wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu shule ya...

21
Nyaraka ya Kufanyia Kazi k Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya kwanza ya mtoto ni mzazi Mtemi G. Zombwe

Upload: ngoanh

Post on 30-Mar-2019

358 views

Category:

Documents


0 download

TRANSCRIPT

Page 1: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi

HakiElimu imeanzisha Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi (Working Paper Series) kwa lengo la kuchapisha upya makala mbalimbali za uchambuzi katika muundo ambao ni rahisi

ni makala ambazo uandishi wake bado unaendelea, hivyo hazikukusudiwa kuwa ni nyaraka

Maoni yanayotolewa humu ni ya mwandishi (waandishi) mwenyewe na si lazima yawe

fupi zilizo wazi na bayana na tungependelea zaidi ziwe na urefu wa kati ya kurasa sita hadi

kielektroniki kwa kutumia anuani inayooneshwa hapo chini:

HakiElimu

HakiElimu inafanya kazi kuleta usawa, ubora, haki za binadamu na demokrasia katika Elimu, kwa

HakiElimu Nyaraka za Kufanyia KaziSLP 79401 Dar es Salaam TanzaniaSimu (255 22) 2151852 / 3 Faksi (255 22) [email protected] www.hakielimu.org

Nyaraka ya Kufanyia Kazi

k

Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya kwanza ya mtoto ni mzazi

Mtemi G. Zombwe

Page 2: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

1

Wazazi wanavyoweza kuwasadia watoto

kupata elimu

Shule ya kwanza ya mtoto ni Mzazi

Mtemi Gervas Zombwe1

1.0 Utangulizi Ni dhahiri kwamba mchakato wa kumpatia binadamu elimu bora unahusisha vipengele vingi, mbinu nyingi na wadau wengi ambao kwa jitihada za pamoja wanajenga msingi bora wa upatikanaji wa elimu kwa mtu. Lakini katika makundi ya wadua wanaohusika na kumsaidia mtoto kupata elimu, kundi la wazazi na walezi linapaswa kuwa mstari wa mbele kabla ya makundi mengine yoyote. Wajibu wa mzazi kumwandaa mtoto wake kupokea maarifa na kumjengea utayari wa kujifunza ni wajibu muhimu na wa kwanza katika maisha ya malezi. Mwalimu Nyerere amewahi kubainisha mara kadhaa kwamba, wale wenye wajibu wa kufanya kazi na watoto wadogo, ndio kundi pekee lenye umuhimu zaidi katika jamii kwa kuzingatia mustakabali wa taifa letu la kesho. Kama ninavyomnukuu; “…wale wenye wajibu wa kufanya kazi na vijana wa umri mdogo wana nguvu kubwa zisizozidiwa na nguvu za yeyote yule kwa kutilia maanani hali ya baadaye ya jamii. Nguvu hizi zipo katika makundi mawili-wazazi na Walimu.’’(Nyerere. 27Agosti 1966) Wazazi na walezi ni kundi muhimu sana katika jamii linaloweza kuwasaidia watoto kufikia ndoto zao wakiwa kama walimu wa kwanza kwa mtoto. Mzazi ama mlezi anajukumu kubwa la kumjenga mtoto awe mtu wa aina fulani. Watoto wengi hupenda kuiga tabia za wazazi au walezi wao au watu wengine wanaowazunguka katika makuzi yao, hivyo ni vyema kabisa wazazi na walezi kuweza kuelewa majukumu na kazi zao katika malezi ya watoto (kama yalivyoainishwa hapo chini). Katika majukumu haya yote, elimu ni msingi mkubwa katika kumkuza na kumuelekeza kijana au mtoto kukua kwa kufuata maadili, kuwa raia mwema na kumwezesha kujiamini na kumsaidia kupambana na changamoto mbali mbali za maisha. Ni muhimu kundi hili likatimiza wajibu wake huo muhimu ili kulinda taifa letu na watu wake. Elimu ni suala la jamii ambalo mipango na taratibu zake zinahitaji kushirikisha wadau wote katika jamii. Madhumuni ya Elimu kwa ujumla ni kuifanya dunia kuwa mahali pazuri pa kuishi watu wa kizazi cha leo na vizazi vijavyo, wakiwa na uwezo na maarifa ya kupambana na maradhi, ujinga, umaskini, rushwa na unyanyasaji au uonevu wa aina zote kwa maendeleo yao. Inakusudiwa kuwapa watu maarifa na ujuzi watakao utumia vizazi na vizazi ili kuwasaidia kupata njia mpya na bora zaidi za kutatulia matatizo yao ya kiafya, kiuchumi, kijamii na mengine yanayohusu mazingira wanayoishi. (Qorro, 2008).

1 Mtemi Gervas Zombwe ni Mchambuzi wa Sera HakiElimu. Anapatikana kupitia barua pepe

[email protected], au [email protected]

Page 3: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

2

Wazazi wanapaswa kufahamu kuwa Elimu lazima imkomboe binadamu kiakili na kimwili, imuwezeshe binadamu kujikwamua na kumpa uwezo wa kupambana na matatizo au changamoto zinazomkabili katika maisha. Elimu Inapaswa kuipa jamii utambuzi au ujuzi kuwa wao ni nani, wanatoka wapi, wanakwenda wapi, na wajipange vipi ili wafike huko wanakotaka kwenda

2. Malengo ya msingi ya elimu ni

kumkomboa binadamu. ‘Kumkomboa maana yake ni kumweka huru, na kumweka huru kutoka hali au jambo fulani’ (Nyerere 1974). Ina maanisha pia kuwa itamwezesha kama kuna vikwazo basi aweze kuvishinda. Tanzania mara tulipopata uhuru mwaka 1961 tulisema kuwa tuna maadui watatu: ujinga, maradhi na umaskini. Maadui hawa bado tunao hadi leo, tena kwa bahati mbaya na maadui wengine wengi wameongezeka katika nchi yetu kama vile rushwa, ufisadi na uonevu wa aina nyingi za ukiukaji wa misingi ya haki za binadamu. Ni vikwazo ambavyo tunaweza kuvishinda tukipata elimu iliyo bora, ambayo wazazi ndio wadau muhimu zaidi kuifanya elimu kuwa bora na ipatikane kwa usawa na haki. Popote duniani mtoto hujifunza kupitia shule za aina tatu; shule ya kwanza ni elimu isiyo rasmi ambayo inajumuisha maelekezo ya msingi na malezi anayopata mtoto kutoka kwa mzazi au mlezi. Shule hii ndio ya msingi kabisa katika makuzi na maendeleo ya mtoto. Shule ya pili; mtoto anaiga matendo ya mzazi wake kimya kimya na kujaribu kufanya kama anavyoongea au kama anavyofanya kwa utofauti kidogo. Kama mzazi anapenda kupiga kelele na mtoto anaiga kimya kimya, kama mzazi anapenda kutukana, na mtoto anaiga kimya kimya na kama mzazi atakuwa mwenye kuonesha tabia njema na maadili mema basi mara nyingi mtoto naye ataiga hivyo. Wazazi na walezi ndio walimu wa shule hizi mbili za kwanza

3.

Shule ya tatu: hii ni elimu rasmi-ambayo watoto wanaipata darasani wanapojiunga na shule mbalimbali. Aghalabu shule hii ya tatu wananchi wengi wanaifahamu japo wapo baadhi na wachache hawana uhakika wa kile wanachokijua. Na katika elimu rasmi hapa mzazi anakuwa na mchango mdogo. Ukilinganisha na walimu pamoja na wasimamizi wa mchakato wa utoaji elimu. Kwa bahati mbaya, kwa sasa wazazi hawatimizi wajibu wao kikamilifu. Malezi ya watoto yamekuwa duni, na kufanyakazi kuwa ngumu sana kwa walimu shuleni. Ufuatiliaji wa mchakato wa kujifunza na kufundishwa kwa watoto bado ni dhaifu kwa wazazi wengi. Na kibaya zaidi, watoto ambao wanapaswa kuwa shule sasa wanaonekana wako mitaani wakifanya biashara walizotumwa na wazazi wao, aidha kutokana na ugumu wa maisha, uvivu wa baadhi ya wazazi ama baadhi ya wazazi kutoona thamani ya elimu. Wazazi hawana muda wa kukaa na watoto. Hivyo, kila mtoto anakua na kulelewa kwa mazingira ya kubahatisha. Wenye bahati, wanaendelea vizuri; wenye bahati mbaya wanaishia mitaani. Elimu ya watoto wetu

2 Sehemu ya ufafanuzi wa kina juu ya elimukombozi katika makala ya Mhadhiri mwandamizi wa kitivo Idara ya Lugha za kigeni na Isimu: Dk Martha Qorro. Kwenye kitabu chake chenye jina la Elimukombozi, Lugha na Upashanaji Habari nchini Tanzania, katika Muktadha wa Utandawazi. 3 Sehemu ya ufafanuzi wa Mtaalamu wa Hisabati na saikolojia Nderakindo Kessy kuhusu wajibu wa wazazi katika kumsaidia mtoto kupata elimu, mada aliyoitoa kwenye semina ya wazazi kuhusu mbinu rahisi za kukuza uelewa wa hisabati, iliyofanyika Shule ya Msingi Sakana, kibamba tarehe 14.08.2010.

Page 4: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

3

imekua siyo kipaumbele tena kwa wazazi wengi. Kwa sasa kipaumbele ni pesa. Utu na wajibu wetu wa kuwasaidia watoto kupata elimu umezikwa taratibu. Lakini, ikumbukwe kuwa wazazi kutotimiza wajibu wao mkubwa kama ulivyobainishwa hapo chini. Au kuutimiza wajibu huo nusunusu kutokana na sababu zisizo muhimu, kumesababisha kuibuka kwa makundi mabaya ya vijana wasio na dira wala mwelekeo wa maisha. Wazazi waliotimiza wajibu wao katika kuwajenga watoto wao, wanafurahia matunda ya kuzaa. Wana furaha na amani ya kudumu. Na wana maendeleo katika familia zao na jamii zao. Kukwepa jukumu la malezi na kumfuatilia mtoto wako ni kukaribisha balaa au msiba hapo baadaye katika familia yako. Hata vitabu

4 vitakatifu vimebainisha hili. Maana kuna usemi usemao asiyefunzwa na

mamaye hufunzwa na ulimwengu. Hatupaswi kungoja watoto wetu wafunzwe na ulimwengu. Bado tuna fursa ya kuwasaidia ili wawe wazalishaji wazuri katika familia na jamii. Chapisho hili ni kauli ya hamasa kwa wazazi wote. Lina lengo la kufufua upya fikra na dhamira kwa wazazi, kurudisha ari ya kutimiza wajibu wao kama wazazi ili kuwasaidia watoto wetu kupata elimu. Chapisho limefafanua kwa kina hali ilivyo sasa katika jamii. Limeweka bayana mapendekezo ya mikakati mahususi na mbinu ambazo wazazi wanaweza kuzitumia kuwawezesha watoto wao kupata elimu. Tunaamini kitabu hiki kitakuwa chachu kwa wazazi wote; hasa wapenda elimu ili waweze kutekeleza vyema jukumu lao la kuwasaidia watoto wetu kupata elimu. Nawasihi kusoma na kumweleza jirani yako mikakati hii, ili kwa pamoja tuweze kuboresha hadhi na utu wa watoto wetu. Ndipo watakapoweza kufanikiwa kupata elimu bora na hatimaye maisha bora!

2.0 Maana ya Elimu

Sera ya Elimu na Mafunzo (1995) inafafanua elimu kuwa “..ni mchakato ambapo mtu hupata maarifa na ujuzi wa kujitambua na kujiweka sawa katika kupambana na mazingira na mabadiliko ya mara kwa mara ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Aidha kama njia ya mtu kutambua uwezo wake kamili. Elimu ni mchakato wa kumtayarisha mtu kwa njia ya mafunzo, katika mazingira yake na kutekeleza wajibu wake katika jamii. Mwl. Julius Nyerere (1968), alifafanua elimu kama mchakato unaomuandaa mtu aweze kukabili mazingira anayoishi. Maana mchakato huo unampatia mtu maarifa, ujuzi, maadili, stadi za maisha, hamasa ya kufanyakazi na kujitegemea, kujitambua na kutambua majukumu yake katika jamii. Maarifa, ujuzi na stadi hizi ni za mwendelezo hazina kikomo; hivyo elimu ni mchakato usio na mwisho. Hivyo, elimu kwa ujumla wake ni mchakato unaokuza stadi za msingi kwa mtu zinazomuwezesha kuishi kama vile; uwezo wa kufikiri, uwezo wa kutatua matatizo, ubunifu, fikra zenye udadisi, uhodari, ujasiri, weledi na kujiamini. Pia mchakato huu unazaa watu wenye maarifa tele na ujuzi wa kubainisha masuluhisho ya changamoto

4 Bibilia imeweka wazi kwamba, Mwana mpumbavu ni msiba kwa wazazi.

Page 5: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

4

zinazoikabili jamii5. Elimu inakuza Uwezo wa kuvumbua na kuchunguza taarifa,

kuwasiliana na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo katika jamii. Wazazi wanapo mpeleka mtoto shule wanatarajia haya. Yote haya kwa ujumla wake ndio elimu.

3.0 Wajibu wa wazazi na hali ilivyo sasa

Wazazi wana wajibu mkubwa sana katika malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wao. Wajibu wa kwanza kabisa ni kuwakuza watoto tangu wanapozaliwa kwa kuwapatia chakula safi na bora, kuwakinga na kila hali ya hatari. Kuwakinga na magonjwa, maradhi, na mambo mengine yote yanayoweza kuwadhuru watoto wao. Wajibu wa pili ni kuwapatia mahitaji yao muhimu kama vile kuwaandikisha na kuwapatia hati ya kuzaliwa inayohalalisha uraia wao na kupokelewa na jamii na serikali katika kushiriki kwenye shughuli mbalimbali hapo baadae, k.m. kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi. Pia kuwapatia malazi, mavazi pamoja na upendo ili wakue wakiwa karibu zaidi na wazazi wao. Pia, wajibu mwingine wa wazazi ni kuhakikisha watoto wao wanafanikiwa katika maisha yao kwa kuwapatia malezi bora pamoja na maelekezo ya msingi ili wakue kwenye mwelekeo sahihi. Baada ya jukumu la msingi la kuwapatia watoto mahitaji yao ya msingi linalofuata ni elimu; kuanzia nyumbani hadi shuleni. Je wanafanya hivyo. Hali ikoje sasa ndani ya jamii yetu? Ni wazi; wazazi wa leo tumetelekeza kwa kiwango kikubwa sana wajibu wetu muhimu katika kuwajenga na kuwaandaa watoto wetu ili waje kuleta faida kubwa katika jamii. Tunaona wazi kuwa, hata malezi ambayo ni jukumu lao la msingi bado linafanyika hovyo hovyo. Mali na pesa vimetangulizwa mbele. Na sababu ya hili ziko wazi; ni ugumu wa maisha. Lakini, ugumu wa maisha hauwezi kuwa mbadala wa wazazi kutotimiza wajibu wao. Maana, wasipofanya hivyo ugumu wa maisha utaendelea vizazi na vizazi badala ya kuisha. Wazazi wa leo (japo sio wote) hawagusi madaftari ya watoto wao. Wamewasukumizia walimu kila aina ya majukumu na wajibu wao kwa watoto kama wazazi. Hawaendi kwenye mikutano ya wazazi, hawaendi shuleni kuongea na walimu kuhusu maendeleo ya mtoto. Kibaya zaidi, hawakai na mtoto kujaribu kumsikiliza mtoto anasema nini na anataka nini kuhusu taaluma yake. Hatuna muda wa kuwapima watoto wetu kwa kuwapa kitabu au kusoma kitabu pamoja na mtoto ili wajue mtoto anapata nini kwa muda wote awapo shuleni. Pia hatuko tayari kuhoji na kuchambua na kudadisi mambo ambayo hayaendi sawa katika Elimu, wala hatutetei walimu wapate haki zao, hatuwathamini na hatuwaadabishi wanapokosa, kama kutembea na mabinti zetu.japo sisi wazazi ni sehemu ya shule. Wazazi hatuna shauku ya kugharamia vifaa vinavyoweza kumsaidia mtoto kukuza vipaji na akili yake. Wazazi tuko radhi kutembelea gari la milioni 100 kuliko kununua kitabu cha sh 5000 kwa ajili ya mtoto. Wazazi tuko tayari kununua baiskeli nne, lakini hatuko tayari kununua daftari la kujifunzia watoto wetu. Wazazi tuko tayari kusafiri nchi 5 hadi kumi Ulaya na Amerika kuliko kusafiri kilomita 5 kwenda shuleni kwa mtoto wako kujua maendeleo yake. Wazazi tuko tayari kuongea na

5 Mjadala wa mafunzo juu ya umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya jamii, uliofanyika Meatu

Julai 11-14 2010 kwa watendaji wa Halmashauri na kata, ulihitimisha kwa kukubaliana kuwa elimu ni kile anachopata mtoto baada ya kujifunza.

Page 6: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

5

wapambe na marafiki zetu masaa 7 kwenye kilabu ya pombe (baa) au hoteli za kifahari, lakini hatuko tayari kuongea na watoto wetu au walimu wetu kuhusu taaluma za watoto wetu. Wazazi tuko tayari kuchangia harusi 5 kwa mwezi kwa gharama ya laki mbili, lakini hatuko tayari kuchangia ziara za mafunzo za watoto wetu kwenye mbuga za wanyama au maeneo ya kihistoria kujifunza na kujionea rasilimali zetu zilizotukuka. Wazazi tuko tayari kujenga ghorofa la kiwanda na hata kumjengea (nyumba ndogo) nyumba ya kifahari, lakini hatuko tayari kumtengenezea mtoto hata chumba kimoja au sehemu ndogo ya nyumba kama maktaba na eneo lake la kusomea. Tuko tayari kuwa na suti 15 za kifahari lakini hatuko tayari kununua hata kabati moja au shelfu la kuwekea vitabu vya watoto wetu. Na wazazi wengine wanaharibu hata vitabu na madaftari ya watoto kwa kuchana na kuvutia sigara na hata kufungia vitumbua. Kuanzia watawala hadi mwananchi kijijini, wote tunaona kugharamia elimu ni ufujaji wa pesa. Lakini kugharamia vitu vya kifahari kama magari, simu, mavazi ya kifahari na hata pombe za kifahari ndio matumizi sahihi ya pesa. Tukisahau kwamba hata vitu hivyo vya kifahari vimekuwepo kutokana na elimu. Wenye elimu sahihi ndio wanaotengeneza hayo. Wazazi tuko tayari kugharamia msiba (mtu aliyekufa), siasa porojo na mapambo ya mwili kuliko kugharamia vifaa vya mtoto vya kujifunzia. Akina baba wako tayari kugharamia nyumba ndogo lakini hawako tayari kutoa muda wao kuongea na watoto wala kugharamia mahitaji yao. Wazazi tuko tayari kukesha kwenye vilabu (baa) tukiangalia mpira na kuwasifia wachezaji wa Ulaya, lakini hatuko tayari kukaa hata saa moja na watoto wetu kukagua madaftari yao, kuthibitisha ukweli wa ripoti zake na kujifunza pamoja ili kumtia moyo mtoto kwa kile anachojifunza shuleni na kile anachopaswa kufahamu. Eti utandawazi. Laana inayotafuna watanzania kuelekea ujinga wa kudumu! Tunaweza kubadilika!

4.0 Wajibu wa wazazi kutambua malengo ya elimu

Kabla ya kumpeleka mtoto shule, mzazi anawajibu wa kutambua malengo na madhumuni ya elimu katika jamii. Akitambua malengo na madhumuni ya elimu ni rahisi kwake kuwa na matarajio sahihi ya nini mtoto anakwenda kupata shuleni. Mzazi asiyejua malengo ya elimu nchini anampeleka mtoto wake bila kujua anakokwenda. Na ni vigumu mzazi wa namna hiyo kuwa na vigezo mahususi vya kupima kama malengo yamefikiwa au la. Na ndio kosa tunalofanya wazazi wengi. Japo mitaala na silabasi zipo wazazi bado hatutimizi wajibu huu mkubwa wa kujua malengo ya elimu yetu, ili kuweza kuwasaidia vyema watoto wetu kufikia malengo. Mwl Julius Nyerere (1968), aliwahi kusisitiza umuhimu wa wazazi katika jamii kwa kusema kuwa: “... tunatumia fedha nyingi sana zisizolingana na uwezo wetu kuwasomesha watu wachache ili baadaye na wao walete faida kubwa kiasi hichohicho katika nchi. Tunatumia fedha kutafuta faida katika akili za mwanadamu, kama vile tunavyotumia fedha kununua trekta. Na kama vile ambavyo tukinunua trekta tunatarajia kufanyakazi

Page 7: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

6

kubwa zaidi kuliko kazi ya mtu na jembe lake la mkono, vile vile tunatarajia mwanafunzi tuliyemsomesha chuo kikuu kutusaidia kiasi kikubwa zaidi katika kazi za maendeleo kuliko yule ambaye hakupata bahati hiyo”. ( Februari 29, 1968). Bado mitaala, sera za nchi na mipango ya kimikakati ya taifa inatoa ufafanuzi mzuri wa malengo ya elimu hapa nchini, ambayo ni muhimu sana kwa kila mzazi kuyaelewa. Kwa mfano, mwongozo mama (sera ya elimu) wa sekta ya elimu hapa nchini unatoa maelezo ya kina juu ya malengo ya elimu hapa Tanzania. Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka (1995) inayataja malengo ya elimu Tanzania kuwa ni:- • Kuelekeza na kukuza maendeleo na kuboresha haiba ya wananchi wa Tanzania,

rasilimali zao na matumizi bora ya rasilimali hizo katika kuleta maendeleo ya mtu binafsi na ya kitaifa.

• Kukuza kujifunza na matumizi bora ya kujua kusoma, kuandika na kuhesabu, maarifa na stadi za kijamii, kisayansi, kiufundi, kiteknolojia, kiutaalamu, na kwa aina nyingine ya ujuzi, stadi na uelewa katika maendeleo na uboreshaji wa hali ya mtu na jamii.

• Kuendeleza na kukuza kujiamini na kuwa na moyo wa kudadisi, weledi na heshima kwa utu na haki za binadamu, na kuwa tayari kufanya kazi kwa kujiendeleza na kwa maendeleo ya taifa.

• Kuwezesha na kupanua upeo wa kupata, kuboresha na kukuza stadi za maisha za kiakili, ki-vitendo, za uzalishaji na nyingine zitakiwazo katika kutosheleza mahitaji ya kiuchumi na kiviwanda yanayobadilika badilika mara kwa mara.

• Kumuwezesha kila raia kuelewa misingi ya katiba ya taifa pamoja na haki za binadamu na uraia, wajibu na majukumu yanayoendana nayo.

• Kukuza utashi wa kuheshimu kazi za kujiajiri na kuajiriwa na uboreshaji wa mwenendo katika sekta za uzalishaji na huduma;

• Kujenga misingi ya maadili ya kitaifa yanayokubalika, ushirikiano wa kimataifa na kitaifa, amani na sheria kwa njia ya kujifunza, kuelewa na kuzingatia vipengele vya katiba ya taifa na matamko mengine ya msingi ya kimataifa.

Pia, Nelson Mandela (1981) amewahi kuifafanua kwa kusema, “..elimu inawapa wanajamii stadi za mawasiliano na kujiamini ili wawasiliane kwa usahihi na kwa manufaa..msomi yeyote anapaswa kuwa na ujasiri wa kujieleza, kudadisi, na kuhoji mienendo isiyoenda sawa. Aidha kuhoji na kudadisi kunapaswa kuambatana na mibadala ya suluhu za matatizo. Watu wasio na uwezo wa kuhoji, kujieleza na kutumia haki ya kupata habari na kutoa habari ni mazao ya elimu duni”. Msomi sio mtu wa kukubali kila kitu, kuona kila kitu na kunyamaza na kujivika ububu bandia. Jamii inamhitaji msomi aiongoze kwenye nuru ya maendeleo kupitia michango ya mawazo katika mijadala, makongamano, katika familia na kwenye jamii kwa ujumla. Msomi asiyefanya hivi anakuwa msaliti kwa jamii iliyomsomesha na kwa taifa zima

5.0 Mbinu za kuwasaidia watoto kupata elimu Ziko mbinu nyingi sana ambazo wazazi na walezi wanaweza kuzitumia kufanikisha makuzi na elimu ya watoto wao. Mbinu hizi sio pekee na wala siyo mpya. Ni jitihada za kila siku ambazo tunazifanya kwa kujua ama bila kujua. Hapa zimeainishwa mbinu chache ambazo tunadhani zinaweza kumsadia mzazi kufanikisha makuzi ya mwanaye

Page 8: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

7

na hasa kumsaidia mtoto wake kupata mafanikio ki-elimu na kimaisha. Mbinu hizo ni kama zifuatazao:

5.1 Malezi bora nyumbani kwa kumpa maadili mema bila kumfundisha ukondoo na nidhamu ya woga. Tunaweza kuwajengea uwezo watoto wetu kutambua uwezo wao ili kujijengea msingi mzuri katika maisha yao kwa kuwapa maadili ya msingi tangu wakiwa watoto wadogo nyumbani. Wazazi tumekaa mara ngapi na watoto wetu kuwauliza wanataka kuwa akina nani wakikua? Na tumefanya jitihada gani kuhakikisha wanatimiza ndoto zao? Je tumewajenga kwa maadili husika na kuvifanya vipaji vyao vichanue? Ni muhimu sana kutambua vipaji vya watoto na kumjengea msingi mzuri katika juhudi zake za kutimiza ndoto zake. Ni jukumu la mzazi kumsikiliza mtoto na kumpatia msaada atakaohitaji. Imani ya mzazi juu ya mtoto ni muhimu sana, kwa sababu watoto wenyewe wana hulka asilia ya kujiamini na kuthubutu kila wakati.

Shuleni, walimu wana mchango mkubwa sana katika kumsaidia mtoto kutambua uwezo au kipaji chake, kwani huwasimamia katika maendeleo yao ya elimu na makuzi kila siku. Mwalimu humjua zaidi mtoto katika uwezo wake darasani na jinsi anavyoshirikiana na wenzake, kujituma, kufikiri, kuuliza, udadisi, ubunifu na mengineyo. Mwalimu mzuri siyo yule tu anayeingia darasani bila kukosa na kufundisha, bali ni yule mwenye uwezo wa kutambua vipaji vya mwanafunzi wake, kumjenga kitaaluma na kinidhamu. Kwa kutambua uwezo wa mwanafunzi mwalimu amshauri mzazi ni jinsi gani anaweza kumuendeleza kwani wanafunzi wengi wana uwezo. Ila kwa kushindwa kupewa muongozo na wazazi au walimu wao hujikuta wanahangaika kujitambua na kushindwa kujua vipaji na uwezo wao.

Wazazi wote ambao ni sehemu ya jamii inayomzunguka mtoto haina budi kumsaidia katika kujiendeleza. Ile dhana potofu iliyojengeka kwamba mtoto hatakiwi kucheza au kushiriki katika michezo inabidi ipigwe vita kwani ushiriki katika michezo ni mojawapo ya njia ya kutambua kipaji cha mtoto, na ni njia inayo mwendeleza mtoto haraka kiakili na kiafya. Jamii isaidie maendeleo ya mtoto kwani katika ukuaji wake huwezi kutenga jamii inayomzunguka. Majirani na watu wa karibu washiriki katika kumjenga mtoto, kuwashauri wazazi juu ya maendeleo ya mtoto ni jambo zuri.

5.2 Kumsimulia hadithi au ngano zenye kumjenga mtoto na sio za kumbomoa. Wazazi wengi tumeacha wajibu huu kwa watoto wetu. Zamani yalijengeka mazoea kuwa mtu anayesimulia hadithi ni babu au bibi. Lakini jukumu hili ni la wazazi wa mtoto wenyewe hasa ukizingatia babu na bibi wa leo hawaishi na wajukuu wao. Kama mzazi unaweza kukaa vikao vya harusi masaa 4 au zaidi, unaweza kuhudhuria mikutano ya kampeni siku nzima, na unaweza kulinda matokeo ya mgombea wako usiku mzima.

Unashindwaje kumsimulia mtoto wako hadithi au ngano za kumpa mafunzo? Utakosaje muda wa kukaa na mtoto na kumsimulia hadithi nzuri zenye tunu ya mila na utamaduni wetu ili kumjengea hamu ya kuipenda nchi na mila zetu, pia kufaulu katika masomo yake? Wazazi tunaweza kufanya hivi. Tukijitahidi kufanya hivyo, watoto wetu watakuwa katika msingi mzuri wa maadili, maarifa na upana wa fikra zitakazowasaidia wao kuishi maisha mema siku zijazo.

5.3 Kumpa majibu sahihi kila anapouliza swali na kumpongeza kwa kufanya

hivyo. Hii ni mbinu nzuri sana ya wazazi kuwatia moyo watoto wao. Mara nyingi watoto wanakuwa na maswali mengi maana wanaona vingi katika jamii. Kila wanachokiona wanataka kuwa na ufahamu nacho na hata kukigusa ili wajiridhishe.

Page 9: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

8

Baadhi ya wazazi wakiulizwa maswali na watoto wao, wanakuwa wakali sana. Wanatoa majibu kwa ukali. Wengine hawajibu na kuwafukuza watoto kwa kudai wanasumbuliwa.

Baadhi ya wazazi wanajaribu hata kuwadanganya watoto wao ilimradi tu waondoe kero hiyo ya kuulizwa maswali. Mathalani, mzazi anaondoka na kumuahidi mtoto wake kuwa “nitakuletea pipi, baki ucheze” lakini akirudi jioni amelewa na hana pipi. Mtoto akimkumbusha, pipi yangu iko wapi? Mzazi anamdanganya, au anamkaripia mtoto kwa kudai hakuwa na pesa au kasahau. Kama hukuwa na pesa mbona umelewa? Umekunywa pombe bure? Hii sio sahihi. Mzazi kumbuka kuwa mtoto anapouliza maswali, yuko katika mchakato wa makuzi, kujifunza na hasa kukuza akili na ufahamu. Jibu la mzazi ndiyo kithibitisho cha ukweli wa jambo ambalo mtoto anataka kufahamu. Mzazi ukiwa muongo, mdanganyifu, mkali, mdokozi, msema hovyo; na mtoto ataiga hayo. Wazazi na walezi tuacheni jamani! Tukumbuke pia kuwasikiliza na kuwapa majibu sahihi kunawatia moyo na kuna wajengea maarifa ya mwanzo. Watoto huwa hawasahau kiurahisi mambo wanayojifunza wenyewe na mambo wanayotaka kujua

6. Tusiwadanganye. Ndio

maana mtoto anaweza kutoa ushahidi mahakamani kwa kile alichokiona na kile alichokisikia. Hawasahau kiurahisi. 5.4 Kumnunulia mahitaji yake muhimu kadiri ya uwezo wako unavyokuruhusu- wazazi wote tunaweza kumpa mtoto mahitaji yake kadri ya uwezo wetu, kwenye mazingira yetu. Hata kama mzazi anachangamoto nyingi za kimaisha. Bado anaweza kubuni vifaa vya kujifunzia kutokana na mazingira alipo. Wazazi wengi wanajidanganya kuwa mahitaji ya mtoto yanaweza kupatikana tu kwenye maduka ya kifahari au mijini. Wanajidanganya kuwa mahitaji ya mtoto yananunuliwa kwa fedha tu. Mtoto hahitaji vitu vya madukani au Super market. Mtoto siku zote anahitaji vifaa vya kuchezea bila kuchagua wala kubagua. Kama uko kijijini unaweza kumpatia majani ya miti, fimbo, mabua, mtoto anacheza bila shida na kukuza akili yake. Tena muda mwingi mtoto hujitafutia mwenyewe vifaa vya kuchezea. Wazazi wengi hasa mijini wanashindwa kuwapatia vifaa vya kuchezea watoto wao, eti kisa hawana fedha. Ukweli ni kwamba tatizo sio pesa ni kukosa ubunifu!

Hata kama wewe mzazi ni fukara, kuwa mbunifu. Kama mtoto anahitaji toi la gari ili achezee unaweza hata kutengeneza maboksi likawa kama gari ukampa achezee. Na mtoto wanaridhika na anaendelea na shughuli zake. Kumfokea mtoto eti kwa sababu kalilia kitu ambacho huna uwezo nacho sio sahihi. Mzazi ni mbunifu. Hivyo, wote tunapaswa kuwa wabunifu. Vifaa vya kuchezea watoto pamoja na uwanja wa kuchezea ni dhana muhimu sana kwa kumjenga mtoto. Ndio maana hata shuleni kuna viwanja vya kuchezea. Ni lazima! Vivyo hivyo, hata nyumbani mtoto anapaswa kuwa na muda wa kucheza pamoja na vifaa vya kuchezea bila kujali ni vya aina gani. Hapo ndipo utakapoona kukua kwa fikra na ubunifu wa mtoto wako. Ni muhimu sana kwa maendeleo na makuzi yake

6Hata Mhadhiri mwandamizi wa Saikoloji ya ualimu. Mama Tungaraza, amesisitiza sana juu ya malezi ya kumkuza mtoto kwenye Mihadhara yake kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Page 10: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

9

yenye vipawa vya aina mbalimbali. Mtoto anayekosa fursa ya kucheza hudumaa kiakili na kudhoofika afya yake ya mwili.

5.5 Kumjengea matarajio makubwa na faida kubwa ya elimu kwa kumuonesha mifano halisi ya faida ya kusoma. Ni jambo muhimu sana kwa wazazi kuwajengea watoto wao matarajio makubwa ya kujifunza. Mzazi anapaswa kumweleza ukweli mtoto wake kuhusu faida za elimu na kujifunza. Mzazi anapaswa kumuonesha mtoto wake mifano halisi ya watu waliofanikiwa kutokana na elimu. Unaweza kumuonesha watu mashuhuri waliofikia hadhi hizo kutokana na elimu. Muoneshe wafanyabiashara mahiri waliofika hapo kutokana na elimu. Mkumbushe madaktari bingwa waliomtibu alipokuwa anaumwa ili ajue umuhimu wa kusoma. Muelezee namna wasomi wanavyo leta mabadiliko katika jamii kwa kubuni miradi na kuziendeleza jamii zao. Usisite kumkumbusha na kumtajia jinsi wanasayansi wanavyoichunguza na kuvumbua mambo mbalimbali duniani kutokana na kupata elimu, watu wanaozitumia rasilimali vizuri ni wasomi. Na mwisho muoneshe vifaa vya elektroniki pamoja na teknolojia kubwa kama vile ndege, kompyuta, Televisheni, Magari na vinginevyo, mwambie kuwa waliotengeneza hayo waliipenda shule; na walisoma. Hivyo na yeye kama anataka kupata hayo inambidi asome kwa bidii.

5.6 Kumtia moyo anapoonekana kukata tamaa hasa akifeli masomo sio kumlaumu au kumkatisha tamaa. Watoto wengi huwa hawapendi kufanya vibaya katika masomo yao. Hata hivyo, hali hiyo hutokea wakati fulani. Kila inapotokea watoto huwa na huzuni au hofu ndani ya mioyo yao. Wazazi wanapaswa kuwatia moyo watoto wao kwa kuwapongeza hata kwa kile kidogo walichopata na kuwapa mbinu mbadala za kuweza kufanikisha zaidi. Tumezoea kuwafokea watoto wetu wanapofanya kosa, na hasa wanaposhindwa masomo yao tukidhani kuwa wamependa kufanya vibaya au wazembe. Sio sahihi! Mtoto hata kama amefanya kosa-hasa makosa ya kitaaluma anahitaji kutiwa moyo na kuelekezwa zaidi. Maana safari yake kitaaluma bado ndefu sana. Hili si jukumu la mtu mwingine; bali ni mzazi wa mtoto mwenyewe. Kuwafokea na kuwadunisha kwa kuwaita wajinga, wapumbavu, mbwa, wazembe, eti kwa sababu wamefeli si mbinu bora ya kuwasaidia watoto. Wengine tunathubutu hata kuwapa majina ya ajabu ajabu. Mfano, mtoto wangu kilaza, taburalasa, mjinga, haelewi. Majina haya yanajenga uasi wa kudumu ndani ya moyo wa mtoto. Unamjengea mtoto wako kaburi la kitaaluma na kukaribisha laana katika familia yako. Hata kama mtoto amepata sifuri. Yeye sio kilaza wala mjinga. Kuna sababu za kupata hivyo, msikilize na kuwa karibu naye. Utagundua tatizo; litatue na mtoto wako atafanikiwa huko mbele siku zijazo. Tusiwakatishe tamaa watoto wetu, bali tuwatie moyo na kuwachochea kufanya vizuri zaidi. Na Siku zote tukumbuke; Watoto wadogo wote wana haki

7 ya kufanya makosa!

5.7 Mchunguze na kumsoma mtoto wako ili ujue ana uwezo gani wa kuelewa au anapenda nini. Kisha msaidie kufanikisha anachokipenda. Wazazi tuna wajibu wa kuwafanyia utafiti watoto wetu na kugundua vipaji vyao, matamanio yao, hobi zao, na vitu au fani wanazopendelea. Kugundua hobi au vipaji vya watoto ni muhimu sana ili kuwa na uhakika wa kuvikuza. Mzazi anayejua kipaji au hobi ya mtoto wake huweza kumsaidia mtoto kufikia ndoto yake. Wazazi wengi hatufanyi vizuri jukumu hili. Wengi tunawalazimisha watoto wetu kufanya vitu ambavyo

7 Tamko la Kimataifa juu ya Haki za Mtoto la mwaka 1989, linabainisha wazi kuwa mtoto ana haki ya kufanya makosa

Page 11: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

10

hawana hobi navyo na wala vipaji vyao haviko huko. Kwa mfano, una mkuta mzazi yeye ni Mhandisi anajaribu kumlazimisha mtoto wake mwenye kipaji cha kuimba na kuchora kuwa mhandisi. Mtoto anahangaika bila mafanikio, mwisho wake anakata tamaa. Anaona shule chungu!

Lakini kama mzazi angegundua kipaji cha mtoto wake kuwa ni kuchora angeweza kumsaidia mtoto huyo kuwa mchoraji maarufu duniani. Akajikusanyia kipato kikubwa na hadhi kubwa katika jamii. Na hatimaye akaweza kuchangia maendeleo ya jamii yake. Maana hata rangi za kompyuta tunazoziona zimetokana na watu wenye vipaji vya kuchanganya rangi na kuchora. Kumlazimisha mtoto wako kufuata hobi asiyopenda kunajenga utumwa ndani ya fikra zake. Na kunazuia ustawi wa maisha yake kwa kuua vipaji vyake. Mtoto mwenye kipaji cha kucheza mpira, tambua kipaji chake na msaidie kufikia viwango vya juu vya kimataifa, atafanikiwa sana katika maisha yake kuliko kumlazimisha kusomea sheria unayodhani ndio sahihi.

5.8 Hakikisha ana furaha muda wote kadiri uwezavyo. Kuwa na furaha na amani moyoni ni jambo muhimu sana katika makuzi na maendeleo ya watoto. Kwa kawaida, watoto wameumbwa na furaha halisia. Kila mtoto anazaliwa katika hali hiyo. Ili aweze kufikiri vizuri ni lazima awe na furaha na amani ya moyo. Ndipo fikra zake na mawazo yake yanafunguka zaidi. Mathalani, Jaribu kumwangalia hata mtoto mchanga kabisa aliyezaliwa jana, ana uwezo wa kucheka mara kwa mara. Tena chunguza mahali wanapocheza watoto. Mara nyingi huwa ni kelele muda wote. Lakini asilimia 90 ya kelele zao ni maneno ya furaha, kuimba na kucheka. Furaha ndio inaleta ukamilifu wa ubinadamu wa mtoto. Ni sehemu ya utu wao! Mtoto akiwa hana furaha hawezi kuwa tayari kupokea mafunzo wala maarifa yoyote. Hawezi kushiriki michezo kikamilifu, hawezi kuwa huru kuonesha mawazo na vipaji vyake. Hivyo, wazazi tunapaswa kuhakikisha watoto wetu wana furaha muda wote ili waweze kujifunza vyema na kuruhusu vipaji vyao kuchanua. Mtoto mwenye huzuni na masikitiko muda wote ana fursa finyu ya kukuza vipaji vyake na kujifunza

8.

5.9 Mfahamishe vyanzo muhimu vya maarifa na taarifa, ili ajenge mazoea ya kufuatilia na kutafuta maarifa tangu akiwa mdogo. Kwa mfano, muelekeze vipindi muhimu ambavyo anapaswa kuvisikiliza kwenye Luninga au Redio, kama vile taarifa ya habari, na vipindi vingine. Mweleze kuwa magazeti yanayouzwa kila mahali hasa mijini ni chanzo kikubwa sana cha taarifa na maarifa-lakini aepuke yale magazeti ya udaku. Msisitizie kuwa anapaswa kusoma vitabu vya aina mbalimbali kulingana na ngazi yake na umri wake maana vitabu ndio kisima cha maarifa yote hapa ulimwenguni.

Muoneshe mfano wa kusoma pamoja naye kitabu. Mtafutie habari nzuri itakayo mfurahisha na kumpa hamu ya kusoma. Na pindi ukiwa naye soma kwa raha na furaha ili ajue kusoma sio karaha ni raha kabisa. Kumbuka, ukimsisitiza mtoto kusoma wakati wewe mzazi hajawahi kukuona hata siku moja ukisoma, atahisi unamdanganya. Maana watoto hujifunza vizuri zaidi kwa kuona mifano na kuiga. Hata kama mzazi hupendi kusoma basi mpeleke maeneo ambayo atakutana na wasomi wenzake kama vile maktaba kwenye maeneo ya watoto. Msaidie au mwandikishe maktaba za taifa kama zipo eneo unaloishi. Na mhimize kwenda kusoma kwa kumweleza umuhimu wa maktaba, kwenda shuleni, kambi za watoto.n.k 8 Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa, watoto wanapocheza ndio karakana ya kuandaa watalaamu katika jamii ya leo na kesho

Page 12: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

11

Kwa wale wenye fursa ya kuwa na mtandao wa intaneti, hakikisha mtoto wako anafahamu kompyuta. Tena kwa wale watoto wenye umri mkubwa kidogo ni muhimu wafahamu hata matumizi ya intaneti ili waanze kuchukua maarifa na taarifa kwenye vyanzo hivyo muhimu. Kama ni vijijini kuna maeneo mengi yenye taarifa kama vile maeneo ya kihistoria, lakini pia hadithi za wazee na vitabu vya shuleni vinaweza kuwasaidia sana watoto kufanikisha maisha yao.

5.10 Kagua madaftari yake mara kwa mara ili ubaini ubora wake na udhaifu wake. Pia chunguza sana kazi za walimu. Maana walimu wengine wanafundisha uongo. Hili ni eneo ambalo wazazi wengi hatufanyi. Ni muhimu sana kwa mzazi kuwa na utamaduni wa kukagua kazi na madaftari ya mtoto ili kujua maendeleo yake. Mara nyingi ripoti za walimu hazilingani na uhalisia. Walimu wengi hasa shule binafsi wanaandika ripoti za maendeleo ya wanafunzi kwa kuziongezea mambo na kuzipamba. Unajikuta mzazi anakuwa na matarajio makubwa kwa mtoto wake, kumbe hajui kitu. Mzazi unapokagua madaftari ya mwanao, unaonesha unajali. Utagundua ubora wa kazi za mtoto wako au udhaifu wake. Utaona aina ya mwandiko anaoandika mtoto wako. Utaona mahali fulani anafanyiwa kazi na wengine-hivyo utapaswa kuchukua hatua. Kwa wazazi wanaofuatilia watagundua makosa ya mtoto na makosa ya mwalimu. Na hivyo, kuanza kutafuta suluhu za mapungufu hayo.

Ukiyabaini mapungufu utakuwa na uwezo wa kuwakosoa walimu na kuwashauri kufanya vizuri zaidi. Na hata kama mzazi ulikuwa huna tabia ya kukutana na walimu mara kwa mara, ukijenga mazoea ya kukagua madaftari ya watoto wako utapata hamu ya kufuatilia mchakato wa kujifunza na kufundisha. Maana kuna masuala utahitaji kuyajua, au kupata ufafanuzi toka kwa mwalimu. Lakini, pia utakuwa na fursa ya kujua jinsi walimu katika shule ya mtoto wako walivyo makini au wasivyo makini. Ndipo utaweza pia kutoa maoni yako ya kujenga siku ya mkutano wa wazazi. Tusikague tu masanduku ya nguo, magari yetu, mifugo yetu, mashamba yetu, misitu yetu. Tukague na kufuatilia mchakato wa kujifunza wa watoto wetu. Tutagundua mengi na kubaini mikakati ya kuwasaidia. Bila kufanya hivyo hatuwezi kubaini ukweli wa hali ya utendaji wa watoto wetu na walimu wao.

5.11 Usimjengee mtoto wako mtazamo hasi kwa walimu wake, hata kama walimu ni dhaifu. Mfanye awaheshimu na kuwapenda. Hii itamsaidia sana mtoto kufanikisha katika maisha yake. Kuna baadhi ya wazazi wamefanya makosa makubwa sana ya kuwadharau walimu wa watoto wao, na kuwafundisha watoto wao kuwadharau walimu. Hili ni kosa kubwa. Mwalimu kabla hajasema neno lolote, uwepo wake tu darasani ni elimu. Kwa sababu mtoto anaiga mambo mengi sana toka kwa mwalimu kabla ya kusikiliza na kufanya. Cha muhimu ni kumwandaa ili aweze kuchuja makapi na pumba. Na kubwa zaidi aweze kuujua ukweli na kuutetea ukweli muda wote, sio kupambana na walimu.

Mwalimu ana falsafa ya kuweza kumtoa mtoto kwenye ndoto yake ya udaktari na kumpeleka kwenye makundi ya wavuta bangi. Mwalimu ndiye anayekaa muda mrefu na mtoto kuliko hata mzazi. Hivyo, muelekeze mtoto kumheshimu mwalimu na kumpenda zaidi ili aweze kujifunza mengi. Ndio maana siku zote wataalamu na wana harakati wamesisitiza umuhimu wa kuwa na walimu wenye taaluma sahihi ili waweze kuchangia malezi na makuzi ya watoto kwa umahiri, weledi na haiba kubwa. Ni muhimu sana kwa wazazi wa watoto walio shuleni kuwa karibu na shule, pia kuwa karibu na walimu.

Ikumbukwe kwamba; kwa muda mrefu sana tumebaki kwenye kifungo cha mzunguko wa hali ngumu na umaskini wa ubunifu kutokana na kushindwa kuzalisha

Page 13: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

12

watu wenye maarifa na stadi za kushindana. Hali hii ni kwa sababu ya kuviviza na kuvidunisha vipaji vya watoto wakiwa wadogo. Mzazi lazima ajue mtoto anafanya nini shuleni, ana uwezo gani, ana matatizo gani ili ayatatue au kushirikiana na mwalimu kuyatatua.

Mzazi anapokuwa mbali na mwalimu ni vigumu mno kwa mtoto kufanikisha lengo la kuwa shule. Kuwaachia walimu tu sio sahihi. Ni kuwakatisha tamaa walimu.Tuwakunje samaki nyumbani wangali wabichi, maana wakisha kauka walimu hawataweza kuwakunja!

5.12 Msikilize zaidi mnapo tofautiana kuhusu masuluhisho ya matatizo yake. Kosa kubwa tunalofanya wazazi wengi ni kudhani kwamba mtoto mdogo hana akili, hana mawazo ya msingi, hawezi kutoa maamuzi wala kufikiri jambo la msingi. Hivyo, wazazi tu ndio wanapaswa kufanya haya badala yake. Ni kosa! Watoto wote wana akili, vipaji, werevu, na hata uwezo wa kufanya maamuzi. Ili kukuza na kuendeleza vipaji vyao wazazi tunapaswa kuwasikiliza zaidi watoto wanachotaka au wanachopanga na kufikiri kufanya. Tena kwa maoni yangu mzazi anapaswa kumsikiliza kwa umakini sana mtoto wake pale wanapo tofautiana ili afahamu sababu za kutofautiana na kubuni masuluhisho sahihi ya tofauti hizo.

Mzazi anatakiwa kwenda naye taratibu mtoto wake aliye tofautiana hadi aweze kumshawishi kukubaliana na kilichosemwa. Au mzazi kukubaliana na matakwa au mawazo ya mtoto kama ni ya msingi, hata kama hujapendezwa nayo. Maana mtoto anaamini fikra zake kuliko fikra za mtu mwingine yeyote

9. Na pale fikra na maono

yake yakivizwa, kuvurugwa, kuvunjwa moyo au kudhauriwa, mtoto anajenga uasi wa kudumu kwenye fikra zake na mitazamo yake. Matokeo ya udhaifu huu ni hali mbaya zaidi ya ukuaji wa mtoto ambayo inapelekea kuua kabisa matarajio na ndoto za mtoto. Baadaye anageuka kuwa mzigo kwa familia kutokana na kushindwa kufanikiwa katika maisha yake. Wa kulaumiwa hapa sio mwalimu. Ni mzazi aliyeshindwa kumsikiliza mtoto hadi akamvunja moyo.

5.13 Mpe uhuru wa kufurahisha nafsi yake kwa kucheza na wenzake na kushiriki tafrija za makundi rika. Mtoto kushiriki michezo pamoja na wenzake wenye rika moja, ni jambo muhimu sana kwa makuzi na maendeleo yake ya kitaaluma. Wazazi ni lazima wawape watoto uhuru wa kucheza zaidi na kushirikiana na wenzao. Katika makundi rika ndimo vipaji vyao na akili hukuzwa na kuchanua kikamilifu. Maana wakiwa katika makundi na wenzao wanakuwa na uhuru mkubwa wa kutoa mawazo na kuonesha kila talanta waliyonayo. Jambo la msingi ni kuwapa angalizo la kuwa waangalifu katika kuchagua mambo ya kuiga kutoka makundi rika. Wazazi kuwafungia majumbani watoto ni kuwafanya kuwa mazezeta. Ili mtoto afanikishe maisha yake na elimu yake lazima ashirikiane na wenzake, hasa kwa kucheza na kujumuika na wenzake kwa mambo mbalimbali kama midahalo, makongamano au kushiriki kambi za watoto n.k.

5.14 Mshauri mara kwa mara anapotaka kupotoka. Kama mzazi, mpe sababu za wewe kumshauri na umuhimu wa ushauri wako ili aache. Usimkanye na kumfokea kwa hasira-muelimishe taratibu. Watoto mara nyingi hukata tamaa mapema kama

9 Wanasaikolojia wa makuzi na maendeleo ya watoto wamethibitisha kuwa mtoto huamini

fikra zake zaidi kuliko za mwingine.

Page 14: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

13

mtazamo wa mzazi au mlezi ni hasi juu ya jambo analolifanya. Wazazi tunapaswa kuwaelimisha watoto wanapofanya makosa na sio kukimbilia adhabu za kumpiga, kumtukana, au kumuonesha ishara mbaya usoni au mwilini. Mtoto akifanya kosa ni sehemu ya kujifunza. Na ana haki ya kufanya makosa. Akielimishwa ni vigumu kufanya makosa. Tuwakosoe na kuwaelimisha kwa upendo. Tuyabebe madhaifu yao kwa upendo. Huku tukijua udhaifu huu ni wa kila mtu. Fikiria: baba akirudi amelewa na kuvunja bilauri au kikombe nani humfokea au kumpiga? Mama akikosea na akamwaga mboga jikoni nani humpiga ua kumfokea?

5.15 Hakikisha anakuwa katika mazingra salama muda wote, awapo shuleni, maktaba au nyumbani. Tunaposema mazingira salama tuna maanisha pamoja na usalama wake kimwili, usafi wake, maeneo anayotembelea, vyakula anavyokula na pia utulivu wake wa akili. Mtoto siku zote yuko huru. Anapenda kuzunguka kila mahali na kucheza. Akiwa katika mazingira hatarishi mara nyingi hushindwa kuonesha vipaji vyake na hukosa muda wa kujifunza zaidi.

Mathalani, watoto katika miji mikubwa kama Dar es salaam wanasoma shule za mbali sana. Wengine wanalazimika kusafiri umbali mkubwa sana toka makwao. Wanaamka usiku wa manane kupanda mabasi. Wengine wanachelewa mabasi jioni na kufika nyumbani usiku wakiwa wamechoka hoi. Na baadhi hupata matatizo njiani. Huko nako vijijini watoto wanavuka msitu mkubwa kufuata shule. Katikati ya misitu kuna wanyama na watu wabaya. Haya mazingira yote si salama kwa mtoto

10 (HakiElimu,

2008).

Mtoto anakuwa na hofu siku zote. Na hata akiwa shule anafikiri namna ya kuvuka pori lililo katikati ya nyumbani na shuleni kwake. Au kwa wale wa miji mikubwa kama Dar es salaam wanawaza namna ya kupambana na makondakta wasio na maadili. Wazazi tujitahidi kuwaandikisha watoto wetu kwenye shule za karibu na mazingira yetu. Kama ni mbali ni bora wasindikizwe au kutafuta namna ya kuwalinda ili wasipate msongo wa mawazo. Hofu inazuia utayari wa akili ya mtoto kupokea mafunzo.

5.16 Mpunguzie kazi za nyumbani; lakini mpe kazi za kujifunza kwa wingi ili akuze maarifa. Katika jamii zetu watoto hasa wa kike wamekuwa ni msaada mkubwa katika familia kusaidia majukumu madogo madogo ya kupika, na shughuli nyingine za nyumbani na shambani. Baadhi ya wazazi wanafikiri mtoto wa kike ni punda wa kumfanyisha kazi nyingi za nyumbani bila kuchoka wala kupumzika. Si kweli. Mtoto anapochoka, uwezo wake wa kufikiri unapungua sana. Na hawezi tena kuwa tayari kujifunza. Wazazi tunapaswa kufahamu kwamba, ukimwandikisha shule mtoto, huyu tayari anakuwa amepata kazi maalumu ya kufanya. Yaani- kusoma ndio inakuwa kazi yake.

Hivyo, anapaswa atumie muda mwingi kusoma, kwenda shule, kucheza, kufanya mazoezi na kazi za kitaaluma na hata kujisomea vitabu. Akirudi nyumbani pia anapaswa kuwa na muda mwingi wa kuyaendeleza haya. Lakini baadhi ya wazazi wanadhani mtoto akirudi toka shule basi, hakuna tena masuala ya usomaji nyumbani. Sio kweli. Nyumbani ni shule pia. Mpe muda wa kutosha mtoto ili akuze maarifa. Kitu cha kusikitisha sana ni kwamba, baadhi ya wazazi wanawatumia watoto wao kama chanzo cha mapato. Hawawapi hata muda wa kusoma wala kwenda shule.

10Wilayani Simanjiro, watoto katika baadhi ya shule wanalazimika kutembea karibu kilomita 15 kukatisha msitu huku wakiwa na njaa. Hii imeleta athari kubwa kielimu.

Page 15: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

14

Hasa watoto wa kike wanatumika sana kufanya biashara ndogo ndogo ili kuingiza kipato cha familia. Eti wazazi wanatumia kigezo kwamba watoto wa kike ni waaminifu sana. Wanarudisha fedha na kuleta mapato bila ujanja ujanja kuliko wanaume, ndio maana wanatumiwa sana na wazazi kuuza biashara ndogondogo

11. Pamoja na uaminifu

wao, isiwe kigezo cha kuwatumia kuuza biashara. Waacheni wasome shule watapata manufaa makubwa ambayo yatakuja kuwanufaisha nanyi wazazi.

5.17 Kwenye uhaba wa walimu tafuta walimu wa ziada wawasaidie watoto ili kukidhi mahitaji yao ya kimasomo. Wazazi wengi tunafanya kosa kubwa la kudharau umuhimu wa walimu kwa maendeleo ya taaluma za watoto wetu. Vipo vijiji ambavyo shule zinakuwa na walimu wawili. Lakini, kijiji kina wakazi laki mbili. Watoto wa wanakijiji wanakosa elimu kisa hakuna walimu. Bila mwalimu darasani hakuna elimu.

Majengo mazuri hayasaidii lolote kama hakuna mwalimu. Mwalimu pekee ndio msingi wa elimu ya mtoto wako awapo shuleni. Wazazi, ni jukumu letu kuhakikisha watoto wetu wanafundishwa, tena wafundishwe vizuri na ukweli. Sio kudanganywa kama baadhi ya walimu wasio na taaluma wanavyofanya sasa. Kama hakuna mwalimu shuleni mzazi lazima ahakikishe mtoto anapata mwalimu hata kwa kumlipia mwalimu wa ziada. Tena huwa nashangaa, baadhi ya viongozi wa vijiji ambao hawataki hata kufanya jitihada za kupata walimu.

Wazazi katika shule wanayosoma watoto wao wana wajibu wa kuchangishana pesa na kuajili angalau walimu wa muda; wakati wakisubiri wanaotoka serikalini. Wanaweza kuchanga fedha kila mwaka na kuajili walimu. Maana shule ikikosa walimu, Waziri wa Elimu haathiriki na chochote. Shule ikikosa walimu Mbunge wa eneo hilo haathiriki na chochote-maana mawaziri wetu na watu wenye pesa hawapeleki watoto wao katika shule za vijijini. Watoto wao wanasoma katika shule za kimataifa, seminari au nje ya nchi zenye walimu wa kutosha na wenye sifa stahiki.

Hivyo, wazazi kuendelea kuchangia harusi na misiba huku shule wanakosoma watoto wako haina walimu ni kuua elimu ya mtoto wako. Na kusaliti matarajio mema ya mwanao. wapo viongozi walio makini wanahamasisha wazazi kuajiri walimu. Mfano, niliwahi kufika shule ya sekondari Morembe iliyoko Musoma ambako taarifa za shule zinasema kwamba, wazazi waliamua kuajiri walimu wa ziada ili wasaidie elimu ya watoto wao. Wako walimu 10

12 walioajiriwa na wazazi wa watoto. Haya ni mafanikio

makubwa.

5.18 Pandikiza fikra za uzalendo kwa mtoto tangu akiwa mdogo. Mzazi au mlezi, mfundishe mtoto kuwa mzalendo na kuipenda nchi yake ili aje kuwa mtu na raia mwema

13. Mfundishe mila na desturi za kiafrika na za kitanzania ambazo zina

mtazamo chanya ili asiige za wageni akaja kuwa mtumwa wa fikra na matendo yake. Ni vema mtoto akue akifahamu kuwa Tanzania ni nchi yake, ina lundo la rasilimali. Mweleze mara kwa mara rasilimali za nchi yetu ili afahamu na hata kupata kiu ya kuzimiliki na kuzitumia. Kama unaweza mwimbie nyimbo za zamani zilizokuwa zinakuza uzalendo wetu. Na kuitukuza nchi yetu. Mfano, wimbo kama

11Maoni ya baadhi ya wazazi tuliofanya nao mahojiano kuhusu sababu za watoto wa kike kukatisha masomo. Mkoani Tanga: tarehe 12 Mei 2010. 12Taarifa ya Mkuu wa Shule tuliefanya nae mahojiano Mwezi Mei 2010 huko Musoma 13Sehemu ya msisitizo kwa vijana kuwa raia wema na wazalendo; rai iliyotolewa na Mkurugenzi wa HakiElimu Bi Elizabeth, kwenye Kongamano la vijana. Lililofanyika ukumbi wa Karimjee, Dsm 12 Agosti 2010.

Page 16: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

15

“Tanzania!Tanzania, inchi yenye Mali nyingi watu wengi wa Ulaya wanaililia sana..” Hapa ataanza kuwa mzalendo wa kweli.

Wazazi tunafanya kosa kubwa kukaa na kusifia maendeleo ya wenzetu na kubeza nchi yetu nzuri iliyotukuka. Maendeleo ya nchi maskini hayaletwi na fikra za kutukuza maendeleo ya wengine.

Uzalendo wa mtoto uendane na moyo wa kuthamini kazi, kufanya kazi na kujitegemea. Ajengewe uelewa na ufahamu kuhusu usawa wa jinsia, haki za binadamu, haki za watoto pamoja na umuhimu wa kushirikiana na wenzie katika jamii. Tunaweza kudharau kuwa haya mambo ni mengi sana mtoto hawezi kuelewa. La hasha. Watoto wana uelewa mkubwa sana tangu wakiwa wadogo.

Tunapowaelekeza tusiwapeleke darasani kuwaeleza nadharia nyingi zisizo na maana. Muelekeze mtoto kwa kutumia mifano halisi, na vitu vilivyopo ili kushadidia maarifa aliyonayo. Mtoto akianza kutambua haki zake na za wengine, akipata fikra za uzalendo na kuipenda nchi yake, atakuwa na mitazamo chanya itakayo muwezesha kufanikiwa katika maisha yake. Wazazi tusifanye makosa katika hili.

5.19 Pale pale ulipo, mzazi unaweza kuleta mabadiliko: kwa kushiriki katika vikao vya shule, kamati za vijijini na hata vikao vya serikali ya mitaa vinavyojadili maendeleo ya eneo husika. Katika mikutano na vikao hivyo, ndimo huzaliwa mambo mengi kama mipango endelevu ya kuboresha utoaji elimu. Kujadili mapato na matumizi ya shule, mapungufu ya pesa za uendeshaji na hata kushiriki kuhoji matumizi mabaya ya pesa.

Jamii inapogeuka kuwa watekelezaji tu wa kile kilichoamriwa toka juu bila kujua athari zake, ni jambo baya ambalo hushusha maendeleo ya jamii husika. Maana wanajamii wanaoizunguka shule fulani ndio wanaojua kwa kina matatizo na mafanikio ya shule yao. Na ndio inawahusu zaidi kuliko mtu mwingine yeyote. Hivyo, wazazi kushindwa kuyajadili kwa kina matatizo yanayoikabili shule yenu kwa uwazi na umakini ni kuficha tatizo. Waziri hawezi kuyajua matatizo ya shule ya msingi au sekondari iliyoko Chabutwa Sikonge kama hajafika au kupelekewa taarifa. Yeye muda mwingi anategemea taarifa toka kwa watendaji wake wa chini. Na baadhi ya watendaji wake hao sio makini na wana ajenda zao; na hivyo siku zote wanafanya kazi kwa mazoea tu bila ubunifu wala kuwa na uchungu na shule au jamii. Hivyo, bila kuwa na wazazi wenye uchungu na maendeleo ya watoto wao ambao wanasoma katika shule hizo, hasara huwa ni kwa jamii ya mahali husika sio watendaji wa serikali. Watendaji wengi ni watu wa kuja, na watoto wao wengi wanasoma shule bora zenye mazingira mazuri mijini. Hivyo, jamii lazima ielewe kuwa shule kukosa mwalimu sio hasara ya waziri, wala Afisa Elimu au katibu mtendaji wa kijiji. Hasara ni kwa wanajamii hasa wazazi wa watoto. Hata kufeli kwa watoto kunakotokea kila mwaka mikoa yenye changamoto nyingi kama Shinyanga, Waziri husika hapati hasara yoyote. Ila wazazi wenye watoto na watoto wenyewe ndio wenye hasara kubwa. Yapo pia matatizo ya mimba za utotoni ambazo zinaangamiza watoto wa kike. Na baadhi ya maeneo wahusika wanafumbiwa macho na jamii husika. Haya yanapaswa kujadiliwa kiuwazi kabisa na kupatiwa suluhu kwa kuwajibisha wahusika. Jamii ina jumuisha wazazi ambao wanawajibu wa kuzaa watoto na kuwapeleka shule ili wapate maarifa takikana na stadi nyingine muhimu katika maisha. Isitoshe, mzazi anapaswa

Page 17: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

16

kumpatia mtoto wake mahitaji yote muhimu ya shule, pamoja na maadili au ushauri chanya ili mtoto akue katika maadili bora yanayokubalika katika jamii.

6.0 Umuhimu wa wazazi na walezi kuwasaidia watoto kupata elimu

Taifa lenye watu wanaojitambua na kutambua wajibu wao, ndio taifa lenye mafanikio na ustawi wa maisha ya watu. Ustawi huu huletwa na elimu ambayo pia huletwa kwa jitihada za wazazi, walezi na walimu. Wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kama ilivyoainishwa hapo juu kutazaa watu wenye maarifa, uwezo wa kufikiri, vijana wenye dira na mielekeo sahihi ya mitazamo na maono yao ya mbali. Tutapata watu wenye uwezo mkubwa wakufikiri, kuchunguza na kupambanua mambo. Hatimaye hao ndio watakaokuja kuleta mabadiliko kwa kuvumbua njia mpya. Kwa mifumo na michakato ya elimu inayoendeshwa kisiasa na huku wazazi wakiwa wamelala fofofo, tunajikuta, tunawafundisha watoto/wanafunzi wetu kushindwa! Wengi wa wanafunzi hawa wanajifunza kutodadisi, kutofikiri, kutouliza maswali, kunakili na kukariri, kuwa waoga, kutojiamini, kukubali kila hali, na kukata tamaa kwa kauli ya “yote maisha”. Kwa maana nyingine wanafunzi walio wengi katika shule na vyuo vya Tanzania hawapati elimu iliyokusudiwa, achilia mbali Elimukombozi, kwa kuwa uwezo wa walimu wengi ni mdogo na uelewa wao wa lugha inayotumika kufundishia ni mdogo. Kwa hiyo, badala ya elimu yetu kutokomeza ujinga, inapalilia ujinga! (Qorro, 2008) Ni vema tukajiuliza, hali hii ya kuandaa vijana wasioweza kuelewa, kujadili, kufikiri, kuchambua na kuchanganua masuala na dhana mbali mbali zinazofundishwa ni kwa maslahi ya nani? Ni wazi kwamba tunahitaji Elimubora; na kwamba ili kufanikisha Elimubora shuleni na vyuoni, ni lazima wazazi wawe macho na wachangie kila hatua katika mchakato wa kujifunza wa watoto wao.

7.0 Hasara zitokanazo na wazazi kutotimiza wajibu wao

Wazazi tukishindwa kutimiza wajibu wetu kama walezi, wakufunzi, washauri na walimu wa kwanza kabisa wa watoto wetu kuna madhara mengi kuanzia ndani ya familia na jamii kwa ujumla. Baadhi ya madhara yanayotokana na wazazi kutowajibika ni: 7.1 Watoto wetu kukua bila kuwa na dira wala mwelekeo sahihi wa maisha yao. Huu ni ugonjwa mkubwa kuliko ugonjwa mwingine wowote hapa ulimwenguni. Mtoto akikua bila kuwa na dira ya maisha yake, ni sawasawa na gari linalotembea usiku wa giza nene bila kuwa na taa. Watoto ambao hawana dira wanafuata kila njia wanayoiona hata kama inawapeleka kuzimu, maana hawajui waendako. Wanakuwa vijana hadi watu wazima bila kujitambua, maana hawana dira

14. Hawa ndio wanaunda

vikundi vya watoro shuleni. Wengine wanaacha shule na kujiunga na makundi mabaya kwenye jamii ambao wanakuwa ni tatizo kubwa. Mfano, wavuta bangi,

14 Dira ndio mwongozo wa maisha ya mtu. Kijana wa leo aliyepoteza dira anatumikishwa na kutumika na kila mtu mwenye maarifa na ujanja. Maneno aliyosisitiza Dk. Bashiru Ally, kwenye kongamano la vijana. Karimjee, Dar es salaam 12 Agosti 2010.

Page 18: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

17

madawa ya kulevya, wabwia unga, hawa wote ni mazalia ya malezi duni ya wazazi tangu wakiwa wadogo. Je, mzazi unakubali mtoto wako kupoteza dira ili aje kuwa mzigo kwako na jamii kwa kutowajibika ipasavyo juu yake?

7.2 Pili, watoto wanapokosa malezi bora ya wazazi wao wanatafuta malezi mitaani. Ndipo tunaona tabia mbaya zisizo na maana ndani ya jamii zinaibuka. Watoto wakijiongoza wenyewe mara nyingi hutumbukia shimoni. Na shimo lenyewe ni kuua ndoto zao kabisa. Kama alikuwa ana ndoto za kuwa daktari kamwe hawezi kuwa daktari. Kama alikuwa anaota kuwa mwalimu, kamwe hawezi kuwa mwalimu. Atabatizwa majina mapya ya mtaani na ambayo maana yake itatafsiriwa kwa umahiri wa kutekeleza uovu katika jamii na hata katika familia. Je, mzazi utakubali msiba huu ukufike kwa kutowajibika ipasavyo?

7.3 Kuongezeka kwa wanafunzi wasiohitimu elimu yao. Mara nyingi watoto wanaodondoka na kuacha shule wengi wao wanahusishwa na malezi duni ya wazazi au walezi wao. Wazazi wanaposhindwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu, hasa wa kushauri, kuwasaidia kitaaluma na kuwapatia mahitaji muhimu katika kusoma kwako, watoto wanakata tamaa. Tena kama wakiwa katika vikundi vya watoto wanaopata mahitaji yao kwa ukamilifu, wanavunjika moyo haraka na kujiona kama wao wametengwa. Takwimu za elimu bado zinaonesha kuwa wanafunzi wanaoacha shule au kukatisha masomo yao ni zaidi ya asilimia 20, (BEST 2005-2009). Je tuendelee kuona watoto wanaacha shule na kujiunga na makundi mabaya kwa kutotimiza wajibu wetu kama wazazi?

7.4 Kupunguza nguvu kazi ya taifa. Hii ni hasara kubwa sana tunaposhindwa kuwasaidia watoto wetu kufanikisha elimu yao. Watoto wetu wanakosa stadi za msingi ambazo zingewawezesha kuishi maisha bora na yenye ustawi mkubwa. Wazazi wanaoshindwa kuwalea watoto wao vizuri au kuwasaidia kufanikisha elimu yao, wanawachimbia watoto wao kaburi wakati bado wangali hai. Watoto wasioangaliwa na wazazi wao wengi hawafanikishi masomo yao hivyo, wanakosa ule upana wa uwezo wa kufikiri, wanakosa maarifa yanayohitajika ili kumfanya awe mzalishaji. Wanakosa ubunifu utakaowaongoza kuvumbua au kuibua kiurahisi masuluhisho ya matatizo yetu. Wanashindwa kujitambua na kutambua wao ni akina nani, wana majukumu gani, wanapaswa kufanya nini, wakati gani na kwa faida gani. Na kutokana na haya wanashindwa kuwa wazalishaji wazuri katika maeneo yao. Wanakuwa tegemezi na mzigo kwenye familia zao, serikali yao na taifa lao. Huzuni!

7.5 Inawezekana kabisa hata kuibuka kwa wimbi la kughushi vyeti, alama za mitihani na hata kuiba vyeti vya wasomi waliokufa, kumetokana na wazazi kushindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu. Tulisema hapo juu (rejea kifungu na 4.0), kuwa wazazi ili watimize jukumu lao vizuri la kuwasaidia watoto wao kupata elimu wanapaswa wao kwanza kuelewa malengo ya elimu hapa nchini. Wakifahamu elimu ina malengo gani kwa wananchi wote watakuwa na hamu ya kufahamu zaidi na kuwasaidia watoto wao kufahamu zaidi malengo ya elimu ili wajibidiishe kuyafikia.

Wazazi kutofahamu malengo ya elimu ndio sababu ya kushiriki moja kwa moja kwenye kughushi vyeti vya watoto wao. Kununua alama za mitihani, kununua vyeti vya wahitimu waliokufa na hata kuchangisha pesa kwa ajili ya kufanya udanganyifu kwenye chumba cha mtihani. Wazazi wa namna hii wanajibidiisha kutafuta vyeti badala ya kutafuta maarifa, wana wadanganya watoto wao watafute alama kubwa za kununua au kuwaibia mitihani ili waione kabla ya siku za kufanya, badala watafute ubunifu. Wanahangaikia watoto wao wamalize silabasi badala wamalize ujinga. Wakiwapotosha watoto wao kuwa elimu ni kupata ajira maofisini badala ya

Page 19: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

18

kuwaeleza elimu ni kupata uwezo wa kuzitumia fursa na kuzitengeneza fursa. Tukitimiza wajibu wetu inawezekana. Hakuna njia ya mkato.

8.0 Hitimisho Wazazi pamoja na watanzania kwa ujumla yatupasa tuelewe kwamba hakuna njia ya mkato kuyafikia maendeleo tunayoyahitaji. Hakika hakuna njia ya mkato! Kama kuna mtu anafikiri nchi inaweza kuendelea kwa kupitia njia za panya, huyu ana fikra mgando! Hakuna kitu kama hicho. Maendeleo yanaletwa na mikakati rasmi, mbinu muafaka na mipango mizuri inayotekelezeka pamoja na utayari wa wananchi kufanya kazi kwa bidiii, kufikiri kupita mipaka tuliyoizoea, na kubuni fursa mpya zitakazo zaa ustawi wa maisha ya watu. Haya yote yanawezekana tu kama jamii kubwa imeelimika. Elimu isiwe jambo la kuchagua kuipata au la! Elimu japo ya msingi ni bidhaa muhimu sana katika maisha ya kila mwanadamu. Katika dunia ya leo elimu ndiyo msingi, nguzo na njia muhimu sana ya kuleta ukombozi wa kweli kijamii na kiuchumi, na wala halina mjadala tena.Wananchi walioelimika ndio wanaoweza kuleta mabadiliko ya haraka katika jamii zao. Elimu tunayoitegemea kuondoa changamoto zetu ili kutuletea utukufu

15, ustawi na maisha bora ni hii inayoanzia kwa mzazi mwenyewe

nyumbani. Sio vyeti vingi, alama nzuri kwenye mitihani ama umahiri wa kupiga porojo kwa lugha za kigeni. Kwa mantiki hii kama tunataka maendeleo hatuwezi kukwepa kuwasaidia watoto wetu kukuza vipaji na maarifa tangu wakiwa wadogo nyumbani. Pia kama wazazi hatuwezi kukwepa kugharamia mahitaji ya elimu ya watoto wetu. Hatuwezi kuuza wajibu wetu huu muhimu kwa visingizio dhaifu, vilivyojaa uzembe, uvivu, kutowajibika na kukosa dira. Kila mzazi akitimiza wajibu wake hata walimu watafanya kazi yao kwa urahisi na tija kubwa. Ndipo tutakapounda kizazi cha wasomi walioelimika, wenye maarifa na vipawa lukuki ambavyo vitawasaidia kupambana na changamoto zilizo ndani ya jamii. Wazazi tuungane pamoja kuhakikisha kuwa tunaisaidia na kuikumbusha serikali pale panapohitajika, ili watoto wetu wapate haki yao ya msingi, elimu bora. Hatimaye tutapata maendeleo katika familia jamii na taifa kwa ujumla. Tunaweza tukiamua. Tutimize wajibu wetu!

15Mwalimu Nyerere, amewahi kusisitiza kuwa, elimu sio kwa ajiri ya sifa na heshima, ni kwa ajili ya kumuwezesha mtu atawale mazingira yake na kumletea utukufu au maendeleo ya maisha yake. (Nyerere 1975)

Page 20: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

19

9.0 Marejeo

Feldman R(2001) Child Development. Prentice Hall International (UK) limited . London

Jeynes, W ed (2010) Family factors and the Educational Success of Children

MOEC, (1995). Education and Training Policy, Adult Education Press, Dar es Salaam

Nyerere, J. K. (1967). “Elimu ya Kujitegemea”, Hotuba kuhusu Waraka wa Sera, ya Marchi

1967, Dar es Salaam.

Nyerere, J. K. (1968). “Education for Self-Reliance”, in Freedom and Socialism, Uhuru na

Ujamaa, Oxford University Press, Oxford.

Nyerere, J. K. (1974). “Education for Liberation”, a speech at Dag Hammarskjold Seminar on

20th May, 1974, Dar es Salaam

Page 21: Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya ...hakielimu.org/files/publications/document170wazazi_wanavyoweza... · kuandikishwa shule, kupiga kura au kugombea uongozi

Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi

HakiElimu imeanzisha Mlolongo wa Nyaraka za Kufanyia Kazi (Working Paper Series) kwa lengo la kuchapisha upya makala mbalimbali za uchambuzi katika muundo ambao ni rahisi

ni makala ambazo uandishi wake bado unaendelea, hivyo hazikukusudiwa kuwa ni nyaraka

Maoni yanayotolewa humu ni ya mwandishi (waandishi) mwenyewe na si lazima yawe

fupi zilizo wazi na bayana na tungependelea zaidi ziwe na urefu wa kati ya kurasa sita hadi

kielektroniki kwa kutumia anuani inayooneshwa hapo chini:

HakiElimu

HakiElimu inafanya kazi kuleta usawa, ubora, haki za binadamu na demokrasia katika Elimu, kwa

HakiElimu Nyaraka za Kufanyia KaziSLP 79401 Dar es Salaam TanzaniaSimu (255 22) 2151852 / 3 Faksi (255 22) [email protected] www.hakielimu.org

Nyaraka ya Kufanyia Kazi

k

Wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto kupata elimu Shule ya kwanza ya mtoto ni mzazi

Mtemi G. Zombwe