nairobi ni miguna · kuushinda ubinafsi kwa kwa bidii yetu. tunafaa kushinda siasa hasi za...

23
NAIROBI NI MIGUNA MIGUNA RUWAZA ya KUONA KAUNTI YA NAIROBI INABADILIKA MPANGO WA MIAKA MITANO KIMUHTASARI Manifesto kwa ajili ya Nairobi www.migunamiguna.com Haki zote zimehifadhiwa © Miguna Miguna 2016

Upload: others

Post on 02-Feb-2021

1 views

Category:

Documents


0 download

TRANSCRIPT

  • NAIROBI NIMIGUNAMIGUNA

    RUWAZA ya KUONA KAUNTI YA NAIROBI INABADILIKA

    MPANGO WA MIAKA MITANO KIMUHTASARIManifesto kwa ajili ya Nairobi

    www.migunamiguna.comHaki zote zimehifadhiwa © Miguna Miguna 2016

  • WAKATI NI SASACHAGUO BORA LIKO WAZI!WASHA TAA. CHAGUA MIGUNA!VIVA NAIROBI!VIVA!

  • Kujitolea kuleta maendeleo na kuboresha uchumi.

    Uongozi wenye ujasiri wakati wa utawala wa kidikteta wa chama kimoja. Mgombeaji wa wadhifa wa kisiasa akiwa katika chuo kikuu cha Nairobi, mwezi Novemba tarehe 13 mwaka wa 1987.

  • Yaliyomo

    Salamu i

    Utoaji wa huduma bora 1

    Kuzingatia Maadili Uongozini 1

    Udhamini wa Kimasomo kwa Watoto Werevu wa Familia Maskini 2

    Miundo-msingi ya Kisasa 3

    Mfumo wa Kisasa wa Kudhibiti Taka Taka 5

    Wachuuzi Wa Reja Reja na Biashara Ndogo Ndogo 5

    Mazingira Safi 6

    Maji safi ya mfereji 6

    Mfumo Bora wa Uchukuzi wa Umma 7

    Makazi bora kwa bei nafuu 7

    Maeneo ya burudani yenye kumfaa kila mtu 8

    Maeneo salama ya watu wanaotembea kwa miguu na baiskeli 8

    Jiji lenye usalama na maendelo 9

    Serikali isiyokuwa na ufisadi na inayowajibika 10

    Kujitolea kwangu kwa mwisho 13

  • i

    Salamu

    Wakazi Watukufu wa Nairobi

    Wakenya wenzangu,Mkakati wetu haufai tu kuvamia ufalme bali kuuteka. Kuunyima hewa. Kuuaibisha na kuubeza. Kwa kutumia sanaa yetu, muziki wetu, fasihi yetu, ukakakamavu wetu, utajiri wa kiakili, furaha yetu, kutokufa moyo-na uwezo wetu wa kueleza hadithi zetu wenyewe. Hadithi ambazo ni tofauti na zile tunazofumbwa nazo macho na kuziamini.

    Inawezekana kubadili hali hii. Na mabadiliko yako njiani (Imetafsiriwa) - Arundhati Roy, War Talk

    Amkeni, Nairobi! Amkeni!

    Wakazi wa Nairobi: Mnalipa kodi lakini hamupati huduma bora.

    Mnalipa kiwango cha juu cha kodi lakini hamuna usalama wa kutosha.

    Mamilioni kati yenu hamuna maji safi.

    Mamilioni kati yenu mnaishi kwenye nyumba ambazo ziko katika hali duni.

    Zaidi ya asilimia 90% ya wakazi wa Nairobi wenye bidii walioajiriwa na wale wasiokuwa na ajira wanaishi katika mitaa ya mabanda.

    Wengi wetu tunaishi katika maeneo yaliyozungukwa na uchafu.

    Nairobi haina mfumo bora wa kukusanya takataka.

    Barabara za Nairobi ni chache, nyembamba na zilizoharibika.

    Hizi ni huduma ambazo mnazilipia na ambazo ugatuzi ulifaa kutoa.

    Nitaleta huduma hizi kwa wakazi wote wa Nairobi; sio tu kwa wakenya wa-naojiweza kifedha wanaoishi katika mitaa ya Muthaiga, Karen, Lavington, Runda, Kiuna, Ridgeways, Roselyn, Kitisuru na Lower Kabete.

  • ii

    DAI heshima, ajira ya maana, na mazingira mazuri ya kuishi.

    Kama hayati Ndugu Samora Machel (Mungu aipe kudura roho yake milele) alingeuliza, “Mapambano yanaendelea dhidi ya nini?”.

    Mapambano yanafaa kuendelea dhidi ya nini?

    Samora Machel aliwakumbusha raia wa Msumbiji mara kwa mara kwam-ba mapambano dhidi ya umasikini, ujinga, ukosefu wa makao, ukosefu wa ajira, unyanyasaji na dhuluma yanafaa kuendelea.

    ‘Haya ndiyo mambo MUHIMU!”, angenguruma.

    Nakubaliana naye.

    Mapambano yetu ya kuikomboa Kaunti ya Nairobi ni kwa ajili ya mambo yanayowekezana na si ndoto tu.

    Wakazi Wenzangu Watukufu wa Nairobi!

    Kundi maalum litaleta mabadiliko yenye manufaa Nairobi.

    Ninaongoza Vuguvugu la Ukombozi wa Nairobi, vuguvugu linalowajumui-sha watu wote: vijana na wanawake na wanaume wachapa kazi.

    Watu wa kiwango cha maisha ya wastani, sawa na wale wasiokuwa na makazi, wasiokuwa na ajira, wanafunzi, wachuuzi wa rejareja na hata mama mboga wana jukumu muhimu. Ingawa wamenyanyaswa kiuchumi; wao si wajinga.

    Wakenya wajasiri na wazalendo wa Nairobi wanatoka katika maeneo mba-li mbali nchini, makabila tofauti na dini mbali mbali. Wameunganishwa pamoja kwenye dhiki na unyanyasaji wao. Wakazi watukufu wa Nairobi! Mmeungana pia katika kukerwa na wizi wa rasilimali – ardhi ya umma na kodi – na “viongozi” walafi,

  • iii

    wadanganyifu na wanafiki.

    Kaunti ya Jiji la Nairobi inastahili gavana mwenye maono ya mbele na ajen-da murua kwa wakazi wote watokao kwenye matabaka, utamaduni, dini, uwezo na miamko mbalimbali. Nairobi inahitaji gavana ambaye anaelewa kwamba uongozi unafaa kuwa wa uwazi.

    Nairobi inastahili gavana ambaye ana bidii kama watu wa Nairobi; mtu am-baye amejitolea kila dakika ya kila siku kukuza uchumi, kuleta kazi, kujenga miondo-msingi ya hali ya juu kama vile nyumba, barabara, taa, barabara za baiskeli, barabara za kutembelea na kuimarisha uchumi wa wastani.

    Haya na MAMBO YANAYOWEZEKANA! Si ndoto tu.

    Kinyume na wapinzani wetu wasiokuwa na maono na ambao wananawiri katika unafiki wa kutoa hongo eti huo ni huruma; Mimi ni mkweli, na mtu wa vitendo atakayeleta mabadiliko.

    Nafahamu kwamba madiliko ya kikweli yatakumbwa na upinzani kutoka kwa wale wanaopenda fujo, upuuzi na mafisadi ambao wameteka nyara uongozi ndani ya City Hall.

    Lakini Watu Watukufu wa Nairobi wanafahamu kwamba ili jiji liendelee, lazima tuyaondoe magenge yote pamoja na vikembe vyao, wajumbe wao na wamali wao.

    Ninajitolea kutekeleza yale ambayo ninajua kwamba nitayafanya.

    Kinyume na wapinzani wetu wenye historia duni na rekodi ya utepetevu, uporaji, wizi, usimamizi ovyo wa raslimali za umma – rekodi yangu na histo-ria yangu haina doa.

    Mimi ndiye mgombe wa pekee wa Ugavana wa Nairobi ambaye si mfisadi.

    Ndio, Nairobi inastahili gavana ambaye amejitolea kikamilifu kusaidia

  • iv

    wakazi wasiojiweza kujiinua na kuingia katika kiwango wa uchumi wa wastani ili wawejimudu na kupata maendeleo.

    Yaani, Nairobi inastahili gavana ambaye atafanya maamuzi bora, ya busara, murua, wazi na mema kuliko yalivyowahi kufanywa siku za nyuma.

    Najitolea kuongoza na kusimamia serikali kwa njia bora na ya maadili.

    Kuanzia siku ya kuapishwa kwangu, kutakuwa na sera rasmi wa serikali kutoka ngazi ya juu isiyotoa nafasi yoyote kwa ufisadi, utepetevu, ufujaji, na utendakazi duni.

    Ili kuafikia lengo hili, tunafaa kuushinda uoga kwa matumani. Tunafaa kuushinda ubinafsi kwa kwa bidii yetu. Tunafaa kushinda siasa hasi za mga-wanyiko, za kichama na za ukabila kwa kuunga mkono maono ya kuwaleta wakazi wa Nairobi pamoja.

    Huu ni uchaguzi muhimu. Ni kati ya watu wasiojali sheria – wezi, majamba-zi, na wauzaji mihadarati – dhidi ya mtu mwadilifu.

    Nitatimiza NDOTO hii.

    Miguna MigunaMgombeaji wa kujitegeaWa Ugavana wa Kaunti ya Nairobi.

  • 1

    MIMI, MIGUNA MIGUNA, NIMEJITOLEA

    1. KUWAHUDUMIA wakazi wa Nairobi KWA MOYO MMOJA bila kujali kabila wala kiwango cha maisha na kuwapa huduma za kiwango cha juu wanazohitaji.

    Kuanzia katika ofisi ya gavana kwenda chini, tumejitolea kutoa huduma za ubora wa juu masaa 24 kila siku.

    Ajira na kupandishwa cheo kwa wafanyakazi wa kaunti kutazingatia tajiriba, uwezo wa kufanya kazi na maadili.

    Kuzingatia Maadili Uongozini

    2. KUHAKIKISHA kwamba idara zote zinazingatia maadili bila ukabila, uongozi wa kutegemewa na heshima katika utoaji huduma na kuhifadhi rasilmali.

    Ofisi zote za kaunti zitakuwa zinafunguliwa kuanzia saa mbili unusu asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni kuanzia siku ya Jumatatu hadi Ijumaa.

    Huduma muhimu na za dharura kama vile ambulensi na magari ya zima moto zitakuwa zinatolewa saa 24 kila siku.

    Maafisa wa usalama wa jiji (askari) watachujwa na kupewa mafunzo ya hali ya juu. Wanaoendelea kuhudumu kwa sasa watapewa mafunzo upya. Watakaoshindwa kubadilika watafutwa kazi na kutafutiwa njia mbadala ya kujipatia riziki.

    Hakuna mtu mwenye rekodi ya uhalifu, mwenye (ma)kesi ya uhalifu iliyokwama na/au inayoendelea au ambaye maadili yake yametiwa doa na Kamati za Umma (za Bunge au za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) ataruhusiwa kutumika au kuajiriwa na Serikali ya Kaunti.

    Utoaji wa huduma bora

  • 2

    Gavana, Naibu wa Gavana, Maafisa wa Baraza Kuu la Kaunti na maafisa wengina watakuwa wanafanyiwa tathmini kila mwaka na kama mmoja wao atapatikana na hatia ya kufuja mali ya umma atafutwa kazi na kuchukuliwa hatua kulingana na sheria. Serikali yangu itashirikiana kikamilifu na maafisa wanaofanyia uchunguzi kesi za ufisadi.

    Kutakuwa na nambari za simu za dharura zitakazo kuwa wazi saa 24 za kupiga ripoti kuhusu uhalifu, ukosefu wa usalama, dharura za afya, ufisadi na uhalifu wa kiuchumi.

    Udhamini wa Kimasomo kwa Watoto Werevu wa Familia Maskini3. NITATAFUTA, NIPATE na NIWAPE udhamini wa masomo ya Vyuo

    Vikuu kwa takriban wanafunzi 20,000 wanaotoka katika familia maskini katika wadi zote kwenye taaluma za biashara, teknolojia, sayansi, ufanyi biashara, sanaa na masomo ya kijamii kila mwaka.

    Tunatilia mkazo kujenga uchumi uliojikita kwenye ujuzi.

    Tunahimizi ubunifu, uhalisia na bidii.

    Tutawapa vijana uwezo kupitia elimu, mafunzo na ajira za maana.

    Mbali na mipango yetu iliyomo kwenye Manifesto hii, tutashirikiana na sekta ya kibinafsi kuwapa vijana nafasi zaidi za kujiendeleza kimaisha wengi wao wakiwa wale waliofaidika na msaada wa masomo.

    Tutakuwa makini katika kuboresha uchumi na utangamano miongoni mwa jamii.

  • 3

    Tutatumia elimu, viwanda na ufanyi biashara kama mbinu ya kumaliza umasikini na uzoefu wa kutegemea misaada ambao unashusha hadhi yetu.

    Miundo-msingi ya Kisasa 4. TUTAJENGA barabara bora katika kaunti ya Nairobi.

    TUTASULUHISHA tatizo la misongamano ya magari Nairobi kupitia kwa ujenzi wa barabara pana na kutoa barabara zote za mzunguko na kuweka taa za barabarani zitakazokuwa zinatumika.

    Barabara zote za humu nchini zikiwemo za jiji la Nairobi ni nyembamba, chache, zilizojengwa vibaya na ambazo hazifanyiwi ukarabati.

    Barabara zote za humu nchini hazina mabomba ya kupitishia maji hasa maji chafu na ya mvua.

    Tutajenga barabara za mkato katika barabara kuu ili kupunguza misongamano ya magari na kuhakikisha kwamba wanaotembea kwa miguu wanakuwa salama.

    Tutatumia mbinu za kimataifa katika ujenzi wa barabara. Chini ya kila barabara kunafaa kuwa na bomba la kupitishia maji taka na ya mvua.

    Nguvu za umeme, mtandao na maji safi yanafaa kuwa chini ya barabara.

    Kwa sasa barabara za Nairobi zinajengwa bila miundo msingi inayohitajika ndiposa barabara hizo hazidumu.

    Waendeshaji magari wasiozingatia taa za barabarani watatozwa faini.

  • 4

    Tutapanua barabara zote ili kuzuia ajali za barabarani, kuwapa nafasi wanaotembea barabarani na waendeshaji baiskeli.

    Tutajenga barabara za akiba kwa magari ya dharura kama vile polisi, ambulensi na magari ya zima moto.

    5. TUTAKARABATI miundo-msingi katika kaunti ya Nairobi.

    Tutaiangalia upya idara ya mipango ya kaunti na kuajiri watu wenye tajiriba ya juu.

    Tutawapa mafunzo upya wafanyakazi wa sasa pamoja na kuwafuta kazi wale wasiofaa.

    Tutakagua miundo msingi yote ya kaunti ili kutambua pale panapo hitaji kufanyiwa ukarabati.

    Tutayafanyia tathmini majengo kabla na baada ya kujengwa Nairobi.

    Tutabuni sera za jinsi ya kutoa vibali vya ujenzi katika kaunti ya Nairobi.

    Tutabuni Idara ya Ukarabati ambayo ini bora na inafoyofanya kazi ili:

    i. Kujenga na kukarabati mabomba ya kisasa ya kupitishia maji taka.

    ii. Kujenga na kukarabati mabomba ya kisasa ya kupitishia maji ya mvua.

    iii. Kujenga na kukarabati mapipa ya kuhifadhia maji na kuyasafisha.iv. Kukarabati barabara kuu za kaunti.v. Kujenga vituo vya wazima moto vyenye vifaa vya kutosha kwenye

    mahali pote pa makazi.

  • 5

    vi. Kukarabati majengo yote yanayomilikiwa na kaunti.vii. Kupaka rangi mali yote yanayomilikiwa na kaunti.

    Mfumo wa Kisasa wa Kudhibiti Taka Taka 6. TUTAZINDUA mfumo wa kudhibiti taka na kusuluhisha tatizo la

    mirundiko ya uchafu Nairobi.

    Kaunti ya Nairobi inaendelea kunuka uchafu.

    Uchafu umetapakaa kila mahali hivyo basi kuhatarisha maisha ya wakenya.

    Uchafu utakuwa unakusanywa kila baada ya wiki mbili ili ukarabatiwe na kutumiwa tena katika mitaa yote.

    Hatua hii itawezesha takriban watu 100,000 wapewemafunzo wakiwemo vijana na wahandisi na kubuni nafasi za ajira kufikia mwaka wa 2018.

    Wachuuzi Wa Reja Reja na Biashara Ndogo Ndogo 7. UJENZI wa masoko ya kisasa yatakayotumika na wachuuzi wa reja

    reja na wafanyabiashara wengine ili waweze kuuza bidhaa zao katika mazingira safi bila kuhangaishwa.

    Wachuuzi wa reja reja ni wafanyabiashara wenye bidii hivyo basi wanahitaji mazingira bora ya kufanyia biashara ili waweze kufanikiwa maishani. Serikali yangu imejitolea kuwahudumia wachuuzi hao ifaavyo.

  • 6

    8. KUBORESHA matumizi ya mazingira

    Tutapiga marufuku matumizi ya plastiki jijini kama ilivyo jijini Kigali, Rwanda.

    Mto Nairobi pamoja na mito kama vile mto Ruaka utasafishwa na kulindwa.

    Upandaji miti utakuwa jambo la kawaida kwa wakazi wa Nairobi. Tutahakikisha miti milioni moja imepandwa kila mwaka. Wale watakao kata miti watachukuliwa hatua kulingana na sheria.

    Katika muda wa miezi miwili nitakapo ingia mamlakani, nitabuni sheria ya kupiga marufuku ukataji wa miti kiholela, utumizi wa plastiki na kukata miti bila kujali uovu huo umetekelezwa katika ardhi ya kibinafsi ama ya umma.

    Tutajenga kituo cha kuziweka tena katika matumizi bidhaa zilizotumika katika mitaa yote.

    Kama mfumo wa kukusanya na kudhibiti uchafu unavyofaa kuwa, hatuta bagua jinsi uchafu unavyo kusanywa, kushughulikiwa na kutumika tena.

    Vyoo vya umma vitajengwa katika maeneo yote jijini Nairobi.

    Maji safi ya mfereji 9. TUTATOA maji safi kwa wakazi wote wa Nairobi.

    Maji ya mfereji ni hitaji muhimu na haki ya kila mtu. Kila mtu atapata maji safi katika mitaa yote.

    Hakutakuwa na ubaguzi katika usambazaji wa maji safi.

    Mazingira Safi

  • 7

    10. TUTATOA huduma bora ya uchukuzi wa umma kwa bei nafuu.

    Tutaanzisha mfumo bora wa uchukuzi kwa bei nafuu unaojumuisha mabasi na magari ya moshi.

    Tunalenga kutoa huduma ya uchukuzi kwa wakenya kutoka eneo la kati kati mwa jiji hadi mtaani Eastlands.

    Miradi hii yote itasimamiwa na fedha za kodi za biashara, mali, maeneo ya kuegesha magari, kutoa upya leseni na malipo mbali mbali kutoka kwa wizara ya fedha.

    Tutahakikisha kwamba kaunti ya Nairobi inapokea fedha kulingana na katiba.

    Makazi bora kwa bei nafuu

    11. KUINUA na kujenga nyumba kwa bei nafuu zenye maji safi kwa wakenya wasiojiweza kifedha.

    Tutazindua mpango wa kuwapa makazi mbadala watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda. Lengo ni kuhakikisha kwamba hakuna mitaa ya mabanda Nairobi.

    Fedha za kufanikisha malengo haya zitatoka kwa wafadhili na wasamaria wema kutoka humu nchini na katika mataifa ya kigeni.

    Tunakisia kwamba miradi ya ujenzi itabuni zaidi ya nafasi 500,000 za ajira kwa wakazi kila mwaka. Hii itatoa mafunzo, ajira na kusababisha ukuaji wa uchumi.

    Mitaa itakayo jengwa na kukarabatiwa ni Kibera/Kibra, Mathare, Kawangware, Huruma, Kangemi, Korogocho, Majengo, Mukuru kwa Njenga, Baba Ndogo, Kayole, Githogoro, Fuata Nyayo, Eastleigh, Kariobangi, Nyalenda na Ziwa la Ng’ombe.

    Mfumo Bora wa Uchukuzi wa Umma

  • 8

    Kariobangi, Nyalenda na Ziwa la Ng’ombe.

    Maeneo ya burudani yenye kumfaa kila mtu

    12. TUTAYAPATA, tujenge na kusimamia maeneo ya burudani ya umma katika maeneo yote ya kaunti ya Nairobi hasa katika mitaa ya Kibera, Mathare, Lang’ata, Dangoreti, Dandora, Umoja, Kwangware, Huruma, Kangemi, Korogocho, Majengo, Mukuru kwa Njenga, Baba Ndogo, Kayole, Roysambu, Fuata Nyayo, Eastleigh, Kariobangi, Buru Buru, Embakasi, Nyalenda, Ziwa la Ng’ombe, Greenfields, Donholm, Kasarani na Kahawa ambayo yamenyakuliwa kinyume cha sheria.

    Maeneo salama ya watu wanaotembea kwa miguu na baiskeli

    13. KUJENGA na kusimamia maeneo ya watu wanaotembea kwa miguu na yale ya watu wanaoendesha baiskeli.

    Cha kuhuzunisha ni kwamba maeneo mengi ya makazi ya watu hayana barabara za watu wanaotembea kwa miguu. Hali hii inahatarisha maisha ya watu hao, wale wanaoendesha baiskeli na wanao fanya mazoezi ya kukimbia barabarani.

    Kwa sasa hakuna barabara za watu wanaotembea kwa miguu mtaani Eastleigh pamoja na mitaa mbali mbali ya mabanda. Maeneo ambayo ni nyumbani kwa robo tatu ya wakazi wa Nairobi.

    Hakuna barabara za kuendeshea baiskeli humu nchini. Ujenzi na usimamizi wa barabara hizo utabuni nafasi za ajira kwa wakenya wengi.

  • 9

    Pamoja na barabara za kuendeshea baiskeli, tutajenga maeneo salama ya kuegesha baiskeli kwa bei nafuu Nairobi.

    Jiji lenye usalama na maendelo

    14. TUTASAIDIA uwekezaji katika sekta ya kibinafsi ili kuwavutia wawekezaji wa humu nchini na wale wa kimataifa.

    15. TUTAANZISHA sera ya kuwa na kiwango cha chini kinachokubalika cha mishahara kwa wakazi wa Nairobi na kuweka mfumo utaoongozwa na serikali ya Kaunti ikishirikiana na Serikali Kuu na Vyama vya Wafanyikazi na Sekta ya Kibinafsi.

    Serikali yangu itayapa kipaumbele maisha bora ya wakazi wote wa Nairobi.

    16. UUNGANISHA mifumo ya HABARI na MAWASILIANO kwa seikali na michakato ya kibiashara ya sekta ya kibinafsi.

    Tutahakikisha kwamba kutakuwa na mfumo wazi wa malipo kwa kutumia mtandao utakao tumika kulipa kodi, leseni za vileo, ardhi, kulipia vibanda sokoni, biashara na ada ya kuegesha magari.

    Mfumo huo wa malipo utakuwa wa hali ya juu utakao boresha utoaji huduma.

    17. TUTADUMISHA mifumo bora ya usalama ili kuhakikisha kwamba mali zinalindwa ifaavyo pamoja na wakenya.

    18. TUTABORESHA miundo msingi ili kuhakikisha kwamba kaunti nzima inashuhudia maendeleo.

    19. TUTATIA NGUVU elimu bora kwa wote na huduma bora za afya kupitia kwa kuhakikisha kwamba vituo vya elimu na

  • 10

    afya vinakarabatiwa na kujengwa upya.

    20. TUTATATUA tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kwa kuhakikisha kwamba nafasi za ajira zinaongezeka. Tumejitolea kuanzisha mpango utakao buni takriban nafasi milioni moja za ajira kwa wakazi wa Nairobi katika muda wa miaka miwili.

    Watu wasiojiweza kifedha na ambao hawaja ajiriwa watakuwa wanapata msaada kutoka kwa serikali kwa ushirikiano na sekta ya kibinafsi. Hawa ni wakenya wenye bidii. Watu hawa wanastahili kuheshimiwa na kusaidiwa. Nchini Namibia kwa mfano, ni taifa lililo jangwani na limejinyakulia uhuru mnamo tarehe 21 mwezi Machi mwaka wa 1990 lakini lina mpango wa malipo ya uzeeni ulio shamiri kwa raia wake.

    Ujenzi wa kituo cha kisasa cha kusimamia taka pekee utabuni nafasi za ajira 200,000.

    Zaidi ya nafasi za ajira 500,000 zitabuniwa wakati wa mradi wa kuboresha mitaa ya mabanda. Mitaa yote ya mabanda Nairobi itaboreshwa. Makazi safi na ya bei nafuu yenye maji safi yatajengwa ili wakenya wasiojiweza kifedha waweze kufaidika. Serikali yangu itashirikiana na mashirika ya kutoa misaada ya humu nchini na yale ya kimataifa ili kutimiza ndoto hii.

    Ujenzi na usimamizi wa barabara utapewa kipaumbele. Hii itabuni nafasi za ajira kwa maelfu ya wakenya katika sekta mbali mbali.

    Serikali isiyokuwa na ufisadi na inayowajibika

    21. TUTAONDOA wafanyikazi wasiojiweza, ufisadi wa aina zote na ubadhirifu wa mali ya umma na kuhakikisha kwamba wakazi wa Nairobi wanafaidika na huduma bora.

  • 11

    Tutafanya kazi na ofisi ya mhasibu mkuu wa serikali na idara ya upelelezi ili kufanya tathmini ya mali za umma kila mwezi katika idara zote za serikali.

    Tutabuni mfumo wa kuwazawaidia wafanyakazi wa kaunti wenye bidii kazini.

    22. TUTAHAKIKISHA rasili mali za kaunti zinatumika vyema ili ukuaji wa uchumi uweze kushuhudiwa.

    Kila fedha zinazotengewa kuwahudumia wakenya zitatumiwa kama inavyo hitajika.

    Mhasibu mkuu, ofisi ya idara ya upelelezo pamoja na vitengo vyengine vya kisheria vitapata ushirikiano mwema kutoka kwa serikali yangu ili fedha za umma zisifujwe.

    Mfumo wa ununuzi wa bidhaa za serikali utakuwa wenye uwazi. Hakuna atakaye hudumu katika idara ya ununuzi wa bidhaa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

    Tutahakikisha hakuna uhusiano wowote kati ya maafisa wa serikali ya kaunti na wasambazaji wa bidhaa pamoja na wanakandarasi.

    Tutavunjavunja magenge yote na kuharibu mitandao yao kupitia uchunguzi wa kina, kuwashtaki, kutwaa mali na kuwapa adhabu kali.

    23. TUTAWATAMBUA, kuwaweka hadharani na kuwachukulia hatua watakao fuja mali ya umma.

    Wataalamu huru watahusishwa ili kuziba nafasi zote za wizi wa mali ya umma.

    Tutashirikiana na vitengo vya sheria na taasisi mbali mbali ili yeyote atakaye shukiwa kuiba mali ya umma anachukuliwa hatua kulingana na sheria.

  • 12

    Tutabuni mifumo ya kisasa kutambua uharibifu wa mali ya umma.

    Hakuna afisa yeyote wa serikali atakaye pendelewa katika serikali yangu.

    24. TUTATAFUTA, tupate na kutwaa mali yote ya umma yaliyoibwa pamoja na kutwaa tena Makazi Rasmi ya Meya wa Zamani wa Jiji la Nairobi.

    Tutashirikiana na idara ya upelelezi kubuni mbinu za kuzuia wizi wa mali ya umma.

    Tutahakikisha mali za kaunti ya Nairobi zilizoibwa kama vile mkufu wa dhahabu wa meya, makazi rasmi ya meya, makazi ya jaji mkuu pamoja na ardhi zinapewa wamiliki wake halisi. Wakazi watukufu wa Nairobi.

    25. TUTAFANYIA tathmini rasilimali zote za Nairobi ikiwemo mali za wafanyakazi wa sasa na wa zamani wa serikali.

    Lengo hili litaafikiwa kupitia kwa kuajiriwa kwa wapelelezi huru.

    26. TUTALINDA sera za kidemokrasia, katiba na kutii sheria vitakuwa kwa manufaa ya wote.

    Kila mwezi nitakuwa na mkutano utakao peperushwa moja kwa moja kwenye runinga na wakazi katika mitaa mbali mbali ili serikali yangu ikaweze kukusanya maoni kutoka kwa wakazi wote wa Nairobi.

    Uongozi huru na uwajibikaji ni mambo yenye umuhimu mkubwa kwangu na nitahakikisha serikali yangu itakuwa ya watu wote.

    Nitakuwa kiongozi mwenye manufaa kwa wakazi wote wa Nairobi.

    Nitahakikisha huduma zote zinalingana na katiba ya Kenya iliyozinduliwa mwaka wa 2010.

  • 13

    Nitatekeleza katiba ili kila mtu afaidike na ugatuzi.

    Hakutakuwa na ahadi za uongo.

    Kujitolea kwangu kwa mwisho

    SIKILIZA WAKAZI WA NAIROBI: Mnalipa kodi za kiwango cha juu kila mwaka lakini viongozi wenu wafisadi wanaziiba fedha hizo. Nitahakikisha kodi mnayolipa kila mwaka inatumika vyema kwa kutoa huduma za msingi kwa wakazi. Kaunti ya Nairobi itakuwa yenye manufaa kwa wakazi, wafanya biashara na wawekezaji.

    27. Nitaifanya Nairobi kuwa eneo salama tena: Watoto wetu watacheza, kusoma na kushamiri katika mazingira safi yasiyokuwa na dawa za kulevya, majambazi wala uchafu.

    28. Nitaifanya Nairobi kuwa bora tena: Watoto wetu watakumbatia tamaduni na mafanikio kupitia kwa kusoma na bidii.

    29. Nitaitajirisha tena Nairobi: Ambapo vijana, wanawake na wanaume watafanya kazi kwa umoja na uzalendo; haitakuwa tena maisha ya kuvumilia.

    30. Nairobi itakuwa yenye kujitegemea tena: Ambapo wakazi hawataomba msaada kutoka kwa wale wanao wanyanyasa.

    31. Nitaifanya Nairobi kuwa yenye kujivunia tena: Ambapo wakazi, wageni na wafanyabiashara watashamiri katika tamaduni ya ubunifu.

    32. Nitaifanya Nairobi kuwa ya burudani tena: Ambapo wakazi watakuwa huru, salama, wenye kujiamini, wenye kujiweza kifedha na wenye furaha.

    33. Nitaiongoza Nairobi kidemokrasia: Uwazi na maadili

  • 14

    vitakuwa ada ya serikali yangu.

    34. Nitaibadilisha Nairobi kutoka eneo lenye uchafu, lenye msongamano wa watu hadi kuwa eneo safi na la ubora wa kimataifa.

  • 15

    MAPAMBANO YANAENDELEA (ALUTA CONTINUA!)

    Babatunde Fashola (2007-2015) aliitendea Lagos.

    Nina lengo pia la kuitendea mema Nairobi – kupitia kwa ushirikiano wenu.

    Jiungeni nami katika kutoa wito wangu:

    KURA YANGU, NGUVU YANGU! KURA YAKO, NGUVU YAKO!

    KURA YETU, NGUVU YETU!

    WAKATI NI SASA, WA KUMALIZA UFISADI!

    WAKATI NI SASA, KUWEKA WEZI WA MALI YA UMMA KOROKORONI!

    WAKATI NI SASA!WAKATI NI SASA!

    WAKATI NI SASA. TIK TOK, TIK TOK.

    MPIGIE kura MIGUNA MIGUNA kama GAVANA wa NAIROBI 2007!Twitter: @MigunaMiguna

    FaceBook: Governor Miguna MigunaMigunaBarua pepe: [email protected]

    [email protected]@gmail.com

    KUMBUKA: Mgombeaji mwenza atafahamika katika wakati ufaao. Mimi ndimi mgombeaji pekee wa ugavana ambaye amechapisha malengo yake kufikia sasa. Gavana wa sasa wa Nairobi hajachapisha malengo yake zaidi ya miaka minne tangu kuchaguliwa kwake mwaka wa 2013. Hivyo basi, kundi la maendeleo liko mbele huku wengine wakisalia nyuma wakiiba mali ya umma.