somabiblia | mafundisho ya biblia · web viewukitoa kwa sababu unamwogopa au unamwonea aibu...

47
MAMBO YA ZAKA, UTOAJI, SADAKA, FUGU LA KUMI NA PESA Lengo la makala hii siyo kuweka sheria yo yote! Lengo langu siyo kukuambia wala kukuagiza utoe kiasi hiki au kiasi kile katika utoaji wako! Kama umeokoka itakuwa tabia yako kutoa, na baada ya kusoma makala hiyo, ni matumaini yangu kuwa utoaji wako utaongezeka tu na utatoa kwa furaha ya moyo. Najua wapo wengi wanaifuata desturi ya kutoa fungu la kumi pasipo nia mbaya, ndio maana sehemu kadhaa za makala hiyo hayawahusu watu kama hao moja kwa moja (hasa sehemu za mwisho). Kama unaifuata desturi ya kutoa fungu la kumi kwa moyo safi mbele ya Mungu kwa sababu umefundishwa na wengine ufanye hivyo, ni tuamaini langu utapata uelewa zaidi na bora kwa kusoma makala hii. Pia inawezekana kabisa, wapo wachungaji wanaofuata mambo hayo kutokana na mafundisho na mfumo wa madhehebu yao bila nia mbaya, hapo pia ni tuamaini langu watapata kitu kwa kusoma makala hii. Naomba utambue muktadha wa kila sehemu ya makala hiyo bila kufikiri kwamba lazima kila sehemu inahusu wewe! Sitaki kuwakosea watu ovyo ovyo! Mzigo na lengo la makala hii ni lifuatalo: kuondoa kila nafasi, kila hoja na kila hila ambazo viongozi mbalmabli wanazozitumia ili kukulazimisha - kwa kukutisha na kwa kupotosha neno la Mungu – kutoa pesa kanisani kadiri ya maagizo yao. Lengo la makala ni kuwa tunalotoa, tutalitoa kwa moyo mnyofu sawasawa na neno la Mungu. Naomba ukumbuke hayo unaposoma makala hiyo. Upo mchanganyiko mwingi, na mafundisho ya uwongo kuhusu somo hili la utoaji ni mengi. Tatizo hapa si kwamba maandiko ya Biblia hayapo wazi, la hapana; tatizo kubwa ni pale watu huifundisha mistari ya neno la Mungu nje ya kile Biblia yenyewe inenavyo na inavurugwa ili kuwashinikiza na kuwatisha waumini ili watoe. Msukumo wa yote hayo mara zote ni uchoyo uliopo kwa upande wa wachungaji na viongozi wa madhehebu. Matokeo ya kufanya hivyo ni kwamba waumini wananyonywa na kutumiwa vibaya na hao ambao walipaswa kuwatumikia vizuri na kuwaongoza watu katika maarifa ya Kristo na wokovu wake. Sasa nataka wote tutazame juu ya kile kilichofundishwa na kutendwa na KANISA LA AGANO JIPYA. Tunapoendelea kufanya hivyo, tafadhali tukumbuke kuwa mitume walioliandikia kanisa katika Agano Jipya walijua wazi na kwa uhakika kabisa kile kilichokuwa kinasemwa na sheria ya Musa (juu ya fungu la kumi) , na kwa kweli wao wenyewe mitume wamelelewa na kukuzwa na sheria hizo. Kwa hiyo katika kuwaandikia hao waumini juu ya mambo ya utoaji kwa Mungu, wangeweza kabisa kupata fursa ya kufanya mrejesho na nukuu wa sheria ya Musa - au hata kutoka katika sehemu yoyote ya nyaraka za Agano la Kale - iwapo sehemu yoyote ya Agano lile ingewahusisha waumini wa kikristo.

Upload: others

Post on 27-Jan-2021

5 views

Category:

Documents


1 download

TRANSCRIPT

MAMBO YA ZAKA, UTOAJI, SADAKA, FUGU LA KUMI NA PESA

Lengo la makala hii siyo kuweka sheria yo yote! Lengo langu siyo kukuambia wala kukuagiza utoe kiasi hiki au kiasi kile katika utoaji wako! Kama umeokoka itakuwa tabia yako kutoa, na baada ya kusoma makala hiyo, ni matumaini yangu kuwa utoaji wako utaongezeka tu na utatoa kwa furaha ya moyo. Najua wapo wengi wanaifuata desturi ya kutoa fungu la kumi pasipo nia mbaya, ndio maana sehemu kadhaa za makala hiyo hayawahusu watu kama hao moja kwa moja (hasa sehemu za mwisho). Kama unaifuata desturi ya kutoa fungu la kumi kwa moyo safi mbele ya Mungu kwa sababu umefundishwa na wengine ufanye hivyo, ni tuamaini langu utapata uelewa zaidi na bora kwa kusoma makala hii. Pia inawezekana kabisa, wapo wachungaji wanaofuata mambo hayo kutokana na mafundisho na mfumo wa madhehebu yao bila nia mbaya, hapo pia ni tuamaini langu watapata kitu kwa kusoma makala hii. Naomba utambue muktadha wa kila sehemu ya makala hiyo bila kufikiri kwamba lazima kila sehemu inahusu wewe! Sitaki kuwakosea watu ovyo ovyo!

Mzigo na lengo la makala hii ni lifuatalo: kuondoa kila nafasi, kila hoja na kila hila ambazo viongozi mbalmabli wanazozitumia ili kukulazimisha - kwa kukutisha na kwa kupotosha neno la Mungu – kutoa pesa kanisani kadiri ya maagizo yao. Lengo la makala ni kuwa tunalotoa, tutalitoa kwa moyo mnyofu sawasawa na neno la Mungu. Naomba ukumbuke hayo unaposoma makala hiyo.

Upo mchanganyiko mwingi, na mafundisho ya uwongo kuhusu somo hili la utoaji ni mengi.

Tatizo hapa si kwamba maandiko ya Biblia hayapo wazi, la hapana; tatizo kubwa ni pale watu huifundisha mistari ya neno la Mungu nje ya kile Biblia yenyewe inenavyo na inavurugwa ili kuwashinikiza na kuwatisha waumini ili watoe. Msukumo wa yote hayo mara zote ni uchoyo uliopo kwa upande wa wachungaji na viongozi wa madhehebu. Matokeo ya kufanya hivyo ni kwamba waumini wananyonywa na kutumiwa vibaya na hao ambao walipaswa kuwatumikia vizuri na kuwaongoza watu katika maarifa ya Kristo na wokovu wake.

Sasa nataka wote tutazame juu ya kile kilichofundishwa na kutendwa na KANISA LA AGANO JIPYA. Tunapoendelea kufanya hivyo, tafadhali tukumbuke kuwa mitume walioliandikia kanisa katika Agano Jipya walijua wazi na kwa uhakika kabisa kile kilichokuwa kinasemwa na sheria ya Musa (juu ya fungu la kumi), na kwa kweli wao wenyewe mitume wamelelewa na kukuzwa na sheria hizo. Kwa hiyo katika kuwaandikia hao waumini juu ya mambo ya utoaji kwa Mungu, wangeweza kabisa kupata fursa ya kufanya mrejesho na nukuu wa sheria ya Musa - au hata kutoka katika sehemu yoyote ya nyaraka za Agano la Kale - iwapo sehemu yoyote ya Agano lile ingewahusisha waumini wa kikristo.

Kile ninachokiandika hapa kisimwongoze yeyote yule kutoa kwa uhafifu au kidogo kuliko kile wanachokitoa sasa, lakini pengine hii isaidie kukuchochea wewe uweze kumtolea Mungu zaidi na kumtolea kwa moyo wa furaha.

UTOAJI KATIKA MAKANISA YA AGANO JIPYA.

Neno la Mungu liko wazi! Tusome tu! Kila mtu anaweza kuelewa mambo yale yaliyofundishwa na mitume makanisani katika Agano Jipya. Kwa hiyo, sasa tuyaangalia mistari yote ambayo moja kwa moja inahusu jambo hili la utoaji - kwa kuwa hata Biblia yenyewe haijakaa kimya juu ya jambo hili kubwa la kumtolea Mungu katika kizazi hiki cha Agano Jipya.

Mstari wa kwanza ambao tutauangalia unapatikana katika kitabu cha Matendo ya Mitume 11:29,

“…njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio. Na wale wanafunzi, kila mtu kulingana na uwezo wake alio nao, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Uyahudi.”

Hapa sasa tunakiona kigezo kimojawapo kilichohamasisha kiwango ambacho waumini walikitoa ili kuwasaidia waumini wengine ambao walikuwa wakiteseka kwa kupungukiwa na mahitaji yao ya lazima - waumini walitoa kila mmoja kulingana na uwezo wake alio nao (hiyo ni tafsiri ya Kigiriki. Union Version ya Kiswahili inasema, “kwa kadiri ya alivyofanikiwa”. Tutakutana na maneno hayo baadaye). Kulingana na lugha hii iliyotumika hapa, basi ni wazi kuwa watu walitoa pesa zao kwa viwango tofauti kabisa. Na inawezekana baadhi yao walitoa viwango vya fedha zaidi kuliko hata asilimia kumi ya mapato yao. Katika mazingira ya jinsi hii kiwango walichokitoa watu hawa hakikuzingatia mfumo wa kikumi unaofundishwa leo makanisani na wahubiri walio wengi wao. Badala yake utoaji ule ulizingatia uwezo wao wa kutoa.

Lakini pia tunagundua kuwa waumini wale walizikusanya pesa hizo kwa niaba ya Wakristo wenzao waliokuwa wanateseka kwa upungufu wa mahitaji ya lazima. Tutakuja kuona kuwa matoleo mengi maalum yalikuwa yakitolewa na kufanyika na kanisa lile la kwanza kwa nyakati hizo ilikuwa ni kwa ajili ya kuwasaidia waumini masikini waishio katikati yao - hasa wale waliokuwa wamepungukiwa na mahitaji yao ya lazima katika maisha yao.

Hebu basi tuangalie tena mstari mwingine muhimu wa neno la Mungu ambao unahusika moja kwa moja na somo letu ambao unaonyesha kwa uwazi kabisa kuwa utoaji haukuzingatia kanuni yoyote ile ya asilimia katika Agano Jipya.

“Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu. Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. Siku ya kwanza ya kila juma (yaani, jumapili), kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake…” (1 Wakor.16:1,2).

Kutokana na mistari hiyo hapo juu sasa tunaweza kupambanua mambo muhimu matatu. Jambo la kwanza ni kuwa wazo au desturi ya kutenga pesa jumapili ilifanyika kwa lengo la kuwasaidia Wakristo waliokuwa wakiteseka kwa ajili ya kukosa mahitaji muhimu na ya lazima.

Jambo la pili ni kwamba, haijatamkwa popote pale hapa wala mahala pengine popote pale kwenye Agano Jipya lote kwamba eti, pesa zilizokuwa zikikusanywa siku ya jumapili zilikuwa ni mali ya mchungaji - ya kwamba eti hiyo ilikuwa ni haki yake.

Na jambo la tatu ni kwamba kiwango cha pesa walichokuwa wanakitoa waumini wale hakikuzingatia mifumo ya asilimia kumi (kikumi) kama inavyodaiwa na kusukumwa leo makanisani, lakini badala yake walitoa kadiri ya kufanikiwa kwake mtu yule atoaye pesa hizo. (Huu hapa ni ukweli unaofanana na yale tuliyoyaona hapo juu ambapo watu walitoa kulingana na uwezo alionao mtu yule.) Maelekezo hayo yanamaanisha nini? Kwa baadhi, kwa mfano, ingemaanisha kuwa Mungu amewafanikisha zaidi kiasi kwamba hata wasingehitaji nusu ya mapato yao kwa wiki ile au mwezi ule, hivyo wangeweza kutoa nusu ya mapato yao. Usinielewe vibaya! Hii sio sheria. Hapa naelezea tu lile neno kuwa ‘kwa kadiri ya kufanikiwa kwake’ inavyomaanisha katika baadhi ya mazingira mengine.

Mstari mwingine ambao nao tutauangalia ni mmoja ya mstari iliyo wazi juu ya kanuni ya utoaji katika Agano Jipya. Mstari huo inaweka kwa ufasaha wa hali ya juu kabisa juu ya misingi inayotupasa kuifuata katika jambo hili la utoaji.

“Kila mtu ATOE KAMA ANAVYOKUSUDIA MOYONI MWAKE, SI KWA UCHOYO au kwa KULAZIMISHWA, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu.” (2 Wakor.9:7).

Hapa tena tunaona ya kuwa kutoa hakukuzingatia mfumo wa asilimia, lakini ilikuwa ni kutoa kulingana na nini kila mtu aliamua ndani ya moyo wake mwenyewe. Hii bila shaka inaweza kutushangaza, lakini hayo ndiyo mafundisho ya mitume. Hata hivyo kwa fundisho hilo bado mitume hawatupatii sisi fursa ya kuwa wanyimivu au wavivu katika kumtolea MUNGU. Mambo yote yaliyoandikwa hapo juu yanapaswa kututia moyo katika mwelekeo wa kinyume. Anasema kile unachokiamua moyoni mwako kinapaswa kiwe ni kitu kinachompendeza Mungu - na inampendeza Mungu kuwa tutoe kwa furaha na wala si kwa uchoyo. Mioyo yetu inapaswa iwe imefunguliwa na mitepetevu. Mtume Paulo anaendeleza hii kwa undani zaidi katika ukweli unaofunua kuwa mambo mengi yanayofanyika makanisani leo yapo kinyume na neno la Mungu - ni kwamba hatupaswi kabisa kutoa kwa kulazimishwa na kusukumwa.

Na hapa sasa ndipo tunafikia katika ukweli wa umuhimu wa hali ya juu katika somo hili la utoaji. Tafakari sana:

Hapa inasema kuwa ni kosa iwapo utakuwa unatoa kwa kuwa umelazimishwa. Ni makosa kutoa iwapo unajisikia kuwa unalazimishwa kutoa na mtu mmwingine! Iwapo itatokea kiongozi anakutishia kwa laana kwa sababu eti hutoi, basi pia ni makosa. Kutoa kwa sababu unataka kutoa ili uikwepe laana, ni makosa. Ni makosa kutoa kwa kuinyenyekea sheria - hii inawakilisha utoaji usio wa lazima utokanao na hofu kwa sababu ya shinikizo na wala si kwa uhuru utokanao na upendo. Mambo haya yote ni kumtolea Mungu kwa sukumwa na mambo ya hofu, kulazimishwa pamoja na mafundisho maovu na matendo ya uovu.

Nasema tena, ikiwa wewe utatoa kwa sababu umefanywa na mtu ujisikie ni lazima kutoa, ndipo utakuwa hutoi kwa moyo wa furaha. Ikiwa mtu fulani atakusukuma wewe kutoa kwa sababu ya sheria iliyopo katika Agano la Kale, kwa kufanya hivyo watu hao wanafanya kinyume kabisa na neno la Mungu kama lilivyotangazwa na mtume Paulo. Ikiwa mtu fulani atakutishia wewe kwa laana katika Agano la Kale ili kukulazimisha wewe kutoa, ndipo sasa watu hao watakuwa wanatenda dhambi dhidi yako, pia wanamtenda dhambi Kristo.

Na wachungaji wengi pamoja na viongozi wengi wanakosea sana, na wanafanya dhambi dhidi ya washirika wao kwa kuwaambia, “Utalaaniwa kama usipotoa zaka au fungu la kumi”. Fundisho la jinsi hiyo limejaa uwongo mtupu! Mitume wenyewe hawakufundisha hivyo. Bwana Yesu mwenyewe wala naye hakufundisha hivyo. Hakuna mahali popote katika Agano Jipya ambapo utakuta mitume wanawasukuma watu au kuwatisha waumini katika kutoa kwa kunukuu Malaki 3:8 -10! Kadhalika hakuna mstari wowote wanaounukuu kutoka katika Agano la Kale ili kuwasukuma waumini wao katika kutoa. Mitume walijua vizuri sana kile ambacho Agano la Kale kinafundisha juu ya utoaji kikumi pamoja na zaka, (sio tu kulingana na kile kinachosemwa na sheria lakini walijua kuhusu Abrahamu na Yakobo pia). Lakini pamoja na kuyajua kwao hayo yote hatuoni mahali popote ambapo mitume wanawatisha waumini kwa kuitumia mistari hiyo ya Agano la Kale kwamba ETI watalaaniwa iwapo watakuwa hawatoi; wala hakuna popote ambapo waliitwa ni waasi, kwa kutokutoa kwao kulingana na shinikizo la matakwa ya mchungaji; wala hakuna mahali popote ambapo wanatishiwa kufukuzwa kanisani eti, kwa sababu hawakutoa kulingana na matarajio ya viongozi wao wa kanisa. Mistari ya neno la Mungu katika Agano la Kale inatumiwa vibaya; na kisha watu wa Mungu wanachezewa na kutumiwa vibaya na wachungaji pamoja na viongozi wao wanaotafuta kuwanyonya washirika wao pesa zao kwa kujitafutia faida yao wenyewe au kwa faida ya madhehebu yao. Wanachokifanya wachungaji hao ni upinzani wa moja kwa moja wa neno la Mungu tulilolinukuu hapo juu. Wachungaji na viongozi wa jinsi hii wanajiweka wenyewe chini ya hukumu ya Mungu kwa kuwatendea dhambi watu wake Mungu, kwa kuitumia vibaya misitari ya neno la Mungu kwa faida zao.

Kama nilivyokwisha kusema, 2 Wakorintho ile sura ya 9, pamoja na sura ya 8, ni sura za umuhimu kwetu kwa vile imejaza mafundisho ya lazima yahusuyo kutoa. Katika ile sura ya 8 na ule mstari wa 7, Mtume Paulo anawaambia Wakoritho, “Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote…basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia.” Paulo anawatuia moyo ndugu waumini wa huko Korintho waige / wafuate mfano wa waumini wa huko Makadonia katika kukusanya pesa kwa ajili waumini masikini. Lakini sasa sikiliza kile akisemacho katika mstari unaofuatia hapo (v.8),

“Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu”

Mitume wa Bwana kwa MAKSUDI KABISA walijiepusha kuweka sheria katika jambo hili la utoaji. Tutambue pia, Paulo aliita utoaji huu ‘neema’. Anawatia moyo wapate ‘wingi wa neema hii’! Sasa je? Vipi unavyoweza kulazimisha ‘neema’? Katika kuelekeza kwao, hawatumii maneno kama vile “kama usipotoa basi utalaaniwa na Mungu kutokana na Malaki 3:9!”, au, “Kama usipotoa basi utatengwa na kanisa!” Mitume wanakataa kuwaamuru waamuni kutoa. Hawawaambii kwamba ni lazima kufuata ‘sheria’ fulani. Hataki kuwaagiza kuifuata sheria iliyoandikwa kwenye mawe au kutoka katika kitabu - bali anawataka wafuate upendo wa Mungu ambao umemwagwa kwa wingi ndani ya mioyo yao kwa Roho Mtakatifu. (1 Yoh. 3:17). Anachokifanya ni kuwaonyesha kuwa kile ambacho upendo wake Mungu ndani ya mioyo ya waumini wa Mekodania ilivyowaongoza waumini hao kutenda! Na mitume nao wanatamani kuona matunda hayo hayo ya upendo kutoka kwa wale waumini wa huko Korintho!

Anaelezea ukweli huo pia kwa waumini walioko huko Filipi wanaotuma pesa ili kumsaidia. Akiongelea kuhusu zawadi alizozipokea kutoka kwa hao waumini wa huko Filipi, anasema, “Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu.” Paulo anafurahia si tu kwa sababu amepokea zawadi, lakini zaidi ya yote anafurahia kile kinachowakilisha zawadi hiyo, ambacho ni tunda la upendo ndani ya maisha ya waumini wale ambayo Mungu mwenyewe anayahesabia ni ya thamani. Paulo anafurahishwa zaidi kuona kuwa waumini hao wanapaswa kubarikiwa zaidi yake yeye mwenyewe. Na je, mwelekeo huu ni mwelekeo wa wachungaji na viongozi wa siku hizi za leo? Na kama tunataka kukua kiroho na kuwa na matunda katika maisha yetu, basi ni wazi kabisa kuwa kutoa kwa moyo ulio huru ni ishara ya kukua huko na tunda hilo.

Kwa hiyo kulingana na Agano Jipya, mambo ya ukweli uliokuwa unaelekeza utoaji wao, ulikuwa kama ifuatavyo. Wakristo walitoa “kadiri ya kufanikiwa kwao”, na “kulingana na uwezo wake alio nao”, au hata “atoe kama anavyokusudia moyoni mwake.” (1 Wakor.16:2; Matendo 11:29; 2 Wakor.9:7).

Agano Jipya halitoi maelekezo yoyote mengine kwa Wakristo yanayohusiana na kiwango ambacho muumini anapaswa kukitoa katika utoaji wao - mbali na mistari hiyo hakuna mistari mingine yoyote inayowamuru kuhusu kikumi (asilimia kumi ya mapato yake).

Lakini si jambo zuri kupunguza kile unachokitoa kwa sababu ya mambo haya, kwani Mungu anaona mioyo yetu na “humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu”. Kwa sababu hiyo, mtume Paulo anatupatia onyo moja linaloonekana ndani ya Agano Jipya, ambalo si kama ni onyo lakini linaonekana ni kama ukiri wake wa kweli kwamba tunapaswa kuchochea mioyo yetu katika utoaji. Jambo hilo ni hili,

“Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.” (2 Wakor.9:6).

Lakini tafadhali angalia vizuri sehemu hiyo; Paulo hatishi wala hatengenezi sheria ili kuwasukuma waumini katika utoaji. Badala yake YEYE anafunua ukweli wa kiroho ambao utatufanya sisi kufikiri kuhusu hali ya mioyo yetu katika jambo hili. Ninaamini kuwa mstari huu wa neno la Mungu unaonyesha kuwa iwapo mtu mmoja atachagua kutoa ‘kidogo’ au ‘kwa uchache” (yaani, kichache kile alichotoa kinalinganishwa na ukweli wa vile alivyo navyo), ndipo na wao watavuna kwa uchache, si tu katika hali ya vitu, lakini ya kiroho, kwani kile unachotoa kinawakilisha au kudhihirisha pia hali ya moyo wako. Lakini hatuwi watu wa kiroho kwa kuyatazama na kuyafuata mambo ya nje, kwa kufuata sheria. Matendo yetu ya nje yawe ni mng’aro wa hali ya moyo. Utoaji wetu lazima utokane na mioyo yetu kwamba umeguswa na kubadilishwa kwa upendo wa Mungu. Hii ndiyo sababu hakuna hata mtume mmoja katika mafundisho yao anaweka sheria katika mambo ya utoaji.

Makusudi yote ya Agano Jipya ni kwamba ili tuweze kuzaliwa mara ya pili, na kupata upendo wake Mungu uliomwagwa ndani ya mioyo yetu kwa Roho Mtakatifu - na kwa Roho wake Sheria za Mungu zimeandikwa ndani ya mioyo yetu (Hebr 8:10). Kama vile ilivyo maisha yetu sasa yaongozwe kwa nguvu ya Roho wa Kristo ndani yetu, na wala si kwa kujaribu kutii sheria zilizoandikwa kwenye mawe, hivyo basi utoaji wetu uongozwe na upendo wa Mungu ndani ya mioyo yetu, sio kwa kulazimishwa na sheria ya nje. Sisi ni watu tuliozaliwa mara ya pili! Katika Kristo sisi tumefanyika kuwa ni viumbe vipya, mambo ya kale yamepita na mambo yote yamekuwa mapya - na mambo yote ni ya Mungu. Ni Agano Jipya ambalo ndani yake Mungu ametupatia moyo mpya na Roho mpya (Ezek. 36:26) na maisha mapya, ambayo ni maisha yake Kristo, ambayo ni maisha ya milele! Sasa tutarudije tena kwenye mambo ya kale? Tutaishije tena kwa mambo ya kale (kutegemea Agano la Kale).

Kama tumezaliwa toka juu kweli kweli, itakuwa tabia yetu kuwasaidia watu wa Mungu – hasa washirika maskini - watumishi wa Mungu na kazi ya Mungu. Tunapaswa kuongozwa na upendo na Roho ya Mungu ndani ya mioyo yetu kadhalika katika utoaji wetu. Simaanishi kuwa unapaswa kusubiri Roho akuambie cha kufanya kila wakati, bali mioyo yetu iwe imebadilishwa haswa kwa Roho wa Mungu hadi kwamba tunafurahia kusaidia watu wa Mungu na kazi ya Mungu.

Huwezi kutengeneza sheria kwa upendo! (Warumi 13:10).

Unaweza kufundisha, kuonya na kusihi, lakini kama utafanya sheria ili watu waweze kuziishia hizo ndipo basi utakuwa unalipinga Agano Jipya ambalo Kristo Yesu alimwaga damu yake na utakuwa unarejea kwenye ukale. Hiyo sasa itawaongoza watu katika kutoa kwa ulazima ambapo ni kinyume cha mambo yote tuliyoyasoma hadi sasa katika Agano Jipya. Mengi ya yale aliyoyaandika Paulo kwa waumini wa huko Galatia imeungana na pambano hili la vita kinyume na wale wanaotaka kuwarudisha watu katika kutunza sheria mbalimbali za Agano la Kale.

Katika Matendo sura ya 15, pale mitume wanapoyaandikia makanisa kuwaonya kuhusiana na wale wanaodai kuwa washirika lazima waitunze sehemu ya sheria ya Musa, hapo hapo mitume bado hawalitaji suala la kikumi hata mara moja, kana kwamba ni jambo la lazima kwa mshirika kutoa kikumi hicho wanapotoa maamuzi yao katika jambo kama hili. Zaidi ya hiyo, jambo hilo halikuwa tu ni maamuzi yao, bali yalikuwa ni maamuzi yaliyofanywa kwa maelekezo ya Roho Mtakatifu (Mtd.15:28)

Hakuna mahala popote katika Agano Jipya ambapo panaagiza mambo kama hayo au hata kushauri tu kwamba Wakristo wafuate mambo ya kisheria katika mfumo wa kutoa kikumi. Wala hakuna mahala popote katika Agano Jipa ambapo panaelezea kiasi gani cha mapato ya mshirika au muumini anayopaswa kuyatenga ili kumtolea Mungu.

Mitume walisikiliza mafudisho ya Yesu, pia walijua yaliyoandikwa katika Torati, lakini hawakufundisha juu ya ‘fungu la kumi’ au juu ya ‘sheria ya utoaji’, wala hawakuwatisha waumini kwa laana! Kama wao hawakutumia cheo wala mamlaka yao kama mitume wa Bwana Yesu kuwatisha na kuwakamia watu wa Mungu lazima watoe zaka au fungu la kumi vinginevyo watawalaaniwa na Mungu, je, wahubiri / wachungaji hawa wanapata wapi na kutoka kwa nani mwongozo huu wa kutisha watu wa Mungu kiasi hiki? Hawapati mamlaka wala ruhusa kutoka Biblia wala kutoka kwa Mungu Mwenyewe bali wanajiinua juu ya neno la Mungu, na wanawatenda dhambi washirika!

ANANIA NA SAFIRA

Lakini sasa niseme neno kidogo juu ya Anania na Safira. Watu hawa hawakufa eti, kwa sababu walikataa kutoa kikumi (kama watu wengi wavyoweza kufikiri), bali walikufa sababu walidanganya. Waumini wengi tu walikuwa wakiuza ardhi na nyumba zao, na walileta pesa zote kwa mitume. Wanapozileta pesa hizo kwa mitume hazikuwa kama kikumi au nusu ya ya mapato ya mali zao, bali wao kwa hiari yao walikuwa wakileta asilimia kwa mia ya mauzo yote ya ardhi na nyumba zao! Anania na Safira waliuza ardhi yao kisha WAKAJIFANYA ILI WAONEKANE kuwa wanaleta pesa zote za mauzo ya mali zao kwa mitume. Sasa ilikuwa ni kwa sababu ya udanganyifu (uongo wao huo) ndicho kilicho wasababishia kufa.

Ebu tusome mtume Petro alichosema kwa Anania, 'Anania mbona shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu. Ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? Je, kabla hujauza hicho kiwanja SI KILIKUWA MALI YAKO? Hata baada ya kuuza fedha ulizopata SI ZILIKUWA KWENYE UWEZA WAKO?” (Mtd 5:1-5). Kwanza kabisa mtume Petro anamwambia Anania kuwa amemdanganya Roho Mtakatifu, ndipo anamweleza kuwa hakukuwa na haja ya kudanganya (kusema uongo), kwani uwanja uliouza ulikuwa ni mali yake. Hawakuhitajika kuuza kiwanja hicho! Lakini hata baada ya kukiuza bado pesa hizo zilikuwa ni mali yao; hawakulazimika kuzileta pesa hizo kwa Petro. Unaona, haikuwepo sheria yoyote kuhusu jambo hili, bali waumini walitoa vitu vyao kwa hiari na kutokana na pendo. Anania na Safira walitenda dhambi kwa sababu wao WALITAKA KUIGIZA WATU WENGINE lakini jumbe mioyoni mwao walikuwa na uchoyo, hivyo walidanganya kuhusu kiasi halisi walichotoa. Uchoyo huu ndani ya mioyo yao na udanganyifu (uongo) ndiyo ilikuwa dhambi yao. Mtume Petro aliweka wazi kabisa kuwa hawakuwa chini ya sheria yoyote katika kuuza ardhi yao na kisha kuleta pesa hizo kwake! Yote yalikuwa jambo la hiari tu!

Kama wangekuwa hawajauza ardhi yao wasingeweza kuhukumiwa; lakini pia kama wangeuza ardhi yao kisha wakasema kuwa wameuza ardhi yao na wameleta nusu tu ya mauzo yao na kuyaleta kwa mitume hapo pia wasingeweza kuhukumiwa.

Lakini sasa walidanganya; walitafuta waonekane kama wengine wao. Ilikuwa ni kwa sababu ya udangaanaayifu huu na uwongo huu ndipo walihukumiwa. Wachungaji au viongozi wanaotumia mistari hii ya neno la Mungu ili kuwatishia watu katika kutoa wanalichafua neno la Mungu kisha wanawatendea dhambi watu wa Mungu.

KUTOA PASIPO KUHESABU GHARAMA

Tunaona kwa waumini katika Agano Jipya pengine utoaji hauna mipaka!

“Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, WAKIUZA MALI ZAO, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama KILA MTU ALIVYOKUWA NA HAJA.” (Matendo 2:44,45).

“…wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, WAKALETA THAMANI YA VITU VILIVYOUZWA, wakaiweka miguuni kwa wale mitume, kila mtu akagawiwa KADIRI YA MAHITAJI YAKE.” (Matendo 4:34,35).

Unaona? Wengi wa waumini wa Yerusalemu waliuza mashamba na nyumba zao, nao walileta thamani kamili ya vitu walivyouza - walitoa 100%, siyo fungu la kumi. Jambo kama hilo halikutokea kabla yake. Kulitokea nini hata kusababisha watu wa Mungu kutoa kwa jinsi hiyo pasipo sheria yoyote iliyotolewa kwao? Kilichotokea hapo ni lile Agano Jipya. Siku ile ya Pentecoste wanafunzi walibatizwa katika Roho Mtakatifu, na wakauza mali zao kwa hiari yao kabisa kwa sababu ya pendo la Mungu ambalo lilikuwa limemiminwa ndani ya mioyo yao na Roho Mtakatifu. (Hii haimaanishi kuwa tunapokuwa tumekwisha batizwa katika Roho Mtakatifu basi tunapaswa sasa kuuza nyumba zetu. Hii sio sheria ya kuifuata, bali ni maelekezo kuonyesha kuwa nini kinatokea wakati watu wanapokuwa wamejazwa na Roho wa Mungu. Katika Matendo ya Mitume hatusomi popote juu ya kutokewa na mambo kama hayo baadaye tena katika miji mingine ambako Injili ilikuwa ikihubiriwa. Hebu niongeze hapa kuwa ninaamini kuwa watakatifu waliokuwepo Yerusalem kwa ujumla waliuza nyumba na ardhi ilikuwa ni zidio la yale wanayoyahitaji katika matumizi yao ya kila siku.)

Pendo halifanyi kazi yake kutokana na sheria za Agano la Kale.

Pendo halitambui wala halina mipaka! Hilo ndilo Agano Jipya!

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee…” (Yoh.3:16).

Bwana apewe sifa! Kwa hiyo imeandikwa ‘Pendo ndilo utimilifu wa sharia.’ (Warumi 13:10). Kutoa ni hiari, ni tendo la hiari la upendo na kuabudu ambalo linavuka utii wa sheria ya nje. Halitokani na madaraka au wajibu. Halihesabu. Ni tendo la mwitikio la mara moja la yeye anayempenda Mungu na anayetaka kuona jina lake Mungu likitukuzwa hapa duniani na watu wake wakibarikiwa.

Kazi au matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu ni kwamba tutoe kwa hiari kwa sababu ya upendo wa Mungu mioyoni mwetu. Onyo ni mmoja tu katika Agano Jipya, yaani, “Ye yote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache…”. Katika Agano Jipya tunafundishwa kwamba, “Kusudi (au mwisho) la maagizo (sheria) haya ni upendo, utokao katika moyo safi,…” (1 Tim.1:5). Kama Wakristo tunapaswa kutoa kutokana na upendo wa Mungu ndani ya mioyo yetu kwa hiari, kwa furaha, siyo kwa sababu ni lazima nishike maagizo yaliyopo nje yangu au kuepuka laana! Kama upendo wa Mungu upo ndani ya moyo wangu utoaji ni jambo la kawaida kwangu! Lakini hiyo haimaanishi kwamba hatuwezi kuwahamazisha watu kwa mafundisho watoe kadiri ya upendo wa Mungu, kama vile tunavyofanya juu ya mambo mengine, na kama vile Paulo anavyofanya. Lakini kama ukitaka kuwafundisha waumini lazima watoe zaka au fungu la kumi sawasawa na Torati (Toarati inazingatia vitabu vitano vya kwanza ya Agano la Kale), lazima utuonyeshe angalau hata mstari mmoja katika Agano Jipya ambapo waumini wanafundishwa na Mitume kufanya hivyo! Lakini haupo!

Kama tumezaliwa toka juu kweli kweli, kama tumebatizwa na Roho Mtakatifu, itakuwa TABIA YETU kuwasaidia watu wa Mungu, watumishi wa Mungu na kazi ya Mungu!

Hata hivyo, hata kwa wale walioishi bado chini ya sheria ya Musa, pendo kwa Mungu na kwa kazi Yake mioyoni mwao halikutambua mipaka! Tunasoma,

“Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” (Marko 12:41-44).

Kwa mujibu wa maneno ya Yesu, thamani ya sadaka mbele ya Mungu inategemea SIYO na thamani yake kwake anayeipokea, BALI na thamani yake kwake anayetoa ile sadaka! “Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote.”

Tumeiangalia mistari ya neno la Mungu ambayo imetujulisha kuwa waumini walimtolea Mungu kulingana na uwezo waliokuwa nao, kulingana na jinsi Mungu alivyowabarikia, na pia kulingana na kila mmoja wao alivyoamua kataika moyo wake. Hivyo basi kutokana na mistari hiyo tunatambua kuwa hakuna asilimia yoyote ya matoleo iliyotajwa. Na waumini wangeweza kumtolea Mungu zaidi hata ya hicho kikumi. Lakini tena, hizo sio kanuni iliyowekwa na Agano Jipya - hayo ni maelekezo yanayoonyesha nini kilitokea na ni miongozo ambayo Wakristo wanaagizwa katika mambo yahusuyo kutoa.

-------------------------------

Sheria ilitolewa na Musa lakini kweli na neema imekuja kupitia Kristo Yesu. Katika Agano Jipya, kama nilivyosema, mambo yamebadilika! Sisi si mali yetu wenyewe, tumenunuliwa kwa gharama yenye thamani kubwa (1Wakor. 6:19,20). Kwa hiyo, hatupaswi kuishi maisha yetu wenyewe isipokuwa tuishi maisha kwake Yeye aliyetufilia (2 Wakor.5:15). Kutokana na hayo tunatambua kwamba sio tu sisi wenyewe, bali vyote tulivyo navyo na tunavyo vimiliki ni vya Bwana. Yesu mwenyewe aliwafundisha watu katika Luka 12:32,

“Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu.”

Yesu Kristo anadai maisha yetu yote - jinsi tulivyo na vyote tulivyo navyo. Tumeona matokeo ya kujazwa na ujio Roho Mtakatifu katika Matendo ya Mitume, ile sura ya 2 na ya 4, mahali ambapo baadhi ya waumini waliuza nyumba zao na mali zao ili kuwasaidia waumini walio masikini. Mambo ya asilimia kumi au kikumi ilikuwa haipo. (Narudia tena, haitupasi kuuza nyumba zetu ili kwamba tujikute hatuna mahala pa kuishi na tunaishia kurandaranda mitaani pamoja na familia zetu!)

Lakini pia kuna mifano mingine inayoonyesha utoaji wenye uwingi mkubwa katika Agano Jipya kama tulivyokwisha kuonyesha hapo juu, kuwa upendo hautambui/hauna mipaka, wala upendo hauzuiliwi na sheria kama tunavyoweza kurudi kusoma katika 2 Wakorintho,

“…maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu. (2 Wakor.8:2-5).

Hii ni mistari mizuri ajabu! Waumini hao walikuwa ni maskini na walikuwa wakipitia njia ya ugumu na mateso kwa maisha yao. Hata hivyo, pasipokujali ugumu wa maisha yao wao wenyewe, waumini hao walikuwa na moyo uliotamani kutoa na kutoa kwa utoshelevu mkubwa kabisa! Kwa hiyo kwanza, walijitoa wao wenyewe kwa Bwana na bila shaka wakikiri kuwa wao wenyewe na vyote walivyokuwa navyo ni mali yake Bwana. Kutokana na upendo huu wa Mungu walikuwa walihiari kumtolea Mungu zaidi na kuzidi. Hivyo ndivyo upendo wa Mungu katika mioyo yetu unavyoweza kutuongoza!

Unapojisomea mistari hii, je, unapata hisia kuwa watakatifu hao walitoa pesa zao ili kwamba waje kupata pesa zaidi baadaye? Je, unafikiri kuwa labda mioyoni mwao walifikiri kuwa, “tukipanda kwa uhaba basi tutavuna haba - basi ebu tutoe pesa ili tuweze kubarikiwa kwa kupata pesa nyingi zaidi? Hapana! Mawazo kama hayo hayakuwemo katika mioyo yao kabisa, kwa sababu huo ungekuwa ni uchoyo na kubadilisha utoaji kuwa ni mfumo wa kibiashara. Na kwa sababu ya upendo wake Mungu ndani ya mioyo yao walikuwa wanashauku kubwa ya kuwasaidia ndugu waliokuwa waahitaji - pasipo hata kufikiria chochote kile au hata bila aya kujitafutia faida yoyote ile. Walijitoa katika utoaji wao. Tufuate mfano wao! Yeye apandaye kwa uhaba anavuna kwa uhaba. Huo ni ukweli wa kiroho ambao unapaswa kuyachonga maisha yetu. Lakini hiyo sio sababu inayompelekea mtu kutoa. Usijaribu kutoa ili kuja kupokea, huo ni uchoyo na sio upendo; hiyo ni biashara na sio kujitoa. Nitagusia jambo hili muda mchache unaofuatia.

Nilionyesha hapo juu kuwa kulikuwa na aina nyingi sana za utoaji katika Agano la Kale. Na hii ni kweli kwa mujibu wa mistari ya neno la Mungu. Kulingana na mistari ifuatayo inaonyesha kuwa kulikuwa na kikumi kwa Walawi (Hesabu 18:21,24); kulikuwa pia na kikumi kwa ajili ya karamu na sherehe (Kumb. 14:22-27). Na kisha kulikuwepo na kikumi kwa ajili ya Walawi na watu masikini kila mwaka wa tatu (Kumb.14:28-29). Matoleo hayo yote yangepaswa kupanda zaidi hata ya kikumi ya kile kilichotolewa. Zaidi ya hayo, tunao pia mfano wa matoleo ya hiari, ambayo wana wa Israel waliyatoa kwa hiari yao na kwa utoshelevu mkubwa. Basi tunasoma katika kitabu cha Kutoka kuwa wito ulipotolewa kwa wana wa Israeli ili kuchangia ujenzi wa hekalu la Mungu,

“Wakaja kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza, na kila mtu ambaye roho yake ilimfanya kuwa apenda, nao wakaleta sadaka za kumpa Bwana, kwa kazi ya hema ya kukutania, … Wana wa Israeli wakaleta sadaka za kumpa Bwana kwa hiari; wote, waume kwa wake, ambao mioyo yao iliwafanya kuwa wapenda kuleta kwa hiyo kazi, … nao wakasema na Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo Bwana aliagiza ifanywe.” (Kutoka 35:21; 35:29; 36:5).

Ni jambo la kushangaza kwamba waandishi wengi wanalinganisha utoaji wa sheria katika mlima wa Sinai na siku ile ya Pentekoste, na kama tunavyosoma katika kitabu cha Matendo 2, hapa pia tunakutana na furaha ya utoaji wenye utoshelevu usio na mipaka, hata kwamba mwisho wa utoaji wao kulipatikana matoleo mengi zaidi.

Naitaja mifano hii si kwa ajili ya kutengenea sheria kwa ajili yetu. Hapana, bali ni kutaka kuonyesha kuwa hata nyakati za Agano la Kale utoaji haukuwekewa mipaka kwa asilimia kumi tu; hakukuwepo na utoaji wa kulazimu tu, bali kulikuwepo pia na utoaji wa hiari kama huo nilioutaja hapo juu. Kadhalika huo utoaji wa hiari Waisrael waliweza kuleta wakati wowote (Walawi 1:3). Nayataja mambo haya ili kuonyesha kuwa hata katika nyakati za Agano la Kale kulikuwepo na wazo la kutoa pasipo mipaka. Je, hiyo haipaswi kuwa ni kweli kwetu sisi katika Agano hili Jipya ambapo upendo wake Mungu umemiminwa katika mioyo yetu kwa Roho Mtakatifu?

Mtu yeyote asemaye kuwa makala haya yatapunguza kipato cha kanisa, au kitawafanya watu wasitoe au kupunguza kile wanachokitoa kwa sababu mimi ninaonyesha wazi kuwa utoaji hauna sheria, wala mipaka kuhusiana na mifumo ya utoaji katika Agano Jipya, basi mtu huyo hajaelewa chochote katika yote niliyoyaandika katika makala hii.

NENO ‘KIKUMI’ AU ‘ZAKA’ KATIKA AGANO JIPYA

Ni muhimu pia kugundua kuwa neno ‘ZAKA’ (‘kikumi’ - asilimia kumi) haijatajwa kwa mujibu wa kanisa lake Mungu. Imetamkwa katika muktadha 3 katika Agano Jipya - mara mbili kuhusika na mafarisayo (Luka 18:12; 11:42); na mara moja tu katika kitabu cha Waebrania 7, ambapo inaelekeza mahala ambapo Ibrahimu alimtolea Melkizedeki na kile kilichokuwa kinatolewa na kabila la Walawi (Nitaongea juu ya jambo hili baadaye kidogo kadiri tunavyoendelea na makala hii). Lakini hii ndiyo kumbukumbu za mwandishi kwa nyakati zilizopita kuonyesha kuwa Melkizedeki (Yesu) alikuwa ni mkuu kuliko Ibrahimu. Mistari hiyo hapo haimfundishi Mkristo chochote kile kuhusu kutoa kikumi leo!

Hebu pia iwekwe wazi kuwa katika nyaraka za mitume kwa makanisa, sio tu kwamba hakuna popote panapotajwa juu ya kikumi, lakini zaidi ya hilo hakuna pia popote pale panapotaja utofauti wa matoleo kama vile kikumi, zaka na dhabihu, au matoleo ya mwaka mpya, tunda la kwanza na mambo mengine mengine mengi yanayokuzwa na wahubiri na ‘manabii’ wa leo katika makanisa. Watu wengine wanapenda kuleta mawazo ya Agano la Kale yahusuyo kutoa katika kanisa la Kristo leo. Pia wanapenda kuelezea namna mbalimbali ya matoleo na utofauti wa aina zake na kisha kuyawekea kanuni katika kanisa.

Mambu hayo yote ujue kuwa yapo kinyume kabisa na fundisho la Agano Jipya, ni kinyume pia na fundisho la Mitume wa Yesu, na zaidi ya yote ni kinyume na maelekezo ya Roho Mtakatifu ndani ya mioyo ya wote wanaolazimishwa kutoa kwa jinsi hii. Mitume hawakuweka jambo kama hilo katika mafundisho yao, na jambo lingine linalolingana na hayo tunasoma juu ya watu wafanyao mambo ya aina hiyo katika 1 Timotheo 1:6,7:

“Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili; wapenda kuwa waalimu wa sheria, ingawa hawayafahamu wasemayo wala mambo yale wayanenayo kwa uthabiti.”

Iwapo kama inakupendeza wewe kuufanya huu utofauti, na kisha ukaongozwa na mfumo wa aina hiyo ya utoaji, basi fanya hivyo wewe mwenyewe kwa usiri wa nafsi yako tu, lakini usiwapeleke watu wa Mungu katika vifungo vya utoaji wa jinsi hiyo kwa kuwafanyia sheria wengine! Pia, kama wewe unapenda kuishi katika mifumo ya Agano la Kale huo ni uchaguzi wako, lakini katika Agano Jipya Wakristo wao hutoa tu kwa Mungu wao na wakati mwingine hutoa hata asilimia miamoja. Na matoleo yao yote yanakusudiwa kuwa ni “harufu ya manukato, sadaka yenye kibali impendezayo Mungu.” (Wafilipi 4:18).

TATIZO LA FUNGU LA KUMI LENYEWE

Tatizo moja kubwa au hatari yakufuata sheria katika mambo yahusuyo kutoa fungu la kumi ni kwamba, unapokuwa umekwisha kulitoa fungu la kumi hilo, utaweza kuamini kuwa umefanya kilicho sawa, kile kinachohitajika. Unafikiri kwamba jukumu lako la kutoa sasa limekwisha kwa wiki ile au kwa mwezi ule! Hapo ndipo hasa ni mahala au ni fikra ambayo sheria inakuingiza uwazie, kwa sababu wewe sasa unafanya utoaji ule kana kwamba ni jukumu ulilopewa ulifanye au kazi fulani ili kutimiliza sheria. Utoaji sasa unageuka kuwa ndio jukumu la kidini badala ya kuwa ni tendo la uhuru na upendo tu! Kwa hiyo hatari kubwa hapo ni kwamba utakuwa unajisikia ni mwenye haki, au upo sawa mbele za Mungu kwa sababu tayari unajiona kuwa umekwisha timiza (unalofikiri ni) ‘wajibu’ wako wa kutoa fungu la kumi wiki au mwezi ule! Tukumbuke onyo la Bwana Yesu tusianguke katika fikra za Mafarisayo ambaye alisema moyoni mwake, “Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.” (Luka 18:12).

Ni vilevile kama ilivyotokea kwa waumini wa kanisa la Galatia, ambao wao waliamini kuwa wanapaswa kutimiza aina fulani fulani za sherehe za Agano la Kale kushika sabato, kutahiriwa ili kwamba wawe na haki mbele za Mungu! Mtume Paulo anawaonya kwa nguvu sana dhidi ya ya mawazo kama hayo. Tatizo lingine kubwa na hatari zake ni kuwa kama wewe unaamini katika mambo ya kutoa hilo fungu la kumi, basi itaweza kukuwekea mipaka juu ya upendo wa Mungu na katika utendaji kazi wa Roho Mtakatifu ndani ya moyo wako, kuhusiana na jambo hili la kutoa zaidi ya kikumi kila mwezi. Hakuna mahala popote katika Agano Jipya panapoelezea kuwa Waakristo tutakuwa tumetimiza wajibu wetu pale tutakapokuwa tumetoa kikumi kanisani kila mwezi.

MSAADA KWA WACHUNGAJI

Hebu sasa, tuone maandiko katika Agano Jipya yanasemaje kuhusu utoaji au msaada wa wachungaji na watumishi wengineo. Ipo sehemu moja tu katika Agano Jipya inayojishughulisha na jambo kama hili mjoa kwa moja, yaani, 1 Timotheo 5:17,18:

“Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, ‘Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka’. Na tena, ‘Mtenda kazi astahili ujira wake.’” (Kwa lugha ya Kigiriki neno ‘wazee’ na sawa na ‘wachungaji’.)

Maana ya maneno hayo hapo ni wazi kabisa; ikiwa mchungaji hana kazi nyingine (yaani, hana mapato mengine) kwa sababu mtu huyu anafuata mwito wake kwa kuwalisha washirika na neno la Mungu, basi ni jambo la haki na ni la upendo washirika watambue kujitoa kwa mchungaji wao huyo mzuri kwa ajili ya kanisa la Bwana na hivyo kumsaidia na riziki zake, sawasawa na mahitaji yake. Ni jambo la maana sana kwa somo hili tutambue lugha ya mtume. Hapo hataji ‘fungu la kumi’ wala hafundishi kwamba makusanyo yote ya jumapili lazima yawe mali ya mchungi kama vile ilivyofanyika kwa walawi na makuhani walivyopata fungu la kumi sawasawa na sheria ya Kumbukumbu sura 18 na Hesabu 20:20,21. Hapana, hafundishi hivyo! Paulo ananukulu maneno ya Yesu (Luka 10:7) na sheria ya Torati la Musa juu ya ng’ombe (Kumbu.25:4), kwamba yule ng’ombe anayefanya kazi kwa ajili yako lazima umhurumie na kumruhusu kula. Kwa hiyo, Paulo anasema tunapaswa tutambue kazi nzuri ya mchungaji kwa ajili yako na kumhurumia na kumheshimu kwa ajili ya kazi hiyo aliyoifanya kwa ajili ya watu wa Mungu. Lakini utoaji huo haupaswi kutumika ili kumtajirisha mchungaji au mtume au mtumishi yoyote; au utoaji huo usimfanye mchungaji aonekane kuwa ni tajiri kuliko makutano anayoyahudumia.

Na pia jambo la kuzingatia hapa ni kwamba utoaji huo uwe ni wa hiari kutoka moyoni mwa mtu, yaani, tunaona kutokana na maneno ya Paulo yeye haweki sheria wala hatoi mfumo wa rasmi wa kuwasaidia wachungaji, ila anawakumbusha waumini juu ya daraka lao ya haki na ya upendo. Nilisema utoaji hautokani na sheria fulani ila uwe ni wa hiari na siyo ‘kwa kulazimishwa’, lakini tena hayo hayamaanishi tuwe wavivu katika jambo hili. Katika mambo yote haki na upendo ndio unaopaswa kutuongoza sisi, na sio sheria na hii ndiyo sababu inayowafanya mitume wasite kuweka kanuni – badala yake wanatukumbusha, anatusihi, anatutia moyo kufuata mambo ya haki.

Mafundisho hayo ya Paulo (1 Tim.5) tunayapatia pia 1 Wathesalonike 5:12,13:

“Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni; mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao.”

Sehemu hii mtume Paulo hataji chochote juu ya msaada kwa ajili ya watumishi wa Mungu lakini naamini kuwa lile neno ‘muwatambue’ na ‘mkawastahi sana’ pamoja na lile alilolisema katika 1 Timotheo 5 linatuongoza tuweze kufahamu hivyo.

Nimesema kuwa tunapaswa kuongozwa na upendo, huruma na haki katika utoaji wetu. Hivyo basi ebu nitoe mifano michache ili kukionyesha kile ninachomaanisha hapa. Kwa mfano, nawafahamu baadhi ya wachungaji katika vijiji fulani ambako washirika wao ni masikini, na makusanyo ya sadaka zao za jumapili zinaweza kufikia kati ya sh. 2000 hadi 5000. Kiwango hiki cha pesa sio kikubwa sana. Ingewezekana katika hali kama hiyo, basi washirika wangesema kuwa Mchungaji, “Shiling elfu tano si kiasi kikubwa sana, tafadhali chukua hizi shilingi elfu tano kwa ajili ya matumizi ya familia yako pale nyumbani.” Kwa hiyo katika hali kama hii washirika hao wangechagua kumpa mchungaji wao makusanyo hayo yote ya sadaka ya siku hiyo ya jumapili. Hili sasa ni jambo la huruma na upendo na haki pia. Amina!

Nilipokuwa nahudumu kama mchungaji mshiriki katika kanisa, hakuna makusanyo yoyote ya sadaka za jumapili nilizokuwa napewa mimi, wala hata kwa wale wachungaji wenzangu wawili tuliokuwa tukihudumu pamoja. Makusanyo hayo ya pesa yalikuwa yanatumika kwa ajili ya kulipia gharama za uendeshaji wa kanisa hili kama vile umeme n.k. Lakini nyingi ya pesa hizo zilikuwa zinatolewa kusaidia kazi ya Mungu kwa baadhi ya maeneo katika nchi ile pia hata nje ya nchi ile. Lakini ilikuwa inatokea iwapo mshirika yeyote alipenda kunipa mimi, au hata yoyote kati ya wachungaji wenzangu tuliokuwa tukitumika pamoja, basi kulikuwa na sanduku limewekwa kanisani humo ambamo mtu huyo angeweka pesa hizo ndani ya kijisanduku kile. Wangeweka pesa hizo katika bahasha na juu ya bahasha ile wangeandika jina la mchungaji yule wanayependa kumsaidia. Lakini hauweki jina lako wewe unayetoa pesa hizo juu bahasha yako, kwa kuwa tunaamini kuwa si sawa kwa mchungaji kuelewa ni nani anayempatia pesa hizo. Huo ulikuwa ni wakati wangu mzuri kabisa katika maisha yangu kwa sababu nilikuwa ninamtegemea Mungu - naye alikuwa mwaminifu kwangu. Sikuwa na pesa nyingi katika familia yangu, lakini nilipata amani na furaha kubwa katika moyo wangu kwa sababu niliamini Mungu ameniita mimi kwa jambo hili na moyoni mwangu nilipata utoshelevu kumwekea yeye Mungu matumaini yangu. Hii (yaani, viongozi wa kanisa kusaidiwa na utoaji wa hiari na kujitolea wa washirika wale) inaonekana ilikuwa ni hali ya kanisa la Agano Jipya pia kama tulivyouona Mtume Paulo alivyo kuwa akiwasihi kama nilivyo nukuu hapo juu.

Au, washirika wa makanisa makubwa ya mijini wanaweza kuamua kumsaidia mchungaji wao kwa kutenga pesa kiasi ya sadaka zinazokusanywa siku ya jumapili ili zimfae kwa mahitaji yake pamoja na familia yake. Hicho ndicho kinachofanyika kwa makanisa mengi ulimwenguni kote. Kwa upande mmoja hii inamfanya mchungaji awe na uhakika wa kipato kusaidia familia yake katika mahitaji ya lazima, lakini kwa upande mwingine inaweza kuonekana kana kwamba mchungaji huyo anaifanya huduma hiyo ni ajira. Wengi wanaona uhakika huu wa kipaato ni mzuri na ni jambo la haki, lakini mimi sina uhakika kama tunaweza kuifanya huduma ya kichungaji ionekane kama vile ni kazi zingine za ajira - kama afisa mifugo, kilimo, menega, n.k. Ila hilo ni wazo langu tu.

Hata hivyo, Biblia haitoi haki au ruhusa ya mtu fulani kuyachukua makusanyo yote yanayofanyika jumapili eti yawe ni yake. Hapana! Inapotokea mtumishi yoyote anadai pesa za sadaka jumapili kuwa ni haki yake kuzichukua, basi mtu huyo anafanya biashara zake mahala hapo, anafanya biashara na kuwanyonya watu wa Mungu. Hii ni dhambi kubwa sana. Hakuna fundisho lolote katika makanisa ya Agano Jjipya linaloelekeza hivyo wala hatuoni mfano wowote wa aina hiyo. Punde tu nitakwenda kuonyesha jinsi baadhi ya wachungaji na makanisa wanavyowatendea vibaya na kuwaharibu washirika wao katika jambo hili la utoaji.

MSAADA KWA WENGINE WAFUNDISHAO NA KUHUBIRI INJILI

Sasa nataka kurudi na kuangalia juu ya mistari inayoelezea juu ya kuwasaidia wale waliomo katika huduma. Msaada huu hauhusu wachungaji wa kanisa tu bali pia na kwa wengineo. Tunaona kuwa mtume Paulo anafundisha kuwa utoaji unaotelewa na washirika unaweza kumhusu mtumishi wa Bwana yeyote yule anayejitaabisha kwa ajili ya watu wa Mungu na kazi yake. Na ukweli huu tunauona katika mistari mingine ya neno la Mungu. Mtume Paulo aliwashukuru waumini wa Filipi kwa msaada wao. Yeye anaandika.

“Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji…Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu. Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu.” (Wafilipi 4:10-17).

Mtume Paulo anawaeleza Wafilipi kuwa walifanya vema kumsaidia katika shida zake. Kwa ukweli kutokana na mstari huu tunauona ukweli kuwa ni jambo la upendo na la haki kuwa tunapaswa kuwasaidia wale wanaoteseka na kupungukiwa kwa sababu ya ile kazi ya Mungu wanayoifanya kwa niaba yetu. Na mtume Paulo anafurahia kwa sababu anayaona matoleo wanayompelekea au zawadi zile kama ishara ya kukua kwao katika upendo katika Kristo. Na huwezi kulazimisha kukua kwao. Kukua ni matokeo ya uchaguzi tunaoufanya sisi wenyewe kwa hiari mbele ya Mungu! Kutokana na mistari hiyo hapo juu, tunaona Wafilipi walichagua wenyewe kwa hiari yao kumsaidia Paulo kwa ajili ya kazi yake kwa ajili yao na kwa ajili ya Injili. Na utoaji huo ulitokana na upendo wa Mungu ndani ya mioyo yao - wala hamna aliyewalazimisha kufanya hivyo! Pia lilikuwa ni kanisa la Filipi tu ndilo lililomsaidia Paulo kwa jinsi hiyo. Lakini Paulo mwenyewe hakulalaminika, badala yake Paulo anaeleza kuwa yeye hakutamani kile kipawa, bali alifurahi kwa ajili yao kwa sababu kipawa kile ni dalili ya pendo la Mungu mioyoni mwao na Paulo anafurahia kuyaona matunda haya ndani yao.

“Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu.” (mstari 18).

Wakorintho wa kwanza sura ya 9 ni sura nyingine tena ya Biblia ambayo ni muhimu sana katika mafunzo yetu haya. Katika eneo hili mtume Paulo anaeleza kwa ukamilifu kabisa ule ukweli anaougusa anapowaandikia Wafilipi 4. Paulo hakuomba msaada wala fedha anapowandikia Wakorintho. Yeye anasema alifanya kazi kwa mikono yake ili apate kuihubiri Injili kwa uhuru zaidi kwao. (Soma Matendo 20:34; 1 Wakor.4:12; 1 Wathess.2:9; 2 Wathess.3:8). Wengi wa Wakorintho hawakuelewa na jambo hili! Lakini alikazia kuwaeleza kuwa yeye kama mtume alitegemea kuwa angeweza kupata msaada wa fedha kutoka kwao kama ilivyo kwa mitume wengine kama Petro ambao walipata msaada huo (1Wakor 9:1-18). Anawaelezea kwa ufasaha na uwazi kabisa juu ya msingi ya haki ambayo ingemfanya aweze kupata msaada wao kwa kutoa mifano mingi,

“Ni askari gani aendaye vitani wakati wo wote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi?” (m.7).

Kwa kutoa mifano hiyo, hapo anaweka mambo uwazi zaidi kwamba wale walioingia katika kazi ya Mungu wanapaswa kupata msaada wa msingi wa mahitaji yao kwa kazi ile waifanyayo. Kwa maneno mengine, yeye ahubiriye kwa muda wote kikamilifu anapaswa kupokea msaada ili kukidhi mahitaji yake ya maisha ya kila siku kutoka kwa wale anaowatumikia. Na baada ya hapo ananukulu kutoka katika Agano la Kale. Je, hapo ananukuu kuhusu sheria ya fungu la kumi kwa ajili ya makuhani? Hapana! Anataja ng'ombe tena; ananukulu, “kwa maana katika torati ya Musa imeandikwa usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng'ombe? Au yamkini ananena hayo kwa ajili yetu. Naam yaliandikwa kwa ajili yetu.” (m.9,10). Anaendelea kusema, “Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini?” (m.11). Ndipo anathibitisha hayo yote kwa kusema, “Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.” (m.13,14).

Katika mfano huo wa mwisho, mtume Paulo anaelezea tu ukweli ule ule kwa kutumia mfano mwingine kupitia katika Agano la Kale. Huo mfano wa mwisho Paulo hanukulu mstari moja kwa moja kutoka katika Agano la Kale lakini anadhihirisha ukweli kwamba kama vile wale wazifanyao kazi za hekaluni walikula katika vitu vya hekalu (tunasoma hayo katika Kumbu.18:3), vivyo hivyo wale waihubirio Injili wanavyopata riziki kwa hiyo Injili. Hebu sasa tugundue kupitia mstari huo hapo kuwa mtume Paulo hatamki au hataji chochote kile kuhusu kutoa kikumi! Angeweza kufanya hivyo kwa urahisi tu kwa kulinganisha kuwa kama vile Walawi na Makuhani walivyopokea kikumi toka kwa Wasraeli, basi vivyo hivyo na wachungaji na wahubiri wanahusika na kupokea kikumi toka kwa waumini wao! Mtume Paulo angeweza kuagiza hapo juu neno hilo kwa uwazi kabisa! Lakini hakufanya hivyo. Hakufanya hivyo kwa sababu jambo kama hilo (yaani, kuwapa wachungaji fungu la kumi kila wiki/mwezi) halipo kwa matumizi ya Agano Jipya, na wala halimo katika mpango wa Mungu kwa watu wake katika Agano Jipya. Badala yake, mtume anachagua kututolea mfano ambao unatukumbusha kwamba makuhani katika Agano la Kale sawasawa na agizo la Mungu waliweza kula sehemu ya dhabihu zilizotolewa na Waisraeli, lakini agizo hili halihusu jambo la kikumi – lilkuwa agizo tofauti kabisa! Labda pia ni la maana kwamba hapo anaepuka kutumia neno ‘makuhani’ - anasema ‘wale wazifanyao kazi za hekaluni’. Labda alifanya hivi kwa kusudi kwa sababu katika Agano Jipya sisi sote ni makuhani (1Petro 2:5,9).

Nafikiri watumishi wa Mungu mahala pote katika ulimwengu huu wa Biblia wangekaa kimya na kuwaza au hata kutafakari kwa nini jambo kubwa kama hili katika maisha yetu kwa Agano Jipya lipo kimya, ambalo jambo hilo hilo lileta heshima kwa makuhani, kwa Ibrahmu baba yetu mbele ya Melkizedeki. Leo Mungu mwenyewe awe kimya, Biblia iwe kimya, Yesu awe kimya, mitume wawe kimya na wala Agano lenyewe tunalo litumikia sisi, yaani, Agano Jipya lisiseme chochote juu yake? Ni kwa sababu ya mfumo wa Mungu wa pendo lake kwa wakazi wanaolitumikia Agano Jipya ametuondolea kongwa la utumwa, kongwa la Sheria, na makali ya maumivu yalaiyokuwemo ndani ya amatoleo hayo ya kusukumwa. Atupatia njia nyingine “apenda wanaomtolea kwa moyo wa hiari.”

Mifano hiyo yote inathibitisha ukweli mmoja ambao tayari tumekwisha kugundua, ya kwamba ni jambo la haki na la huruma kwa wao wapatao faida za kiroho kupitia huduma ya wale walioacha kazi ili kumtumikia Mungu waweze kusaidiwa riziki zao na mahitaji yao. Lakini kwa upande wa mitume na wahubiri hatuna mfano hata mmoja katika maandiko ambao wanawalazimisha washirika waape pesa, wala hakuna mfano hata mmoja unaowalazimisha waumini kutoa pesa kwa mitume, au wachungaji kama wafanyavyo mitume na wachungaji wa leo. Aina ya mtu mmoja aliwalazimisha washirika kutoa pesa - yaani, “mitume wa uongo watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu maana shetani mwenyewe hujigeuza, awe mfano wa malaika a nuru.” (2 Wakor.11:13,14). Lakini kwa kiasi Wakorintho walifurahia mitume wa uongo kama hao kwani Paulo anasema juu yao, “Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni.” (m.20).

Lakini ingawa mtume Paulo angaliweza kutazamia waumini wa huko Korintho kumsaidia na riziki zake aliikataa haki yake hiyo, na akafanya yote kwa ajili ya faida ya watu aliowapenda. Hapa anatangaza, “Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo…. Lakini mimi sikutumia mambo hayo hata moja. Wala siyaandiki hayo ili iwe hivyo kwangu mimi.” (1 Wakor.9:12,15). Huyo ni mtu wa Mungu twaona hapo hafanyi kitu, hatendi kitu, haandiki kitu ili watu wampe pesa! Anajitoa kwa ajili ya watu wa Mungu na kazi ya Mungu bila kutafuta faida yake mwenyewe. Sikiliza maneno yake ya ajabu na yenye neema na ya upendo kwa watu. “Maana sivitafuti vitu vyenu bali nawatafuta ninyi…” (2 Wakor. 12:4). Sikiliza ushuhuda wake “Sikutamani fedha wala dhahabu wala mavazi ya mtu.” (Mtd 20:30).

Waumini kadhaa wa huko Korintho hawakutambua huduma ya Paulo (1 Wakor.9:1-3; 2 Wakor.10:7-10). Walikuwa wakisema wao kwa wao kuwa, "Paulo akiwapo mwilini ni dhaifu na maneno yake si kitu." Pamoja na maneno hayo, Paulo hakushurutisha wampe pesa kama mtume wakati akihubiri Injili miongoni mwao! Kwa hiyo wengine waliopo huko Koritho walifikiri kuwa Paulo si mtu muhimu kwa sababu wao walimtazama katika sura ya nje - walihukumu hukumu ya macho tu, “Yaangalieni yaliyo mbele ya macho yenu.” Wao waliamini kuwa kama mtu ni mtume basi angewashurutisha kupewa pesa kwa ajili ya huduma yake. Mawazo yao hayakuwa ya kiroho, hivyo Paulo aliwauliza swali hili, “Je! Nilifanya dhambi kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila ujira?” (2 WaKor 11:7). Mtume Paulo anauliza swali hapo kuwa je, alifanya dhambi kwa kutokuwalazimisha kumpatia pesa!? Hapana, kwa vyovyote hajawatendea dhambi yoyote, bali alikuwa anajaribu kuwaonyesha jinsi ambavyo wanakosea katika kufikiri kwao. Na hata siku hizi waumini wengi wanayo mawazo kama hayo ya kukosea kuhusu huduma, wanapenda kuona kama mtu akijiinua na kudai kuwa yeye ni mtume, nabii au muhubiri mkuu, na kama akija na fahari na kuanza kuwasukuma watu ili kutoa pesa “kwa ajili ya kazi ya Mungu” (kama wanavyodai), ndivyo ilivyo kuwa nyakati za Paulo. Kama tulivyosoma, hata yeye mwenyewe mtume Paulo anawaambia, "mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza akiwapiga usoni.” (2 Wakor.11:20). Lakini mtume Paulo anasemaje juu wa mitume wa aina hii? Yeye anasema, “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki.” (2 Wakor.11:13-15). Hili ni neno kubwa na zito kwa wale wote ambao nia zao ni kutengeneza faida kubwa kwa kuwatumia wale wanaowahudumia.

Iko wazi hapa kuwa kutokana na yote hayo tuliyoyaona na kuyajadili, hii haimanishi kuwa eti, kwa kuwa Paulo yeye hakuomba sadaka hizo na wakati mwingine yeye alikataa kupokea msaada wa fedha, basi wale watendao kazi za kiroho za kumtumikia Mungu na watu Wake, kwamba wasipewe msaada kukidhi mahitaji yao ya lazima! Kinyume chake sasa, Biblia inatutia moyo kuwasaidia wale waatendao kazi kubwa kwa niaba yetu kulingana na mahitaji yao wanayoweza kuwa nayo. Na hii sasa ni kwa ajili ya upande wa washirika, kutokana na upendo na haki basi wanapaswa kuwasaidia wao wanaowahudumia katika Bwana. Na kwa upande wa wachunaji na wahubiri wanapaswa kuwahdumia watu wa Mungu kutokana na wito wao, na upendo wa Mungu na Roho ya Kristo. Tuwe tunaoishi sawasawa na pendo la Mungu lililomiminwa ndani ya mioyo yetu na Roho Mtakatifu. Au tunaishi sawasawa na sheria ya Torati iliyoandikwa katika vibao vya mawe? Yatupasa tuelewe tofauti ya mambo haya mawili kama tukipenda kuishi kama Wakristo.

DESTURI YA WAKRISTO/MAKANISA KUWASAIDIA WAUMINI MASIKINI.

Kama nilivyosema, mzigo na desturi wa Wakristo na makanisa katika Agano Jipya ulikuwa kutoa pesa kwa kwa ajili ya washirika MASKINI. Karibu mistari yote ya neno la Mungu iliyomo katika Agano Jipya inayoelezea juu ya taratibu za ukusanyaji wa pesa inaelezea na kufananishwa na ukusanyaji kwa ajili ya washirika walio masikini - Matendo 4:33-35, 6:11:29, 11:29; War.12:13; 15:25,26; Wagal.2:10; 1 Wakor.16:1-3; 2 Wakor.8:1-7; 1 Tim. 5:3,5; Waebr.6:10; Yakobo 1:27; 1 Yoh.3:17. Ina maana, sehemu kubwa ya sadaka (utoaji) za waumini zilitumiwa kuwasaidia washirika maskini. Kama tulivyoona, mistari mingine inahusu msaada kwa ajili ya watumishi wa Mungu.

Ile desturi yetu ya kuchanga pesa jumapili (siku ya kwanza ya juma), je, jambo hili linatokana na nini? Na waumini walitoa pesa zao kwa ajili ya nini katika Agano Jipya? Ebu na tuisome ile desturi iliyoanzishwa na mtume Paulo aliyoianzisha,

“Kwa habari ya ile changizo kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo. Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja; nami nitakapofika nitawatuma kwa nyaraka wale mtakaowachagua, wachukue hisani yenu mpaka Yerusalemu.” (1 Wakor.16:1-3).

Huko Yerusalemu walikuwepo waumini maskini wengi kwa hiyo Paulo aliwasihi na kuwatia moyo waumini wale huko waliokuwa na uwezo kuwasaidia ndugu zao maskini waliopo Yerusalemu. Na hapo Paulo anatoa mipango juu ya namna changizo hilo litakavyofanyika. Basi sasa, kutokana na maneno ya Paulo ni wazi tu kwamba jambo hili la kuchanga pesa kwa ajili ya ndugu maskini ilikuwa jambo la kawaida kati ya makanisani ya Agano Jipya. Kwa Warumi aliwaandikia ifuatavyo,

“Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumu watakatifu maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya watakatifu huko Yerusalemu walio maskini.” (Warumi 15:25,26).

Kwa matendo yake pamoja na mafundisho yake mtume Paulo aliwaonyesha waumini ni baraka kutoa kwa ajili ya wadhaifu na maskini bila kutazamia kupata kitu! “Katika kila jambo nililofanya, nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia WADHAIFU, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘ni baraka zaidi, kutoa kuliko kupokea.’ ” (Matendo 20:35).

“Changieni katika mahitaji ya watakatifu…” (Warumi 12:13). Kutoa pesa kwa ajili ya ndugu maskini ilikuwa jambo la muhimu sana makanisani wakati wa mitume! Petro alipozungumza na Paulo juu ya Injili alimwambia, “Walichotuomba ni kwamba tuendelee KUWAKUMBUKA MASKINI, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.” (Wagalatia 2:10).

Mtume Paulo anawafariji Wakorintho wakue katika utoaji wao kama vile wafanyavyo katika mambo mengine katika maisha yao ya kiKristo, “Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote: Katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa.” (2 Wakor.8:7).

Kutokana na haya yote basi tunaona wazi kuwa: 1. Waumini walianzisha desturi ya kuchangishana pesa kwa ajili ya ndugu zao maskini. 2. Walitoa kwa kadiri ya kufanikiwa kwa kila mtu! Maneno ya mtume Paulo hapo ni wazi kabisa kuwa yeye haweki sheria juu ya kipimo cha utoaji; yeye anaagiza juu ya namna ya kuchanga tu! Mtume Paulo hawakamii waumini wa huko na wazo kulaaniwa wasipotoa!

Kama tukiangalia mistari yote iliyopo hapo juu ihusuyo mafundisho juu ya utoaji, ni wazi kabisa kuwa mzigo wa kwanza waliokuwa nao waumini ni kuwasaidia waumini (ndugu zao) maskini. Kuanzia katika Matendo ya Mitume hadi waraka wa Yohana, ilikuwa ni desturi ya makanisa kuwahurumia ndugu zao maskini.

Hayo yanahusu hususan wajane na yatima katika makanisa, na makanisa ya Agano Jipya walikuwa na mfumo kuwasaidia wajane – Matendo 6:1-6; 1 Tim.5:3,5,9,10; Yakobo 1:27.

SABABU YA KUTOA.

Tunatoa kwa sababu Yesu Kristo alitoa maisha yake kwa ajili yetu na ametuokoa! Tulinunuliwa kwa thamani kubwa sana na sisi si mali yetu bali Yake sasa. Tunatoa kwa sababu hiyo ni tabia ya Mungu, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee…”. Na sisi tumefundishwa kufanya vivyo hivyo alivyo Mungu alivyofanya - “Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.” Na tunafanya hivyo hasa kwa ajili ya waumini maskini, “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?” (1 Yoh.3:16,17). Tunafanya hivyo “kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.” (War.5:5). Utoaji wetu ni sehemu ya upendo wetu kwa Mungu, na kwa watu Wake, na kwa kazi Yake duniani; ni sehemu ya kuabudu kwetu kwa Bwana!

Ni jambo la kuhuzunisha sana tena sana kumwona mchungaji au kiongozi fulani ajifanye kama bwana juu ya watu wa Mungu na ‘kupiga mjeledi’ kwa mafundisho makali yake akisema, “Toe zaka, toe zaka, au utalaaniwa!” – kana kwamba washirika ni watumishi wake! Kiongozi wa namna hiyo anaharibu au kupotosha sura ya Mungu, yaani, tabia ya Mungu machoni pa wasikilizaji, na anaharibu (angalau kwa kiasi) uhusiano kati ya washirika na Mungu. Yampasa mchungaji awe mtumishi wa washirika ni siyo kujiinua kama bwana! “Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. LAKINI HAITAKUWA HIVYO KWENU; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Hiyo ni tabia ya mchungaji kweli kweli. Yampasa mchungaji au kiongozi awakilishe ‘sura’ au ‘mfano’ au ‘chapa’, yaani, tabia ya Yesu Kristo mbele ya watu, machoni pao.

Shida mmoja ni hiyo, viongonzi na wanchungaji wengi kwa lengo lao la kupata faida (pesa) kwa ajili yao wenyewe, au kwa ajili ya madhehebu yao, kila jumapili, walibuni mafundisho makali ili kuwalazimisha washirika kuleta pesa kwao kila wiki! Kwa upande moja wanawatisha washirika kwamba watalaaniwa na Mungu kama wasitoe fungu la kumi (wananukulu hasa Agano la Kale kujaribu kuthibitisha udanganyifu huo), au kwa upande wengine wanawatia moyo kupa pesa kwa kuahidi watapata mengi kwa kurudishwa. (Kwa kawaida wananukulu Malachi 3:10 na Luka 6:38). Mafundisho haya mawili yote ni udanganyifu na dhambi dhidi watu wa Mungu ambao Yesu alikufa kwa ajili yao! Kwa yale ya kwanza yanajaribu kuwalazimisha washirika watoe kutokana na ‘hofu’ na ‘sheria’ badala ya upendo. Kwa yale ya pili yanachochea uchoyo mioyoni mwa waumini. Wachungaji na viongozi wengine wanafundisha, ‘Unaona, kama ukitoa elfu moja, kumbe, utapata laki moja! Panda mbegu!’ Hiyo ni dhambi. Hiyo ni biashara! Wanaharibu imani ya watu wa Mungu!

Sitoi ili nipate!

Inaandikwa “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.” (Luka 6:38).

Hiyo ni uthibitisho wa uaminifu na wema wa Mungu, sio sababu kutoa! Baraka hizi za Mungu ni matokeo ya kutoa kwako – siyo sababu ya kutoa! Ukitoa kwa uchoyo wa kupata, unaharibu thamani ya utoaji wako mbele ya Mungu na pamoja na hayo kwa hakika utakosa baraka zile Bwana Yesu alizozitaja kwenye Luka 6!

Yesu alizidi kufundisha, “Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu.” (Luka 6:35). Kwa mujibu wa Biblia, tunabarikiwa zaidi kupitia kutoa, kuliko kupitia kupokea! “Ni baraka zaidi kutoa kuliko kupokea.” (Matendo 20:35).

Uwe mwangalifu sana! Usidhanie kuwa unaweza kununua au kulipa kwa ajili ya baraka za Mungu! Ikiwa kuna mtu anayejiita mwenyewe kuwa ni mtumishi wa Kristo Yesu, na anataka pesa zako ili akuombee, mtu huyo ni mdanganyifu na hamtumikii Kristo kabisa. Ikiwa umefundishwa kuwa unapaswa kutoa pesa katika matoleo yako iwapo utakuwa umebarikiwa na Mungu katika mkutano, ndipo utakuwa umefundishwa vibaya - mtumishi wa aina hiyo sio tu kuwa anamwakilisha vibaya Mungu, bali anakosa. Ebu sikiliza mstari huu, ili ukweli huu uingie katika moyo wako,

“Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali… moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.” (Matendo 8:21,29)

Wazo ya kwamba tunapaswa kulipia ili kupokea baraka za Mungu, au wazo ya kwamba tunadaiwa na Mungu pale tunapokuwa tumebarikiwa, ni fundisho la uovu. Wazo hili limeimarishwa kwa kiasi kutokana na tamaa za watumishi ambao wanajitumikia wenyewe. Watumishi wanaozurura kule na kule wakitafuta mbinu za kuwaibia waumini mali zao na pesa zao kwa kisingizio kuwa Mungu anazitaka pesa hizo ili wao waweze kubarikiwa. Huo ni uongo wa mchana kweupe. Usinielewe vibaya! Sisi, kama watu wa Mungu, kwa hakika tutayaleta matoleo yetu, lakini tunatoa pesa kwa sababu ya upendo wetu kwa watu wa Mungu ambao wanasumbuka kwa kukosa mahitaji ya lazima, na kwa ajili ya upendo wetu kwa ajili ya kazi ya Mungu; kadhalika na kuwapa watu wengine kwa moyo wa huruma na upendo. Lakini hatutoi kwa moyo wa uchoyo wala ‘kununua’ baraka za Mungu. Ndiyo, Mungu anaweza kutugusa mioyo yetu kwenye mikutano na kutuelekeza kutoa kwenye eneo maalumu lihusulo kazi yake Mungu. Lakini hiyo ni mwitikio wa kile ambacho Mungu anakifanya ndani ya moyo wako kwa wakati huo, ambalo ni jambo la tofauti kabisa na lile la kufanya kitu kwa ulazima au sheria.

Zaidi ya yote, Yesu Kristo alifundisha, “bali wewe utoapo sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume.” (Mathayo 6:3). Utoaji wetu unapaswa uwe kwa wepesi utokanao katika upendo wetu kwa ajili ya Mungu na watu wake na wengine pia. Utoaji wetu usiwe ni mbinu ya kutengeneza faida fulani katika maisha yetu, kama ifanywavyo au kuamuliwa na watumishi wengi kuwa “Panda mbegu”. Mafundisho ya jinsi hii ya kupanda mbegu na mawazo ya aina hiyo ni ya uovu mtupu.

Napenda kumaliza sehemu hiyo kwa kunukuu maneno ya Dr. Frank Philip Seth (anayetoka Dar Es Salaam), ambaye huweka mambo hayo kwa ufasaha mzuri,

“Mafundisho mengi kuhusu UTOAJI wa SADAKA yamekuwa na shida ya kuelemea upande fulani, hivyo kupelekea watu kushindwa kufanya yawapasayo na kuishi kwa hofu, bila kupata baraka zinazostahili katika utoaji wao.

Lengo la msingi kabisa ni KUMCHA Mungu. Mambo mengine yatafuata hapo, kwenye kusudi/lengo la utoaji wako, ila anza na Mungu. Kama lengo sio kumpendeza Mungu, au kutoa kwa kumcha Mungu, fikiri tena kwa habari ya utaoji wako. KANUNI ya msingi ya utoaji wowote ni kutoa kwa MOYO wa kupenda. Ukitoa kwa sababu ya KULAZIMISHWA, angalia tena kusudi la huo utoaji. Jifunze kutoa kwa UKARIMU kwa maana utavuna kwa ukarimu pia.

Sasa najua watu wamefundishwa kutazama baraka, kama ndio kichocheo cha kutoa zaka na sadaka zao. Kumbuka baraka ni matokeo - kichocheo cha kutoa na lengo la MSINGI ni kumcha Bwana Mungu wako. Ukitoa kwa sababu unamwogopa au unamwonea aibu mchungaji wako, hiyo ni shauri yako, ila leo nakupa shauri, toa zaka na sadaka zako kwa sababu unataka KUMCHA Mungu na kumpendeza. Fuata maagizo yake, na ujue kiasi, mahali na muda wa kutoa …sadaka zako. Bila kusahau kwamba Bwana alisema sadaka ni SIRI; “mkono wako wa kushoto usijue nini mkono wa kulia unafanya”.

Nisikilize kwa makini. Sisemi kuwekewa mikono au kuombewa baraka ni vibaya, ila HAKUNA namna mtu atatoa sadaka zake kwa MOYO MBOVU kama wa Kaini, halafu akawekewa mikono, ikamsaidia kupokea baraka, hakuna! Kwa upande wa pili, hakuna mtu atatoa sadaka zake “kwa SIRI”, bila kuwekewa mikono na mtumishi yeyote, ila ametoa sadaka zake kwa MOYO MZURI kama wa Abeli, asipokee baraka zake kwa kipimo cha kujaa, kusukwa-sukwa, na kufurika. Thamani ya sadaka yako ni MOYO wa shukrani, uelekevu na ibada mbele za Mungu wako. Usisahau hata siku moja, baraka za Mungu hazinunuliwi kwa sadaka, ila kwa “moyo wa uelekevu” mbele za Mungu wako.

Sasa, nataka uone kwa undani kidogo habari ya sadaka…, ili usijivune sana utoapo. Kwanza, imekupasa kujua kwamba Mungu hana shida na hiyo pesa yako, ila HALI ya moyo wako utoapo hizo sadaka zako. Angalia tena hapa, “Je! BWANA atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta?...BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.” (Mika 6:6-8). Bwana Yesu akiona shida iliyoko kati ya taratibu za KIDINI, akasema maneno haya, ambayo nabii Mika alisema pia, “Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia” (Mathayo 12:6,7). Yesu anasema, kuna mmoja aliye mkuu zaidi kuliko hekalu lako, naye ni Mungu; na anachotaka kwako sio SADAKA ila REHEMA. Sasa usisahau kwamba Rehema ni “hali ya moyo inayompelekea mtu kutenda au kuenenda kwa namna fulani”; sasa ukiwa na MOYO wa REHEMA, kisha ukatoa sadaka zako, umefanya jambo jema sana. Ukisukumwa kutoa ILI ubarikiwe, jua umepoteza lengo la MSINGI la utoaji wako;…chunguza moyo wako na uhusiano wako na Mungu.” (Dr.F.P.Seth: “Zaka ya Fungu la Kumi”).

Kumbuka, ‘Mungu huuangalia moyo’. Thamani ya utoaji inazingatiwa na hali ya moyo wako.

JE, PESA ZIKUSANYWAZO JUMAPILI KAMA SADAKA ZINAMHUSU NANI?

Pesa zangu nizitoe kwa nani na kwa ajili gani? Hili ni swali muhimu sana na ni la msingi. Ikiwa wewe ni Mkristo, basi bila shaka utakuwa unahudhuria ibada mara kwa mara. Kwa hiyo, ni haki kulisaidia kanisa kwa ajili ya gharama zinazotumika hapo. Kwa mfano gharama kwa ajili ya kulipia umeme au mafuta zinazotumika kanisani hapo n.k. Lakini pia ni haki kumsaidia mtumishi anayetumika hapo kanisani kwa moyo wa uaminifu; kumsaidia ili apate kukutana na mahitaji yake ya muhimu na ya lazima, na sio kumfanya awe tajiri.

Lakini ni uhakika ulio wazi kabisa kuwa halipo fundisho lolote katika Agano Jipya linalosema kuwa makusanyo yote ya sadaka, au hata sehemu yoyote ya pesa hizo kwamba eti, zinamhusu mchungaji au kiongozi wa kanisa. Lakini tafadhali usinielewe vibaya! Kama nilivyokwisha kuonyesha katika mistari niliyoitaja hap juu, nami nitaendelea kuitaja hapo chini - ni wazi kuwa Wakristo wanapaswa kuwasaidia wale wanaowatumikia kwa kazi. Lakini ni makosa kwa wachungaji na viongozi wengine wao kujifanya kana kwamba ni wakurugenzi huko makanisani na kuwekeza mifumo kwa washirika wao ambayo ipo kinyume kabisa na neno la Mungu. Zaidi ya hayo yote, waumini katika Agano Jipya walijua wazi kuwa wanamtolea nani na nini wakitoacho. Mifumo ya utoaji ambayo waumini wanatoa pesa kisha wao hawaambiwi kuwa pesa hizo zinaenda wapi ni makosa makubwa na ni kinyume cha haki mbele za Mungu. Hata katika mifumo tu ya dunia watu hutambua jambo hili - makampuni, mashirika au hata serikali, wao huchapisha mahesabu yao yanayoonyesha ni kiasi gani cha pesa kilichotumika.

Sasa je, kanisa linapaswa kutenda kinyume na haki na kutokuwa na uwazi kuliko hata wafanyavyo wasioamini? Je, viongozi wanasumbuliwa na jinsi wanavyozitumia pesa hizo kiasi kwamba sasa wanajitafutia njia za kuwaficha ukweli wa taarifa ya makusanyo ya pesa hizo wale wanaozitoa pesa hizo? Hii ni inaingizwa ni makosa na ni mchezo usio na haki hata kidogo.

Kama tulivyoona, waumini walitoa pesa kuwasaidia waumini maskini na watumishi wa Mungu mbalimbali. Lakini lipo fundisho la uongo lisemalo kwamba lazima ulete sadaka (utoaji) zako ZOTE kanisani ambapo unaabudu (kwa ajili ya huduma). Hiyo ni ubuni wa kibinadamu kabisa! Fundisho hili halitokani na Biblia. Kama hili ni kweli, hatuwezi kuufuata mfano wa Msamaria mwema, na mithali hiyo ya Yesu haina maana sasa! Aidha, Yesu alitufundisha, “Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.” (Mt.5:42). Fundisho hili halina msingi katika neno la Mungu. Fundisho hili linafanya kanisa liwe kama biashara na msukumo wa fundisho hili inaonekana kuwa ni uchoyo tu. Tunajua kwamba waumini huko Jerusalemu mwanzoni waliileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume, lakini hiyo ilikuwa tendo la pekee kabisa na haliwakilishi utaratibu ambao waumini na makanisa waliufuata baadaye, kama tayari tumeshaona! Ulikuwa mfano mmoja wa utoaji tu!

Watu wanajaribu kuhalisisha fundisho hili kwa kudai Malaki 3:10 inathibitisha wazo hili lao! Mara moja tunatambua dai lao halina msingi katika Agano Jipya kwani wanakimbilia Agano la Kale ili kujaribu kuthibitisha wazo lao! Kama tulivyoona, kwa ujumla ni jambo la kawaida kuleta sadaka zetu kanisani – hiyo ni wazi, hamna hoja – lakni ni wapi Yesu au mitume wafundishapo kwamba lazima ulete sadaka zako zote kanisani unapoabudu? Hamna fundisho hili katika Biblia. Njia mmoja ni kupotosha maana ya Malaki 3:10, na wao wanafanya hivyo. Mstari huo unatufundisha mambo yale tayari tuliyoyajifunza katika makala hiyo, yaani, kama sehemu ya kuabudu kwetu kwa Mungu tunapaswa kuwasaidia watumishi wa Mungu na washirika maskini kupitia sadaka zetu kutokana na upendo wa Mungu ndani ya mioyo yetu. Hiyo tu.

‘Zaka’ iliyotajwa katika Malaki 3:10 haihusu ‘walawi’ tu (wao waliohudumia hekaluni)! Ilihusu ‘mgeni’, ‘wajane’ na ‘yatima’ pia! Tena hapo napenda kunukuu kutoka mafundisho ya Dr.F.P.Seth yanayohusu sehemu hiyo na sehemu ifuatayo,

“Pamoja na sababu BINAFSI za utoaji, ambazo msingi wake uko katika KUMCHA Mungu na KUMWABUDU, kuna mambo ya msingi ya kuangalia hapa. Kwanza, imekupasa kujua kwamba mfumo wa sadaka uliwekwa ili kuwepo na CHAKULA katika nyumba ya Mungu, au katikati ya watu wa Mungu. Angalia hapa, “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu”. Hili neno “ghalani” limekuwa na tafsiri kwamba (ghala ni ‘kanisani’ ambapo mtu anaabudu). Lakini nakwambia leo, hili neno “ghalani” ni zaidi ya kanisani kwako (Malaki 3:10). Sasa tafsiri ya Chakula ni Chakula, yaani hiki chakula cha kujenga mwili na sio cha roho (Neno). Hata kama itakuwa sadaka ya pesa, lengo ni kiwemo “chakula” na sio tafsiri ya “Neno” au “mahubiri”.

Watu wengi wamejaribu kubadili hili neno “chakula”, na kusema ni “mahubiri”… Neno la Mungu ni chakula, ila hapa kwenye Malaki, hasemi habari ya mahubiri (Neno), anasema habari ya chakula cha mwilini kabisa (ugali, mchele, nyama, nk.). Lengo la Mungu kusema watu “walete chakula (zaka)” ni hili hapa, “Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba”. (Kumb. 14:28,29). Hapo hakuna kitu kama mahubiri, ni chakula kabisa cha damu na nyama. Je! Masikini, wajane, na yatima wako wapi wakila na kushiba katikati yetu?

Angalia tena, Mungu aliweka mfumo wa kutoa sadaka kwa ajili ya watu wasio na KIPATO au URITHI katika jamii husika. Ndipo tunaona Walawi … wanatajwa hapa, WAKICHANGANYWA na mgeni, yatima, wajane, nk., yaani watu wenye UHITAJI katika jamii. Hawa wote hawakuwa na chakula cha kutosha, kwa sababu hawakuwa na urithi (Mlawi na mgeni) AU mtu waliyemtegemea amekufa (yatima na mjane), na kupitia ZAKA, wanapaswa wale na kushiba. Sasa ukiangalia “ghala” kwenye kitabu cha Kumbukumbu la Torati, utaona unaagizwa “uliweke ndani ya malango yako”. Sasa sisemi kupeleka kanisani kwako ni makosa, ila SIO lazima ufanye hivyo… Ukitaka kuona shida katika mafundisho ya utoaji, jiulize maswali yafuatayo, Je! Mtumishi fulani akipewa ZAKA au SADAKA na kondoo asiye wa kundi lake, anakataa na kumwagiza huyo kondoo apeleke kwa mchungaji wake? Kama anapokea kutoka kwa kondoo wasio wa kundi lake, kwa nini anazuia kondoo wake wasiongozwe na Mungu wao kutoa sadaka zao mahali pengine? Jiulize tena swali, Je! Mungu akisema “kuanzia sasa, wanadamu wote wasitoe tena sadaka za fedha na vitu”, Je! Hao watumishi wataendelea na huduma kwa moyo ule ule? Jibu mwenyewe maswali haya kwa nafsi yako, wala usimtazame mwingine.

Umewahi kufikiri watumishi wanasema “leteni zaka yote na sadaka zenu kwa sababu mnakula kiroho hapa kanisani”, na ghafla! Mungu anabadilisha utaratibu na kusema, “wapeni watumishi wangu vitu vya rohoni tu, yaani faraja na maombi, ila msiwape pesa na vitu”. Fikiria mwenyewe ni huduma ngapi zingesimama. Halafu ujiulize kwa nini zimesimama? Je! Hawana chakula au hawana faida? Ndipo utagundua tofauti kati ya mchungaji wa halisi na mchungaji wa mshahara.

Hebu piga picha uone jinsi wajane, yatima na masikini WANAJIKAMUA kupeleka zaka zao kanisani kwa sababu “wametishiwa maisha” kwamba watalaaniwa wasipofanya hivyo. Kweli imewapasa watu WOTE kutoa zaka na sadaka zao, ila kwa KUMCHA Bwana, na kwa MOYO wa KUPENDA kutoa, sio kwa HOFU na VITISHO. Kama mtumishi angechagua vyema, angewalazimisha watu kwa ukali ZAIDI wasitende dhambi, kuliko kuwalazimisha watu kutoa zaka na sadaka zao wakiwa dhambini; mtumishi wa namna hii angekuwa upande wa Bwana na sio wake mwenyewe.

Soma maandiko na uongozwe na Roho Mtakatifu kujua mambo haya, kwa maana iko baraka katika KUWATUNZA wajane (hasa), masikini, yatima na wahitaji wengine, bila kuwasahau watumishi wa Mungu aliye hai, ili kazi ya huduma iendelee na mwili wa Kristo ujengwe.” (Dr.F.P.Seth: “Zaka ya Fungu la Kumi”).

Nilinukuu haya siyo ili tufuate sheria ya Agano la Kale, lakini Dr. Seth aliweka wazi kutokana na Malaki 3, na mstari 10 mwenyewe, kuwa hata Agano la Kale linathibitisha mambo tuliyoyaona kwenye Agano Jipya na niliyoyaandika hapo, yaani, sadaka ya watu zilitumiwa kwa ajili ya watu maskini na kwa ajili ya watumishi wa Mungu. Zaidi ya hayo, wale wanaotumia Malachi 3:10 ili kufundisha kuwa lazima ulete utoaji wako wote kanisani mwako, wanakosa sana! Ni jambo la uchoyo tu.

Aidha, Kwa ujumla, siyo shughuli ya mwingine ajue utoalo - siyo shughuli ya ndugu yako, wala kanisa lako, wala mchungaji wako ajue utoalo! Haimhusu mtu yeyote yule kujua ni kiasi gani umeweka ndani ya kapu la sadaka au umeweka kwa ajili ya nini, jambo hili ni kati yako wewe na Mungu, basi. Wale, wanaokulazimisha kuwajulisha viongozi wa kanisa kiasi unalotoa wanafanya dhambi, “Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume.” (Mathayo 6:3).

------------------------------

‘Nyumba ya Mungu’, Ukuhani na ‘Madhabahu’.

Wengine wanafundisha lazima ulete pesa yako YOTE (ya zaka au kadhalika) mahali ambapo washirika wanakusanyika jumapili kwa sababu madhabahu yapo pale pale tu. Hiyo ni kosa kubwa sana. Kwa ajili ya upungufu wa nafasi, nitanukuu kwa kiasi kidogo kutoka makala yangu iitwayo “‘Nyumba’ ya Mungu na ‘Madhabahu’ ni nini?” Lakini unaweza kusoma makala nzima kupita link hiyo: https://somabiblia.com/nyumba-ya-mungu-ni-nini/ Kwa hiyo, haya kwa ufupi:

“Kama kuna mtu yeyote atasema kuwa jengo au chumba ambacho Wakristo hukutanika siku za jumapili kuwa hiyo ni 'nyumba ya Mungu' au akisema ‘Karibuni kwenye nyumba ya Mungu,’ basi watu hao watakuwa wanaupotosha ukweli mkuu wa Agano Jipya. Ni makosa na watakuwa wanawafundisha watu wa Mungu kimakosa - wanawafanya wafikiri kuwa ukweli huu wenye nguvu za kiroho unahusu tu mambo ya nje. Kama vile matofali na chokaa. Sisi (watu wa Mungu) tu kanisa. Sisi ni hekalu la Mungu kiroho (Waefeso 1:22,23; 2:21,22). Mahali pale wanapokutanika watu wa Mungu hapo ndipo kanisa la Mungu lilipo – hata kama mahali hapo ni chini ya mti! Nyumba ya Mungu ni kanisa, na kanisa ni watu wa Mungu (1 Timotheo 3:15).

Hakuna tena mwendelezo wa kuhani wala ukuhani kati yetu sisi na Mungu - kwa sababu sisi tumefanywa kuwa ukuhani mtakatifu, ukuhani wa kifalme (1 Petro 2:5-9), na Yesu ndiye kuhani wetu mkuu (Waebr4:14). Na yeye pekee ndiye mpatanishi kati ya mwanadamu na Mungu. (1 Timotheo 2:5). Kwa hapa duniani sisi ambao ni watu wa Mungu, tu hekalu la Mungu. Kupitia Yesu Kristo tunayo nafasi ya kuingia katika uwepo wa Mungu, katika patakatifu pa patakatifu mbinguni (Waebr. 4:16,10:19).

Kama mtu yeyote yule kudai kuwa bado ipo madhabahu hapa duniani ambayo inawapasa Wakristo kuiendea, huo ni udanganyifu kwa ujumla wake. Kusema au kudai kuwa kuna aina fulani ya madhabahu ya kidunia inayoonekana ambapo Wakristo wanakutana pamoja huko ni kulikataa Agano Jipya. Ye yote asemaye lazima ulete pesa yako YOTE (ya zaka au kadhalika) mahali ambapo washirika wanakusanyika jumapili kwa sababu madhabahu yapo pale pale tu, anakosa sana. Anajaribu kufanya kanisa liwe kama biashara! Hamna mafundisho hayo katika kanisa la Bwana, katika Agano Jipya. Usinelewe vibaya, kwa ujumla ni jambo la kawaida kuleta pesa ya sadaka yetu ‘kanisani’, hata hivyo hamna fundisho kuwa lazima utoe pesa yako yote kwa kanisa. Wazo hili inakaribia ushirikina. Upendo wa Mungu mioyoni mwenu utatuongoza kutoa pesa yetu kwa ajili ya mahitaji aina ya mbalimbali.”

Ufupisho

Tumeuona utoaji wa waumini mara nyingi katika kanisa la kwanza katika Agano jipya ukilenga katika kuwasaidia waumini ambao ni masikini. Sio kuwafanya wawe wavivu, la, bali ni kwa sababu wao ni masikini halisia. Biblia inalionyesha jambo hili kwa uwazi sana, na utoaji wa kuwasaidia watumishi wengine wanaoteseka ni msisitizo wa wazi ulioainishwa katika Agano Jipya – na katika Agano la Kale pia. Kama kanisa lako linahusika na utaratibu kama huu, basi hata wewe unaweza kusaidia kwa kuchangia kwa ajili ya mambo kama haya. Lakini hamna mafundisho kuwa utoaji wako wote ni lazima uende kwenye kanisa lako lile tu unalosali? Kwa hakika kabisa sio hivyo! Kama unawajua Wakristo maskini – hasa yatima na wajane - au hata mtumishi mwaminifu anateseka mahala fulani katika huduma kwa mahitaji ya lazima, kwa vyovyote unaweza kuwasaidia watu hao; au kuisaidia huduma ambayo inahusika na kusaidia watu masikini katika kuwapatia chakula, nguo, Bibilia n.k. Sababu kuu inayoyafanya makanisa haya yadai kuwa matoleo yako yote ni lazima uyatoe hapohapo unapoabudu tu au ni lazima matoleo hayo yapitie kwao, ni hii hapa - wakuu wa hapo wanazitamani pesa zako! Je, ipo sababu nyingine! Je, Msamaria mwema awezaje kumsaidia mtu anayeteseka iwapo ataambiwa, “Oh, samahani sana ndugu, siwezi kukupa msaada huu kwa sababu matoleo yangu kwanza lazima nitoe kanisani kwangu ninakoabudu au yapitie kwa kiongozi wangu kanisani.” Je, Msamaria huyo atakuwa ameokoa hali ya ndugu ambaye anamwona anateska kwa kupungukiwa na mahitaji ya lazima? Lakini uovu huu ndio unaofundishwa makanisani, na wengi wanaridhia fundisho hilo!

UTARATIBU WA KUTOA

Tunachokionyesha ndani ya makala hii, ni kwamba kukuelezea kuwa haikuwepo sheria kwa Wakristo kwa ajili ya utoaji katika kanisa la Agano Jipya, na wala hakukuelekezwa ni kiasi gani tunapaswa kukitoa. Kwa hiyo, hata sasa na mimi sitengenezi sheria yoyote kwa ajili yako hapa, lakini hebu niseme hivi: Mtu anaweza kusoma makala hii niliyoiandika na akaamini, na bado yeye akapenda kupanga kutoa mara kwa mara na sio kuwa mvivu katika kutoa kwake - hataki kutokujali jambo la utoaji - kwa hiyo mtu kama huyo anaweza kupanga kiwango fulani kila wiki au kila mwezi, kama msingi wake kila wiki au mwezi, lakini pia akatoa mara nyingine kadiri mahitaji yanavyozidi kujitokeza au kadiri Mungu anavyomfanikisha. Hakuna tatizo lolote katika jambo kama hili. Hii inatokana na kuitunza kanuni tuliyoisoma, ambayo ni kwamba kila mmoja alitoa kadiri alivyoamua moyoni mwake, kulingana na uwezo wake na kadiri Mungu alivyomfanikisha. Lakini hii inahusiana na mahusiano ya muumini yule na Mungu katika maisha yake binafsi. Haihusiki na kanuni yoyote ambayo mtu yoyote anaweza kuitengeneza ili kuwalazimisha watu kutoa kanisani. Ule utoaji ni uamuzi wa mtu mwenyewe na kama nilivyokwisha kusema kuwa makala hii imeandikwa ile kurekebisha matumizi mabaya ya utoaji (upotoshwaji wa utoaji makanisani) yanayofanywa kwa upande wa viongozi na wachungaji wengi. Hapa sitengenezi sheria mpya, bali naonyesha kupitia mistari ya neno la Mungu misingi inayowafanya watu watoe.

Labda utashangaa juu ya maneno hayo, lakini kama nilivyosema, lengo langu siyo kukuambia wala kukuagiza utoe kiasi hiki au kiasi kile katika utoaji wako, ila kuondoa kila nafasi, kila hoja na kila hila ambazo viongozi mbalmabli wanazozitumia ili kukulazimisha - kwa kukutisha na kwa kupotosha neno la Mungu – kutoa pesa kanisani kadiri ya maagizo yao; badala yake, tutoe kwa moyo mnyofu sawasawa na neno la Mungu.

MISTARI INAYOITUMIWA NA WATU KUUNGA MKONO UTOAJI WA KIKUMI.

MALAKI 3

Wachungaji na watumishi, pamoja na viongozi wanaowatisha watu kwa laana, au wanaojaribu kuwashawishi watu waweze kutoa pesa kwa kuwaahidi kuwa Mungu atawarudishia pesa hizo mara mia zaidi, watu hao wanapinga mafundisho ya Kristo Yesu mwenyewe. Kuna eneo moja tu katika Agano la Kale mahala ambapo panakemea kuhusiana na utoaji wa kikumi (Malaki 3:8-10). Kukemea huko kulikuja moja kwa moja kutoka kwa Mungu kupitia mtumishi wake Malaki. Kama unasoma kitabu hiki na muktadha wake utaona kuwa Mungu anawakemea Waisraeli kutokana na ibada zao za sanamu, na kwa kumpa Mungu mgongo wao. Alama moja ya uasi wao ilikuwa walizidharau matoleo ya Mungu, na kwamba anachokitafuta Mungu hapo ni kuwataka Waisraeli waache dhambi zao na kumrudia Bwana, ndipo watakapomheshimu Yeye kwa kutoa kilicho cha haki - na hiyo ingekuwa ni ishara kuwa Israel wamerejesha mioyo yao kwake Mungu. Kimsingi hapo Mungu anaelezea hali ya mioyo yao. Ebu sikiliza kile ambacho Mungu anakisema kwa IsraelI katika Malaki 1:10,

“Sina furaha kwenu, asema Bwana wa majeshi, wala sitakubali dhabihu yo yote mikononi mwenu.”

Unaona hapo kuwa matoleo au sadaka zetu tunazomtolea Mungu hazina maana yoyote mbele zake Mungu mpaka pale mioyo yetu iwe imemrudia yeye au ipo sawa mbele yake. Unaweza kusoma kitu hicho hicho katika Malaki 2:12-13. Mungu anasisitiza jambo hilo kwenye Agano la Kale lote kama ilivyo katika Isaya 1:11. “Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana.” Na tena, kupitia Amosi Mungu anasistiza kwamba zaka na sadaka hazina maana wakati tunapofuata dhambi, “Njoni Betheli, mkakose; njoni Gilgali, mkaongeze makosa; kaleteni dhabihu zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu.” (Amosi 4:4). Tukiifuata dhambi kama Waisraeli walivyofanya wakati wa Amosi, hata zaka yetu ni dhambi – kwa sababu ni jambo la unafiki na udanganyifu.

Sadaka ya Abeli ilikubaliwa na Mungu, lakini sadaka ya Kaaini ilikataliwa, na hiyo ilitoka na hali ya moyo wake. Katika kitabu cha Malaki nabii yule anaelezea juu ya hali ya moyo wa Israel, na Mungu anawaambia watu wake kuleta sadaka ya kweli, hii ni kutoka moyoni ambako kuna amwabudu Yeye kwamba iwe ni ishara kwamba wamemrudia Yeye kutoka kwenye dhambi yao na kuabudu kwao sanamu zao.

Hivyo basi wachungaji na watumishi wengi mara nyingi huwaonya na kuwakemea waumini wao ili kuwafanya waogope na waanze kutoa, jambo ambalo Agano Jipya linafundisha wazi kuwa utoaji usiwe ni wa kulazimishwa. Watu hawa wanaangalia mambo kwa nje katika kutoa, badala ya kuangalia hali ya moyo ndiyo inayoleta thamani katika kutoa kwao. Lakini kwa vyovyote watu hao hufanya hivyo kwa sababu hawafurahishwi na hali ya kiroho ya wasikilizaji wao, bali wao hufanya kila njia ili kuvuna pesa nyingi kadiri wanavyoweza kutoka kwa waumini wao. Huu ni ukatili mkubwa wa kiroho wanaotendewa watoto wa Mungu katika kanisa la leo. Bila shaka, tuliyoyasoma katika Agano la Kale hapo juu kuhusu Israel yanatuonyesha kwa wazi kuwa lengo la Mungu ni mioyo ya uasi ya watu Wake ibadilishwe kwanza, na utoaji safi ikafuata kama matokeo ya mabadaliko hayo! Ni jambo tupu na la udanganyifu kukosa katika utaratibu huu, yaani, kuwalazimisha watu wa Mungu watoe pesa na kumbe, kwa ghafla sasa watu hao ni watu wa kiroho kwa ajili ya utoaji huo! Lakini wachungaji wengi wanafanya vivyo hivyo.

Kumbuka, ‘Mungu huuangalia moyo’. Thamani ya utoaji inazingatiwa na hali ya moyo wako.

-------------------------------

Baadhi ya watu hufikiri kuwa Waebrania 7 inatufundisha sisi kwamba tunapaswa kutoa vikumi. Katika sura hiyo mwandishi anatuonyesha kuwa Ibrahimu alitoa kikumi chake kwa Melkizedeki, kwa namna moja hata kabila la Lawi lilitoa kikumi kwa Ibrahimu. Hata hivyo ukiangalia kwa umakini sura hiyo, hakuna fundisho lolote linaloonyesha kuwa Wakristo wanapaswa kutoa kikumi. Eneo hilo mwandishi anawaonyesha wasomaji wake wa kiyahudi (wakati ule) kwamba waelewe kuwa Yesu Kristo ni mkubwa kuliko Ibrahimu. Hiyo tu! Ibrahimu alitoa kikumi chake kwa yeye ambaye alikuwa hana mwanzo wala mwisho wa siku zake! Katika ujumla wake kitabu chote cha Waebrania kiliandikwa ili kuonyesha kuwa Yesu, Mwana wa Mungu, ni mkubwa kuliko malaika, mkubwa kuliko Musa, mkubwa kuliko Ibrahimu na ni mkuu kuliko ukuhani wa Walawi.

Zaidi ya hayo yote, hakuna popote katika Agano Jipya ambapo panafundisha kuwa wachungaji wanafananishwa na makuhani wa Agano la Kale na kwa hiyo watu wa Mungu watoe kikumi cha mapato yao kwa mchungani wao! Kuna mpatanishi mmoja tu kati ya Mungu na wanadamu naye ni YESU KRISTO (1Tim 2:5). Hatunaye kuhani yeyote hapa duniani ambaye anaweza kusimama kama mpatanishi wetu kwa Mungu isipokuwa Yesu Kristo pekee basi! Je, hawajasoma katika Biblia yao kuwa sisi watakatifu wa Mungu ya kwamba sasa wote ni makuhani! Sisi ni “ukuhani mtakatifu, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, mzao mteule watu wa miliki yake Mungu”. (1Petro 2:5,9). Inapaswa ieleweke wazi kuwa heshima hii ya kikuhani haiwaendei wachungaji tu na viongozi fulani fulani wa dini zao. Hapana. Heshima hii Mungu ameiwekeza kwa kila amwaminiye Yesu! Na huu ndio wema wa Mungu wetu leo katika Agano Jipya.

Iwapo baadhi watapinga kuwa utoaji wa kikumi alioufanya Ibrahimu ulifanyika kabla ya ujio wa sheria ya Mus