uzalishaji bora wa mahindi - coa.sua.ac.tz · virutubisho hivyo ni pamoja na madini muhimu kama...

20
Matumizi sahihi ya mbolea na mbinu nyingine za kilimo nchini Tanzania Uzalishaji bora wa mahindi

Upload: others

Post on 14-Oct-2019

44 views

Category:

Documents


0 download

TRANSCRIPT

1

Matumizi sahihi ya mbolea na mbinu nyingine za kilimo nchini Tanzania

Uzalishaji bora wa

mahindi

2

Chapisho hili ni pato kutoka mradi unaofadhiliwa na AGRA nchini Tanzania uitwao:

‘Scaling up Minjingu phosphate utilization for balanced fertilization of crops in Tanzania’‘Mradi wa kukuza matumizi ya mbolea za Minjingu fosfati na matumizi sahihi ya mbolea mbalimbali, Tanzania’

na msaada kutoka Africa Soil Health Consortium ambayo inaratibiwa na CABI

Chapisho hili limeandikwa na:This publication has been written by:

1J.M.R. Semoka, 1N. Amuri, 2C.P. Msuya-Bengesi, 3S.T. Ikerra na 4I. Kullaya1. Idara ya Sayansi ya Udongo, S. L. P. 3008, SUA, Morogoro, Tanzania

2. Idara ya Elimu na Ushauri wa Kilimo, S. L. P. 3002, SUA, Morogoro, Tanzania3. Mlingano Agricultural Research Institute, S. L. P. 5088 , Tanga, Tanzania

4. Selian Agricultural Research Institute, S. L. P. 6024, Arusha, Tanzania

3

UdongoUdongo una rutuba ya asili yaani virutubisho katika udongo, mboji (organic matter), na viumbe mbalimbali vinavyoishi kwenye udongo. Rutuba ya udongo inategemea sana hali ya udongo kikemia, kibiolojia na kifizikia.

Makundi ya udongoKuna makundi makuu matatu ya udongo, kutokana na ukubwa wa chengachenga za udongo:

• Kichanga (Sand soil) - una uwezo mdogo wa kuhifadhi maji na unyevunyevu. Hivyo, hukauka upesi.• Tifutifu (Loam soil) - unahifadhi maji vizuri na upatikanaji wa maji na virutubisho kwa mimea ni mkubwa. • Mfinyanzi (Clay soil) - unahifahdi maji mengi zaidi, bali upatikanaji wa maji na virutubisho kwa mimea ni mdogo.

Vipimo vinavyoonyesha hali ya rotuba ya udongo ni:• Tindikali ya udongo• Kiasi cha mboji• Kiasi cha Naitrojeni, Fosfati, Potashi, Salfa, Chokaa (Calcium) na Magnesium. Vilevile kiasi cha zinki, shaba, manganese na boroni vinapimwa.

pH ya udongo (Soil pH)pH ni kipimo kinachoonyesha kiwango cha tindikali au nyongo katika udongo. Udongo waweza kuwa tindikali (ph ndogo kuliko 7), nyongo (ph kubwa kuliko 7), au katikati (neutral) - ph ya 7. Tindikali au nyongo ya udongo hupimwa kwa kutumia pH mita. Mazao mengi hustawi zaidi katika udongo wenye hali ya tindikali ya wastani (kipimo cha pH 5.5 hadi 7.0).

Mahindi hustawi kwenye udongo wa tifutifu wenye tindikali ya wastani na virutubisho vya kutosha.

4

Mbolea

Mbolea ni chakula cha mimea, ambayo ni mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali vinavyoongezwa kwenye udongo au vinavyowekwa moja kwa moja kwenye mimea ili kuongeza ukuaji na uzalishaji wa mimea.

Virutubisho hivyo ni pamoja na madini muhimu kama vile naitrojeni, fosfati na potashi. Madini mengine ni pamoja na salfa, chokaa (calcium), magnesium, boroni, shaba, chuma, manganese, molybedenum na zinki. Haya madini kwa asili, yanapatikana katika udongo kwa viwango tofauti. Yanapopungua kutokana na kilimo, inabidi yaongezwe kwa kutia mbolea.

Aina za mboleaKuna aina mbili kuu za mbolea ambazo ni:

1. Mbolea za asili (organic fertilizers)2. Mbolea za viwandani (inorganic or industrial fertilizers)

Mbolea za asili (organic fertilizers)

Hizi ni mbolea zinazotokana na wanyama na mimea. Mbolea za asili ni kama vile:

• Mbolea vunde: inajulikana pia kama biwi au compost. Hutokana na mchanganyiko wa manyasi au mabaki ya mbao na samadi na majivu.

• Samadi: kutoka kinyesi cha wanyama kama mifugo na ndege.• Mbolea za kijani: hutokana na kupanda mimea aina ya mikunde

ambayo hukatuliwa na kuchanganywa na udongo.• Majivu: ni mbolea ya asili yenye madini aina ya potashi kwa wingi,

fosfati, chokaa na magnesium.• Matandazo (mulch): ambayo baadaye yakioza huwa mbolea.

5

Mbolea za viwandani (inorganic fertilizers)

Hizi ni mbolea zinazotengenezwa viwandani kwa kutumia virutubisho mbalimbali kwa kufuata viwango maalum vilivyowekwa ili kukidhi mahitaji ya mimea. Mbolea hizi zinatengenezwa kwa lengo maalum la kupata aina na kiasi fulani cha kirutubisho/ virutubisho vinavyohitajika na mimea.

Mbolea za kupandia mahindiMbolea maarufu za kupandia katika soko la Tanzania ni: TSP, DAP, Minjingu Phosphate na Minjingu Mazao. Lakini zile ambazo zimechaguliwa kwenye mradi wa ‘Kukuza matumizi ya Minjingu Phosphate’ ni DAP, Minjingu Phosphate na Minjingu Mazao.

Diammonium Phosphate (DAP)Ina virutubisho viwili - naitrojeni ambacho kiko kwa kiwango cha asilimia 18, na fosfati (P2O5) ambacho kiko kwa kiwango cha asilimia 46. Inapatikana katika hali ya chengachenga (granules).

6

Minjingu PhosphateIna kiwango cha fosfati (P2O5) asilimia 29 na inatumika zaidi kwa kutoakirutubisho hiki. Lakini inaongeza vilevile kirutubisho cha chokaa (calcium) ambacho kipo kwa kiwango cha asilimia 40. Chokaa inasaidia vilevile kukabili tindikali (acidity) ya udongo.

Minjingu MazaoHii ni mbolea mpya inayotokana na Minjingu Phosphate lakini imeongezwavirutubisho vingine vitano ambavyo ni naitrojeni (10%), salfa (5%), zinki (0.5%), shaba (0.5%), boroni (0.1%), pamoja na chokaa (25% CaO) na magnesium (1.5% MgO). Virutubisho vilivyoongezwa hususani naitrojeni na salfa ni vile ambavyo vinakosekana katika aina nyingi za udongo.

Zinki, shaba na boroni vimeongezwa kwa tahadhari kwa sababu vinaonyesha dalili za upungufu katika baadhi ya maeneo. Minjingu Mazao iko katika hali ya chengachenga.

Jinsi ya kuchagua mbolea ya kupandiaMbolea za kupandia hasa Minjingu Phosphate na Minjingu Mazao zinahitaji hali maalum ya udongo ili ziweze kufanya kazi vizuri.

Kwa mfano hali ya tindikali ya udongo inabidi iwe chini ya 6.2 ili mbolea za Minjingu ziyeyuke kwa kiwango cha kutosha. Kwa udongo wenye tindikali zaidi ya 6.2, tumia DAP wakati wa kupanda. Ikiwa kuna upungufu wa potashi, tumia mbolea zinazorejesha madini hayo.

Tumia mboji pamoja na mbolea za viwandani ili kuongeza mazao. Mboji huwa haibebwi na mvua na faida yake hudumu kwa muda mrefu. Mboji husaidia udongo kuhifadhi maji na virutubisho. Zinapowekwa kwenye mashimo ya kupandia mbegu ni vyema kufukia mbolea kabla ya kuweka mbegu (kutenganisha mbolea na mbegu).

7

Dalili ya upungufu wavirutubisho mbalimbali 1. Upungufu wa naitrojeni (Nitrogen)Kwa ujumla mmea unakuwa mdogo, mwembamba na hutoa suke dogo, na mwishowe hutoa mazao kidogo (picha A). Kama upungufu ni mkubwa sana mmea unaweza usitoe mhindi kabisa.

• Kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mmea - ambayo husababisha mmea kudumaa.

• Rangi ya kijani kwenye mmea hufifia na kugeuka taratibu kuelekea kwenye njano. Upungufu ukiwa mkubwa sana, majani hugeuka rangi ya njano kutoka pembeni. Majani yaliyokomaa ndio huanza kugeuka.

• Majani ya mwanzo hukauka mapema kwenye mimea yenye upungufu kuliko ile yenye naitrojeni ya kutosha.

2. Upungufu wa fosfati (Phosphorus)• Dalili ya kwanza ni kupungua kwa kasi ya kukua na mashina kuwa

membamba. • Upungufu ukiwa mkubwa, mmea unakuwa na rangi ya zambarau

(picha B). Rangi hii inaanzia pembeni mwa majani na kwenye mashina na baadaye husambaa kwenye jani lote. Rangi inaonekana vizuri zaidi upande wa chini wa jani.

• Majani ya mwanzo hukauka mapema na mizizi haikui vizuri kwenye mimea yenye upungufu kuliko ile yenye fosfati ya kutosha.

A

B

8

3. Upungufu wa potashi (Potassium)• Kupungua kasi ya ukuaji wa mimea, ambayo inasababisha mmea

kudumaa (picha C). • Upungufu ukiwa mkubwa rangi ya kijani inafifia na mwisho

kutoweka kabisa na sehemu iliyoathirika inakauka (necrosis) kwenye mazao mengi km mahindi, mazao mengine ya nafaka na miti ya matunda. Kutoweka kwa rangi ya kijani na kukaukakunaanzia pembeni mwa majani na kwenye ncha. Majani yanakuwa na michirizi ya manjano na vinundu nundu kama migongo ya bati (yellowish streaks and corrugated).

• Majani ya mwanzo hukauka mapema kwenye mimea yenyeupungufu kuliko ile yenye potashi ya kutosha.

Jinsi ya kuchagua mbolea ya kutumia

C

C

9

1. Kuandaa shamba, kusafisha, kulima/kutifuaNi vyema mashamba yaandaliwe mapema kabla ya msimu wa kupanda haujaanza ili kumpa mkulima fursa ya kupanda kwa wakati unaotakiwa.

Kuna njia mbalimbali zinazotumika kuandaa mashamba. Kati ya njia hizi ni pamoja na kufyeka, kung’oa visiki na kulima. Shamba linaweza kulimwa kwa kutumia:

i). Jembe la mkono - wengi wanatumia ii). Jembe la kukokotwa na wanyama kama ng’ombe iii). Power tillers iv). Matrekta

Matumizi ya trekta, power tillers na jembe la kukokotwa na wanyama yanapunguza nguvu kazi kwani vinachimbua udongo na kuufanya kuwa tifutifu (kufanya isiwe na mabonge makubwa, wala isiwe vumbi vumbi). Hii husaidia:

i). Mizizi ya mimea kupenyeza ardhini kirahisiii). Udongo kuweza kuhifadhi majiiii). Udongo kuwa na hewa inayohitajika na mimeaiv). Ukuaji mzuri wa mimea hivyo kuongeza mavuno

2. KupandaMbegu boraMatumizi ya mbegu bora ni muhimu katika upatikanaji wa mavuno mengi na bora. Kuna makundi mawili makuu ya mbegu ambayo ni:

i). Mbegu za asili: Ni zile ambazo zimetumika miaka mingi katika historia ya kilimoii). Mbegu zilizoboreshwa: Hizi ni zile zilizoboreshwa kutoka mbegu za asili. Kundi hili linagawanywa kwenye makundi mawili - composite varieties na mbegu chotara (Hybrids).

Kuandaa shamba, kupandana kupalilia

10

Ushauri wa matumizi ya mbegu zilizoboreshwa unatofautiana kutoka eneo moja na lingine kwa sababu ya:

i). Mwinuko kutoka usawa wa bahariii). Kiasi cha mvua katika eneo husikaiii). Muda unaotumia mbegu hadi kukomaa

Mbegu za mahindi zilizoboreshwa ni kama TMV1, TAN 250, TAN 254, Staha, Situka na zingine zote zinazoanza na herufi “H” kama vile H 250, H 251 na H 615.

Jinsi ya kuweka mbolea za kupandiaMbolea hizi zinawekwa shambani kabla ya kupanda/kusia mbegu. Zinawekwa kwa njia mbalimbali kama vile kusambaza kwenye eneo husika na kuchanganya na udongo, au kuweka kwenye mistari au mashimo ya kupandia. Ni bora zaidi kuchanganya mbolea za Minjigu Phosphate au Minjingu Mazao na udongo kuliko kutia kwenye shimo la kupandia. Pia kuchanganya mbolea na udongo huondoa athari za mbolea kwenye uotaji wa mbegu, hasa kama kuna uhaba wa unyevunyevu.

Viwango vya mbolea za kupandiaKiwango cha mbolea za kupandia kilichopendekezwa ni kilo 20 fosfati (P) kwa hektari ambayo ni sawasawa na kiasi cha aina mbambali za mbolea za kupandia kama inavyoonyeshwa kwenye jedwali namba 1.

Jedwali na. 1: Kiasi cha mbolea za kupandia kwa inayopendekezwa kwa eneo (hektari au ekari)

Aina ya mbolea za

kupandia

Idadi ya mifuko ya kilo 50

kwa hektari

Idadi ya mifuko ya kilo 50

kwa ekariViwango kwa kila shimo

DAP 2 1 Nusu kizibo cha soda

Minjingu fosfati 3 1½ Kizibo kimoja cha soda

Minjingu Mazao 4½ 2 Kizibo kimoja na nusu cha soda

11

Muda wa kupandaMuda wa kupanda unatofautiana kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na majira ya mvua. Kwa mfano katika wilaya ya Morogoro tarehe za kupanda ni kuanzia februari 15 hadi Machi 15. Mkulima anashauriwa afuate kalenda ya muda wa kupanda kama anavyoshauriwa na bwana shamba wake.

Kupanda kwa nafasiKupanda kwa nafasi ni kati ya njia bora za kilimo inayomwezesha mkulima kupata mazao bora. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kupanda kwa mistari na kufuata nafasi zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo. Kwa mfano nafasi zifuatazo zinaweza kutumika katika upandaji wa mahindi:

Nafasi Idadi ya mbegu kwa kila shimo Kiwango cha mbolea kutumia kizibo cha chupa

90 sm X 30 sm 1 1

90 sm X 25 sm 1 1

90 sm X 50 sm 2 2

* Nafasi hizi zote hutoa mimea 44,000 katika heka.

12

3. KupaliliaNi muhimu shamba lipaliliwe baada ya mimea kuota ili kuondoa magugu. Magugu ni mimea hivyo hushindana na mimea iliyopandwa na mkulima kwa kunyonya virutubisho ardhini. Magugu yanaweza pia kuhifadhi wadudu na magonjwa yanayoweza kushambulia mimea iliyopandwa na hivyo kupunguza mavuno.

Mbolea za kukuziaNi mbolea zinazotumika baada ya mimea kuota kwa lengo la kuikuza mimea ili itoe mavuno bora. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha naitrojeni. Mbolea maarufu za kukuzia katika soko la Tanzania ni kama:

AIna ya mbolea Kiwango cha kirutubisho cha naitrojeni

Urea 46%

Calcium Ammonium Nitrate (CAN) 23%

Sulphate of Ammonia (SA) 21%

13

Urea inakirutubisho cha naitrojeni (N) kwa kiwango kikubwa na watu wengi wanauzoefu nayo. Vilevile bei yake ni nafuu ikilinganishwa na mbolea zingine za kukuzia. Mbolea hii iko katika hali ya chengachenga za mviringo (granules) za rangi nyeupe. Kiwango cha urea ni nusu kizibo cha soda kwa kila shina.

Mbolea hizi hazidumu kwenye udongo kwa muda mrefu kwa hiyo huwekwa shambani wakati mimea inapokuwa na mahitaji makubwa ya kirutubisho cha naitrojeni na wakati udongo una unyevunyevu na shamba halina magugu.

Mbolea za kukuzia huwekwa kuzunguka kila shina la mimea au pande mbili au tatu au nne za kila shina. Cha muhimu ni kwamba mbolea isirundikwe sehemu mmoja.

14

Viwango vya mbolea za kukuzia vinavyoshauriwaKiwango kinachopendekezwa ni kilo 60 naitrogeni kwa hektari, ambacho ni sawasawa na kiasi kama inavyoonyeshwa kwenye jedwali namba 2. Mbolea inayotumika mara kwa mara ni Urea. Hata hivyo mbolea zingine kama SA inaweza kutumika kama kuna mahitaji ya salfa. CAN inaweza kutumika kama kuna mahitaji maalum ya nitrate na ammonium. Kwenye mahindi mbolea ya kukuzia inawekwa baada ya palizi ya kwanza ambayo ni kama wiki tatu mpaka wiki nne baada ya kupanda.

Jedwali na. 2: Kiasi cha mbolea za kukuzia kwa inayopendekezwa kwa eneo (hektari au ekari)

Aina ya mbolea za kukuziaIdadi ya mifuko ya

kilo 50 kwa hektari

Idadi ya mifuko ya

kilo 50 kwa ekariViwango

Urea 2 1 Nusu kizibo cha soda

CAN 4½ 2 Kizibo kimoja cha soda

SA* 3 1 Nusu kizibo cha soda

* Kiwango kilichowekwa hapa ni kwa ajili ya kupata kirutubisho cha salfa kinachosha - ambacho ni kilo 20 ya salfa kwa hektari. Na kupata sehemu ya mahitaji ya naitrojeni ambyao ni kilo 21. Hii ina maana kwamba kilo 39 za naitrojeni inabidi ziwekwe kama Urea au CAN.

15

Mambo muhimu ya kuzingatia•Kuweka mbolea: Sehemu za nchi ambazo muda wa kukua mahindi ni mrefu (zaidi ya miezi mitatu),

ni vyema kuweka mbolea za kukuzia mara mbili, yaani nusu ya kiwango kinachopendekezwa baada ya mwezi mmoja, na kurudia tena (kutumia nusu iliyosalia) baada ya wiki tatu.

•Kupalilia: Katika kilimo cha mahindi, ni muhimu shamba lipaliliwe siku 14 hadi 21 baada ya mimea kuota kufuatana na hali ya shamba wakati wa kupanda. Wataalamu wanashauri kwamba katika kilimo cha mahindi, shamba lipaliliwe mara 2-3, kufuatana na hali ya magugu katika shamba.

- Utafiti unaonyesha kwamba, shamba la mahindi ambalo halijapaliliwa linaweza kupunguza mavuno kwa asilimia 60 hadi 100 ya mavuno yanayotarajiwa. Hata kama mkulima atatumia mbegu bora, aina na kiasi cha mbolea zinazoshauriwa, kupanda kwa mstari pamoja na mbinu nyingine bora zinazoshauriwa, bila kupalilia hali hii itaathiri mavuno yake.

16

Kudhibiti magonjwa na wadudu wanaoshambulia mahindiMagonjwa yanayoshambulia mahindii) Maize streak virus (picha A)Dawa/Kudhibiti: Mbegu bora inayostahimili ugonjwa, kupanda mapema, kung’oa mimea iliyoathirika ama kunyunyiza dawa za kuua ‘vectors’ kama vile inzi weupe (whiteflies).

ii) Smut (Fugwe) (picha B).Dawa/Kudhibiti: Tumia Helerat ukifuata maagizo kamili.

iii) Cob rot (kuoza kwa mhindi) (picha C)Dawa/Kudhibiti: Tumia mbegu zinazostahimili kuoza.

Wadudu na wanyama wanaoshambulia mahindii) Stalk borer (picha D)Dawa/Kudhibiti: Tumia Malathion, sumithion, vumbi ya cymbush au Sevin 5G na ufuate maagizo kamili.

ii) Cutworms (Vikata Shina) (picha E)Dawa/Kudhibiti: Tumia Dragnet FT na ufuate maagizo kamili.

iii) Wanyama waharibifu (picha F)Kudhibiti: Kuwatishia na kuwafukuza wanyama.

Ili mkulima aweze kupata mazao mengi na bora inashauriwa kutumia dawa za kuzuia magonjwa na wadudu washambuliao mimea na njia zinginezo.

A

B

C

D

E

F

17

Kuvuna, kukausha, kusafisha na kuhifadihiKuvunaMahindi yako tayari kuvuna wakati kikonyo kimekuwa dhaifu na mahindi yanaangalia chini. Mahindi yakishakauka vizuri yanatenganishwa na bua halafu majani ya mhindi kutolewa.

KukaushaKama mahindi hayajakauka vizuri hukaushwa zaidi katika juani siku 3-4 ili kupunguza unyevunyevu kufikia kiwango kinachofaa kwa kuhifadhi (14%). Ni muhimu mahindi yakauke vizuri ili yasioze yakiwekwa ghalani.

Ili kujua kama mahindi yamekauka vizuri, tia mahindi kadhaa kwenye chupa ya soda iliyokauka na uongeze kiganja kimoja cha chumvi. Tingisha chupa halafu uwache itulie kwa dakika tatu. Chumvi ikikwama kando ya chupa, basi mahindi haijakauka vizuri.

KusafishaMahindi yaliyokauka vizuri hupepetwa na vilevile mahindi mabovu huondolewa.

KuhifadhiMahindi safi huchanganya na dawa za kuua wadudu kama vile ‘Actellic Super’ ambayo ni vumbi nyeupe na kisha kuhifadhiwa kwenye ghala.

18

Manufaa ya matumizi ya mboleai). Kuongeza mavunoii). Ubora wa mazaoiii). Kuhifadhi rutuba ya udongoiv). Kuongeza kipato kutokana na mavuno mengi na bora

Mambo muhimu ya kuzingatiaNi muhimu kutumia mbolea za viwandani katika kilimo cha mahindi ili kumuwezesha mkulima kupata mavuno mengi. Lakini ikumbukwe kwamba matumizi ya mbolea ni lazima yaambatane na matumizi ya mbinu nyingine bora za kuzalisha mahindi, kama vile:

• Kuandaa shamba• Matumizi ya mbegu bora• Kupalilia• Kupiga madawa ya kuzuia na kuua wadudu na magonjwa• Kuvuna kwa wakati unaostahili• Kuhifadhi vizuri mahindi

Kwa maelezo zaidi, muone au wasiliana na:1. Bwana/bibi shamba wako.2. Muuza pembejeo aliye karibu nawe.3. Kitivo cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, na taasisi zingine vya utafiti wa

kilimo kama Katrin, Ilonga, Mlingano na Selian (SARI).

19

Jedwali 1. Tafsiri ya matokeo ya vipimo vikuu vine vya upimaji wa udongo kwa ajili ya kilimo

Kipimo Kiwango Ufafanuzi/tafsiri Mapendekezo/Ufafanuzi

pH ya udongo

Ndogo kuliko 5.5 Tindikali kaliWeka chokaa au tumia mbolea zisizo za tindikali kama Minjingu fosfati au Minjingu Mazao kwa kiwango kinachoshauriwa

5.5 hadi 7.0Tindikali ya wastani hadi katikati (neutral)

Mimea mingi hushawi vyema katika udongo wenye pH hizi

7.0 hadi 7.5 Nyongo ya watani Mimea mingi hushawi vyema katika udongo wa pH hizi

Kubwa kuliko 7.5 Nyongo kali Weka madini ya salfa

Naitrojeni (N) (%)

Ndogo kuliko 0.2 Kiasi kidogo

Kiasi hiki hakitoshelezi mahitaji ya naitrojeni kwa mimea. Ni lazima kuweka mbolea ya kupandia yenye naitrojeni kidogo (<20%N) na pia ni lazima kuweka mbolea za kukuzia

0.2 hadi 0.5 Kiasi cha wastaniKiasi hiki hakitoshelezi mahijaji ya naitrojeni kwa mimea kwa msimu mzima. Mbolea za kukuzia zinahitajika ili kukidhi mahitaji ya naitrojeni kwa uzalishaji mzuri

Kubwa kuliko 0.5 Kiasi kikubwaKiasi hiki kinaweza kutosheleza mahitaji ya naitrojeni kwa msimu mmoja. Mbolea za kukuzia zaweza kuwekwa kwa kiwango kidogo

Fosfati (mg/kg)

Ndogo kuliko 15 Kiasi kidogoWeka mbolea za kupandia kwa kiwango kinachoshauriwa

15 hadi 25 Kiasi cha wastaniChaweza kutosheleza mahitaji ya mimea kwa msimu mmoja tu. Weka mbolea za kupandia kwa kiwango kinachoshauriwa ili kuwa na uhakika wa mavuno mengi

Kubwa kuliko 25 Kiasi kikubwa

Haihitaji mbolea za kupandia kwa misimu miwili na kuendelea kutegemea na wingi wa fosfati kwenye udongo. Waweza kuweka kiasi kidogo tu cha mbolea za kupandia (kwa mfano nusu au robo ya kiwango kinachoshauriwa)

Potashi (cmolc/kg)

Ndogo kuliko 0.2 Kiasi kidogoWeka mbolea za kupandia au kukuzia zenye potashi kwa kiwango kikubwa (NPK 10-20-18 au 10-24-18)

0.2 hadi 0.4 Kiasi cha wastaniKiasi hiki kinaweza kutosha kwa misimu miwili kama mabaki ya mazao yataachwa shambani

Kubwa kuliko 0.4 Kiasi kikubwa Haihitaji mbolea ya potashi

*Ufafanuzi ni kutoka Landon (1991)

20

Kufanya kazi kwa pamoja na wadau/wabia kutayarisha taarifa zinazohusu mbinu husishi za afya ya udongo

Chapisho hili ni pato kutoka mradi unaofadhiliwa na AGRA nchini Tanzania uitwao:

‘Scaling up Minjingu phosphate utilization for balanced fertilization of crops in Tanzania - (Mradi wa AGRA - 2009 SHP 016)’ ‘Mradi wa kukuza matumizi ya mbolea za Minjingu fosfati na matumizi sahihi ya mbolea mbalimbali, Tanzania’

na msaada kutoka Africa Soil Health Consortium ambayo inaratibiwa na CABI

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo,Idara ya Sayansi ya UdongoP. O. Box 3001, Morogoro, Tanzania Tel.: +255 23 260 4 649

ISBN 978-9987-9673-5-3