working paper cover manufaa 4 (2) - hakielimuhakielimu.org/files/publications/elimu jumuishi...

12
11. Elimu Jumuishi kwa Maendeleo ya Elimu kwa Wote Tanzania Tujifunze pamoja tujenge jamii inayowakubali watu wa aina zote Mtemi Gervas Zombwe 11.4.k Nyaraka ya Kufanyia Kazi

Upload: others

Post on 02-Feb-2020

3 views

Category:

Documents


0 download

TRANSCRIPT

Page 1: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

11.

Elimu Jumuishi kwa Maendeleo ya Elimu kwa Wote TanzaniaTujifunze pamoja tujenge jamii inayowakubali watu wa aina zote

Mtemi Gervas Zombwe

11.4.k

Nyaraka ya Kufanyia Kazi

Page 2: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

1

Manufaa ya Elimu Jumuishi kwa Maendeleo ya Elimu kwa Wote, Tanzania

“Tujifunze pamoja tujenge jamii inayowakubali watu wa aina zote”

Na Mtemi Gervas Zombwe1

1.0 Utangulizi

Miongoni mwa malengo muhimu ya elimu Tanzania ni kuendeleza na kukuza upatikanaji wa fursa na mahitaji ya watu ya kimaendeleo katika jamii. Ili kufikia malengo ya elimu nchini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeazimia kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapatiwa fursa ya elimu [URT], 2001a). Wizara imeazimia kuhakikisha kuwa watoto wote wanaoishi katika mazingira magumu, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata fursa ya elimu (ibid). Ili kutimiza malengo ya elimu, Tanzania imejiwekea mikakati, miongoni mwayo ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapewa fursa ya elimu ifikapo mwaka 2010 kwa asilimia 100 (ibid., uk.7). Ili kufikia malengo na matarajio ya elimu kwa wote, watoto wenye ulemavu wanapaswa kuandikishwa na kumaliza elimu ya msingi na kuendelea.

Kuna njia tatu ambazo zinaweza kutumiwa ili kuendeleza pamoja na kutoa fursa zaidi za elimu mahususi kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu wakiwemo wenye ulemavu. Njia hizo ni: shule maalumu, shule zenye watoto mchanganyiko na elimu jumuishi. Shule maalumu mara nyingi hutoa huduma kwa ajili ya watoto wenye ulemavu tofauti na shule za kawaida. Shule mchanganyiko hutoa mafunzo kwa watoto wenye ulemavu sambamba na wale wasio na ulemavu. Hata hivyo, muda wa ziada hutengwa kwa ajili ya kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ulemavu. Elimu jumuishi huwawezesha watoto wote kusoma katika shule moja na katika mazingira ya aina moja (kama vile darasa moja) bila ya kuwabagua watoto wenye mahitaji maalumu pamoja na wenye ulemavu.

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikitilia mkazo elimu ya watu wenye ulemavu kupitia elimu kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu. Bila shaka, elimu kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu imekuwa ikipewa kipaumbele katika sekta ya elimu, sambamba na elimu ya awali, elimu ya msingi, elimu ya watu wazima, elimu ya sekondari, na elimu ya ualimu (URT, 2001b). Elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu

1 Mtemi Gervas Zombwe ni Mwalimu, Mtafiti na Mchambuzi wa Sera, HakiElimu. Anapatikana kwa barua pepe [email protected] au [email protected]

Page 3: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

2

ni ile inayotolewa kwa watoto wenye ulemavu. Kimsingi aina saba za ulemavu zimeweza kutambuliwa nazo ni ulemavu wa macho, ulemavu wa kusikia, ulemavu wa ngozi, ulemavu wa akili, ulemavu wa viungo, ububu na ukiziwi (URT, 2001b, uk. 11).

Elimu jumuishi katika siku za karibuni ndiyo imepewa kipaumbele zaidi kuliko aina nyingine na inachukuliwa kama njia bora zaidi katika kufanikisha malengo ya elimu kwa wote. Kimsingi, Tanzania imeridhia matamko mbalimbali ya kimataifa ambayo yamelenga kuinua elimu jumuishi mashuleni, miongoni mwa matamko hayo ni tamko la Haki za Watoto, 1386/1959, Tamko la Haki za Watu wenye Ulemavu, 3447/1975 na Tamko la Salamanka na Hatua za utekelezaji wake (UNESCO, 1947). Tamko la Salamanka na Hatua za utekelezaji wake (UNESCO, 1947), kwa mfano, limeridhia haki za elimu kwa kila mtu kama lilivyoelezwa katika tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, 1948, na kuboreshwa katika mkutano wa Dunia wa Elimu wa mwaka 1990 ambao ulitilia mkazo elimu kwa wote kwa msingi wa haki za binadamu bila kujali tofauti baina ya watu (uk. Vii).

Misingi ya Tamko la Salamanka na namna ya kulitekeleza ni kuhakikisha kuwa shule zote zijenge mazingira mazuri ya kusomea kwa watoto wote bila kujali tofauti ya viungo, uwezo wa akili, jamii atokayo mtoto, lugha pamoja na mambo mengine; yakiwemo watoto wasiojiweza pamoja na wale wenye uwezo wa juu kiakili bila kuwasahau wale wanaotoka katika maeneo yaliyotengwa kielimu na yale makundi ya watu waliosahauliwa (uk.6).

Pia Tanzania imeridhia Azimio la Elimu kwa Wote (EFA). Elimu kwa wote huendana na kutoa fursa katika elimu ya msingi kwa watoto wote, ni elimu endelevu, huzingatia ubora wa elimu pamoja na kuwahusisha watoto wote, wakiwemo wenye ulemavu (UNESCO, 2000). Hii ina maana kwamba bila kuendeleza sera za elimu jumuishi katika elimu na kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapatiwa fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya Elimu kwa wote yanaweza yasifikiwe.

2.0 Maana ya Elimu Jumuishi

Dhana ya elimu jumuishi imekuwa ikibadilika kulingana na wakati. Mwanzoni elimu jumuishi ilimaanisha kitendo cha kuwajumuisha watoto wenye mahitaji maalumu katika madarasa yenye watoto wasio na ulemavu. Wanazuoni wa siku hizi wamekuwa wakitumia elimu jumuishi kumaanisha dhana pana zaidi, ambayo mbali na kuwahusisha watoto wenye mahitaji maalumu (wenye ulemavu), dhana hii sasa inatumika kumaanisha pia watoto wanaoishi katika mazingira magumu (Beyers & Hay, 2007).

Kwa hiyo waandishi wengi wamekuwa wakitumia dhana ya elimu jumuishi kumaanisha watoto wenye aina mbalimbali za uwezo na wale wenye ulemavu (Salend, 2001; 1996; Roach, 1995). Kwa hali hiyo elimu jumuishi ni aina ya elimu inayowaweka pamoja watoto wenye mahitaji maalumu, wale wenye uwezo wa juu kiakili na wale wenye

Page 4: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

3

ulemavu (Lloyd, 2008). Dhana ya elimu jumuishi imejengeka katika falsafa kwamba watoto wote, bila kujali aina ya ulemavu pamoja na uwezo wao kiakili, wanapaswa kuelimishwa katika madarasa ya kawaida ambapo watasoma pamoja na watoto wenzao wenye umri unaofanana (Crawford, 1994).

Kujumuishwa katika elimu ni mbinu ya kuwaelimisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu ya kielimu. Chini ya mfumo jumuishi, wanafunzi wenye mahitaji maalumu hutumia muda wao mwingi au muda wao wote na wanafunzi wasio na ulemavu. Utekelezaji wa vitendo hivi hutofautiana. Baadhi ya shule mara nyingi huchagua aina fulani ya watu wenye ulemavu ndiyo huwajumuisha

Elimu jumuishi hutofautiana na mtazamo wa zamani wa 'shule mchanganyiko' na 'shule zenye vitengo vya walemavu', ambazo zilikuwa zinashughulikia zaidi ulemavu na mahitaji maalum ya kielimu.

Tofauti na mtazamo huo, elimu jumuishi kwa sasa inahusu haki ya mtoto ya kushiriki na wajibu wa shule kumkubali mtoto mwenye ulemavu. Elimu jumuishi inapinga matumizi ya shule maalumu au madarasa yanayowatofautisha wanafunzi wenye ulemavu na wale wasio na ulemavu. Mkazo umewekwa kwenye ushiriki kamili wa wanafunzi wenye ulemavu na juu ya heshima kwa haki zao za kijamii, kiraia na kielimu.

3.0 Hitaji la Elimu Jumuishi Hitaji la elimu jumuishi liko kwenye misingi mikuu mitatu, kwanza ni hitaji la msingi la kuzaliwa kwa binadamu wote; yaani ni haki ya binadamu wote kujumuika na kujifunza pamoja. Pili, linaleta usawa katika upatikanaji wa elimu bora inayokuza vipawa kwa pamoja. Kila mtu ana vipaji na vipawa vyake, hivyo wanapokusanyika wanafunzi wenye sifa tofauti wanabadilishana uzoefu, maarifa na kusaidiana kujenga vipawa kwa pamoja. Mmoja anaweza kuiga kwa mwenzake na akapata faida ya maarifa ya mwenzake. Na tatu; ni kujenga jamii moja yenye watu wa-moja wenye kuheshimiana na kupendana bila kujali tofauti zao. Msukumo wa hitaji hili umejengwa kwenye masuala yafuatayo:-

3.1 Watoto wote wana haki ya kujifunza pamoja. Watoto wote bila kujali ulemavu au rangi hawapaswi kudunishwa, kudharauliwa, kubaguliwa wala kutengwa kwa sababu ya ulemavu wao au uwezo wao mdogo katika kujifunza. Ni kinyume na haki za binadamu.

3.2 Watu wazima wenye ulemavu, wanaelezea wenyewe mfumo wa nyuma katika shule maalumu ulivyowafanya kuwa waathirika wa kubaguliwa, na wanadai mwisho wa ubaguzi.

3.3 Hakuna sababu za kuwatofautisha watoto kwenye haki yao halali ya kupata elimu bora pamoja. Watoto ni wamoja - kwa faida na manufaa kwa kila mtu.

3.4 Utafiti unaonesha watoto hufanya vizuri, kimasomo na kijamii katika mazingira jumuishi.

3.5 Hakuna mafunzo au huduma katika shule baguzi ambazo hazifanyiki katika shule za kawaida.

Page 5: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

4

3.6 Kutokana na kuwepo kwa ushirikiano, elimu jumuishi ni matumizi mazuri zaidi ya rasilimali za elimu.

3.7 Ubaguzi unawafundisha watoto kuwa waoga, wajinga na wenye chuki na visasi. 3.8 Watoto wote wanahitaji elimu ambayo itawasaidia kukuza uhusiano na kuwaandaa

kwa ajili ya kuyatawala maisha.

3.9 Kujumuishwa kunaleta uwezekano wa kupunguza hofu na kujenga urafiki, heshima, kuelewana zaidi miongoni mwa jamii. 4.0 Uhalali wa Elimu Jumuishi Elimu imejengwa katika msingi wa haki za binadamu. Yaani kila binadamu ana haki ya kujumuika na kupata mahitaji yake kamilifu akiwa ndani ya jamii bila kutengwa wala kubaguliwa. Haki ya kujumuika, kuwa pamoja, kutambuliwa na hata kuthaminiwa ndio msingi wa utu wa mwanadamu (Zombwe, 2008). Lakini pia elimu jumuishi inapata uhalali mkubwa kutoka kwenye sheria, maazimio na mikataba mbali mbali ya kimataifa na kitaifa inayohimiza ujumuishi na kuthamini utu pamoja na kuondoa aina zote za kutengwa au kubaguliwa. Vyombo hivi vya kitaifa na kimataifa baadhi yake vimeorodheshwa hapa chini:-

4.1 Maazimio ya kimataifa yanayohimiza Elimu kwa watu wenye Ulemavu

Tamko la umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu,UDHR, 1948 Ibara 26

Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu(2006)

Mkataba wa Haki za Mtoto (1989)

Kanuni za Kimataifa kuhusu Usawa wa Fursa kwa watu wenye ulemavu(1993)

Tamko la Salamanka juu ya Usawa Ki-elimu(1994)

Tamko la Dakar kuhusu Elimu kwa Wote (EFA 2002)

Malengo ya Milenia (MDG,II 2000)

4.2 Vyombo vya kitaifa vinavyohimiza Elimu kwa watu wenye Ulemavu

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977(Ibara 12; 4, 5)

Sera ya Taifa ya Maendeleo ya watu wenye Ulemavu (2005; 5)

Sera ya Elimu na Mafunzo (ETP: 1995;Uk 17, 18:3.2.1)

Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA: 2005-2010, B. 1.3)

Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES 2005-2009, lengo II)

MMEM Awamu wa pili (2007-2011, lengo I)

Page 6: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

5

5.0 Msingi mkuu wa Elimu Jumuishi

Elimu jumuishi imejengwa kwenye msingi wa utu na ubinadamu wa kuishi pamoja na kushirikiana. Kiasili jamii zote ulimwenguni zina asili ya kuwa pamoja na kuthaminiana, ndio maana kuna familia, kuna jumuiya kuna vikundi na kuna wananchi katika kila taifa. Elimu jumuishi inaleta fikra za kuheshimiana, kujaliana na kufurahia kwa pamoja uumbaji wa Mungu huku kila mmoja akitambuliwa thamani yake na vipawa vyake ndani ya jamii moja. Umoja na mshikamano miongoni mwa watu, ndio msingi wa kujenga utulivu kwa watu wanaoshirikiana kwa kila jambo. Je, iweje leo baadhi ya watu kwa sababu tu za maumbile yao au mapungufu ya sifa za maumbile yao watengwe na wengine, wakati upungufu wa kiungo kimoja hauathiri ubora wa kiungo kingine? Iweje leo jamii ziwaone watu wenye ulemavu kama watu nusu wasiokamilika? Iweje leo thamani ya watu wenye ulemavu iwe kwenye masuala yasiyo ya maana kama sherehe na misiba, na isiwe kwenye masuala ya muhimu kama elimu, ugawaji wa rasilimali, na fursa za ajira na maisha bora kwa kila binadamu?

6.0 Sifa muhimu za Elimu Jumuishi2

Elimu jumuishi ina sifa kuu zifuatazo:-

6.1 Ni falsafa inayojenga umoja, thamani na upendo kwa kila mmoja ili kuyafikia mafanikio kwa pamoja na kuondoa ubaguzi miongoni mwa wanajamii.

6.2 Ni chimbuko la utu unaojenga jamii yenye ushirikiano na usawa katika kunufaika fursa za elimu na rasilimali za jamii. Inaleta tija kwenye kuondoa fikra za kutengwa na kudunishwa kwa baadhi ya wanajamii kutokana na ulemavu au kutoka makundi yenye changamoto nyingi.

6.3 Inajenga fikra za kujiamini na kukuza vipaji kwa watu wenye sifa tofautitofauti za kimaumbile na hali ya kiuchumi. Kupitia elimu jumuishi watu wenye ulemavu hujiona wenye thamani na wanaweza. Na hivyo, watajiamini kufanya lolote kwa muda wowote; maana jamii inakuwa tayari inafahamu uwezo wao na hivyo haitakuwa kikwazo kwao.

6.4 Elimu jumuishi inajenga vizazi vyenye fikra na matendo jumuishi. Watoto waliosoma na watu wenye ulemavu darasa moja watakuwa na fikra za kuthamini watu wenye ulemavu na wataweza kuendeleza fikra jumuishi nyumbani kwao, kazini na hata kwenye vyombo vya maamuzi iwapo watapata nafasi za kufanya hivyo. Hawataweza kuwashangaa au kuwafikiria tofauti watu wenye ulemavu;

2 Elimu jumuishi imejengwa katika msingi wa umoja na mshikamano, falsafa ambayo Mwl Nyerere aliiamini sana na akahamasisha ujamaa miongoni mwa jamii.

Page 7: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

6

maana wamekuwa nao, wamecheza nao, wamefurahi nao, wamesoma nao, na wameshirikiana nao kwa mambo mengi.

6.5 Elimu jumuishi ni shirikishi zaidi. Haimwachi mtu nje ya makundi ya kijamii. Watu wote wanashirikishwa katika kila jambo. Hivyo, jamii inakuwa na faida zaidi maana kila aina ya elimu au taarifa itajulikana pia kwa watu wenye ulemavu.

7.0 Fursa3 za Elimu Jumuishi Tanzania Kama taifa, na wananchi wa Tanzania tuna fursa nyingi sana ambazo tunaweza kuzitumia kutoa elimu jumuishi kwa wananchi wetu, na makundi yote ya wanajamii wakanufaika na elimu hiyo. Baadhi ya fursa hizo ni:- 7.1 Kuna sheria za kimataifa na kitaifa ambazo zinatoa fursa kwa wananchi wote kupatiwa elimu bila ubaguzi. Nchi yetu imeridhia mikataba mingi ya kimataifa ambayo inapaswa kutekelezwa kwa vitendo. Kwa kupitia mikataba hii serikali inalazimika kuitekeleza kwa vitendo ili kutoa elimu kwa wote. Mifano ya mikataba hiyo imeoneshwa kwenye kipengele namba 4. 7.2 Pia tuna rasilimali nyingi ambazo zimeizunguka nchi yetu, ambazo kwa njia moja au nyingine zinaweza kutumika kusaidia utoaji elimu jumuishi. Ziara za mafunzo, mbao za kutengenezea vifaa vya kujifunzia na kufundishia, ardhi nzuri kwa ajili ya majengo pamoja na rasilimali watu ambao ndiyo nguzo ya ufanikishaji wa elimu jumuishi. 7.3 Tuna wingi wa majengo ya madarasa (shule) ambayo tunaweza kuyaboresha tu na yakafaa sana kutolea elimu jumuishi kwa watanzania wote. Mathalani, tuna shule za sekondari karibu kila kata. Hivyo, watu wenye ulemavu wanaweza kupata nafasi zaidi maeneo ya karibu kusoma pamoja na wenzao kwenye shule hizo. Pia tuna shule nyingi za msingi ambazo zinasaidia sana katika utoaji elimu kwa watu wote. 7.4 Kuwepo kwa asasi za kiraia zilizo sambaa kote nchini ni fursa nzuri ya kufanikisha elimu jumuishi. Asasi hizi zina mchango mkubwa sana katika kutoa elimu jumuishi na kuelimisha umma kuhusu kuthamini makundi ya watu tofautitofauti, kuanzia nyumbani hadi maeneo ya kazi. Asasi za kiraia pia zina mchango mkubwa wa kuboresha miundombinu ya watu wenye ulemavu ili washiriki kiurahisi katika kupata elimu na fursa nyingine za kijamii.

3 Waliofanikiwa ni wale wanaoziangalia na kuzitumia fursa zilizopo sio wanaoangalia vikwazo na changamoto walizonazo.

Page 8: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

7

7.5 Uwepo wa vyombo vya habari kwa wingi ni fursa pia inayosaidia utoaji elimu jumuishi. Wanahabari wana mchango mkubwa katika kuelimisha jamii kuhusu elimu jumuishi; pia kutoa taarifa za vitendo vibaya vinavyoashiria uonevu, udhalilishaji na ubaguzi wa baadhi ya makundi katika jamii. 7.6 Kuwepo kwa taasisi nyingi za dini ambazo pia zinachukua sehemu kubwa ya wanajamii na zinafanya kazi ya kutoa elimu kwa jamii. Asasi hizi bado zinaheshimika sana katika jamii. Hivyo, zinaweza kutumika kuhamasisha jamii kujenga fikra jumuishi na kuwa pamoja na watu wenye mahitaji muhimu. Pia taasisi hizo zinaweza kuwa mfano bora kwa kuwajumuisha wanafunzi wa sifa mbalimbali kwenye madarasa yaleyale na kutoa elimu bora. 7.7 Uwepo wa serikali za mitaa na viongozi hadi ngazi za msingi kabisa ni fursa pia katika utoaji wa elimu bora jumuishi. Viongozi ni chachu ya mabadiliko. Wakihamasishwa na kuelimishwa kuhusu elimu jumuishi nao wanaweza kuwahamasisha wananchi wao ili kujenga fikra4 jumuishi na wakasimamia utoaji elimu kwa makundi yote katika shule zote nchini.

8.0 Changamoto katika kutoa Elimu Jumuishi

Kuna changamoto nyingi zinakwaza utekelezaji wa elimu jumuishi katika jamii zetu na nchini kwetu. Licha ya ukweli kwamba elimu jumuishi inawezekana, bado changamoto hizo hazijapata utatuzi. Na hivyo, kubaki kuwa vikwazo vya kufanikisha elimu jumuishi. Baadhi ya changamoto kubwa ni:- 8.1 Wanajamii wengi pamoja na viongozi wa serikali na taasisi mbalimbali bado hawana mawazo na fikra jumuishi. Matendo yao na maamuzi yao bado yametawaliwa na fikra za zamani za kuwatenga, kuwabagua na kuwadunisha watu wenye ulemavu. Ndio maana hata kwenye ujenzi wa miundombinu ramani zinazochorwa hazijengi mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu na hata sheria na sera za nchi katika maeneo mengi zimewabagua watu wenye ulemavu. Kama kiongozi akiwa na fikra zisizo jumuishi hawezi kufanya maamuzi yaliyojumuishi. Kama bunge halina fikra na mtazamo jumuishi haliwezi kufanya maamuzi na kutunga sheria zilizojumuishi. Kama mzazi5 hana fikra jumuishi hawezi kumjumuisha mtoto wake kwenye fursa za elimu na rasilimali za familia kwa ukamilifu kama watoto wengine wasio na ulemavu. Hii ndiyo changamoto kuu (zombwe, 2008). 8.2 Ukosefu wa malengo ya wazi na ushahidi ulio wazi wa manufaa ya elimu jumuishi kwa jamii pana imekuwa ni changamoto. Mafanikio ya elimu jumuishi yanategemea

4 Kiongozi mwenye fikra zisizo jumuishi, mwenye ubaguzi na ubinafsi hawezi kutunga sera jumuishi, mipango jumuishi. 5 Baadhi ya wazazi ndani ya jamii wamethubutu hata kuwatupa watoto wenye ulemavu au kuwaua. Mzazi kama huyu hawezi kuhakikisha mtoto wake anapata elimu katika mazingira jumuishi.

Page 9: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

8

sana jinsi nchi inavyoelewa na kuelezea ubora na manufaa ya elimu jumuishi pamoja na namna ya kutekeleza kupitia mtaala rasmi. Hili bado ni tatizo.

8.3 Changamoto kubwa katika kuendeleza elimu jumuishi pia iko kwenye nyenzo na vifaa vya kuendeshea elimu jumuishi kama vile (1) wanafunzi kuandikishwa, kuwepo shuleni na viwango vya kuacha shule na kukatisha masomo, (2) kutafuta, kutambua, na kuhimiza watoto kwenda shule; (3) umaskini na kuhusishwa sifa za familia anakotoka mwanafunzi; (4) mitazamo yao wanafunzi wenye ulemavu; (5) mazingira ya ufundishaji na ujuzi wa walimu; (6) aina ya mtaala na kazi za kujifunza - ujuzi wa mitaala husika kwa maisha ya ujifunzaji wa wanafunzi. 8.4 Kwa upande wa mchakato, mazingira ya shule, ushirikiano, msaada, na huduma za pamoja / mafunzo ya walimu na utayari wa walimu kujituma na kuwasaidia wanafunzi wenye sifa tofauti vimekuwa changamoto kubwa. 8.5 Vikwazo vya kimitizamo na kimazingira katika elimu ambapo mazingira ya shule hayakujengwa kwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.

8.6 Walimu hawajaandaliwa kufundisha watoto wenye ulemavu, hivyo kazi ya kuwachanganya watoto wa kawaida na wale wenye mahitaji maalumu imeonekana kuwa nzito sana kwao.

8.7 Walimu wakuu walio wengi pamoja na walimu wa kawaida wana uelewa mdogo kuhusu masuala yanayohusu watu wenye ulemavu. Hali hii ni kikwazo kikubwa katika kuwatambua watoto wenye mahitaji maalumu na wale wenye ulemavu.

8.8 Wazazi wengi wenye watoto wenye ulemavu hawako tayari kuwapeleka watoto wao shuleni, wengi hawawajali kikamilifu. Matokeo yake watoto wengi wenye ulemavu wamekuwa wakibaki nyumbani pamoja na kwamba wamefikia umri wa kuanza shule.

9.0 Elimu Jumuishi Inawezekana Tanzania

Kujenga fikra zetu kiusahihi kuhusu elimu jumuishi, mitazamo chanya na maamuzi yetu ya leo yanaweza kufanikisha elimu jumuishi nchini kwetu licha ya changamoto nyingi zinazotukabili. Tukifanya haya tunaweza kutoa elimu jumuishi na kusonga mbele zaidi kielimu.

9.1 Kukuza uelewa wa pamoja kuhusu elimu jumuishi na manufaa yake kwa jamii nzima na kwa watu wenye ulemavu wenyewe. Uelewa huu utabadili mitazamo hasi na fikra za kibaguzi kwa wanajamii wengi, na hivyo kuwajumuisha watu wenye ulemavu kuanzia nyumbani, shuleni na hata kwenye taasisi mbalimbali na kazi mbalimbali. Bila kubadili mitazamo yetu hatuwezi kusonga mbele.

9.2 Kuna haja ya kuwa na mipango ya muda mrefu inayolenga kuwapatia walimu mafunzo kuhusu namna ya kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu pamoja na elimu jumuishi. Katika mpango wa muda mfupi, inafaa serikali pamoja na wadau

Page 10: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

9

wengine wa elimu kuanzisha mafunzo kwa njia ya semina na warsha katika wilaya na mikoa mbalimbali.

9.3 Kuna haja ya kuingiza katika mtaala wa elimu ya ualimu, mafunzo yanayohusu watoto wenye mahitaji maalumu pamoja na elimu jumuishi. Na kupeleka walimu wengi zaidi kwenye chuo cha elimu maalumu ili wapate mafunzo yatakayo wasaidia kufundisha kwa tija watoto wenye ulemavu pamoja na wale wenye mahitaji maalumu.

9.4 Majengo mengi hata yale yaliyojengwa kupitia MMEM hayakuzingatia mahitaji pamoja na hali za watoto wenye ulemavu. Kwa hiyo, kuna haja katika awamu ya pili ya MMEM kuyarekebisha majengo katika shule ili yafae vilevile kutumiwa na watoto wenye ulemavu. Pia ofisi mbalimbali na hata nyumba za watu binafsi ziwe rafiki kwa watu wenye ulemavu.

9.5 Na ni vyema kujenga utamaduni na utashi wa kimaamuzi kwa kuweka mikakati inayoshikika kama vile kujenga majengo muda wote yanayokidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu. Na pia kutenga pesa ya kutosha kwa ajili ya vifaa vya watu wenye ulemavu. Kuna haja ya kupitisha sheria itakayolazimisha ujenzi wa majengo kuzingatia pia mahitaji ya watoto wenye ulemavu.

9.6 Kuna haja ya kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuongeza uhamasishaji juu ya umuhimu na hatima ya kielimu kwa watoto wenye ulemavu nchi nzima. Uhamasishaji huu uendane na uboreshaji wa mahitaji ya kiuchumi kwa watoto wenye ulemavu pamoja na wale wenye mahitaji maalumu.

Ni muhimu ieleweke kuwa malengo ya MMEM ya kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa hayatafikiwa kama watoto wenye ulemavu hawatapewa fursa ya kupata elimu kama wale wasio na ulemavu. Ni utashi tu na uamuzi kivitendo watu wenye ulemavu watafurahia haki yao ya kupata elimu na kujumuishwa kwenye fursa zote za kijamii. Tuwajibike kwa pamoja!

==

Page 11: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

10

Marejeo

Beyers, C. & Hay, J. (2007). Can inclusive education in South (ern) Africa survive the HIV and AIDS pandemic? International Journal of Inclusive Education, 4, 387-399.

Bryman, A. (2006). Integrating quantitative and qualitative research: how is it done? Qualitative Research, 6, 97-113.

Crawford, C.B. (1994). Full inclusion: One reason for opposition. Retrieved on June 14, 2008 from http://my.execpc.com/~presswis/inclus.html.

Richardson, J.T.E.(Ed.) (2003). Handbook of Qualitative research methods for psychology and the social sciences. UK: BPS Blackwell.

Roach, V. (1995). Supporting inclusion: Beyond the rhetoric. Phi Delta Kappan, 77, 295- 2999.

Salend, S.J. (2001). Creating inclusive classrooms: Effective and reflective practices (4th ed.). Upper Saddle River, NJ: Merrill.

Thomas, R.M. (2005). Blending qualitative & quantitative research methods in theses and dissertations. Thousands Oaks, California: Corwin Press.

UNESCO (2000). Inclusion in Education. The participation of disabled learners. Paris, France

United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization (UNESCO) [1994]. The Salamanca Statement and Framework for Action on special needs education. Paris: UNESCO.

United Republic of Tanzania [URT) (2001a). The education and training development programme document. Final Report. Dar es Salaam: Ministry of Education and Culture.

URT (2001b). Education in a global era: Challenges to equity, opportunity for diversity. Dar es Salaam: Ministry of Education and Culture.

Zombwe G (2008) When Will Exclusion from Education End? Jamana printers, Dar es salaam

Page 12: working paper cover manufaa 4 (2) - HakiElimuhakielimu.org/files/publications/Elimu Jumuishi kwa... · 2014-05-04 · fursa ya elimu bila kujali tofauti baina ya watoto, malengo ya

HakiElimuS L P 79401 • Dar es Salaam • TanzaniaSimu (255 22) 2151852 / 3 • Faksi (255 22) 2152449 [email protected]

HakiElimu

HakiElimu inafanya kazi kuleta usawa, ubora, haki za binadamu na demokrasia katika Elimu,kwa kuziwezesha jamii kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa shule, kuwa na ushawishi katika

utayarishaji wa sera, kuhamasisha majadiliano ya kibunifu ya umma kwa lengo la kujiunga pamojakuleta mabadiliko, kuendesha tafiti zinazohoji na kuchambua mambo kwa kina, kuendesha

kampeni za utetezi na kushirikiana na wabia wengine ili kufikia malengo ya pamoja na kupigania haki ya jamii.

Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi

HakiElimu imeanzisha Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi (Working Paper Series) kwa lengo la kuchapisha upya makala mbalimbali za uchambuzi katika muundo ambao ni rahisi kuwafikia na kusomwa na watu wengi. Mlolongo wa nyaraka hizi unatarajiwa kuchangia katika kujenga ufahamu wa jamii na katika mdahalo kuhusu masuala ya elimu na demokrasia.

Mlolongo huu unajumuisha taarifa na makala mbalimbali zilizoandikwa na wafanyakazi na wanachama wa HakiElimu, mashirika na watu binafsi waliokuwa na ubia nasi. Baadhi ya nyaraka hizi zimeandikwa mahsusi kwa ajili ya mlolongo huu, wakati nyingine zinatokana na kazi zilizokwisha chapishwa hapo awali. Nyaraka nyingi zilizochapishwa katika mlolongo huu ni makala ambazo uandishi wake bado unaendelea, hivyo hazi-kukusudiwa kuwa ni nyaraka zilizokamilika kabisa.

Maoni yanayotolewa humu ni ya mwandishi (waandishi) mwenyewe na si lazima yawe yanawasilisha maoni ya HakiElimu au taasisi nyingine yoyote. Mawasiliano yote kuhusu makala mahsusi katika mlolongo huu yafanywe moja kwa moja kwa waandishi wake; kwa kadiri inavyowezekana, anuani zao zimeonyeshwa katika tanbihi/rejea chini ya ukurasa wa 1 wa makala husika.

Nyaraka hizi zinaweza pia kupatikana katika tovuti ya HakiElimu: www.hakielimu.org. Nyaraka zote zinaweza kuchapishwa kwa minajili isiyo ya kibiashara baada ya kupata idhini ya maandishi kutoka kwa Hak-iElimu na mwandishi husika. Lengo letu ni kuchapisha makala fupi zilizo wazi na bayana na tungependelea zaidi ziwe na urefu wa kati ya kurasa sita hadi kumi na mbili. Hata hivyo, makala zenye urefu wa hadi kurasa ishirini zinaweza kufikiriwa. Tunakaribisha sana makala zenu. Makala hizo ziwasilishwe kwetu zikiwa katika mfumo wa kielektroniki kwa kutumia anuani inayooneshwa hapo chini: