sura ya pili - web viewdata ilikusanywa katika jamii ya wagogo wanaoishi kata za kikuyu,...
TRANSCRIPT
SURA YA PILI
MAPITIO YA VITABU NA MACHAPISHO
2.1 Utangulizi
Sura hii itajadili marejeo ya vitabu na machapisho yanayohusiana na mada ya utafiti huu. Itaonesha
mtazamo wa watalaam mbalimbali ulimwenguni kuhusu visasili. Kwa kufanya hivyo maana na
fasili mbalimbali za visasili zitatolewa kama zilivyotolewa na watalaam hao. Sehemu ya kwanza
ya sura hii ni utangulizi, inafuatiwa na sehemu ya pili, ambayo ni mapitio ya vitabu na machapisho
na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
2.2 Mapitio ya Vitabu na Machapisho
Jamii zinazopatikana Afrika, kama jamii nyingine duniani, zina mila na amali zake. Mojawapo ya
amali hizo ni fasihi. Fasihi ya Kiswahili, au tuseme ya Kiafrika, kwa ujumla imegawanyika katika
makundi makubwa mawili, ambayo ni fasihi simulizi na fasihi andishi. Makundi haya yote mawili
ya fasihi yamekuwa na athari kubwa katika maisha ya Watanzania na Waafrika kwa ujumla wake.
Hivyo basi, fasihi ni chombo muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Ni chombo kinachowezesha
jamii kujua ilipotoka, ilipo na inakokwenda. Jamii isiyokuwa na fasihi ni jamii ambayo
haijakamilika. Fasihi ya Kigogo kama ile ya Kiswahili imegawanyika katika sehemu mbili vile
vile, ambazo ni fasihi simulizi na fasihi andishi. Makundi haya mawili ya fasihi kila kundi
limegawanyika tena katika vipengele vingine vidogo vidogo vinavyoitwa tanzu. Fasihi simulizi ya
Kigogo ni pana, imepevuka na ina idadi kubwa ya tanzu. Hata hivyo hakuna uchunguzi mwingi na
wa kina kuhusu fasihi simulizi. Mulokozi (1983) katika makala yake ya “Utafiti wa Fasihi
Simulizi” anaonesha umuhimu wa kufanya utafiti wa fasihi simulizi anasema:
Tukizingatia maelezo yetu yaliyotangulia kuhusu uhusiano wa fasihi simulizi na maendeleo na migogoro ya kijamii na jinsi utafiti wowote ule ulivyo chombo muhimu cha kiitikadi cha tabaka linalotawala au linalotawaliwa ni wazi kuwa haja ya kufanya utafiti wa fasihi simulizi bado ipo (Mulokozi 1983):
Visasili ni moja ya tanzu kongwe za fasihi simulizi, imekuwapo toka awali kabla ya fasihi andishi.
Utafiti katika visasili umetupa baadhi ya majibu ya maswali mengi yaliyopo kuhusu visasili na
fasihi simulizi kwa ujumla. Licha ya nadharia mbalimbali za watu mbalimbali zilizopo hata sasa,
bado historia ya visasili haijaandikwa vya kutosha. Kutokuwa na utafiti wa kutosha wa visasili
kumesababisha upungufu wa data kuhusu visasili na hivyo kuwa na mapengo mengi kuhusu
visasili na fasihi simulizi kwa ujumla.
Hatuwezi kuukataa ukweli kwamba tanzu nyingi za fasihi andishi zimetokana na visasili na tanzu
nyingine za fasihi simulizi. Hivyo kuna uwiano mkubwa kati ya fasihi andishi na visasili na tanzu
nyingine za fasihi simulizi, kwa ujumla. Wataalamu na wanazuoni mbalimbali kutoka sehemu
mbalimbali ulimwenguni wamezungumzia kwa undani utanzu wa visasili ambao ni utanzu
mojawapo kati ya tanzu nyingi za fasihi simulizi ya Kiswahili. Mitazamo yao inatofautiana kutoka
mtaalamu mmoja hadi mwingine. Tuone maoni ya wataalamu na wanazuoni mbalimbali kuhusu
visasili. Finnegan (1970:361) anafafanua visasili kuwa ni:
Masimulizi ambayo yanaposimuliwa katika jamii yanaaminiwa kuwa ni mambo ya kweli yaliyotokea zamani. Ni masimulizi ambayo yanakubalika kama imani ya dini na yanafundishwa ili yaaminike katika jamii, na ni masimulizi ambayo yana nguvu za ziada zisizo za kawaida hivyo hutumika kama jawabu kwa maswali magumu na mashaka katika jamii.(Tafsiri yangu)
Anaeleza kuwa visasili vinafungamana na imani katika dini na miviga. Wahusika wake wakuu ni
pamoja na wanyama, miungu na mashujaa wa kiutamaduni ambao matendo yao ya kishujaa
yalijulikana kwenye ulimwengu wa zamani ambao ulikuwa tofauti sana na ulimwengu wa sasa, au
katika ulimwengu mwingine kama angani au chini ya ardhi. Hata hivyo, Finnegan anaeleza kuwa
visasili ni hadithi zinazohusu zaidi wanyama. Ametoa mifano ya hadithi kama hadithi ya “Mwewe
na Kuku”, “Fisi na Sungura” Pia anatoa mifano ya hadithi chache zinazohusu watu kama “Huwezi
Kumsaidia Mtu Asiye na Bahati”.
Finnegan (ameshatajwa), anaona kuwa kuelezea visasili ni vigumu maana vinachukua karibu aina
zote za hadithi zinazohusu wanyama na binadamu. Na hii ndiyo maana baadhi ya wanafasihi
simulizi hawatofautishi kati ya visasili kama utanzu wa fasihi simulizi na tanzu nyingine hasa
ngano na visasuli. Wataalamu hawa wameathiriwa na mtazamo wa Finnegan.
Wanafasihi wengine wana maoni na mtazamo tofauti na ule wa Finnegan. Hawakubaliani na
mawazo kwamba aina zote za hadithi zinazohusu wanyama na binadamu ni visasili. Wao wanaona
kuwa kuna tofauti kubwa kati ya visasili na hadithi nyingine kama ngano. Knappert (1977:11)
anatoa maana ya visasili, anasema:
Visasili vinajumuisha masimulizi ya vitendo vya miungu na mizimu ambayo katika hadithi huaminika kuwa ni kweli. (Tafsiri yangu).
Knappert akiwasilisha mawazo tofauti, anahusisha visasili na matendo ya miungu na mizimu wa
kale. Miungu na mizimu wanapewa nafasi ya pekee katika visasili kwa mujibu wa Knappert.
Tofauti na hadithi za fisi na sungura au kuku na mwewe, masimulizi hayo ya matendo ya miungu
na mizimu yanaaminika kuwa ni mambo ya kweli yaliyotokea zamani. Fasili nyingine ya visasili
tunaipata toka kwenye The Longman Encyclopedia (1989) ambayo inaeleza kuwa,
Visasili ni mambo ya kidini yanayoaminika kuwa ni kweli, yanayohusu namna ulimwengu unavyotokea na kuwa kama ulivyo, ulimwengu na nguvu za asili.
Inaendelea kueleza kuwa, visasili ni hadithi za asili zilizotokea na kusimuliwa zamani na hadithi
hizo zinaelezea zaidi kuwapo kwa nguvu za asili. Visasili vinaelezea kuumbwa kwa ulimwengu na
watu waliomo na mabadiliko ya jamii kwa ujumla.
Rettova (2007:126) ameeleza maana ya visasili, anasema:
Visasili vya asili ni maelezo kuhusu asili ya kifo, asili ya mwanadamu, hasa mtu mweusi, kutokana na mchanganyiko wa utaifa (rangi) kusini mwa Afrika.
Rettova hahusishi kabisa visasili na wanyama au vitu isipokuwa mwanadamu. Isitoshe
anatofautisha kabisa kati ya visasili na ngano, kwamba, visasili ni historia ya taifa fulani wakati
ngano ni hadithi zinazosimuliwa watoto wakati wa mapumziko. Ngano mara nyingi zinasimuliwa
na nyanya au babu na kwamba mbali na kuburudisha watoto, pia zinatoa maarifa kuhusu vyanzo
vya magonjwa, zinaelezea kuhusu maumbile ya wanyama mbalimbali na mahusiano yao, na pia
hufunza maadili kwa watoto. Visasili vinaeleza huhusu asili ya kifo au mwanzo wa binadamu.
Naye Gould (1964:450) anatoa fasili ya visasili inayokaribiana na ile aliyotoa Materu (1989) na
Soyinka (1979) lakini yeye ameongeza wazo la maisha na maana ya ulimwengu na watu,
anasema:-
Visasili ni masimulizi yanayohusu miungu, maisha na maana ya ulimwengu na watu. Katika upande wa siasa na mazingira ya jamii inamaanisha kwamba ni jumla ya mambo yote ya dunia yanayochukuliwa, na watu wanavyothaminiwa.
Hapa tunaona Gould anahusisha visasili na suala zima la siasa tofauti na wanafasihi wengine
ambao hawajagusia kabisa suala la siasa. Isitoshe, anaongelea kuhusu suala zima la mazingira,
yaani jumla ya mambo yote yanayomzunguka mwanadamu. Fasili hii
ni pana zaidi ukilinganisha na nyingine, hata hivyo suala la miungu na mizimu bado limepewa
nafasi ya pekee katika fasili hii.
Balisidya (Materu), (1989) anaona kuwa miungu na binadamu ni wahusika kati ya wahusika
wengi wa aina mbalimbali katika visasili. Yeye anaongeza kitu ambacho Knappert
(ameshatajwa) hakukisema, kwamba visasili husimuliwa juu ya matokeo ya kiada na hueleza
miviga na imani za dini.
Naye Mulokozi (1996:56), mbali na kutoa fasili ya visasili ametoa aina tatu za visasili. Anasema,
Visasili ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na mwenendo wake, kuhusu asili yao wenyewe, na maana na shabaha ya maisha yao. Mara nyingi hadithi hizi huaminika kuwa ni kweli tupu, na hutumika kuelezea au kuhalalisha baadhi ya mila na madhehebu ya jamii inayohusika.
Mulokozi naye pia anaona kuwa, huwezi kutenganisha visasili na suala zima la imani za dini, na
kwamba visasili vinaweza kuwa mwanzo au asili ya madhehebu mbalimbali ya dini. Tofauti na
watalaam wengine, Mulokozi hakuishia tu kutoa maana ya visasili bali amekwenda hatua moja
zaidi na kutoa aina mbalimbali za visasili na kueleza tofauti ya aina moja na nyingine kwa kutoa
maana na mifano ya kila aina ya visasili hivyo. Kwa mujibu wa Mulokozi kuna aina tatu za visasili
kama ifuatavyo, aina ya kwanza ya visasili anasema ni visasili vya usuli.
Visasili vya usuli ni visasili vinavyojaribu kuelezea asili au chimbuko la Taifa au jamii fulani au
wanadamu kwa ujumla. Anatoa mfano wa hadithi ya Wayahudi ya kuumbwa kwa ulimwengu na
kutokea kwa wanadamu (Adam na Hawa) kuwa ni mfano mzuri wa kisasili cha usuli. Anasema
kuwa, hadithi hii hivi sasa imeenea dunia nzima kupitia katika dini za Ukristo na Uislamu.
Mulokozi anaendelea kufafanua kuwa, hapa Afrika Mashariki, karibu kila kabila linacho kisasili
chake cha usuli. Anatoa mfano wa kisasili cha “Gikuyu na Mumbi”cha Wagikuyu (kinasimulia
chimbuko la koo tisa za Wagikuyu), hadithi ya “Kintu ya Waganda”(inahusu asili ya wanadamu),
hadithi ya “Mrile” ya Wachagga (inahusu asili ya moto), na hadithi zihusuzo chimbuko la
Wamijikenda wa Pwani ya Kenya. Hivi vyote ni mifano ya visasili vya usuli. Anasema kuwa
baadhi ya visasili vya usuli huelezea asili ya mila au madhehebu fulani ya jamii.
Aina ya pili ya visasili, kwa mujibu wa Mulokozi, ni visasili vya ibada na dini. Hivi huhusu
matendo ya ibada na imani mbalimbali za dini na mara nyingine hutendwa kisanaa yaani huigizwa
katika ibada. Kwa mfano, katika dini ya Kikristo, ekaristi (kula pamoja chakula cha Bwana) ni
maigizo ya chakula cha mwisho ambacho Yesu Kristo anasemekana alikula na wanafunzi wake
kabla ya kusulubiwa, na kusimuliwa katika kisasili kihusucho tukio hilo.
Aina ya mwisho ni visasili vya Miungu na Mizimu. Visasili hivi hupatikana zaidi katika mataifa
yenye miungu wengi, kwa mfano Asia na Ulaya ya Kale. Pia Misri ya kale ilikuwa navyo vingi.
Visasili vya aina hii husimulia matendo na visa vya miungu ya jamii inayohusika. Hapa Afrika
visasili hivi hupatikana kwa wingi katika jamii ya Wayoruba huko Nigeria, na katika falme
zinazozunguka Viktoria Nyanza.
Naye Soyinka (1979) anatoa maana ya visasili inayofananafanana sana na ile aliyotoa Materu.
Mwanafasihi mwingine aliyefasili neno visasili ni Kipury (1983). Hata hivyo fasili aliyotoa
inakaribiana sana na fasili zilizotolewa na wataalamu wengine kama tulivyoona hapo awali.
Hakuna wazo jipya analoibua. Visasili ni aina ya ndoto zilizokusanywa ambazo ni rahisi
kutafsiriwa ili kuleta maana iliyofichika. Visasili kama matokeo ya vitu vya kufikirika juu ya
ukweli wa vitu vilivyotokea vinahusu zaidi hisia na siyo sababu ya kitu fulani. Pia ni kuhusu zaidi
jinsi Miungu wanayofanya mambo makubwa, ukuu wao na uhusiano na vitu au viumbe vya asili.
Chimera na Njogu (1999:151) pia wametoa maana ya visasili, nao wanasema:
Visasili ni aina ya hadithi zilizojikita katika asili ya vitu au mambo kama visa vinavyohadithia asili ya kwa mfano maisha ya binadamu, viumbe, dunia, mwezi na jua, magonjwa, kifo na kadhalika.
Hata hivyo wanafasihi hawa, wanaonekana kuwa na mtazamo tofauti na ule wa Mulokozi
(ameshatajwa) kwani wanachanganya dhana ya visasili na miviga. Wakati vile ambavyo Mulokozi
anaona kuwa ni aina za visasili wao wanaona kuwa ni utanzu mwingine wa fasihi simulizi yaani
miviga. Wanasema:
Miviga ni hadithi ambazo ukiweka katika mizani ya kisayansi, kihistoria, au hata ya kimaumbile, hazioneshi ukweli wowote , lakini wenyewe waliozitunga, kuzisimulia na kuzirithisha vizazi vyao vichanga, huziamini kwamba ni kweli tupu. Matukio katika hadithi hizo basi huaminika yalitendeka kweli na ni ya kihistoria.
Wanaendelea kueleza kuwa hadithi hizi zinahusu, kwa mfano, chimbuko la makabila. Kila kabila
duniani, au kundi lolote la watu ambalo linajichukulia kuwa mlango mmoja, huamini kuwa kuna
mwanzilishi wa kabila hilo ambaye ajulikana vizuri sana. Aghalabu, jina la mwanzilishi huyo
huwa ndilo jina la kabila lenyewe. Wanatoa baadhi ya mifano ya miviga kuwa ni pamoja na kisa
cha Adamu na Hawaa. Wanasema;
Siku hizi za Uislamu na Ukiristo kutawala dunia nzima, watu wengi ulimwenguni wamekuja kuamini kwamba mvyele wao wa awali ni Adamu na mama yao ni Hawaa, mkewe Adamu. Hata hivyo, zamani imani haikuwa hiyo kwa watu wote, hata kidogo. Zamani hizo zitajwazo hapa, Adamu aliaminiwa tu
kwamba ni baba wa Wayahudi na Waarabu, na Hawa ndiye mama yao wa kwanza.
Wakati Njogu na Chimerah wanaona kuwa huu ni mfano wa aina ya kwanza ya miviga, mfano huu
huu Mulokozi anauweka kwenye kundi la aina mojawapo ya visasili yaani visasili vya usuli. Hii
inajidhihirika pia hata kwenye mifano mingine iliyotolewa na watalaamu hawa. Hata hivyo hoja ya
msingi hapa inabaki kuwa miviga ni sehemu ya visasili, kwa mujibu wa watalaamu mbalimbali.
Kwa mfano kisa cha Gikuyu na Mumbi ambacho kimetolewa mfano na Mulokozi (ameshatajwa),
kimeelezwa pia na Njogu na Chimerah japo wao wamekielezea kisa hiki kama mfano wa aina za
miviga na si visasili. Wanaeleza kuwa;
Wakikuyu wanaamini kwamba baba yao wa kwanza kabisa ni Gikuyu, mama yao ni Mumbi.
Gikuyu ndiye mtu wa kwanza aliyeumbwa na Mungu na kisha akaumbiwa mke, Mumbi. Mungu
wao aliitwa Murungu au Mugai (Ngai). Huyu Murungu alizoea kukalia kiti chake kinachong’ara
daima hapo kileleni, mlima wa Kerinyaga (Kenya).
Maelezo haya ya watalaamu hawa japo yanatofautiana kidogo hapa na pale, lakini yote
yanashadidia kuwa suala la miviga, imani katika miungu na mizimu na imani ya dini kwa ujumla
ni jambo la msingi na la muhimu tunapozungumzia suala zima la visasili. Tunaweza kusema kuwa
hii ni sifa muhimu sana ya visasili inayoweza kupambanua na kutofautisha kati ya utanzu huu wa
visasili na tanzu nyingine za fasihi simulizi kama ngano na nyingine.
Hivyo, visasili ni hadithi za “kwa nini” na “kwa vipi” kwa sababu zinaelezea asili na tabia ya
wanyama mbalimbali, mimea desturi na mila za jamii na hata kuhusu sura ya nchi yaani milima,
mito, na mabonde. Visasili vina sifa kubwa ya umajumui kwani vinaeleweka duniani kote;
vinaeleza kuhusu jua, mwezi na tabia za binadamu. Kwa mfano, kuna visasili vinavyoeleza “kwa
nini wanaume wengi hupiga wake zao”, na vingine vingi. Visasili ni matukio ya kibunifu na ya
kizamani yanayooanishwa na sababu au asili ya jambo, kitu au hali fulani. Tuna, kwa mfano,
visasili vinavyozungumzia kwa nini ikawa vinyama kama paka na panya au tumbili na mbwa
havipatani, au kwa nini kuna vinyama vyenye maumbile haya au khulka zile, kama vile sungura
kuwa na masikio marefu, ndovu kuwa mpole, na au mbuzi kuwa na papara.
Wanaendelea kusema kuwa, kitu cha kukifahamu ni kuwa visasili si mikasa inayosimuliwa kwa
kufurahisha tu watu, bali kusudio lake hasa ni kupeleka ujumbe au kutoa funzo fulani kwa
mlengwa. Kwamba hao kina mbwa na tumbili, paka na panya, au sungura na fisi watajwao humu,
huwa hawakusudiwi wao hasa, bali ni wanadamu wenye sifa kama za hao wanyama. Maana
kwenye maisha halisi wako wanadamu wenye papara kama za mbuzi, uroho kama wa fisi au
mahasimu kama mbwa na tumbili! Katika tafsiri hii tunaona kuwa mfasili anahusisha wanyama
katika visasili. Mtazamo kama huu tumeuona pia kwa Finnegan (ameshatajwa), jambo ambalo
linapingwa na wataalamu wengine kama tulivyoona kwenye mjadala hapo juu. Jambo la pekee
linaloelezwa hapa , tofauti na anavyoeleza Finnegan, ni kwamba pamoja na kwamba hadithi hizo
zinahusu wanyama ndani yake zina mafunzo yanayolenga kumfundisha mwanadamu mambo
kadha wa kadha kuhusiana na maisha ya kila siku.
2.3 Hitimisho
Sura hii imeshughulikia maoni ya watalaamu mbalimbali ulimwenguni kuhusu visasili. Imeangalia
kwa undani maana ya utanzu huu wa visasili kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali. Imebainika
kuwa watalaam mbalimbali wa fasihi simulizi pamoja na kueleza kwa namna mbalimbali kuhusu
visasili, wana mtazamo sawa kuhusu dhana hii. Mtafiti ana mtazamo sawa na watalaamu wa fasihi
waliotoa fasili ya neno visasili. Mbali na kujikita kuangalia maana ya visasili, sura hii pia
imejishughulisha na kubainisha sifa bainifu za visasili. Tumeona kuwa watalaamu wa fasihi
wametoa sifa ambazo zinawezesha kutofautisha baina ya utanzu wa visasili na tanzu nyingine za
fasihi simulizi. Kwa ujumla sura hii imepitia marejeo mbalimbali yanayohusu mada husika.
a teacher has to do some administrative works that sometimes stand as a hazard for him. A teacher spends more time by filling the OMR sheet or signing on different places than the time he spends for checking the answer scripts. No doubt, both the works need time and both of them are important but unfortunately the examiner gives importance to the administrative work rather than checking the answer scripts. On an average, a teacher gets maximumo4262008
Assessment may be defined as a method, which is used for better understanding the current knowledge that a student possesses. (Elison, 1999). It means that with the assessment a teacher can easily justify students ‘ability. Hence, the importance of assessment is not ignorable. According to “Pittsburg State University 2005”. Assessment helps departments to focus on those things in their curricula and courses that are going well. Assessment also helps to identify what is not going well, and often points to the specific changes that might be needed. Thus, assessment is an ongoing and continuous effort to improve the quality of instruction, student learning, and overall effectiveness of a department or unit. It is the systematic collection and analysis of information to improve students’ learning
SURA YA TATU
MBINU ZA UTAFITI
3.1 Utangulizi
Sura hii ya tatu inajadili mbinu mbalimbali zilizotumika katika utafiti huu. Mbinu hizo za utafiti ni
kama kubainisha na kuelezea eneo la utafiti, sampuli ya utafiti, taratibu za usampulishaji, mbinu za
ukusanyaji wa data na taratibu zilizotumika katika kuchambua data. Kadhalika, mkabala
uliotumika pamoja na kiunzi cha nadharia kilichotumika katika utafiti huu vimeelezwa. Pia usanifu
wa utafiti huu umeelezwa katika sura hii.
3.2 Usanifu wa Utafiti
Utafiti huu, kwa sehemu kubwa, ni wa uwandani na sehemu ndogo ilifanyika maktabani. Kwa
mujibu wa Kombo na Tromp (2006) usanifu wa utafiti ni ule muundo wa utafiti. Hivyo usanifu wa
utafiti ni mpangilio wa taratibu zinazotumika kukusanya na kuchambua data kwa namna
inayounganisha data zinazopatikana na malengo ya utafiti. Mbinu za ukusanyaji wa data
zilizotumika ni mahojiano, usaili na dodoso. Mbinu hizi inawezesha upatikanaji wa data za
kutosha kwa urahisi na kwa haraka. Mbinu ya uchambuzi matini pia ilitumika kupata data za
msingi ambazo zilipatikana maktabani kwa kusoma matini mbalimbali zinazohusiana na mada ya
utafiti huu. Data zilizopatikana zilichambuliwa kulingana na malengo ya utafiti huu.
3.3 Eneo la Utafiti
Utafiti huu ulifanyika mkoa wa Dodoma. Kutokana na malengo ya utafiti, data zilizotakiwa
zilipatikana kwa kuwahoji baadhi ya wakazi wa Dodoma wakiwemo wazee ambao wanafahamu
vizuri historia ya Wagogo na waliweza kutoa data za kutosha na zilizotakiwa na mtafiti. Kati ya
wilaya tano za mkoa wa Dodoma, wilaya ya Dodoma mjini ndiyo inasemekana kuwa na Wagogo
asilia, ukilinganisha na wilaya nyingine. Eneo jingine la utafiti huu ni mkoa wa Dar es Salaam.
Wahojiwa wanne toka mkoa wa Dar es Salaam walihojiwa ili kupata data zaidi. Pia data
zilipatikana maktabani na makavazini, hasa maktaba ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, makavazi
ya Taifa na makavazi ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili.
3.4 Sampuli ya Utafiti na Usampulishaji
Babbie (1992) anasema sampuli ni sehemu ya idadi watu ambayo mtafiti anavutiwa nayo katika
kupata taarifa na kutoa hitimisho la utafiti wake. Pia Kombo na Tromp (2006) wanasema jambo la
msingi ni kuanza na idadi kubwa na kadri utafiti unavyoendelea, mtafiti atabaki na eneo husika la
utafiti ambamo data zitakusanywa. Sampuli ya kimakusudi imetumika nyanjani kuteua wahojiwa
kwa sababu mtafiti anawafahamu baadhi yao. Aidha mtafiti alitumia sampuli elekezi ili kuwa na
utoshelevu wa wahojiwa waliochangia pakubwa utafiti huu. Wahojiwa wanawake kumi na tano
(15) na wanaume kumi (10) waliteuliwa kutoka kata za Makole, Mailimbili, Kizota, Uzunguni na
Kikuyu. Kwa hiyo, jumla ya watafitiwa katika mkoa wa Dodoma ilikuwa wahojiwa ishirini na tano
(25). Wahojiwa waligawanywa kama ifuatavyo:
a) Wazee wanawake na wanaume kumi na tano (15).
b) Vijana wa kike na wa kiume sita (6)
c) Watoto wa kike na wa kiume wanne (4)
Kutoka mkoa wa Dar es Salaam sampuli ilikuwa na wahojiwa wanne (4). Wahojiwa watatu (3) ni
wanaume na mmoja (1) mwanamke. Umri wao ni kati ya miaka ishirini na nane (28) na hamsini na
nane (58). Hawa walipatikana toka sehemu mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam, lakini wote ni
Wagogo toka sehemu mbalimbali za mkoa wa Dodoma. Hivyo jumla ya wahojiwa wote ni ishirini
na tisa (29). Idadi hii ilikidhi malengo na mahitaji ya utafiti.
Sampuli ya kimakusudi na elekezi ndiyo iliyomwongoza mtafiti kuteua wahojiwa ishirini na tisa
(29). Sampuli elekezi haihitaji idadi kubwa ya wahojiwa kwani huchukua muda mrefu kwa mtafiti
kuwapata na pia gharama za kukamilisha zoezi la ukusanyaji data zinakuwa kubwa. Wahojiwa
walioteuliwa wamekuwa ni wawakilishi wa wanajamii wote wa jamii ya Wagogo kwa kuzingatia
maoni yao.
Visasili viwili vya jamii ya Wagogo vilipatikana kwa kutumia mbinu bahatishi na kwa kuzingatia
malengo ya utafiti. Visasili viwili vimezingatiwa kwa sababu hakuna visasili vingi vilivyopatikana
katika jamii ya Wagogo. Kupata idadi kubwa ya visasili inawezekana lakini ingemlazimu mtafiti
kufanya utafiti katika eneo kubwa zaidi na pia kuongeza muda wa kufanya utafiti. Hata hivyo,
mtafiti aligundua kuwa utanzu wa visasili haujulikani sana ukilinganisha na tanzu zingine za fasihi
simulizi. Sababu zake zimeelezwa kwa kina katika sura ya nne.
3.5 Vyanzo vya Data na Taarifa
Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya kukusanya data, mtafiti aliweza kupata data za msingi na
data za ziada.
3.5.1 Data za Msingi
Data za msingi zilikusanywa uwandani ili kufidia upungufu uliandikwa kuhusu jamii ya Wagogo
na pia ndio kiini hasa cha kupata data za msingi za utafiti huu. Sababu za kwenda uwandani ni
pamoja na kutimiza lengo la utafiti kwani utafiti huu toka awali ulikusudiwa kufanyika uwandani,
ili kuchunguza na kubainisha dhima ya visasili katika kabila la Wagogo. Vilevile, hatukutegemea
sana data za maktabani kutokana na sababu mbalimbali. Sababu hizo ni pamoja na ukweli
kwamba, hakuna data za kutosha zilizohifadhiwa kuhusu visasili vya Wagogo na hii ndiyo sababu
iliyomchochea mtafiti kufanyia utafiti mada hii. Pia, data chache zilizohifadhiwa maktabani ni za
muda mrefu, tukizingatia ukweli kwamba fasihi hubadilika kuendana na mabadiliko yanayotokea
katika jamii, suala la kwenda uwandani lilikuwa ni muhimu na la lazima. Mtafiti alisikiliza
mazungumzo na kushuhudia matendo wakati wa usimuliaji, jambo ambalo alinufaika nalo kwa
kupata data za msingi. Kadhalika, mtafiti aliweza kunasa yaliyosimuliwa na watafitiwa kutokana
na kuwapo na utulivu. Zoezi la kurekodi lilikubalika kwa wahojiwa. Mtafiti alinukuu daftarini
maelezo yanayohusiana na uchunguzi husika. Mtafiti basi alikuwa ni mmoja kati ya washiriki wa
shughuli na hivyo kumrahisishia zoezi la ukusanyaji wa data. Kanda za sauti zilizorekodiwa na
watu mbalimbali zinazohusu visasili na historia ya jamii ya Wagogo kwa ujumla zilizingatiwa
wakati wa ukusanyaji wa data za msingi. Isitoshe kanda za sauti zilitumiwa na mtafiti kunasa
maelezo ya wahojiwa wakati wa mahojiano kati ya mtafiti na watafitiwa mbalimbali. Kanda hizo
zilimsaidia mtafiti wakati wa uwasilishaji, uchambuzi na mjadala kwani aliweza kujikumbusha
yale yaliyosemwa na watafitiwa kwa kusikiliza tena kanda hizo. Vilevile, watafitiwa walihojiwa
ili kupata uhalisi wa data kulingana na malengo ya utafiti.
3.5.2 Data Fuatizi
Maandishi mbalimbali yalipitiwa maktabani, ikiwa ni pamoja na vitabu, makala, majarida na
kwenye mtandao wa mawasiliano ili kupata mwelekeo muafaka kuhusu mada ya utafiti. Aidha
maandishi jumulifu ya fasihi na utamaduni yamesomwa ili kumwongoza mtafiti katika uchunguzi
wake. Tafiti tangulizi zimesomwa kupata mwangaza kuhusu nadharia, mbinu za ukusanyaji data,
uwasilishaji, na uchanganuzi wa matokeo ya utafiti. Vitabu na tasnifu juu ya visasili na fasihi
simulizi kwa ujumla vilitiliwa mkazo zaidi kwani ndicho kiini cha utafiti huu. Maandishi yahusuyo
jamii ya Wagogo pia yaliufaa utafiti huu kwa kupata historia na maelezo kuhusu utamaduni wa
jamii ya Wagogo.
3.6 Ukusanyaji wa Data
Ikumbukwe kwamba katika utafiti wowote ule, ukusanyaji wa data unahusu kukusanya taarifa
mahsusi zilizokusudiwa kutoa au kupinga uhalisia wa mambo fulani (Kombo na Tromp 2006).
Halikadhalika, katika utafiti huu taarifa mbalimbali zilikusanywa kutoka maktabani na uwandani
kwa kutumia mbinu na vifaa mbalimbali vilivyoandaliwa na mtafiti.
Data ilikusanywa katika jamii ya Wagogo wanaoishi kata za Kikuyu, Mailimbili, Makole,
Uzunguni na Chizota. Kata hizi zilizingatiwa kwa kuwa zina wakazi wengi ambao ni Wagogo na
pia ni kata zilizokaribiana hivyo ilimwezesha mtafiti kukusanya data kwa urahisi. Pia ukusanyaji
wa data ulifanywa katika mkoa wa Dar es Salaam kwa sehemu ndogo. Usaili wa ana kwa ana
ulihusishwa wakati wa kukusanya data za msingi. Hii ni kwa sababu baadhi ya data kama vile
utendaji haziwezi kupatikana katika kanda zilizorekodiwa. Pia data ilikusanywa kwa kuzingatia
kanda zilizorekodiwa na watu wengine zinazohusu jamii ya Wagogo, pamoja na zile kanda
alizorekodi mtafiti wakati akiwa uwandani akiwahoji watafitiwa. Kanda hizi zilifidia upungufu
uliojitokeza kwani si rahisi mtafiti kunukuu kila kitu. Ili kukusanya data ya kutosha mtafiti
alinukuu daftarini yale yote muhimu yaliyomwezesha kufikia malengo ya utafiti kwa kupata data
toshelevu na ya kina.
3.6.1 Vifaa vya Kukusanyia Data
Mtafiti aliandaa vifaa vya utafiti kulingana na mada na malengo ya utafiti. Vifaa hivi
vilimwezesha mtafiti kukusanya data husika na kupata taarifa sahihi za utafiti wake. Katika utafiti
huu, data na taarifa zilikusanywa kwa kutumia vifaa mbalimbali, vifaa hivyo ni pamoja na dodoso,
tepurikoda, kamera, kompyuta, shajara na kalamu.
Hojaji ni maswali yaliyoandaliwa na mtafiti kwa lengo la kumhoji mtafitiwa, na maswali haya
yanafungamana na malengo ya utafiti husika. Mtafiti alitumia maswali hayo kama mwongozo
wake katika kupata data husika kutoka kwa mtafitiwa. Hivyo, hojaji ilimwezesha mtafiti kupata
data za msingi na fuatizi. Hojaji lililotumika katika utafiti huu limeambatishwa mwishoni pamoja
na viambatisho vingine.
Shajara na kalamu: Vifaa hivi vilimsaidia mtafiti katika kunukuu na kuhifadhi baadhi ya data za
msingi kama vile tarehe, majina ya wahojiwa na mahali pa wahojiwa na data fuatizi katika utafiti
huu.
Tepurikoda ni kifaa kinachotumika katika kunasa na kurekodi sauti wakati wowote katika
muktadha wowote ule. Katika utafiti huu, tepurikoda ilitumika uwandani ambako mtafiti alirekodi
mahojiano baina yake na watafitiwa. Taarifa zilizorekodiwa katika tepurikoda zilitumika katika
uchambuzi wa data katika utafiti huu.
Kamera ni kifaa kilichotumika katika kupata taarifa mbalimbali za kuona ambazo haziko katika
maandishi. Kwa mfano picha za wahojiwa na maeneo mbalimbali ambayo yanahusiana na mada
husika. Kwa mfano kuna picha inayoonesha mahali ambapo inasadikiwa kuwa ni asili ya neno
Dodoma.
Kompyuta ilitumika katika kutafutia matini kutoka katika tovuti na wavuti na pia kuhifadhi taarifa
mbalimbali. Data zilizohifadhiwa zilichambuliwa na kutolewa mahitimisho kisha kuandaa ripoti ya
utafiti. Pia kompyuta ilitumika kama sehemu ya maktaba tembezi.
3.6.2 Mbinu za Ukusanyaji wa Data
Kutokana na malengo ya utafiti huu ya kuangalia dhima ya visasili katika kabila la Wagogo, data
zilizokusanywa ni data asilia kutoka uwandani kwa wanajamii wa kabila la Wagogo. Mbinu
zilizotumika ni pamoja na mahojiano, majadiliano na kushiriki.
Mtafiti alitumia mbinu ya kushiriki katika kukusanya data, na alikuwa sehemu ya hadhira wakati
wa kusimulia visasili. Mbinu za majadiliano na mahojiano vile vile zilitumika.
3.6.2.1 Mbinu ya Mahojiano
Hii ni njia ya kupata data kwa kutumia maswali na majibu yanayofanywa kwa mazungumzo kati
ya mtafiti na mtafitiwa (Kothari 2008). Katika utafiti huu mtafiti aliongozwa na hojaji katika
kuwauliza watafitiwa wake maswali ya utafiti wake. Mojawapo ya maswali yaliyoulizwa
uwandani ni pamoja na maswali ya utafiti huu. Je, kuna visasili katika kabila la Wagogo? Swali
jingine lilikuwa, Je, visasili katika kabila la Wagogo vina dhima yoyote, unaweza kueleza?
Maswali mengine yalikuwa, Je jamii ya Wagogo inaamini nini kuhusu mizimu na miungu? Je,
kuna matambiko yanayofanyika katika kabila la Wagogo? Je, nini asili ya kabila la Wagogo? Je,
Wagogo wanaamini kuhusu kuumbwa kwa dunia na ulimwengu? Na mengine mengi. Majibu
yaliyopatikana kuhusiana na maswali haya yalitofautiana kutoka mhojiwa mmoja na mwingine.
Kuna wahojiwa waliosema kuwa kuna visasili katika jamii yao, na walifanikiwa kutoa mifano ya
visasili. Idadi kubwa ya wahojiwa japo walikubali kuwa kuna visasili, mifano waliyotoa haikuwa
visasili. Walichanganya visasili na tanzu nyingine za fasihi simulizi kama visasuli, visakale na
ngano. Changamoto kubwa katika utafiti huu ilikuwa ni suala la neno visasili kuwa msamiati
mgumu kwa baadhi ya wahojiwa. Ilimlazimu mtafiti kufafanua maana ya visasili kwa undani ili
kuhakikisha kuwa data zinazopatikana ni sahihi. Wakati mwingine ilimlazimu mtafiti kutumia
lugha ya Kigogo kufafanua dhana ya visasili ili kuhakikisha kwamba watafitiwa wanaelewa vizuri.
Changamoto nyingine iliyojitokeza ni kwamba baadhi ya wahojiwa hawakuwa tayari kuzungumza
kuhusu vitu kama matambiko na miviga kwa sababu waliamini kuwa mizimu na miungu
watakasirika. Jambo hili lilisababisha ugumu wa kupata data zilizotakiwa.
3.7 Mkabala wa Uchambuzi wa Data
Data zilizokusanywa zilitolewa maelezo, zilichambuliwa na kufupishwa kwa kutumia mkabala wa
kimaelezo yaani mkabala usio wa kiidadi. Kothari (1990) anasema mkabala usio wa kiidadi ni njia
ya kuchambua data katika muundo wa maelezo pasipo kufuata taratibu za kitakwimu. Katika
utafiti huu mkabala huu ulimwezesha mtafiti kupata data zilizo katika maelezo kupitia njia ya
mahojiano kwa kutumia hojaji lililoandaliwa na mtafiti. Data hizo zilifupishwa kwa namna
ambayo ni rahisi kuchambuliwa na kueleweka kwa kuzingatia malengo ya utafiti huu. Katika
utafiti huu, visasili viwili vya jamii ya Wagogo vilivyopatikana vilichambuliwa ili kubainisha
dhima ya visasili katika jamii husika kama malengo ya utafiti huu yanavyoonesha
3.8 Uchambuzi wa Data
Data zilikusanywa kutoka vyanzo kwa kuzingatia malengo ya utafiti. Mtafiti kwa kutumia mkabala
wa kimaelezo amechambua visasili viwili vya jamii ya Wagogo vilivyopatikana. Uchambuzi pia
umehusisha visasuli, visakale pamoja na ngano zilizotolewa mifano na wahojiwa waliokuwa
wanachanganya tanzu za fasihi simulizi. Dhima ya visasili viwili vya kabila la Wagogo
vilivyopatikana zilibainishwa. Hali kadhalika ubainishaji wa dhima ulihusisha visasuli, visakale na
ngano zilizotolewa mifano na wahojiwa.
3.9 Kiunzi cha Nadharia
Zipo nadharia nyingi ambazo zinaweza kutumika katika utafiti wa fasihi simulizi. Finnegan (1970)
ametoa muhtasari mzuri wa shughuli za utafiti wa fasihi simulizi ya Afrika katika karne ya kumi
na tisa na nadharia zilizoongoza utafiti huo. Kwa mujibu wa Finnegan utafiti kuhusu fasihi simulizi
ya Afrika ulianza katikati ya karne kumi na tisa. Nadharia ambazo amezijadili Finnegan na
zinaweza kutumika katika utafiti wa fasihi simulizi ni pamoja na nadharia ya mageuko (evolution
theory), nadharia ya mweneo au msambao (diffusion theory), nyingine ni nadharia ya Umuundo-
uamilifu (structural functional) na nadharia ya kimuziki (musicological approach). Tutajadili kwa
undani kidogo baadhi ya nadharia hizo zilizotajwa na Finnegan.
Nadharia ya mageuko kuhusiana na jamii kwa ujumla ilianza karne ya kumi na tisa (19) na
mwanzoni mwa karne ya ishirini (20). Ilikuwa ni nadharia changamani sana na ilichukua sura au
umbo au mtindo tofauti tofauti. Nadharia hii iliamini kwamba jamii yoyote lazima ipitie kwenye
hatua za mabadiliko ya kijamii na ya kiutamaduni ambayo hayafuati mstari mnyoofu. Inaweka
msisitizo kwenye asili au mwanzo wa kitu chochote kuwa ni muhimu sana. Pia inaamini kuwa
mwelekeo wa hayo mabadiliko ni kukua au kubadilika kuelekea juu yaani kutoka kwenye ujinga
kwenda kwenye uelewa.
Nadharia hii pia iliweza kutumika katika utafiti wa fasihi simulizi hasa kwenye karne ya ishirini
(20). Ilitumiwa zaidi na wanazuoni wa Uingereza. Msisitizo uliwekwa kwenye asili na mabadiliko
ya fasihi. Swali liliulizwa; aina gani ya fasihi ilianza kuwepo katika historia ya mwanadamu? Je, ni
ngano yaani hadithi (folk literature) au ni sanaa ya jadi (folk-lore). Walilinganisha fasihi ya wakati
huo na hatua ya jamii ya mabadiliko ya wakati huo yaani ujima. Waliona kuwa fasihi simulizi
ilikuwa sawa kwa jamii zote na watu wote waliokuwa wanapita katika hatua moja ya mageuko.
Fasihi katika jamii zilizokuwa katika hatua ya ujima ilikuwa tofauti kabisa na ile ya jamii
zilizokuwa “zimestarabika” au zimeendelea.
Nadharia nyingine ni ile ya mweneo au msambao. Hii ni nadharia inayojikita katika kuangalia
ueneaji wa vitu katika eneo la kijiografia. Katika karne ya kumi na tisa (19) na ya ishirini (20),
msukumo mkubwa wa wanazuoni ulikuwa ni kujua eneo la kigeografia na historia nzima ya
hadithi za aina mbalimbali katika ulimwengu. Hivyo, ilikuwa inalenga zaidi katika kutafuta
mweneo wa fasihi simulizi kihistoria na kijiografia.
Nadharia hii ilianzishwa na Boas na wenzake kwenye karne ya ishirini (20) huko Marekani. Jambo
la msingi la kukumbuka hapa ni kwamba nadharia hii haikujihusisha na uchunguzi wa kina wa
kujua umuhimu wa tanzu za fasihi simulizi katika jamii. Wala haikujihusisha sana na ukusanyaji
wa tanzu hizo za fasihi simulizi ili kupata rekodi ya kutosha japokuwa hayo yote yalikuwa
yanatakiwa sana. Msisitizo mkubwa uliwekwa kwenye masimulizi ambayo motifu zake zingeweza
kupatikana kwa urahisi. Hata hivyo msisitizo mkubwa zaidi ulikuwa kwenye ushairi kuliko tanzu
nyingine.
Nadharia hii ilianzia huko Amerika ikaenea kwingineko. Kwa kuwa lengo lake kubwa ni
kuangalia asili na chanzo cha kijiografia cha hadithi na mweneo wake toka sehemu moja hadi
nyingine, wakati mwingine inatambua hadithi moja ambayo inapatikana katika jamii mbalimbali
ili kurahisisha upatikanaji wa eneo halisi ambapo hadithi hiyo ilianzia na baadaye kuenea sehemu
nyingine. Mifano mingi ya uchanganuzi wa namna hii imetolewa, mfano mmojawapo ukiwa ni ule
wa Stith Thompson’s unaoitwa Motif- Index of Folk-literature ambamo motifu mbalimbali za
hadithi zimeorodheshwa kwa ajili ya rejea na ufananishaji wa asili yake.
Zipo nadharia nyingi ambazo zimependekezwa na Finnegan kutumika katika utafiti wa fasihi
simulizi, hata hivyo hatuwezi kuzijadili zote. Nadharia hizo zinaweza kutumika katika utafiti wa
tanzu mbalimbali za fasihi simulizi.
Kutokana na malengo, maswali na tatizo la utafiti huu, nadharia iliyotumika ni ile ya kiuamilifu.
Nadharia zilizojadiliwa hapo juu haziwezi kutumika katika utafiti huu kwa kuwa haziendani na
malengo na maswali ya utafiti husika. Nadharia ya Mweneo au Msambao kwa mfano, inajikita
katika kuchunguza eneo la kijiografia ilipoanzia fani fulani ya fasihi simulizi na jinsi ilivyosambaa
au kuenea katika maeneo mengine. Hili si lengo la utafiti huu. Wala nadharia hii haitasaidia kujibu
maswali ya utafiti huu.
Nadharia ya kiuamilifu hutumika katika uchunguzi wa fasihi simulizi ambapo huwawezesha
watafiti kuchunguza dhima za tanzu mbalimbali za fasihi simulizi mathalani, methali, ngano
vitendawili na visasili. Japokuwa nadharia hii haijihusishi moja kwa moja na uchunguzi wa utanzu
wa visasili peke yake, bado ni nadharia inayofaa kutumika kwa kuwa visasili ni mojawapo ya
tanzu za fasihi simulizi ambazo zinaweza kuchunguzwa kwa kutumia nadharia hii.
Nadharia hii ilianzishwa na Herper Spencer ilianzia kwenye stadi ya biolojia. Nadharia hii
inalinganishwa na mwili wa binadamu jinsi unavyofanya kazi. Viungo vya mwili vinafanya kazi
kwa kushirikiana na hivyo vinahusiana kimoja na kingine na vinategemeana. Viungo vyote kwa
pamoja ndivyo vinavyosababisha kuwepo kwa maisha ya kiumbe. Hivyo basi, nadharia hii ina
mtazamo huohuo kuhusu jamii, kwamba asasi mbalimbali katika jamii zinafanya kazi kwa
kushirikiana na nyingine ili kuelimisha jamii. Kwa hiyo nadharia hii inaweza kutumika kuchunguza
na kuchambua tanzu za fasihi simulizi, visasili vikiwemo. Katika visasili mtafiti anaangalia
maudhui kwa kuzingatia vipengele vinavyojenga maudhui, dhima zake na mchango wa kila
kipengele katika kujenga visasili. Nadharia hii ilisaidia sana katika utafiti huu uliolenga kuelezea
visasili vya jamii ya Wagogo na kubainisha dhima za visasili vya kabila hilo.
3.10 Mipaka na Mawanda ya Utafiti
Jamii ya Wagogo ina aina na tanzu nyingi za fasihi simulizi zilizofanyiwa utafiti na nyingine
nyingi bado hazijafanyiwa utafiti wowote. Tanzu hizo ni kama vile hadithi, vitendawili, ngano,
methali, nyimbo na nyinginezo. Hata hivyo utafiti huu umejikita katika kuchunguza visasili vya
jamii ya Wagogo na kubainisha dhima yake katika jamii hiyo. Uchunguzi umejikita katika
manispaa ya Dodoma kata za Makole, Mailimbili, Kizota, Uzunguni na Kikuyu. Pia data nyingine
ilipatikana kutoka mkoa wa Dar es Salaam kwa baadhi ya Wagogo wanaoishi sehemu mbalimbali
za mkoa wa Dar es Salaam.
3.11 Muhtasari wa Sura ya Tatu
Kwa ujumla sura hii imeelezea mbinu mbalimbali zilizotumika katika ukusanyaji wa data ili
kujibu maswali ya utafiti huu. Mbinu hizo ni pamoja na eneo la utafiti, sampuli ya utafiti,
michakato ya usampulishaji, njia na mbinu za ukusanyaji wa data, michakato ya uchambuzi wa
data, mipaka na mawanda ya utafiti. Aidha kiunzi cha utafiti, mafanikio na matatizo ya mbinu za
ukusanyaji data na vikwazo vilivyojitokeza wakati wa ukusanyaji wa data pia vimeelezwa.
Uchambuzi na mjadala wa data zilizokusanywa pamoja na uwasilishaji wa data zilizochambuliwa
utafanyika katika sura inayofuata.