni kwamba kunawapa wanfunzi fursa ya kukuza kipawa chao
cha kubuni. Vile vile mwanafunzi anapoigiza anapata nafasi ya kujihusisha na kuhisi
uhalisi wa ukweli wa mambo ambayo kwa kawaida asingeyatilia maanani. Pia anapata
nafasi ya kutumia lugha kulingana na mkutadha maalum wa mawasiliano.
66
Jukumu lako kama mwalimu ni kuwashauri wanafunzi watilie maanani
ushirikishaji wa mwili na kiimbo kulingana na ujumbe unaowasilishwa. Ikiwa ni huzuni,
kwa mfano, sura na sauti ya mwanafunzi vionyeshe huzuni.
Masimulizi:
Mwanafunzi mmoja baada ya mwingine anaweza kupewa nafasi kusimulia juu ya
tukio au kisa fulani. Anapofanya hivyo huwa anakuza uwezo wa kupanua na kupanga
mawazo yake kwa mtiririko. Vile vile wanafunzi wengine wanaposikiliza huwa
wanaendeleza stadi ya kusikiliza kwa ufahamu.
Mwanafunzi anapomaliza kuzungumza wenzake wanaweza kupewa fursa ya
kuuliza maswali juu ya yale yaliyosemwa. Wajibu wako kama mwalimu ni kuona
kwamba zoezi haligeuki kuwa kitu kingine. Masimulizi yanaweza kuchukuliwa kama
insha ya mdomo. Kwa hivyo, ukitaka unaweza kutoa vichwa vya habari tofauti na
kuwambia wanafunzi watoe masimulizi juu yake. Kwa mfano, unaweza kuwambia
wanafunzi tofauti watoe kisa kinachobainisha ukweli wa moja kati ya methali zifuatazo:
(a) Kichwa cha nyoka hakibandiki mtungi.
(b) Kamba ya mbali haifungi kuni.
(c) Kitanda usicholalia huwajui kunguni wake.
(d) Dalili ya mvua ni mawingu.
Majibizano.
Majibizano yanaweza kuwa: kati ya mwalimu na mwanafunzi au, kati ya
mwanafunzi na mwanafunzi. Unaweza kuonyesha wanafunzi kifaa fulani cha maono.
Kisha wanafunzi wanaweza kuulizana na kujibiana maswali juu ya kifaa hicho. Nawe
vile vile unaweza kuwauliza na kuwadadisi wanafunzi kadhaa juu ya kifaa
kinachohusika. Unapouliza maswali unapaswa kuhakikisha kuwa wanafunzi hawatoi
majibu ya pamoja. Mifano ya vifaa vya maono unavyoweza kutumia ni kama vile: picha,
vibonzo na michoro ya aina mbali mbali. Vifaa hivi vinaweza kuwavutia wanafunzi na
kuwapa motisha ya kuongea. Ukijitahidi huwezi kukosa kupata vifaa katika vitabu na
magazeti.
Mfano mwingine wa majibizano ni zoezi la kutegeana na kutegua mafumbo.
Kupitia zoezi hili mwanafunzi hupata nafasi ya kupanua fikra zake, kupanga mawazo na
kujieleza kwa nafsi yake. Zoezi hili pia husaidia kukuza ubunifu katika kutumia lugha.
Kwa upande mwingine, mwanafunzi msikilizaji anaendeleza ustadi wa kusikiliza kwa
makini na uwezo wa kutatua matatizo.
Kuna njia nyingine ambazo unaweza kutumia ili kuchangia uwezo wa wanafunzi
wa kuongea. Matokeo mazuri yatatokea ikiwa utateua kwa uangalifu njia zinazofaa,
kuwahamasisha wanafunzi wako na kuwashirikisha kwa utaratibu.
67
ZOEZI 5.9
A. Chagua au tayarisha kifaa cho chote cha maono
unachotaka kutumia kama chombo cha kufundisha
mazungumzo kwa wanafunzi wa kidato cho chote
unachotarajia kufundisha. Kisha eleza jinsi
utakavyotumia kifaa hicho ili kutekeleza lengo
lako.
B. Eleza hatua unazoweza kuchukua ili kushughulikia
wanafunzi wenye shida zifuatazo:
(i) Kutotaka kuongea.
(ii) Kuongea kwa kupindukia.
(iii) Kutozingatia mada inayohusika
wanapoongea.
HITIMISHO
Mkazo katika somo hili umetiliwa juu ya kusikiliza na kuongea na umuhimu
wake katika utaratibu wa kujifunza lugha. Mawasiliano kila siku hufanyika zaidi kupitia
kusikiliza na kuongea kuliko kusoma na kuandika. Kwa hivyo wewe kama mwalimu
unapaswa kuhakikisha kwamba mambo haya unayapa uzito unaostahili katika mpango
wako wa kufundisha Kiswahili.
Ni wajibu kuona kwamba unatumia mbinu zo zote zile ambazo kwa maoni yako
zinaweza kuchangia kukuza uwezo wa wanafunzi wako wa kusikiliza na kuongea vizuri
Kiswahili.
68
SOMO LA 6
KUSOMA NA KUANDIKA
6.0 Utangulizi
Kusoma na kuandika ni stadi za lugha andishi ambazo zinatiliwa sana mkazo
katika mfumo wa elimu. Mwanafunzi akimudu vizuri stadi hizi mbili anaweza kujitimizia
mahitaji yake ya kimawasiliano.bila kutegemea msaada wa nje.
Katika somo hili tutatoa mapendekezo ambayo, wewe kama mwalimu, unaweza
kufanya ili kuendeleza na kuimarisha uwezo wa wanafunzi wako wa kusoma na kuandika
Kiswahili kama inavyostahili.
MADHUMUNI YA SOMO
Kufikia mwisho wa somo hili, inatarajiwa kuwa utaweza:
(i) Kueleza tanzu tofauti za kusoma na kuandika, na kueleza
umuhimu wake katika utaratibu wa kufundisha Kiswahili.
(ii) Kupendekeza na kueleza mbinu tofauti zinazofaa
kutumiwa ili kuboresha usomaji na uandikaji Kiswahili wa
wanafunzi wako
6.1 Kusoma Kwa Sauti.
Kwa kawaida mtu akisoma anaweza kufanya hivyo kimya au kwa sauti kulingana
na mkutadha wa kimawasiliano unaohusika. Kama kuna haja ya watu wengine kusikia
ujumbe wa mwandishi, msomaji atasoma kwa sauti, lakini ikiwa hakuna haja atasoma
kimoyomoyo ili ujumbe huo uwe siri yake.
Katika ufundishaji wa lugha, zoezi la kusoma kwa sauti ni muhimu kutokana na
ukweli kwamba kupitia zoezi hili mwanafunzi anapata fursa ya kuimarisha hali ya
matamshi yake. Kila anaposoma kwa sauti huwa anafanya mazoezi ya kutamka maneno
ya Kiswahili na kiimbo cha Kiswahili kwa jumla. Ikiwa, kwa mfano, kuna vitamkwa
tatanishi ambavyo unataka wanafunzi wajifunze matamshi yake unaweza kupanga
maneno yenye vitamkwa hivyo, kuyaweka katika sentensi na kisha kuwasomea
wanafunzi sentensi hizo kwa sauti. Pia wanafunzi nao wanapewa fursa ya kusoma
sentensi hizo kwa sauti. Kwa mfano ukitaka kushughulikia matamshi ya /z/ na /s/
unaweza kusomea wanafunzi wako sentensi kama zifuatazo:
(a) Wakereketwa wa haki za kibinadamu wanapinga sana utengenezaji wa zana
za vita.
(b) Alimzomea baada ya kumsomea barua yake.
Wakati mwingine kusoma kwa sauti kunaweza kuambatanishwa na zoezi la
kusoma kimya kama njia ya kutilia maki ujumbe uliyojikita katika maandishi. Maneno
yakisomwa kwa sauti yanaweza kuzua na kuibua hisia fulani ambazo si rahisi kuibuka
69
yanaposomwa kimya. Maana ambayo haiwezi kubainishwa kwa urahisi kupitia
maandishi inaweza kubainika wazi zaidi kupitia sauti. Kwa mfano, hisia kama vile
mshangao, huzuni, na furaha zinaweza kuwasilishwa mtu anaposoma kwa sauti. Kusoma
kwa sauti kunampa mwanafunzi nafasi bora ya kujihusisha na hisia za mwandishi au
mhusika fulani. Wakati wa kufundisha somo la fasihi, kwa mfano, unaweza kuamua
kuchagua sehemu fulani katika riwaya, hasa zile za majibizano kati ya wahusika na
kuzisoma kwa sauti ili wanafunzi wajihusishe na kile kinachoendelea.
Aidha kusoma kwa sauti, kunasaidia mwanafunzi kuwa mwangalifu. Ni lazima
kwanza atambue maneno yaliyoandikwa kisha ayaambatanishe na matamshi yake sahihi
ndipo aweze kuwasilisha ujumbe unaohusika. Ikiwa anaweza kusoma ujumbe
uliyoandikwa kwa njia ambayo inaleta maana hiyo ni ishara kwamba ana uwezo wa
kusoma vizuri kwa sauti. Mazoea haya yanakuwa msingi mzuri kwa zoezi la kusoma
kimoyomoyo.
Wakati mwingine kusoma kwa sauti ni njia mwafaka ya kuandaa na kuhamasisha
wanafunzi katika somo la fasihi ili wawe tayari kwanza kusoma kitabu kinachohusika
kwa hamu. Unaweza kutanguliza ufundishaji wako kwa kuwasomea kwa sauti sehemu
fulani kutoka kitabu ambacho wanatarajiwa kuanza kusoma. Lengo hasa la kufanya hivyo
ni kuwatia wanafunzi wako hamu ya kusoma kitabu hicho wakiwa na shabaha maalum.
ZOEZI 6.1
A. Eleza jinsi kusoma kwa sauti kunavyohusiana
na kutofautiana na kusoma kimya.
B. Jadili umuhimu wa kusoma kwa sauti katika
utaratibu wa kufundisha Kiswahili.
6.2 Matatizo Ya Kusoma Kwa Sauti.
Msomaji kwa sauti anaweza kukumbwa na aina mbali mbali za matatizo, ambayo
yanaweza kumfanya msikilizaji ashindwe kuzingatia vizuri yale yanayosomwa. Matatizo
hayo yanaweza kusababishwa na sababu kama zifuatazo:
Matamshi mabaya
Kuruka na kupachika maneno.
Kusoma kwa mwendo usiyofaa.
Kutosikika.
Matamshi Mabaya.
Matamshi mabaya yanatokea pale ambapo msomaji anaposhindwa kutamka
maneno kama inavyostahili na kuishia kwa kuupotosha ujumbe unaowasilishwa. Wakati
mwingine anaweza kushindwa kuzingatia vituo na kutumia kiimbo sahihi kulingana na
maana ya ujumbe unaohusika. Shida nyingine ya kimatamshi inahusu ile tabia ya
kuvunjavunja maneno na kumfanya msikilizaji afuate kwa shida. Usomaji wa namna hii
70
husumbua wasikilizaji, na wasipokuwa wavumilivu wanaweza kukata tamaa na
kumpuuza msomaji.
Urukaji na Upachikaji wa Maneno.
Kuna wasomaji ambao kwa sababu ya kutokuwa waangalifu, hawasomi maneno
yaliyomo kwenye taarifa wanayosoma na badala yake wanasoma maneno mengine
ambayo pengine hayana uhusiano wo wote na ujumbe. Msomaji asiposoma neno fulani
katika sentensi anasababisha pengo katika mfululizo wa mawazo; na matokeo yake
yanaweza kuwa upotoshaji wa ujumbe unaokusudiwa. Tuchukue mfano wa sentensi
ifuatayo:
(a) Watoto walifika nyumbani karibu saa mbili usiku.
Ikiwa msomaji ataruka neno karibu sentensi itakuwa : (b.) Watoto walifika nyumbani saa mbili asubuhi
Katika hali kama hii, msikilizaji atapokea ujumbe ambao ni tofauti
kabisa na ule anaowasilishwa na mwandishi. Hali kadhalika, msomaji akitamka neno
jingine badala ya lile lililoandikwa atapotosha ujumbe asilia. Hivyo ndivyo ilivyo pia
akiongeza neno jingine katika sentensi. Sentensi zifuatazo zinaonyesha matokeo ya hali
hii:
(c) (i) Tutakutana karibuni
(ii) Tutakutana kaburini
(d) (i) Watoto walikuwa wamechoka
(ii) Watoto walikuwa wamechoka sana.
Kusoma Kwa Mwendo Usiyofaa:
Mwendo usiyofaa unaweza kuwa ama wa kasi sana au wa kujikokota. Msomaji akisoma kwa mwendo wa kasi inakuwa vigumu kwa wasikilizaji kuzingatia ujumbe
vizuri. Kwa upande mwingine, akisoma kwa kujikokota anaweza kuwatamausha
wasikilizaji. Mwendo unaofaa ni ule wa wastani.
Kutosikika:
Kuna wasomaji ambao wanasoma kama kwamba hakuna watu wanaowasikiliza.
Kusoma kwa namna hii hakuridhishi hata kidogo. Mawasiliano hayakamiliki ikiwa
ujumbe unaowasilishwa hauwezi kumfikia mpokeaji. Kwa hivyo, wewe kama mwalimu
unapaswa kuwahimiza wanafunzi wanaposoma wahakikishe kwamba wanasikika
ipasavyo.
Kwa ufupi unaposhirikisha wanafunzi katika zoezi la kusoma kwa sauti ni lazima
uzingatie na kutilia maanani mambo yafuatayo:
Wanafunzi wahimizwe kusoma kwa mwendo wa wastani.
Wasome kwa mkumbo wa maneno kulingana na maana.
Wazingatie vituo.
Watumie kiimbo sahihi kulingana na maana.
Wasome kwa matamshi sahihi ya maneno.
Wasome kwa njia ya kusikika.
Wasifiche nyuso zao katika matini inayosomwa.
71
ZOEZI 6.2
Jadili matatizo ambayo kwa maoni yako
huwakumba wanafunzi wanaposoma Kiswahili
kwa sauti. Je unaweza kuchukua hatua gani
kushughulikia matatizo hayo?
6.3 Kusoma Kimoyomoyo
Mwanafunzi anaposoma kimoyomoyo huwa anajisomea yeye mwenyewe bila
kutamka yale asomayo. Kama ilivyo katika zoezi la kusikiliza, kupitia zoezi la kusoma
kimoyomoyo mwanafunzi anaweza kujiongezea maarifa., kupanua msamiati wake na
kuimarisha ujuzi wake wa lugha. Vile vile kupitia zoezi la kusoma kimya kimya
mwanafunzi anaweza kujiburudisha na kukuza uwezo wa kuchunguza na kudadisi
(kuhakiki) mambo.
Katika sehemu hii tutazungumzia kusoma kimoyomoyo tukitilia mkazo fani ya
kusoma kwa ufahamu (Ufahamu andishi). Kinyume na ufahamu sikizi, ufahamu andishi
ni fani ya lugha andishi ambayo kwayo msomaji anapokea ujumbe wa mwandishi na
kuuambatanisha na maana inayostahili. Madhumuni hasa ya kushirikisha wanafunzi
katika zoezi la ufahamu andishi ni nini? Zoezi hili linalenga hasa kusaidia wanafunzi
wakuze uwezo wao wa kusoma upesi bila shida na kufahamu ipasavyo. Linalenga pia
kukuza uwezo wa mwanafunzi wa kusoma kwa makini na kung’amua yaliyo muhimu na
yasiyo muhimu.
Ili wanafunzi wako waweze kusoma kwa ufahamu unapaswa kushughulikia
matatizo ambayo yanaweza kuwazuia kusoma kwa ufahamu. Baadhi ya matatizo hayo ni
kama yale yaliyotajwa katika somo lililotangulia (Rej 5.3). Zaidi ya matatizo hayo
tunaweza kuongeza yafuatayo:
Upachikaji wa maneno.
Kufuta maneno.
Kutozingatia vituo.
Upachikaji Wa Maneno.
Asili ya jambo hili ni utovu wa umakinifu kwa msomaji. Na matokeo yake, kama
ilivyoonyeshwa katika sehemu 6.2 ya somo hili, ni kupotosha ujumbe asilia kama katika
mfano ufuatao:
(a) Tutaonana kesho.
(b) Tutaonana kesho kutwa.
Mwanafunzi akisoma (b) badala ya (a) atapotosha ujumbe asilia. Hali kadhalika,
akifuta maneno yaliyomo kwenye taarifa anayosoma ataishia kwa kutoelewa kama
ilivyotarajiwa. Tuchukue mfano ufuatao:
(c) Tukutane kabla ya saa nne.
(d) Tukutane saa nne.
72
Akisoma sentensi (d) badala ya (c) atakuwa ameshindwa kuelewa ipasavyo
ujumbe asilia.
Kutozingatia Vituo:
Mwanafunzi asipozingatia vituo kwa mfano viulizi anaweza kuchukulia swali
kama kauli ya kawaida. Matokeo yake ni ufahamu mbaya.
Jambo jingine unaloshauriwa kutilia maanani ukitaka kuwezesha wanafunzi
kusoma kwa ufahamu ni maandalizi bora. Mambo unayoweza kufanya kutekeleza jambo
hili ni kama yale yaliyotajwa katika somo lililotangulia (Rej 5.4).
ZOEZI 6.3
Ukitoa mifano ya kutilia maki jibu lako eleza
mambo ambayo yanaweza kumfanya mwanafunzi
asisome kwa ufahamu. Unaweza kuchukua hatua
gani kumsaidia mwanafunzi anayekabiliwa na
shida ulizotaja?
6.4 Maswali Ya Ufahamu
Maswali ni chombo muhimu ambacho unaweza kutumia kuelekeza wanafunzi
wako kusoma kwa ufahamu wa ndani. Pia ni kigezo muhimu cha kupimia kiwango cha
ufahamu wa wanafunzi. Kwa hivyo ukitaka wanafunzi wako wasome kwa ufahamu
kamili ni lazima utayarishe na kutunga maswali ya ufahamu kwa uangalifu.
Wanaposoma, kwa mfano, kifungu fulani kutoka katika kitabu kinachotumiwa darasani si
lazima utegemee maswali ya mwandishi. Unaweza kutunga na kuuliza maswali yako
mwenyewe. Kwa ufupi maswali unayouliza ni lazima yazingatie masharti kama
yafuatayo:
Kuwa wazi.
Matini inayohusika.
Kuzingatia kikamilifu ufahamu.
Kumpa mwanafunzi nafasi ya kujieleza.
Uwazi.
Ni lazima uhakikishe kwamba maswali unayouliza hayana utatanishi wa aina yo
yote. Yawe na mwelekeo maalum. Kumbuka kwamba lengo la maswali siyo
kuwatatanisha wanafunzi na kuwatumbukiza katika makosa. Ukiuliza maswali
yasiyoeleweka vizuri hata majibu yao yatakuwa ya kutatanisha.
Matini Inayohusika
Maswali unayouliza yahusiane kimantiki na matini inayohusika. Ni lazima
yatokane na matini hiyo na wala siyo nje yake. Sharti yawe maswali ambayo yanaweza
kujibiwa kwa kuzingatia mambo yaliyomo katika matini inayohusika. Lengo lake ni
73
kutathimini uwezo wa mwanafunzi wa kusoma kifungu fulani na kuelewa ujumbe wake.
Kwa hivyo ni lazima maswali yanayoulizwa yajikite katika kifungu hicho hicho.
Kuzingatia Kikamilifu Ufahamu.
Mtu anaposoma kifungu fulani cha habari anaweza kukichunguza na kufahamu
kifungu hicho kwa viwango mbali mbali. Kwa hivyo unapotunga maswali ya ufahamu
juu ya kifungu kilichosomwa na wanafunzi ni wajibu wako kuona kuwa maswali
unayatunga kwa kuzingatia maenezi yote ya stadi za ufahamu. Usiulize maswali ya aina
moja; lakini uliza maswali ambayo yanashirikisha viwango mbali mbali vya ufahamu.
Mfano wa viwango hivi ni kama:
Ukweli halisi wa mambo.
Ufahamu kwa kuhusisha mambo kimantiki (Ufahamu fasirizi)
Uhakiki/ Utathimini.
Matumizi ya lugha.
Kiini cha taarifa n.k…..
Ukweli halisi unahusu habari halisi kama ilivyo. Kama mwandishi anasema kuwa
mtu fulani alitenda jambo fulani wakati fulani, msomaji anapaswa kuelewa vivyo hivyo
na wala siyo vingine.
Ufahamu kwa kuhusisha mambo kimantiki unahusu uwezo wa mwanafunzi wa
kudadisi na kufikia ukweli uliojikita ndani ya ujumbe wa mwandishi. Unamwezesha
mwanafunzi kuchimbua na kubaini mambo yasiyoelezwa wazi wazi. Mwandishi kwa
mfano, si lazima aseme kinagaubaga kwamba jambo analozungumzia ni la kuaibisha,
kufurahisha au kuhuzunisha. Inampasa mwanafunzi ang’amue mwenyewe kwa
kuzingatia maneno yaliyotumiwa pamoja na mkondo wa hadithi kwa jumla.
Unapotunga maswali inafaa uulize maswali ambayo yanatoa kwa mwanafunzi
fursa ya kujieleza kwa mfululizo wa maneno. Usiulize maswali yanayoweza kujibiwa
kwa neno moja tu: siyo, ndiyo, hapana! Ikiwa swali linahitaji jibu la aina hiyo inafaa
mwanafunzi aagizwe kutoa hoja za kutilia nguvu jibu lake. Inafaa aeleze kwa nini
anasema ndiyo au hapana.
Kuhusu maswali yanayolenga kutathimini ufahamu wa lugha inafaa yaulizwe kwa
kurejelea kipengele kinachotahiniwa katika mkutadha wa sentensi kinamotumiwa.
Maneno au mafungu ya maneno yasiulizwe maana yake bila kuhusishwa na mkutadha wa
matumizi yake katika kifungu kilichosomwa. Sababu mojawapo ya kufanya hivi ni
kusaidia wanafunzi kujizoeza kutafuta maana kwa kuzingatia mkutadha. Maana ya neno
inaweza kubadilika kulingana na mkutadha ambamo limetumiwa. Tuseme kwa mfano
maneno yafuatayo yametumiwa katika kifungu kilichosomwa: donge, chai. Utakuwa
umeuliza vibaya ukimwambia mwanafunzi:
Eleza maana ya maneno yafuatayo:
(a) donge
(b) chai
Njia bora zaidi ni kunukuu sentensi ambamo maneno hayo yametumiwa na
kumtaka mwanafunzi aeleze maana ya maneno hayo kulingana na matumizi yake katika
sentensi.
74
ZOEZI 6.4
Ukirejelea kifungu mahsusi cha kusoma eleza hatua
ambazo utachukua kuwasaidia wanafunzi wako
kukisoma kifungu hicho na kufahamu ipasavyo yale
wasomayo.
6.5 Kuandika Ufupisho
Ufupisho ni aina ya mawasiliano ambayo kwayo ujumbe fulani unaopokelewa na
msomaji au msikilizaji unawasilishwa upya kwa njia ya mkato inayozingatia tu hoja
muhimu. Zoezi la kuandika ufupisho ni muhimu kwa mwanafunzi kwa sababu linasaidia
kukuza stadi ya kusoma kwa ufahamu. Ni aina fulani ya kufahamu kwa sababu uwezo wa
mwanafunzi wa kufupisha unategemea kiwango chake cha kufahamu yale asomayo.
Asipofahamu vizuri asomayo itamwia vigumu kufupisha kwa usahihi. Pia zoezi hili latoa
nafasi kwa mwanafunzi ya kuendeleza na kupanua ujuzi wake wa lugha. Kwa ufupi zoezi
hili linachangia kuelekeza mwanafunzi katika mambo yafuatayo:
Kusoma kwa makini na dhati.
Kung’amua hoja muhimu.
Kutambua uhusiano kati ya hoja tofauti.
Kujieleza kwa ufupi bila kurudiarudia wala kupotosha ujumbe.
Kujieleza kwa lugha yenye mtiririko na mpangilio mzuri wa mawazo.
Je, unaweza kuwaongoza vipi wanafunzi wako ili waibuke na ufupisho wa
kuridisha? Unaweza kuwaongoza kwa kupitia mfuatano wa hatua zifuatazo:
Usomaji wa kifungu chote cha taarifa.
Udondozi wa hoja aya kwa aya.
Mchujo wa hoja zilizodondolewa.
Kuandika kwa kuunganisha hoja zilizoteuliwa.
Kutathimini ufupisho kwa kuulinganisha na kifungu asilia.
Kwa ufupi, kabla wanafunzi hawajajishughulisha na kazi ya kufupisha ni wajibu
wako kuona kwamba wanakipitia kifungu kinachohusika ili kutambua maudhui yake
muhimu. Kisha majadiliano yanaweza kuibuka juu ya maudhui hayo. Wakati huo huo
matatizo ya lugha yanaweza kushughulikiwa. Baada ya majadiliano hayo sasa unaweza
kuwauliza wanafunzi maswali yanayolenga kuwaongoza kutaja hoja ndogo ndogo
ambazo mwandishi anatoa katika juhudi za kujenga na kutilia maki hoja yake kuu.
Kifungu kizima kichambuliwe aya kwa aya na kisha baadaye hoja hizo zipangwe kwa
mtiririko mzuri wa mawazo. Hoja ziteuliwe kulingana na uzito wake katika kuendeleza
maudhui yanayohusika. Swali la kuuliza hapa ni: Je, hoja hii inachangia kutilia maki
maudhui au la? Ni marudio kwa namna nyingine ya hoja iliyotajwa tayari? Ni hoja
ambayo inaweza kujisimamia yenyewe au la? Kama inaweza kujitegemea inafaa
kuhifadhiwa, lakini kama haiwezi itupiliwe mbali.
75
Baada ya kuzichagua hoja zote, zipangwe kulingana na uzito wake. Kisha
unaweza kuwaagiza wanafunzi waanze kuandika ufupisho wao bila kurejelea kifungu cha
taarifa kinachohusika wala kukikariri neno kwa neno. Wanafunzi wakimaliza kuandika
ufupisho wao kila mwanafunzi ahimizwe kusoma ufupisho wake na kuulinganisha na
kifungu asilia kuhakikisha kwamba maudhui yake yamezingatiwa vilivyo. Vile vile
lugha, mtiririko na uhusiano wa mawazo vichunguzwe na kutiliwa maanani.
Maelezo haya yamejishughulisha zaidi na mapendekezo kuhusu jinsi unavyoweza
kuongoza wanafunzi waweze kufupisha kifungu chenye ukubwa wa zaidi ya aya moja.
Lakini kabla mwanafunzi hajafikia kiwango cha uwezo wa kufupisha vifungu nya aina
hii anapaswa kuwa na uzoefu wa kueleza ujumbe kwa ufupi kupitia mazoezi kama
yafuatayo:
Kusoma na kupendekeza vichwa vinavyofaa kwa vifungu vya taarifa
visomwavyo.
Kupanga kwa mtiririko mzuri baadhi ya sentensi zilizopangwa kwa mfuatano
usiyofaa.
Kuandika kwa ufupi sentensi zinazowasilisha ujumbe kwa mtindo wa
kujirudiarudia
Mwanafunzi anapofanya zoezi hili la mwisho anaweza akaambiwa ataje maneno
katika sentensi hiyo ambayo yana maana sawa kabla hajaiandika upya. Ikiwa kuna
vifungu vya maneno ambayo maana yake inaweza kuwasilishwa kwa maneno machache
zaidi au kwa neno moja moja mwanafunzi anaweza kuagizwa ataje vifungu hivyo na
kupendekeza njia ya mkato inayoweza kutumiwa kuwasilisha ujumbe unaowasilishwa na
vifungu hivyo vya maneno. Ifuatayo ni mifano ya kubainisha jambo hili:
(a) Akina mama na baba, wasichana na wavulana ambao wanaishi katika mtaa
wa Sokomjinga, na ambao siku mbili zilizopita hawakuweza kuhudhuria
mkutano wa harambe uliyofanyika wakati huo na kutoa mchango wao
wanaarifiwa sasa kuwa mkutano mwingine kama huo utafanywa tena katika
muda wa siku tatu zijazo. Kila mtu anahimizwa kutoa mchango wa aina yo
yote kulingana na uwezo wake, iwe pesa, kuku, mbuzi, kondoo, bata au
machungwa, maembe, mapapai na kadhalika.
(b) Mwanaume mmoja mwenye asili ya Kihindi alijikuta mashakani wakati
ambapo alipelekwa mahakamani. Baada ya kushitakiwa na kusikilizwa kwa
kesi yake makama ilimhukumu kwenda jela na kukaa ndani yake pamoja na
wafungwa wengine kwa muda usiyozidi wala kupungua miezi kumi na miwili
hivi baada ya mahakama kumpata na hatia ya kuingia na kuanza kufanya
kazi nchini bila kuwa na kibali rasmi kinyume na masharti ya sheria za nchi
yetu
Sentensi kama hizi ni kielelezo cha matumizi ya lugha kwa njia ya mzunguko.
Unaweza kutumia mifano kama hii kutayarisha wanafunzi kwa zoezi la kuandika
ufupisho. Kabla wanafunzi hawajafanya ufupisho inakubidi mwenyewe ufanye ufupisho
wako. Pia kabla wanafunzi hawajajaribu kuzifupisha unaweza kujadiliana nao juu yake ili watoe maoni yao juu yake. Wanapomaliza kuzifupisha, ufupisho wa wanafunzi
ulinganishwe na wanafunzi wengine watoe maoni yao juu yake.
76
ZOEZI 6.5
A. Eleza maana ya ufupisho na umuhimu wa kuufundisha
katika mpango wa kufundisha lugha.
B. Utajua namna gani kuwa mwanafunzi ameandika
ufupisho wa kuridhisha?
C. (i) Andika vifungu vitatu kila kifungu kikiwa na
sentensi zisizozidi tatu zinazoeleza juu ya maudhui
fulani kwa njia ya mzunguko.
(ii) Eleza jinsi utakavyofundisha kila mojawapo ya
vifungu hivyo.
6.6 Kuandika Imla.
Umuhimu wa zoezi la imla kwa mwanafunzi ni kwamba linamfanya ajitahidi
kusikiliza kwa makini. Pia kupitia zoezi hili, mwanafunzi anajifunza jinsi ya kuendeleza
maneno pamoja na kuzingatia masharti ya kuwakifisha. Pamoja na hayo, mwanafunzi
anaposhiriki katika zoezi la imla anapata fursa ya kukuza uwezo wake wa kukumbuka
yale anayoyasikia.
Je, ni mbinu gani ambazo unaweza kutumia kufundisha imla?
Unapaswa kwanza kutambua kwamba zoezi la imla linahusisha uwezo wa namna
mbili kwa wakati mmoja. Mwanafunzi anaposhirikishwa katika zoezi hili anapaswa
kwanza kukumbuka maneno ambayo anasikia, na kisha baadaye anatakiwa kuandika
maneno hayo kwa njia iliyo sahihi. Kwa hivyo, wewe kama mwalimu ni sharti uelewe
vizuri ni lipi kati ya mambo haya mawili unataka kushughulikia. Hata hivyo, kwa vyo
vyote vile ni lazima uhakikishe kuwa kazi ambayo unapatia wanafunzi haihusishi mambo
mengi magumu. Lengo la kazi ya imla siyo kuwakanganya wanafunzi na kuwatumbukiza
katika ufanyaji wa makosa, bali ni kuendeleza uwezo wao wa kusikia maneno
yanapotamkwa na kisha kuyaandika kama inavyotakikana kulingana na masharti ya
uwakifishaji.
Unapotoa zoezi la imla uanshauriwa kutilia maanani mambo haya yafuatayo:
Kusoma na kutamka maneno kwa njia sahihi bila kupotosha maana.
Kusoma kwa kuzingatia mafungu mazima ya maneno yaletayo maana.
Maneno au sentensi vinavyotakwa kuandikwa visomwe mara ya kwanza mara
moja. Kisha vikishomwa kwa mara ya pili wanafunzi waandike.
Kuhimiza wanafunzi kusema kimoyomoyo, bila kufungua midomo, yale
wanayosikia. Pia wafanye vivyo hivyo wakati wanapoandika.
Wanafunzi wakimaliza kuandika, wasomee tena kazi inayohusika ili waweze
kusikiliza tena na kurekebisha kazi yao ikiwa kuna haja ya kufanya hivyo.
77
N. B. Ikiwa lengo lako hasa ni kutilia mkazo uandikaji wa maneno maalum inafaa
maneno hayo uyatumie katika sentensi halafu uwambie wanafunzi waandike maneno
hayo tu badala ya kuandika sentensi nzima. Mfano:
(a). Andika neno dhamini katika sentensi ifuatayo:
Masumbuko anatafuta bado mdhamini wa kumlipia mtoto wake karo
(c) Andika neno chombo katika sentensi ifuatayo:
Chombo cha kupikia samaki chanuka shombo.
ZOEZI 6.6
A. “Imla haifai kama njia ya kufundishia Kiswahili”.
Jadili.
B. Kwa maoni yako, kusema kimoyomoyo kuna faida
gani kwa mwanafunzi wakati anapofanya zoezi la
kuandika imla?
6.7 Umuhimu Wa Uandishi Wa Insha
Insha ni mtungo wa kinathari ulioandikwa juu ya mada fulani na kupangwa kwa
mfululizo wa aya. Mwanafunzi anapoandika insha huwa anajieleza juu ya jambo fulani
kwa mtiririko wa mawazo ambayo yamepangwa katika aya tofauti zinazofuatana kwa
utaratibu maalum. Ili mwanafunzi aweze kujieleza ni sharti atumie lugha, ambayo ni
chombo muhimu cha kumfanikishia malengo yake ya kimawasiliano. Kutokana na
ukweli huu ni wazi kwamba zoezi la uandishi wa insha linatoa nafasi kwa mwanafunzi ya
kufanya mazoezi ya lugha. Kupitia zoezi hili, kwa mfano, mwanafunzi hupata nafasi ya
kutumia msamiati wa aina tofauti pamoja na madondoo mbalimbali ya kisarufi.
Anapoandika insha za aina tofauti huwa anajifunza kutumia Kiswahili kwa adabu
kulingana na mikutadha tofauti ya mawasiliano.
Jambo jingine ni kwamba uandishi wa insha hutoa changamoto kwa mwanafunzi
kufikiria juu ya mada ambazo anatarajiwa kuandika juu yake. Hali kama hii humsaidia
kuwa na nidhamu, kujenga na kupanua fikra zake. Zaidi ya haya mwanafunzi
anapoandika huwa anafanya mazoezi ambayo yanamsaidia kuimarisha ujuzi wa kanuni
zinazotawala uandishi wa Kiswahili.
Wewe kama mwalimu unapaswa kuutambua umuhimu wa zoezi hili. Jambo hili
litakusaidia kupata fununu juu ya mambo ambayo unastahili kutilia mkazo
unaposhirikisha wanafunzi katika kazi ya kuandika insha.
Licha ya kutambua umuhimu wa zoezi ni sharti pia ufahamikiwe vizuri malengo
ya zoezi hili. Je, kwa maoni yako ufundishaji wa kuandika insha unapaswa kuwa na
malengo gani? Kwa njia ya ufupi tunaweza kusema kwamba lengo lake ni : kumsaidia
mwanafunzi aweze kujieleza juu ya mada fulani akiandika kwa utoshelevu wa mawazo,
mtiririko bora wa mawazo na kwa usahihi wa lugha.
Kwa kurejelea kauli hii inabainika kwamba unapofundisha uandishi wa insha
unapashwa kutilia maanani mambo yafuatayo:
78
Utoshelevu wa mawazo.
Mtiririko wa mawazo.
Matumizi ya lugha na
Maandishi .
Ni sharti kuona kwamba unasaidia wanafunzi wako kuzingatia mambo hayo
katika insha zao kwa sababu, kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya waalimu, wanafunzi
wengi wanaandika insha ambazo haziridhishi kutokana na kushindwa kuzingatia
utimizaji bora wa mambo hayo yaliyotajwa. Usipowasaidia kuhusu mambo hayo
watakosa kuwa na msingi bora wa uandishi wa insha. Pia huenda wakazoea kufanya
makosa ambayo yasipokomeshwa mapema yatakuwia magumu kuyarekebisha. Baadhi
yao wanashindwa kuzingatia kikamilifu anwani ya insha na kufafanua mawazo juu yake.
Wanakumbwa pia na shida ya kupanga mawazo yao kwa njia nzuri. Kutokana na hali ya
kupungukiwa mawazo wanafunzi wanashindwa kujikita katika anwani ya insha na
kuandika mambo ambayo hayana uhusiano wo wote nayo.
Njia moja ya kukabiliana na matatizo ya namna hii ni kuhakikisha kwamba wewe
kama mwalimu huwashirikishi wanafunzi wako moja kwa moja katika uandishi bila
mwongozo unaofaa. Wanafunzi, hasa wa vidato vya chini inafaa washirikishwe kwanza
katika kuandika insha za mwongozo. Unapowashirikisha katika uandishi wa insha za aina
hii unaweza kuwaongoza kuibuka na insha nzuri kwa kutilia maanani mambo kama vile:
anwani, mawazo na lugha.
Anwani ni kichwa cha mambo ambayo unataka wanafunzi wayaandike.
Unapaswa kuchagua anwani hiyo kwa uangalifu sana ukitilia maanani uwezo wa
wanafunzi. Usiwe na mazoea ya kuchagua anwani ya aina yo yote na kuwapatia
wanafunzi waandike juu yake. Anwani hiyo ikiwa ngumu au kama haina maagizo
yanayoeleweka vizuri, wanafunzi watashindwa kujieleza vizuri juu yake. Kwa hivyo ni
lazima uchague anwani ambayo itampa mwanafunzi fursa ya kueleza mawazo yake
kadiri ya uwezo wake. Akipewa anwani ngumu atashindwa kupata mawazo na matokeo
yake yatakuwa kwamba mwanafunzi ataandika mambo mengine ambayo hayana
uhusiano na anwani hiyo. Ili kuziuia matokeo kama haya unashauriwa uwape wanafunzi
anwani ambazo zinaambatana na hali ya mambo katika maisha yao. Pia baada ya kuwapa
anwani ambayo unatarajia waandike juu yake ni sharti uhakikishe kwamba wanaelewa
vizuri kile ambacho wanatarajiwa kuandika juu ya anwani hiyo. Ni lazima utoe maagizo
ambayo yanaeleweka wazi. Maagizo kama yafuatayo kwa mfano hayafai:
(a) Andika insha kuhusu mmomonyoko wa udongo.
(b) Andika kuhusu ajali.
Je, maagizo haya yana kasoro gani?
79
ZOEZI 6.7
A. Jadili umuhimu wa kushirikisha wafunzi katika uandishi
wa insha.
B. (i) Kuna tofauti gani kati ya insha ya mwongozo na
insha isiyo ya mwongozo?
(ii) Ukitoa mifano ya kutetea jibu lako eleza kwa nini
wanafunzi wa vidato vya chini hawastahili kuandika
insha zisizo za mwongozo.
Kuongoza Wanafunzi
Lengo la kuongoza wanafunzi ni kuzuia ufanyaji wa makosa ya aina mbali mbali.
Unatoa mwongozo ili wanafunzi wako waweze kuandika insha zenye utoshelevu wa
mawazo, mtiririko bora wa mawazo, usahihi wa lugha na mtindo unaofaa. Unaweza
kuwaongoza wanafunzi kwa kutumia mbinu tofauti kulingana na kiwango cha ujuzi wao
pamoja na aina ya vifaa vya kufundishia vinavyopatikana. Miongoni mwa mbinu hizo ni
pamoja na:
Majadiliano
Vifaa vya maono
Vidokezi vya maneno
Mfano kamili wa insha
Majibu ya maswali
Upangaji wa sentensi.
Majadiliano
Baada ya kuteua anwani ya insha usiwapatie wanafunzi na kuwaagiza waandike
juu yake moja kwa moja. Ni jukumu lako kuona kwamba wanapewa maandalizi mazuri
ya kuwasaidia kushughulikia anwani inayohusika kikamilifu. Majadiliano hayo
yanalenga kufafanua anwani ya insha na kuelekeza wanafunzi kuhusu matarajio ya insha
inayohusika. Ni muhimu kwa sababu, licha ya kutoa nafasi kwa wanafunzi ya kujieleza
katika mazungumzo, yanawasaidia kukusanya mawazo kuhusu anwani ya insha.
Majadiliano juu ya anwani yanasaidia kupanua fikra za wanafunzi juu ya anwani na
kuipa insha yao mwelekeo unaofaa. Jambo hili linapunguza ile hali ya kupungukiwa
haraka mawazo na kuanza kuandika nje ya anwani.
80
Wakati wa majadiliano, kila mwanafunzi ahimizwe kutoa mchango wake. Hoja
zinazotolewa ziandikwe kwa ufupi kwenye ubao. Kisha wanafunzi, wakiongozwa nawe,
watoe mapendekezo kuhusu jinsi hoja hizo zinavyofaa kufuatanishwa katika aya tofauti
za insha. Wapendekeze mgawanyiko wa hoja katika aya tofauti.
Vifaa vya maono.
Kama ilivyoelezwa hapo awali, wanafunzi mara nyingi wanakumbwa na tatizo la
upungufu wa mawazo. Njia moja ya kusaidia wanafunzi kukusanya mawazo ya
kuwasaidia katika insha zao ni kutumia vifaa vya maono kama vile vitu halisi, michoro,
picha, vibonzo n k…. Ukiamua kutumia kifaa cha maono unapaswa kuchagua kifaa
kinachobainisha mambo tofauti tofauti ambayo mwanafunzi anaweza kuyazungumzia
katika insha yake. Unaweza kuwaongoza wanafunzi kwa kuwauliza maswali kadhaa juu
ya kifaa kinachohusika. Kila mwanafunzi ajaribu kueleza kile anachokiona. Uzuri wa
kifaa hiki ni kwamba kinatoa mkutadha mzuri wa kuendeleza mazoezi ya kutumia
msamiati na sarufi. Ukirejelea kifaa hicho unaweza kuwapa wanafunzi vidokezo vya
maneno ambayo wanaweza kuyatumia katika insha yao.
Uteuzi wako wa kifaa utategemea lengo la insha ambayo wanafunzi wanatarajiwa
kuandika. Vifaa fulani, kwa mfano vinafaa kwa insha za maelezo wakati ambapo vingine
vinaweza kuibua mawazo yanayofaa kwa insha za masimulizi. Ikiwa huwezi kupata kwa
urahisi vifaa vinavyoweza kuyakidhi mahitaji yako usisite kujitayarishia vifaa vyako
mwenyewe, au kutafuta msaada wa watu wengine wenye ujuzi wa kutayarisha vifaa
hivyo. Kwa mfano baada ya kusoma kisa fulani cha kusisimua unaweza kufikiria jinsi
unavyoweza kuwasilisha matukio katika kisa hicho kwa njia ya maono. Kama wewe
huna kipawa cha uchoraji unaweza kumtafuta mtu mwenye kipawa na kumwomba
akuchoree (picha) mchoro unaoonyesha matukio muhimu katika hadithi uliyosoma.
Kisha unaweza kutumia mchoro huo kama chombo cha kufundishia insha ya masimulizi.
Unapofika darasani unaonyesha mchoro wako wanafunzi watoe maelezo yao kuhusu kile
kinachoendelea. Mbali na kueleza kile ambacho wanafikiri kinaendelea, wanafunzi
wanaweza kujaribu kupendekeza anwani ambazo kwa maoni yao zinafaa kueleza
matukio katika mchoro unaohusika. Ukitaka unaweza kuchagua moja kati ya anwani
zilizopendekezwa na kuwataka wanafunzi wako waandike insha yenye anwani hiyo.
Ukifanya hivyo utawahamasisha wanafunzi kwa kuwa watahisi kwamba hata wenyewe
walishirikishwa katika uteuzi wa kazi ya uandishi.
Utumiaji wa vifaa vya maono ni njia bora ya kulipa somo uhai na kulipunguzia
ukavu. Hulifanya somo kuwa la kuvutia kwa wanafunzi.
Videkezo Vya Maneno.
Ukitaka wanafunzi waandike kuhusu anwani fulani unaweza kuwapa vidokezi
vya maneno ili kuwasaidia wakati wanapoandika. Unachagua maneno hayo kwa kutilia
maanani lengo la insha. Haimanishi kwamba ni lazima kwa wanafunzi kutumia maneno
ambayo umependekeza. Si lazima pia kwao kuyatumia yote.
Tuseme kwamba unataka wanafunzi wako waandike insha ya kubuni kuhusu ajali
ya gari ambayo walishuhudia. Unaweza kuwapatia vidokezo kama vifuatavyo:
Jumamosi jioni, kijana na wenzake, gari la kifahari, kulewa chakari, mvua nyingi,
barabara kuteleza, mtelemko, gari ya mbele kusimama ghafla, piga breki, kosa
81
mwelekeo, gari kupinduka, mayoe, damu kutiririka, wasamaria wema, majeruhi
kupelekwa hospitalini n k…. Matokeo ya kuwapatia wanafunzi vidokezo vya maneno ni kuwa wanapata
mazoezi ya kujieleza wakitumia maneno fulani bila usumbufu mwingi.
Mfano Kamili Wa Insha.
Kuna waalimu ambo wana mazoea ya kufundisha uandishi wa insha kwa kutoa
maelezo tu kuhusu muundo wa insha na mitindo ya kuandika aina tofauti za insha.
Ufundishaji wa namna hii hauna faida yo yote. Wanafunzi hawawezi kujifunza kuandika
kwa kusikiliza tu maelezo yako. Inafaa uwatolee mifano kamili ya insha zilizoandikwa na
watu wengine. Kisha zungumzia vipengele vya insha unavyotaka kueleza kwa kurejelea
mfano mahsusi wa insha. Ukitaka kwa mfano kuzungumzia sehemu tofauti za insha
inafaa uwapatie nakala ya insha uzungumzie sehemu hizo hatua kwa hatua ukirejelea
nakala uliyowapatia wanafunzi. Sehemu hizo ambazo inafaa utilie mkazo ni: utangulizi,
katikati na mwisho. Pamoja na sehemu hizi inafaa uzungumzie aya kama kiungo muhimu
cha insha. Wasaidie wanafunzi kuelewa kila mojawapo ya sehemu hizo kwa kuwauliza
maswali yaliyojikita katika mfano wa insha uliotolewa. Ukiwaeleza umuhimu wa sehemu
hizo kwa kuambatanisha maelezo yako na mfano mahsusi wataelewa vizuri zaidi kuliko
vile wangeelewa bila kuwa na mfano wa kurejelea.
Baada ya kuwaonyesha mifano kamili ya insha unaweza sasa kuwashirikisha kwa
kuwapa kazi ya kuandika wakijishughulisha na sehemu moja tu ya insha. Baada ya
kuwapa, kwa mfano, anwani ya insha unaweza kumwambia kila mwanafunzi aandike
sentensi moja inayoweza kuwa utangulizi wa insha wanayotarajiwa kuandika.
Wakimaliza kuandika wapewe fursa ya kusoma sentensi zao. Kisha wape mawaidha
kuhusu lengo la sentensi ya utangulizi.
Njia nyingine ya kuwaongoza wanafunzi ni kutoa mfano wa utangulizi wa insha
na kuwataka wakamilishe kwa kuandika sehemu nyingine. Unaweza pia kuawatolea
hitimisho na kuwataka waandike utangulizi na sehemu ya katikati vinavyofaa
kukamilisha insha.
Majibu Ya Maswali.
Njia nyingine ya kusaidia wanafunzi kupata na kupanga mawazo wanayohitaji
katika insha ni kuwauliza kwa utaratibu maswali ambayo yakijibiwa, majibu yake
yanaweza kuleta habari kamili. Mbinu hii inafaa sana, kwa mfano, unapowataka
wanafunzi kuandika insha ya maelezo. Lengo hasa la kuuliza maswali ni kutoa fursa kwa
wanafunzi ya kufikiria kwa mapana juu ya mada wanayotarajiwa kuandika juu yake.
Huwasaidia kutilia maanani vipengele vya mada ambavyo, pengine, wasingefikiria juu
yake. Ni wajibu wako kama mwalimu kuona kwamba, kupitia maswali unayomwuliza
unamsaidia mwanafunzi kuzingatia mada inayohusika kikamilifu. Tuseme, kwa mfano,
unataka wanafunzi waandike insha wakieleza matokeo mbali mbali ambayo
yameonekana tangu utekelezaji wa masharti mapya katika magari ya abiria. Unaweza
kutoa maagizo kama yafuatayo: Andika insha isiyokosa kujaza angalau kurasa tano za
daftari ukieleza jinsi utekelezaji wa masharti mapya kwa magari ya usafiri wa umma
ulivyoathiri na kuendelea kuathiri watu katika eneo lako.
Mfano wa maswali unayoweza kuuliza ni kama vile:
82
Eneo lako ni la mjini au shambani?
Masharti mapya yanuhusu nini? Yalianza kutekelezwa lini?
Kwa nini waziri wa uchukuzi aliwajibika kuweka masharti haya mapya?
Masharti haya yalipokelewa vipi na watu wa tabaka mbali mbali.
Je, utekelezaji wa masharti haya umekuwa na matokeo gani kwa wananchi
ambao hutetgemea magari ya umma?
N.B: Sambamba na maswali haya unaweza kuwaonyesha wanafunzi picha za
magazetini. Unaweza pia kuwahimiza wasome magazeti yanayozungumzia tukio hili.
Upangaji Wa Sentensi;
Ili kuendeleza uwezo wa wanafunzi wa kupanga vizuri sentensi katika aya
unaweza kuwapatia sentensi kadhaa ambazo zimefuatanishwa vibaya na kuwaagiza
wazipange upya kwa mtiririko bora. Zoezi la kupanga sentensi katika mtiririko unaofaa
hutoa nafasi kwa wanafunzi ya kujizoesha kuandika wakizingatia mtiririko wa kimantinki
na kiwakati. Ni wajibu wako kuona kwamba unapotoa mazoezi ya kupanga sentensi
unazingatia aina zote mbili za mtiririko. Wapewe mazoezi ya kupanga sentensi kwa
msingi wa kimantiki pamoja na mfuatano wa matukio kiwakati. Ufuatao ni mfano wa
zoezi la sentensi ambazo zimefuatanishwa vibaya.:
(a) Kisha lilianza kumporomoshea makombora ya ngumi kama kwamba lilikuwa
limerukwa na akili. Ghafla jambazi moja lilitokea likauchovya mfuko wa
kijana huyo. Ulikuwa wakati wa asubuhi. Kufumba na kufumbua, utingo
aliligeukia na kulikaba kooni, lakini liliweza kujisalimisha kwa kumrushia
teke tumboni.
Juzi juzi wakazi wa mtaa wa Somali mjini Kakamega walijionea sinema ya bure
na kutumbuizwa kwa mchezo wa ndondi.
Kisha alichomeka pesa yake katika mfuko wa nyuma wa suruali yake na
kujitayarisha kuingia ndani ya gari. Utingo mmoja alikuwa tayari kumwarifu dreva
aondoe gari kwa sababu lilikuwa limejaa tayari. Aliondoa kibao cha kutangazia wasafiri
mwisho wa safari:
(b) Mtiririko unaofaa:
Juzi juzi wakazi wa mtaa wa Somali mjini Kakamega walijionea sinema ya bure
na kutumbuizwa kwa mchezo wa ndondi.
Ulikuwa wakati wa asubuhi. Utingo mmoja alikuwa tayari kumwarifu dreva
aondoe gari kwa sababu lilikuwa limejaa. Aliondoa kibao cha kutangazia wasafiri
mwisho wa safari. Kisha alichomeka pesa yake katika mfuko wa nyuma wa suruali yake
na kujitayarisha kuingia ndani ya gari.
Ghafla, jambazi moja lilitokea likauchovya mfuko wa kijana huyo. Kufumba na
kufumbua, utingo aliligeukia na kulikaba kooni, lakini liliweza kujisalimisha kwa
kumrushia teke tumboni. Kisha lilianza kumporomoshea makombora ya ngumi kama
kwamba lilikuwa limerukwa na akili.
83
ZOEZI 6.8
A (i) Toa hoja za kutetea na kupinga mazoea ya waalimu ya
kuwapatia wanafunzi insha za mwongozo.
(iii) Je, kulingana na maoni yako wanafunzi wanastahili
kuongozwa kwa kiasi gani?
C. Andika anwani yo yote ya insha ambayo ungetaka wanafunzi
wa kidato fulani (kitaje) waandike insha juu yake. Kisha eleza
kinagaubaga jinsi utakavyoelekeza na kuwasaidia wanafunzi
kuandika juu ya anwani hiyo insha yenye utoshelevu wa
mawazo na mtiririko bora.
Usahihishaji.
Je ni mambo gani ambayo unapaswa kuchunguza na kuzingatia unaposahisha
insha za wanafunzi na kuwapatia alama?
Miongoni mwa mambo muhimu ambayo unashauriwa kutilia maanani wakati wa
kusahihisha insha ni pamoja na:
Sarufi
Msamiati
Maudhui
Mtindo
Kuhusu sarufi unapaswa kuchunguza jinsi mwanafunzi anavyozingatia kanuni za
utungaji wa sentensi. Kwa mfano, unachunguza jinsi mwanafunzi anavyotumia
viambisho vya ngeli kulingana na ngeli tofauti za majina na mambo mengine
yanayohusiana na sarufi ya lugha.
Kwa upande wa msamiati, unachunguza uteuzi wa maneno. Je, mwanafunzi
ameteua maneno yanayofaa kulingana na maudhui ya insha? Je maneno hayo
ameyatumia kwa usahihi au la?
Swali muhimu la kuuliza kuhusu maudhui ni ikiwa mwanafunzi amezingatia
kikamilifu mada inayohusika au amekiuka maagizo aliyopewa. Ametoa hoja za kutosha
kuendeleza maudhui ya insha kwa kadiri ya kiwango cha ujuzi wake?
Mtindo kwa upande mwingine unahusu mambo kama vile mtiririko wa sentensi
katika aya na mtiririko wa aya katika insha nzima. Unahusu vile vile unadhifu wa kazi,
kusomeka kwa mwandiko, utumizi wa herufi kubwa na ndogo kwa usahihi, maendelezo
ya maneno na utumiaji wa vituo.
Ni lazima uwe na mwongozo ambao unaonyesha alama ambazo utatoa kwa kila
mojawapo ya mambo hayo. Jumla ya alama ambazo mwanafunzi atapewa inafaa iwe
kielelezo bora cha uwezo wa mwanafunzi katika vipengele tofauti vya uandishi wake.
84
Hali kadhalika, unashauriwa kuwa na mtindo wa kusahihisha ambao unatoa fursa
kwa wanafunzi ya kutambua makosa yao na kuyasahihisha wao wenyewe. Unaweza kwa
mfano kupiga mstari chini ya kosa na kuonyesha aina ya kosa kwa kutumia alama
mahsusi. Ni lazima uhakikishe kwamba wanafunzi wanafahamu vizuri maana ya alama
unazotumia. Mfano wa alama hizo ni kama vile:
Sf: sarufi
Ms: msamiati
Mt: mtindo
Mz: maendelezo
Mfano wa mwongozo wa kusahihisha:
Hitimisho
Somo hili na lile la tano ni masomo ambayo yamejishughulisha na stadi za
kiisimu ambazo ni kama uti wa mgongo wa lugha. Stadi hizi ni: Kusikiliza, Kuongea,
Kusoma na Kuandika. Hizi ni stadi ambazo zinaingiliana na kutiliana nguvu. Kusikiliza
na kuongea ni stadi ambazo zinajikita katika lugha andishi.
Kwa upande mwingine, Kusikiliza na Kusoma ni stadi ambazo zinahusu upokezi
wa habari wakati ambapo Kusema na Kuandika ni stadi zinazohusu upashaji wa habari.
Kwa mujibu wa wataalamu, stadi hizi zinachukua asilimia ifuatayo ya shughuli za
mawasiliano ya kila siku:
Je unaweza kujifunza nini kuhusu mkabala wa kufundisha Kiswahili kutokana na
tarakwimu hizi?
Stadi Asilimia
Kusikiliza
Kuongea
Kusoma
Kuandika
45%
30%
16%
09%
Sarufi
Msamiati
Maudhui
Mtindo
6
5
5
4
Jumla 20
85
SOMO LA 7
SARUFI NA MATUMIZI YA LUGHA (MSAMIATI NA SARUFI)
7.0 Utangulizi:
Mtu anapojifunza lugha ni lazima aumudu msamiati pamoja na sarufi yake.
Msamiati ni jumla ya maneno yanayopatikana katika lugha, na sarufi ni mfumo wa
kanuni zinazotawala utaratibu wa kutumia maneno katika vielelezo vya sentensi. Neno
pekee halina maana kamili, ila tu liwe limetumika katika mpangilio wa maneno mengine.
Haina faida kwa mtu kujifunza maneno chungu nzima kama hana uwezo wa kutumia
maneno hayo katika vielelezo sahihi vya sentensi.
Kwa hivyo ufundishaji wa msamiati ni lazima uambatanishwe na ufundishaji wa
sarufi.
Madhumuni.
Kufikia mwisho wa somo hili inatarajiwa kuwa utaweza:
(i) Kueleza matatizo ya kimsamiati na kisarufi yanayowakumba
wanafunzi kutokana na athari za lugha zao za mama.
(ii) Kupendekeza na kueleza mbinu ambazo unaweza kutumia
kusaidia wanafunzi kupanua upeo wa msamiati na kuutumia
ipasavyo.
(iii) Kupendekeza na kueleza mbinu mbali mbali unazoweza
kutumia kukuza uwezo wa kisarufi wa mwanafunzi
7.1 Matatizo Ya Kimsamiati Na Kisarufi.
(a) Msamiati
Mtu anapojifunza lugha yake ya mama anazoea namna fulani ya kutumia maneno
kuashiria vitu na kuzungumzia dhana tofauti kufuatana na mfumo wa kanuni za lugha ya
jamii fulani. Kisha mtu huyu anapojaribu kujifunza lugha nyingine analazimika
kuzungumzia ukweli ambao anaujua tayari kwa kutumia maneno yaliyo tofauti na yale ya
lugha yake ya mama. Kwa mfano, kuna lugha zinazotumia neno moja tu kuzungumzia
kile kitendo cha kusafisha vyombo na nguo kwa kutumia maji. Kinyume na lugha hizi,
lugha ya Kiswahili inatumia vitenzi tofauti kulingana na kile kinachosafishwa. Kwa
hivyo wanafunzi kutoka jamii ambazo lugha zao hutumia neno moja tu itawalazimu
kujifunza kuzungumzia mambo ambayo tayari wana uzoefu nayo, kwa msingi wa
mtazamo wa lugha ya Kiswahili.
Matokeo ya hali kama hii ni kwamba wakati mwingine wanafunzi hushindwa
kufuata mfumo wa lugha ya Kiswahili na kuishia kwa kufanya makosa ya kimsamiati.
Wanafanya makosa kwa sababu inakuwa vigumu kwao kuacha kufikiria kwa njia
86
ambayo wamezoea na kuanza kufikiria kwa njia mpya. Kwa ufupi mwanafunzi anaweza
kufanya makosa katika kiwango cha msamiati kutokana na sababu kama zifuatazo:
Maneno yenye umbo sawa / karibu sawa kuwa na maana tofauti.
Maneno yenye umbo sawa / karibu sawa kuwa na maenezi tofauti ya maana.
Kuwasilisha kwa neno moja dhana zinazowasilishwa kwa maneno tofauti.
Ukweli ni kwamba kuna baadhi ya maneno katika Kiswahili na lugha za
wanafunzi ambayo yanafanana au yanakaribiana kimaumbo lakini yana maana tofauti
katika lugha zote mbili. Asipokuwa mwangalifu au asipoelezwa, mwanafunzi anaweza
kufikiri kwamba neno la Kiswahili lina maana ile ile ya lugha ya jamii yake. Na
akilitumia kwa maana hiyo hiyo ataeleweka visivyo, na watu wengine wakitumia neno
hilo hilo kwa maana ya Kiswahili huenda asielewe kama ilivyotarajiwa. Kwa mfano
katika Kiluhya kuna neno indama ambalo linakaribiana na neno ndama la Kiswahili.
Wakati mmoja neno ndama lilitumiwa katika kifungu cha habari ambacho wanafunzi
walitakiwa kusoma wakati wa kipindi cha Kiswahili. Kwa bahati mbaya mwalimu
mwenyewe hakuelewa maana ya neno hili kama ilivyotarajiwa! Kwa hivyo, wanafunzi
walipomaliza kusoma alitoa agizo na kuwambia: Shikeni ndama.
Mfano mwingine wa maneno yanayofanana au yanayokaribiana sana ni mzigo na
kifo ambayo katika Luganda huandikwa: muzigo, kifo. Maana ya muzigo katika Luganda
ni aina fulani ya mafuta ya kupikia, na maana ya kifo ni nafasi au mahali. Siku moja
mtawa mmoja kutoka Uganda alishituka kwenye kizuizi cha barabarani nchini Kenya
alipomwona askari akigusa mzigo wake huko akiuliza: “Mzigo huu ni wa nani?” Kwa
mshangao mkubwa, mtawa huyu alijiuliza katika lugha yake ya mama kama mtu huyu
alifikiri kuwa yeye angeweza kuweka muzigo kwenye nguo!
Kwa upande mwingine kuna uwezekano kwamba baadhi ya maneno katika lugha
za wanafunzi na Kiswahili ambayo yana umbo sawa au yanakaribiana yana maana ya
pamoja. Lakini licha ya kuwa na maana ya pamoja yanaweza kutofautiana kuhusu
maenezi yake. Kwa mfano maneno kunywa na mchele yanapatikana katika lugha za
wanafunzi. Lakini kinyume na lugha nyingine lugha ya Kiswahili inatumia maneno hayo
kwa maenezi finyu ya maana. Kutofanana na Kiswahili, maneno haya yana maenezi pana
katika lugha nyingine. Kutokana na ukweli kwamba maneno haya yana maenezi pana
katika lugha za wanafunzi si ajabu kwa mwanafunzi kutunga sentensi kama zifuatazo:
(i) Watoto wa shule walifumaniwa wakinywa sigara*
(ii) Nimechoka kula mchele kila siku*
Shida hasa ni kwamba katika mfumo wa lugha ya mwanafunzi anayehusika dhana
ya kunywa na kuvuta hazipambanuliwi. Hali kadhalika, dhana ya mchele na wali
hazipambanuliwi. Lugha yake hutumia neno moja kutaja mambo ambayo kwa mtazamo
wa utamaduni wa Waswahili yanapaswa kutajwa kwa kutumia maneno tofauti.
Mwanafunzi anapowasiliana katika Kiswahili ni lazima atambue kwamba kinyume na
hali ilivyo katika lugha ya jamii yake mfumo wa lugha ya Kiswahili unapambanua kati
ya: mpunga, mchele na wali. Ni lazima ajue pia kwamba mfumo wa Kiswahili
unapambanua kati ya kunywa na kuvuta. Hauruhusu kitenzi kunywa kuambatanishwa na
nomino sigara kama kitendwa.
Tatizo lingine kuhusu matumizi ya maneno linabainika wakati ambapo lugha ya
mwanafunzi hutumia neno moja kuwasilisha dhana ambazo katika Kiswahili
87
zinapambanuliwa na kuwasilishwa kwa maneno yaliyo tofauti. Tofauti iliyopo na mfano
uliotangulia ni kwamba maneno yanayohusiana katika mfano huu hayafanani kabisa
katika lugha zote mbili. Mfano unaobainisha vizuri tatizo hili unahusu dhana ya idadi na
ukubwa. Katika baadhi ya lugha za wanafunzi dhana hizi mbili huwa hazipambanuliwi
kileksia kwa kutumia maneno yaliyo tofauti. Lakini katika Kiswahili dhana hizi huwa
zinapambanuliwa kileksia kwa kutumia maneno –chache na dogo. Ni kutokana na hali
kama hii, kwa mfano, ndipo unaweza kuona mwanafunzi akitumia sentensi kama
ifuatayo akiwa na maana ya uchache wa watu:
(iii) Mkutano uliahirishwa kwa sababu watu waliokuja walikuwa wadogo
sana.
Kutokana na mifano hii ni wazi kwamba unapofundisha msamiati wajibu wako
siyo kufundisha wanafunzi maneno mapya tu, bali pia ni kuona kwamba wana uwezo wa
kuzingatia matumizi yake sahihi katika vielelezo vya sentensi.
(b) Sarufi:
Lugha ni mfumo wa maneno. Hii inamaanisha kwamba maneno ya lugha huwa
yanapangwa kwa kuzingatia kanuni maalum za lugha inayohusika. Mfumo wa sarufi ya
Kiswahili una sifa zake ambazo wakati mwingine zinatofautiana na zile za lugha za
wanafunzi. Hali kama hii inaweza kuwa chanzo cha baadhi ya makosa ambayo
wanafunzi wanafanya katika Kiswahili. Kwa mfano, lugha ya Kiluo haiweki majina
katika makundi ya ngeli na kupambanua majina hayo katika umoja na wingi kwa kutumia
viambisho kama ifanywavyo katika Kiswahili. Mifano ifuatayo inabainisha ukweli huu:
Mara nyingi watu kutoka jamii ya Waluo wanakuwa na shida ya kutumia
viambisho vya ngeli kwa usahihi. Sababu mojawapo ya shida yao inatokana na mfumo
wa lugha ya jamii yao. Hata wale ambao wana mfumo wa ngeli katika lugha zao
wanafanya makosa ya kutumia viambisho vya ngeli visivyofaa. Asili hasa ya kukosea ni
kwamba majina yanayohusika huwa yanawekwa katika ngeli tofauti katika lugha ya
Kiswahili na zile za wale wanaohusika. Kwa kawaida, baadhi ya lugha za kibantu
huweka majina ya wadudu na wanyama katika ngeli ya 9/10. Hali ni tofauti katika
Kiswahili ambapo majina hayo huwekwa katika ngeli ya 1 / 2.
Kutokana na ukweli huu, unaweza kushuhudia sentensi kama zifuatazo kutoka
kwa wanafunzi:
Kiswahili Luo
Chakula kizuri.
Msichana mzuri.
Samaki wazuri.
Kiti kimevunjika.
Mti umevunjika.
Miti imevunjika.
Chemor maber.
Nyako maber.
Rech maber.
Kom otur.
Yath otur.
Yiem otur.
88
(iv) Kuna mbu nyingi hapa.*
(v) Kuku yangu imekufa.*
Aina nyingine ya kosa inahusu majina ya ukoo yanapohusishwa na kimilishi. Kwa
mujibu wa sarufi ya Kiswahili ni lazima kimilishi kiambatanishwe na kiambisho cha
ngeli ya 9/10. Kwa upande mwingine, lugha nyingine za kibantu zinatumia kiambisho
cha ngeli ya 1 /2. Kwa sababu hii unaweza kuwasikia wanafunzi wakisema:
(vi) =Alienda kwa nyanya wake.*
Kosa lingine la kisarufi ambalo hutokea mara kwa mara linatokana na tabia ya
wanafunzi ya kuhamisha moja kwa moja madondoo ya kisarufi kutoka lugha zao za
mama na kuyaingiza katika matumizi ya Kiswahili. Ifuatayo ni mifano inayobainisha
tabia kama hii:
(vii) Ninataka kumwonako padre.*
(viii) Tulipitianga hapo zamani.*
Hali kadhalika wanafunzi wanaweza kukanganywa na wakati mwingine kufanya
makosa kutokana na ukweli kwamba dondoo fulani la kisarufi linatumiwa kwa njia
tofauti na ile waliyozea katika lugha yao. Ni kawaida, kwa mfano, kusikia mwuzaji
ambaye anataka mteja anunue kitu fulani kutoka kwake akisema,
(ix) Customer, njo uninunulie……
Msemaji huyu huwa anazungumza hivi kwa sababu katika lugha ya jamii yake
huwa wanatumia kauli ya kutendea katika mkutadha kama huo. Mwanafunzi kutoka jamii
hii anapojifunza sarufi ya Kiswahili itambidi kutambua kwamba katika Kiswahili kauli
ya kutendea haiwezi kutumiwa katika mkutadha kama huo.
Ni wajibu wako kama mwalimu kuwa chonjo ili uweze kutambua aina mbali
mbali za matatizo ya kimsamiati na kisarufi yanayoweza kuwakumba wanafunzi wako
kutokana na tofauti kati ya Kiswahili na mfumo wa lugha mama za wanafunzi wako. Ni
baada ya kutambua matatizo hayo ndipo utakapoweza kuchukua hatua zinazofaa
kuyashughulikia.
ZOEZI 7.1
(a) Ukitoa mifano inayofaa eleza jinsi utumiaji wa maneno katika
lugha za jamii za wanafunzi na Kiswahili unavyoweza
kutofautiana na kutatiza mawasiliano ya wanafunzi katika
Kiswahili.
(b) Onyesha jinsi wanafunzi wanavyoweza kuhamisha kanuni za
kisarufi za lugha za jamii zao katika Kiswahili na kuishia kwa
kufanya makosa ya kisarufi.
89
7.2. Uhusiano Kati ya maneno.
Maneno ya lugha yanaweza kugawanywa katika makundi kulingana na jinsi
yanavyohusiana na kuingiliana kwa msingi wa maana (kisemantiki). Kwa mfano,
tukirejelea maneno katika kundi la kwanza tunaona kwamba kila moja kati ya maneno
hayo linaweza kuambatanishwa na zaidi ya maana moja. Kwa hivyo maneno yenye sifa
hizi yanaweza kuainishwa pamoja. Vile vile maneno yaliyopangwa jozi kwa jozi katika
kundi la pili nayo yanahusiana kwa namna maalum. Manenao katika jozi hizi yana karibu
maana sawa. Kwa upande mwingine yale katika kundi la tatu ni maneno yenye maana
kinyume.
Aina nyingine ya uhusiano ni ile inayobainika katika jozi za maneno ambayo
yanaashiria hali ya mshikamano au ya mambo ambayo huwa yanapatikana kwa wakati
MFANO WA MANENO AINA YA UHUSIANO
1 Panda Kaa
Ua meza Vitate
2 (i) panda kwea
(ii) iva komaa.
(iii) zunguka zurura
(iv) shida taabu
Visawe
3 (i) panda shuka
(ii) chini juu
(iii) mbele nyuma
Vinyume
4 (i) giza usiku
(ii) nuru mchana
(iii) jua joto
Viandamizi
5 (i) mchana giza
(ii) usiku nuru Vikingamizi
6 kupiga magoti
kupiga simu
kukata shauri
kukata tamaa
kula kiapo
kupiga kidoko
Nahau
90
mmoja. Kwa kawaida usiku huandamana na giza; na mchana huwa unaandamana na
nuru. Kwa upande mwingine yale katika kundi la tano huashiria hali ya mambo
yanayotengana. Uhusiano wa maneno katika jozi hizi ni wa utenganifu. Kwa kawaida,
kwa mfano, giza haipatikani mchana; na wala nuru haipatikani usiku. Kwa Kingereza
uhusiano katika kundi la nne hujulikana kama collocation na ule katika la tano hujulikana
kama exclusion.
Kundi la sita lina semi ambazo hujulikana kama nahau. Nahau ni usemi ambao
maana yake haiwezi kutabiriwa kwa kuzingatia maana ya neno moja moja katika usemi
huo. Unaweza kuwa unafahamu kila neno ambalo limetumiwa katika usemi fulani lakini
ukashindwa kuelewa maana ya usemi huo. Kupiga magoti, kwa mfano, hakuna maana ya
kushika fimbo au kifaa cho chote kile na kuyatwanga magoti.
Ni muhimu kwako kama mwalimu kuwa na fununu kuhusu vile ambavyo maneno
ya lugha yanaingiliana na kuhusiana. Jambo hili litakusaidia kupanga ufundishaji wako
wa msamiati kwa utaratibu ukitilia maanani uhusiano huo. Badala ya kuchanganya
maneno ya aina tofauti na kuyafundisha kwa pamoja unaweza kutumia uhusiano kama
kigezo kinachoweza kukuongoza kuteua maneno utakayofundisha.
ZOEZI 7.2.
Licha ya kueleza aina tofauti za makundi ya maneno, kila kundi
linapewa jina maalum. Pendekeza istilahi ambazo, kwa maoni
yako zinafaa zaidi, na kisha utoe hoja za kutetea pendekezo lako.
7.3 Kufundisha Msamiati
Maneno ni chombo muhimu cha ufanikishaji wa mawasiliano. Mtu asipokuwa na
maneno ya kutosha anakuwa na shida ya kuwasilisha ujumbe. Vile vile, anakuwa na
shida ya kufahamu kwa urahisi ujumbe unaowasilishwa na wengine. Kwa hivyo
ufundishaji wa msamiati unalenga kuwezesha mwanafunzi kuwa na maneno ya kutosha
ili aweze kuwasilisha na kupokea bila shida ujumbe katika miktadha tofauti ya
mawasiliano. Unalenga kumwezesha kusoma, kusikiliza, kuzungumza na kuandika kwa
ufahamu bora.
Ujuzi wa msamiati siyo jambo ambalo linaweza kufanyika kwa ghafla au katika
muda mfupi wa mafundisho. Unatokana na mazoea ya kushiriki katika matumizi ya lugha
kwa muda mrefu. Kwa hivyo wewe kama mwalimu usichukulie ufundishaji wa msamiati
kama wakati wa kushindilia maneno chungu nzima kwenye vichwa vya wanafunzi. Pia
ujuzi wa msamiati hautegemei idadi ya maneno magumu ambayo mwanafunzi anaweza
kuwakanganya nayo watu wengine. Ni kazi bure kwa mtu kujua maneno mengi au
maneno magumu kama hana uwezo wa kutumia maneno hayo kuwasiliana kwa ufahamu
na watu wengine. Kwa hivyo unapofundisha msamiati usiwe na mazoea ya kufundisha
maneno mengi katika muda wa kipindi kimoja cha somo. Usiwe pia na mazoea ya
91
kufundisha tu maneno magumu. Inafaa ufundishe maneno machache, na uambatanishe
ufundishaji wake na mambo mengine. Kile unachopaswa kukazania ni kuona kwamba
unashirikisha wanafunzi wako katika shughuli mbali mbali za mawasiliano ambayo
yanaweza kutoa nafasi kwao ya kujiongezea msamiati na kuimarisha uwezo wa kutumia
msamiati huo kama inavyopaswa.
Je ni mbinu gani ambazo unaweza kutumia kufundishia msamiati, na unaweza
kuzitumia namna gani? Miongoni mwa mbinu hizi ni pamoja na zifuatazo:
Mkutadha Wa Maneno
Maono
Maigizo
Visawe
Vinyume
Asili ya neno
Tafsiri
Mkutadha Wa Maneno
Aghalabu neno likitumiwa pekee yake bila kuambatanishwa na maneno mengine
katika muundo wa senstensi inakuwa vigumu kutambua maana yake mahsusi. Maana ya
maneno mengi inategemea mtagusano wake na maneno mengine. Kwa mfano, neno piga
linakuwa na maana tofauti kulingana na maneno mengine yanayotumiwa pamoja nalo
kama katika mifano ifuatayo:
magoti
yowe
mbizi
Kupiga kalamu
ngumi
kofi
kidoko
pasi
Uzuri wa kutolea neno mkutadha ni kwamba unasaidia mwanafunzi kutambua
maana kwa urahisi. Ni rahisi pia kwa mwanafunzi kukumbuka maneno yanayohusika
pamoja na matumizi yake. Mbinu ya mkutadha inafaa sana kwa sababu inatilia maanani
ukweli kwamba lugha ni chombo cha mawasiliano. Kwa hivyo unapotaka kufundisha
neno lo lote inafaa ulitolee mkutadha maalum utakaowasaidia wanafunzi kung’amua
maana yake. Kwa ufupi unaweza kufuata hatua kama zifuatazo:
(a) Bainisha matumizi ya maneno yanayohusika katika mkutadha wa
mawasiliano.
92
(b) Fahamisha wanafunzi maneno yaliyolengwa, na kuwasaidia kufafanua
maana kwa kurejelea mkutadha wa matumizi yake.
(c) Shirikisha wanafunzi katika mazoezi yanayolenga kutoa kwao nafasi ya
kutumia maneno yanayohusika ili waweze kubainisha na kuendeleza ujuzi
wao wa maneno.
Tuseme kwa mfano mada ya somo lako ni “maneno yenye maana zaidi ya moja”.
Umeamua kufundisha mada hii na miongoni mwa maneno ambayo umeamua kutoa kama
mfano ni neno panda. Je, utafundisha vipi ukitumia mbinu ya mkutadha?
Kwanza utalitolea mkutadha neno hili kama katika mfano ufuatao:
PANDA.
(a)
Miaka ishirini iliyopita Mzee Omari alipanda koko la embe. Mwembe
ulupokomaa alitwambia tupande hadi katika panda la mti ili tukate matawi kiasi ya
kutengeneza panda za kuwindia ndege na panda za nguzo kwani alisikia fununu kwamba
vifaa hivi vimepanda bei huko mjini.
Baada ya kutayarisha vifaa vyake, Mzee Omari alipanda matatu kuelekea mjini.
Matatu ilichomoka mbio na kupanda milima kwa kasi sana bila kusimama mpaka
ilipofika kwenye njia panda. Kutoka hapo, ilielekea kulia, njia inayopitia msituni ambako
Mzee Omari alimwona panda akiwa malishoni. Walipofika mjini walisikia sauti ya
parapanda ikilia kwa mbali.
(b)
Hapo kale palikuwa na watoto wawili Karisa na Kitsao. Karisa alikuwa binamu
ya Kitsao. Alfajiri moja walitoka kwa mbalamwezi wakaenda shambani kulima. Baadaye
kidogo walichukua mbegu za mtama na kuanza kuzipanda humo shambani.
Walipomaliza kupanda mbegu, Kitsao alimshauri binamu yake waende kuwinda ndege,
na Karisa akajibu ya kwamba hakuwa amebeba panda yake na kwa hivyo asingeweza
kwenda kuwinda. Kitsao alimwarifu kwamba yeye aliwahi kubeba panda mbili.
Basi waliandamana kwenda mawindoni. Muda kidogo hivi Karisa aliona ndege
juu ya matawi ya mwembe, akalenga shabaha na ile panda na kumpiga kwa sokota moja.
Lakini badala ya kuanguka chini, yule ninga alisaki juu ya kitagaa cha mwembe. Kuona
hivyo, Karisa alipanda juu ya mwembe na kumtoa yule ndege.
Vijana hawa wawili waliendelea kuwinda ndege huko mwituni kwa muda mrefu.
Walichelewa kurudi nyumbani; na katika ile hali ya kurejea nyumbani walifika njia
panda. Walitatizika sana kwa kutojua njia ipi kati ya zile mbili ndiyo inayokwenda kwao.
Karisa alimwambia mwenzake wabahatishe kwa kufuata moja kati ya njia hizi mbili.
Waliifuata na punde si punde wakajikuta wamewasili kwao nyumbani. Walieleza mkasa
uliowapata wakapewa pole.
Ilipofika liamba siku ya pili, Kitsao alitumwa dukani kununua mkate, maziwa na
majani chai. Kufika dukani akatoa senti alizopewa na mama yake lakini mwenye duka
93
akamwambia bei za vitu zilikuwa zimepanda siku iliyopita. Kitsao alipanda baiskeli yake
akarudi nyumbani kumwambia mama yake. Aliongezewa pesa akarudi huko dukani
kununua vitu alivyotumwa.
Baada ya chai ya asubuhi, Kitsao na Karisa walitumwa kwenda sokoni kununua
vifaa mbali mbali vilivyohitajiwa siku hiyo. Walipomaliza shughuli zilizowapeleka huko
walipanda gari wakarudi nyumbani. Kufika nyumbani walistaajabu kuona umati wa
watu. Walipouliza, waliambiwa kwamba walikuwa wamekusanyika kwa vile mjomba
wao alikuwa amepandishwa cheo kazini.
Ufundishaji.
Ukifika darasani unaweza kufuata hatua zifuatazo:
Kuwasomea wanafunzi kwa sauti nakala. Wewe au mwanafunzi mmoja.
Kuwapatia wanafunzi nakala ili wasome kimya.
Kuwataka wataje neno ambalo limerudiwa mara kwa mara.
Ukirejelea sentensi tofauti ambamo neno panda limetumiwa wambie
wanafunzi wajaribu kueleza maana ya neno hilo.
Wanafunzi watunge sentensi zaidi zinazobainisha maana tofauti za neno
panda.
Waulize wanafunzi jinsi maneno ya namna hii huitwa.
Watoe mifano mingine ya maneno ya namna hii na kuyatumia katika sentensi
tofauti kubainisha maana mbali mbali.
Mfano mwingine wa kutumia mkutadha:
(c)
Bwana Kizenga aliishi katika mtaa wa Makogoro. Hapo alikaa katika maisha ya
taabu. Aliyamudu maisha yake kwa kufanya kazi ya kuchoma makaa. Kwa kuuza makaa
hayo aliweza kujipatia pesa akaanza starehe. Alijijengea nyumba ya mawe inayoweza
kukaa kwa miaka mingi sana. Nyumba yake ilijengwa kwa ustadi hivi kwamba mtu
angeweza kukaa ndani mchana kutwa bila kuchukizwa.
Mimi mwenyewe niliyashuhudia haya nilipomtembelea hivi majuzi. Yeye na
familia yake walikuwa wamevalia nguo zilizowakaa vizuri. Tulikaa kwenye viti kabambe
vilivyopambwa kwa vitambaa maridadi tulipokuwa tukikaribishwa kwenye mlo wa
mwaka.
Nje ya nyumba na au la miti, na pembeni mlikuwa na bwawa dogo ambamo
Bwana Kizenga liwafuga wanyama wadogowadogo wa majini kama vile kaa, vyura na
hata samaki kwa minajili ya kupendeza wageni.
Vifaa Vya Maono.
Hii ni mbinu ambayo inahusisha utumiaji wa vifaa kama vile vitu halisi, picha au
michoro ya aina tofauti. Unapotumia mbinu hii mwanafunzi anapata fursa ya kung’amua
maana ya neno kwa kuliambatanisha moja kwa moja na kitu, kielelezo cha kitu
kinachohusika, au kitendo kinachoashiriwa. Pamoja na hayo utumiaji wa vifaa vya
maono hulipa somo uhai licha ya kuzoesha wanafunzi kukumbuka kwa urahisi. Hali
kadhalika ni mbinu kabambe ya kuhamasisha wanafunzi kujieleza kwa nafsi zao.
94
Wakati unapotumia mbinu hii unaweza kutunga maswali na kuwataka wanafunzi
wajibu maswali hayo. Wakati wa kujibu maswali juu ya picha au mchoro wanafunzi
watakuwa wakifanya mazoezi ya kutumia lugha. Tukirejelea mfano wa neno panda
unaweza kuonyensha vitu na michoro kama vile:
Manati.
picha ya mtu anayekwea juu ya mti.
watu wakiingia ndani ya matatu.
watu wakiweka mbegu ardhini.
kifaa cha kushikilia nguo zinapoanikwa n.k..
Kufundisha kwa njia hii ni bora zaidi kuliko kufundisha kwa kuwaagiza
wanafunzi wataje maana tofauti za neno. Kufanya hivyo hakuwasaidii kuzingatia
ipasavyo matumizi ya neno linalohusika.
Maigizo.
Maigizo ni namna ya maonyesho kwa vitendo. Humpa mwanafunzi nafasi ya
kukisia maana ya neno kwa kuliambatanisha moja kwa moja na kitendo kinachoigizwa au
kinachofanywa. Uigizaji huo unaweza kufanywa na wanafunzi au na wewe mwenyewe.
Uzuri wa mbinu hii ni kwamba inaambatanisha maono na vitendo, mambo ambayo
yanachangia kufanikisha hali ya kukumbuka na kufahamu. Aghalabu, ukiona
unakumbuka rahisi zaidi, na ukitenda jambo unafahamu zaidi kuliko unaposikia tu.
Maneno kama yafuatayo yanaweza kufundishwa kwa maigizo: chungulia, nyemelea,
mshangao, huzuni, chomoa, dundadunda, kujipinda, myayo, nong’ona.
Visawe:
Maana ya maneno inaweza kuelezwa kwa kutaja neno lingine lenye maana karibu
sawa. Lakini lazima ikumbukwe kuwa si rahisi kupata maneno mawili ambayo maana
yake ni sawa kabisa. Hata maneno yanayotambuliwa kuwa ni visawe yanatofautiana.
Kwa mfano, maneno iva na komaa yanafikiriwa kama visawe. Kila mojawapo ya maneno
haya linaweza kutumiwa badala ya lingine kama inavyobainika katika sentensi zifuatazo:
(a) Tunda hili halijakomaa vizuri.
(b) Tunda hili halijaiva vizuri.
Lakini neno komaa haliwezi kutumiwa badala ya iva katika sentensi ifuatayo:
(c) Chakula kimeiva vizuri.
Hali kadhalika neno iva haliwezi kutumiwa mahali pa komaa katika sentensi
ifuatayo:
(d) Kijana huyu amekomaa kiakili.
Mifano hii inaonyesha wazi kwamba hata maneno ambayo yanafikiriwa kuwa
sawa hayamo katika mpishano huria katika mikutadha yote ya mawasiliano. Ni lazima
uhakikishe kwamba wanafunzi wanatambua ukweli huu kuhusu maneno hayo.
Unapotumia kisawe pia kama njia ya kufundishia neno unapaswa kuhakikisha kwamba
neno ambalo unataja kama kisawe ni neno ambalo tayari wanafunzi wanalijua. Ukitumia
neno ambalo ni geni kwao utawakanganya zaidi badala ya kurahisisha ufahamu wao.
Ni wajibu wako kuona kwamba wanafunzi wanatambua vizuri ukweli kwamba
visawe havimo katika mpishano huria katika kila mkutadha wa mawasiliano. Kutambua
ukweli huu kutawasaidia sana hasa wanapotumia kamusi kutafuta maana za maneno. Ni
95
kawaida katika kamusi kukuta maneno kadhaa yakiwa yameorodheshwa kama visawe
vya neno ambalo maana yake inafafanuliwa. Wanafunzi wasipotambua ukweli huu,
huenda wakatumia kimakosa maneno yaliyotajwa katika mkutadha ambamo hayastahili
kutumiwa. Ujuzi wao wa msamiati hautakuwa kamili kama hawana uwezo wa kutumia
kwa usahihi kisawe kinachohusika katika vielelezo vya sentensi.
Kwa hivyo unapotumia mbinu hii usiishie kwa kutaja visawe peke yake.
Unapaswa pia kushirikisha wanafunzi katika mazoezi yanayolenga kuendeleza uwezo
wao wa kutambua mikutadha ambamo maneno yanayohusika yanaweza kutumiwa moja
badala ya lingine na ile ambamo haiwezekani kufanya hivyo. Kwa mfano, unaweza
kuwapatia zoezi la kukamilisha sentensi kwa kujaza katika pengo neno linalofaa kutoka
orodha ya visawe ulivyoorodhesha. Ikiwa inawezekana kutumia maneno yote
yanayochukuliwa kuwa visawe wajaze yote mawili, neno moja likiwekwa katika mabano.
Unaweza pia kuwapa maneno yanayofikiriwa kuwa visawe na kuwambia:
(i) Watunge sentensi ambamo kila mojawapo ya maneno hayo linaweza
kutumiwa badala ya lingine.
(ii) Watunge sentensi ambamo moja kati ya maneno hayo haliwezi kutumiwa
badala ya lingine.
Vinyume.
Unapotumia kinyume unajaribu kueleza maana ya neno fulani kwa kutoa mfano
wa neno lenye maana inayopingana na ya neno hilo. Kwa mfano:
Ili uweze kufaulu vizuri ni lazima uhakikishe kwamba neno unalotaja kama
kinyume si geni kwa wanafunzi. Kama sivyo utawatatiza zaidi. Lazima ukumbuke pia
kwamba siyo kila neno linaweza kuwa na kinyume. Kwa hivyo usiwambie wanafunzi
kutaja kinyume cha neno lo lote bila kutilia maanani ukweli huu. Lazima pia
uambatanishe utajaji wa kinyume na zoezi la kutumia katika sentensi maneno
yanayohusika ili maana inayopingana iweze kubainika wazi.
Neno linalohusika Kinyume
nyuma
zima
chungu
kuasi
furaha
chali
juu
mbele
washa
tamu
kutii
huzuni
kifudifudi
chini.
96
Asili Ya Neno
Wakati mwingine unaweza kuongoza wanafunzi kukisia maana ya neno kwa
kuwaonyesha chanzo cha neno hilo ikiwa inawezekana. Unaweza, kwa mfano, kusaidia
wanafunzi kukisia maana ya maneno yafuatayo kwa kurejelea mwanzo wake:
Tafsiri:
Ikiwa huna njia yo yote ya kueleza maana ya neno unaweza kueleza maana yake
kwa kutumia lugha nyingine ambayo wanafunzi wanaielewa. Lakini unapotumia mbinu
hii inafaa ukumbuke kuwa siyo kila neno linaweza kutafsiriwa moja kwa moja kutoka
lugha moja hadi nyingine. Vile vile, mbinu hii haistahili kutegemewa sana kwa sababu
wanafunzi wakiizoea sana huenda wasitilie maanani lugha ya Kiswahili kama lugha
kamili ambayo inaweza kujitosheleza kama chombo cha kufanikisha mawasiliano.
Uteuzi Wa Msamiati:
Msamiati ambao utafundisha wanafunzi wako unategemea sana vitabu
vinavyotumiwa katika viwango unavyofundisha. Lakini, hata hivyo, unashauriwa mara
kwa mara kuteua msamiati ambo unafaa wanafunzi wako na kuufundisha. Ni wajibu
wako pia kuwaongoza wanafunzi kusoma vitabu mbali mbali na makala tofauti ili waweze kupanua msamiati wao.
ZOEZI 7.3.
A. Pendekeza mbinu nyingine zaidi unazoweza kutumia
kufundishia msamiati. Kwa kila mbinu
unayopendekeza toa mifano kuonyesha jinsi
unavyoweza kuitumia .
B. Jadili uzuri na udhaifu wa mbinu zifuatazo kama njia
za kufundishia msamiati:
(i) Kutumia vitu halisi.
(ii) Kutumia visawe.
(iii) Kutafsiri.
Neno Asili yake
Kutafakari
Kutarazaki
Tarathimini
Fikiri
Riziki, ruzuku
Taarifa, tathimini.
97
7.4 Ujuzi wa Sarufi:
Ufundishaji wa sarufi unalenga kuwezesha mwanafunzi kutumia maneno ya lugha
inayohusika katika utaratibu unofaa. Kwa hivyo unapofundisha sarufi ya Kiswahili
unapaswa kushirikisha wanafunzi katika mazoezi ya matumizi ya lugha ambayo yanatoa
kwao fursa ya kung’amua na kutumia kanuni zinazotawala matumizi ya maneno katika
utaratibu unaotakikana kulingana na mkutadha wa mawasiliano. Wanafunzi wakiwa na
uwezo huu watakuwa wanafahamu sarufi.
Mwanafunzi akiimudu sarufi ya Kiswahili atakuwa na uwezo wa kufanya mambo
kama yafuatayo:
Kutumia maneno ya Kiswahili katika vielelezo sahihi vya sentensi.
Kutambua miundo ya sentensi inayokiuka utaratibu wa Kiswahili.
Kutambua maana ndani ya sentensi kwa kuzingatia mfuatano wa maneno
yaundayo sentensi kama:
(i) Ali alimzomea Amina
(iii) Amina alimzomea Ali.
Kutambua uhusiano wa maana katika sentensi tofauti k.m.
(i) Baba alipiga mtoto
(ii) Mtoto alipigwa na baba
Kutambua maana ya sentensi kwa kuzingatia mageuzi yanayotokea katika
maumbo ya maneno k.m.
a.
(i) Tunda hili haliliwi.
(ii) Tunda hili haliliki.
b..
(i) Mama alipika chakula.
(ii) Mama alipikisha chakula.
(iii) Maama alipikiwa chakula
Kung’amua utata ndani ya sentensi k.m.
(i) Watoto walipanda miti.
(ii) Musa aligombana na Ali akampiga teke akaangukia mbuzi
Kutumia Kiswahili kwa njia ya ubunifu.
Kutokana na mambo haya ni wazi kwamba wewe kama mwalimu una jukumu la
kujitahidi kusaidia wanafunzi wawe na uwezo wa kutekeleza mambo haya yaliyotajwa.
ZOEZI 7.4
A. Toa mifano ya sentensi zenye utata ndani yake. Kwa kila
mfano eleza chanzo cha utata huo, na kisha pendekeza
jinsi ya kuondoa utata huo.
B. Ukitoa mifano ya kutilia maki jibu lako eleza maana ya
kutumia Kiswahili kwa njia ya ubunifu.
98
7.5 Kufundisha Sarufi:
Somo la sarufi ni mojawapo ya masomo ambayo hayapendwi na wanafunzi.
Sababu mojawapo ya kutopendwa ni kwamba baadhi ya walimu wana mazoea ya
kufundisha sarufi kama kwamba ni lugha ya aina ya pekee ambayo inatumika katika
mazingira ya darasa. Walimu wa namna hii wanafundisha sarufi kama kwamba haina
uhusiano na lugha ya nje ya darasa. Wengine wanachukulia wakati wa kufundisha sarufi
kama wakati wa kufundisha kanuni za matumizi ya lugha na uchambuzi wake kwa
misingi ya kiisimu. Matokeo ya mtindo huu ni kuwafanya wanafunzi wachukie vipindi
vya sarufi. Ni wajibu wako kama mwalimu kuhakikisha kwamba unafundisha sarufi kwa
kutumia mbinu ambazo zinawezesha wanafunzi wako kujifunza sarufi ya Kiswahili bila
kupoteza hamu.
Kwanza kabisa kabla ya kufundisha sarufi, ni lazima uwe na lengo maalum
unalotarajia kutimiza. Ukifika darasani ni bora zaidi kuwasilisha dondoo la kisarufi
unalolenga kufundisha kupitia mkutadha wa mawasiliano kuliko kutoa maelezo ya moja
kwa moja juu ya dondoo hilo. Inafaa uonyeshe matumizi ya dondoo la sarufi
linaloshughulikiwa katika mkutadha mahsusi wa mawasiliano. Wanafunzi wanapaswa
kupewa fursa ya kung’amua kanuni zinazotawala matumizi ya dondoo linalohusika
kutokana na mkutadha maalum wa mawasiliano. Ni baada ya kushuhudia matumizi yake
ndipo unapoweza kutoa maelezo kuhusu kanuni za kisarufi. Kwa mfano, ikiwa unapanga
kufundisha wakati uliopita unaweza kutafuta kisa cho chote kinachofaa kinachosimulia
matukio ya wakati uliopita. Baada ya wao kusoma kisa hicho au wewe kuwasomea
unaweza kudondoa sentensi za wakati uliopita na kuzungumzia jambo hilo kwa kurejelea
mifano mahsusi. Ikiwa unataka unaweza,kabla ya kuzungumzia jambo hilo, kuuliza
wanafunzi maswali ya ufahamu juu ya kisa hicho. Wakati wanapojibu maswali hayo
watalazimika kutunga sentensi zilizomo katika wakati uliopita. Kisha, baada ya majibu
hayo unaweza kutoa maelezo kuhusu wakati uliopita.
Tuseme umepanga kufundisha jinsi ya kutendea katika kidato cha kwanza.
Unaweza kutayarisha lengo kama lifuatalo na kufundisha ukifuata hatua
zinazopendekezwa hapo chini.
Kidato : 1
Mada : Jinsi ya kutendea.
Lengo : Kufikia mwisho wa kipindi wanafunzi watatunga angalau sentensi nne
kuonyesha matumizi tofauti ya jinsi ya kutendea.
Utangulizi:
Ukionyesha kifaa fulani, wambie wanafunzi wataje kifaa hicho k.m. ufunguo,
wembe, kijiko, panda.
Waulize wanafunzi kifaa hicho kinatumiwa kufanya nini. Kisha andika
sentensi hiyo ubaoni na upige mstari chini ya kitenzi cha jinsi ya kutendea.
Kwa mfano: Mpishi hutumia kisu kukatia nyama.
99
Mpatie mwanafunzi mmoja kifaa fulani halafu umwagize mwingine atunge
sentensi inayoeleza kitendo ambacho umefanya. Mwanafunzi anaweza
kutunga sentensi kama ifuatayo:
Umempatia wembe wa kukatia uzi.
Endelea kuuliza maswali tofauti ambayo yatalazimisha wanafunzi kutoa
majibu ambayo yanahusisha vitenzi katika jinsi ya kutendea.
k.m Ulizaliwa wapi?
Ulikulia wapi?
Ulisomea wapi masomo ya msingi?
Maelezo Rasmi.
Waeleze wanafunzi kwamba katika Kiswahili maana ya kitenzi inaweza
kubadilika kufuatana na matumizi ya viambisho tofauti kama katika mifano ya
vitenzi vilivyopigwa mstari chini yake katika sentensi zilizo ubaoni.
Mabadiliko ya namna hii huitwa jinsi /kauli katika Kiswahili. Waeleze pia
kwamba kuna jinsi / kauli tofauti. Vitenzi katika mifano iliyo kwenye ubao
vimo katika jinsi ya kutendea. Eleza pia kwamba jinsi ya kutendea inatumiwa
kuwasilisha maana tofauti kama katika mifano iliyotolewa.
Toa mifano zaidi ya vitenzi ili kubainisha sheria zinazotawala uundaji wa jinsi
ya kutendea kufuatana na utangamano wa irabu kama katika mifano ifuatayo:
Kitenzi Jinsi ya kutendea
pata
panga
pita
zima
funga
nunua
soma
zoma
tenda
jenga
patia
pangia
pitia
zimia
fungia
nunulia
somea
zomea
tendea
jengea
100
Mazoezi ya Kuendeleza Matumizi ya Jinsi ya Kutendea.
Wape wanafunzi mazoezi yanayolenga kuendeleza ufahamu wa jinsi ya
kutendea. Wanaweza kwa mfano, kutoa mifano zaidi ya vitenzi na kuvitumia
katika sentensi vikiwa katika jinsi ya kutendea.
Washirikishe wanafunzi katika zoezi la kusoma au kusikiliza kifungu fulani
cha habari kilicho na vitenzi katika jinsi ya kutendea. Kisha waulize maswali
juu ya kifungu hicho ambayo majibu yake yatahusisha vitenzi vilivyo katika
jinsi ya kutendea.
Kwa ufupi unapofundisha sarufi usifundishe ukiwa na lengo la kufafanulia
wanafunzi kanuni za kisarufi na istilahi zake. Inafaa lengo lako kuu liwe kuwezesha
wanafunzi wako kutambua na kuzingatia kanuni hizo kutokana na mifano kamili ya
vielelezo vya sentensi. Unapofundisha ngeli, kwa mfano, haifai kuwaeleza tu jinsi
kiambisho fulani hubadilika katika wingi na kisha kuwapatia orodha ya majina na
kuwaagiza wataje majina hayo katika hali ya wingi. Njia bora zaidi ni kuonyesha
mabadiliko hayo kupitia kifungu fulani kinachohusisha mifano ya majina ya ngeli tofauti
unazotaka kuzungumzia. Wanafunzi wasome au wasikilize kwanza kifungu hicho ili waweze kushuhudia moja kwa moja jinsi majina ya ngeli kadhaa hubadilika na kuathiri
maneno mengine yanayoambatanishwa nayo katika sentensi. Ukizungumzia mabadiliko
hayo baadaye maelezo yako yatakuwa na maana zaidi. Lazima ukumbuke kwamba
inawezekana kwa mtu kujifunza na kuimudu lugha bila kuelezwa moja kwa moja kanuni
zinazotawala miundo ya lugha inayohusika. Mtoto mdogo, kwa mfano, anajifunza na
kuelewa miundo mbali mbali ya lugha ya jamii yake kwa kuiambatanisha na mikutadha
maalum ya mawasiliano ambamo inatumiwa. Kwa mfano, akiona baba yake akiondoka
nyumbani na kusikia mama akisema Baba anaenda kazini, au wakati ndugu na dada zake
wakienda shuleni huenda akisikia mama akisema Fulani anakwenda shuleni. Kadiri
muda unavyoendelea mtoto huyo ataanza kufasiri kiambishi –na- na kukiambatanisha na
kitendo kinachoendelea kufanyika. Kwa upande mwingine mtoto huyu akisikia mama
akisema ‘Baba ameenda kazini’, wakati baba yake akiwa ameshaondoka, ataanza
kutambua kwamba kiambishi –me- huashiria wakati uliopita hali timilifu.
Kutokana na mifano hii ni wazi kwamba unapofundisha sarufi si lazima
utangulize ufundishaji wako kwa maelezo ya kanuni za kisarufi. Unaweza kutaja kanuni
hizo baada ya ubainishaji wake katika mikutadha maalum ya vielelezo vya sentensi.
101
ZOEZI 7.4
A. Eleza uhusiano uliopo kati ya sarufi na msamiati. Je, mafunzo
ya sarufi ya Kiswahili yana manufaa gani kwa mwanafunzi?
B. Ukitoa mifano ya kutilia maki jibu lako eleza jinsi
unavyoweza kufundisha mambo yafuatayo kwa wanafunzi
wako:
(i) matumizi ya –enye, -enyewe
(ii) matumizi ya –ji-, kwa
(iii) ukanusho katika wakati uliopita
Aina Za Mazoezi
Mazoezi unayopatia wanafunzi yanachangia pakubwa katika kuimarisha na
kuendeleza udhibiti wao wa sarufi. Unaweza kutayarisha mazoezi tofauti kulingana na
mahitaji ya wanafunzi pamoja na kiwango cha uwezo wako. Miongoni mwa aina za
mazoezi unayoweza kupatia wanafunzi ni pamoja na:
Mpishano wa maneno.
Ugeuzi wa umbo.
Ukamilishaji.
Mpishano Wa Maneno.
Mazoezi ya mpishano wa maneno humpa mwanafunzi fursa ya kutunga sentensi
mbali mbali za muundo fulani kwa kubadilisha maneno yenye ukoo mmoja. Kupitia
mazoezi ya namna hii mwanafunzi hujizoesha muundo fulani wa sentensi kwa kuurudia
mara kadhaa. Mazoezi ya mpishano wa maneno yanafaa sana hasa unapotaka wanafunzi
wajizoeshe kutumia viambisho vinavyofaa kulingana na ngeli ya jina. Baada ya kumpatia
mwanafunzi kielelezo fulani cha sentensi, kwa mfano, unamtaka aandike sentensi hiyo
upya akitumia maneno unayopendekeza badala ya neno fulani katika sentensi hiyo. Kila
anapotumia neno jipya itamlazimu kufanya mabadiliko yanayotakiwa kwa kuzingatia
ngeli ya jina.
Mfano:
Kitabu ambacho kilikuwa hapa sikioni tena.
Agizo: Andika sentensi hii upya ukitumia maneno yafuatayo badala ya kitabu:
tunda, vitabu, mfuko, matunda, wembe, nyuzi, mifuko.
Mfano wa sentensi mpya
Tunda ambalo lilikuwa hapa silioni.
102
Vitabu ambavyo vilikuwa hapa sivioni.
Mfuko ambao ulikuwa hapa siuoni.
Zoezi la namna hii ni zuri kwa wanafunzi ambao wana shida ya kutumia
viambishi sahihi vya ngeli.
Njia nyingine ya kushirikisha wanafunzi katika zoezi la mpishano wa maneno ni
kutumia jedwali la mpishano wa maneno kama katika mfano ufuatao:
Wakirejelea jedwali hili, wanafunzi wanaweza kutunga sentensi mbali mbali.
Ukitaka kuwapa mazoezi zaidi ya kutunga sentensi wakitumia majina ya ngeli tofauti
unaweza kuwambia watumie majina ya ngeli tofauti zaidi ya yale yaliyopendekezwa.
Kwa mfano mwanafunzi akitumia shoka, matunda, mfuko n.k., anaweza kutunga sentensi
kama zifuatazo:
Shoka hili ni la Bakari.
Matunda yale yalikuwa ya watoto.
Mfuko huu si wa Atieno.
Ugeuzi wa Umbo:
Umbo asilia la sentensi linabadilika mwanafunzi anapoziandika upya kulingana
na maagizo ambayo unampatia. Kwa hivyo mwanafunzi anaweza kuandika sentensi za
aina mbali mbali kulingana na maagizo anayopewa.
Mfano:
(1) Andika upya sentensi zifuatazo ukigeuza majina katika hali ya wingi:
Kitabu hiki ni kizuri.
Mtoto yule alilia sana.
Ukuta huo ulijengwa vibaya.
Ufa huo unastahili kuzibwa.
Tunda hili haliliwi.
(2) Kanusha sentensi hizi:
Simama hapa.
Mtoto amelala.
Walifika jana.
Jina Kionyeshi Kitenzi Kiunganishi
Kimilishi
Jina
Kitabu
Kikombe
hiki
kile
hicho
ni
si
kilikuwa
kitakuwa
cha
Makhoha
Atieno
Bakari
nk
103
Tutaonana kesho.
Watoto wanakula ugali.
Wapatieni watoto chakula.
Ukifika mapema tutasafiri pamoja.
(3) Ziandike upya sentensi zifuatazo ukianza na neno la mwisho.
Mbwa alifukuza mtoto.
Mtoto amepika chakula.
Mama amejengesha nyumba.
Umeona mtoto?
Ukamilishaji:
Zoezi la aina hii hutoa nafasi kwa wanafunzi ya kukamilisha sentensi kwa
kutumia neno linalofaa. Wakati mwingine huenda mwanafunzi akapewa arodha ya
maneno na kuambiwa achague neno linalofaa kutoka maneno aliyopewa.
Mfano.
Kamilisha sentensi hizi kwa kutumia maneno yanayofaa:
Fahali wawili……………..zizi moja.
Mama …………………chakula bado. (pika)
Watoto………………shuleni kesho. (enda)
Kama ningalimwona mwizi……………….
Nikifika nyumbani………………………
Kama tusingekuwa hapa………………..
Kama wangalikuja nasi…………………….
Mwenye pupa……………………kula utamu.
Usichukulie aina hizi za mazoezi kama ndizo tu unazoweza kutumia. Ni jukumu
lako kama mwalimu kujitahidi kuibuka na aina nyingine zinazoweza kukuwezesha
kusaidia wanafunzi wako kuimudu sarufi ya Kiswahili.
104
ZOEZI 7.5
Ukirejelea kila moja kati ya sentensi zifuatazo:
Andika sentensi hiyo kwa usahihi.
Eleza mbinu utakazotumia kusaidia mwanafunzi ambaye
ametunga sentensi inayohusika ili aweze kutambua na
kuyarekebisha makosa yake.
Sentensi.
(a) Matunda na viazi zenye zilikuwa kwa mfuko yangu
zimeharibika zaidi.
(b) Nataka kisu ya kukatisha nyama kabla niende kwa
nyumba.
(c) Tukule kwanza; utaongea na simu baada ya kukula.
HITIMISHO.
Katika somo hili la saba tumezungumzia juu ya ufundishaji wa sarufi na
msamiati. Mambo haya ni kama pande mbili tofauti za sarafu moja. Kila upande una sifa
zake lakini pande zote mbili huwa zinaingiliana na kutegemeana. Haina maana
kufundisha msamiati bila kuonyesha utaratibu ambamo msamiati unaohusika unapaswa
kutumiwa. Kwa hivyo, msamiati na sarufi vinapashwa kufundishwa kwa pamoja katika
mkutadha fulani wa mawasiliano. Vile vile ufundishaji wake unapaswa kuambatanishwa
na ufundishaji wa mambo mengine. Ni wajibu wako kama mwalimu kuhakikisha
kwamba unatumia mbinu zinazoweza kuwashirikisha kikamilifu wanafunzi na
kuwawezesha kuumudu msamiati pamoja na sarufi kwa njia yenye maana na manufaa
kwao. Na unapofundisha maneno ni lazima uhakikishe kwamba wanafunzi
wanayamuudu maneno yanayohusika katika viwango vifuatavyo: matamshi, maendelezo
na maana.
Pia ni jukumu lako kuona kwamba mambo haya yanafundishwa kwa kipimo
kinachofaa.
105
SOMO LA 8
FASIHI
8.0 Utangulizi
Waalimu wengi hufikiria kwamba kila mwanafunzi anafahamu dhana na dhima
ya fasihi katika jamii. Hivyo waalimu wengi hawazingatii kueleza kwa ufasaha dhana za
kimsingi kuhusu maana ya fasihi na nafasi yake miongoni mwa jamii. Pia kama
inavyoonekana kwamba tamthilia, riwaya na shairi vina maumbo tofauti, basi hufikiriwa
watu hufahamu jinsi unavyoweza kuzibainisha nyanja hizi tatu za fasihi andishi kwa
urahisi na hawazitangulizi sura bainishi. Si ajabu kwamba hata vyuoni, licha ya shule za
upili, swali la kuzibainisha huleta utata kwa wengi. Mwalimu haachilii hoja yoyote kwa
matumaini kwamba mwanafunzi anafahamu tayari ama kuwa ni rahisi kufahamika, hivyo
si lazima kufunzwa darasani. Unapoanza kufunza, kulingana na daraja unalofunza na
utaratibu wa mafunzo, ni vyema kuwapa wanafunzi utangulizi utakaowatayarisha na
kuwasaidia kuzielewa hoja nyeti za somo hilo kadri linavyoendelea. Katika sehemu hii
msimamo huu ndio uliofuatwa katika kufunza hata ingawa kila jambo haliwezi
kuzungumziwa kwa ajili ya wakati.
MADHUMUNI YA SOMO
Kufikia mwisho wa somo hili, inatarajiwa kwamba utaweza:
Kufafanua dhana ya fasihi kwa upana wake
Kubainisha kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi
Kueleza umihimu wa fasihi miongoni mwa jamii
8.1 Dhana ya fasihi
Ni muhimu kabla ya kuzungumzia juu ya nyanja mbalimbali za fasihi mwalimu
amweleze mwanafunzi mambo mawili mahususi:
1. Dhana ya fasihi.
2. Dhima ya fasihi
Katika kutekeleza haya, jambo la kwanza ni kueleza fasihi ni nini.
1. Dhana ya fasihi
Fasihi ni maandishi ya kisanaa yanayoweza kuwa ya kihalisia ama ya kifantasia,
yaani kidhahania. Maudhui ya fasihi huchukuliwa miongoni mwa jamii na huwahusu
jamii anamoishi mwandishi. Tofauti ya maandishi ya kifasihi na maandishi mengine ni
ile hali ya fasihi kutumia kitengo cha ubunifu, kwamba mwandishi anaelezea maudhui
yake kwa njia ya kipekee. Fasihi hata ikiwa juu ya mambo halisia, haiwezi kuwa historia
106
ya jambo linaloelezwa. Hoja za kihistoria katika fasihi hunakshiwa kwa usanii hivyo japo
jambo ni la kweli, maelezo yake hayakubaliki kama historia. Msanii anaweza kutia katika
habari hizo za ukweli mambo ya kidhahania ili kuondoa kazi yake isifananishwe moja
kwa moja na hali zinazoonekana katika jamii hiyo.
Fasihi andishi hugawanyika katika nyanja tatu muhimu:
1. Riwaya
2. Tamthlia
3. Shairi
Tofauti ya nyanja hizi za fasihi ni katika umbo la uandishi wake.
8.2. Dhima ya fasihi
Wakati mwingi waalimu hawaoni haja ya kueleza dhima ya fasihi. Hili ni kosa na
upungufu wa ujuzi kwa upande wa mwalimu. Kujua fasihi ni nini pekee bila kutambua
nafasi na kazi yake miongoni mwa jamii hakutoshelezi. Kufahamu fasihi ni nini pekee
hakuifanyi fasihi kuwa mashuhuri na kufunzwa shuleni na vyuoni. Ujuzi huu hukamilika
unapoongezwa na ule wa umuhimu, na nafasi yake katika jamii.
Dhima ya moja kwa moja ni kuelemisha na pia kuwa kama kiliwazo katika
burudani ya jamii. Huelimisha kwa sababu msanii wa fasihi hujaribu kutatua matatizo ya
jamii, kuhusu maswala yanayowakumba. Mwandishi huwa tayari amechunguza
yanayoendelea miongoni mwa jamii yake, kuchambua na kudhihirisha masuala
yanayokumba jamii na kujaribu kuyatatua katika uandishi wake.
Kazi ya fasihi huhamasisha jamii hali kadhalika kuhusu fikra mpya ambazo huwa
chochezi kwenye mawazo ya jamii kuhusu hali zao za maisha katika mazingira yao.
Mwandishi huhamasisha kwa makusudi ya kuzingatia jinsi jamii inavyoweza
kujiendeleza, kubadilisha hali zao kuwa bora zaidi, kama watu binafsi ama jamii nzima.
Dhima nyingine yahusu kuliwaza jamii kwa ambavyo lugha ya fasihi huandikwa
kwa fani ya kupendeza, maudhui yake huazimiwa kuwafurahisha watu na wasomaji
wengi husoma fasihi ili wafurahike moyoni kwa sanaa hiyo. Mwanafunzi anatakikana
kutoa mifano kudhihirisha kuwa usomi wa fasihi hutumika kama kiburudisho kwa wengi.
Mfano watu wengi husoma vitabu vya hadithi jioni baada ya kazi za mchana koma. Nia
yake ni kujiburudisha kutokana na mawazo mazito ya shughuli za mchana kutwa. Pia
wengi hutazama maonyesho ya michezo ama filamu kwa kuburudika, haya yote yakiwa
katika kundi la fasihi na sanaa, isipokuwa kwa njia tofauti.
Katika kueleza maana ya fasihi watu wengi husahau kuifasiri fasihi kwa dhana
yake pana. Wengi wanapofikiria fasihi huzingatia tu kazi za sanaa zilizoandikwa.
Wengine pia hufikiria fasihi kuwa maandishi ya jamii fulani iliyoishi wakati fulani.
Wengine huona fasihi andishi kuwa zile kazi zilizopata umaarufu wa kisanaa. Kama
mwalimu ni muhimu ufahamu upotofu wa baadhi ya tafsili hizi. Aidha ukwepe kutoa
fasili finyu ya fasihi kwa wanafunzi wako.
Katika kupanua uwezo wa fikra wa mwanafunzi, utahitaji kuitazama fasihi kwa
hali ya kipragmatiki kulingana na maendeleo na mabadiliko ya kijamii. Kwa mfano,
tunaweza kutazama fafanuzi zifuatazo kuhusu fasihi.
107
TAFAKARI
Bainisha kati ya dhima ya fasihi na dhana ya fasihi. Toa mifano
inayodhihirisha dhima na dhana kama ulivyoelezea .
8.3 Mitazamo tofauti ya maana ya fasihi
Fasihi kama sanaa yo yote nyingine
Maelezo yanayotokana na mtazamo huu hudai kuwa fasihi ni kama kazi ya sanaa
yoyote nyingine kama vile michoro, michongo, ufundi na ustadi wa tungo tofauti. Sanaa
hutumia nakshi ya aina fulani, kusawiri ujumbe fulani ambao msanii anatarajia kuelezea
jamii kupitia kwa chombo alichochagua. Chombo hiki chaweza kuwa matumizi ya lugha,
ama uhunzi, au kuchora tu picha.
Katika usanii msanii huchanganya ubunifu na mambo halisia anayoyaona
yakiendelea mazingarani anamoishi. Fasihi hivyo huwasilishwa kwa maneno yenye
usanii ndani yake. Maneno haya yanaweza kuandikwa ama kusimuliwa . Basi maandishi
ama masimulizi ni nyenzo tu za kuwasilisha mawazo yanayohitajika kuelezwa jamii na
msanii ama mtungaji. Wanafunzi wafahamu wazi kuwa mbinu ya usimulizi kama ile ya
uandishi ni vyombo tu vya kuwasilisha na kuendeleza fasihi kwa aina na madhumuni ya
uwasilishaji kwa wakati wake.
Tunapolinganisha na sanaa nyingine, mbinu za usimulizi ama uandishi ni kama
uchoraji ambapo msanii hupaka rangi karatasi na brashi. Basi mtu hutumia usimulizi kwa
maneno, ama uandishi kwa kalamu na karatasi kueleza hisia ama ujumbe uliopo. Vile
vile ni kama mfumi anavyochukua kitambaa, sindano (fumo) na uzi kufuma nakshi katika
kitambaa hicho.
Ipo dhana ya fasihi kuwa mtungo wa maneno katika kueleza jambo fulani.Vile
vile, kama mtungo tunaweza kufananisha na msanii wa shanga za kuvaliwa shingoni,
ama zinazotungwa kwa kunakshi mavazi ya Wamasai kwa mfano. Kazi hizi zote
zinaonyesha usanii wa aina yake, na kama tungo zote huwasilisha maana fulani kwa jamii
inayohusika.
Ni muhimu kwa mwanafunzi kutambua kwamba sanaa hutokana na ubunifu wa
msanii kulingana na mambo halisi maishani anayoyaona na pia udhahania anaofikiria
yeye mwenyewe, bora uwe unawasilisha ujumbe fulani. Kama sanaa nyingine kwa hivyo
fasihi ina sifa hii pia. La muhimu ni kufahamu kuwa iwe sanaa ama fasihi inatokana na
hali halisi katika mazingira ama yatokana na fikra za msanii mwenyewe, lazima, ubunifu
wa msanii binafsi ndio utakaoifanya sanaa ama fasihi hiyo kufanikiwa na kuonewa
fahari. Pia ubunifu huu ndio utakaotoa ujumbe kwa hali ya wazi ili ufahamike bila
tashwishi.
Ambapo sanaa nyingine hutumia vitu kama vyuma, karatasi, rangi nguo na
kadhalika, sanaa ya fasihi hutumia lugha katika utunzi wake. Matumizi haya ya lugha
katika utunzi wake ndiyo hufanya watu wengine kuwa na maoni kuwa fasihi ni sanaa ya
lugha. Hii itaelezwa katika sehemu ifuatayo.
108
Fasihi kama sanaa ya lugha.
Mtazamo huu wa pili wazingatia fasihi kuwa chombo kinachodhihirisha ufanisi
wa lugha katika matumizi mbalimbali yanayotokea kwenye uandishi wa fasihi. Kama
tulivyosema fasihi hujumuisha umbuji na ubunifu wa msanii. Jinsi lugha inavyotumiwa
kwa madhumuni ya kupendekeza kazi hiyo kwa wasomi huweza kufananishwa na nakshi
juu ya sanaa ya mchongo kwa mfano ama urembo wa rangi zilizojitokeza katika mchoro
fulani.
Kwa mtazamo huu aidha ni vyema kumfahamisha mwanafunzi jinsi mtu binafsi
anavyotumia lugha kisanii huweza kumbainisha kutokana na msanii mwingine. Hii ni
kusema, baada ya msomaji kusoma vitabu vya fasihi vya mwandishi mmoja, anaweza
kujua kitabu kingine cha mwandishi huyo hata kama hajaangalia jina, kwa sababu ya ule
mtindo wa uandishi wa kitabu. Kwa mfano, jinsi Katama Mkangi anavyoandika ni tofauti
na Shaaban Robert, ijapokuwa wote wawili waliandika riwaya. Kando na maudhui kitu
nyeti kinachowatenganisha ni mtindo. Mtindo huu hudhihirika katika matumizi ya lugha
sahali, lugha ya mafumbo, matumizi ya masimulizi katika hadithi, nyimbo na kadhalika.
Kwa upande wa lugha kuna matumizi ya tanakali za lugha kwa mfano : sitiari, tashbihi,
majazi, kinaya, kupiga chuku,taashira, tashtiti, lakabu, taniaba, na tashhisi miongoni mwa
nyinginezo.
Aina nyingine za mitindo hutumia aina za misamiati tofauti ambayo mwandishi
hupendelea kuliko mingine. Uchaguzi huu wa msamiati hutegemea aina ya maudhui, na
madhumuni ya fasihi ile na pengine hadhira lengwa pia. Hapa inadhihirika kwamba si
jambo la bahati nasibu kwamba mwandishi ametumia lugha kwa namna fulani.
Mwandishi mpevu hudhamiria kutumia lugha jinsi anavyotumia anapoanza kuandika,
mara anapofikiria maudhui yake, hadhira yake na madhumuni ya kazi yake miongoni
mwa jamii.
Katika ufafanuzi uliotangulia hapo juu, tunapata fikra ya kuifafanua fasihi kuwa ni
mtindo wa mtu. Mwalimu aweza kueleza dhana hii kwa kutumia vitabu vinavyojulikana
na wanafunzi kutofautisha jinsi kwa mfano waandishi wawili wanavyotumia lugha.
Mfano wa rahisi kubainisha waweza kuchunguza urefu na ufupi wa sentensi. Waandishi
wengine hupenda kutumia sentensi ndefu ndefu ambapo wengine hutumia sentensi fupi
fupi. Bado wengine hutumia istilahi nzito na ngumu na wengine hutumia lugha sahali. Ni
kweli mwanadishi anaweza kugeuza mtindo wake, bali kazi zake nyingi hufuata kawaida
yake katika tabia yake ya matumizi ya lugha. Mlinganisho huu waweza kufanywa hata
kwenye uteuzi wa maudhui. Mfano Mkangi kazi zake za fasihi zimejikita katika maudhui
ya utetezi wa wanaonyanyaswa, watu wasiojiweza kiuchumi na kijamii.
Fasihi ni kioo cha jamii
Kumbuka kwamba tumetangulia kusema kwamba fasihi ama sanaa inaweza kuwa
ya jambo halisi hivyo ikaitwa fasihi ya kihalisia, ama kuwa ya kidhahania kwa ambavyo
imechimbuka kutokana na fikra za msanii. Mwanafunzi anapaswa kuelezwa tofauti hii
aifahamu tangu awali.
Tunnapozungumzia fasihi kuwa kioo cha jamii/lugha, tunasema kwamba fasihi
humwirika, ama huangaza maisha ya jamii fulani ambayo mwandishi anaishughulikia.
Mara nyingi jamii hii ni ya pale mahali mwandishi mwenyewe anapoishi. Kazi ya kiyoo
109
ni kuonyesha sura ya mtu ama kitu, jinsi kilivyo moja kwa moja. Mtu ama kitu hicho
huwa kimesimama mbele ya kiyoo ili sura hiyo itokee. Kiyoo hakionyeshi kufanana bali
mtu ama kitu halisia.
Mwalimu atumie maelezo haya kuwafanya wanafunzi wafahamu maana ya fasihi
kama kiyoo cha jamii, kwamba mwandishi hujaribu kueleza shughuli zinazoendelea
maishani miongoni mwa jamii waziwazi ili jamii ile ijione kupitia kwa kazi za fasihi ile.
Jambo hili hutekelezwa kupitia kwa maudhui teule ya kitabu, wahusika jinsi
wanavyosawiriwa na mazingira mathalan, muktadha na mandhari.
TAFAKARI:
Zingatia jinsi unavyoweza kuchambua fasihi ukajua madhumuni ya
mwandishi na somo alilotaka kuwafunza hadhira yake. Je ni nini
unachopata kama ujumbe unapochanganua mchoro wa picha kwa mfano ya
Dedan Kimathi kizimbani na minyororo?
ZOEZI 8.1
1. Eleza kwa ufasaha kwa nini unadhani fasihi yalinganishwa na sanaa
nyingine kama michoro, michongo na kadhalika.
2. Ukitoa mfano wa kitabu cha fasihi ulichosoma, eleza dhihirisho la
fasihi kuwa sanaa ya lugha.
3. Zingatia kitabu cha Mazrui, KILIO CHA HAKI ujadili hoja ya kuwa
fasihi ni kiyoo cha jamii.
8.4 Tanzu za fasihi
Baada ya kuzungumzia yaliyotangulia, ni bora sasa wanafunzi kuelezwa kwamba
fasihi ni pana na inajidhihirisha kwa tanzu zake. Tanzu za fasihi ni mbili kwa jumla:
1) Fasihi Simulizi
2) Fasihi Andishi
Tanzu hizi mbili za fasihi hujitambulisha kwa mbinu zake za mawasilisho, jinsi
zinavyohifadhiwa na kupendekezwa kwa watu. Utanzu mmoja wa fasihi huwasilishwa
kwa njia ya masimulizi. Hii huitwa Fasihi Simulizi. Utanzu wa pili huwasilishwa kwa
matumizi ya maandishi, na huitwa Fasihi Andishi. Kati ya aina hizi mbili, Fasihi
Simulizi ilianzia awali zaidi ya Fasihi Andishi. Ambapo fasihi Andishi ilitokea wakati
ambapo hati na maandishi yalibuniwa, Fasihi Simulizi ilitokea mara tu mawasiliano baina
ya binadamu yalipotukia.
Kwa upande wa dhima ya fasihi, aina zote mbili zina nafasi yake miongoni mwa
jamii. Aidha nafasi hizo zinapolinganishwa, nyingine ni bainishi na nyingine ni
unganishi. Pengine kwanza tuichunguze kila aina pekee yake kwa undani ili tufahamu
sifa unganishi na bainishi tunazozizungumzia.
110
Fasihi Simulizi
Fasihi simulizi huwasilishwa kwa njia ya maongezi. Aidha huhifadhiwa kutoka
kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya masimulizi na kukumbukwa katika fikra za jamii
mwaka baada ya mwaka. Si ajabu kwamba hadithi moja inaweza kuwa tofauti
inapotambwa na watu mbalimbali kwa sababu ya kutegemea kiasi cha kila mtu
atakavyokumbuka masimulizi ya awali. Kila msimulizi wa tungo hupewa sifa za kuwa
msanii na ana uhuru wa kueleza tungo hizo kwa umbuji wake mwenyewe. Hivyo
anaweza kuongeza fani mpya na kuendeleza maudhui anavyopenda. Ndiposa, tungo
katika fasihi simulizi hazina mtu maalumu anayesemekana kuwa msanii wake. Wingi wa
tungo hizo huwa mali ya jamii zinamoshughulikiwa.
Sifa za fasihi simulizi
Yapasa mwalimu amuongoze mwanafunzi kuzibainisha sura mbalimbali za aina
hizi za fasihi kando na kufahamu mbinu za mawasilisho yake.
1. Masimulizi hufanyika kwa njia ya maongezi, hivyo, chombo maalum cha fasihi
simulizi ni lugha ya maongezi. Tena kama ambavyo maongezi huhusisha hadhira,
hali kadhalika fasihi simulizi huhusisha hadhira katika kuiwasilisha, wakati
hadhira inaposikiza yanayosimuliwa. Masimulizi yanapoendelea, hadhira
huruhusiwa kuchangia na kumpa motisha msimulizi kwa kuitikia, kuimba naye,
ama kuuliza maswali na kushangilia hapo kwa hapo. Msanii ama mtunzi katika
fasihi simulizi hupata fursa ya kuingiliana na hadhira yake ana kwa ana na hata
katika majibizano.
2. Ni muhimu kwa wanafunzi kujua kwamba mtunzi ama msimulizi wa fasihi hii
huwa miongoni mwa wasimulizi wake. Wakati anaposimulia hutumia ishara za
miondoko ya mwili na anaweza kujua wakati huo huo kwamba anayosimulia
yapendeza hadhira ama la. Aidha msanii anaweza kujua ikiwa ujumbe katika
masimulizi yake wafahamika ama la.
3. Sifa nyingine bainifu ni kwamba fasihi hii haihifadhiki kwa njia nyingine
isipokuwa akilini mwa wale wasikizi waliopo. Kwa ajili hii hupitishwa chini kwa
vizazi vya baadaye kupitia masimulizi vile vile. Hivyo kadri ya vizazi
vinapoadimika ndivyo fasihi nyingi simulizi za jamii zinavyoadimika katika fikira
na myoyo yao.
4. Fasihi simulizi hubadilikabadilika kulingana na mapisi ya wakati, msimulizi na
madhumuni ya masimulizi yale. Kwa mfano, ngano iliyosimuliwa miaka ya
hamsini, sasa hata kama inajulikana bado kwa kupitishwa vizazi kwa vizazi,
itakuwa na tofauti katika maelezo yake, kwa ajili ya mengine kusahaulika, ama
mengine kuongezwa ama jinsi ilivyopokelewa na kufahamika tofauti na watu wa
eneo jingine.
111
5. Kwa ambavyo chombo kikuu cha Fasihi Simulizi ni mazungumzo, basi sifa
yake kubwa ni kwamba hubuniwa na kuwasilishwa wakati huo huo na yule
mtungaji kwa hadhira iliyipo na mara moja kuhifadhiwa katika akili za watu.
6. Baada ya miaka kadha kupita Fasihi Simulizi huwa miliki ya jamii. Watunzi
asilia huweza kusahaulika na nyimbo, ngano za mtunzi fulani zikawa urithi wa
jamii yake. Huu ni mfano mzuri wa sifa ya nne hapo juu.
7. Fasihi simulizi huwaunganisha watu wa vizazi vilivyopita na vya kisasa katika
kusikiliza mapisi ya wazee wao katika masimulizi yaliyojenga jamii hiyo, kwa
upande wa burudani, ufundishaji na maonyo.
8. Fasihi simulizi pia zimedhihirisha ushupavu wa matumizi ya lugha. Katika
umbuji wa ngano, vitendawili nyimbo na hata sarakasi, walioshiriki walihitaji
kuifahamu lugha kwa undani ili kuweza kuibua utungo wa sanaa miongoni
pengine mwa wasanii wengine. Hoja hii ni muhimu tunapofikiria nyimbo za
majigambo, mashairi ya ngonjera na kadhalika.
Aina za fasihi simulizi.
Aina za fasihi simulizi ni nyingi kuambatana na tajriba za wana-jamii. Hivyo, aina
zake zinaweza kuainishwa ifuatavyo:
Ngano
Hadithi
Mafumbo:
Vitendawili
Methali,
Semi
Ushairi:
Nyimbo
Majibizano
Ngonjera
Sarakasi
Tumeainisha aina hizo kwa makundi manne kwa jinsi ya utekelezaji na utenda kazi wake
na matazamio ya hadhira. Pengine ni vyema kusema kwamba aina za fasihi simulizi
hutegemea jamii mbalimbali na vitengo vya kijamii katika mazingira na utamaduni
fulani.
112
TAFAKARI:
1. Unapotafakari aina za fasihi simulizi katika jamii yako, unaweza
kuainisha makundi mangapi? Andika aina hizo kwa makundi uliyoainisha.
2. Fikiria ngano/hadithi ama wimbo unaosifika zaidi miongoni mwa jamii
yako ( si wa redioni, wala kanda zozote) na uchunguze wasanii asilia hasa
walikuwa akina nani. Ikiwa wasanii hao hawajulikani wafikiri ni kwa
sababu gani? Eleza na utoe ithibati.
ZOEZI 8.2
1. Linganisha na ulinganue sifa za fasihi andishi na fasihi simulizi
2. Kwa nini wafikiria vitendawili, methali na semi vimeainishwa katika
kundi moja?
3. Wasaidie wanafunzi wakupatie sifa za sarakasi katika jamii zao.
Bainisha sifa hizo na sifa za tamthlia.
4. Chunguza na ueleze jinsi fasihi simulizi inavyoendelezwa katika jamii
yako.
Sifa za Wasanii wa Fasihi Andishi na Fasihi Simulizi
1. Sifa muhimu yahusu wasanii wenyewe. Msanii wa fasihi andishi huwa pekee na vifaa
vyake vya uandishi anapokuwa akitunga kazi yake. Bali msanii wa fasihi simulizi tangu
awali huhusisha jamii ambao huwa hadhira yake anaposimulia na kueleza ujumbe wake
katika tungo anayowasilisha.
2. Ambapo mwandishi wa Fasihi Andishi ana nafasi ya kusahihisha kazi yake, kabla ya
kuitoa kwa wasomaji, msanii wa Fasihi Simulizi hana wakati huo, hivyo lazima
atahadhari kutoa utungo unaopendeza anapoanza kutunga. Msanii wa Fasihi Andishi
hukumbukwa hata baada ya karne kadha kupita kwa sababu kazi zake za kisanii
huhifadhiwa na jina lake kuendelea kuishi milele. Kinyume na haya msanii wa Fasihi
Simulizi kama tulivyotangulia awali kusema jina lake husahaulikwa kadri wakati
unavyopita na kazi kumilikiwa na jamii, kwa sababu ya kutojua mtunzi asilia.
Kumbuka kuwa wewe mwalimu, una jukumu la kuwasaidia wanafunzi wafikirie jamii
zao na tajriba wanazopitia katika jamii hizo kuhusu fasihi simulizi. Wahimize wanafunzi
kutoa mifano ya fasihi zinazopatikana katika jamii zao, na wachambue tofauti
zinazodhihirika.
113
ZOEZI 8.4
1. Chunguza jamii yako na jirani jinsi fasihi simulizi inayoendelezwa humo.
2. Linganisha aina za fasihi simuliza kama iliyoelezwa hapa na ile
inayopatikana katika jamii yako.
3. Chunguza jinsi fasihi simulizi inavyoendelezwa katika jamii yako.
4. Toa fafanuzi ya fasihi kama ilivyoelezwa hapa. Je, unakubaliana na dhana
hiyo?
8.4 Tanzu za Fasihi Andishi
Sehemu tuliyotoka tulishughulika na fasihi simulizi na tanzu zake mbalimbali. Sehemu
inayofuata tutashughulikia fasihi andishi.
MADHUMUNI YA SOMO
Kufikia mwishi wa sehemu hii, inatarajiwa kwamba utaweza:
Kubainisha kati ya tanzu tatu za fasihi andishi
Kufafanua jinsi kila utanzu unavyoendelezwa
Kubainisha aina mbalimbali za kila utanzu
Kuonyesha mahali pa tanzu hizi katika jamii.
RIWAYA
Kwa ufupi riwaya ni hadithi ndefu ambayo msanii ametumia maandishi kuisimulia. Ni
muhimu kumueleza mwanafunzi tofauti hii kati ya hadithi ndefu na dhana ya riwaya. Je,
hadithi yatakikana kuwa na urefu gani ili ikiandikwa iwe riwaya? Je, ni urefu na uandishi
vinavyounda na kufafanua riwaya? Ni sura gani zinazobainisha riwaya? Je, ni umbo
maalumu, matumizi ya fani na lugha? Fikra hizi zote zaonyesha jinsi ambavyo fafanuzi
ya riwaya ina utata unaohitaji kutatuliwa. Aidha yaonyesha matatizo yaliyopo ya
kubainisha aina za hadithi zinazowezekana kuwa riwaya.
Ni vyema kuwaeleza wanafunzi maoni mbalimbali kuhusu riwaya. Baadhi ya wataalamu
wanasema kuwa riwaya ni hadithi ndefu ambayo ina visa na vitushi na migogoro
inayoashiria shughuli zinazoendelea miongoni mwa jamii. Wengine husema kwa jumla
kuwa riwaya ni hadithi au kisa kirefu kilichoandikwa katika umbo la mtiririko wa
masimulizi. Ijapokuwa masimulizi haya yanahusiana na shughuli za jamii huu huwa ni
114
msingi tu. Ujengaji wa matini hujumuisha ubunifu wa msanii, jinsi ambavyo anauona
ulimwengu katika mazingira yake. Ubunifu huu hujumuisha uhalisia wa mambo na hali
ya kidhahania katika umbuji wa msanii. Mtindo wa aina hii huifanya riwaya kufahamika
kama sanaa ya kubuni. Ubunifu kwa hivyo, umejikita katika hali halisia za maisha ya
kijamii na viumbe vingine katika mazingira anamoishi mtungaji wa riwaya hiyo.
Kutokana na yaliyoelezwa basi yamkinika kwamba riwaya ni hadithi ndefu iliyoandikwa
kwa mtiririko fulani kuambatana na ubunifu wa mwandishi mwenyewe.
Yamkinika riwaya ama hadithi andishi barani Afrika ilijitokeza mnamo karne ya 19
na 20. Twasema hivi kwa sababu hati za uandishi zilijitokeza wakati huo kwa majilio ya
kisomo cha kiarabu cha dini na kuruhani, na vile vile, kisomo cha dini ya kikristo. Fasihi
andishi nyingi nchini Kenya zilichipuka wakati huu, kutokana na waandishi wa kiafrika,
ambapo zamani riwaya za Kiswahili na vitabu vya tafsiri kutokana na vitabu
vilivyoandikwa kwa Kiingereza kama vile:
Boi, “wema hawajazaliwa,”
“Juliasi Kaizari,”
“Kisima chenye hazina” n.k.
Siku hizi vitabu vilivyoandikwa asilia kwa Kiswahili ni vingi madukani na
vinaendelea kuchapishwa. Baadhi yavyo vimetia fora katika kutambaa kwenye maudhui
mbalimbali yanayoweza kuwavuta wasomaji wa Kiafrika. Aidha kwenye nchi
zilizotaarabika zamani, riwaya zimekuwa zikiandikwa kwa muda mrefu zaidi, kwa
sababu utamaduni wa kisomo ulianza zama hizo
Awali tumeuliza swali kutaka kutafakari kile kigezo cha urefu wa riwaya, ikiwa
urefu huu waweza kupimwa kuhusu ukamilifu wa riwaya
Yasemekana urefu wa riwaya watambulika katika matumizi yake au kuwa na
tukio zaidi ya moja, kujumuisha visa vingi, ujenzi wa wahusika wa aina mbalimbali
wanaoendelezwa katika hali za maendeleo na upevu wao maishani, na katika mazingira
wanamoishi. Baadhi ya wataalamu hueleza urefu wa riwaya kutokuwa chini ya maneno
35000. Katika urefu wake lazima mwandishi awe anafululiza maudhui kwa kuoanisha
vipengele hivyo vyote, na kuonyesha mwanzo unaendelea kupevuka hadi hatima ya
riwaya hiyo. Mtiririko huu uwe wa kuaminika na unaoweza kumshawishi msomaji
usahihi na uhalisi wa maudhui hayo. Kama hadithi inavyohusisha hadhira yake wakati wa
masimulizi, riwaya yatakika kuwaathiri na kuteka bakunja wasomaji wake na kuwatia ari
ya kusoma tangu awali hadi mwisho wa kitabu.
La ziada, pamoja na urefu, kuna upana wa mazingira na miktadha tofauti
inayopatikana katika riwaya. Mfano riwaya haiwezi kuanzia,” Sebuleni” na ikaendelea na
kuishia hapo tu bila kwingineko. Riwaya hujumuisha wahusika wengi na kila mmoja
huwa na nafasi maalum katika mfululizo wa maudhui ya riwaya.
Katika uandishi wa riwaya kutokana na yale yaliotangulia kuzungumzwa
unahusu: vipengele kadha kama vijenzi vya riwaya maudhui, ploti (kiini cha hadithi),
wahusika, migogoro, mandhari (mazingira), muundo na mtindo wa lugha. Uwiano wa
hayo yote unadhihirika kutegemea kiwango cha umbuji wa mwandishi. Kabla ya
kuchambua nafasi ya vipengele hivi vilivyotajwa kama vijenzi vya riwaya pengine
tungeeleza kuwa riwaya zipo aina tofauti. Kwa mfano, kuna riwaya ya uhalisia,
kijazanda, upelelezi, wasifu, kidhahairia n.k.
115
Jambo la kimsingi hapa mradi wanafunzi wafahamu msingi, muhimu na bainishi
ya riwaya kama ilivyozungumziwa hapo juu. Vigezo vya jumla vya riwaya hupatikana
katika aina hizi zote, ndiposa zikaitwa riwaya. Lakini, kila aina ina sifa, bainifu
zinazoleta ubinafsi wa kila aina, kulingana na jina lake.
AINA ZA RIWAYA
Zipo aina kadha za riwaya kama zilivyoainishwa na waandishi tofauti. Kwa mujibu
wa Wamitilla (2003), kuna aina nne dhahiri:
1. Riwaya sira
2. Riwaya kitawasifu
3. Riwaya kiambo
4. Riwaya ya kisaikolojia
Waandishi wengineo huzungumzia aina nyingine zinazoambatana na maudhui
yanayoendelezwa kwenye kitabu. Aina hizi ni kama :
Riwaya za upelelezi
Riwaya za Wasifu
Riwaya za uhalisia wa kijamii
Riwaya za Kifalsafa
Katika majina haya yote itabainika kwamba uzingativu wa ujumbe unaoshikilia
hadithi yote na mtindo wa hadithi huweza kumsaidia mwanafunzi kutambua aina ya
riwaya asomayo.
ZOEZI1.8.3
Kutokana na riwaya zilizoainishwa hapo juu jaribu kutafuta kitabu kimoja
kwa kila aina yazo kama ithibati yake.
116
HADITHI FUPI
Tumesema kwamba riwaya ni hadithi ndefu. Hii yamaanisha kuwa zipo hadithi
fupi, tena zilizoandikwa. Hivyo si kila hadithi iliyoandikwa ni riwaya ingawa tulitangulia
kusema kuwa riwaya ni hadithi iliyoandikwa. Pengine maneno, “hadithi fupi au ndefu”
ndiyo muhimu katika ubainishaji wa riwaya na hadithi fupi. Zote zimeandikwa bali
hadithi moja ni fupi na nyingine ni ndefiu. Ufupi wa hadithi hapa wategemea zaidi
upande wa mtindo na vipengele vinavyohusushiwa wakati wa utungaji na vilevile umbuji
wa msanii.
Jambo la kukumbukwa ni kwamba aina zote mbili za kuhadithia, kama ni riwaya
ama ni hadithi fupi – zote hutumia vipengele kadha vinavyolingana. Hivi ni kama
maudhui, mtindo, muundo, mazingira, wahusika, muktadha, migongano na pia dhamira
ya mwandishi au mtunzi.Vipengele hivi vyote huzingatiwa wakati wa uchambuzi wa
riwaya yoyote ile. Ili mwandishi afanikiwe katika riwaya yake, mambo hayo yote yabidi
kuafikiana na kuwa na mtiririko mzuri katika mwumano wake. Hivi ni kusema kwamba
vipengele hivyo vyote vitiririshi, maudhui kwa hali ya kupevusha na kurutubisha ploti ya
kisa/hadithi inayotungwa na kuandikwa.
8.5 Uchambuzi wa fasihi
Sehemu hii itachunguza vipengele vya uchambuzi wa fasihi andishi. Kwa jumla
ni muhimu kujua kwamba uchambuzi wa kazi yoyote ya fasihi iwe fasihi andishi ama
simulizi huwa mfano wa mfanyiko. Ili uweze kuchambua nyanja moja lazima kwanza,
uweze kuibainisha na zile zingine. Pia lazima sura/fani bainishi kuziainisha. Tatu,
vipengele vya jumla vya uchambuzi wa fasihi vitumike kama inavyohitajika. Wanafunzi
hapa yabidi wafahamu kwamba mtu hawezi tu kujitosa kwenye uchambuzi wa kitabu
kiholela ama pasi kuwa na utaratibu wenye mwelekeo. Kila moja wapo ya nyanja hizi
zina misingi yake muhimu ya kuweza kuichambua. Mwalimu atambue kuwa wanafunzi
wengi wakiona vitabu hivyo vitatu huweza kusema hiki ni kitabu cha shairi, hiki ni cha
tamthilia na kile: cha riwaya – bila kutambua sifa bayana. Mwalimu achukue jambo hili
kama jukumu la kimsingi.
SIFA BAINISHI ZA RIWAYA
Kwanza tumesema riwaya ni hadithi ndefu inayojumuisha visa vingi
vilivyoendelezwa kwa hali ya muumano na maafikiano kufanikisha maudhui ya
riwaya yenyewe.
Huwa kuna ploti inayoendelezwa na visa vingi vinavyojitikeza kwenye
riwaya na huwa vinaendeleza ploti hii moja. Ploti ni kama shina linalochomoza
miche inayonawirisha mti.
Riwaya ina mgawanyiko wa sura. Nambari ya sura katika riwaya inategemea
urefu wa sura, visa vinavyoendeleza ploti na utofauti wa mandhari, wakati,
muktadha na wahusika, dhamira ya sura hiyo katika riwaya na migongano
117
inayotukia miongoni mwa jamii husika. Sura hizi huifanya riwaya isichoshe
msomaji kwa urefu wake.
Maudhui wakati mwingi huwa ni ile kubwa/msingi na maudhui ndogondogo
kulingana na visa vinavyoandikwa. Ifahamike kuwa maudhui ndogo zote
zitakikana kuchangia maudhui kubwa/msingi ya riwaya. Haiwezekani mwandishi
mweledi kuiruhusu maudhui yoyote ndogo kujisimamia, kwani ingepnekana kuwa
hadithi ya pekee. ……
Maudhui ya riwaya hujikita katika jamii ya mwandishi kwa kawaida. Tajriba
ya mwandishi maishani huathiri sana maudhui ya riwaya.
Wahusika huwa wengi kulingana na urefu wa riwaya. Hawa hugawanyika
katika wahusika wakuu na wahusika wadogo kuambatana na nafasi wanayochukua
katika mtiririko wa maudhui.
Lazima kila riwaya iwe na kilele chake. Kilele ni upeo wa riwaya katika
uandishi na hata usomaji ambapo visa vilivyosimuliwa hupamba moto na
mgongano kutokea ama suluhu kupatikana. Hiki ni kilele kinachojengwa tangu
mwanzo wa uandishi wa riwaya hadi mwisho
Dhamira ya mwandishi hujitokeza kadri maudhui na mtiririko wake na aina
ya wahusika na jamii wanavyoendelezwa.
Sura hizi zote husaidia kuifanya riwaya ipendeze kwa msomaji na humpa mwelekeo
mwandishi katika kufanikisha riwaya yake kwa wanii unaofanya kazi hiyo ya fasihi
ijipendekeze kwa wasomaji.
ZOEZI 8.5
1. Sifa zilizoorodheshwa hapo juu ni za riwaya. Zingatia hizo na uorodheshe
sifa za hadithi kulingana na jinsi inavyosimuliwa katika jamii yako.
3. Je kuna tofauti zozote? Hebu zieleze.
Pengine tungeeleza kwa jumla uchambuzi wa fasihi andishi , yaani vipengele vya kijumla
vinavyohitajika kufahamika na mwanafunzi.
Maelezo ya kumwelekeza mwanafunzi kuhusu uchambuzi wa fasihi kwa jumla ni kama
uzingatifu kuhusu:
1. Ploti,
2. Maudhui,
3. Wahusika walivyosawiriwa,
4. Mgogoro
5. Taharuki
6. Mtindo wa mwandishi,
7. Matumizi ya lugha,
8. Mandhari.
118
1. Maudhui
Hapa mwanafunzi aongozwe zaidi ya kuona tu ujumbe wa hadithi unaojitokeza. Ni
muhimu mwalimu kumsaidia mwanafunzi kuiona dhamira ya mwandishi katika kutunga
riwaya ile pia. Jambo analodhamiria mtunzi ndilo linaloendelezwa kwenye maudhui ya
riwaya. Kwa kutofautisha bayana, dhamira hasa yahusu fikra ya mwandishi
inayokaririwa katika visa na maswala yote yatakayoshughulikiwa katika riwaya hiyo,
kama kazi ya sanaa.
Ploti
Katika kuchambua maudhui mradi mwanafunzi azingatie ploti ya mwandishi. Ploti ni
wazo kuu ambalo ni kama uti wa hadithi inayoandikwa. Ni kutokana na ploti ambapo
maudhui huendelezwa na kuwekewa mipaka ya mapana na marefu yake; ujengaji wa
wahusika na vitushi vitakavyosimuliwa. Ploti hushikilia vipengele mbalimbali
vinavyohitimisha hadithi kama muktadha, mazingara na nafasi za wahusika katika
riwaya.
Wahusika
Mchambuzi wa Fasihi yapasa atambue viwango vya wahusika waliomo kwenye
riwaya ama tamthlia, na nafasi zao katika usimulizi wa hadithi yote. Huwako muhusika
mkuu anayeanza hadithi na kuendelea hadi tamati. Tena wako wahusika saidizi . Hawa
husaidia kumjenga muhusika mkuu katika tabia na hulka yake kwa jumla. Hawa ndio
wanaoendeleza maudhui kadri yanavyotiririka hadi kufikia kikomo.
Yapasa mwanafunzi aelezwe kuwa msanii wa kazi ya fasihi huchagua lugha
anayoitumia katika utunzi wake kwa makini zaidi. Wakati wa kuchambua itabidi
kuchunguza kama lugha inaeleweka vyema na kufaa maudhui yaliyopo au la. Je, ni lugha
ngumu ama rahisi kwa wasomaji wa kazi hiyo.
Mwalimu atalazimika kuelezea jinsi kila kipengele kinavyochangia ufanisi wa
matini inayochambuliwa.
La kutaja hapa ni kwamba uchambuzi wa shairi utakuwa tofauti kiasi kwa ajili ya
mtindo wake tofauti. Ingawaje, tofauti kubwa ni kule kutokuwa na wahusika
waliosawiriwa kama katika tamthlia na riwaya. Ni juhudi ya mwalimu aweze kumfanya
mwanafunzi wake apende mashairi pasi kuogopa. Wengi huyaona mashairi kuwa
magumu kueleweka, pengine ni kwa sababu, hata waalimu wenyewe hawachukui wakati
wa kuyasoma na kuyaeleza vilivyo.
VIFAA VYA KUFUNZA FASIHI
Mwalimu anaweza kutumia vifaa tofauti kulingana na umbuji wake na kiwango
cha wanafunzi wake. Ikiwa wakati upo, ni vyema kwa mfano kuiga onyesho moja la
tamthlia unayoifunza darasani. Hivyo watapata tajriba ya wahusika, kuupa uhai mchezo
na kuzua hisia zinazotakikana kudhihirishwa na uteuzi wa lugha iliyotumika.
Wakati mwingine kama ni tamthlia, riwaya ama shairi, hata kusoma kwa sauti
darasani husaidia kuwafanya wanafunzi wakumbuke hoja muhimu. Na, ikiwa yapo
makundi ya watu wanaoweza kukariri mashairi, ama kuiga michezo jukwani, ni vyema
kujaribu kuwapeleka wanafunzi wako wakajionee. Yote haya yategemea mwalimu
mwenyewe na mbinu atakazofuata za ufundishaji.
119
MAREJELEO.
1. Rocha Chimerah & Njogu Kimani (1999): Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia Na
Mbinu. Jomo Kenyatta Foundation. Nairobi.
2. Vincent Kawoya (1988), Mbinu za Kufundisha Kiswahili. Nairobi University
Press
3. Goeffrey K. King’ei & Paul M. Musau (2002), Utata wa Kiswahili Sanifu,
Didaxis, Nairobi, Kenya
4. Musau P.M. & Chacha L.M. (2001): Mbinu sa Kisasa za Kufundisha Kiswahili,
Kenya Literature Bureau.
5. Gerald Njagi Matti (2002), Introduction to The Study of Literature, Institute of
Open Learning, Kenyatta University.
6. K. W. Wamitilia (2002), Uhakiki wa Fasihi Msingi na Vipengele Vyake. Phoenix
Publishers Ltd
7. Wilkins, D. D. (1972) Linguistics in Language Teaching, Edward Arnold,
London..
8. Kiswahili Syllabus for Kenya Certificate of Secondary Education, K.I.E.
.