umuhimu wa mafunzo bora ya ualimu kwa …hakielimu.org/files/publications/document166mafunzo.pdfchuo...

25
Umuhimu wa Mafunzo ya Ualimu kwa Maendeleo ya Elimu Bora Kuwaandaa walimu katika ulimwengu unaobadilika

Upload: others

Post on 30-Dec-2019

53 views

Category:

Documents


0 download

TRANSCRIPT

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

Umuhimu wa Mafunzo ya Ualimu kwa Maendeleo ya Elimu Bora

Kuwaandaa walimu katika ulimwengu unaobadilika

1

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

1.0 Shukrani

Kazi hii ya kitafiti imeandaliwa na Gervas Zombwe na Fredrick Msigallah wafanyakazi wa HakiElimu. Hawa walisoma nyaraka na vitabu mbalimbali pamoja na ripoti za kitafiti zinazofafanua dhana ya mafunzo ya ualimu. Aidha, kwa jitihada kubwa walifanya mahojiano na wahadhiri wa ualimu wa vyuo vikuu, mahojiano na walimu, wakufunzi, wanaharakati wa elimu, wazazi na wanafunzi. Tunawashukuru sana wadau wote waliochangia maoni na taarifa katika mchakato wa kuandaa kitabu hiki. Aidha shukrani za pekee ziwaendee walimu wa Chuo cha Ualimu Morogoro pamoja na Mkuu wa Chuo hicho W.K. Ngonyani, wahadhiri wasaidizi wa Chuo Kikuu kishiriki cha Ualimu Dar es Salaam-DUCE pamoja na wahadhiri Kitivo cha Ualimu, Chuo kikuu cha Dar es salaam. Tunatambua pia mchango wa Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania, Dk Joseph Kisanji, Mratibu wa Muungano wa vituo vya Walimu Tanzania Nalogwa Shani, walimu na wanafunzi wote tuliofanya nao mahojiano. Mchango wa uhariri umetolewa na Elizabeth Missokia na Robert Mihayo wafanyakazi wa HakiElimu. Tunawashukuru sana kwa michango na utayari wao wa kufanyakazi nasi. © HakiElimu, 2009 ISBN 9987-423-90-6 HakiElimu SLP 79401 Dar es salaam, Tanzania Simu: (255 22)2151852/3, Faksi: (255 22)2152449 Sehemu yoyote katika kitabu hiki inaweza kutolewa kwa namna nyingine yeyote kwa madhumuni ya kielimu na yasiyo ya kibiashara, kwa kuzingatia kuwa chanzo kitatajwa na nakala mbili ziwasilishwe HakiElimu.

2

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

Utangulizi

Ni ukweli uliodhahiri kwamba maendeleo ya jamii yoyote yanahitaji elimu ili wananchi wake waweze kushiriki kikamilifu kutatua matatizo na kupambana na changamoto zinazoikabili jamii. Matarajio ya elimu bora ndani ya jamiii yanatokana na mafunzo bora ya walimu ambao ndiyo watendaji wakuu katika mchakato wa kujifunza na kufundisha. Kumekuwa na jitihada nyingi za serikali na wadau mbalimbali kuboresha elimu hapa Tanzania kupitia Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo Elimu ya Sekondari (MMES). Jitihada hizo zimezaa matunda ya ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi walio shuleni, ongezeko la madarasa na wingi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Hata idadi ya walimu imeongezeka ikilinganishwa na siku za nyuma kabla ya kuanzishwa kwa MMEM na MMES. Jitihada hizi za serikali yafaa zipongezwe na kutambuliwa na jamii. Pamoja na juhudi hizi kubwa za kuboresha elimu, ubora wa elimu (kile wanachopata wanafunzi wawapo darasani) unaendelea kushuka siku hadi siku. Ni jambo la kawaida kabisa kuona wanafunzi wanamaliza darasa la saba bila kujua kusoma wala kuandika1. Isitoshe uduni wa elimu kwa sasa unaendelea kushamiri ngazi zote; yaani kuanzia shule za msingi, sekondari2 vyuo vya kawaida na hadi Vyuo Vikuu ambako wanafunzi wanamaliza na kutunukiwa vyeti wakiwa na maarifa finyu na uwezo mdogo sana wa kufikiri na hivyo, kushindwa kuchangia kikamilifu maendeleo ya jamii inayowazunguka. Sababu kuu ya kushuka kwa kiwango cha elimu ni nini? Ingawa zipo sababu nyingine za kushuka huku, sababu moja kuu ni uduni wa walimu wetu wa sasa. Uduni huo unaotokana na kuzidiwa mzigo wa kufundisha watoto wengi madarasani bila kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Kutokana na uchache wa walimu ukilinganisha na idadi ya wanafunzi wanaopaswa kufundishwa, walimu kukata tamaa kutokana na kubinywa haki zao na maslahi yao kama wafanyakazi. Lakini kibaya zaidi, ni uduni unaotokana na mafunzo duni ya ualimu na hamasa ndogo wakiwa vyuoni. Shule zenye walimu wa kutosha, wenye hamasa na waliopata mafunzo kikamilifu hufanya vizuri siku zote. Ushahidi ni shule za seminari na shule za binafsi tunazoziona kila mwaka zikiongoza katika matokeo ya mitihani, na tunakopigana vikumbo kupeleka watoto wetu. Mafunzo ya ualimu nchini Tanzania kwa sasa hayatabiriki. Muda wa walimu kukaa vyuoni umepunguzwa, mitaala ya ualimu imepitwa na wakati na hamasa kwa walimu haipo3. Inawezekana maeneo haya ndiyo dirisha la kuingizia uduni wa walimu wetu na elimu yetu. Swali gumu la kujiuliza tunapoleta mabadiliko kama vile kupunguza miaka ya walimu kukaa vyuoni, kubadili baadhi ya vyuo vya ualimu kuwa vyuo vikuu, tunataka nini hasa? tunaongozwa na dhamira ipi? Kuelekea wapi?

1 Sehemu ya utafiti wa HakiElimu uliopima uwezo wa watoto kusoma, kuandika, kutafsiri na kuchora wilaya sita za Tanzania Bara mwezi Agosti, 2007. 2 Matokeo ya NECTA- PSLE 2007 na CSSE 2008 yanaonesha kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi shule za msingi na sekondari. 3 Kauli ya hisia ya mhadhiri mwandamizi wa Ualimu, niliyefanya naye mahojiano Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Mei 2009.

3

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

Mathalani, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la wanafunzi shule za msingi na sekondari, ili hawa wapate elimu inayotakiwa wanahitaji walimu waliofuzu mafunzo yao na wenye moyo wa kufanya kazi. Tarajio la wengi lilikuwa ni kuona walimu wengi sana wanaandaliwa vyema ili kuweza kukabili ongezeko la wanafunzi hawa ambalo limeleta mahitaji makubwa ya walimu. Cha kushangaza idadi ya walimu tarajali wanaojiunga na vyuo vya ualimu nchini imepungua maradufu hasa mwaka 2008, kutoka asilimia 11.5 hadi asilimia hasi(-11.0%)4. Hii inadhihirisha upungufu mkubwa wa walimu tulionao hapa nchini. (Angalia jedwali 2) Kwa mujibu wa kitabu cha takwimu za elimu cha serikali, kupungua kwa udahili wa walimu vyuoni kumetokana na kubadilishwa kwa baadhi ya vyuo kuwa sekondari na vyuo vikuu.5 Inawezekana mabadiliko kama haya yakawa na nia nzuri tu, lakini yasiwafae maelfu ya watoto wa kitanzania walio vijijini wanaohitaji sana walimu wenye sifa na moyo wa kufanyakazi. Mabadiliko haya yanaweza kuwafaa sana watunga sera, lakini yakawa ndiyo chanzo cha kuwachimbia kaburi watoto masikini walioko vijiini wanaotegemea sana walimu kutoka vyuo hivyo ili wawaendeleze wapate maarifa takikana. Isitoshe, katika kuitikia tatizo la upungufu wa walimu wenye sifa, serikali imechukua hatua ya kutumia walimu wasio na sifa; yaani walimu wasio na mafunzo sahihi kutoka vyuo vya ualimu. Zaidi sana, kwa sasa wanaajiriwa walimu ambao wamekwenda kwenye ualimu kwa sababu ya kufuata ajira; hawana hisia za kufundisha wala maadili ya kazi. Tangu mwaka 2005 walimu hawa wanachukuliwa na kusambazwa shuleni hasa vijijini kwenye wingi wa watoto kutoka familia masikini. Walimu hawa wamesaidia sana kujaza takwimu za idadi ya walimu na kuwapa hamasa watoto kuwa wana walimu. Lakini, kwa uhalisi hawa sio walimu. Pamoja na kuwa wanapewa leseni ya kufundishia bado hawastahili hata kuitwa walimu. Wengi wao wamekwenda kuua elimu katika shule zetu6 kwa sababu mapungufu ya walimu hawa yako dhahiri. Wengi hawana hata hisia wala nia ya kufundisha, kitu ambacho ni muhimu sana, na ni sifa ya kwanza ya mwalimu yeyote anayeipenda kazi yake ya ualimu. Walimu wengi wanafanya kazi kwa kutimiza wajibu tu. Wengi wao wako njia panda; pindi wapatapo nafasi za kusoma au ajira sekta nyingine wanaacha kazi maramoja na kwenda sehemu zenye maslahi zaidi na wanazozipenda. Kibaya zaidi, wamegeuka mzigo kwa walimu wachache waliosomea ualimu kuwaelekeza namna ya kufanya maandalio ya masomo na hata jinsi ya kufundisha vyema. Hali hii imesababisha walimu wenye sifa kuwa na mzigo mkubwa pasipo sababu. Wanafanya kazi mbili kufundisha wanafunzi wengi na kuwaelekeza walimu wapya bila malipo yoyote. Kitu ambacho wengi hawakifurahii na wanaona adha kwa kuongezewa mzigo mara mbili. Hii inawakatisha tamaa sana!7 Walimu hao pia wanashindwa kufundisha masomo muhimu kama sayansi, kiingereza na hisabati. Wengi wakipewa vipindi wanakataa au kuyafundisha hovyo kiasi cha kupotosha wanafunzi8

4 BEST 2004-2008: Uk 80 5 Takwimu na ufafanuzi wa kupungua kwa udahili wa walimu tarajali, zilizotolewa na kitabu cha Takwimu za Elimu (BEST 2004-2008) ukurasa wa 80 6 Sehemu ya mahojiano na mhadhiri mkongwe Chuo Kikuu cha Dar es salaam; Prof Mbise 2008 7 Sehemu ya mahojiano na walimu wa Sekondari ya Kilangalanga iliyoko Mlandizi Pwani, Agosti 2007 8 Mchango wa walimu wa leseni tuliozungumza nao, kutoka shule 7 za Manispaa ya Dodoma. Desemba 2008

4

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

Hali hii ni ushahidi tosha kwamba tunapotaka kuboresha elimu ili kuchochea maendeleo katika jamii hakuna njia ya mkato ya kuandaa walimu. Kufanya hivyo ni kuliweka taifa rehani ndani ya wananchi wajinga! Walimu ni lazima waandaliwe vyema ili wawaandae vyema watoto, na kujenga jamii bora yenye maendeleo na ustawi wa maisha ya watu. Dhamira hii itafikiwa tu iwapo mafunzo ya ualimu yataboreshwa na mitaala ya kufundishia walimu itashabihiana na mahitaji ya watoto na jamii ya kitanzania. Hapo walimu watafundisha kile wanafunzi wanachopaswa kujua na kile jamii inatarajia kuona kwa watoto wao; sio kile wanachopenda walimu au kile wanachopenda wanasiasa. Chapisho hili limezingatia ushahidi uliopo juu ya elimu ya ualimu na kutoa mapendekezo ambayo yanaweza kuwasaidia walimu wapya kujifunza kwa ufanisi zaidi. Ripoti hii haitoi vigezo vipya vya ubora wa elimu ambavyo mwalimu anapaswa kuvifahamu. Badala yake ripoti imejumuisha mapendekezo yanayozungumzia juu ya umuhimu wa kuingiza katika mtaala wa elimu maarifa ambayo mwalimu tarajali anapaswa kufahamu. Ripoti hii haizungumzii mambo yote yaliyopo kwenye mtaala ambayo pengine watu wanaweza kuyaona kama ni muhimu kwa walimu tarajali kuyafahamu, ila imezingatia taarifa za utafiti na makubaliano ya kitaalamu. Jambo kubwa linalosisitizwa ni juu ya kuwaandaa walimu ili baadaye waweze kujifunza kwa ufanisi zaidi kama wataalamu. Tunaamini huu ni mwongozo juu ya kile ambacho walimu wanapaswa kukijua pamoja na kile ambacho wanapaswa kukifanya. Pia, msaada kwa jamii kutambua, kuwasaidia na kuwafanyia tathimini walimu wetu popote walipo ili kubaini ubora wao, mapungufu yao katika kutoa elimu bora, na hivyo kuweza kuandaa mikakati ya kukabiliana na mapungufu hayo. Aidha chapisho hili ni mwendelezo wa juhudi mbalimbali za shirika la HakiElimu zinazolenga kuboresha elimu. Mwaka 2008, HakiElimu ilitoa chapisho kama hili linalomfafanua mwalimu na majukumu yake katika kuboresha elimu. Chapisho hili limebainisha vigezo vya ubora wa mafunzo ya ualimu ambavyo ni muhimu walimu, watunga sera na wananchi wavifahamu na ndipo watakuwa na uwezo wa kufuatilia na kupima utendaji wa walimu wetu. Kitabu hiki kinawalenga walimu, watunga sera pamoja na wadau wengine wa elimu. Kitabu hiki kinatathmini matokeo ya maarifa yanayotokana na mafunzo ya ualimu kama hatua ya awali na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuboresha elimu. Ni matumaini yetu chapisho hili litasaidia kutoa mwanga na maarifa kuhusu kujifunza, kufundisha na elimu ya walimu. Pia litachagiza uelewa wa namna walimu wanavyopaswa kuandaliwa ili kuwapatia maarifa na stadi mbalimbali zitakazowajengea moyo wa kujitolea ili waweze kuwasaidia wanafunzi kufaulu katika masomo yao. Kama alivyowahi kusema mwanazuoni wa elimu ndugu Shulman kuwa, “Wale wanaoweza-wafanye, na wale wanaoelewa-wafundishe!” Elizabeth Missokia Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu Septemba, 2009

5

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

2.0 Maana ya mafunzo ya ualimu Kuna ufafanuzi wa aina nyingi wa nini hasa maana ya mafunzo ya ualimu, katika kupata ufafanuzi sahihi, mapitio ya vitabu/nyaraka na maoni ya wadau mbalimbali wa elimu na wanazuoni yametoa ufafanuzi wa maana ya mafunzo ya ualimu, ufafanuzi huo ni:- Ni mafunzo ya maandalizi maalumu ya mtaalamu ili aweze kutimiza jukumu lake vizuri. Katika utaalamu wowote kuna mafunzo tarajali; yaani kabla ya mtu kuanza kazi, lakini pia kuna mafunzo kazini wakati mtu anaendelea kufanya kazi, malengo ya mafunzo kazini ni kukumbusha, kuongeza kuchagiza na kuamsha maarifa na utaalamu wa mtu ili amudu na aweze kutekeleza wajibu wake vizuri zaidi, na awe na uwezo wa kuyakabili mabadiliko ya kitaalamu yanayoibuka kila siku katika jamii anayoifanyia kazi.

Mafunzo ya ualimu ni mchakato wa kuwaandaa watu ili wawe walimu. Mchakato huo unahusisha vitu vingi vikiwemo; sifa za kuchaguliwa kujiunga na masomo, kudahiliwa, mazingira ya kujifunzia kama madarasa, mabweni, maabara, zana za kufundishia, mitaala, wakufunzi wenye sifa na kuwa na madaraja ya ngazi za walimu wanaotarajiwa.(Mkuu wa Chuo cha Ualimu Morogoro, Mei 2009). Mafunzo ya ualimu ni maandalizi ya walimu wa baadaye kupitia mafunzo katika mbinu za kufundisha, masomo ya kitaaluma, usimamizi wa elimu, malezi na ushauri, pia inahusisha maadili ya ualimu kitabia na mwenendo pamoja na masuala ya kiutawala9 Mafunzo ya ualimu ni mfumo rasmi wa kuwaingiza vijana wanaopenda kuwa walimu katika stadi za kufundisha na kujifunza na mbinu za kufundisha, pamoja na maarifa ya kitaaluma yatakayo wawezesha wao kufundisha wanafunzi. Maudhui ya mafunzo ya ualimu hutolewa na mitaala kwenye mihutasari ya mafunzo husika, tena yanatolewa kwa kipindi maalumu. Mafunzo ya ualimu yanaweza kutolewa hata baada ya mtu kuwa mwalimu kwa malengo ya kukuza ujuzi na maarifa ya mwalimu.(Afisa Programu, Muungano wa vituo vya walimu, Aprili 2009.) Mafunzo ya ualimu ni mchakato ambapo mwalimu mtarajiwa anapatiwa mbinu kamilifu za ufundishaji, anapatiwa maarifa ya masomo mbalimbali ya kufundisha na stadi za malezi na ushauri wa wanafunzi. Ni mchakato wa kumuingiza mtu kwenye utaalamu wa kufundisha kwa kumpatia maarifa na ujuzi wa somo na njia ambazo atazitumia kupeleka maarifa hayo kwa wanafunzi na kwa maendeleo yake. Mtu yeyote hawezi kujiita mwalimu kama hajapitia mfumo wa mafunzo haya unaompa sifa ya kuwa mwalimu.(Afisa Elimu Mwandamizi, Wizara ya Elimu na Mafunzo, Mei 2009) Mafunzo ya ualimu ni program ya mafunzo yenye lengo la kuwaandaa watu kuwa walimu katika ngazi tofauti tofauti za kiutaalamu, kama walimu wa awali, walimu wa daraja A, walimu wa stashahada, na walimu wenye shahada toka vyuo vikuu. Mafunzo hayo pia yanawaandaa walimu kuwa washauri, watawala na wasimamizi katika sekta ya elimu.10

9 Sehemu ya ufafanuzi wa wahadhiri wasaidizi wa Chuo Kikuu cha Ualimu-DUCE, tuliofanya nao mahojiano tarehe 11 Mei, 2009. 10 Sehemu ya mchango wa jopo la walimu wanafunzi tuliohojiana nao Chuo cha Ualimu Morogoro, Mei 2009.

6

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

Kwa ufupi tunaweza kusema, mafunzo ya ualimu ni mchakato maalumu wa kumwandaa mtu kwenda kufundisha, unaoendeshwa kwa muda maalumu, mazingira maalumu nadharia na vitendo maalumu. Mafunzo haya ni lazima yamjenge mwalimu mtarajiwa kwenye maeneo matatu muhimu; kwanza ni lazima apate taaluma na maarifa ya kutosha ya somo analolifundisha ili aweze kulimudu somo analolifundisha. Pili, ajue mbinu za kutosha za kufundishia na nadharia zinazoambatana na mbinu hizo; na tatu, aifahamu falsafa na dira ya taifa ya elimu ili awasaidie watoto kuitafsiri falsafa ya nchi na malengo ya elimu.

3.0 Nadharia na utendaji wa kazi ya ualimu

Kwa mpenzi wa muziki pale unapotazama onesho, huamini kuwa kazi ya kondakta, yaani Muongozaji wa waimbaji na wapiga vyombo vya muziki ni rahisi kuliko kazi zote duniani. Kwa kuwa husimama na kunyooshanyoosha mikono yake akiendana na muziki, na kwamba bendi ya muziki hutoa sauti vizuri pale jukwaani kwa wakati huohuo. Mtazamaji wa muziki huwa hafahamu mambo mengine yaliyofichika kama vile uwezo anaopaswa kuwa nao kondakta wa muziki wa kuzisoma na kuzielewa sauti zote, uwezo wa kupiga vyombo vingi na kuelewa ufanisi wa kila chombo cha muziki, kupanga na kuunganisha sehemu tofauti tofauti, kuwapa motisha waimbaji pamoja na kuwasiliana na bendi nzima. Vivyo hivyo kwa kazi ya kufundisha. Mtu akionekana akizungumza na wanafunzi na kuwasikiliza, akishughulika na makaratasi na kutoa mazoezi kwa wanafunzi huonekana anafanya kazi rahisi. Mambo yaliyojificha juu ya taaluma ya ualimu ni ugumu wa kazi yenyewe kwa kuwa mwalimu ndiye anayepaswa kuamsha, kuchagiza, kutoa na kukuza maarifa kwa wanafunzi kutoka upeo mmoja wa uelewa hadi mwingine kwa kipindi maalumu. Kila siku walimu hukumbana na masuala mengi na magumu ambayo wanapaswa kuyatolea uamuzi. Masuala haya yanategemea maarifa na maoni binafsi ya mwalimu na yana athari kwa maisha ya baadaye ya mwanafunzi. Ili kuchukua uamuzi mzuri, walimu lazima wawe na uelewa juu ya tendo la kujifunza linavyoweza kufanyika katika nyanja za maendeleo, tofauti zilizopo katika kujifunza, lugha na athari za kitamaduni, tofauti za mtu mmoja mmoja, upendeleo na mbinu za kujifunza. Mbali na hayo, mwalimu pia anapaswa kufahamu njia bora zitakazomsaidia mwanafunzi kujifunza kwa ufanisi zaidi. Katika kutoa uamuzi, walimu wanapaswa kuzingatia maslahi ya wanafunzi wao. Hili linaonekana kama jambo dogo, lakini ni jambo gumu na lina athari kubwa juu ya kile kinachotokea kwa mwanafunzi mmoja mmoja na wanafunzi wengine shuleni. Umuhimu wa kuwaandaa walimu ili waweze kuchukua uamuzi bora ambao umejengwa kwenye msingi wa maarifa wanayopewa, ni suala linalopewa kipaumbele katika jamii ya sasa. Viwango vya kujifunza vimepanda kuliko ilivyokuwa hapo awali. Raia na wafanyakazi wanahitaji maarifa ya kutosha pamoja na utaalamu utakaowasaidia kuishi na kufanikisha masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao. Fikiria! Meli kubwa inayobeba maelfu ya tani za mizigo, inayosafiri maelfu ya maili, inayobeba maelfu ya roho za watu. Je, meli hii ikikosa nahodha! Ikakosa mafuta! Ikakosa

7

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

ukarabati hatima ya mali na watu waliomo ni nini? Meli ni Mwalimu, mafuta ni sawa na nahodha na ukarabati ni mafunzo ya Ualimu.

4.0 Malengo ya mafunzo ya ualimu Tanzania

Mafunzo ya ualimu yana malengo mahsusi yanayoongozwa na dira na falsafa ya elimu nchini. Hapa Tanzania malengo ya mafunzo ya ualimu yamefafanuliwa vyema katika Sera ya Elimu na Mafunzo. Kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo11, madhumuni na malengo ya elimu ya mafunzo ya ualimu ni:

Kuwapa wanachuo nadharia ya msingi ya elimu, saikolojia, unasihi na ushauri Kuwapa wanachuo msingi na mbinu za kufundisha, ubunifu na bidaa Kuinua kiwango cha uelewa wa misingi ya mtaala wa shule Kunoa walimu tarajali, walimu na wakufunzi kimaarifa na umahiri katika baadhi ya

masomo, stadi, na teknolojia Kuwapa ujuzi na mbinu za upimaji na tathimini katika elimu kuwawezesha wanachuo na

walimu wa shuleni na wakufunzi kupata ujuzi wa elimu na mafunzo ya uongozi na utawala.(ETP 1995; 5).

Hata hivyo, kwa uchambuzi wa kina malengo ya kuwaandaa walimu ili wapate maarifa watakayoyatumia kuwasaidia wanafunzi ili waweze kujifunza kwa ufanisi, yanaweza kutazamwa kiundani zaidi kwa kujiuliza maswali kadhaa; kwa mfano:

Je, ni maarifa gani ambayo walimu wanapaswa kuwa nayo ili waweze kuwafundisha wanafunzi wao kwa ufanisi?

Je, ni stadi zipi walimu wanapaswa kuwa nazo ili ufundishaji wao uzae matokeo mazuri

kwa wanafunzi wa aina tofautitofauti na pia walimu waweze kutathmini na kuziboresha mbinu zao za ufundishaji?

Je, walimu wanahitaji msaada gani wa kitaaluma ili waweze kujitoa kwa moyo wote

kumsaidia kila mtoto ili aweze kufanikiwa na kuendeleza maarifa na stadi, kama mwanajumuiya na mwanataaluma?

Majibu ya maswali haya yanaweza kutuongoza kwenye ukweli wa nini walimu wetu tarajali wanapaswa kufahamu ili wakawafundishe akina nani, kwa faida zipi, na kwa kipindi gani. Kwa sababu sio kila anachofundishwa mwalimu ni kitu kizuri kwa mwanafunzi, na sio kweli kwamba wanafunzi wana mahitaji yanayofanana, na kwamba mafunzo ya ualimu yanapaswa kuwa ya aina moja. Ikumbukwe kuwa Malengo ya Mafunzo ya Ualimu ni kuwaandaa walimu wapya ambao watatambua kuwa huchukua miaka mingi ya uzoefu ni muhimu ili kujenga utaalamu. Tunaelewa kuwa walimu huendelea kujenga maarifa mapya pamoja na stadi mpya kupitia mazoezi katika kazi zao kuliko maandalizi mafupi ambayo huyafanya kabla ya kuingia

11 Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, ni mwongozo-mama wa Elimu na mafunzo hapa Tanzania. Program zote, mipango, sheria na mikakati inayohusu elimu inapaswa kufuata na kulingana na tamko la sera hii.

8

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

darasani. Lengo la elimu tarajali ni kuwapatia walimu maarifa ya msingi pamoja na uelewa wa jinsi ya kufanikisha kazi zao. Mtazamo huu huwachukulia walimu kama “chanzo na watoa maarifa na ujuzi unaohitajika na uhamasishaji wakati wa tendo la kujifunza” badala ya wao kuwa watoaji wa maarifa pekee (Cohen na Ball, 1999, Uk.6). Hivyo, mafunzo bora ya walimu lazima yalenge kuwasaidia walimu ili wawe “wataalamu wanaokwenda na wakati” ambao watakuwa wamejiandaa kwa ajili ya elimu ya maisha ambayo itawawezesha kuongeza maarifa na ujuzi wao kila siku. (Hatano & Inagaki, 1986). Mbali na malengo ya kuwaandaa walimu ili wawe watu wa kujifunza katika maisha yao yote, tunawajibika kueleza maarifa ambayo mwalimu anapaswa kuwa nayo ili aweze kuwafundisha wanafunzi wake kikamilifu. Tunaamini kuwa wanafunzi wote bila kuwabagua wanaotoka vijijini na familia masikini, wana haki ya kupewa mafunzo yanayoeleweka na kwamba itakuwa ni jambo baya iwapo watapoteza miaka mingi shuleni (kama wanavyopoteza watoto wengi shule za vijijini)12 wakifundishwa uongo na mwalimu asiyefundisha kwa ufanisi au mwalimu anayefundisha kwa kubahatisha. Kwa sasa nchini Tanzania, suala hili ni muhimu sana lizingatiwe kwa kuwa walimu wanaojifunza kazi na wale wasiokuwa na uwezo wa kufundisha ndiyo wanaopangiwa kufundisha katika shule zenye wanafunzi wenye kipato cha chini, wanafunzi waliotengwa katika elimu pamoja na wale wanaoishi katika mazingira magumu ambao wanahitaji wafundishwe na walimu wenye utaalamu wa kutosha ili waweze kufanikiwa katika masomo yao. 5.0 Aina za mafunzo ya ualimu nchini Tanzania Nchini Tanzania hadi sasa muundo wa mafunzo ya ualimu umegawanyika katika aina kuu mbili ambazo zinatekelezwa katika ngazi zote za mafunzo ya ualimu na aina ya walimu wanaoandaliwa. Aina hizo mbili za mafunzo ya ualimu ni:- 6.1 Mafunzo ya walimu tarajali: Haya ni mafunzo rasmi ambayo humwandaa mtu kuwa mwalimu na humpa sifa mtu ya kuwa mwalimu na mtaalamu wa taaluma ya kufundisha. Mafunzo ya walimu tarajali humjenga mtu katika nadharia za elimu, utaalamu na maarifa ya somo analokwenda kulifundisha, utaalamu wa falsafa ya elimu ya nchi, mbinu za kufundishia, mahitaji ya jamii, maadili ya kitaalamu na maadili ya mwenendo binafsi. Kutokana na umuhimu wa kuwa na sifa hizi mchanganyiko mafunzo haya yanapaswa kutolewa kikamilifu ili anayeandaliwa asiwe nusunusu. Maana akiwa nusu au akiwa amepotoka tangu mwanzo naye atakwenda kuwapotosha wanafunzi na hatima yake jamii nzima itakuwa imepotoshwa. 6.2 Mafunzo ya walimu kazini: Haya ni mafunzo yasiyo rasmi ambayo hutolewa kwa walimu walio kazini. Mafunzo haya yanapaswa kuwa ya mara kwa mara na ya aina

12 Utafiti wa Ubora wa Elimu (uliofanywa na HakiElimu, Agosti 2007) ulipima stadi za watoto katika kusoma, kuandika, kufanya hesabu rahisi, imla, na kutafsiri sentensi rahisi ulibainisha watoto wengi wa shule za vijijini hawajui hata kusoma na kuandika, japo wengi walikuwa wamefika darasa la saba. Wale wa mijini wanauwezo mkubwa.

9

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

mbalimbali. Malengo ya mafunzo ya ualimu kazini ni kuamsha na kuongeza ujuzi na maarifa kwenye utaalamu na taaluma ya ualimu katika nadharia na vitendo vya kufundisha, kuchagiza maadili na hisia za kufundisha, kuchochea ari ya kufundisha na kusimamia mchakato wa kufundisha. Aidha mafunzo haya yana lengo la kumjengea mwalimu hali ya kujiamini na kupanua uwezo wake wa kufikiri ili aweze kukabiliana na maarifa mapya, mbinu mpya na mahitaji mapya ya kielimu ya jamii inayomzunguka. Bila kuwepo kwa mafunzo haya walimu wengi hupitwa na wakati, na hivyo kupoteza uwezo wao wa kufanya kazi kwa bidii. Pia hukosa furaha na kazi yao, kutojiamini na kupoteza ladha ya kazi yao ya ualimu. Ni muhimu ikumbukwe kuwa walimu ni wanafunzi wa kudumu; kwa maana kwamba siku zote wanahitaji kupata maarifa mapya ili wawe bora zaidi kuchagiza kujifunza kwa watoto. Mara nyingi mafunzo ya ualimu kazini hutolewa kupitia kozi fupifupi, semina, warsha, mikutano, makongamano na mafunzo maalumu yanayotolewa na Serikali vyuoni au wadau wengine wa elimu hapa nchini na nje ya nchi. Muundo wa sasa wa ngazi za mafunzo ya ualimu ni wa aina tatu; kuna wale walimu wa cheti daraja A ambao wanaandaliwa kufundisha shule za msingi, walimu wa stashahada/diploma hawa wanaandaliwa kufundisha shule za sekondari na za msingi, na pia walimu wa shahada ambao wanaandaliwa kufundisha shule za sekondari ngazi ya juu pamoja na vyuo vya ualimu.( kwa ufafanuzi zaidi angalia jedwali na 1)

10

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

Jedwali 1: Muundo wa sasa wa mafunzo ya Ualimu Tanzania Na Ngazi ya ualimu Ufafanuzi muhimu

1. Ualimu Daraja A Hawa ni walimu wanaoandaliwa vyuo vya ualimu kwa ajili ya kufundisha watoto wa chekechea (elimu ya awali13) na wanafunzi wa shule za msingi. Kwa kawaida wanapaswa kuhitimu kidato cha nne na kufaulu angalau daraja la nne bila kuzidi alama 28. Ndipo wanajiunga na Chuo cha ualimu kwa muda wa miaka miwili. Mtaala wao vyuoni unakazia zaidi mbinu za ufundishaji na maadili ya ualimu.

2 Ualimu ngazi ya Stashahada (diploma)

Hawa ni walimu wanaolengwa kufundisha shule za sekondari. Japo bado wengi wanafundisha pia shule za msingi. Kwa kawaida wanadahiliwa baada ya kumaliza kidato cha sita na kufaulu. Ndipo wanajiunga na vyuo vya ualimu kwa kozi ya ualimu ya miaka miwili. Kutokana na upungufu wa walimu kwa sasa wanavyuo hawa wanakaa chuoni mwaka mmoja kwa ajili ya nadharia na mwaka wa pili wanatumia shuleni wakijifunza kwa vitendo. Mitaala ya mafunzo ya ualimu ngazi hii inatilia mkazo masomo ya ualimu na maadili.

3 Ualimu ngazi ya Shahada(digrii)

Ni ngazi ya juu ya maandalizi ya mwalimu. Kwa kawaida walimu wa shahada huandaliwa kwa ajili ya wanafunzi wa sekondari pamoja na vyuo. Mafunzo ya walimu ngazi hii huchukua miaka minne. Lakini kwa sasa imepunguzwa hadi mitatu ili kukidhi mahitaji ya walimu wanaohitajika. Mafunzo ya ualimu ngazi ya shahada yamegawanyika zaidi. Kuna walimu ambao wamelenga kuwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu. Hawa hukazia zaidi katika kubobea utaalamu wa mbinu za kufundishia na masomo ya ualimu. Lakini wapo wanaolenga kufundisha masomo shuleni, wao hukazia masomo watakayokwenda kufundisha na masomo ya ualimu yanakuwa kwa uchache. Hata hivyo, kwa sasa kuna mwingiliano mkubwa wa walimu katika kufanya kazi zao.

Licha ya kuwa na upungufu mkubwa wa walimu katika shule zetu bado juhudi za kuwapata walimu wapya wenye sifa ni hafifu sana. Badala ya idadi ya walimu tarajali kuongezeka vyuoni kwetu sasa idadi ya walimu hao wanafunzi inapungua kila mwaka. Mathalani, mwaka 2004 walimu-wanafunzi waliodahiliwa vyuo vya ualimu walikuwa 30,893, lakini mwaka jana tu 13 Kwa mujibu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 ukurasa wa 10, elimu ya awali haiko kwenye mfumo rasmi, lakini watoto kuanzia umri wa mika 4-6 wanafaa kupata elimu hiyo katika shule za msingi au binafsi. Na walimu wao ni hao wa cheti daraja A

11

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

(2008) idadi ya walimu-wanafunzi waliodahiliwa vyuoni ilishuka hadi 16,700 tu, japo wanafunzi wanaoandikishwa wanaendelea kuongezeka. (Tazama jedwali namba 2 linafafanua zaidi). Je watafundishwa na nani wanafunzi hao?

Jedwali 2: Udahili wa walimu-wanafunzi vyuo vya ualimu vya Serikali 2004-2008

Wanaume Wanawake Mwaka

idadi asilimia idadi asilimia

Jumla

2004 16245 52.6% 14647 47.4% 30892

2005 12502 52% 11513 48% 24015

2006 10155 53.2% 8929 46.8 19084

2007 10036 53.5% 8718 46.5% 18754

2008 9209 55.1% 7491 44.8% 16700

Chanzo: ukokotozi wa mwandishi kwa kutumia kitabu cha BEST, 2004-2008 uk 80

7.0 Sifa za mafunzo bora ya Ualimu Mafunzo bora ya ualimu ni yale yenye sifa zinazokubalika kiutalaamu, kitaaluma na kijamii. Ni lazima yamjenge mwalimu kufanya anachotarajiwa na wanafunzi na jamii inayomzunguka. Baadhi ya sifa muhimu za mafunzo ya ualimu ni hizi:-

7.1 Kumjengea mwalimu mtarajiwa uelewa mpana na wa kina wa namna wanafunzi wanavyojifunza, makuzi yao kiakili na kitabia. Mwalimu aelewe jinsi wanafunzi wanavyojaribu kuutafsiri ulimwengu kwa kutumia maarifa na uzoefu walionao. Afahamu kile ambacho tayari wanafunzi wanakijua na kukiamini, na awe na uwezo wa kuyaoanisha maarifa ya wanafunzi waliyonayo na maarifa mapya. Afahamu jinsi wanafunzi wanavyopokea taarifa, wanavyozitunza na kuzitumia baadaye. Afahamu jinsi wanafunzi wanavyojifunza kusimamia kumbukumbu zao na uwezo wao wa kufikiri na afahamu vitu vinavyowatia hamasa wanafunzi ili wasome na kujifunza zaidi. Eneo hili ni muhimu sana kwa mafunzo yoyote ya ualimu. Bila kuwajua wanafunzi wake namna wanavyoelewa, jinsi wanavyofikiri, udhaifu wao, ubora wao, matakwa yao, mitazamo na mielekeo yao na vitu wanavyopendelea, mwalimu hawezi kuwa mwalimu bora. Inawezekana dosari hii ikamfanya mwalimu aione kazi ya ualimu kuwa ngumu na haishabihiani na wito wake. Na hii imekuwa ni moja ya sababu ya walimu wengi kuacha kazi ama kufundisha hovyo hovyo.

7.2 Yamjengee mwalimu ufahamu wa maarifa yapi wanafunzi wanatarajia kupata baada

ya kujifunza, ujuzi na stadi zipi ni muhimu kwa wanafunzi, mitazamo na maadili gani ni ya

12

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

lazima kwa mwanafunzi na namna watakavyoyatumia maarifa, stadi, ujuzi na mitazamo hiyo kuishi katika jamii inayowazunguka. Hali ilivyo sasa ni tofauti kabisa na dhamira hii. Walimu wengi wanakazania kuwakaririsha wanafunzi dhana rahisi na mitihani iliyopita ili wafaulu mitihani tu. Wanafunzi wengi kwa sasa wanaelewa kuwapo kwao shule lengo kuu ni kufaulu mitihani ili wasonge mbele, lakini hawajui na wala hawahitaji kujua ujuzi, stadi na maarifa wanayopata yana umuhimu gani na watayatumiaje katika kukabiliana na maisha yao ya kila siku. Hiyo ni dosari kubwa ya walimu wetu na mafunzo wanayopata.

7.3 Kumjengea mwalimu uelewa mpana wa makuzi na maendeleo ya

binadamu(mwanafunzi) ili aweze kulisimamia vyema darasa analofundisha na kuwawezesha wanafunzi kujifunza vyema. Makuzi na mabadiliko ya kibinadamu ni muhimu sana kutambuliwa na mwalimu yeyote. Mabadiliko na maendeleo ya wanafunzi yako kimaumbile, kiakili, kijamii, kihisia, kimihemko, kiutambuzi na ki-umahiri wa lugha. Mabadiliko haya yako kwa kila mwanafunzi, na hayafanani, na wala hayatokei kwa pamoja. Ili mwalimu apange vyema somo na mtaala wa wanafunzi ni lazima ajue mabadiliko haya ili aweze kuwasaidia wanafunzi wenye sifa tofautitofauti kufanikiwa malengo yao ya kuwepo shuleni. Utambuzi wa mabadiliko ya kibinadamu utamsaidia mwalimu kutambua nani anapenda nini, nani anafaa kuwa wapi, nani ajue nini, kazi hii afanye nani, mbinu zipi nzuri za kumfundisha nani. Nani anazuiliwa na nini kuelewa, nani akiwa wapi hawezi kufanya nini. Utaalamu katika eneo hili ni muhimu sana katika kufikia malengo ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi.

7.4 Yamjengee mwalimu mtarajiwa uelewa mkubwa wa malengo ya elimu ya taifa, Sera

za elimu za nchi, falsafa ya nchi ya elimu na mitaala inayoshabihiana na mahitaji ya jamii. Hii ni muhimu sana maana atajua anapaswa kufanya nini kwa matarajio ya jamii inayomzunguka na taifa kwa ujumla. Mwalimu mwenye maarifa na ufahamu wa kutosha wa mitaala atakuwa mbunifu wa namna ya kuyafikia malengo ya elimu kupitia mitaala iliyopo. Atakuwa mwepesi wa kutoa mapendekezo ya maboresho ya mitaala kulingana na mahitaji mapya ya jamii. Dira ya mitaala ni lazima ieleweke vyema kwa mwalimu (Miller, 1980; O’Malley, 1970; Lagemann, 1983). Mwalimu anayefahamu dira ya mitaala na malengo ya sera anakuwa na uwezo mkubwa wa kujiamini na kufanya kazi yake bila kubahatisha. Cha kushangaza maelfu ya walimu wetu pamoja na wale wanaotoka vyuoni hawazijui sera za elimu wala malengo ya elimu ya taifa.14 Kama walimu hawaijui sera ya elimu, mafunzo ya ualimu yamekamilika kweli? Watawezaje kutekeleza vyema sera wasiyo ijua?

7.5 Yamjengee mwalimu mtarajiwa uelewa mpana wa somo analokwenda kulifundisha

ili aweze kupanga vyema mbinu za kulifundisha somo hilo kwa lengo la kukidhi mahitaji ya wanafunzi na malengo ya kujifunza ya wanafunzi. Kuwa mahiri wa somo

14 Karibu asilimia 90 ya walimu tuliowauliza (manispaa ya Dodoma, Morogoro Nov-Dese 2008) kama wanafahamu malengo ya elimu kwa mujibu wa sera ya elimu ya taifa, walikiri hawafahamu na wala hawajawahi kuiona sera ya elimu japo wao ni walimu na wamesomea ualimu

13

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

unalolifundisha ni muhimu sana kwa mwalimu yeyote, kwa sababu: kwanza, utafundisha ukweli na uhalisia wa dhana, nadharia na mifano halisi ili kushadidia uelewa wa wanafunzi. Walimu wasiolijua vyema somo wanalolifundisha mara nyingi huwa wanawadanganya wanafunzi au kuwapotosha kabisa. Pili, kuwa na maarifa na somo unalolifundisha kunamjengea mwalimu kujiamini na furaha ya kulifundisha somo hilo. Na zaidi sana, mwalimu anakuwa na uwezo mkubwa wa kuchagua, kubuni, kuunda na kutumia vifaa mbalimbali vinavyoweka fursa tele ya wanafunzi kupata maarifa na kuyafikia malengo ya somo.

7.6 Yamjengee mwalimu uzalendo wa kweli kwa nchi yake, jamii yake na rasilimali za

nchi. Mwalimu mwenye uzalendo wa kweli ataongozwa na hisia za utaifa na hivyo atawasaidia sana raia wenzake kufanikiwa maishani kwa kuwafundisha ukweli bila kuchoka, kuwapa hamasa ya kutambua rasilimali zao, kukuza amani ya jamii waishimo, kukuza maelewano na kushiriki vyema kwenye jamii watokako. Bila roho ya uzalendo wa kweli mwalimu atafundisha yaliyo kwenye karatasi tu bila kujali masuala ya ziada ya ki-utu. Mwalimu mwenye uzalendo atapandikiza mbegu ya uzalendo wa taifa kwa wanafunzi wake, atatetea vipaji vya maelfu ya raia wenzake(wanafunzi) wanaobaguliwa na kunyanyaswa sehemu aliko.

Mwalimu mwenye uzalendo, atatetea rasilimali za taifa popote alipo, na atajitoa kwa moyo kulitumikia taifa lake bila kuchoka kwa maslahi ya wengi wanaomzunguka. Bila uzalendo kwa walimu wetu ajira zao zinakuwa sehemu ya kupitia kuelekea ajira nyingine. Uzalendo wake utamfanya awe mwana demokrasia na ashirikiane kikamilifu na wanafunzi. Wanafunzi wanapaswa kushirikishwa katika nyanja zote za elimu badala ya masuala yote yahusuyo elimu kushughulikiwa na utawala au idara zinazohusu elimu pekee. Walimu wanapaswa kuwa sehemu ya maisha ya wanafunzi na wanapaswa kutoa huduma mbalimbali kwa wanafunzi zikiwemo zile za ushauri nasaha. Ushauri wa kitaaluma ndiyo unaosisitizwa zaidi ukizingatia vikwazo vinavyokabili sekta ya elimu”.15

7.7 Yamuandae mwalimu kufanya na kufikiri kupita mipaka aliyoizoea ili awe wabunifu na awasaidie watoto kufikia malengo. Ubunifu ni muhimu sana kwa mwalimu. Mafunzo ya ualimu yasiyojenga ubunifu hayawezi kumfanya mwalimu amudu mabadiliko na changamoto zinazomkabili. Taasisi ya Elimu Tanzania mwaka 2007/2008 ilitoa miongozo ya kiutendaji ambayo mwalimu anapaswa kufanya zaidi ya mipaka aliyo izoea ili kufikia malengo yanayotarajiwa. Masuala saba muhimu yaliyoanishwa ni kuwa; mafunzo ya ualimu ni lazima yampe uwezo mwalimu wa kuwahimiza wanafunzi kufanya shughuli na usomaji unaojenga uwezo wao. Kuwajengea wanafunzi matumaini na matarajio makubwa ya kile

15 May Garland, “Warsha ya hisabati: sehemu ya mahojiano na mtaalamu wa elimu Uri Treisman, katika Jarida

la Maendeleo ya Elimu, 16 na 3 la 1993, uk. 14 – 16, lenye kichwa kisemacho“Kuwasaidia wanafunzi waliotengwa katika elimu kufanikiwa katika malengo,” mbinu za kufundisha na kujifunza.

14

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

wanachopaswa kuelewa. Kuwapa mrejesho wa mara kwa mara kwa kile wanachohitaji toka kwa mwalimu katika mchakato mzima wa kujifunza na kufundisha. Kutambua na kushughulikia staili tofuati tofauti za kujifunza na kukuza maendeleo ya vipawa na weledi unaotofautiana wa wanafunzi. Kutoa mifano ya uhalisia wa vitu vinavyoonekana katika jamii, kuweka fursa za kujadiliana na kushirikiana kwa wanafunzi na walimu na kutambua na kuzitumia mbinu mbalimbali za kutathimini na kupima maendeleo ya wanafunzi na kukazania kujiendeleza kitaaluma na kibinafsi muda wote.16

7.8 Yamjengee mwalimu nidhamu ya kudumu. Katika ulimwengu huu hakuna kitu kinachokwenda na kufanikiwa bila kutanguliza nidhamu. Hasara kubwa ambayo dunia imepata, na inaendelea kupata ni kutokana na kukosa nidhamu.

Hebu fikiria! nchini Tanzania ni watu wangapi wanakufa kutokana na madreva kukosa nidhamu ya kuheshimu sheria na alama za barabarani, kuheshimu aina ya barabara anayopita na kukosa nidhamu binafsi kwa kunywa pombe kupindukia na kuendesha gari hovyo. Hata katika jeshi; kitu pekee kinachofanya jeshi kuwa imara na kuwa na mafanikio ni nidhamu. Bila nidhamu hakuna jeshi.

Vivyo hivyo, kwa walimu ni zaidi ya hapo. Mafunzo ya ualimu yanapaswa kumjengea mwalimu nidhamu ya kiakili, nidhamu ya kiutaalamu, nidhamu ya kiujuzi, nidhamu ya kitabia, nidhamu ya weledi na nidhamu ya kijamii na kisiasa. Mwalimu aliyepata mafunzo yaliyomjengea nidhamu huwa ni mfano wa kuigwa katika jamii, na ni daraja zuri la kuwavusha maelfu ya watoto toka familia masikini kuelekea kwenye maendeleo ya kweli. Tuna mifano halisi ya walimu kukosa nidhamu: ndiyo wanaohusika zaidi na kuwapa mimba watoto wa shule kutokana na kukosa nidhamu ya maadili binafsi, ndiyo wanaoongoza kwa kuwadanganya wanafunzi kwa kuwafundisha uongo darasani, kuwapotosha wanafunzi, kuchelewa kazini, kukwepa vipindi na hata kugushi vyeti na kupokea hongo toka kwa wanafunzi ili wawape alama za kufaulu mitihani. Walimu kukosa nidhamu inasababisha migogoro mingi shuleni na wazazi kupoteza imani na walimu huku taaluma ya watoto wetu inaporomoka17

Mwanazuoni maarufu wa elimu aliwahi kusema,... “tunakosa nidhamu nyumbani, shuleni, maofisini, mitaani, barabarani na kuliingizia taifa hasara kubwa kwa kupoteza wingi wa mali na nguvu kazi ya taifa. Kukosa nidhamu katika elimu ni kubaya zaidi maana kunaweza kupoteza dira na falsafa ya taifa na kuliacha taifa likiwa na watu mbumbumbu na ombaomba”(Paulo Freire 1998:89).

16 Sehemu ya Mada iliyowasilishwa na Mkuza Mitaala bwana Mwinuka wa Taasisi ya Elimu Tanzania, yenye kichwa kisemacho,”competence based curriculumu for promoting learners centred –learning”aliyowasilisha mkutano wa Oxfam ukumbi wa TEC Dar es salaam tarehe 18 Agosti 2008. 17 Sehemu ya mahojiano na wazazi kijiji cha Mbalagane wilaya ya Meatu kuhusu tabia na mwenendo wa walimu, kama sehemu ya utafiti wa HakiElimu, tarehe 21 Julai 2009.

15

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

7.9 Mafunzo ya ualimu yanapaswa yamjengee mwalimu uelewa mpana wa mbinu nyingi tofautitofauti za kufundishia na namna ya kuchagua mbinu hizo kufundishia wanafunzi wa aina gani. Hii inampa mwalimu umahiri mkubwa wa namna ya kuyatoa maarifa aliyonayo kwenda kwa mtu mwingine na namna ya kuamsha vipaji vya watu wengine ili vichanue na vikue. Mbinu hizi zinaongozwa na nadharia za kiualimu ambazo huchagiza kujifunza na kupata kiu ya kujua na kuelewa masuala mengi kwa upana wake. Hii ndiyo inaleta umaana wa saikolojia ya ualimu na mbinu za ufundishaji kuwa muhimu sana kwa mwalimu yeyote. Kuwa na maarifa ni kitu kimoja, na kuwa na uwezo wa kujua mbinu za kuyatoa na kuyapeleka maarifa hayo kwa watu wenye tabia tofauti na sifa tofauti za kupokea na kuelewa ni kitu kingine. Wengi hujidanganya kuwa mtu yeyote mwenye maarifa anaweza kufundisha; ni sawa na mtu mwenye miguu miwili yuko nje ya uwanja akitazama umahiri wa wachezaji na kujigamba kuwa anaweza kufanya hivyo akiingia uwanjani!

7.10 Ni lazima mafunzo yamjengee mwalimu hisia za kufundisha vyema na kuchagiza

tendo la kufundisha na kujifunza. Mwanamziki ambaye hana hisia wakati wa kuimba hawezi kuimba vyema, hawezi kuvuta hisia za wasikilizaji na hawezi kukonga nyoyo za wanaomsikiliza. Ndivyo ilivyo kwa mwalimu. Hisia za ufundishaji zinaongozwa na upenzi wa somo analolifundisha, kuithamini kazi ya kufundisha, kuwa na ari ya kufundisha, nia ya kufundisha, moyo wa kutaka kufundisha na fikra za kuridhisha wanafunzi wako ili ujivunie mafanikio mazuri ya wanafunzi wako wanapohitimu. Hisia za kufundisha ni muhimu sana kwa maendeleo ya mwalimu. Mafunzo ya ualimu ni lazima yapandikize hisia za kufundisha kwa walimu wetu ili wafanye vyema. Ukweli huu ulibainishwa pia na mhadhiri mkongwe wa ualimu, kama alivyonukuliwa;

... “kama mwalimu, ikiwa huna maarifa ya kutosha kuhusu somo unalolifundisha huwezi kutumia hisia za ualimu kuchagiza mchakato wa kujifunza na kufundisha, inawezakana walimu wetu sasa hawana hisia za kufundisha. Maana ukiwa unafundisha kwa hisia za kufundisha, kwa sababu unapenda, unafurahia, na kuguswa na kazi yako, ukiwa huna hisia hizi huwezi kuwezesha usomaji mzuri kwa wanafunzi”(Joseph Kisanji; Mratibu Mtandao wa Elimu Tanzania. Aprili 2009). 8.0 Mafunzo ya ualimu na mazingira ya kufundishia

Uboreshaji wa elimu una malengo maalumu na wala si suala la kuwaandaa walimu wazuri na kuwapeleka shuleni tu. Kama tunataka walimu wafundishe kwa ufanisi, tunapaswa kuwaandalia pia mazingira mazuri ili waweze kutumia maarifa yao vizuri. Walimu ni vyema waandaliwe mazingira mazuri yatakayowawezesha kuchangamana na wanafunzi pamoja na familia za wanafunzi pamoja na uwezo wa kushirikiana na walimu wenzao ili kufanikisha tendo la ufundishaji.

16

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

Pia ni vyema walimu wafanye kazi katika mazingira ambayo mtaala wa elimu umeandaliwa vizuri, mazingira ambayo upatikanaji wa vitabu ni wa kutosha ili waweze kuwafanyia wanafunzi tathimini nzuri pamoja na kuwaongoza kujifunza kwa ufanisi zaidi. Mtaala unapaswa kuandaliwa katika kiwango kizuri ili kuwasaidia walimu kufanikisha tendo la ufundishaji kwa ufanisi zaidi. Kwa bahati mbaya, kutokana na matatizo ya kisera na kimaamuzi, mazingira mazuri kwa ajili ya kufanikisha ufundishaji hayapo katika shule nyingi za Tanzania. Ukweli wa shule nyingi za Tanzania kwa sasa ni kwamba hazijaandaliwa katika mazingira ambayo zinaweza kuwawezesha wanafunzi kukaa na mwalimu mmoja kwa zaidi ya mwaka mmoja na wala hazijaweka mazingira ambayo walimu wanaweza kupanga mipango ya elimu pamoja na kujifunza pamoja. Zaidi ya hayo, mtaala wa elimu wa Tanzania haumjengei mwalimu mazingira ya kuboresha mbinu zake za ufundishaji. Nchini Tanzania ni shule chache sana ambazo zimeandaa mazingira ambayo walimu wanapata fursa ya kuwasilisha pamoja na kutetea mawazo yao. Wanapata fursa ya kufanya tathmini, kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo yanayojitokeza wakati wa kujifunza. Bado lipo tatizo la kutowaendeleza walimu pamoja na ubaguzi katika elimu, ambapo walimu wengi wenye sifa hupangwa shule za mijini na vijijini ni wachache sana. Mazingira ya kuishi hasa nyumba za kuishi walimu ni duni sana. Lakini pia msaada toka jamii husika ni mdogo. Kutokana na hali hii wengi wanakata tamaa na kuacha kazi. Kutokana na changamoto zinazokabili usomaji wa siku hizi, itakuwa ni kujidanganya kudhani kuwa kitu kinachohitajika ni kuandaa walimu bora ambao wataleta matokeo mazuri katika tendo la kujifunza. Lazima tuzingatie mambo yote mawili ambayo huenda sambamba na mfumo bora wa elimu. Shule lazima zibadilike na zijenge mazingira mazuri ambayo yataweza kufanikisha tendo la kujifunza na kufundisha na walimu ni muhimu wajiandae kwa ajili ya mchakato huu. 9.0 Umuhimu wa mafunzo bora ya ualimu kwa walimu

na elimu Tanzania Uwezo wa mwalimu ni muhimu sana katika kufanikisha tendo la kujifunza kwa wanafunzi na uwezo huo unatokana na mafunzo sahihi na ya kutosha ya ualimu ( Ferguson, 1991a; Ruvkin, Hanushek, na Kain, 2000). Na hii ni kutokana na ukweli kwamba umuhimu wa elimu katika mafanikio ya wanafunzi na mwalimu unazidi kuongezeka. Zaidi ya hayo, mahitaji ya walimu yanaongezeka kila kukicha kutokana na kuongezeka kwa wanafunzi. Si kwamba walimu wanahitaji kutoa maarifa yanayohitajika kwa wanafunzi tu, bali pia wanatakiwa kutoa ujuzi kwa wanafunzi ili waweze kuutumia kutatua matatizo yanayojitokeza wakati wa kujifunza pamoja na kuwa na uelewa wa kusoma na kuelewa maarifa magumu yenye uwezo wa kujenga stadi mbalimbali. Ili mwalimu azifikie sifa hizi mafunzo ya ualimu yaliyo sahihi ni lazima kwake. Na pindi apatapo mafunzo hayo atakuwa na uwezo wa kuwaandaa watoto ndani ya jamii kuwa wazalishaji. Mwalimu ndiye mtendaji mkuu kwenye

17

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

mchakato wa kujifunza, hivyo ni lazima awe na uelewa mpana. Kama inavyotamkwa na waraka wa serikali hapa chini:-

“mwalimu ndiye mtendaji muhimu katika elimu na mafunzo. Mwalimu huwaandaa na kuwaelekeza wanafunzi katika kujifunza na kuhusiana na yaliyomo kwenye mtaala na kukuza, wakati wote fikra za mwanafunzi na kuwa tayari kujifunza mwenyewe (Sera ya Elimu na Mafunzo 1995, uk 5) Mafunzo ya ualimu ndiyo yanatoa upekee wa taaluma ya ualimu kulinganisha na taaluma zote katika jamii. Upekee huo uko kwenye nyanja nyingi baadhi ni hizi; Ualimu ni utaalamu kwa sababu mwalimu halisi hubobea katika kazi ya kutoa maarifa na kushughulika na binadamu, na ana saikolojia ya kuwalea na kuwakuza binadamu wenzie wenye tabia na sifa tofauti tofauti ili wawe watu muhimu kwenye jamii yao. Ni tofuati na mhandisi anayeshugulika na majengo na mitambo, isiyosema wala kubadili tabia na hisia. Mwalimu amesomea saikolojia ya binadamu, kwamba watoto wakiwa na umri fulani wakoje, uwezo wao wa kuelewa ukoje, namna yao ya kufikiri ikoje na jinsi wanavyobadilika kitabia. Na pia utaalamu huo wa mwalimu unamuonesha ni nadharia gani aitumie kutoa maarifa hayo, kwa wakati gani, katika mazingira yapi, na kwa nani na kwa sababu zipi18 Hapa ndipo tendo la ukuzaji wa maarifa kwa wanafunzi linafikiwa, na kuwafanya wananchi wawe wazalishaji wazuri ndani ya jamii. Mafunzo ya ualimu ndiyo yanayotoa mwelekeo wa taifa linakotaka kwenda kwa kuwaandaa wananchi wake. Kama mafunzo ya ualimu yatakuwa dhaifu, walimu pia watakuwa dhaifu na wanafunzi wanafundishwa na walimu dhaifu watapata maarifa dhaifu na watashindwa kuondoa changamoto zinazoikabili jamii, na hivyo kubaki na umasikini wetu huku tukizungukwa na rasilimali lukuki. Tazama (chati na 1) hapo chini inayofafanua mahusiano ya mafunzo bora ya ualimu na maendeleo ya jamii husika.

18 Sehemu ya Chapisho la kitafiti la HakiElimu (Mwalimu ni Nani-utaalamu na upekee wa taaluma ya ualimu), lilitolewa mwaka 2008 uk 20

18

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

Chati 1: Mahusiano ya mafunzo bora ya ualimu na maendeleo ya jamii.

Chanzo: Kielelezo cha mwandishi kutafakari mahusiano ya muunganiko wa nadharia ya mafunzo ya ualimu na utendaji wa walimu katika kuchochea maendeleo ya jamii.

10.0 Hatari za kukosa mafunzo bora ya Ualimu Kwa watu makini hatari ya kukosa mafunzo bora kwa walimu wetu iko wazi ndani ya jamii. Nianze na kauli ya hamasa ya Mhadhiri mkongwe wa ualimu aliyeitoa kuonesha kutoridhishwa kwake na kukosekana kwa mafunzo bora ya ualimu. ....“walimu wengi wameanza kudanganya badala ya kufundisha, hii ni kutokana na ukweli kwamba masuala mengi ya kiualimu na kitaaluma hayafahamiki kwao, hayatoshelezi na ama hayajulikani kwenye maisha yao ya kazi ya kila siku. Lakini ikumbukwe kwamba wanafunzi hawako shuleni ili wadanganywe, bali wafundishwe-tena wafundishwe ukweli.”(Ishumi: 2008)

Mafunzo ya ualimu yaliyopo kamili, sahihi na bora

Sera, mipango na falsafa ya Elimu ya nchi.

Mchakato bora wa kujifunza

na kufundisha

Walimu bora

Elimu bora kwa wanafunzi

Maarifa Ujuzi Ajira tele

Kujitambua Uwezo mpana wa

Stadi kufikiri

Ustawi na maendeleo ya jamii nzima

19

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

Pamoja na athari nyingi zinazojitokeza kutokana na walimu wetu kukosa mafunzo bora ya ualimu, athari hizo zinatofautiana kiukubwa na kutokana na makundi yanayoathirika. Baadhi ya athari kubwa za walimu wetu kukosa mafunzo bora ya ualimu ni:- 10.1 Kuuawa kwa vipaji vya watoto wetu: Mwalimu asiye na mafunzo ya ualimu kwa kawaida anakwenda darasani kuua vipaji vya watoto na kuvuruga akili za watoto. Falsafa za makuzi na maendeleo zinabainisha kwamba kila mtoto amezaliwa na uwezo wa kufikiri, maarifa na vipaji vya aina mbalimbali. Vipaji hivyo vinapaswa kuendelezwa, kukuzwa, na kupaliliwa ili vichanue vizuri na vizae matunda bora. Siyo kazi rahisi kukuza na kupalilia vipaji vya watoto wetu. Kuna maandalizi muhimu na utaratibu mzuri wa kufanya hivyo ambapo walimu ndio watendaji wakuu. Mwalimu asiye na mafunzo ya ualimu hawezi kujua ni nadharia ipi aitumie kukuza vipaji vya watoto na kupalilia vipawa vyao ili vikuzwe. Matokeo yake badala ya kukuza yeye anavididimiza na kubinya vipaji hivyo au kuvivuruga kabisa. Na hatimaye kufa. Bila walimu wenye mafunzo bora ya ualimu elimu itaanguka nchini! Tuna mifano mingi. Mtoto anaweza kuhitimu elimu ya msingi akiwa na maarifa ya kutosha ya somo la hisabati na sayansi, anafaulu kujiunga na sekondari ambako anakutana na mwalimu asiye na mafunzo ya ualimu; hajiwezi, hajui lugha na hana maadili. Hapa hawezi kupata kitu matokeo yake hata uelewa aliokuja nao toka shule ya msingi unapotea. Maana anafundishwa na mwalimu asiyejua anachokisema, asiyejua lugha ya kiingereza, asiyetoa motisha wowote wa kujifunza na pengine asiye na ufahamu na maarifa ya kutosha kuhusu somo analofundisha. Haya ndiyo yanayoendelea katika shule zetu nyingi za vijijini. Ndiyo maana hata viongozi wetu hawapeleki watoto wao katika sekondari za vijijini, hata watoto wao wakifaulu huko wanahamishwa na kupelekwa kwenye shule zenye walimu waliopata mafunzo bora ya ualimu. Wanaogopa watoto wao kufa kiakili na kivipaji. 10.2 Kukuza matabaka katika jamii: Mwendelezo wa harakati za kusaka elimu bora zimewatenga watoto wanaotoka familia masikini hasa kutokana na kuwepo kwa walimu duni shuleni. Shule za vijijini na hasa za serikali ndizo zinazoongoza kwa kuwa na walimu duni- wasio na mafunzo bora ya ualimu. Na kutokana na kuwepo kwa walimu duni na elimu inayotolewa ni duni sana. Hivyo, wenye pesa na nafasi nzuri kiuchumi wamewatenga watoto wao na wale wanaotoka familia masikini. Wao wanapeleka watoto wao kwenye shule za kimataifa, seminari na shule binafsi zenye walimu bora. Lakini watoto masikini hawana mbadala wowote. Wanapokea kile kilicho mbele yao kwa sababu hawana pa kukimbilia. Hapa ndipo matabaka yanapokuzwa na kumomonyoa umoja wa kitaifa ambao waasisi wa taifa hili waliujenga kwa nguvu nyingi. Je, ndiko tunakopaswa kwenda? 10.3 Kuliandaa taifa kuwa soko la bidhaa za wabunifu na wenye maarifa: Kuwa vibarua wa watu wenye maarifa na ujuzi, kuwa watumishi wa ndani na watumwa wa watu wenye pesa na kuwa watumwa wa utamaduni wa mataifa yanayoelimisha watu wake kupitia

20

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

uandaaji bora wa walimu wao. Ukweli huu uko wazi. Maana walimu duni wanazaa wanafunzi duni ambao hawana uwezo mkubwa wa kufikiri wala uwezo wa kuhoji na kutatua matatizo. Hawezi kushindana katika ulimwengu wa sasa wa utandawazi na muingiliano wa maarifa na biashara ya nguvu kazi na utaalamu. Watoto waliofundishwa na walimu duni watakuwa watazamaji ndani ya dunia ya utandawazi huku wakigeuzwa bidhaa rahisi na nguvu kazi za dezo kwa watu wenye maarifa na ujuzi waliofundishwa na walimu bora. Mifano iko hai; ambako kila leo maelfu ya watanzania wanakimbilia mijini kuja kutafuta angalau kazi za ulinzi na utumishi wa ndani kwa wahindi, waarabu, wazungu na watanzania wenzao wenye maarifa, huku nyumbani kwao watokako wameacha rasilimali za thamani kubwa wasizozijua kwa sababu hawana macho (maarifa) ya kuziona fursa na rasilimali zinazowazunguka na kuzitumia kuendeleza maisha yao. Fikra za nani zisizoguswa na udhaifu huu wa walimu wetu? 10.4 Ongezeko la migogoro shuleni: Uduni wa mafunzo ya ualimu umechangia pia katika kuleta migogoro shuleni. Walimu walio na mafunzo duni ya ualimu wengi wanakosa msingi wa maadili ya ualimu, na hivyo wanajiingiza kwenye vitendo viovu kama kuwapa mimba wanafunzi wa kike, kulewa kupindukia, kukwepa vipindi na kutoa adhabu zisizostahili kwa wanafunzi wao. Masuala haya yamejenga uhasama na jamii husika na baadhi ya maeneo ya nchi yetu yamesababisha migogoro mikubwa shuleni, migomo ya wanafunzi na kufukuzwa shule wanafunzi wengi. Jamii huwatarajia sana walimu katika maeneo yao kiushauri na malezi ya watoto. Lakini, walimu wa sasa wanaopelekwa shuleni bila mafunzo sahihi ya ualimu, hawamudu kazi ya ulezi, uzazi na ualimu. Matokeo yake wanakuwa chanzo cha kuharibu tabia na mwenendo wa watoto.19 Na haya siyo matarajio ya jamii kubwa ambayo siku zote inawaamini walimu na kutarajia mengi mema toka kwa walimu na sio balaa kwa watoto wao. 10.5 Kufifisha maendeleo ya jamii nzima: Panapokuwepo na walimu duni wanaozaa jamii duni hakuna kasi ya maendeleo katika jamii ile. Maana hakutakuwa na wataalamu katika sekta nyingine zote, maana hawana maarifa. Na Kwa sababu wengi hawawezi kushiriki kuleta maendeleo kwa sababu hawana maarifa, badala yake wengi watageuka kuwa mzigo kwa wale wachache wenye uwezo wa kuzalisha ndani ya jamii. Taifa lolote lenye wazalishaji wachache na kuwa na wategemezi wengi hudumaa kimaendeleo. Na ndipo tulipo! Ndipo tunakotaka kwenda? 19 Sehemu ya mchango wa wazazi tulioongea nao kijiji cha Mbalagane-Meatu-Shinyanga 21 Julai 2009.

21

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

11.0 Hitimisho/Mapendekezo Matarajio ya jamii yote ya watanzania wanaoandikisha watoto wao shule ni kuona watoto wao wanapata maarifa, uwezo wa kufikiri, ubunifu, stadi na ujuzi muhimu, uwezo wa kuwasiliana na uwezo wa kutatua matatizo ili wachangie juhudi za wazazi wao kutatua changamoto za jamii na kujiletea maendeleo ya kweli ndani ya jamii yao na taifa kwa ujumla. Elimu yoyote isiyofikia ndoto hizi za jamii kubwa inasaliti matamanio na matarajio ya vizazi vijavyo, na kuliweka pabaya taifa. Taifa lolote lisilo na watu wenye maarifa kamwe haliwezi kupata maendeleo. Tuna ushahidi wa mabilioni ya fedha za misaada toka Benki ya Dunia na mataifa tajiri ya wahisani zinazomwagwa kila uchao nchini, lakini hakuna maendeleo yanayoonekana. Na inawezekana hata kama pesa zitaendelea kutolewa hatutafikia maendeleo ya kweli bila kuwapatia elimu watoto wetu ili wajue namna ya kuzalisha pesa na kutatua changamto zinazowakabili. Nchi zote zilizoendelea zilisomesha watoto wao na siyo kupokea misaada! Ukweli huu aliujua sana Mwalimu Nyerere ndiyo maana siku zote alisisitiza kuwa; “..ukitaka kumsaidia masikini somesha watoto wake”. Na elimu kwake aliona kama mkombozi pekee wa taifa la Tanzania. Maana aliamini ni muhimu sana kumjenga mtu kwanza ili mtu huyu ajenge vitu anavyohitaji20 Walimu wenye mafunzo bora ya ualimu pekee ndiyo wanaojenga taifa lenye mwelekeo na matumaini ya maisha bora ya baadaye. Tukitambua ukweli huu, tukaongozwa na umakini ndani ya uzalendo wa kweli tunaweza kuboresha haiba za wananchi wetu kwa kuandaa mitaala ya mafunzo ya ualimu inayoshabihiana na mahitaji ya jamii, na sio kunakili na kuiga mitaala ya wakoloni ambayo haiwapi maarifa wala nguvu walimu wetu kufundisha kile jamii inataka kujua. Tuboreshe mazingira ya kufundishia na kurudisha miaka sahihi ya kutoa mafunzo ya ualimu na sio kukatisha mafunzo ya ualimu kwa sababu tu ya maamuzi ya kisiasa ambayo hayawaathiri watoto wa wanasiasa. Mathalani, walimu wote tuliofanya nao mahojiano wanashangazwa na uamuzi wa kupunguza miaka ya walimu –wanafunzi kusomea ualimu ngazi ya stashahada na shahada. Wanashindwa kuoanisha sababu za kupunguzwa mwaka mmoja wa mafunzo na athari kubwa ambazo zinajitokeza shuleni. Ukweli bado uko pale pale; walimu wanahitaji kipindi kirefu cha kufundishwa nadharia na vitendo sahihi ili wawe bora katika kazi zao. Ni muhimu pia kuboresha mfumo wa upimaji na usimamizi wa mafunzo ya walimu kwa vitendo, kwa sababu wakufunzi na wahadhiri nao wanapita kutathimini kwa muda mfupi, na mara nyingi wanawapima walimu wanafunzi siku moja au mbili tu. Muda huu hautoshi

20 Maneno aliyosisitiza sana Nyerere katika kitabu chake cha “Binadamu na Maendeleo”. Na bado amerudia rudia sana katika hotuba zake nyingi.

22

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

kumpima mwalimu-mwanafunzi na kumwelekeza njia bora anazoweza kutumia kuboresha utendaji wake ili awe mwalimu bora na aweze kuwasaidia wanafunzi. Hili linafaa liambatane na dhamira ya kweli ya kuboresha mafunzo ya ualimu kazini ili walimu wetu wapate fursa ya kuboresha utaalamu wao, kujikumbusha masuala mengi, kuamsha maarifa na kuchagiza vipaji vyao. Suala hili haliepukiki ndiyo maana hata viongozi wa kada nyingine hasa wanasiasa wana semina na warsha nyingi za kuboresha utendaji wao. Mafunzo haya yanapaswa kuwa na program maalumu na uendeshaji maalumu; siyo ya kubahatisha kama ilivyo sasa. Na mwisho, ni muhimu sasa Watanzania tukatenganisha siasa na utaalamu ili kusaidia kukuza elimu. Maamuzi mengi ya kisiasa kwenye utaalamu wa elimu yamechangia kuifikisha elimu hapa ilipo. Na wanasiasa wanaochangia maamuzi ya hovyo, hawaathiriki na dosari zinazojitokeza maana watoto wao hawasomi katika shule zenye mapungufu makubwa yanayotokana na maamuzi yao. Huo ni usaliti mkubwa wa vizazi vya Watanzania. Utaalamu utangulie siasa ifuate. Na cha muhimu zaidi ni lazima ifikie kipindi sekta ya elimu iwe na mamlaka au wakala wake maalumu wa kuiendesha kama ilivyo katika nchi nyingi zenye mafanikio. Ndipo taaluma ya ualimu na utaalamu wa walimu utathaminika na kuendelea kwa manufaa makubwa ya Watanzania. Tuliokoe taifa kwa kuokoa vipaji vya maelfu ya Watanzania wanaofundishwa na walimu bandia, kwa kuboresha mafunzo ya ualimu. Tukiweka nia thabiti, tunaweza.

23

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

12.0 Marejeo

American Federation of Teachers. (2000). Building A profession: Strenthening Teachers preparation and induction, a report of the K-16 Teachers Education Task force. Washindton, DC USA.

Benner, A.D.(2000). The Cost of Teachers Turnover. Austin, TX:Texas Center for Education

Research Cranton, P. (1996) Professional Development as Transformational learning: New perspectives for

Teachers of Adult, Jessey Base.San fransisco Darling-Hammond L. & Bransford, J. (2005). Preparing Teachers for a Changing World; what

Teachers should Learn and be able to do. Jossey-Bass a Wiley Imprint, San Fransisco USA Darling-Hammond, L. & Baratz-Snowden, J. (2005).A good Teacher in Every Classroom;

Preparing the highly qualified Teachers our children deserve, The national Academy of Education, USA

Danielson, C. (1996). Enhancing Proffessional Practice: A frame work for teaching; Alexandria,

VA: Association for supervision and curriculum development Donna, T. (2004). What Every Teacher Should Know about: A sage Publication Educationa International/ActionAid (2007) Building Strategic Partnerships between teachers’Unions

and NGOs; The need for Quality teachers to achieve EFA Galabawa, J.C (2005).Returns to Investment in Education: Startling Revelations and Alternatives

Before Tanzanians, Professional Inaugural Lecture Series No.45, university of Dar es Salaam.

HakiElimu (2008) Elimu ni uwezo siyo Cheti: Wananchi wanasemaje? Insha na michoro HakiElimu, (2008). Elimu bora ni nini? Taarifa ya utafiti kuhusu Mitazamo ya wananchi na

stadi za msingi za watoto: HakiElimu. (2007). Mafanikio gani yamefikiwa Elimu ya msingi: Taarifa za muhimu kutoka katika

mapitio ya serikali. HakiElimu. (2008). Mwalimu ni nani?; Mwalimu bora kwa Elimu bora, Print factory LTD,

Dar es Salaam. Jackson, T.(1993). Activities That Teach, Red Rock publishers Mamdani M, Rajani R &Valerie L (2009). Influencing Policy for Children in Tanzania: Lessons

from Education, Legislation and Socila Protection, Research on Poverty Alleviation, special Paper 09.30

24

Nyaraka za Msimamo wa HakiElimu 03

25

Michael A.A. (1998). Distance Education and Training of Primary School Teachers in Tanzania:

Uppsala Studies in Education 74 Naker Nipak, N.(2007). Shule nzuri ni Ipi? Raising voices Uganda, HakiElimu publishrers. Nyerere, J. (1968) Freedom and Socialism. A Selection from Writings & Speeches, 1965-1967, Dar es

Salaam: Oxford University Press. This book includes The Arusha Declaration; Education for self-reliance; The varied paths to socialism; The purpose is man; and socialism and development.

Nyirenda, S. D. & Ishumi GM. (2002). Philosophy of Education.An Introducation to concepts,

Principles and Practice. Dar es salaam University press Freire, P.(1998). Teachers as Cultural Workers: Letters to Those Who Dare Teach, WestVeiew

Press Qorro, M (2006) Does language of Instruction Affect Quality of Education. HakiElimu working

paper series 8 Scapp, (2003) Teaching Values; Routledge New York Severson, (2003). Helping Teachers Learn, Principal of Leadership for Adult growth and

Development: A Sage publication Company; Califonia Senge J. (2000). Schools that Learn, DoubleDay Publishing Group New York Tyler, R. (1969). Basic Principal of Curriculum and Instructions: University of Chicago Press TRCC, (2009). Tushikamane: Teachers Must be More Professional; Newsletter for Coalition

of Teachers Resource Centre, URT. (1995). Sera ya Elimu na Mafunzo; Wizara ya Elimu na Utamaduni URT, (2008) Program ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu, Mkakati Wa Maendeleo na Managementi

ya Walimu-TDMS;Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi URT, (2008). Basic Education Statistics in Tanzania 2004-2008, National Data Zombwe, G. (2007). Elimu ina Umuhimu gani katika Jamii Nyaraka za Kufanyia Kazi:

HakiElimu Zombwe, G. (2008). Kutengwa Katika Elimu Kutakwisha Lini?; HakiElimu Working paper no 3,

The Color print Ltd, Dar es Salaam www.pefchattanooga.org/www/docs/2-110